Jumapili, 8 Juni 2025

Maana Mungu hakutupa roho ya woga !


2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”



Utangulizi

Nyakati za Kanisa la kwanza kuwa mkristo na kuwa muhubiri wa injili maana yake ilikuwa ni pamoja na kukabiliana na mateso, maumivu, kukataliwa, kutishiwa, kuonewa, kukandamizwa na hata kuuawa, Wakristo wengi waliotawanyika duniani wakati ule waliuawa na kuteswa kwa kutupwa gerezani, kutupwa katika matundu ya simba, kuchomwa moto na kupingwa vikali kwaajili ya wokovu, kwa sababu hiyo wakristo wengi na watumishi wengi wa Mungu waliingiwa na hofu au woga, na kwa sababu hiyo maendeleo yao ya kiroho na kihuduma yalikumbwa na vikwazo kwa sababu waliingiwa na shaka na hivyo kuogopa kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwaajili ya haya wakristo wengi waliingiwa na hofu na walihitaji kutiwa moyo kujua tuko katika njia ya dhiki nyingi

Matendo 14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”

Ni katika hali kama hii Paulo mtume akiwa gerezani huko Rumi akiwa mfungwa aliyehukumiwa kama muhalifu kwaajili ya injili anaandika waraka huu kwa kusudi la kumtia moyo Mtumishi wa Mungu Timotheo ambaye kwaasili alikuwa mwoga, akimkumbusha kuwa Mungu hakutupa Roho ya woga, bali ya nguvu na upendo na moyo wa kiasi, Timotheo ni kama sisi tulivyo leo, Tunahitaji kujikumbusha kuwa Tunaye Roho wa Mungu ndani yetu ambaye anatupa nguvu katika wakati wa mahitaji yetu, bila kujali kuwa tunakutana na magumu kiasi gani, au tuko hatarini kiasi gani, tunauwezo wa kukabiliana na hali yoyote ile inayotishia maisha yetu bila kuogopa kwa sababu Roho Mtakatifu yuko juu yetu na hivyo Hatuogopi! Kwa msingi huo basi Leo wakati huu wa juma la Pentekoste tutachukua Muda kujikumbusha tena na tena umuhimu wa Roho Mtakattifu katika kutupatia ujasiri unaotusaidia kusonga mbele bila kujali kuwa ni vikwazo gani tunakutana navyo katika maisha yetu ya Ukristo katika jina la Yesu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Mungu hakutupa roho ya woga!

·         Roho Mtakatifu ni roho wa ujasiri

·         Jinsi ya kutupilia mbali woga.

Mungu hakutupa roho ya woga!

Moja ya adui mkubwa sana wa watu waliookoka ukimuacha shetani ni woga, kwa kweli woga ni mtego mkubwa sana unaopunguza uwezo wetu wa kutenda mambo makuu pamoja na Bwana, Maendeleo yetu ya kimwili na kiroho na hata kisaikolojia yanaweza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa sana na woga, wako watu wanaogopa hata kuanza biashara, wako watu hawaoi kwa sababu wanaogopa wataoaje, wako watu hawafanikiwi kwa sababu wanaogopa kuingia gharama na kujitosa katika kufanya majaribio, woga unaleta mashaka, woga unaleta kutokujiamini, woga ni mtego unaotuzuia kufikia ndoto zetu na kuona ahadi za Mungu zikitimia katika maisha yetu, woga hutuletea kukata tamaa, woga unaweza kuchelewesha kwa kiwango kikubwa maendeleo yetu! Wana wa Israel walishindwa kuirithi inchi ya ahadi mapema kwa sababu zilizochangiwa na woga!

Hesabu 13:25-33 “Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”     

Hesabu 14:1-3 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

Woga uliwachelewesha wana wa Israel kuirithi inchi ya Kanaani kwa miaka 40,  woga ni adui mkubwa wa Imani, unapokuwa na woga ni sawa kabisa na kukosa Imani, na unapokosa Imani ni vigumu kabisa kumpendeza Mungu, huwezi kamwe kuzifurahia ahadi za Mungu na kuziona kwa uhalisi katika maisha yako, woga unaua maono, woga unachelewesha ndoto zako kutimia, Paulo mtume alifahamu kuwa kama Timotheo ataruhusu woga, kufungwa na kutiwa gerezani hata kuuawa kwaajili ya Kristo, atakuwa kikwazo kikubwa kwa injili kwake na kwa wale anaowaongoza kwa hiyo alimkumbusha kuwa Mungu hakutupa Roho ya woga, hii pia inatukumbusha na sisi leo kuwa hatukupewa Roho ya woga kwa jambo lolote lile linalotukabili, kwa kuwa Roho Mtakatifu sio Roho wa woga yeye atatupa ujasiri kuendelea mbele na injili na kusonga mbele hata kama tunakutana na magumu na vipingamizi na vitisho na hofu kamwe hatupaswi kuogopa na tusonge mbele kwa sababu hatujapewa roho ya woga

2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”

Neno woga linalotumika katika kifungu hiki, linasomeka kama “Deilia” katika lugha ya kiyunani likiwa na tafasiri ya fear au timidity ambalo tafasiri yake ni kukosa ujasiri, au kutikujiamini, au kuwa na aibu, kutishika na kuingia hofu hasa unapojilinganisha na kile unachokabiliana nacho ni kwaajili ya woga Israel walishindwa kumkabili Goliathi hata alipkuwa akiwatukana

1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.nBasi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Roho Mtakatifu ni roho wa ujasiri

Moja ya kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ndani ya mwamini, ni pamoja na kutuumbia Roho ya ujasiri, kila mwanadamu ndani yake kuna aina Fulani ya hofu au woga, tunaogopa kukosea, tunaogopa kushindwa, tunaogopa majaribio, tunaogopa kuchekwa, tunaogopa watu, lakini pia tunaogopa magonjwa, tunaogopa njaa, tunaogopa mateso na kadhalika, Lakini Roho Mtakatifu hutujengea ujasiri usiokuwa kawaida wa kuwa tayari hata kuwa mashahidi (kufa) wa Yesu Kristo kwaajili ya injili

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Warumi 8:15-18 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”

Roho wa Mungu ndani yetu hutupa ujasiri wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu bila kujali vikwazo vya aina yoyote tunavyokutana navyo, anatufanya tushuhudiwe ndani yetu kuwa sisi ni wana wa Mungu na kuwa hatuna kitu cha kupoteza, ndani yetu, Paulo anaona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kama ule utukufu utakaofunuliwa kwetu, kwa sababu hiyo hatuogopi wala hatupaswi kuogopa kwa sababu ndani yetu uko ujasiri kuwa sisi sio watu wa kawaida, tu wana wa Mungu na kama Yesu alivyo ndivyo tulivyo, na kama ikiwa sisi tuko kama Yesu je unaogopa nini hapa duniani?             

