Ijumaa, 7 Agosti 2026

HUDUMA KATIKA MAKANISA YA NYUMBANI


Matendo 2:46-47 “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.”




Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za kanisa la kwanza licha ya kuwa walikuwa wakikutana hekaluni kuabudu lakini pia walikuwa na tabia ya kukutana na kuabudu nyumba kwa nyumba, jambo hili lilichangia kwa kiasi kikubwa washirika kuwa na uwezo wa kutambuana kushirikiana na kutiana moyo lakini pia makanisa ya nyumbani yalichochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kanisa mama, Ukiacha hilo pia wahudumu wenye huduma ya kichungaji, watenda kazi, Wanafunzi na wenye hekima wanapata nafasi ya kutumia vipawa vyao, na kujifunza kivitendo, malezi ya kanisa na kutengeneza njia rahisi ya kufungua matawi ya kanisa katika sehemu zingine za mji wetu, tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa huduma ya makanisa ya nyumbani ni mpango wa Mungu wa ukuaji wa kiroho, kihuduma na kiidadi, lakini ni moyo wa kutengeneza umoja na ushirikiano wa karibu kwa huduma ya kichungaji.

Warumi 16:3-4. “Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.”

Ukiichunguza Biblia utaweza kuona kuwa nyakati za karne ya kwanza wakati kanisa linaanza watenda kazi walikuwa na makanisa nyumbani, kwa hiyo huduma katika makanisa ya nyumbani halikuwa swala geni au lisilo la kibiblia, na huduma hizi za makanisa ya nyumbani zimeonyesha mafanikio makubwa sana katika maeneo mengi duniani ikiwemo Afrika na Asia  na sehemu nyingine duniani, lakini pia makanisa ya nyumbani yameonyesha mafanikio makubwa katika maeneo ambayo injili inapigwa marufuku, leo basi tutachukua muda kujifunza somo hili Huduma katika makanisa ya nyumbani kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

  • Maana ya makanisa ya nyumbani
  • Huduma katika makanisa ya nyumbani
  • Faida ya huduma katika makanisa ya nyumbani               

 

Maana ya makanisa ya nyumbani

Makanisa ya nyumbani au kanisa la nyumbani ni mkusanyiko mdogo wa washirika wa Kanisa la mahali pamoja au katika mji mmoja ambao wanakusanyika katika mitaa yao, katika nyumba mojawapo ya mtenda kazi au mtu aliyejitoa kutoa nyumba yake kwa ajili ya  ibada, kwa kusudi la kukusanyika pamoja kwa ibada katika siku mojawapo ya juma inayokubalika kwaajili ya kufanya ibada za pamoja, kuomba pamoja, kujifunza neno la Mungu, kuumega mkate na kushirikiana na kujuana hali kwa ukaribu na kwa pamoja, makanisa ya nyumbani yanaweza kukutana katika sebule ya mshirika mmojawapo na yakiwa na uwezo wa kuwa na wanachama kuanzia 6-10 au 10-30 kulingana  na uwezo wa sebule au mahali pa kuabudia wanakokutana washirika hao, Makanisa ya nyumbani sio mbadala wa kanisa mama hata kidogo lakini ni vikundi vidogo vidogo vinavyoundwa na watu kwa kusudi la kulifanya kanisa mama kuendelea kuwa na nguvu na kukua katika upendo na ushirika, makanisa haya yanasaidia sana kuleta umoja wa kweli Maandiko yanaonyesha kuwa kulikuwa na makanisa ya namna hii nyakati za mitume:-

Kanisa katika nyumba ya Prisila na Akila – Warumi 16:3-4 “Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.”

1Wakorintho 16:19-20 “Makanisa ya Asia wawasalimu. Akila na Priska wawasalimu sana katika Bwana, pamoja na kanisa lililoko ndani ya nyumba yao. Ndugu wote wawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.”

Nimfa pia anatajwa kuwa alikuwa na kanisa la Nyumbani huko Kolosai – Wakolosai 4:14-15 “Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu.Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake.”

