Andiko Zaburi 20:7 “ Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu”
Hawa wanataja magari na hawa farasi,
Bali sisi tutalitaja BWANA, Mungu wetu
Utangulizi.
Ni muhimu kufahamu kuwa Zaburi
hii chimbuko lake ni Mfalme Daudi, kiongozi wa nyimbo au kwaya wa Daudi aliimba
wimbo huu, au Daudi alitunga na kuwapa watu wa sifa waimbe hivyo Zaburi hii
inahesabika kama moja ya zaburi ya Daudi, Hata hivyo kihistoria Zaburi hii
ilitumiwa sana na wafalme waliofuata baada ya Daudi kama njia ya maombi
walipokuwa wanakwenda kupigana vita, Mfalme aliomba na kutoa sadaka kisha watu
walisindikiza maombi na dua za mfalme wao kwa Zaburi hii, hivyo ni zaburi
maarufu kama maombi kwaajili ya kukabiliana na mambo ya kutisha! Ilitumika wakati
wa shida na wakati wa kuhitaji msaada.
Kuna mambo mengi sana yaliyomo
katika zaburi hii, lakini kubwa likiwa ni Dua ya kumuombea Mfalme, kwa nini
mfalme aliomewa sana kwa sababu yeye alitangulia mbele wakati wa vita, alikuwa
ndio mpambanaji mkuu na hivyo waimbaji na waombaji walimuombea angalia Mstari wa 1-4 Biblia inasema
“1. Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa
Yakobo likuinue. 2. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza
toka Sayuni. 3. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. 4.
Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.”
Baada ya dua na maombi ya
kumuombea Mfalme waliweka matumaini yao kuwa Mungu anakwenda kuwapa ushindi
hivyo walianza kushangilia ushindi, walilitumia jina la bwana na waliweka
bendera tayari kwa imani na pia
walimkumbusha Mungu kwa imani kuwa atamwokoa masihi wake na kumjibu Maombi yake
walikuwa na ujasiri kuwa watajibiwa Mstari
wa 5-6 na kuwa ni lazima Mungu atafanya mambo makubwa kwa mkono wake
“5. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu
wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote. 6. Sasa najua
kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.”
Katika mstari wa 7 na wa 8
waimbaji hawa walionyesha tofauti iliyoko kati ya wanaoamini na wasioamini
lakini pia walionyesha kwamba ndipo mahali pa kuzingatiwa sana katika utendaji
wa Mungu, “Hao (wasiamini) au wenye kiburi wanataja Magari na hawa
wasiomtegemea Mungu wa kweli wanataja Farasi, Bali sisi tunaoliamini Jina la
Mungu tutalitaja jina la bwana Mungu wetu! Ni muhimu kupaangalia mahali hapa
kwa makini sana
Mungu alikuwa amewafundisha
Isarael siku nyingi sana kumtegemea yeye na kumwangalia kwaajili ya ushindi na
dhiki ya aina yoyote, na katika nyakati za vita moja ya vitu vilivyokuwa
vinaogopewa sana katika nyakati za vita za zamani ni magari ya vita na magari
ya wapiganaji walikuwa wakipigana juu ya farasi, watu hao walikuwa hodari hata
kufukuzia na hivyo katika nyakati za biblia watu au mataifa yaliyokuwa na
magari ya vita na wapanda farsi hodari waliogopwa zaidi kwani ndio waliokuwa
hatari na wenye kutisha sana katika nyakati za leo Magari haya tungeweza
kufananisha na tanks au vifaru wakati wa vita wote tunajua namna vinavyotisha
sana
Mungu aliwaonya mapema Israel
kutokuogopa Kumbukumbu la taorati 20: 1
“Utokapo kwenda
vitani kupigana na adui zako na kuona farasi na magari na watu wengi sana
kuliko wewe usiwaogope, kwa kuwa Bwana Mungu wako yu pamoja nawe aliyekukweza
kutoka nchi ya Misri” pia Yoshua 17:16
Nchi ya Misri na Syria ndio
zilikuwa hatari zaidi kwa aina hii ya vita katika nyakati hizo na makabila
mengine pia Israel hawakuwa na aina hiyo ya silaha wakati huo, wala hawakuwa na
jeshi kubwa sana, hivyo wale wasiomuamini Mungu waliweka tumainilao katika hayo
magari ya chuma nay a farasi na wapanda farasi, Israel walikuwa wamekwisha
kupata somo kubwa kwamba Misri ilifanywa nini pamoja na kuwa na Magari ya
farasi na wapanda farasi Kutoka 15:1-4, Mungu
alikwisha kuwafundisha kutokuyategemea magari na wapanda farasi, Mungu
aliwajulisha kuwa hufanya mambo kwaajili ya jina lake na kwaajili ya utukufu
wake, Mungu hatakuinamisha bali Mungu atakusimamisha mungu hatakuaibisha bali
Mungu atakuokoa Mstari 8-9 waimbaji wanaonyesha kuwa hawataaibika na kuwa adui
zao watainama
Ndugu yangu haijalishi ni hila kiasi gani adui anazo,
Haijalishi watakuwa na nguvu kiasi gani
Haijalishi magonjwa yamekutesa kiasi gani, yamekuandama na
kukukandamiza kwa kiwango gani mtegemee Mungu tu
Haijalishi watakuwa na mbinu za
kibinadamu kiasi gani, wana silaha na magari ya chuma kiasi gani, wana watetezi
kiasi gani, wana uzoefu kiasi gani, wana akili kiasi gani, wana mitego kiasi
gani, wana nguvu kiasi gani tunachokiangalia wanatumainia nini, je wanatumainia
fedha, majeshi, nguvu waimbaji wakasema wao wanataja Farasi namagari sisi
tutalitaja jina la Bwana Mungu wetu, wapendwa na tuchangamke, tunaye Mungu,
tunaye shujaa, anauwezo, ana nguvu, ni hodari wa vita atatupigania anakwenda
kutupa ushindi anza kuufurahia ushidni wako leo yuko Mungu wa Yakobo atatuokoa
na ataisikia sauti yetu,
Bwana Mungu nimekutegemea wewe, tumaini langu si kwa wanadamu Bali ni
katika jina lako
Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake*
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!