1Yohana 4:17-19 “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI HUMU. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.”

Tukijitambua kuwa sisi ni nani katika Kristo na kuwa hatukupewa Roho wa woga bali  ya nguvu na ya upendo, nay a kiasi hatutaogoa lolote hata ijapotetemeka nchi, ijapobadilika milima, vijapotikisa vilindi vya bahari bado hatutaogopa Roho Mtakatifu atatukumbusha kumtegemea Mungu, atatukumbusha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu msaada uonekanao tele wakati wa mateso, na sio hivyo tu anatukumbusha kuwa sisi ni wana wa Mungu na kuwa hatuna cha kupoteza duniani, hatutaweza kupoteza ujasiri kamwe ikiwa tu Roho Mtakatifu atapewa nafasi kubwa ndani yetu, Roho wa Mungu hutupilia mbali hofu na kutusaidia kukabiliana na hali yoyote ile inayotakiwa kukabiliwa ndani yetu! Na nje yetu mbele yetu na nyuma yetu!

Matendo 21:10-13 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.”          

Jinsi ya kutupilia mbali woga.

Ni muhimu kufahamu kuwa wewe sio matokeo ya mazingira wala sio matokeo ya kile watu wanachokisema wewe ni matokeo ya kile Mungu anachokisema kukuhusu, kwa msingi huo ili kutupilia mbali hofu na woga katika maisha yetu ya kila siku hatuna budi kujitazama kwa kulitazama neno la Mungu linavyosema kutuhusu  Neno la Mungu linasema:-

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.

Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”

Yoshua 1:9 “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

Neno la Mungu linatueleza kuwa hatupaswi kuogopa wala hatupaswi kuwa na visingizio wala sababu za kibinadamu, hakuna sababu zozote za kibinadamu zinazoweza kuhalalisha sisi kutokutumiwa na Mungu kwa sababu zozote zile, wala hakuna maumbile yoyote ya kibinadamu yanayoweza kuhalalisha Mungu kuto kutimiza kusudi lake ndani yetu kwa sababu hiyo hakuna kisingizio huusani pale Mungu anapotutia Muhuri kwa Roho wake mtakatifu!

Ni kwa sababu hiyo Paulo mtume alikuwa akimtia moyo Timotheo kuweka mbali hofu na aibu ili kumshuhudia Yesu Kristo kwa ujasiri, Kila mkristo anapaswa kujiandaa na kuwa tayari kukabiliana na aina yoyote ya mateso, kukabuliana na vita vya kiroho na kufungwa nahata kuuawa, au kupigwa na changamoto nyinginezo zote kwaajili ya injili haya yote yanawezekana ikiwa tutamruhusu Roho Mtakatifu ambaye ni Roho ya ujasiri na nguvu kutawala maisha yetu na hisia zetu.

Kila mmoja wetu anamuhitaji Roho Mtakatifu katika wakati huu wa sasa ili atupe ujasiri tusione haya wala tusiogope kumshuhudia yeye kwa ujasiri hata kama kuna hatari zinayakabili maisha yetu ni nguvu za Roho Mtakatifu peke yake zinazoweza kutusaidia na kutubeba kwa neema kuendelea kuwa na nguvu hata wakati ambapo tunakabiliwa na magumu kwaajili ya injili, na kwaajili ya maisha ya kawaida Roho Mtakatifu hutusaidia kuwa imara na kutokuogopa kikwazo chochote kinachosimama mbele yetu kwani kila kitu kinawezekana alipo yeye na sio kwa akili zetu na nguvu zetu, kwa hiyo kumbuka kuwa woga na hofu sio sehemu ya maisha yetu, woga na hofu si sehemu ya mtu aliyejaa nguvu za Roho Mtakatifu badakla yake akija juu yetu hofu zote na woga wa jambo lolote hutupiliwa mbali kabisa, leo hii tunapoadhimisha sikuu ya Pentekoste kumbuka kuwa Mungu hakutupa roho ya woga! , Mwamini Mungu, kabiliana na lolote lile linalokuja mbele yako, kabiliana na lolote lile kabiliana na kila changamoto na matisho, na mateso, na uhdia, na adha, na lolote lile linaloonejkana kuwa kama kwazo au kuwa kama mlima mbele yako jua ya kuwa kwa Roho wa Bwana litasambaratishwa na kuwa tambarare na makusudi ya Bwana yatatimizwa maishani mwako!

Zekaria 4:6-7 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima! 

Jumatano, 4 Juni 2025

Kwa hiyo hatulegei!

 

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika dunia hii iliyojaa changamoto, maumivu, majaribu, mateso, uonevu, dhuluma, kukosekana kwa haki, wivu, majungu na kuumizana, maneno ya kuumiza, na vita vya kila aina ni rahisi sana kwa baadhi ya watu hususani wale walio na moyo wa unyonge kulegea na kukata tamaa, na wakati huohuo kupoteza tumaini kwa sababu ya kuwako kwa vikwazo mbalimbali katika maisha, Paulo mtume yeye anasema na kutangaza kwa ujasiri “Kwa hiyo Hatulegei” ujumbe wake Paulo mtume kwa kanisa ni ujumbe wa matumaini na ushindi na nguvu kwa kila anayemwamini Yesu Kristo Bwana wetu, kwamba sisi ni watu wa tofauti na kamwe hakuna awaye yote aliyemwamini Yesu anayeweza kukata tamaa, au kuzimia moyo “Kwa hiyo hatulegei” tunaendelea kukaza mwendo kwa kadiri tunavyokutana na changamoto na majaribu ya namna mbalimbali.

Wafilipi 3:12-14. “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

Leo basi tutachukua muda kujifunza sababu zilizopelekea Paulo mtume kuelezea “Kwa hiyo Hatulegei” na tutajifunza ujumbe huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo yafuatayo:-

·         Maana ya kutokulegea.

·         Sababu za kutokulegea.

·         Kwa hiyo hatulegei.

Maana ya kutokulegea:

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana

Neno kwa hiyo hatulegei katika Biblia ya kiyunani linasomeka “dio ekkakeō ou”  kwa hiyo neno hatulegei kwa kiyunani ni “ekkakeō”  ambalo kwa kiingereza linaweza kutafasirika to become weak, to fail, to faint, to become weary, or to fail in heart, or we do not give up. kwa hiyo kwa Kiswahili maana yake hatuwi dhaifu, hatushindwi, hatuzimii, hatuchoki, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo.

Maana yake hata pamoja na magumu kiasi gani tunayokutana nayo, hata pamoja na dhiki kubwa tunayokutana nayo, hata pamoja na changamoto kubwa tunazokutana nazo, hata pamoja na vipingamizi vikubwa tunavyokutana navyo iwe ni katika imani, iwe ni katika huduma, iwe ni ugumu katika jambo lolote unalokutana nalo, vyovyote vile visisitishe huduma yako, wokovu wako, ndoa yako biashara yako, juhudi zako katika masomo, uwezo wako wa kumtumainia na kumtegemea Mungu, utumishi wako, juhudi yako ya kupambana na umasikini, jitihada zako za kujikwamua, mpango wako wa biashara, mpango wako wa kilimo, mpango wako wa uwekezaji, mpango wako wa ufugaji, mpango wako wa maendeleo, na msimamo wako katika Bwana haupaswi kuzimia kwa sababu zozote zile kwa sababu ya ujuzi wako na maarifa yako ya kina kuhusu Mungu na kazi yake anayoifanya ndani yako! Kamwe Mungu hawezi kukuangusha! Kwa hiyo hatulegei

Hakuna jambo baya sana kama kuzimia, kukata tamaa, kuvunjika moyo, kuchoka, au kuwa dhaifu, adui mkubwa sana wa mwanaridha yoyote yule ni pamoja na kuzimia, au kulegea, kuvunjika moyo, kuogopa, wasiwasi na mashaka, na kufikiri kuwa umezidiwa, wakati wowote mwanadamu anapokata tamaa anazuia maendeleo yake, anatengeneza ugumu wa kushinda vikwazo na kutokusonga mbele mtu awaye yote aliyeokoka hapaswi kamwe kulegea, kulegea na kukata tamaa na kuzimia moyo kunaashiria kuwa uweza wako na nguvu zako ni chache, Jeshi lolote lile halina haja na Askari ambaye anazimia moyo au kukata tamaa.  Mithali 24:10 “Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.”

Kulegea kunafananishwa na mwanamke aliyebeba mimba kwa miezi tisa akipitia shida na taabu mbalimbali kisha akaanza kusikia uchungu alafu muda wa kujifungua unafika wakati anataka kujifungua mwanamke huyu anachoka kusaidia kumsukuma mtoto ili atoke huo unakuwa wakati mgumu sana, unakuwa ni wakati wa dhiki, unakuwa ni wakati wa aibu, kuwa mwanamke huyu amebeba mimba lakini ameshindwa kuzaa, mwanamke huyu atashutumiwa kuwa alipoteza ujasiri na nguvu wakati wa kujifungua, kwa hiyo ni lazima Mwanamke asukume zaidi ili aweze kujifungua kama hakuna nguvu ya kuweza kujifungua maana yake hakuna nguvu ya kushinda kwa hiyo kushindwa kunakuja, aibu inakuja, fedheha inakuja, na jambo gumu zaidi linakabili:-

Isaya 37:1-3. “Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.”

Kwa hiyo kulegea maana yake ni kuzimia, ni kukaribia kushindwa ni kukosa msaada, ni kuchoka, ni kupoteza nguvu ni uwezekano mdogo wa kushinda vikwazo na changamoto mbalimbali zinazokukabili, kwa hiyo watu wa Mungu au watu waliookoka hawalegei, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo, wala hatusitishi juhudi wakati wa mambo magumu tunasonga mbele kama askari wema na waaminifu walioko vitani na ziko sababu kadhaa za kutufanya tusilegee!

Sababu za kutokulegea.

1.       Kwa sababu tunaongezewa neema – Mst 15

 

2Wakorintho 4:15 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.”

 

Mtu wa Mungu anapopita katika changamoto za aina mbalimbali kwa kadiri ya  mateso na majaribu yanavyozidi Mungu aliyemfufua Bwana Yesu anatuongezea neema ya kupita kawaida ya kutusaidia kushinda majaribu, kwa hiyo ndani yetu moyo wa kukata tamaa unabomolewa na Neema inazidi na kutuinua juu zaidi, tunapewa neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

 

Yakobo 4:5-6 “Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

 

Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

2Wakorintho 12:8-10 “Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

 

2.       Kwa sababu mtu wa ndani hachakai        Mst 16

 

2Wakorintho 4:16 “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.”

 

Paulo mtume anasema hatulegei wala hatuishiwi nguvu wala kukata tamaa kwa sababu utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku, wakati kila mkristo anapokutana na majaribu na mateso na machungu ya aina mbalimbali utu wetu wa ndani unapata uzoefu na mabadiliko na ukuaji wa kiroho, kwa hiyo hata kama kwa nje tunaonekana kuchoka, kuugua na kuchakaa utu wetu wa ndani unafanywa upya na kuimarishwa katika imani kupitia uhusiano wetu na Mungu, Imani, maombi, neno la Mungu na uzoefu wa kiroho tunaoupata kila iitwapo leo, wakati wa majaribu unachangia kwamba akili zetu zinakuwa, ujuzi wetu unaongezeka, tunazidi kumjifunza Mungu kutoka katika pito moja kuelekea katika pito lingine  na kama ni hivyo sasa kukatatamaa kunatokea wapi, kuchoka kunatokea wapi, kupoteza nguvu kunatokea wapi, unafungwa gerezani, magereza inaachia, unapigwa mawe mpaka kufa unafufuliwa na unaendelea na injili, unapigwa bakora na kuteseka unazidi kuongezewa neema, unaviziwa getini unashushwa kwenye kikapu na injili inaendelea, utachokaje kwa mfano  unapata ujuzi unapata hekima unajengewa ujasiri na unagundua kuwa hakuna kitu kinaweza kukutenga na wewe na upendo wa Mungu

 

Warumi 8: 38-39 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

3.        Kwa sababu mateso ya sasa ni mepesi na ya muda tu. Mst 17

 

2Wakorintho 4:17 “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;”      

 

Paulo mtume anayaona mateso ya sasa na dhiki hizi ni nyepesi na za muda tu na kuwa dhiki hizi zinatutengenezea utukufu mkubwa sana na wa milele, watu waliookoka ni askari, askari ili awe na utukufu mkubwa na cheo kikubwa sana lazima akasotee katika chuo cha maafisa wa kijeshi ili kuongezewa nyota begani mwake, wakati wote dhiki huwa zinatujaribu na kutukomaza kupata ujuzi wa kiroho na kutufanya tuwe imara zaidi kwa sababu hiyo hatulegei tunapata uzoefu kutoka kwa dubu na simba ili kumpiga Goliathi.

 

Ayubu 23:10-12 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,”

 

1Petro 1: 6-7 “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

 

Paulo mtume alikuwa anaangalia hitimisho kubwa lenye utukufu mwingi baada ya dhiki hizi za muda mfupi, Kule mbinguni Mungu atamtukuza kila mmoja kwa kadiri ya neema na mapito aliyoyavumilia kwa sababu hiyo hatupaswi kuangalia hivi vinavyoonekana ambavyo ni vya muda mfupi bali tuviangalie vile vya milele, mateso na dhiki na maumivu ni vitu vinavyoonekana lakini thawabu na utukufu mkuu Mungu aliotuwekea ni kitu kisichoonekana kwa sasa lakini katika uzima wa milele kuna mambo makubwa yanakuja mbele yetu.

 

2Wakorintho 4:18 “tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.”

 

4.       Kwa sababu huduma hii tumeipata kwa rehema Mst 1

 

2Wakorintho 4:1 “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei;”

 

Mungu aliyetuita katika wokovu na kisha kutupa wito wa kumtumikia ametuheshimu sana ni rehema kwa wewe na mimi kufanywa watumishi wa Mungu, angeweza kumtumia mwingine au hata kuwatumia malaika ambao ni wajumbe wake, lakini kwa rehema kubwa ametupa sisi huduma hii  tunawezaje kulegea? Tunawezaje kukata tamaa, Mungu ametukabidhi sisi kazi ya kuieneza injili ametupenda ametuhurumia ametuheshimisha tupeleke ujumbe wa Mwanae kwa watu wote, huduma hii ni ya rehema tu si kwa saababu tunastahili kwa hiyo kwa vipi tukate tamaa, kwa vipi tuzimie, kwanini tulegee?  Kama ni Mungu ameturehemu tumtumikie ni yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa chanzo cha nguvu zetu , kwa sababu hiyo ni lazima tushinde vizuizi vyote na changamoto zote na kamwe tusizimie moyo, kazi yetu ni kazi njema na ni kazi ya Mungu kwa hiyo tusizimie, Yeye aliyetutuma ana mamlaka yote Mbinguni na duniani kwa sababu hiyo hatupaswi kamwe kuogopa!

 

Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”         

 

Kwa hiyo hatulegei.

Ni muhimu maneno haya yakawa kauli mbiu katika utumishi wetu na maisha yetu ya wokovu, kila wakati unapohisi kuchoka au kuvunjwa moyo ni lazima tukiri kuwa Hatulegei, hatuzimii moyo hatuanguki, tunasonga mbele, kutokulegea kwetu ni ishara ya kuwa tunamjua Mungu kwa kina na mapana na marefu, na tunamwamini, Paulo alipokuwa anasema kuwa hatulegei yeye alikuwa anajua hakunamtu aliyepitia mateso kama yeye lakini hakuwahi kulegea hata siku moja.

2Wakorintho 11:23-33 “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?  Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.”

Mungu hatatuacha katika mapito ya aina yoyote ile aliahidi kuwa atakuwa pamoja nasi na kwa sababu hiyo atatutia nguvu kwa hiyo hata kama tunazingirwa na mazingira magumu kiasi gani hatutaangamia, wala hatutakata tamaa, kila jaribu linao mlango wa kutokea.

2Wakorintho 4:6-10 “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo. Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.”

Kwa hiyo Hatulegei.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatano, 28 Mei 2025

Mleteni huku kwangu!


Mathayo 17:14-21 “Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]




Utangulizi:

Katika kifungu chetu cha msingi wa maandiko leo, tunakutana na kisa chenye kushangaza sana ambapo wanafunzi wa Yesu walishindwa kumsaidia kijana aliyekuwa anateswa na pepo wa kifafa, Baba wa kijana alileta mashitaka hayo kwa Yesu kwamba kijana wake amekuwa akisumbuliwa na pepo hao wa kifafa ambao wakati mwingine wamemtupa kijana wake katika maji na katika moto, na alipomleta kwa wanafunzi wake wao walishindwa kumtoa, Ndipo Yesu kwa uchungu mkubwa alitoa agizo lenye uzito “Mleteni huku Kwangu” agizo hili sio agizo la kawaida ni mamlaka ya kiroho yenye maana pana kwa kila mtu anayetafuta msaada wa kweli.

Mleteni Kwangu!

Ni muhimu kufahamu kuwa ni swala la kawaida kwamba kila mwanadamu anapopatwa na shida au changamoto zozote zile zikiwepo changamoto za kiafya huwa anatafuta msaada, na wakati mwingine wanadamu huwa na tabia ya kupeana taarifa wapi pa kwenda ili changamoto zako ziweze kutatuliwa, Baba wa kijana huyu anaonekana wazi kukosa Amani kwaajili ya afya ya mtoto wake ambaye alikuwa anasumbuliwa na Pepo wa kifafa, na huenda alihangaika sehemu nyingi sana kwaajili ya kujaribu kutatua hali ya kiafya iliyokuwa ikimkabili kijana wake, hatimaye huenda alisikia habari za Yesu, lakini wakati huu Yesu alikuwa mlimani pamoja na Petro na Yakobo na Yohana wanafunzi wengine walibaki, Mzee huyu aliwakabidhi wanafunzi wa Yesu changamoto za mwanae na wanafunzi walishindwa kushughulika nayo, Yesu alipofika baba wa kijana alitoa taarifa kwa Yesu na ndipo Yesu alipotoa amri “Mleteni huku kwangu

Kwanini aletwe kwa Yesu?

Watu wengi sana wanapopatwa na changamoto za namna mbalimbali kwa kawaida huwa hawampi Yesu nafasi ya Kwanza, na badala yake huanza kutumia akili zao za kawaida na za kibinadamu katika kutatua changamoto zinazowakabili na Yesu huwa anapewa nafasi ya mwisho, hii sio tu kwa wanadamu wa siku za leo, bali hata wakati Bwana Yesu alipokuwa duniani bado wako watu waliokuwa na changamoto mbalimbali walianza kupeleka changamoto zao kwa matabibu mbalimbali na kuingia gharama kubwa

Marko 5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake;maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule

Inawezekana umekuwa ukipitia changamoto za aina mbalimbali kama mwanadamu katika maisha yako ya kawaida, ni desturi na jambo la kawaida sana wanadamu kuomba ushauri kwa wanadamu wenzao na kuelezewa kuwa wajaribu hiki au kile, nenda hospitali hii au ile kamuone mwanasaikolojia huyu au yule, kamuone daktari huyu au yule, nenda kwa mganga huyu au yule, changamoto yako hii yuko mama mmoja huyo ni kiboko, changamoto yako hii inangekuwa kule Sumbawanga ingeshughulikiwa, tatizo lako hili lingekuwa kule Kwamsisi ni jambo dogo tu, changamoto yako hii ingekuwa kule Lamu - Mombasa sharifu angekusomea, hili tatizo lingepelekwa kule Korogwe kwa Semangube lingekuwa kama chai tu, hii kitu kuna wazee kule Kigombe Muheza inaisha na kadhalika na kadhalik wanadamu wanaweza kukupa ushauri wa kupeleka matatizo yako huku na kule na ukasumbuka sana kwaajili ya kutafuta uzima, na ikakugharimu sana, Mzee huyu ambaye alihangaika vile vile kwaajili ya kijana wake alipeleka changamoto yake huku na kule hospitali za kawaida zilishindwa, hospitali za rufaa zilishindwa na sasa akawaona wanafunzi wa Yesu ambao nao vile vile walishindwa!

·         Wanafunzi wa Yesu walishindwa – Bado walikuwa wanajifunza, Yesu alikuwa amewapa amri na mamlaka juu ya pepo, lakini walikosa namna na jinsi ya kuachilia nguvu za Mungu na kuitumia mamlaka hiyo kutoa Pepo, hii ni kwa sababu waliogopa, walishindwa kuamini na pia walikosa maisha ya kufunga na kuomba na hivyo mamlaka yao ilikuwa chini, Yesu aliwajulisha kuwa Pepo wana mamlaka za kijeshi na Pepo wa kifafa (aina hii) wana daraja la juu katika mamlaka za kipepo za kuwatesa wanadamu na kuwa wanaweza kutolewa kwa maisha ya kufunga na kuomba

 

Luka 10:17-19. “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

 

Mathayo 17:17-21 “Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

 

Maisha duni ya kufunga na kuomba, pamoja na upungufu wa Imani ya wanafunzi wa Yesu ilikuwa ni sababu ya kushindwa kwao kuwaamuru pepo hawa wa kifafa kumuachia kijana na kumuweka huru Yesu aliwajulisha baadae tatizo lililokuwako, kwa hiyo walishindwa kumsaidia, na mzazi aliwashitaki kwa Yesu.

 

·         Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanadamu – watu wengi sana wanapokuwa na changamoto za aina mbalimbali katika maisha katika akili zao kichwani kwanza huanza kuwafikiri wanadamu, wanafikiria mtu atakayewapa muunganiko “connection” mtu wa kuwaunganishia, wanaelekeza mawazo yao na kuwategemea wanadamu na kama ilivyo ada Mungu anakuwa chagua la mwisho

 

Yeremia 17:5-8 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

 

·         Yesu ndiye suluhisho – Ziko shida ambazo madaktari wa kawaida hawawezi kushughulika nazo, ziko changamoto ambazo wanadamu hawawezi, ziko changamoto ambazo huwezi kuzidhibiti kwa mifumo ya kidini na kiserikali wala kwa uzoefu wako na maarifa yako bila kumkaribia Yesu Mwenyewe!

 

Yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka yote mbinguni na duniani, hata wenye mamlaka na waliopewa mamlaka wanahitaji kumtegemea Yesu kila wakati, Yesu anapoagiza mleteni huku kwangu alikuwa anatualika wote kwamba changamoto yoyote kubwa au ndogo inayokukabili yeye anaweza kushughulika nayo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, jina lake lina kibali kila mahali, yeye ni mwisho wa matatizo zote, na kuwa kwake hakuna jambo lisilowezekana, hakuna linaloshindikana kwake, kila kitu ambacho kimeshindikana kipelekwe kwa Yesu, peleka watoto walioshindikana, peleka mke aliyeshindikana, peleka mume aliyeshindikana, peleka magonja na shida na changamoto zote zilizoshindikana kwa sababu Yesu sio wa kawaida !

 

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”

 

Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

 

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

 

Hakuna mafanikio ya kweli unayoweza kuyapata nje ya Yesu Kristo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, yeye ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega, yeye kwa jina lake kila kitu kitapiga goti kiwe cha kuzimu, duniani au mbinguni, kila kitu kimetiishwa chini yake, mapepo yametiishwa chini yake magonjwa yametiishwa chini yake roho wote wachafu, falme mamlaka wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho yametiishwa chini yake, hakuna shida ambayo yeye hawezi kuitatua, maarifa yako yanaweza kushindwa wagaganga wako wanaweza kushindwa, washauri wako wanaweza kukwama, dini yako inaweza kukwama, wanasaikolojia wako wanaweza kushindwa kukukwamua Lakini Yesu anasema na kutoa mwaliko leo Mleteni huku kwangu, Yako mambo katika maisha yako huwezi kuyashughulikia, unahangaika kwa sababu hujawahi kujaribu kwa Yesu, sikiliza mwito wa Mwana wa Mungu yeye anasema Mleteni huku kwangu, ni mke aliyeshindikana kwa ukorofi, mleteni huku kwangu, ni mtoto aliyeshindikana kwa ukorofi mleteni huku kwangu, ni mume aliyetekwa na makahaba mleteni huku kwangu, ni mlevi aliyepindukia kila mtu amemkataa mleteni huku kwangu, ni huduma yako haieleweki, mleteni huku Kwangu, ni magonjwa madakatari wameshindwa mleteni huku kwangu, ni mwenye nyumba mkorofi mleteni huku kwangu, ni bosi mwenye gubu mleteni huku kwangu, ni shida ya aina yoyote imekushika kooni Yesu anatoa mwaliko mleteni huku kwangu  Yesu habadiliki uwezo wake wa kutoa msaada bado uko pale pale yeye ni yeye yule jana leo na hata milele na hakuna jambo lililo gumu la kumshinda yeye.Hebu twende mbele za Bwana na kupeleka mahitaji yetu yote yaliyoshindikana kwake yeye ni mwema atatusaidia.

 

Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.” Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”

 

Fanya uamuzi leo, wa kumkabidhi Yesu lolote linalokusibu na lolote libnalokusumbua katika maisha yako

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumanne, 20 Mei 2025

Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari!


Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini.Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue. Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa muujiza wa Bwana Yesu kutembea juu ya mawimbi ya bahari ya Galilaya haukuwa muujiza wa kawaida kama wengi tunavyodhani, muujiza huu wa aina yake kati ya miujiza mingi aliyoifanya Bwana Yesu huu umerokodiwa na injili tatu zisizo fanana kwa kusudi maalumu


Mathayo 14:22-33 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”


Marko 6:45-52 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.”


Yohana 6:16-21 “Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa.Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.”


Muujiza huu wa Yesu Kutembea juu ya mawimbi ya bahari kimsingi ulikuwa ni muujiza maalumu wa kujifunua kwa wanafunzi wake mamlaka kubwa aliyokuwa nayo Yesu dhidi ya majanga ya asili na uweza wake wa kiungu, na ndio maana muujiza huu haukufanyika mbele ya watu wote isipokuwa wanafunzi wake peke yao kimsingi muujiza huu ulikuwa unamfunua Yesu kwa wanafunzi wake kwamba yeye ana upekee wa aina yake!


1.       Uwezo wake wa kiungu – Wanafunzi wake wote waliorekodi muujiza huu hawakuacha kutaja neno “NI MIMI” Msiogope, Yesu Kristo alitumia mara kadhaa neno NI MIMI au mimi ndimi moja kwa moja akijifunua kwa mamlaka na uweza wa kiungu sawa na mwokozi aliyemtokea Musa tayari kwa wokovu wa wana wa Israel kutoka utumwani kule Misri neno NI MIMI lilitumiwa na Mungu kujitambulisha yeye ni  nani wakati Musa alipopata wasi wasi kuhusu wovovu wa wana wa Israel mbele za Farao.


Kutoka 3:13-15 “Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.”

 

Kwa kujitambulisha hivyo kwa wanafunzi wake Yesu ni sawa tu na anarudia namna Mungu alivyojitambulisha kwa Musa MIMI NDIMI, NI MIMI “I AM WHO I AM” jina hilo tafasiri yake ndio YHWH au Yahweh ambalo maana yake ni Mungu mwenye kujitosheleza na wa milele ni mwokozi kwa hiyo Yesu aliposema NI MIMI msiogope alikuwa anafunua mamlaka yake kamili ya uungu kwa wanafunzi wake

 

Kuna nguvu kubwa ya kupita kawaida nguvu ya uungu yenye uwezo zaidi ya wanadamu wa kawaida Yesu alipojitambulisha NI MIMI au MIMI NDIMI mwanafunzi wa Yesu Yohana katika injili yake anaonyesha jinsi majeshi ya wakamataji, yaani kikosi kilichotumwa kumkamata Yesu kilivyopata misuko suko mkubwa wakati Yesu alipojitambulisha kwao kwa usemi huo

 

Yohana 18:4-6 “Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.”

 

2.       Uweza wake juu ya maswala ya asili – Kristo Yesu alijifunua kupitia muujiza huu kuwa yeye anazo nguvu juu ya uumbaji na maswala yote ya asili, (Power over nature) kila janga la asili iwe ni matetemeko, iwe ni radi, iwe ni dhuruba, uwe ni upepo au bahari iliyochafuka Yesu ana uweza juu ya majanga ya asili, anauwezo wa kufanya yale yasiyowezekana kibinadamu ama yale yasiyofikirika injili zinaelezea kuwa mara Yesu alipopanda chomboni upepo na dhruruba vilikoma.

 

Mathayo 14:32-33 “Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”

 

Marko 6:49-51 “Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao;”

 

3.       Kutimiza unabii na kufunua uungu wake – Ayubu aliwahi kutabiri miaka 2,000 kabla ya Yesu kuwa ni Mungu peke yake mwenye kuzitandaza mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo kimsingi Yesu Kristo alikuwa anaufanya muujiza huu na maalumu alikuwa akitimiza unabii huu, kitabu cha Ayubu kiliandikwa yapata miaka 1000 kabla ya Yesu  na Yesu aliishi mnamo karne ya kwanza na kwa sababu hiyo kutoka Ayubu mpaka kuzaliwa kwa Yesu Kristo ilikuwa ni zaidi ya miaka 2,000. wanafunzi wa Yesu na watu wengine bila shaka walikuwa wamewahi kuyasoma maneno ya Ayubu na hivyo Kristo alipofanya muujiza huu walishangazwa sana na kujiuliza kuwa huyu ni mtu wa namna gani? Hata Pepo na bahari zamtii?

 

Mathayo 8:26-27 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?                 

 

Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini. Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue.Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?

 

Andiko hilo linafunua kuwa ni Mungu peke yake azitandaye mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo ni Dhahiri na ni wazi kuwa kitendo cha Yesu Kristo kutembea juu ya maji kwa kuyakanyaga mawimbi ya bahari alikuwa akiutimiza unabii huu, kwa hiyo muujiza unatufunulia ya kuwa Yesu hakuwa wa kawaida tu bali alikuwa na mamlaka ya uungu ndani yake, Bahari ilimtii, kanuni za kisayansi zilivunjika na Yesu alitembea juu ya maji, alikemea upepo na bahari na zikamtii.


Mambo ya Msingi ya kujifunza:

Kwanini Kristo anajifunua hivi kwa wanafunzi wake na kwa watu wote leo? Yesu hajifunui hivi kwa faida yake tu kwamba awe na sifa za uungu, Yesu anajifunua hivi kwetu leo ili kwamba wote tupate kumuamini kuwa yeye yuko pamoja nasi katika aina yoyote ya dhuruba, unapomuamini Yesu kwa kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako kumbuka muujiza huu haukuwa wa watu wote huu ulikuwa ni maalumu kwa wanafunzi wake ni muujiza maalumu kwa wale wanaomuamini yeye  kwa hiyo kwanza tunafunuliwa ya kuwa hatuko peke yetu, Wakati wanafunzi walipokuwa wakisumbuliwa na dhuruba na kujifikiri ya kuwa wako peke yao Yesu Kristo aliwatokea na kuingilia kati masumbufu yao, mashaka yao na wasiwasi wao, Leo tunajifunza ya kuwa muumba ulimwengu, mwenye nguvu juu ya majanga yote ya asili yeye ambaye Peke yake anaweza kukanyaga mawimbi ya bahari yuko pamoja nasi na atatutokea na atatuliza dhoruba zote zinazotukabili katika maisha yetu katika namna iliyo nyepesi sana na ya kushangaza, kwa hiyo hatuwezi kuogopa linapotokea janga la aina yoyote yeye ni kimbilio letu na nguvu zetu ona:-

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Tunajifunza kuwa tunapaswa kumwangalia yeye kwa imani bila kuona shaka, Petro alipomtambua Yesu aliyekuwa anatembea juu ya dhuruba na kuomba atembee juu ya dhuruba Bwana alimpa kibali na aliweza, lakini pale alipoona shaka na kuanza kuangalia dhuruba mara alianza kuzama, tunajikumbusha au kukumbushwa kuwa wakati wa changamoto zozote za maisha ni lazima tuendelee kumtazama Yesu, Ni lazima tumwamini na kutambua ya kuwa yeye peke yake anaweza kutusaidia na kuwa tunapoliitia jina lake atatushika mkono

Waebrania 12:2- “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Tunapomtazama Yesu ni muhimu kufahamu kuwa hakuna kuzimia na hakuna kuchoka wala kukata tamaa au kuingia mashaka, tunajifunza uweza mkubwa na mamlaka kubwa ya Yesu Kristo ili kwamba tupate kuamini na tukiisha kumwamini hakuna mtu awaye yote atakayetahayarika, Kama  Bwana wetu Yesu Kristo aliweza kupita sehemu hatarishi na akavuka salama tunajifunza kuwa sisi nasi tukimwangalia yeye tutapita sehemu hatarishi pamoja naye na tutavuka salama, maji na radi na vilindi vya bahari na dhuruba za kila namna vyote vina muogopa Mungu na kwa sababu hiyo hakuna jaribu liltakaloweza kusimama mbele yako lisishughulikiwe kwa jina la Yesu Kristo aliye hai.

Zaburi 77:16-20 “Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka, Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa. Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika; Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana. Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.”

Hitimisho!

Leo nakutangazia kuwa  haijalishi unapitia changamoto ya aina gani, dhuruba ya aina gani, upepo wa aina gani, haijalishi madaktari wamekuambia nini, haijalishi kuwa una rufaa mkononi kwenda hospitali kubwa, haijalishi mapigo yako ya moyo yako juu au chini, haijalishi umevamiwa na virusi vya korona, au ukimwi, haijalishi vipimo vikubwa vimekuja na matokeo magumu kiasi gani, haijalishi una maadui waliojipanga kwa kiwango cha kukutishia, haijalishi unaogopa nini,  haijalishi una madeni ya kausha damu, na mikopo umiza, haijalishi wamekodi mganga gani akuroge, haijalishi kuna vikao gani vya majungu vimekukalia, haijalishi fitina na majungu, na mizengwe unayowekewa nakutangazia ya kuwa yuko yeye akanyagaye mawimbi, kila aina ya wimbi katika maisha yako litakanyagwa na kutulia tuli katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, usiogope, usione shaka, usitikisike, usisitesite, usitetemeke, usikate tamaa, usilie, usiogope na kuwaza itakuwaje nakutangazia ya kuwa yuko akanyagae mawimbi ya bahari kila wimbi linalopita katika maisha yako Yesu atalikanyaga na litatulia kimya kwake yeye aliyezifanya mbingu na nchi katika jina la Yesu. 

“Kumbuka ni Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari! Wokovu una yeye Mungu wetu!”

Tufani inapovuma

sana moyoni mwangu!

Huona pa kujificha 

Mkononi mwa Mungu.

 

Hunificha, hinificha, Adui hatanipata, Hunificha, hunificha mkononi mwake

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Alhamisi, 15 Mei 2025

Nguvu ya maombi!


Isaya 38:1-6 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”



Utangulizi:

Mojawapo ya njia ya kutuletea neema kubwa sana kutoka kwa Mungu ni pamoja na njia ya maombi, wote tutakuwa tunafahamu jinsi maombi yalivyo na nguvu kubwa sana, yana nguvu ya kuteremsha rehema na neema kutoka kwa Mungu hata wakati tunapopitia changamoto za aina mbalimbali katika maisha yetu, maombi yana uwezo wa kumfanya mwanamke aliye tasa kuwa na watoto wengi, maombi yana uwezo wa kusababisha adui kupigwa na ushindi kupatikana, maombi  yana uwezo wa kufungua utendaji wa miujiza na kuchochewa kwa karama, maombi yana uwezo wa kubatilisha hukumu ya kifo na kurejesha uhai, maombi yana uwezo wa kugeuza kesi, maombi yanauwezo wa kubatilisha kile Mungu amesema. Maombi yana uwezo wa kufungua magereza za kimwili na kiroho, Mungu ametupa maombi kama njia ya kufanya kazi na yeye na kumruhusu kufanya kazi duniani. Maombi yana nguvu isiyoweza kuelezeka katika changamoto yoyote unayokutana nayo duniani wewe tumia maombi.

Mathayo 7:7-11 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?

Sisi ndio wenye maamuzi ya mwisho ya kuamua Mungu atafanya nini duniani kwa kutumia maombi, Hapa duniani sio eneo la utawala wa Mungu, ni eneo ambalo Mungu amewapa wanadamu kutawala, yeye utawala wake uko mbinguni, huko mapenzi yake yote hutimizwa kwa ukamilifu, lakini sivyo ilivyo duniani, ili kumpa Mungu kibali cha kufanya mambo duniani ni lazima tuombe, tunapoomba tunamruhusu Mungu kufanya yanayotakiwa yafanyike duniani kama yanavyofanyika mbinguni.

Zaburi 123:1-3 “Nimekuinulia macho yangu, Wewe uketiye mbinguni. Kama vile macho ya watumishi Kwa mkono wa bwana zao Kama macho ya mjakazi Kwa mkono wa bibi yake; Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu, Hata atakapoturehemu.”

Mwanzo 1:26-28 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”

Kupitia maombi tunaweza kumfungulia Mungu njia ya kututendea mambo makubwa na magumu tusiyoyajua, maombi yana uwezo mkubwa sana wa kubadilisha mambo na utendaji wa Mungu kutoka katika maisha ya mtu binafsi mpaka maswala ya kitaifa na ulimwengu kwa ujumla, tunapoomba tunamruhusu Mungu kuinguilia kati na kufanya jambo kwaajili yetu hapa duniani, tunaruhusu utawala wa kimbingu kuleta msaada wa haraka duniani.

-          Maombi yanaweza kumfanya tasa kuwa na watoto - Hana aliyekuwa mwanamke tasa, alipitia machungu na mateso na mashutumu kutoka kwa mke mwenzake, alinyanyasika hata pamoja na kupendwa sana na mumewe, lakini Penina mara kwa mara alimchokoza na kumkumbusha hali yake ya kukosa mtoto jambo ambalo lilimsikitisha sana na kumfanya kutembea kwa huzuni, Hana hata hivyo alifahamu kuwa njia pekee inayoweza kubadilisha hali yake ni maombi, hivyo alimimina maombi yake mbele za Mungu na hatimaye Mungu alisikia na kubadilisha hali yake aliyokuwa nayo, kutoka hali ya utasa kuwa mama wa watoto wengi.

 

1Samuel 1:1-6 “Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.”

 

1Samuel 1:10-20 “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.”

 

Tunajifunza hapa kuwa maombi yana uwezo wa kubadilisha aibu kuwa heshima, yana uwezo wa kufumba vinywa vya maadui zetu, yana uwezo wa kunyamazisha wanaotubeza, yana uwezo wa kuifanya biashara yako kufanikiwa, mashamba kuzaa, mifugo yako kuongezeka, maisha yako kujawa na mafanikio, Huduma yako kutendeka kwa kiwango na kanisa lako linaloonekana kama tasa likawa kanisa lenye watu wengi, tunaweza kubadilisha hali yoyote inayotukabili iwe ni chungu kuwa furaha, Hana hakukubali kubakia vile alivyo lakini kwa kupitia maombi alibadilisha mwelekeo wa maisha yake na kurejesha heshima yake kama mwanamke kamili kwa njia ya maombi, Maombi yanaweza kubadilisha hatima yako na jina lako.

 

-          Maombi yanaweza kutuletea ushindi vitani - Maandiko yanaonyesha kuwa watu waliookolewa wako vitani, Paulo anasema kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama maana yake hatuna adui wa kimwili sisi, wala hatuwezi kumuhesabu mwanadamu awaye yote kuwa ni adui yetu, lakini adui zetu wako rohoni, ni mamlaka, ni falme ni wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho, hao tunaweza kushughulika nao kwa njia ya kuomba peke yake, maombi yatatupa ushindi dhidi ya nguvu za giza popote.  

 

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

 

Ushindi wetu hauwezi kupatikana kwa nguvu za mwili na akili za kibinadamu na ujanja ujanja ushindi wetu utapatikana kwa kumualika Mungu katika vita zetu kupitia maombi, wakati Musa alipokuwa jangwani wanaikabili Kanaani njiani waameleki walitokea na wakapigana na Israel neno la Mungu linatuambia kuwa Musa na Haruni na Huri walipanda mlimani  na huko Musa alinyoosha mikono yake kwa Mungu na Yoshua  na Israel walipata ushindi, Musa akishusha mikono Israel wanashindwa, watumishi wa Mungu ili tuweze kuwa na ushindi tusikubali kushusha mikono yetu, tuendelee kumuinulia Mungu mikono yetu na ushindi utakuwa upande wetu kwa Dhahiri hapo tunajifunza nguvu ya maombi, kwamba tunaweza kupata ushindi.

 

Kutoka 17:10-13 “Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.”

 

-          Maombi yanaongeza nguvu wakati wa upinzani – Nyakati za kanisa la kwanza Mitume walipoanza kuhubiri injili na kufanya miujiza, walikutana na upinzani, walikamatwa, waliwekwa gerezani, waliadhibiwa na walitishwa na walikatazwa wasizungumze lolote kwa jina la Yesu, kanisa lilipopata taarifa walijua ni namna gani wanaweza kuendelea na injili, walijua dawa ni kuomba na walipoomba mahali pale walipokuweko pakatikiswa wakajaa nguvu  za Roho Mtakatifu na kazi ya Mungu ikaendelea na neno la Mungu linaenea.

 

Matendo 4:21-31 “Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 

-          Maombi yanaweza kubadilisha mpango mbaya wa Serikali na wafalme – Mfalme Herode alikuwa na mpango wa kuwaangamiza viongozi wa kanisa, na alimkamata Yakobo na kumuua na alipoona imewapendeza wayahudi akamkamata na Petro ili naye amuuue vile vile, maandiko yanatueleza kuwa Kanisa lilimuomba Mungu kwa bidii kwaajili ya Petro aliyekuwa amefungwa na Mungu alijibu maombi kwa kumtuma malaika wake aliyemtokea Petro gerezani na kumfungua, hakuna mlango wowote mgumu utakaofungiwa au mnyororo wowote wa adui unaoweza kushindana na nguvu ya maombi, maombi yana nguvu dhidi ya wafalme, Maombi yana nguvu dhidi ya serikali, na yana nguvu dhidi ya magereza yoyote.

 

Matendo 12:5-11 “Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.”

 

-          Maombi yanaweza kufungua milango ya gereza – Paulo na Sila waliokuwa wakiihubiri injili walipata matokeo makubwa sana na watu wengi waliokolewa lakini baada ya kijakazi mmoja kutolewa pepo wa uaguzi bwana zake walikasirika na kuwafanyia ghasia kubwa sana na hivyo mitume waliwekwa gerezani, na kufungwa katika mikatale, tunaelezwa kuwa watu hawa waliimba na kumuomba Mungu usiku wa manane na mara walipofanya hayo tunaelezwa kuwa kila kifungo cha magereza kiliachia sio wao tu na wafungwa wote na matokeo makubwa ni kuwa hata mkuu wa gereza aliokolewa na familia yake yote, tunajifunza kuwa hakuna kifungo chochote kiwe cha kimwili, cha kiroho, cha gereza cha waganga wa kienyeji cha wachawi kinachoweza kusimama mbele ya maombi, hakuna mtu yeyote awe askari awe mfungwa ambaye maombi hayana nguvu za kumgusa, kuna nguvu ya ajabu katika kuomba kwa sababu hiyo kanisa tusipuuzie kuomba kwa kila jambo tuombe, omba kila unapokutana na changamoto yoyote ile omba omba omba!  

 

Matendo 16:25-31 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

 

-          Maombo yanaweza kubadilisha mpango wa maangamizo – Mungu mwenyewe alikuwa amemtuma Yona kwamba aende Ninawi na kuuonya mji ule na kuutangazia kuwa baada ya siku 40 ataungamiza, watu wa Ninawi na mfalme wao walipoambiwa kuhusu mpango huo walimgeukia Mungu wakafunga na kuomba na kumshawishi Mungu kubadili hukumu na Mungu akaghairi maangamizi aliyokuwa ameyakusudia, maombi ya toba yanaweza kubadilisha hukumu ya Mungu ya kitaifa na ya mtu mmoja mmoja na kusababisha neema na rehema za Mungu ziweze kumwagika kwetu.

 

Yona 3:4 -10 “Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.”

 

-          Maombi yana uwezo wa kubatilisha tangazo la kifo – Katika kifungu chetu cha msingi cha somo hili tunamuona nabii Isaya akitangaza mauti kwa Mfalme Hezekia, tangazo hilo nabii Isaya alikuwa amepewa na Mungu, lakini Hezekia alilipuuzia tangazo hilo na kugeukia ukutani aliomba kwa bidii na kwa kulia machozi na kumkumbusha Mungu matendo yake ya rehema hata alipokuwa akiomba katikati ya kuomba kwake Mungu alisema na nabii Isaya kwamba amemuongezea Hezekia miaka 15 ya kuishi kwake, kumbe kupitia maombi tunaweza kukata rufaa kwa Mungu kwaajili ya tangazo lolote la hukumu hata kama tangazo hilo au tamko hilo limetoka kwa Bwana mwenyewe! Tunaweza kumsihi Mungu kwa rehema zake na akafanya kwa maombi

 

Isaya 38:1-6 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”

 

Hitimisho.

 

Tunajifunza hapo kuwa hakuna jambo lolote lililo gumu lisiloweza kubadilishwa kwa maombi, kama watumishi wa Mungu waliotutangulia waliweza kubatilisha maswala kadhaa wa kadhaa katika maisha yao na huduma zao kupitia kuomba sisi nasi leo tunaweza kuliitia jina la Bwana Mungu wetu asiye badilika ambaye ni yeye yule jana leo na hata milele na tukashuhudia matokeo makubwa katika maisha yetu kwa sababu hiyo tusiache kuomba tudumu katika maombi siku zote za maisha yetu

 

Wakolosai 4:2-3 “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa

 

Karibu na wewe, Mungu wangu, Karibu zaidi Bwana wangu……

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.