Pia rafiki wa Paulo Mtume aitwaye Philemoni – Philemoni 1:1-3. “Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo              

Huduma katika makanisa ya nyumbani

Huduma katika makanisa ya nyumbani zinaendeshwa na watendakazi, wanafunzi pamoja na wenye hekima ambao wamepitia mafunzo mbalimbali katika kanisa letu, hawa sasa wanawajibika kuyahudumia makanisa hayo katika makazi karibu na mitaani kwao wanakokaa washirika, Neno la Mungu linaonyesha kuwa huduma za kiroho, maombezi, kuongoza watu katika wokovu, na kuwajenga watu zinaweza kufanyika pia katika nyumba za watu kwa taratibu maalumu, Yesu alithamini pia shughuli za kuwahudumia watu nyumba kwa nyumba ukiacha kuwa alikuwa akihitajika na umati mkubwa wa watu.

Marko 1:29-34 “Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni.Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.”

Luka 19:5-9 “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.”

Luka 10:38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

Tunajifunza hapo kutoka kwa Mwalimu mkuu Yesu Kristo kwamba nyumbani ni mahali ambapo huduma zote zinaweza kufanyika bila shaka yoyote uwepo wa Mungu unakuwepo popote walipo wawili au watatu ambao wamekusanyika kwa jina lake

Mathayo 18:18-20 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

Hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa huduma ya makanisa ya nyumbani ni sehemu ndogo tu ya ushirika mkuu na kwa sababu hiyo kuhudhuria katika hekalu kuu hakuwezi kupoteza maana sawa tu na kuhudhuria katika masinagogi hakukuwahi kuondoa maana ya kwenda Hekaluni, wala kuacha kuhudhuria ibada za muhimu katika kanisa letu, tunajifunza pia kuwa Paulo alihudumu katika kanisa kuu na makanisa ya nyumbani huku akitembelea nyumba kwa nyumba na kuwahudumia hii ilileta mafanikio na ufanisi mkubwa nyakati za kanisa la kwanza:-

Matendo 20:17-21 “Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa.Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.”

Kwa hiyo tunaweza kufundisha, kuomba, kuabudu, kuuliza maswali, kutambuana na  kuhubiri injili, na watu wakaokoka, na kujenga umoja wenye nguvu huku tukifahamiana sana kuliko katika kanisa kubwa na mpango huu ni mahususi sana endapo kanisa mama linalenga kuwa kanisa kubwa lenye kusanyiko kubwa la watu maelfu kwa maelfu

Faida ya huduma katika makanisa ya nyumbani

Kanisa la nyumbani lina faida kubwa sana endapo kanisa mama lina malengo ya kuwa kanisa kubwa lenye nwaamini maelfu kwa maelfu yaani Mega Church, Kanisa linapokuwa kubwa bila kuwa na makanisa ya nyumbani kunakuwa na ugumu wa kutambuana, kuangalia changamoto wanazokutana nazo waamini wetu, kukosa msaada wa karibu anapokuwa mtaani ambako hajui kama kuna wenzake wa karibu wanaishi huko, lakini pia kama mtu ana vipawa na karama ambazo kwa hizo Mungu yu amtumia ni vigumu kutambulika na kutumika bila mfumo wa makanisa ya nyumbani kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa kanisa letu kuwa na mfumo huu wa makanisa ya nyumbani, pamoja na faida lukuki zinazoweza kutolewa na kanisa la nyumbani hapa tunaweza kuona faida kadhaa :-

  1. Makanisa ya nyumbani husaidia kukua kiroho – Kanisa la nyumbani linaleta utulivu na nafasi ambayo kila mmoja hutambulika lakini sio hivyo tu mtu anaweza kupata nafasi ya kuuliza maswali, kueleza  changamoto anazokuta anazo na kupata mtenda kazi wa karibu na eneo lake ambaye anaweza kumsaidia katika kujifunza na kukua kiroho kwa hiyo kanisa la nyumbani ni njia bora zaidi ya kuangaliana sisi kwa sisi katika mazingira yote

 

Waebrania 10:24-25 “tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia

 

  1. Makanisa ya nyumbani yanatoa huduma ya ushirika wa kweli – hakuna mahali ambapo watu watafahamiana kwa ukaribu kama katika ushirika wa makanisa ya nyumbani, watabebeana mizigo kama makanisa ya nyumbani, watashirikiana katika shida na furaha kama kanisa la nyumbani kwa ujumla ule upendo wa kweli katika Kristo tunaweza kuonyeshana  kwa uhalisia katika makanisa ya nyumbani, wakati kanisa kubwa linainua hisia zetu ni kanisa la nyumbani ndilo linaloleta mapinduzi makubwa ya kiroho, na kiushirika.

 

Matendo 2:41-42 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.”

 

  1. Makanisa ya nyumbani yanahusika kwa ukaribu na huduma ya kichungaji – kama mshirika anapitia changamoto za aina mbalimbali mchungaji kiongozi hawezi kujua bila taarifa za wale walio karibu naye ikiwa ni pamoja na kiongozi wa kanisa la nyumbani ambaye ni mtenda kazi pamoja na Mchungaji wetu, Kanisa la nyumbani ni rahisi kumtambua kila mtu, ni rahisi kutambua mtu anayepitia changamoto ni rahisi kumuombea mtu ni rahisi kujua mtu anaye lega lega katika Imani na ni sehemu ambayo hakuna mtu anasahaulika wala kupotea  na ni rahisi kufuatiliwa  na kurejezwa katika Imani

 

Wagalatia 6:1-2 “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”

 

  1. Makanisa ya nyumbani ni nyenzo ya uinjilisti rahisi – Ni vigumu wakati mwingine kumualika mtu katika kanisa mama na akakubali hasa kama hajawahi kuingia katika makanisa ya watu wanaohubiri wokovu, lakini ni rahisi mtu kualikika katika makanisa ya nyumbani anajisikia salama maana ni sebule ya mtu na ni kwa watu anaowajua, ni rahisi kualika majirani, na wakafika hawaogopi kuliko inavyokuwa katika majengo ya makanisa makubwa na kwa njia hiyo ni rahisi kumuhubiri injili na pia kutoa mwaliko wa kuja katika kanisa kubwa huduma za kiroho zaidi.

 

Matendo 5:42 “Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.”

  1. Makanisa ya nyumbani ni nyenzo ya kulea viongozi – wakati mwingine kutokana na programu ambazo zinaendelea katika kanisa kubwa kuna uwezekano wa kushindwa kuwapa watu wengine madhabahu, au kupatikana kwa uhaba, lakini makanisa ya nyumbani kwa sababu ni kundi dogo linaweza kumshirikisha kila mtu na zaidi ya yote viongozi wetu waliopata nafasi ya kupitia shule mbalimbali ya  za kihuduma wanapata nafasi ya kuhudumu na kuombea watu na kuchunga kanisa dogo na kulikuza jambo ambalo linaweza kuwarahisishia uanzishaji wa makanisa wanapokuwa wameitwa katika wito maalumu, Ni katika kanisa la nyumbani viongozi hujifunza kivitendo, karama zinagunduliwa, wachungaji wajao wanabainika, walimu wazuri wanabainika, wainjilisti wazuri wanabainika na watendakazi wapya wanabainika

 

2Timotheo 2:1-2 “Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu. Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

 

  1. Makanisa ya nyumbani ni nyenzo ya kupanuka kwa kanisa – Kanisa hutawanyika kwa haraka kutokana na kuweko kwa makanisa ya nyumbani kama eneo la kanisa kubwa liko mbali sana na sehemu fulani ni kupitia makanisa ya nyumbani tunaweza kuanzisha tawi lingine bila kuhitaji gharama kubwa za kukodisha jengo, aidha makanisa ya nyumbani hayawezi kuzuiliwa na mateso au upinzani, katika nchi nyingi ambazo injili inapingwa makanisa ya nyumbani imekuwa ni njia ya siri ya kulifanya kanisa kuendelea mbele. Makanisa ya nyumbani yametumiwa na watumishi wengi wa Mungu katika huduma zao na kusababisha ukuaji na upoanukaji mkubwa wa kanisa mama hivyo makanisa haya ni nyenzo ya ukuaji wa Kanisa kubwa kiroho, kiidadi, kijiografia na kadhalika  

 

Matendo 6:5-7 “Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.”

 

Matendo 8:1-4 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.”

 

-          Kanisa la The Church of Pentecost huko Ghana – ni moja ya kanisa kubwa sana miongoni mwa madhehebu ya kipentekoste wana mfumo wa makanisa ya nyumbani “cell system” zaidi ya maelfu  na kutokana na watendakazi kuyasimamia makanisa hayo kwa uaminifu kanisa limeweza kuwa na washirika karibu milioni tatu na likatumia makanisa ya nyumbani kuzalisha makanisa 99 katika nchi nyingine na sehemu mbalimbali za Afrika magharibi

 

-          Kanisa la The works and Mission Baptiost Church – Ni moja ya makanisa makubwa sana nchini Ivory Coast kanisa hili linaongozwa na Askofu Dion Robert kanisa lake lina mfumi wa makanisa ya nyumbani  ambayo yamesababisha mfumuko mkubwa wa ukuaji wa kanisa  kanisa lina cell Groups makanisa ya nyumbani 18,000,. 14,000 ya watu wazima na 4,000 ya watoto kupitia mfumo huo kanisa la Bishop Dion sasa lina washirika 150,000 katika ibada moja wakutanano kuabudu

 

-          Christian Rivival Church – Ni kanisa kubwa na linalokua kwa kasi lililoko Afrika ya kusinikanisa hili mlina mfumo wa makanisa ya nyumbani yanayounganisha watu  na majirani, kanisa hili lina maelfu ya makanisa ya nyumbani na linaongezeka kwa kasi

 

-          Lighthouse Chapel International – Ni kanisa kubwa linaoongezeka kwa kazi lina wanafunzi wanaohusika kusimamia makanisa ya nyumbani likitumia mfumo ule ule uliokuwa unatumiwa na mitume nyakati za kanisa la kwanza

 

-          Living Faith Church Woldwide (Winners Chapel, Nigeria) – ni Kanisa lenye watu 50,000 wanaoabudu mahali pamoja pale kwenye makao makuu yao wao wanatumia mfumo wa makanisa ya nyumbani yanayosimamiwa na watenda kazi, kanisa hili kwa sasa lina waamini zaidi ya milioni sita duniani

 

-          Deeper life Bible church Nigeria  - lina waamini wapoatao 65,000 wanaoabudu katika ibada moja, lakini siri mojawapo ya mafanikio yao ni mfumo wa makanisa ya nyumbani yenye viongozi mahiri na walimaanisha

 

-          Full Gospel Bible Fellowship -  Ni moja ya Kanisa la kipekee la kipentekoste lililoanzishwa nchini Tanzania na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe, ukiacha makanisa haya kuenea nchi nzima kanisa kuu lililoko Sam Nunjoma pale Mwenge Dar es Salaam linaundwa na makanisa ya nyumbani zaidi ya 600 yaliyoenea kila mahali katika mji wa Dar es Salaam, viongozi wa makanisa ya nyumbani wana mafundisho maalumu ambayo huyatoa kwa pamoja kila mahali katika mtaa husika na viongzi hao wenye utii wa hali ya juu hutoa taarifa ya kazi wanayoifanya kwa viongozi wao na kwa mchungaji kiongozi, Makanisa hayo ya meunda umoja imara na kulifanya kanisa kuu kuwa imara, aidha zinapofungishwa ndoa kwa wingi makanisa hayo hujishughulisha au kuhusika kwa kiwango Fulani katika usimamizi wa wanandoa hao kuanzia safari zao za uchumba  na kadhalika, makanisa haya pia huusika na matukio ya misiba mazishi na mengineyo

 

Kama tunataka makanisa yetu yakue na kuwa na washirika wengi sana basi ni nashauri tujiandae na mfumo huu maalumu utakaosaidia kufikisha huduma kwa ufasaha katika jamii, na kulifanya kanisa kuwa nyenzo rahisi na inayoweza kuwafikia watu kwa njia nyepesi, tusikusanye sadaka yoyote katika makanisa ya nyumbani, hii itasaidia kuwaondolea kongwa washirika lakini pia itakuokoa na majaribu ya kifedha kama kiongozi wa makanisa ya nyumbani kutokuwa na muda wa kutoa hesabu ya mapato na matumizi, makanisa ya nyumbani yaanzishwe kwa kusudi la kufikisha huduma karibu na watu na sio kwaajili ya kukusanya mapato, washirika wote wa makanisa ya nyumbani watatoa sadaka zao katika kanisa kuu lililoko katika mji husika, makanisa ya nyumbani msisitizo wake ni wa kifamilia kuifanya familia ya Kikristo kuishi pamoja na kushirikiana na kubebeana mizigo, makanisa ya nyumbani pia ni makanisa ya Mungu, kusudi kuu ni kuabudu na kujifunza neno la Mungu  na kutiana moyo, Ni muhimu makanisa haya yakaendeshwa kwa kanuni za kimaandiko na yakatambua viongozi wao na kuwaheshimu, Makanisa ya nyumbani ni kielelezo na nuru katika mitaa yetu kuendelea kumuhubiri Kristo kivitendo na kuuishi kwa upendo kama Mungu alivyotuamuru  

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 

Hakuna maoni: