Jumapili, 16 Agosti 2026

HUDUMA YA USHAURI WA KICHUNGAJI

 

1Petro 5:2 “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”




Utangulizi

Moja ya majukumu ya huduma ya kichungaji, ni pamoja na kulichunga kundi na kulisimamia, Neno kulichunga kundi na kulisimamia katika kiyunani yanatumika maneno mawili “Poimainō” na “Episkopeō  ambayo kwa kiingereza yanatafasirika kama “Feed” na “look deligently” ambayo maana yake kwa Kiswahili ni kulisha na kuchunga “look deligently” “Carefully examine”  “seek with total dedication” kufanya uangalizi makini, kuchunguza kwa makini, kutafuta kwa kujidhabihu, kwa msingi huo huduma ya kichungaji sio kuwalisha kondoo peke yake lakini pia kuwachunga yaani kuchunguza kile wanachopitia, wana ugonjwa gani wanapitia changamoto gani kisha kuzitatua kwa upendo hapo ndipo linapokuja swala la kufanya ushauri nasihi, au ushauri wa kisaikolojia ingawa kazi ya ushauri wa kichungaji ni zaidi ya ushauri wa kisaikolojia kwa sababu kuna ukaribu sana na maswala ya  nafsi na roho.Kazi ya ushauri wa kichungaji ni kazi ya kufariji kwa changamoto wanazopitia watu wa Mungu pamoja na kutafuta suluhu kwa pamoja  katika ile changamoto anayopitia mtu husika.

Ayubu 2:11-13 “Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo. Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.”

Ayubu alipopatwa na mabaya, Rafiki zake walitoka kwa kusudi la kusaidia kubeba pamoja naye maumivu yake na kumfariji na kujadiliana naye kwa pamoja ili yamkini waweze kufikia suluhu ya kifalsafa ya swali kubwa linaloulizwa na wanadamu wanapopitia changamoto nini sababu ya mateso na kwa nini yanipate mimi, kufanya huduma ya aina hii ni sehemu ya huduma ya kichungaji ambayo wahudumu, watendakazi, wanafunzi na wenye hekima tunapaswa kuifanya pia kwaajili ya kuwabebea mizigo kondoo wa Bwana wanaopitia changamoto mbalimbali. Huduma hii ni ya malezi, huduma hii ni ya uangalizi, huduma hii ni ya ulinzi dhidi ya kondoo, huduma hii ni ushauri, na kutia moyo

Wagalatia 6:1-2 “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”

Tutajifunza somo hili ushauri wa kichungaji kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

 

  • Maana ya Huduma ya ushauri wa Kichungaji
  • Umuhimu wa huduma ya ushauri wa kichungaji
  • Misingi ya Ushauri wa Kichungaji

 

Maana ya Huduma ya ushauri wa Kichungaji

Ushauri wa kichungaji  ni mfumo maalumu wa huduma ya kisaikolojia unaotumia njia za kiroho na kisaikolojia kwaajili ya kumtia mtu moyo kiakili ili kumuwezesha mtu huyo kuchukuliana na mazingira ya changamoto ngumu inayomkabili na kuponya majeraha ya kihisia ambayo kwa kawaida inaathiri maendeleo ya kimwili, kiroho na kiakili, Kimsingi njia za kisaikolojia zinaweza kutumika kumponya mwanadamu kiakili na ndio maana wako wanasaikolojia wanaofanya kazi za ushauri hata hivyo huduma ya kichungaji ya ushauri ina nguvu zaidi kwa sababu haiishii katika akili pekee bali huenda mpaka katika roho na kuleta ufumbuzi wenye manufaa, kwa hiyo ushauri wa kichungaji sio tiba ya kitabibu, wala sio ushauri wa kisaikolojia, bali ni huduma inayolenga kuleta uponyaji wa ndani na kujenga mwelekeo mwema wa maisha, Na ndio maana katika sifa za Yesu Kristo yeye pia anaitwa Msahuri wa ajabu unaona!

