Ijumaa, 16 Juni 2023

Basi Ninyi mtakuwa wakamilifu


Mathayo 5:43-48 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya msingi mkuu wa malengo ya Mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo ilikuwa ni kuwafanya watu wote waliomuamini kuwa wakamilifu, katika tabia na mwenendo, Kwa bahati mbaya kanisa la Mungu katika nyakati za leo tumeacha kukazia mafundisho yetu katika uadilifu kama ilivyokuwa kwa Yesu na Mitume na badala yake kuwaelekeza watu katika maswala mengine!. Pamoja na kuwa agizo la Mungu ni pana sana lakini ni muhimu vile vile tusiache kabisa kurudi katika msingi na kuwakumbusha watu kulenga katika kukua kiroho, kimaadili na mwenendo! Hili ndio kusudi mojawapo kubwa la kuwepo kwa kanisa.

Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”         

Nadhani unaweza kupata picha iliyo wazi kusudi la Kristo kulipa kanisa Mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na walimu ni ili watu wa Mungu wajengwe kwa mafundisho na maelekezo wakue na kukomaa na hatimaye waweze kuwa na tabia na mwenendo na sifa sawa na zile alizokuwa nazo Kristo, hakuna gharama kubwa kama hii ya kutokuwa na wakristo waliokomaa kiroho, wasio na ufahamu wala ujuzi wa neno na wanaoacha kukua kiroho na kiuelewa na kubaki katika udumavu, uchanga na kutokuwa na tabia na mwenendo unaofanana na baba yetu wa Mbinguni, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

*      Maana ya neno ukamilifu

*      Kipimo cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.

Maana ya neno Ukamilifu.

Unapoyachunguza mafundisho ya Yesu na Mitume kuhusu ukamilifu utaweza kuona kuwa kuna jambo walilolokuwa wakililenga zaidi katika mafundisho yao, Kwa kawaida mwanadamu hawezi kuwa mkamilifu kama Mungu, Mungu anatajwa kuwa mkamilifu na muadilifu na kuwa hakuna uovu wowote ndani yake ona:-

Kumbukumbu 32:3-5 “Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili. Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.”

Mwanadamu alikuwa na ukamilifu wa uadilifu, haki na kutokuwa na uovu mara alipoumbwa na Mungu katika bustani ya Edeni na ndio maana alikuwa na uhusiano na Mungu wa karibu kama Baba na Mwana wake, Hata hivyo baada ya anguko la mwanadamu, Mwanadamu alipungukiwa kila eneo  la maisha yake, alipoteza haki, alipungukiwa na uadilifu na kupoteza ushirika na Mungu wa moja kwa moja ona:-

Warumi 3:23 -24 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”

Mwanadamu aliyemuamini Yesu Kristo na kazi yake ya ukombozi iliyofanyika pale Msalabani, kama akifunzwa vyema katika kanisa analokuweko anaweza kuwa mkamilifu katika uadilifu kama alivyo Mungu, ukamilifu huu ambao umetajwa katika maandiko tunaweza kujifunza maana zake kama ifuatavyo:-

Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Neno hilo Nanyi mtakuwa wakamilifu katika maandiko ya kiyunani yanasomeka kama “TELEIOS”  neno hilo linasomeka kama “PERFECT” katika kiingereza, lakini hata hivyo neno hilo halitoshelezi katika kuelezea ukamilifu unaokusudiwa kwa kiyunani neno hilo teleios maana yake ni complete or application of labor growth, mental and moral character  na katika maana nyingine pia ni full of age,  kwa hiyo ukamilifu unaozungumzwa hapo ni kufikia kwenye uwezo wa kujitambua (Maturity), kuacha ujinga, kukomaa kimaadili, na kitabia na kimwenendo  na maandiko yanaonyesha kuwa jambo hili linawezekana kabisa kwa kila mkristo aliyeitwa na Mungu kwa kuokolewa

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Unaweza kuona! kumbe kama mtu ameokolewa na amekuwa mwanafunzi waYesu na kisha bado akawa anaenenda kama kwanza yaani kama ilivyokuwa kabla ya kuokolewa anafanya ujinga, HAJAJITAMBUA, kwa hiyo ni lazima kila mtu aliyeokolewa afunzwe aondoke katika ujinga awe na akili abadilike katika tabia na mwenendo na kuwa na tabia ya uungu, yaani kuwa kama Mungu, unaona utakatifu unaozungumzwa hapo katika waraka wa Petro wayunani  wanautaja kwa kutumia neno HAGIOS  ambalo pia linazungumzia Morally Blemeless  yaani kufikia ngazi ya kutokuwa na lawama kimaadili  na kujiweka wakfu kama wafanyavyo makuhani ona

Waebrania 7:6 “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu;”             

Kwa namna Fulani Mungu anataka wanafunzi wakristo, wakue wakamilike, wakomae, wakue waondoke katika maswala na tabia za kitoto na za kijinga, kutokukua kiroho kunatupelekea kuwa na kanisa yaani watu ambao wameokolewa kwa kumuamini Bwana Yesu lakini wakiwa na tabia mbaya kama tu watu wa kawaida wasiomjua Mungu, watu ambao Hawajajitambua, Paulo mtume anawaita wakristo wa namna hii kama wakristo wenye tabia ya mwilini ona

1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Watu wenye tabia ya mwilini katika kiingereza wanaitwa  “CARNAL”       neno hili la kingereza linalotumika hapo katika kiyunani linatumika neno “SARKIKOS” ambalo maana yake ni tabia za KINYAMA  hii maana yake ni kuwa katika kanisa la Korintho japo wakristo walikuwa wameokoka na kumuamini Yesu kama Bwana na Mwokozi, bado kulikuwa na ukosefu mkubwa wa huduma ya mafundisho ya kichungaji na kitume, kwa msingi huo wakristo wa Korintho japo walibarikiwa sana kuwa na karama za Rohoni lakini vilevile tunaona kuwa kanisa hili lilikuwa limejaa tabia za kinyama  mfano:-

-          Kulikuwa na Mafarakano na ushabiki wa wahubiri wa injili - kama tu ilivyo leo 1Wakorintho 3:4-9 “Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu

 

-          Kulikuwa na husuda na fitina – sio jambo la kushangaza leo katika jumuiya ya Kikristo kuona watu wakiwa wamejaa fitina majungu na mafarakano, wakristo wakisingiziana mambo makubwa ya uongo bila hata kuchomwa mioyo katika dhamiri zao ona 1Wakorintho 3:3 “kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? wakristo katika nyakati za siku hizi wamefikia ujinga wa hata kuchomekeana mambo mabaya, kuuana, kuwekeana sumu au kutumiana watu wasiofaa kitu kufanya mauaji, na kutengeneza keshi na skendo za kuchafuana  sio kiu cha ajabu


-          Kulikuwa  na zinaa za kupita kawaida -  yaani kulikuwa na watu waliozini mpaka na wake za baba zao, yaani zinaa zisizokuweko hata katika mataifa ona 1Wakorintho 5:1-3 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.” Leo hii watu kuzini na wachungaji, wake za wachungaji, wazee wa kanisa na watu wenye sifa katika kanisa limekuwa jambo la kawaida watu wanakula stori za zinaa kama jambo la kawaida tu hofu na hali ya kumcha Mungu imeondoka na neema ya Mungu imechukuliwa kama njia ya kujihurumia katika kuteda dhambi na kuzihalalisha, mwenendo wetu haufanani tena na makusudi ya kuwepo kwa kanisa la kristo duniani

 

-          Watu wasiokubali kuachilia – Katika Kanisa la Kristo kule Korintho na kama ilivyo leo kulikuwaweko watu wasiotaka kupoteza, kila wakati walitaka kuonekana kuwa ni washindi, katika Kristo tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili yake, watu waliokomaa kiroho sio lazima kila kitu washinde, wakati mwingine iko haja ya kuachia na kupoteza Korintho watu walipelekana mahakamani ona 1Wakorintho 6:1-8 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu? Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu.” Je katika siku za leo hujawahi ona watu wakristo wakidhulumiana je hujawahi ona wakristo wakipelekana mahakamani? Wakisingiziana wakitakiana mabaya maswala kama haya yanaweza kutokea tu kama watu hawatatafuta kuwa wakamilifu kama baba wa Mbinguni, niliwahi kumsikia Mkristo mmoja aliyekuwa anahusika na kuajiri watu mahali Fulani akitamka kuwa nitahakikisha huyu kijana (mwajiriwa wake) ananyooka na kukimbia na kurudi kijijini, ni matamshi hatari sana sio ya mwajiri wa kawaida wa dunia hii ni Mkristo akihakikisha kuwa anaharibu maisha ya mtu mpaka mtu huyo akimbie mjini?  Nimewahi kumsikia Mkristo mmoja akipanga njama ya kuharibu kibali cha mtu na akiwa na nia hata ya kusambaza skendo kwa kuhakikisha kuwa anamuandika mtu gazetini ili kumuharibia kibali chake wivu husuda na dhuluma na masingizio leo imekuwa ni tabia ya kawaida ya Wakristo, nataka nikuhakikishie kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na Kanisa la watu walioharibika, waliodumaa kiroho na wasiokua kiroho na kimaadili na wasiojitambua, wanageuka na kuwa wanyama kabisa, Mkristo anadhulumu wenzake na anaendelea kuabudu bila wasiwasi huku akiwatishia wale aliowadhulumu, Wakristo ambao wamedumaa kiroho na kutokukomaa na kukua ni tatizo kubwa sana na linasumbua sana jamii ya Wakristo na makanisa tuliyonayo leo.

 

-          Kuweko kwa wakristo wasio na faida – Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.” Mwandishi wa kitabu cha waebrania anasikitishwa na wakristo walio na miaka mingi kanisani lakini wamedumaa hawakui Kiroho muda mwingi umepita lakini hawawezi kuwa walimu maana yake hawajakua kufikia hata ngazi ya kuweza kuwafundisha na wengine kwa kuhudumu katika kufundisha neno la Mungu lakini pia hata wao wenyewe kushindwa kuwa somo, kuwa kielelezo leo tuna wakristo wana miaka mingi sana katika imani lakini ni wabovu katika kiwango ambacho huwezi kujifunza kitu kutoka kwake, huwezi kuona tofauti yake na watu wa duniani  na wakati mwingine hata wale wa duniani huonekana kuwa wana nafuu, changamoto hii inatokana na kutokujali swala la kuwa wakamilifu katika mwenendo wetu yaani kuwa na tabia ya Kristo!

 

-          Kuwepo kwa karama na miujiza mingi lakini tabia mbaya – Kanisa la korintho lilikuwa ni kanisa lililokuwa na neema ya kuwa na vipawa vingi na karama nyingi na watu wengi sana waliokuwa wakinena kwa lugha lilijaliwa vipawa vingi sana vya rohoni lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi za kimaadili kwa kanisa hilo, unaona Paulo anawafundisha namna bora ya kutumia karama za rohoni lakini vilevile akiwafundiaha njia iliyo bora ambayo ni upendo, kama ilivyokuwa kwao nyakati za leo tuna watu wenye vipawa vingi na Mungu anawatumia sana na watu wanawafuata lakini wana tabia mbaya hakuna uadilifu kuanzia namna wanavyofanya huduma bila adabu, lakini wakiwa na tabia zisizovutia na wakristo wajinga waochukuliwa na mawimbi ya watenda miujiza wakidhani kuwa kila mtenda miujiza ni wa Mungu, Kipimo cha ukomavu wa mtu kiroho sio miujiza bali ukomavu katika uadilifu na upendo, Kristo atawakataa wahubiri wote, na watumishi na manabii ambao kweli kwa jina lake watafanya miujiza na kutoa unabii lakini tabia na mwenendo wao kwa vipimo vyake hauonekani kuwa wenye kufaa.

 

Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

 

Kipimo halisi cha kiroho sio mkutenda miujiza bali kuishi maisha ya utakatifu na kuzaa matunda ya roho, mtu mmoja alisema mnadhani waislamu huenda msikitini kwaajili ya miujiza? Wao huacha maduka yao na biashara zao na kukimbilia katika nyumba za ibada kwaajili ya kusali na kuabudu tu, Wakristo wa leo ni kama wasipoona muujiza kabisa wanadhani kuwa Mungu hayuko mahali hapo Yesu alikisikitishwa na watu ambao hawawezi kumuamini hivihivi tu mpaka ziweko ishara

 

Yohana 4:46-48 “Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?

 

Wakristo wasiokomaa na kukua katika uadilifu na mwenendo hukimbizana huku na huko wakitaka kuona miujiza na ishara hawawezi kumuamini Mungu pasipo miujiza, je unadhani ukuu wa Muhubiri ni miujiza tu hapana! Hatusomi kokote pale ambapo Yohana mbatizaji alifanya muujiza wowote lakini Yesu alimsifika kuwa katika uzao wa mwanamke hakuna aliye mkuu kama Yohana Mbatizaji ona

 

Luka 7:24-28 “Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”

 

-          Watu wanaochukuliwa na upepo wa kila aina ya Elimu – Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KristoNeno la Mungu limemaliza kila kitu kuna upepo wa kila namna wa Elimu na hila za watu na ujanja na njia za udanganyifu hizi zipo, kukosekana kwa Elimu sahihi ya neno la Mungu kumewafanya wakristo wa leo kuchukuliwa na hizi pepo biblia ya NIV inatumia neno “WAVES” yaani neno la Mungu linatambua kuweko kwa mawimbi,  au pepo katika maswala ya neno la Mungu  na kazi zake wakati mwingine hutokea amsho za aina mbalimbali za huduma au watu wengine ni watumishi halisi wa Kristo lakini wengine huangukia katika hayo mawimbi ambayo kimsingi huinuka na kutoweka, kama wakristo hawajaimarishwa vizuri wakabaki wachanga kila wakati  linapotokea wimbi la aina moja utaweza kuona wakristo hao wakristo hao wakiruka na wimbi hili na lile badala ya kukua, kukomaa na kufikia ngazi ya kutumika kwa uaminifu katika eneo lako uliloitiwa. Kwa ujumla tunajifunza na kuona kuwa kuna hasara kubwa sana ya kuwa na wanafunzi wa Bwana Yesu wasiokuwa na moyo wa kutafuta ukamilifu!

 

-          Kubadili neema ya Mungu kuwa ufisadiYuda 1:4 “Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.”

 

Moja ya changamoto kubwa pia inayolifanya kanisa la leo kushindwa kuishi maisha ya ukamilifu ni matumizi mabaya au tafasiri mbaya ya mafundishio kuhusu neema, kupitia mkazo mkubwa na wa kijinga kuhusu neema ya Mungu watu wengi wamejikuta wakiishi maisha ya dhambi na kutokubadilika kwa kisingizio tu kuwa Mungu ametupa neema na tunaishi wakati wa neema, lakini Paulo mtume akifundisha kuhusu Neema ya Mungu aliweka mkazo ulio wazi kuwa neema sio tiketi ya kuishi maisha ya dhambi ona

 

Warumi 6:1 -2 “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? ”  

 

Neema ya Mungu kazi yake ni kuturahisishia kuishi maisha ya haki na utauwa bila kutumia nguvu kama wakati wa sharia, neema inasaidia kuwa kama Kristo alivyo na kama Mungu wa mbinguni alivyo ni neema ya Mungu inayotusaidia kuwa wazuri, wenye maisha ya kiasi na sio kuishi maisha mepesi ya dhambi. Ndani ya neema ya Mungu kuna uweza wa kiungu wa kutuwezesha kuishi maisha ya kumpendeza Mungu  nay a viwango ona

 

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”

 

Unaona neema sahihi inatusaidia kukataa tama na ubaya, kukataa tamaa za kidunia, kutupa uwezo wa kuishi maisha ya kiasi, haki na utauwa katika ulimwengu huu huu, kwa hiyo hakuna neema inayokuelekeza kuishi maisha ya dhambi, lakini kutokana na mafundisho mabaya kuhusu neema kanisa la leo linachukulia dhambi kama jambo poa na lisilo la ajabu. Ni neema ya Mungu ndiyo inayotusaidia kubadilika na kuwa na tabia kama ya baba wa Mbinguni nanyi mtakuwa wakamilifu, ukamilifu huu hauwezekani bila neema sahihi, kama utafundishwa kuwa kuna neema na inakusaidia kuona uko sawa dhambini hiyo itakuwa ni injili nyingine neema ya Mungu itaachilia hukumu ndani yako itakayokuleta katika toba wala sio kuishi dhambini, Moja ya changamoto inayowafanya wanafunzi wa Yesu leo kutokuwa wakamilifu kama baba wa mbinguni ni mafundisho kuhusu neema iliyopitiliza, ambayo inakufanya udumae na sio upokee mabadiliko

                               

-          Kufilisika kiroho  - Kanisa linapopoteza mwelekeo sahihi hususani katika fundisho la kuwa na tabia njema na mwenendo mwema na kuwa wakamilifu na kuishi maisha ya utakatifu na tukakazia maswala mengine  yasiyo na  umuhimu kama kutajirika tunaweza kujikuta kuwa tuna changamoto nyingine mbili, jina la kuwa tajiri, lakini ni masikini yaani kanisa limekuwa na utajiri wa mali za kawaida lakini limekuwa masikini na limepungukiwa na kuwa na umasikini wa tabia za uungu, kanisa lina jina la kuwa hai lakini limekufa  lina mali lakini liko uchi ona

 

Ufunuo 3:1 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.”

 

Ufunuo 3:16-17 “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”  

 

Unaona hali ya kanisa la watu wasiolenga kukamilika hubaki katika kusheherekea mafanikio ya kimwili huku nguvu za rohoni zikiwa zimefilisika, niliwahi kumsikia askofu wa kanisa Fulani msomi mkubwa akinieleza ya kuwa kulikuwa na wachawi kanisani kwake na walikuwa wakikopera sadaka mpaka aliposimama na kuwakemea waache tabia hizo? Ndipo wachawi wakapunguza kukopera sadaka, Kama kweli kanisa la Mungu linaweza kufikia hatua ya kuweza kuwa na wachawi  ndani na wakahudhuria ibada  na wanaamini na kuweza kufikia ngazi ya kukopera sadaka haiingiia akilini kuendelea kufikiri kuwa kanisa lina uhai, afadhali kidogo kama ningesikia kuwa kuna waizi wanaiba sadaka wakati wa kuhesabu na tumewakamata kupitia ccctv Camera kidogo ingeweza kuingia akilini kufikiri hivyo lakini kama zinakoperwa ni wazi kuwa tunahitaji kuwa na uamsho na kuruhusu nguvu za Mungu kutamalaki na kuweka msisitizo mkubwa wa kuweko kwa tabia ya ukamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Bado tunaweza kushuhudia na kuelewa kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kutokulifundisha kanisa kuwa na tabia na mwenendo ulio mkamilifu, tungeweza kuchambua mambo kadhaa wa kadhaa yanayodhihirisha kuwa tunamuhitaji Mungu na tunahitaji kukua kiroho na kuwa wakamilifu lakini nadhani kwa maswala hayo machache umeweza kuona kuwa msisitizo wa kuwa na kanisa lenye ukamilifu kama baba yetu wa mbinguni unahitajika sana katika karne yetu. Sasa ni namna gani tunaweza kujikwamua kutoka katika tatizo hili? Kwanza hatuna budi kujipima kama tunakomaa kiroho, kimaadili na mwenendo.

 

Kipimo cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.

 

1.       Ni jukumu la mtu mmoja mmoja kutamani kuwa mkamilifu kama alivyo baba wa Mbinguni – Neno la Mungu linatuonyesha kuwa tunaweza kuwa wakamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa msingi huo ni vema sasa kila mmoja wetu akawana na shauku ya kuwa kama Kristo ambaye ni kiongozi mkuu wa wokovu wetu na ambaye ametuachia kielelezo tukifuate Mathao 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”

2.       Ni jukumu la kila mmoja kutamani kuuweza mwili wake na hisia zake katika utakatifu 1Wathesalonike 4:3-4 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;”

3.       Ni jukumu la kila mmoja kuwa na Upendo kwa Kristo mwenyewe alisema mkinipenda mtazishika mari zangu Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”

4.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa najijengea upendo wa kupenda maswala ya kiroho yanayochangia ukuaji wa kiroho mfano kujisomea neno la Mungu, kuomba, kusikiliza mahubiri, kuhudhuria ibada, kufunga, kujitoa kwa Mungu na kutimiza agizo kuu

5.       Ni jukumu la kila mmoja kutamani kukaa katika uwepo wa Mungu na kuimarisha uhusiano wako na Yesu Kristo

6.       Kukubali kusamehe na kuachilia au kushindwa na kupoteza haki zetu kwa faida ya ufalme wa Mungu

7.       Kukubali kuwa na maisha ya mfano na kuhubiri kile ambacho sisi wenyewe tunakifanyia kazi 1Wakoritho 11:1 “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.”

8.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa anajaa Roho Mtakatifu na kuwa na maisha yaliyojaa muongozo wa Roho Mtakatifu Waefeso 5:18 -20 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;”

9.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha nya kuwa anakubali maonyo makemeo na marekebisho kutoka kwa watu wanaoaminika kuwa wamekomaa kiroho na kama wameona kuwa kuna jambo sahihi la kukemea katika maisha na mafundisho yetu

10.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kukubali kufundishika na kukiri makosa yetu pale tunapokuwa tumekosea

11.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kutambua na kukubali ya kuwa hatujui kila kitu 1Wakorintho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”      

12.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kujilinda na kiburi na majivuno pamoja na kuchukua utukufu wa Mungu

13.   Kukubali kujifunza kutoka kwa wengine na kutambua huduma na ubora wa wengine katika eneo Fulani la maisha yetu

14.   Kuamini kuwa neno la Mungu ndio mamlaka ya mwisho na ya kuwa hakuna mtu aliyejuu ya neno la Mungu

15.   Kukubali kuitambua na kuelewa na kupambanua ili kuitii na kuifuata sauti halisi ya Roho Mtakatifu na mapenzi ya Mungu

16.   Kuwa na uhusiano ulioshiba na Roho Mtakatifu

Siku hadi siku katika maisha yetu kama tutayatendea kazi maswala kadhaa tunayojifunza hapo juu uwezekano wa kuishi maisha ya ukamilifu na kuwa na tabia alizosema Kristo, uwezo wa kusamehe maadui na kuwaombea, uwezo wa kuvumilia, kuwasalimia hata wale wasiotupenda na kadhalika, hakuna jambo zuri na la kupendeza ni kuwa kama baba yetu wa Mbinguni alivyo.

Rev. Innocent Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Jumatatu, 29 Mei 2023

Jipe moyo; inuka anakuita!


Marko 10:46-50 “Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita.  Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.”


Utangulizi:

Moja ya stori zenye mvuto mkubwa sana katika maandiko ya neno la Mungu (Biblia) ni pamoja na stori ya kuponywa kwa kipofu Batimayo, Katika stori hii kuna mambo mazuri sana ya msingi yakujifunza lakini kwa bahati mbaya wakati mwingine tunakosa kuyagundua mambo hayo, kuna kitu kikubwa na cha ziada cha kujifunza katika mwenendo mzima wa stori hii ukiacha uponyaji wenyewe! Lakini kuna mambo ya msingi ambayo Kristo anatufundisha kupitia tukio hili, kipofu mwenyewe na jamii ya watu waliokuwa wana mzunguka na kisha tutaweza kujiona sisi wenyewe tunapokuwa katika uhitaji, tabia ya uungu katika kushughulika na changamoto zetu na tabia ya watu wakati wa changamoto zetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na macho ya rohoni tunapojifunza somo hili katika jina la Yesu Kristo amen!, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

*      Dhana potofu wakati wa changamoto!

*      Tabia ya Mungu wakati wa changamoto

*      Mambo ya kujifunza kutoka kwa Batimayo 

Dhana potofu wakati wa changamoto!

Stori ya uponyaji wa kipofu Batrimayo inaenda pamoja na ukweli kuwa mwandishi alikusudia chini ya uwongozi wa Roho Mtakatifu kutufungua macho, ili hatimaye tuweze kuona moja ya changamoto iliyojengeka katika jamii ya watu wanayoyajua maandiko kama ilivyokuwa kwa wayahudi dhana hii iko hata leo, hii ni ile dhana ya kufikiri kuwa kila changamoto inayomtokea mtu katika maisha yake imesababishwa na dhambi, katika kipindi cha muujiza huu kulikuwa na dhana potofu miongoni mwa wayahudi ya kuwa watu wenye changamoto kama hii ya kipofu Batrimayo labda huenda imesababishwa na dhambi, aidha ya mtu mwenyewe au wazazi wake kwa hiyo analipia, hivyo mtu kama Batrimayo licha ya kuwa na tatizo la upofu lakini vilevile alikuwa amekataliwa na jamii kwa kufikiri ya kuwa anastahili kubaki katika hali kama hiyo kwa vile yeye au wazazi wake wanalipia hali anayoipitia ona

Yohana 9:1-3 “Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.”

Unaona? Ni ukweli ulio wazi kitheolojia kuwa dhambi ina changamoto zake inazoweza kusababisha majanga katika maisha yetu, lakini ni muhimu kuweka uwiano kuwa sio kila changamoto inaweza kuwa na uhusiano na dhambi, hapo wanafunzi pamoja na jamii walihesabu watu waliokuwa vipofu walikuwa na laana Fulani au malipo Fulani kutokana na dhambi walizozifanya, sio hivyo tu hata kulipotokea majanga ya asili yaliyosababisha tatizo katika jamii Fulani haraka sana ilifikiriwa kuwa huenda ni kwaajili ya dhambi nyingi huku wale walio salama wakidhani wako sawa na Mungu ona mfano

Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.  Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.  Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”

Unaweza kuona! majanga yanapotokea na kuwapata watu haimaanishi kuwa wale waliopatwa na majanga ni waovu kuliko wale waliokuwa salama dhana hii Yesu alikuwa akiifundisha na kuwaelekeza watu kuwa wanapaswa kumzalia bwana matunda na kuacha kufikiri kuwa changamoto wanazozipitia watu wengine zimetokana na dhambi, Yesu alionyesha kuwa hitaji la toba ni hitaji la kila mmoja na hitaji la kuzaa matunda ni la kila mmoja na hivyo majanga yanaweza yasiwe na uhusiano wa moja kwa moja na hali ya dhambi au kiroho cha mtu husika

Ni katika dhana hiyo hiyo tunaona kuna jambo ambalo lilijitokeza hali kadhalika wakati wa uponyaji wa kipofu Batimayo wakati kipofu huyu alipokuwa anamuita Yesu na ikaonekana kana kwamba Yesu anapita au kama hajali makutano waliokuwa wakifikiri vibaya waliona kuwa Kipofu huyo anatakiwa kupambana na hali yake na kuwa hapaswi kumsumbua Yesu wala Yesu hajali hali yake, Maandiko yanatutaarifu kuwa wakati Yesu anapita na kipofu huyu anapaaza sauti yake kumuita makutano walimweleza wazi kwa kumkemea anyamaze ni kama walikuwa wanamwambia acha usumbufu wako, Yesu hawezi kushughulika na watu kama wewe pambana na hali yako ona

Marko 10:46-48a “Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze,…..

Unaona kutokana na dhana ya kufikiri kuwa watu wenye ulemavu na changamoto mbalimbali na hata walio na magonjwa ni kama wanaadhibiwa na Mungu kwaajili ya dhambi zao au za wazazi wao au babu zao na kadhalika kwa hiyo maandiko yanaonyesha kuwa wengi wakamkemea acha kelele zako, acha ujinga acha usumbufu hana mpango na wewe pambana na hali yako katika lugha ya kiingereza tunaweza kusema hivi “A BLIND BEGGAR WAS HUSHED BY THE CROWD” ni kama sio kunyamazishwa tu bali kunyamazishwa kwa ukali,kunyamazishwa kwa kunyanyaswa, ni ili unyamaze, ukae kimya usisumbue, uache fujo tulia, shiiiiii, funga domo lako, nyamaza! Katika hali moja ama nyingine katika maisha yetu inawezekana tumewahi kunyamazishwa katika namna ya ukali kama ilivyotokea kwa kipofu Batrimayo, unaonywa kuto kudai chochote kunyamaza na kulazimika kupitia au kipitishwa katika hali ambayo watu wanataka, ni katika hali kama hiyo Batimayo alikuwa anakutana na kipingamizi kikubwa cha kubakizwa katika hali ileile na jamii, hawataki asonge mbele wanaona kama wale walio na miguu na macho wao ndio wanaostahili, kuendelea mbele na Yesu na sio watu hovyo na wenye kutupwa na kudharaulika kama kipofu Batrimayo!  Jambo moja kubwa la msingi ni kuwa yeye aliendelea kupaza Sauti akimuita Yesu! Akihitaji rehema zake !

Tabia ya Mungu wakati wa changamoto!

Ni muhimu kufahamu kuwa katika mchakato mzima wa uponyaji wa Batimayo Yesu alionekana kama anapita na ni kutokana na hali hii nadhani hata makutano waliomkemea Batimayo walikuwa wanadhani kuwa hata Yesu hakuwa anajali hali aliyokuwa anaipitia kipofu, Yesu ni mwana wa Mungu kufikiri ya kuwa Yesu hangemjali Batimayo ni kufikiri vibaya, kufikiri kuwa Mungu hatujali ni fikra mbaya, ambayo iko kinyume na ukweli kuhusu wema wa Mungu, wakati tunapoliitia jina lake na kuhitaji rehema zake na kuona kama amekawia kuitikia na kudhani kuwa hajishughulishi tena na mambo yetu ni dhana isiyofaa kitu kabisa; Mungu ni mwema wakati wote maandiko yanatuthibitishia wazi ya kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu ona

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

Tofauti na mawazo ya Mwanadamu Yesu alikuwa anapita huku anamwazia mema kipofu Batrimayo, kimsingi hata kupita njia ile ilikuwa ni maalumu sana kwa Batimayo wala sio kwaajili ya umati uliokuwa unamfuata, Ni huyu kipofu ndiye aliyekuwa amelengwa na Yesu siku ile kwanini unawezaje kujua ? Yesu alisimama na alisimama maalumu kwaajili ya huyu mtu mtu dhaifu, aliyekataliwa katika jamii na kudharauliwa masikini asiye na msaada, Yesu alimjua alijua historia yake alifahamu mahitaji yake kamwe hangeweza kumpita, wale watu kimsingi ndio waliokuwa vipofu hawakuweza kujua imani ya Batrimayo wala hawakuweza kujua namna Mungu anavyoshughulika na mahitaji ya watu wake.  Mungu ana njia zake na namna yake jambo jema hapa ni kuwa watu hawakumlaumu Yesu kama wakati alipokuwa amelala katika boti ambapo wanafunzi walimlaumu kuwa Mwalimu si kitu kwako kuwa tunaangamia? Na ni tofauti kiasi na alivyokuwa akishughulika na mwanamke aliyekuwa akitoka na damu kwa kumgusa katika upindo, wanafunzi walimshanga kuwa tunazungukwa na umati mkubwa je si rahisi kwako kuguswa rabbi? Hapa Yesu alisimama na kuamuru kuwa mwiteni! kuna kitu kimejificha hapa kwenye neno YESU AKASIMAMA katika lugha ya kiyunani kusimama kwa Yesu nenola kiyunani linalotumika ni  HISTEMI  ambalo ni neno lililovutwaa kutoka kwenye neno la kiyunani STAO  katika lugha nzuri ya kuelewa kusimama kwa Yesu hapa neno la kiingereza linaloweza kutumika hapa ni ESTABLISH STAND STILL, kwa hiyo neno STAO ni sawa na neno STAND na neno HISTEMI ndio ESTABLISH STAND STILL  kwa hiyo kwa Kiswahili kizuri ni kuwa YESU AKATAFUTA MAHALI PAZURI PANAPOFAA KUSIMAMA, hivyo kimsingi sio kuwa Yesu alikuwa amekusudia kumpita Batimayo lakini Yesu alikuwa anatafuta mazingira mazuri ya kusimama na kipofu ili aweze kumuhudumia vizuri, Haleluya!  Mwandishi maarufu wa karne za mwanzoni mwa kanisa Mtakatifu Jerome anaeleza kuwa Mazingira ya Yeriko ni yenye miamba na mawe ambayo yangeweza kusababisha kujikwaa au kuanguka  hivyo ni kweli kuwa Yesu alikuwa anaangalia mazingira mazuri ya kusimama na mtu asiyeona ili waweze kuzungumza vizuri  na kwa kufanya hivi alikuwa akiitimiza sharia ya Musa katika

Walawi 19:14 “Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.”

Unaona wakati Mungu anaandaa mazingira mazuri ya kushughulika na mtu huyu duni mwenye imani na utambuzi mkubwa kuwa Yesu ni mwana wa Daudi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa Batimayo alikuwa ameamini kuwa Yesu ni Masihi, Unadhani Yesu angemuachaje?  Yanenaje maandiko? na kila amwaminiye hatatahayarika!  katika wakati huo tayari watu wameshapata dhambi kwa kufikiri kuwa (Yesu) Mungu alikuwa hamjali na wala hakuwa na mpango naye, au kusaidia kumnyamazisha Batrimayo.  Mungu alikuwa anaandaa mazingira, acha kuimba usinipite mwokozi, yeye huwa hampiti Mtu mwenye uhitaji na anayemuamini na watu wanyamaze kimya wakati Bwana anashughulika na watu wake maana unaweza kujikuta unatengeneza dhambi wakati Kristo anaandaa mazingira mazuri ya kusema na mtu wake, kwa muda sahihi na mahali sahihi ili akutane na mahitaji yake, watu wale wale waliokuwa wakimkemea na kumwambia nyamaza ni hao hao waliomwambia changamka jipe moyo inuka anakuita, Kwa kawaida kuna watu wengi sana vipofu walioponywa na Yesu lakini hawakutajwa kwa majina yao Huyu alikuwa anatupa somo muhimu sana ndio maana anatajwa kwa jina lake alimuamini Yesu kuwa ni Masihi, Yesu alitengeneza mazingira ya kuzungumza na mtu huyu muhimu kwake kuliko wote wakati wao walikuwa wakimuona hana maana hana faida, Yesu aliwafunga mdomo nao wakamwambia jipe moyo inuka anakuita haleluya ! Yesu ni Mungu mwenye moyo wa ajabu na huruma sana! Anajali, alimjali.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Batimayo

Kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika muujiza huu yako mengi, habari hii inatufunza mengi kwanza wako marafiki au watu ambao sio wazuri kwetu na wasiotutakia mema wanataka tusifanikiwe na tubaki katika hali ile ile tuliyo nayo, watatusaidia kutoa majibu ambayo wala sio majibu ya Mungu,  wanatuzuia kwenda kwenye mwelekeo sahihi wakijua wazi kabisa kuwa ndio mwelekeo wa mafanikio yetu, je unadhani watu wale walikuwa hawajui kuwa Yesu anaponya vipofu? Unadhani walikuwa hawajui kuwa Yesu ameponya vipofu wengi sana? Na je unadhani walikuwa hawaoni ya kuwa Batrimayo ni Kipofu na unadhani walikuwa hawajui kuwa siku ile ilikuwa siku nzuri sana kwa Batrimayo kuponywa kwa vile Yesu alikuwa Yeriko siku ile?  Kumbuka watu ni wale wale ambao tunapolia wanatuambia nyamaza,  ashukuriwe Mungu na aendelee kuwatunza kwani Mungu atageuza mambo hao hao waliokuwa wakikuambia nyamaza ndio watakaokuja kusema jipe moyo inuka anakuita ! Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Batrimayo!

Usikubali mtu yeyote akunyamazishe au akuhesabu kuwa wewe ni wa kutupwa wakati Yesu Kristo amekuja kwaajili yako. Batrimayo ashukuriwe Mungu hakuwajali watu wanamwambia nini yeye aliendelea kumtazama Yesu tu na kulilia Rehema kutoka kwa Masihi mwana wa Mungu!

Uhusiano wako na Yesu ni wa tofauti haufannani na wa mwingine wengine wanafikiria kuwa hakujali! wewe endelea kumtazama kama mwenye kujali na utangundua kuwa kumbe yuko kwaajili yako

Linapokuja swala la wewe na maisha yako na Mungu usiangalie umati unasemaje, Mungu haabudiwi kwa mkumbo uwe na msimamo wako wa kipekee kuhusu Mungu, Batrimayo kwake Yesu ni mwana wa Daudi nani pekee mwenye kutoa rehema

Watumishi wa Mungu ni lazima waandae mazingira mazuri kwaajili ya huduma za uponyaji, nguo za kuwafunika wanaoangushwa na mapepo, wahudumu watakaosaidia kuwahifadhi wanaodondoshwa, mazingira yatakayosaidia kutunza usafi wao na kadhalika Yesu hakutaka Batrimayo ajikwae kwenye mawe alitafuta mazingira mazuri.

Mungu habadiliki, yeye ni yule yule jana, leo na hata milele, yeye ndiye mwenye kipimo cha wema wetu, matendo yetu yawe sawa na kile anachotuelekeza yeye na sio kwenye dhana za watu na yale wanayoyafikiri, wakatim Batrimayo akiwa katika changamoto hii ni ukweli ulio wazi kuwa walioelewana Lugha pale alikuwa Yesu mwenyewe na Batrimayo wengine walitoka kappa, ninapopita katika mapito ninayoyapitia na hali yoyote ile ninayoipitia anayeweza kunielewa vizuri mi Mungu na mimi ninayeipitia ile hali ninyi wengine kaa kimya msininyamazishe ninapomtafuta Bwana wangu, msininyamazishe ninapopiga kelele wala Mungu wangu hanipiti anaaandaa mazingira salama na ya utulivu nipige naye stori nimueleze ninayo yahitaji ana rehema hataniacha yatima hali hii baadaye utakuja kugundua kuwa kumbe mimi na Yesu tunaelewana vizuri sana kuliko umati huu.  Yawezekana unapitia katika changamoto kadhaa wa kadha na unadhani Yesu amekupita au hakujali na watu wanapata nafasi ya kukudhihaki wanatamani ubakie katika hali hiyo hiyo, hawataki ukutane na Yesu akusaidie nataka nikuambie wewe endelea kupiga kelele na kumwambia mwana wa Daudi unirehemu, ususeme usinipite mwokozi kwani yeye hapiti mtu anayemwangalia na kumlilia Rehema zake naye ataandaa mazingira na watu wale wale wanaosema nyamaza watapiga kelele Jipe moyo inuka anakuita! haleluyaa

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Jumapili, 28 Mei 2023

Usiende bila uwezo utokao juu!


Luka 24:46-49 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”



Utangulizi:

Ni muhimu kwa kila mmoja kuwa na ufahamu, ya kwamba uhai wa kanisa unategemeana sana na jinsi au namna Kanisa linavyompa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nasi, Endapo kanisa litaendelea na kazi zake za kutimiza agizo kuu bila kutoa nafasi kwa mwenye kanisa yaani Roho Mtakatifu, itakuwa ni rahisi sana kanisa kupoteza nguvu zake na kubaki na hekima ya kibinadamu, jambo ambalo linaweza kutuletea aibu na kushindwa vibaya, ni kwa kuzingatia hilo leo katika siku ya Pentekoste ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujikumbusha tena umuhimu wa kumpa nafasi Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja nasi vinginevyo au kinyume chake usiende bila Roho Mtakatifu au uwezo utokao juu!.

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-

*      Agizo la kwenda kuihubiri injili

*      Agizo la kutokwenda bila uwezo utokao juu      

Agizo la kwenda kuihubiri injili.

Moja ya agizo muhimu sana na ambalo ndio msingi wa uwepo wa Kanisa duniani ni kuihubiri injili, Yesu Kristo aliwandaa wanafunzi wake kwa muda wa kutosha ili hatimaye aweze kuwatuma kwenda kuihubiri injili

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea.  Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

Unaona kusudi kubwa na Yesu Kristo kuwaita mitume au wanafunzi wake ni ili awafundishe waweze kuwa pamoja naye wakae katika uwepo wake kisha baada ya hayo aweze kuwatuma kwenda kuihubiri injili, haya ndio makusudi makubwa zaidi ya uwepo wa kanisa, kila kanisa linawajibu wa kuihubiri injili, kuhubiri injili ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa watu wote ndio mapenzi ya Mungu, kanisa lisilo hubiri injili ni kanisa lisilo na utii kwa kazi ya Kristo ni kanisa linalozimika katika moto wa injili, nachelea kusema ni kanisa lililokufa; lakini ni wazi kuwa litakuwa ni kanisa lililopoteza mwelekeo, ni lazima tuihubiri injili, ni lazima tuwafikie watu wa mataifa yote na vile vile na kuwafungua kutoka katika nguvu za giza yaani vifungo vya shetani na kutoa pepo wachafu kwa wanaoonewa nao,

Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Agizo hili kubwa ni la muhimu sana watu waokolewe na kufunguliwa kutoka katika nguvu za giza ili wahamishiwe kwenye ufalme wa mwana wa pendo lake, kila kanisa na kila mtu anayetambua umuhimu wa agizo hili kuu anapaswa kulitii na kuhakikisha kuwa linafanyiwa kazi na hayo ndio mapenzi ya Mungu. Kuna changamoto kiasi Fulani katika kanisa la leo, ya kuwa watu wengine wamejikita sana katika kuwafungua watu bila kuhakikisha kuwa watu hao wanatubu dhambi zao na kumwamini Bwana Yesu, mambo haya yanahitaji uwiano, lakini kubwa zaidi tunapolitimiza agizo kuu Bwana mwenyewe atakuwepo kulithibitisha neno kwa ishara na miujiza, hivyo miujiza iwe ni sehemu tu ya kuthibitishwa kwa neno na sio biashara ya kuponywa tu kwa miili ya watu hao ili hali nafsi na roho zao zingali kifungoni, ni muhimu sana kuihubiri injili sawa na agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na hayo ndio mapenzi ya Mungu      

Agizo la kutokwenda bila uwezo utokao juu.

Pamoja na umuhimu mkubwa wa agizo hili kuu na msisitizo wake ni muhimu sana tukatilia maanani kuwa ndani ya agizo kuu Yesu mwenyewe vilevile alisisitiza wanafunzi wake wasiende bila kuvikwa uwezo utokao juu! Ona

Luka 24:46-49  Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

Uwezo huo utokao juu ni nini na unapatikanaje? uwezo huu utokao juu ni matokeo ya nguvu za Mungu kuwa juu ya wale waliomuamini Bwana Yesu na waliotayari kulitimiza agizo kuu, uwezo huu unapatikana baada ya Roho Mtakatifu kuja juu yetu ona

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Kwa nini Yesu Kristo alisisitiza kwamba wanafunzi wake wasiende bila uwezo huo kutoka juu yaani Bila kupokea nguvu kutoka kwa Mungu Roho Mtakatifu? Sababu kubwa mojawapo ni kuwa kazi ya kuihubiri injili ina upinzani, ina upinzani wa aina mbalimbali, kutoka kwa watu, dini zao, tamaduni zao, serikali zao na miungu yao na nguvu za giza, hivyo kuna nguvu za upinzani ambazo ni ngumu kuzikabili katika hali ya kawaida ya kibinadamu bila neema na msaada wa Mungu, kujaribu kufanya kazi za injili na hata kukemea pepo bila kuwa na nguvu za kukabiliana na mapepo hayo na upinzani huo ni hatari sana na rahisi kujikuta unakata tamaa na kuingia katika kuabishwa na upinzani wa kishetani, hatuwezi kuigiza kwa kuwa shetani anaogopa wazi nguvu ya Mungu na anajua watu wanaotumiwa na Mungu na wale wanaoigiza!

Matendo 19:11-20 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Unaona kutoka katika kifungu hiki cha maandiko tunaona mambo makubwa mawili, watu waliojaribu kukemea mapepo kwa jina la Yesu huku wakiwa hawajavikwa uwezo ule utokao juu, wala hata kuokoka!  na matokeo yake walipigwa na kujeruhiwa vibaya kwa sababu hawakuwa na nguvu wala mamlaka ya kutoa Pepo, lakini Paulo mtume alitumiwa na Mungu kwa miujiza Mingi na zaidi sana hata watu waliotumia uganga walibadilika na kuchoma moto vitabu vyao vya uchawi vyenye gharama kubwa sana, Paulo mtume hakufanya haya kwa nguvu zake, alijaa Roho Mtakatifu alitumiwa na Mungu, ikiwa kanisa linataka kuona nguvu za Mungu ni lazima tutii agizo kuu lakini wakati huo huo tusiende bila uwezo utokao juu, yaani bila nguvu za Mungu Roho Mtakatifu ndani yetu!

Mungu hajawahi kumtuma mtu katika kazi fulani bila nguvu zake, nguvu za Roho wake Mtakatifu zinamuwezesha mtu huyo kukabiliana na upinzani kutoka kwa maadui wa injili, alipomtuma Musa dhidi ya Farao, kwa kusudi la kuwaokoa wana wa Israel katika nchi ya Misri, alimpa nguvu za kupambana na serikali ile iliyokuwa ikitumainia miungu na nguvu za giza zilizoongozwa na wachawi maarufu walioitwa Yane na Yambre ambao kimsingi walishindana na Musa na Haruni kwa kufanya kiujiza ya kuigiza ona 

2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”

Unaona hawa walikuwa wachawi wakuu wa serikali pinzani ya Farao ambayo ilijawa na kuabudu miungu na kutegemea uganga na uchawi, Musa na Haruni na wazee wa Israel wangewezaje kudai uhuru katika serikali ya aina ile bila Nguvu za Mungu?  Hatuwezi kuwasaidia watu bila nguvu ya Mungu izidiyo nguvu zote!

Kutoka 7:20-22 “Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena.”

Mwinjilisti Filipo alipokwenda kuihubiri injili katika eneo la Samaria alikutana na mtu aliyekuwa mchawi na aliyekuwa na nguvu za giza ambazo watu wengi waliamini ni uweza wa Mungu, mtu huyu aliiamini injili na kubatizwa lakini bado alikuwa na moyo wa kichawi mpaka alipokuja kushughulikiwa na Roho Mtakatifu wakati Petro na Yohana walipokwenda kutoa msaada wa kihuduma kule Samaria, ni hatari sana kama kanisa litafanya kazi chini ya kiwango cha nguvu za Mungu zinazohitajika na ndio maana leo kuna shuhuda za kuwepo kwa wachawi makanisani wakiingia na kutoka na kujifanyia uchawi wao na kanisa linaogopa tunawezaje kukabiliana na haya usiende bila uwezo utokao juu, lazima tujae ngvu za Roho Mtakatifu katika kiwango cha kufurika ona :-

Matendo 8:5-21 “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.”

Nadhani sasa unaweza kumuelewa Bwana Yesu kwanini alisisitiza usiende bila kuvikwa uwezo utokao juu, upinzani wowote katika injili unaweza kuzimwa endapo tu tutamruhusu Roho Mtakatifu Mungu kuwa pamoja nasi katika kazi hii, sio tu katika nguvu za giza pekee bali hata kuitetea imani na kukubali kuwa mashahidi na kufa kwaajili ya Kristo bila nguvu hizo ni vigumu kustahimili hata majaribu na upinzani dhidi ya injili na watumishi wa kweli ona

Matendo 6: 8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

Katika kila kazi ambayo Mungu anampa mtu na au kumtuma mtu anampa nguvu hizo za Roho Mtakatifu ili kukabiliana na upinzani wake Samsoni aliitwa kuwa mwamuzi dhidi ya wafilisti waliokuwa wakiwaonea Waisraeli wakati huo hakuenda Samsoni bila uwezo huo utokao juu  Nguvu za Mungu zlimfanya samsoni kuwa wa kipekee ona

 Waamuzi 15:14-16 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.”

Vilevile Mungu alipomuinua Eliya dhidi ya manabii wa baali Mungu alimpa Eliya uwezo utokao juu ulioweza kudhihirisha nguvu za Mungu aliye hai na kuwafanya watu waliokuwa wanasita sita kumgeukia Mungu na kurejea kwake 1Wafalme 18:21-40, Pia Paulo mtume alikutana na Elima yule mchawi kule Cyprus Matendo 13:6-12 na Daniel aliweza kuonekana kuwa mwenye majibu katika serikali ya Nebukadreza na Belshaza kuliko wanajimu na wachawi kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yake

Kwa hiyo unaweza kuona ni hatari na aibu kubwa kwenda bila uwezo utokao juu, kanisa tunapaswa kumuomba Mungu wakati wote na kuhakikisha kuwa wakati wote tunajaa nguvu za Mungu, kwaajili ya usalama wetu, na kwaajili ya kuthibitisha uwepo wa Mungu na kukabiliana na nguvu za kipinzani, Roho Mtakatifu ni ahadi ya Mungu, ahahdi za Mungu zimehakikishwa, na Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake, yeye huliangalia neno lake ili aweze kulitimiza ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa kama kuna jambo la Muhimu la kuliombea ni kujaa Roho Mtakatifu, Nguvu hizi ndio silaha yetu ya ushindi wakati wa upinzani, kazi ya Mungu ina vita katika ulimwengu wa roho, ziko protoko za kipepo zinazoshindana na injili na watenda kazi wote kwa hiyo ni muhimu kukumbuka  na kumkumbusha Mungu atupe neema hii tusiende bila uwezo utokao juu, nguvu hii ni moja ya silaha muhimu katika vita zetu za rohoni!

2Wakorintho 10:3-4 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

Unaona iko vita katika ulimwengu wa roho, haionekani katika macho ya kawaida lakini wakati mwingine hujitokeza katika ulimwengu wa mwili asili ya kila kitu ni rohoni, hivyo lazima tuwe hodari katika Bwana na katika uwezo wa nguvu zake kwa kuvaa silaha zote mojawapo ikiwa nimkusali katika Roho, tunawezaje kufanya hivyo lazima tuwe pia tumevikwa uwezo kutoka juu ona

Waefeso 6:10-18 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.  Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

Usiende bila uwezo utokao juu, wanafunzi wa Yesu walimuelewa Bwana na walikaa katika maombi katika chumba cha juu pale Yerusalem wakafunga na kuomba kwa siku kumi, siku ya 50 Pentekoste Roho Mtakatifu alikuja juu yao na kuwafanya kuwa na ujasiri, watu ambao awali walikuwa wakijifungia kwa hofu ya wayahudi, sasa walikuwa tayari kukabiliana na kila aina ya upinzani wakivikwa ujasiri na wakaipeleka injili kwa ujasiri bila kujali mazingira magumu waliyokutana nayo. Injili hiiambayo kanisa limeipokea duniani kote hata leo, ilitokana na kanisa la kwanza kuzingatia sana swala zima kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu, endapo tutafuata nyao zao kanisa halitakuwa na kitu cha kupoteza! Injili itawafikiwa watu, maisha ya watu yatabadilishwa na hakutakuwa na utata kwa miujiza inayofanywa chini ya utendaji wa Mungu mwenyewe, ukomavu wa wakristo na watumishi wa Mungu utaonekana na matunda ya Roho Mtakatifu yataonekana katika maisha yetu ya kila siku! Asante kwa kufuatilia mafundisho yangu uongezewe neema kumbuka usiende bila uwezo utokao juu!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Siri katika Ukuta wa kulia Machozi


1Nyakati 7:12-16 “Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.  Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.”

 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna eneo muhimu sana duniani kwaajili ya maombi kama mahali paitwapo ukuta wa kulia machozi The wailing wall au ukuta wa Mashariki The Western wall, Mahali hapa ni mahali ambapo pana siri kubwa sana ya mafanikio ya kiroho kwa mujibu wa biblia na moja ya siri kubwa sana ya mahali hapa ni pamoja na kujibiwa maombi, Maelefu ya Wayahudi na viongozi wengi wakubwa Duniani, kwa karne nyingi  wamekuwa wakipatembelea mahali hapa kwaajili ya Maombi, Ukuta uliitwa jina ukuta wa Machozi kwa sababu wayahudi hufika mahali hapa na kulia au kuomboleza kwaajili ya kukumbuka kubomolewa kwa Hekalu lililokuwa limesimama mahali hapa, Lakini pia huomba mahali hapa kwaajili ya kumsihi Mungu kwaajili ya ujio wa Masihi, wengine huandika maombi yao katika vikaratasi na kuyachomeka katika nyufa za ukuta huo ili Mungu aweze kuyakumbuka maombi yao daima!. Leo tutachukua Muda kuangalia siri iliyoko katika ukuta huu wa kulia machozi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Historia fupi ya Ukuta wa kulia Machozi

·         Siri ya Ukuta wa kulia Machozi

·         Kila mtu anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi

 

Historia ya Ukuta wa kulia Machozi.

Ukuta wa kulia machozi ni sehemu ya ukuta uliojengwa na Mfalme Herode, Mnamo karne ya Kwanza kwa makusudi ya kuzingira na kutunza eneo la Mlima Moriah ili kwamba eneo la juu yake lipate kujengwa Hekalu lililokuwako Yerusalem, wote tunafahamu ya kuwa Hekalu la Yerusalem liliharibiwa mnamo mwaka wa 70 baada ya Kristo na kuwa mpaka sasa halikuwahi kujengwa tena!, Wayahudi wamekuwa wakihofia kukwea moja kwa moja kwenye eneo hilo kwa kuogopa kumkosea Mungu, na badala yake sasa wamegundua kuwa wanaweza kufanya maombi katika eneo la ukuta huo ambao ulikuwa ni msingi au ukingo wa lililokuwa hekalu ilikuwa ngumu kulipata eneo hilo kwa uhuru zaidi mpaka mara baada ya vita ya siku dita iliyopiganwa mwaka 1967 na kuwapa uhuru mpana wa kupafikia mahali hapo, na tangu wakati huo ndio ilipatikana uwezo usioweza kutikisiaka wa kupatumia mahali hapo Muhimu kwa maombi duniani. 


Siri ya ukuta wa kulia Machozi

Kwa mujibu wa maandiko Mlima wa Hekalu ni mahali muhimu sana ambapo Hekalu la Kwanza la Suleimani lilijengwa na kisha Hekalu la pili ni mahali penye kutazamwa sana na Mungu kwa Mujibu wa Maandiko, Hivyo ukuta wa kulia machozi ni sehemu ya Hekalu lililokuwepo ni msingi, eneo hili kibiblia lina ahadi za ajabu sana,  watu wa Mungu wakiomba katika eneo hilo lazima Mungu atasikia na kufanya:- 


 2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 


Mungu pia ameahidi kuwa macho yake na masikio yake yatafunguka kuelekea maombi yatatakayotolewa kutoka katika mahali hapo  ona 


2Nyakati 7:15-16 “Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.” 


Mahali hapo kama vile tu ilivyokuwepo Nyumba ya Mungu maandiko yameashiria kuwa Mungu ataliweka jina lake mahali hapo milele, eneo hili ni la Wayahudi na lilinunuliwa kwa fedha na Mfalme Daudi ili aweze kutoa dhabihu mahali hapo kwa sababu malaika wa Bwana alisimamisha upanga wake mahali hapo ili asiwaangamize watu ona 


2Samuel 24:18-25 “Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu. Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie Bwana madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama Bwana alivyoamuru. Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi. Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee Bwana madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.  Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni, vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea Bwana, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi Bwana aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.” 


Historia ya mahali hapo inaonekana wazi katika kifungu hicho hapo juu, kwamba ukiacha historia ya kimaandiko, kuwa ni mahali ambapo Mungu alimuamuru Ibrahim akamtoe Isaka kama sadaka katika Mlima Moriah lakini pia unaweza kuona kuwa Daudi alikuja kupanunua kwa kusudi la kumjengea Mungu madhabahu sawa na maelekezo ya kiungu, aidha eneo hili ambalo baadaye Suleimani alijenga Hekalu, na pia Daniel alipokuwa mbali utumwani huko Babeli hata pamoja na kutokuweko kwa hekalu alifungua madirisha ya chumba chake kuelekea mahali hapa kwaajili ya dua na maombi yake yaliyompa mafanikio ona 


Daniel 6:10 “Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.” 


Daniel kupiga magoti na kuelekeza maombi yake katika mji wa Yerusalem miaka mingi hata kabla ya kuweko eneo hili, ni wazi kuwa hakuwa anaelekea Yerusalem peke yake bali mahali hapa muhimu ambapo leo ndio uko ukuta huo wa kulia Machozi kumbuka Daniel alikuwa akifanya hayo wakati Hekalu lilikuwa limebomolewa na Mfalme Nebukadreza, Daniel alifanya hivyo kwa imanina maelekezo ya kimaandiko yaliyoko katika 


1Wafalme 8:35-36 “Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa; basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao.” 


Unaona kumbuka neno wakiomba wakikabili mahali hapa, hii maana yake kama mtunanapana neema ya kufika Yerusalem anaweza kwenda kwenye eneo hili la ukuta wa kulia machozi na kuomba, lakini kama uko nchi ya mbali unaweza kuomba kuelekea eneo hili, hii iko wazi kimaandiko, nafahamu kuwa Yesu ni zaidi ya hekalu, na kuwa maombi yanapaswa kupelekwa kwa Mungu baba kupitia jina la Yesu, lakini hata hivyo ukweli wa kimaandiko unabaki wazi kuwa Mungu alipachagua mahali pale katika ardhi ile aapaweke jina lake mahali hapo hivyo maombi kuelekea mahali hapo bado yanalipa, mtu mmoja alisema unapopata nafasi ya kwenda kuomba mahali hapo usiende na maombi mepesi na ya kawaida bali mazito na ukiwa na imani kubwa kuwa Mungu atayaelekea maombi yako, kutokana na siri hii watu wengi na viongozi wengi wakubwa duniani wamewahi kufika na kufanya maombi katika ukuta wa kulia machozi. 


Kila mtu anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi

Kwanini mahali hapa pana mvuto mkubwa sana kwa watu wa aina mbalimbali, na watu maarufu wa aina mbalimbali na wanasiasa na watu kadhaa wa kadhaa hufika mahali hapa ni kwa sababu mahali hapa ni kwaajili ya watu wote na sio Israel Peke yao, wakati Mfalme Suleimani alipokuwa akiweka wakfu mahali hapa, alimuomba Mungu kwaajili ya waisrael na vilevile kwaajili ya wageni ambao watasikia habari za jina la Bwana Mungu wa Israel na kutoka mbali nao wakihitaji kuomba kuelekea katika nyumba ya Mungu au eneo husika basi Mungu awajibu na kuwasikia mpia ona 


2Nyakati 6:32-33 “Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako.”


Kifungu hicho cha maandiko kinafungua mlango, kwa kila mtu ambaye sio myahudi anaweza kwenda kuomba katika ukuta wa kulia machozi, kwa kusudi la kumtafuta Mungu na kumcha Mungu, na uzuri wake ni kuwa dua hii ya mfalme Suleimani dua nyake na maombi yake yote yalikubaliwa na Mungu, ni kwaajili ya siri hizi watu wengi wamekuwa wakienda Yerusalem kwa ziara mbalimbali wakipata nafasi hawakosi kufika katika ukuta huu na kufanya dua zao na maombi yao na Mungu anajibu maombi, na utafurahia ahadi zote za Mungu ambazo nyingi ya hizo chanzo chake ni hapa

 

Rev. Innocent Mkombozi Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Jumatatu, 8 Mei 2023

Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa!


Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?



Utangulizi

Leo tutachukua muda kwa kutosha kujifunza na kuchambua kwa kina maneno yaliyozungumzwa na Paulo Mtume dhidi ya Kuhani mkuu waliyekuwako wakati huo kama tulivyoweza kuona katika mstari wa msingi

Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Katika tafakari yetu leo kuhusu kifungu hiki cha maandiko tunajifunza somo hili KUPIGWA KWA UKUTA ULIOPAKWA CHOKAA Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Agizo la kutenda haki

·         Paulo hakutendewa haki

·         Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa

Agizo la Kutenda haki

Mojawapo ya maagizo ya Mungu kwa mtu awaye yote mwenye mamlaka, ni kuhakikisha kuwa anatenda haki, kila ngazi ya mamlaka duniani ni ngazi ya maamuzi, kwa msingi huo ni muhimu kwa kila mmoja mwenye mamlaka kuhakikisha kuwa anatenda haki, Kutokutenda haki ni kinyume na mapenzi ya Mungu, Mungu aliagiza watu wasitende yasiyo haki katika hukumu ona

Mambo ya walawi 19:15 “Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki

Mungu ndiye hakimu wetu mkuu atakayemuhukumu kila mmoja sawa na kutenda kwake na hivyo ni muhimu kwetu tunapokuwa katika ngazi za maamuzi kutenda haki au kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kufanya upendeleo tukikumbuka kuwa Mungu ndiye mtoa sheria na ndiye mwenye kuhukumu, hivyo kila aliye kwenye ngazi ya maamuzi na ajiangalie.

Yakobo 4:12Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?

Na ndio maana maandiko yanatuonya kwamba tujihadhari na hukumu kwa kuwa nasi tutahukumiwa, na kujihadhari na kipimo kile tukipimacho kwani kipimo kilekile tupimacho ndicho tutakachopimiwa,  Mungu ndiye Muhukumu wa ulimwengu mzima na kwake ni lazima atatenda haki na kuisimamia na kuhakikisha kuwa inakuja kufanyiwa malipizo kwa namna yoyote (Karma)

 Mwanzo 18:25 “Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki?

Ulikuwa ni utambuzi kamili wa Ibrahimu kuwa Mungu wa Mbinguni Mungu wake ana sifa kadhaa wa kadhaa lakini mojawapo yeye ni Muhukumu wa Ulimwengu ni Jaji mkuu nani mwenye haki hivyo alimsihi Mungu kutenda haki wakati anapotaka kuangamiza watu wote katika miji ya Sodoma na Gomora ya kwamba kwa vyovyote hataangamiza watu wema pamoja na waovu, Tabia hii ya uungu ya kutenda haki inapaswa kuwa na kila kiongozi aliyeko katika nafasi ya kufanya maamuzi duniani kwamba ni lazima atende haki, kutenda haki huambatana na Baraka kubwa sana.

Lakini kutokutenda haki ni hatari sana Katika imani ya Kiislamu, Kitabu chao Quran kina Sura maalumu inayoitwa Al – Qariah  maana yake hukumu au mizani, mkazio wake ni kuhukumu kwa haki au kutenda usawa kama inavyofanya mizani, Katika kitabu cha Mithali, Maandiko yanaonya kuhusu Mizani ya hadaa ikiwa na maana ya kutokutenda haki ni chukizo kwa Mungu ona

Mithali 11:1 “Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.”

Kwa msingi huo maandiko yanatukumbusha hapa umuhimu wa kutenda, haki na kuhukumu kwa haki, na kufanya mambo sawasawa na Mapenzi ya Mungu na kutokuwahukumu wenzetu katika namna isiyo sahihi

Paulo hakutendewa Haki!

Matendo 23:1-3 “Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Mahakama ya kitahudi ambayo huongozwa na kuhani mkuu ikiwa na wataalamu wapatao 70  ambayo ilijulikana kama baraza la wazee (Sanhedrin) ilikuwa imeketi kusikiliza mashauri ya Paulo mtume yaliyoletwa kwa hila na masingizio ya wayahudi, wakati Paulo anapewa nafasi ya kujitetea alianza kwa kuonyesha wazi kuwa ameishi kwa dhamiri safi maana yake yeye hana hatia hata sasa, Neno hilo likiwa kinywani mwa Paulo alipokuwa akianza utetezi wake mara moja hatujui ni kwa chuki au kwa dhamiri gani Kuhani mkuu Anania hakufurahishwa na neno hilo akaamuru waliosimama karibu naye wampige mara moja makofi katika kinywa chake, kwa kitendo hiki Paulo alimwambia Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa, kwa sababu ameketi katika kiti cha hukumu ili ahukumu sawa na sharia lakini anaamuru apigwe kinyume cha Sheria, haki haikutendeka mahali hapo! Paulo kwa ujasiri mkubwa na ushuhuda kuwa anaifanya kazi ya injili sawasawa na wito wake katika Kristo kwa hiyo kimsingi hakuwa na hatia zaidi ya upofu uliokuweko katika baraza ka wazee wa kiyahudi kuhusu mtazamo wao kinyume na injili ya Bwana Yesu! Paulo hakutendewa haki ni kutokana na  na jambo hili Paulo mtume alijua wazi kuwa Mungu atasimama  na kumtetea bila kujali kuwa Anania alikuwa kuhani mkuu andiko linasema hivi

Zaburi 12:5 “Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.”

Kama haki haipatikani mahali ambapo haki inatakiwa ipatikane maana yeke mahali hapo hapana ustaarabu na yanayofanyika hayana tofauti na yanayofanywa na wanyama, Mwanadamu anapaswa kuwa kiumbe kilicho staarabika na kama hakuna ustaarabu maana yake hakuna tofauti na ulimwengu wa wanyama Mungu anataka haki itendeke

Muhubiri 3:16 “Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu. Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi. Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.”

Muhubiri 4:1 “Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”

Dhuluma inapotendeka na haki inapopotoshwa Mungu hataweza kutulia ataingilia kati na kuileta hukumu kwa haraka kama ilivyosema Zaburi 12:5 kwa hiyo ni muhimu kufuatilia na kuona kuwa haki inatendeka katika jamii, Je swala la kumpiga kofi mtume Paulo mdomoni ili asijitetee na  na asiendelee kusema kuwa hana hatia je ni swala dogo? Mbele za Mungu haikuwa jambo jema na hata mbele za Paulo mwenyewe na ndio maana Paulo aliamua kumuachoa Mungu na kumhakikishai kuhani mkuu kuwa Mungu Atampiga! Je kuhani mkuu alipigwa  na Mungu kama Paulo alivyosema?

Kupigwa kwa ukuta uliopakwa chokaa!

Kabla ya kuangalia kama Kuhani mkuu alipigwa na Mungu au la jambo la kwanza ni jina alilopewa na Paulo mtume kwa kuitwa ukuta uliopakwa chokaa! Hii ilikuwa na maana gani, kwa kawaida usemi huu hauna tofauti na ule usemi wa Yesu Kristo alipokuwa akiwakemea Mafarisayo kutokana na tabia zao za kinafiki aliwaita makaburi yaliyopakwa chokaa

Mathayo 23:27-28 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”

Unaona mwanadamu awaye yote anayeketi katika kiti cha hukumu na kuhukumu wengine wakati nay eye mwenyewe akiwa sio mkamilifu, ana dhambi tena chafu kuliko za wale anaowahukumu huyo ni ukuta uliopakwa chokaa ni kaburi ambalo limepakwa chokaa kwa nje linaonekana kuwa jema lakini kwa ndani limejaa mifupa ya wafu, ukuta uliopakwa chokaa ni wa watu ambao ndani ni waovu wana hatia, lakini hawatendi haki, wanajidai haki lakini ni wanafiki wakubwa! Paulo alimkemea kuhani mkuu kwa tabia ya kinafiki ya kuamuru apigwe kinyume cha Sheria wakiwa katika mahakama ya kiyahudi kwaajili ya kutafuta haki lakini pamoja na hayo alitabiri kuwa Mungu atampiga kuhani mkuu je hili lilitimia?

Kwa mujibu wa Historia Mwana historia Mashuhuri aitwaye A.C Harvey anamuelezea Ananias kuwa alikuwa mtu Jeuri sana, mwenye kiburi, mroho mwenye uchu, akiamua ameamua na mwenye utawala wa kiimla maneno anayotumia kumueleza katika ikiingereza ni a Violent, Haughty, gluttonous and rapacious man. Japo alikubalika kwa wayahudi,kwa maelekezo hayo na kwa vyovyote vile mtu huyu hakuwa na wema ndani yake, Mungu alimpiga kwa maelezo ya Mwanahistoria mashuhuri wa kiyahudi wa karne ya Kwanza alitwaye Flavious Josephus , Annania alijihusisha na uasi dhidi ya serikali ya kirumi na kushutumiwa vikali na gavana wa Syria alishitakiwa huko Roma na kupelekwa kwa Kaisari Claudius kati ya mwaka wa 52 baada ya Kristo, Claudius alimuongeza muda wa kuendelea na ukuhani mpaka mwaka wa 58, akiwa kibaraka mkubwa wa warumi, alikamatwa na kuuawa na wayahudi wenye msimamo mkali mwanzoni mwa vita kati ya wayahudi na warumi, Na hivyo kutimizwa kwa maneno ya Mtume Paulo kuwa Bwana atakupiga ukuta uliopakwa chokaa, Mungu hatawaqacha watu wake hususani watumishi wake waonewe, haki tasimama hata kama hao wanaoonea watumishi wa Mungu ni wenye mamlaka ya kifalme au la Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Furaha ya Bwana ni nguvu zetu !


Nehemia 8:9-11 “Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike.”




Utangulizi:

Ni muhimu kujikumbusha wazi Kwamba Mwanadamu katika maumbile yake ni kiumbe chenye Hisia, “Human being is Emotional being” Na kwa sababu ya kuumbwa tukiwa na hisia wakati mwingine tunaweza kukutana na kupanda au kushuka kwa hisia zetu katika maisha ya kila siku, kuna wakati tunaweza kupenda na kuna wakati tunaweza kuchukia, wakati mwingine tunaweza kuwa na furaha na wakati mwingine tunaweza kuwa na huzuni, wakati mwingine kujiamini na wakati mwingine wasiwasi, wakati mwingine ujasiri wakati mwingine hofu, hii ni hali ya kawaida ya maumbile ya mwanadamu, Hisia zetu zinatusaidia kukabiliana na mazingira yetu, kama tutakuwa na siku nzuri tunaweza kuwa na furaha na kama siku hiyo inaweza kuwa mbaya tunaweza kuwa na fadhaa, timu tunazoshabikia zikipata ushindi tunaitikia kwa kufurahi, timu tunazoshabikia zikishindwa tunaitikiwa kwa kuwa na huzuni, tunapopata zawadi za kushitukizwa tunafurahi, tunapopata habari za huzuni, tunahuzunika, ni Muhimu kufahamu kuwa sio mapenzi ya Mungu kuwahuzunisha watu wake ona

Maombolezo 3:31-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha

Tutajifunza somo hili FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 

·         Maana ya  Neno Furaha

·         Mafundisho ya Neno la Mungu kuhusu Furaha

·         Furaha ya Bwana ni nguvu zenu.

Maana ya neno Furaha

Neno Furaha katika Biblia ya kiingereza linasomeka kama JOY na tafasiri ya neno JOY katika kamusi ya kiingereza JOY – “The climax of Great pleasure and happiness”, or Feeling great pleasure and happiness, Katika Lugha ya kibiblia inayotumika katika uhusiano na neno hilo, Kwa Kiibrania ni “CHEDVAH” ambalo tafasiri yake ni Gladness au rejoicing  - a state of well – being, and contentment  katika kiyunani ni “CHARA” ni hali ya kuwa na furaha, na kuona kuwa mambo yako vizuri na kuridhika kuwa hakuna wasiwasi hata kama Mazingira hayaonyeshi kuwa hivyo, Ni uwezo wa kushinda mazingira ya kuhuzunisha na kuonyesha ukomavu hata kama mazingira hayo hayaonyeshi au kutia moyo kufurahi.

Mafundisho ya neno la Mungu kuhusu Furaha

Kama tulivyoona maana ya neno furaha hapo juu, Neno la Mungu linatufundisha kuwa furaha hii sio furaha ya kawaida furaha hii inaitwa furaha ya Bwana

Nehemia 8:10Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”

Ukiifahamu furaha hii nakuhakikishia kuwa maisha yako hayatakuwa kama yalivyo na hasa kama tutahakikisha kuwa tunatembea katika furaha hiyo siku zote za maisha yetu! Furaha hii inatokana na Mungu mwenyewe ona

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

Kwa mujibu wa maandiko furaha hii haitokani na hisia zetu, Furaha hii ni tunda la Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kila siku, Ni furaha inayotoka kwa Mungu mwenyewe, ni furaha kutoka kwa Roho Mtakatifu, furaha hii ikiwa ndani ya Mtu huwa haijalishi mazingira yakoje, Furaha hii inaangalia mbele ya mapingamizi, haikufanyi kuchoka wala haikufanyi uzimie moyo ona

Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”         

Furaha hii sio inayotokana na hisia ni furaha inayotokana na karama ya Mungu kwa watu wake inaambatana na uwezo mkubwa sana wa kuvumilia na kukufanya uwe wa kawaida katika mazingira yoyote

Warumi 5:3-5 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.”

Kuna utamu Fulani kama utasoma kifungu hiki katika lugha ya kiingereza kwa wale wanaokifahamu kidogo ona

Romans 5:3-5 “Not only so, but we also rejoice in our Sufferings, because we know that suffering produces perseverance, Perseverance character and character hope and hope does not disappoint us because, God has poured out his love into our hearts by the Holy Spirit whom he has given us

Unaona kwa hiyo ni furaha inayotokana na upendo wa Mungu uliomiminwa kwetu na Roho Mtakatifu, hivyo hata wakati wa mateso utawezxa kuona bado furaha hiyo inatawala na haiondolewi na chochote kwa sababu inatazama mbele ya mateso ambako kuna utuklufu mkubwa !

Furaha hiyo sio ya muda, sio ya hisia haitokanani na hali ya mazingira kwamba leo nimepata au nimekosa wala haiwi sawa na ya waliovuna mashamba na zabibu  wala ya maadui zetu ambayo hiyo ni ya kitambo tu , Furaha hii inatoka kwa Bwana na inazidi furaha ya kawaida ona

Zaburi 4:7-8 “Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.”

Furaha ya Bwana ni Nguvu zetu !

Baada ya kuwa tumeona maana ya Furaha na jinsi maandiko yanavyoielezea furaha hiyo sasa turudi katika Mistari ya msingi kwa nini Nehemia anasema furaha ya Bwana ni Nguvu yenu?

  Nehemia 8:9-11 “Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike.”

Israel walikuwa wamepelekwa katika utumwa kihistoria na utumwa huo haukuwa mzuri, wanakumbuka historia chungu ya utumwa wao, na sasa Mungu alikuwa amewapa neema ya kurejea katika nchi yao, na chini ya Zerubabeli walikuwa wamelijenga tena Hekalu, na chini ya Nehemia walikuwa wameujenga ukuta wa Yerusalem na  Nehemia akiungana na Ezra, Ezra aliwasomea watu Torati na kuwakumbusha maneno yote ya Mungu, na hivyo Israel waligundua kuwa walikuwa kinyume na maagizo ya Mungu walikuwa wamekengeuka walisahau maagizo ya Bwana hivyo walipoyasikia maneno ya tarati walilia sana na kuhuzunika, walilia machozi, walijihukumu kuwa huenda wamemkose Mungu na labda walitaka kuomboleza  badala ya kulia na kuomboleza Nehemia aliwaambia hapana hakuna sababu ya kulia na kuomboleza badala yake  walitakiwa kufurahia na kuchinja vitu vinono na kufanya sikukuu unaona :-

Nehemia 8:10-12 “Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.”

Kwa kawaida watu wanapokuwa katika huzuni wanafunga na kuomba, wanalia, wanagalagala kwenye majivu na kuvaa magunia, hii ndio ilikuwa nia ya watu, walidhani kuwa kila wakati wanapaswa kuomboleza, unapogundua kuwa umekosea sio kila wakati unapaswa kulia na kuhuzunika na kuomboleza na kufunga na kuomba, unapopita katika magumu sio kila wakati unapaswa kutumia njia ileile  wakati mwingine unachohitaji ni kupiga kelele za shangwe ni kufurahi ni kujisamehe ni kumuachia Mungu atende kazi yake, kile kitendo tu cha kujua kuwa umekosea ni tayari kazi ya Roho Mtakatifu imefanyika ndani mwako wakati mwingine nenda kachinje ule ufurahi kafanye sikukuu! Adui yetu shetani anataka kuona tunalia tu wakati wote anatarajia tuwe katika taharuki tu lakini iko siri mwamini Mungu ya kuwa atakupa siku yenye furaha kila aunapoamka asubihi usiitarajie siku yako wiki yako mwezi wako mwaka wako kuwa mbaya wewe mwambie Mungu aachilie ile karama yake na tunda lake la furaha hilo linatosha sana kutuweka huru

Zaburi 118:24 “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.”

Nisikilize kama Nehemia aliweza kugundua katika nyakati za agano la kale kwamba badala ya watu kulia, badala ya kuhuzunika, badaya ya kufunga na kuomba na kuvaa magunia na kujipaka majivu, Basi wanaweza kutumia silaha ya kufurahia kula pamoja kugawa vyakula kutoa kwa niaba kwaajili ya wengine kwa sababu fuaraha ya Bwana itawapa nguvu, Ni furaha kutioka kwa Roho wake Mtakatifu, kwa hiyo katika changamoto zozote unazozipitia usiangalie mazingira wewe furahi,  Mungu anatupenda kiasi kwamba alimtoa Yesu kufa msalabani kwa niaba yetu, kwa hiyo sio mwakati wetu tena kubeba mateso, ni wakati wetu kufurahi, Hakuna wa kutukwaza,

Hitimisho !

Unawezaje kuwa na furaha ya Bwana katika maisha yako?

-          Hakikisha kuwa unawapoa watu vitu, Matendo 20:35 “Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.” Kutoa kwa kawaida huwa kunaleta furaha, Ne heri kutoa kuliko kupokea, katika andiko la Msingi Nehemia aliwaambia watu wakatioe wawape wakle ambao hawana kitu ili watu wafurahie pamoja kumbe katika kutoa utaweza kuona furaha ya Bwana ndani yako!

-          Kaa katika uwepo wa Mungu 1Nyakati 16:27 “Heshima na adhama ziko mbele zake; Nguvu na furaha zipo mahali pake.”

-          Jawa na wingi wa shukurani, Msifu Mungu  Zaburi 43:4 “Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu.”

-          Uwe mtu wa ibada na kumujua Mungu Zaburi 122:1 “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana”.

Furaha ya bwana ni Nguvu zetu kwa sababu inatupa amani ya kweli ambayo huwezi kuipata katika mitandao ya kijamii, huwezi kuipata kwa fedha, huwezi kuipata kwa marafiki, kwa kwenda pikiniki, kwa kufanya ngono, kwa kula madawa ya kulevya, kwa kunywa pombe, kwa kucheza disco hayo yanaweza kukupa furaha ya muda lakini iliyojawa na majuto, Furaha ya kweli unaweza kuipata ndani ya Yes utu!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!