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Sio hivyo tu Roho Mtakatifu katika utendaji wake kamili, moja ya shughuli anayoifanya ni pamoja na ushauri nasihi

Isaya 11:1-4 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.”

Huduma ya ushauri wa kichungaji huwasaidia watu kihisia, kiroho, na kimaadili na hufanyika kwa kutumia neno la mungu na hekima inayowekwa kwetu na Roho Mtakatifu kwa sababu yeye ndiye anayeyajua mambo ya roho ya mwanadamu na pia anayajua mambo ya Mungu kwa hiyo mtu anayefanya kazi ya ushauri wa kiroho anapaswa kuwa amejazwa Roho Mtakatifu kwaajili ya huduma hii na utumishi huu

1Wakorintho 2:10-14 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho Huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana Ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.”

Kupitia huduma ya ushauri wa kichungaji Bwana Yesu aliweza kumsaidia kimaadili mwanamke msamaria ambaye kimsingi alikuwa anaishi maisha ya kikahaba huku akichukuwa waume za watu, na kuishi katika usumbufu, wa kisaikolojia, alikuwa akichota maji saa za mchana muda ambao wanawake wengine walikuwa wameacha kwenda kuchota maji, alijihukumu mwenyewe kutokana  na maisha ya ukahaba, japo alikuwa na ufahamu fulani kuhusu kuabudu lakini haikuwa katika njia sahihi, Yesu alipokutana naye alimshauri mambo ya ajabu ambayo yaliweza kabisa kugeuza maisha yake na maisha ya watu wa mji mzima wa Samaria

Yohana 4:4-26 “Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka. Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.”            

Ni kupitia huduma ya ushauri wa kichungaji Yesu aliweza kufanikiwa kubadilisha tabia na ufahamu wa kiimani kwa mwanamke Msamaria na Wasamaria wote waliokuja kumsikiliza baada ya ushuda wa kufunguliwa kwa mwanamke huyu, Yako mambo ambayo maombi na maombezi pekee hayatoshi kukamilisha uponyaji wa mtu lakini kupitia ushauri tunaweza kuwafikia watu wa Mungu na kuwasaidia wakapona kiakili kiroho na kisaikolojia, haya yanaweza kufanyika kupitia huduma ya ushauri, kusikiliza, kuuliza maswali na kuelekeza katika ukweli wa mambo!    

Umuhimu wa huduma ya ushauri wa kichungaji.

Kimsingi kila mwanadamu anahitaji ushauri, hakuna mwanadamu anajitosheleza yeye mwenyewe hata kama mwanadamu huyo yuko karibu na Mungu, kuna wakati mtu mwingine anaweza kuliona jambo kwa jinsi nyingine au katika pembe nyingine na akalitolea ufumbuzi, kwa mfano Musa alikuwa akifanya huduma ya ushauri na watu wengi walikuwa wakimuendea, na akawa akiwashauri na kuwaamua, hata hivyo pamoja na haya aliyokuwa akiyafanya kuhani mkuu wa Midian Yethro alikuja na kumshauri kitu cha kufanya ili yeye na watu anaowahudumia  waweze kuwa salama

Kutoka 18:13 -24 “Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani.Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.”

Tunajifunza hapo kwamba kila mwanadamu anahitaji ushauri, Musa alikuwa nabii mkubwa sana na mwenye kuzungumza na Mungu uso kwa uso, Lakini alishauriwa na mkwewe namna njema na bora ya kutumika, ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Musa peke yake angeumia kuifanya kazi hiyo kwali aliifanya asubuhi mpaka jioni, sisi nasi kama watenda kazi hatuiwezi kuiacha kazi hii mikononi mwa wachungaji pekee ni lazima kundi la watu wa makumi, na mamia na maelelfu waluiofunza kama hivi katika shule ya huduma wahusike pia katika kutoa ushauri wa kichungaji kwa washirika wetu kwani sio kila jambo linaweza kuponywa kutokea madhabahuni, watu wanahitaji kusikilizwa, kuuliza maswali na kujibiwa na kufunguliwa pia kwa njia ya mazungumzo na kusaidiwa sana kiroho huduma hii ni muhimu sana kwa sababu

1.       Inawalinda kondoo wasipotee – kuna makundi makubwa ya watu makanisani yaani katika makanisa ya kiroho wanapotea kimya kimya sababu kubwa ni kukaa na changamoto na kukosa msaada na ushauri wa kichungaji unaoweza kuwatatulia shida zao na kuwarejeza ni kama vile laiti wangelipata mtu wa kuwasikiliza kwa kina!

 

Mathayo 18:12-14 “Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea.Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.”

 

2.       Ushauri wa kichungaji husaidia kuleta uponyaji wa ndani – wako watu wengi ambao wana maumivu ya ndani, hawaumwi na hawana mapepo, lakini wana maumivu moyoni kwaajili ya mambo yaliyopita, maumivu ya kihisia, na kadhalika ambao wanahitaji uponyaji wa ndani ambao unaweza kuletwa kwao kwa ushauri wa kichungaji kama watumishi wa Mungu tunajihusisha sana na kondoo wa Bwana, Mchungaji biashara yake ni watu, kwa hiyo mtumishi wa Mungu wa ngazi yoyote ile na wa kundi la kiwango chochote kile huduma ya ushauri wa kichungaji inatuhusu, watu wakipata mchungaji wa namna hii watamuamini na kuona kweli unajishughulisha na mambo yao kuchunga ni pamoja na kujishughulisha na maisha ya waamini wetu  na kuwasikiliza na kuwaganga wapone

 

Matendo 20:28 “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”

 

Zaburi 23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 

3.       Kusaidia kondoo  kufanya maamuzi sahihi – Washirika kama ilivyo kwa kila mtu anahitaji wakati fulani kufanya maamuzi, ulimwengu wa roho una tabia ya kusubiria wakati wa maamuzi kwa sababu wakati huo nafsi ya mwanadamu inaweza kuingia katika uamuzi chanya au uamuzi hasi, kwa sababu hiyo hakuna wakati Muhimu duniani kama wakati wa kufanya maamuzi, kwa sababu hiyo wakati mwingine wanadamu hutafuta mahali sahihi wanapoweza kusaidwa kufanya maamuzi sahihi, kuna maamuzi ya kifamilia, maisha, ndoa, utumishi, kazi, utatuzi wa migogoro, uchaguzi wa mwenza, ununuzi wa vitu vya thamani na kadhalika

 

Zaburi 32:8-10 “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama. Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia. Naye mtu mwovu ana mapigo mengi, Bali amtumainiye Bwana fadhili zitamzunguka.”

       

4.       Ushauri wa kichungaji ni ulinzi dhidi ya matukio mabaya – Kwa kutoa ushauri wa kichungaji waamini wanalindwa dhidi ya hisia, usalama, muongozo wa kiroho na kisaikolojia, kanuni na kuinua nia  vyote inakuwa ngao kwa kila mtu, na kuwalinda dhidi ya uharibifu, skendo na kadhalika kwa kuwapa maelekezo sahihi ya kimaandiko au muongozo wa Mungu, kusahihisha, kulinda na hatari, na mafundisho au Imani potofu

 

Matendo 27:21-25 “Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe.Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”

       

5.       Hujenga uaminifu, upendo na uwajibikaji – Huduma ya ushauri wa kichungaji inajenga uwajibikaji wa wahudumu wa injili kwa washirika wao, lakini pia unapofanikisha mambo yao unajijengea kuaminiwa, na kuunda upendo wa kweli, huduma hii inaashiria kuwa unajali watu, unapenda watu, unaheshimu watu, na unawathamini kwa hiyo washirika watafunguka zaidi kwa kanisa lao na wahudumu wa kanisa lao kwani utawatunzia pia siri zao na kuwaongoza kwa hekima bila kuathiri amani yao kwa hiyo huu ndio moyo wa huduma ya kichungaji

 

1Wakorintho 13:4-8 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”

       

Misingi ya Ushauri wa Kichungaji

Huduma ya ushauri wa kichungaji ina miiko yake na misingi yake ya kimaadili ni huduma ya muhimu sana lakini inahitaji uangalifu mkubwa kwa sababu hiyo inahitaji sana hekima na maarifa na akili, na ndio maana makanisa mengi yameshindwa kuwa na huduma za namna hii na kuwaacha watu wahangaike kwa mataifa kutafuta ushauri, kwa wanasaikolojia, na washauri wengine, Mungu anatarajia watu wa ndani katika kanisa wawe na hekima ya kufanya maamuzi na mashauri badala ya maswala ya kikanisa kupelekwa kwa mataifa, Hata hivyo kama viongozi na watenda kazi katika kanisa watakosa hekima hii na kuzingatia misingi ya ushauri wa kichungaji watu wanaweza kusema heri kwenda kwa mataifa na sisi tutakuwa tumeshindwa kutimiza wajibu wetu ipaswavyo;-

1Wakorintho 6:1-6 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini.”

Mambo yafuatayo yazingatiwe basi na kila mtenda kazi, mhudumu, mwanafunzi, na wenye hekima katika kanisa

1.       Kusikiliza – anapokuja mtu mwenye majanga yake kwaajili ya kutafuta ushauri wa kichungaji ni vema sana akasikilizwa, mtu mmoja alisema ni kama Mungu ametupa masikio mawili na mdomo mmoja ili tusikilize zaidi kuliko kusema sana, kwa hiyo tujitie nidhamu kumsikiliza mtu ajielezee bila kuwa na kiherehere cha kuzungumza au kujibu kwa haraka ama kudhani kuwa tuna ufumbuzi wa haraka ni muhimu kusikiliza kwanza.

 

Yakobo 1:19 “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;”

 

2.       Usiri – watu wanachukizwa wakati mwingine na ushauri wa kichungaji hasa katika makanisa ya kipentekoste kwa sababu  wakati mwingine unatoka tu katika chumba cha ushauri tayari habari zako watu wanazo, au unatolewa habari zako madhabahuni kwenye bomba kama mfano  wakati wa mahubiri labda linaweza kuachwa kutajwa jina lako tu hii ni swala linasikitisha sana ni lazima tuwe na moyo wenye kutunza siri au mafriji yanayogandisha, si vizuri siri za mshauriwa zikatoka nje au kufanyiwa masimulizi au mifano utoaji wa siri huharibu huduma hii, kama madaktari wanavyoficha siri tunza siri za watu, hatupendi kusikia nimekuambia tafadhali usije ukamwambia mtu, na mwingine unamsikia aliyeniambia kaniambia nisimwambie mtu lakini wakati huo huo habari zimeenea

 

Mithali 11:12-14 “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”

 

Mithali 25:2 “Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.”

 

3.       Zingatia mahusiano – Ni vema kujihami kwa sababu katika kutoa ushauri wa kichungaji kumejitokeza changamoto za aina nyingi na ndio maana watumishi wengine wa Mungu hawapendi kufanya huduma hii, jilinde, mlinde na anayekuja kushauriwa msikae faragha sana, epukeni ukaribu wa kimwili na kihisia usiofaa, zingatia kulinda uhusiano na jinsia tofauti kwa tahadhari kubwa ili kujiepusha na kashfa na skendo za aina mbalimbali, Paulo amabye hakuwa na mke alifanya kazi pamoja na Prisila na Akila waliokuwa mume na mke kwaajili ya kutunza ushuhuda ili neno la Mungu lisitukanwe!

 

1Wathesalonike 5:22-23. ”jitengeni na ubaya wa kila namna. Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.”

 

Waefeso 5:3-5 “Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wala wa kutamani kama iwashtahilivyo watakatifu, wala aibu wala maneno ya upuuzi wala ubishi; hayo hayapendezi bali afadhali kushukuru, maana neno hili mnalijua hakika ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu

 

Matendo 18:18 “Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.”

 

4.       Usiutumie ushauri kwa manufaa binafsi – kutokana na huduma hizi kuwa adimu na huduma ya kichungaji ya ushauri kutolewa bure watumishi wengi wa Mungu wamekuwa wakijinufaisha kifedha na kuwatoza watu fedha nyingi hasa wale wanaotaka kuwaona uso kwa uso kwaajili ya Ushauri, kamwe usitumie huduma hii kama njia ya kujinufaisha, kuchukua rushwa, na kuteka watu kingono, au kuwatawala watu, kuwaendesha na kudhibiti nafsi zao hilo jambo sio la haki, aidha ni muhimu kujilinda kwa sababu wakati mwingine yule unayempa ushauri anaweza kuwa ni majibu ya tatizo lako binafsi wewe mtoa ushauri, na mkajikuta manajaribiwa kwa kuwa majibu ya kila mmoja kwa mwenzake.

 

2Wakorintho 2:15-17 “Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo? Kwa maana sisi si kama walio wengi, walighoshio neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo.”

                       

5.       Tambua mipaka ya kihuduma - Unapokuwa umesikiliza vya kutosha wale tunaowahudumia unaweza kugundua kuwa kuna maswala mengine huwezi kuwa na majibu nayo, hayo yanaweza kuwa yanahitaji madaktari au wana saikolojia, kwa hiyo unaweza kumuelekeza mtu aende sehemu sahihi kulingana na changamoto yake na kufanya hivyo sio kushindwa kwa sababu sisi tunashughulikia maswala ya kiroho, Yesu aliweza kumfufua Lazaro  lakini swala la kumfungua sanda haikuwa kazi yake, na Yesu aliweza kumfufua binti Yairo lakini kazi ya kumpa chakula haikuwa ya kwake, unapotoa ushauri fanya eneo lako ambalo kimsingi ni la kiroho na kisaikolojia kwa sehemu na mengine kama yako nje ya uwezo wako mpeleke kunakohusika, mfano Menopouse na Andrepouse Ukomo wa hedhi na changamoto zake na   ukomo wa uzazi kwa wanaume  yanaweza kuzungumzwa na wataalamu wa afya

 

Yohana 11:41-44 “Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”

 

Marko 5:39-43 “Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu.Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.”

 

6.       Uwe muadilifu – huduma ya ushauri inahitaji uwe mwadilifu, wakati mwingine kile unachikishauri inawezekana kikasababisha uwe majibu ya yule unayemshauri, mfano anakuja mwanamke mzuri tu na anakuletea kesi kuwa mumewe hamridhishi kwenye tendo la ndoa, na wewe mhudumu una changamoto nyumbani unanyimwa tendo la ndioa na mkeo au nawe huridhishi unajikuta majibu ya changamoto yako yako kwa mteja wako bila uadilifu binafsi huduma hii inaweza kukuweka pasipo, au unaweza kushauri kwa uchungu mfano anakuja mwanaume ambaye ananyimwa tendo la ndoa na wewe ni muhanga wa kunyimwa unaweza kujikuta mnaungana kuwachukia wanawake uadilifu ni nyenzo muhimu, jilinde na mjaribu, jilinde na tuhuma jilinde na kusingiziwa,

 

1Timotheo 3:2-5 “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) 

 

Wagalatia 6:1-2 “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”

 

Hitimisho

 

Huduma hii ni ya moyo, ni huduma ya usikivu, ni huduma ya huruma, ni huduma ya kujali, ni huduma ya uaminifu, ni ulinzi wa kondoo wa Bwana hatuna budi kumuomba Mungu atupe moyo wa huruma ili tuwahudumie watu wake. uwe na watu karibu ili kama mshauriwa atakuwa na pepo kuwe na msaada wa kihuduma wakati pepo zinakemewa na kutolewa ikiyajua hayo heri wewe ukiyatenda !

 

Yeremia 3:15 “nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: