Jumatano, 26 Agosti 2026

Nafasi ya Mwanaume Katika huduma!


1Timotheo 2:5-8 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa wanaume ni mojawapo ya nguzo muhimu sana katika jamii na katika Kanisa pia, Kanisa lolote ambalo lina afya ya kiroho kamwe haliwezi kupuuzia ujenzi wa wanaume kama wanafunzi wa Yesu ambao wanawajibika kwa kiwango kikubwa katika usimamizi wa jamii, familia na Kanisa, Kanisa linapoweka mkakati kuwaelimisha vizuri wanaume ni dhahiri litapata nguzo muhimu za kiroho zenye nguvu, ushawishi na mamlaka ya kuibadili jamii na kuileta kwa Kristo.

Marko 3:13-19 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea.  Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti. Kisha akaingia nyumbani.”

Kutokana na umuhimu wa wanaume Yesu kwanza aliwaita wanaume 12 ili wawe  pamoja naye  na wawe wanafunzi wake wa msingi, kwa kusudi la kuwafundisha ili kisha waweze kubeba jukumu la kuweka msingi wa kanisa kwa kujenga utamaduni mpya jamii mpya na taifa jipya yaani Kanisa la Mungu ambao ni kama Israel ya Kiroho, Yesu alitamani wajifunze maisha yake ya kila siku, tabia zake na mafundisho yake, kisha wasambaze ujumbe wake wa ufalme wa Mungu, huku wakiwa na mamlaka ya kuponya wagonjwa na kutoa pepo, Yesu hakupuuza wanawake lakini alionyesha wazi kuwa wanaume wana umuhimu mkubwa zaidi katika maongozi ya Kanisa kama ilivyokuwa wana wa Israel 12 ambao walikuwa kabila 12 za Israel ambazo zilikuwa chanzo cha taifa la Israel, kwa sababu hiyo Yesu hata leo bado anawategemea sana wanaume katika kazi yake. Kwa msingi huo leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu Nafasi ya Mwanaume katika huduma kwa kuzingatia vipengele muhimu vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Umuhimu wa mwanaume kwa mujibu wa maandiko

·         Wajibu wa mwanaume kwa mujibu wa maandiko

·         Nafsi ya Mwanaume katika huduma

Umuhimu wa mwanaume kwa mujibu wa maandiko.

Ni muhimu kufahamu kuwa mwanaume ana wajibu mkubwa na wa kwanza kabisa katika jamii duniani kama ilivyo vile vile katika Kanisa mwanaume amaeaminiwa uwakili na Mungu, Mwanaume ni mfadhili, mwamaume ni mlinzi, mwanaume ni mpiganaji, mwanaume ni kiongozi, wakati Mungu anaiumba dunia katika mpango wake mwanaume alipewa kipaumbele kama kiumbe wa kwanza anayeweza kuendeleza na kutunza uumbaji wa Mungu duniani, kule kuumbwa kwanza kulimfanya awe kiongozi wa asili

Mwanzo 2:15-17 “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”

1Timotheo 2:11-15 “Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.

Maandiko yanaonyesha kuwa mwanaume ni nguzo muhimu sana katika jamii na  imani na kuwa anamchango mkubwa sana katika maswala ya ujenzi wa jamii kuanzia na maswala ya kiroho, uongiozi wa familia, ujenzi wa jamii, uchumi, kufanya kazi, na kuwafundisha wengine, Jamii yoyote yenye afya ya kijamii ni ile ambayo wanaume wako mstari wa mbele katika kila jambo, kwa hiyo wanaume wakitangulia huku wakisaidiwa na wanawake wanauwezo mkubwa sana ya kuifanya jamii hiyo kuwa na nguvu likiwepo Kanisa, Kwa bahati mbaya tuko katika nyakati ambazo sasa ambao uanaume unapigwa vita sana au wanaume wanaacha wajibu wao na kuanza kutaka vya dezo, kufanyiwa na kuandalia kila kitu jambo ambalo litatujengea jamii ya ajabu sana na Kanisa la ajabu pia, Mungu alimchagua mwanaume mmoja jina lake Abrahamu kwa sababu alimjua kuwa mwanaume huyu atakuwa mjenzi wa jamii yake hata baada yake akiwafundisha watoto wake baada yake washike hukumu za Mungu na kutenda haki

Mwanzo 15:17-19 “BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”

Maandiko yanaonyesha kuwa wanaume wana umuhimu mkubwa sana katika ujenzi wa jamii inayomcha Mungu, jamii inayofanyakazi, jamii yenye ugunduzi, jamii yenye maendeleo, yenye utulivu na mwelekeo mkubwa wa maendeleo ya kiroho, kimwili, kisayansi na kisaikolojia, bila kujali sera kubwa za sasa zinazokazania usawa wa kijinsia na utambuzi wa wanawake katika jamii, lakini hii haiondoi ukweli wa neno la Mungu kuwa wanaume wana mchango wakipekee kuanzia katika usimamizi wa kifamilia  mapaka katika maswala ya ibada, uchumi na ugunduzi wa teknolojia. Wanaume bado wanabaki kuwa ndio washikadau wakubwa wa mwelekeo wa ulimwengu na kwakweli Mungu anawategemea sana wanaume na anataka wawe mstari wa mbele kila mahali

Kama unadhani wanaume sio wa muhimu fanya utafiti mdogo tu waulizie wanawake ambao wameishi kama “Single Mothers” kwa muda flani utagundua tu kuwa wana changamoto kubwa zaidi na mateso makubwa ya kihisia wakiteswa na upweke, kiburi, migandamizo na mateso ya kihisia wengi wanalia na hata wakikutana na mambo magumu wanasema ninaonewa kwa sababu sina Mume, Mungu alimuumba kila mwanadamu na upekee wake na kila mmoja anamtegemea mwingine kwa hiyo haijalishi mwanamke atakuwa na mafanikio makubwa kiasi gani  lakini utafiti unaonyesha kuwa bila mwanaume mwanamke huyo hana ukamilifu. Mungu ameumba watoto wakue wakisikia sauti ya baba na mama na wanapoikosa sauti mojawapo watakapokuwa watu wazima wataanza kuuliza yuko wapi baba yangu? au wataonyesha athari zinazoashiria kukosekana kwa malezi ya upande mmoja

Na ndio maana leo neno la Mungu linawataka wanaume wasimame katika nafasi yao kuanzia katika ibada mpaka katika majukumu mengine ya kijamii, kama hesabu za Agano la kale zingekuwa zinafanya kazi hata leo, Kanisa letu unadhani lingekuwa na washirika wangapi?  Ninene kiwazimu kila mchungaji asihesabu washirika wanawake, ahesabie wanaume tu kisha tuone!

Mathayo 14:19-21. “Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano.Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. NAO WALIOKULA WALIKUWA WANAUME WAPATA ELFU TANO, bila wanawake na watoto.”             

Muulize jirani yako hapo Mtumishi hiyo miujiza unayoifanya unawafanyia wanaume wangapi? Yesu alifanya miujiza mbele ya wanaume 5000 bila kuhesabu wanawake na watoto, Muulize tena miujiza yako inafanyika mbele ya nani? muulize Kanisa lako wewe ulianza na kina nani? Tunasoma kuwa Kanisa la Efeso lilianza na wanaume 12 tu na walipompokea Roho Mtakatifu kazi ya Mungu ilienea na Kanisa lilikuwa kubwa sana, nadhani kama tungekuwa tunahesabia wanaume tu kanisani basi utagundua kuwa bado makanisa mengi yanalazimika kuwa na wajibu wa kuwafikia wanaume na tukiwa na wanaume wengi tuna washirika wengi

Matendo 19:1-7 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.”

Paulo mtume anamwambia Timotheo nataka wanaume wasimame kila mahali, hili lilikuwa ni agizo la Mungu kwa Kanisa hata leo, Mungu anawataka wanaume, katika mikakati yetu ya kuihubiri injili ni muhimu kwetu tukae tujadili na kutafakari kwamba tunajali ni kwa namna gani tutawapata wanaume? wanaume wakipataikana na wakawa wanasali na kuinua mikono iliyotakata jamii nzima itabadilika, Shetani amewachukua wanaume kwenye mpira wa soka, amewachukua baa na kanisani anatuachia wanawake na kanisa tumekaa na kutumbua macho, mwambie jirani yako nataka wanaume hapa, Basi nataka wanaume wasalishe kila mahali!

1Timotheo 2:8 “Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.”

Wajibu wa mwanaume kwa mujibu wa maandiko.

Kufanya kazi kwa mikono yake mwenyewe – Moja ya wajibu aliopewa mwanaume hapa duniani ni kufanya kazi, Kazi ina Baraka nyingi sana hata kama mtu hajaokoka akifanya kazi kazi huleta matokeo makubwa, Nchi nyingi zenye mafanikio na maendeleo makubwa ni nchi za watu wanaofanya kazi na sio wale wanaopiga soga, Kazi ilikuwa ni wajibu wa kwanza aliopewa mwanadamu hata kabla ya kuagizwa kuabudu, Mungu aliagiza wanadamu wafanye kazi, Mungu mwenyewe aliumba dunia kwa kufanya kazi siku sita, kwa hiyo ni lazima tufanye kazi, maandiko yanaagiza kila mwanaume kufanya kazi, kazi ni wajibu ni ibada.

Mwanzo 2:15-17 “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”

2Wathesalonike 3:6-10 “Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.”                

Mwanaume anapaswa kuwa na Ushujaa, - Maisha ya duniani ni kama mapambano na njia mojawapo ya kufanikiwa ni pamoja na kuwa na ushujaa, kujiamini kuwa mbali na woga na hofu, kila mwanaume anapaswa kumcha Mungu na kumtegemea Mungu lakini kujiamini na kujipa ujasiri, hakuna mafanikio kama hutakuwa na ujasiri, odoa aibu jipe ujasiri pambania hatima ya jamii yako

Yoshua 1:7-9 “Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

1Wafalme 2:1-4 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako, ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.”

1Wakorintho 16:13-14 “Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari. Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.”

Wanaume wanaagizwa kumpenda Mungu – Kila mwanaume anawajibu wa kumpenda Mungu, Mwanaume aliwekwa duniani na Mungu kabla ya wanawake na mambo mengine, Mungu alimchagua mwanaume kuwa mtumishi wake, alikuwa amekusudia awe na uhusiano na yeye, furaha ya mwanaume mkamilifu kamwe haiwezi kuwa kamili kama hana uhusiano mwema na Mungu, Maandiko yanaamuru tumpende Bwana Mungu wetu kwa moyo, kwa akili na kwa nguvu na jirani zetu kama nafsi zetu.

Mathayo 22:37-39 “Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

Wanaume waagiza kuwa na familia – Mojawapo ya wajibu muhumu wa kila mwanaume ni kuanzisha familia kwa hiyo mwanaume ni kiongozi kipenzi wa mkewe, kila mwanaume anatakiwa kuanzisha na kusimamia familia yenye mamlaka na familia imara akiwa msimamizi wa imani, tamaduni, sheria na taratibu za kiungu katika familia hiyo, familia itakayostawisha na mwanaume haiwezi kuwa imara kama mwanaume huyo atamweka Kristo pembeni, mamlaka ya mwanaume inaweza kuwa kamili na ya amani kama itifaki ya kiungu itakaa sawa katika familia hiyo na mwanaume anawajibika kuipenda familia yake na kuisimamia na kuilinda na kuhakikisha kuwa anaipatia mahitaji yao, wale wanaoogopa majukumu na wanaoogopa kuoa na kuwa na familia uanaume wao hauwezi kuwa uanaume kamili, Mwanaume hapaswi kuogopa majukumu wala hapaswi kuyakimbia, wengi leo wamekimbia familia

1Wakorintho 11:3 “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.”

Waefeso 5:25-29 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;  ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.”

Wanaume wanawajibika kutawala au kuongoza – Itifaki ya kiutawala na kiuongozi katika familia  inaonyesha kuwa mwanaume ndiye anatakiwa kuwa Kichwa, neno kichwa  ambalo kwenye kiingereza limetajwa kama  the head” katika lugha ya Kiyunani ni  “Kephalē ambalo maana yake ni the brain  literal na Metaphorical ni Chief, Ruler, Leader, Master, au  a person of high status au the source kwa hiyo kama Kristo alivyo ndiye mkuu wa Kanisa na mume ndiye mkuu wa familia na mkuu wa mke wake utaratibu huu ukikiukwa hata kama hamjafanya dhambi uwepo wa Mungu unaondoka Mungu ni Mungu wa utaratibu na sio Mungu wa machafuko, kwa hiyo mume anawajibu wa kuongoza na kutawala katika ndoa yake “be the head of your wife” hili ni agizo:-  

Mwanzo 3:16-19 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”

Waefeso 5:23-26 “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;”                

Wanaume wanawajibu wa kusalisha – Kama jinsi ambavyo wanaume wamepewa wajibu wa kuwa viongozi wa familia, Mungu amewapa wajibu pia wa kusimamia shughuli za ibada kila mahali, Mungu anawapa wajibu sio tu kusimamia ibada lakini kuwa kielelezo kikubwa cha imani katika familia yake, Neno kusalisha katika Kiyunani ni “Proseuchomai” limetumika mara 90 katika agano jipya kwa kiingereza “to supplicate worship”, au “to be a person in authority to God during prayer” Paulo anawataka wanaume huko Efeso wawe viongozi wa ibada kila mahali, waongoze maombi, waongoze ibada wasalishe

1Timotheo 2:5-8 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.”

Nafasi ya Mwanaume katika huduma!

1Timotheo 2:5-8 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.”

Pauilo mtume hataki wanaume wabweteke tu kanisani anatoa wito kwa kila kanisa kuwa wanaume ndio wawe mstari wa mbele katika kila mkutaniko wa Kanisa la Mungu tena sio waje tu mbele na kuongoza ibada kila mahali lakini pia wakiwa na mikono safi, maana yake wakiwa na maisha matakatifu, wanaume wawe kielelezo, kuwa na mikono iliyotakata maana yake ni wasio na hatia, walio safi kimaadili, Yesu Kristo mwokozi wetu alikuwa mwanaume, ukombozi wetu umetoka kwa mwanaume kwa hiyo kila mwanaume anatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kumuunga mkono mwokozi wetu na sio kukaa nyuma nyuma

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Paulo kwa kusema agizo lake lile alikuwa anamtaka Timotheo kuhakikisha anawekeza kwa wanaume maswala ya kiroho yote kama mwanaume ndio kiongozi wa familia kumchukua mke wake na watoto wake kuja ibadani kisha kumuacha yeye ni sawa na kuteka ufalme wake, na utawala wake.  Kanisa lazima limlenge mwanaume hata kama mwanamke ataokoka kwanza lakini lazima zitafutwe namna na baba afuate nyakati za kanisa la kwanza alikuwa akiokoka baba kwanza na nyumba nzima inafuata, na sio hivyo tu Mwanaume akitangaza msimamo moja kwa moja na familia nzima iliweza kuhusika kuliko mwanamke akitangaza.  

Matendo 10:1-5 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.”

Matendo 16:27-32 “Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.”

Yoshua 24:14-16. “Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine;”            

Mungu akianza na wanaume katika kuokoa ni ukweli ulio wazi kuwa wanawake watafuata tu na watoto pia na migogoro mingi ya watu kuachwa kwaajili ya wokovu itakuwa haiko, hivi ndio Mungu anavyotaka, wanaume wakiwa mstari wa mbele katika mikesha kutakuwa na mafarakano nyumbani kweli? Mwanaume akitangaza msimamo wengine watafuata tu Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, Mungu anatamani wanaume wawe kama Yoshua watangaze msimamo na familia zao zifuate

1.     Kanisa tusiwasahauu wanaume - Kanisa lolote lenye afya njema na familia yoyote yenye afya njema itampa mwanaume kipaumbele, tunapoweka mipango yetu na maombi yetu kwaajili ya wanaume ili waokolewe hata kama hawatakuwa viongozi kanisani watakuwa viongozi katika familia zao na jamii, wanaume wana nafasi kubwa ya kuvunja kuta zote za vizuizi katika jamii na familia na kuwa sauti ya Yesu Kristo kila mahali, mwanaume akipatikana jamii nzima itapatikana  na ndio maana Paulo anataka wanaume wasalishe kila mahali, Yesu mwenye nguvu ya kuokoa hataokoa kwa uonevu ataiokoa wanaume pia

 

1Wakorintho 16:13-14. “Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari. Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.”

 

2.  Kanisa lazima liwaendeleze wanaume kama viongozi wa kiroho, Yesu hakuufikia ulimwengu kwa kuzungumza na watu wengi pee yake lakini aliwekeza muda mwingi, mrefu na wakutosha akiwa na wanaume 12 aliwaandaa kuwa viongozi, aliwatia moyo na kuwajenga ili kuwekeza ukomavu wa kiroho kwao, hebu fikiria nyumba ambayo mama amekomaa kiroho afu baba ni mchanga kiroho?  Ukomavu wa kiroho ukiwekezwa kwa wanaume tunatengeneza jamii yenye amani sawasawa na mpango wa Mungu, ukuaji wa kiroho ni swala linalohiaji mpango, na wanaume kwa taarifa yako ndio wenye ushawishi mkubwa utafiti wa kweli unaonyesha kuwa mama akitangulia kuokoka ni asilimia 30% ya wanafamilia ndio watakaomfuata lakini baba akitangulia kuokoka ni asilimia 93% ya wanafamilia watafuta kwa hiyo tunapopanga kuufikia ulimwengi fikiria namna ya kuwapata wanaume, mafunzo na mafundisho ya kimkakati kanisani yasikose kufikiri kuwafikia wanaume.

 

3.    Kanisa linalotaka kukua ni lazima lilenge kuwahudumia au kuwafikia wanaume – Mungu hajawapuuzia wanaume agizo la Paulo kwa Timotheo linasisitiza kwamba wanaume wahudumiwe kwa wingi na kwa kadiri iwezekanavyo, tutengeneze Ujamaa na wanaume kama neno la Mungu lisemavyo kuwa chuma hunoa chuma, tuwanoe Wanaume tuwafikie wanaume

 

Mithali 27:17-19 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.”

 

4.     Kila mwanaume kanisani atafute rafiki atakayesimama naye bega kwa bega kwa bega katika vita hii ya maisha, na kukumbuka ya kuwa mtu akiwa peke yake nguvu yake inakuwa ndogo lakini unapoungana na mwingine ushindi unakuwa mkubwa lakini watu wanapokuwa zaidi ya mmoja ushindi unakuwa mkubwa zaidi na hakuna atakayeweza kuwazuia maandiko yanaonyesha nguvu hizo, kimwili na kiroho

Kumbukumbu 32:29-30 “Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao.Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa?

Yoshua 23:9-11. “Maana Bwana amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo. Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana Bwana, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia. Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu.”

Mathayo 18:18-20 “ Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”          

Wanaume wakiigundua siri hii na kuungana na wengine kutakuwa na nguvu kubwa sana katika ufalme wa Mungu ambayo haitazuilika Mwanaume mwenye nguvu akiunga ana mwenye nguvu mwingine katika huduma unadhani kanisa litakuwa na nguvu kwa kiasi gani?  Ni kwaajili ya swala kama hili Paulo anataka wanaume wasalishe yaani washiriki maswala yote ya ibada kila mahali na maswala yote ya kiimani, na wawe mstari wa mbele katika Kanisa wakiitetea imani na kuitangaza.

5.     Kuwawezesha wanaume kutazalisha ibada zenye nguvu - Kanisa likiwapa wanaume kipaumbele kutakuwa na mafanikio makubwa sana katika kazi zake na katika maswala ya uchumi, Mwanafunzi mwanaume anapojifunza kumtumikia Mungu atamtumikia Mungu pamoja na mali zake, wanaume watataka kuona kazi ya Mungu inasonga mbele, tukiwaimarisha wanaume tutakuwa na Kanisa imara sana, tutajenga ushirika wenye kusudi, kadiri mtu anavyokua katika Kristo na kukomaa nguvu hiyo itawekezwa kwenye kanisa lake, wanaume wanaweza kutoka na kuhubiri sehemu mbalimbali, wanaweza kufanya mashambulizi yenye nguvu dhidi ya ufalme wa giza, Kanisa litakuwa lenye afya ya kiroho na ya kudumu wanaume wana nafasi kubwa zaidi na nzuri zaidi ya kutekeleza agizo kuu kuliko wanawake hata kimaumbile, fikiria Petro na Yohana!

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa Dahari

 

Matendo 4:5-13 “Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.”

 

Pampoja na ujasiri na ujazo wa nguvu za Roho Mtakatifu hebu jaribu kuwaza kama Petro na Yohana ndio wangekuwa wanafunzi wa kike tuchukulie Marim Magdalena na Salome wamesimamishwa mbele ya wanaume 70 wakihojiwa unapata picha gani?  Sisiemi kuwa wanawake hawawezi kuitetea imani kwa kiwango hiki, lakini hata wangerudi nyumbani huenda wangeambiwa na familia zao usijihusishe na mambo hata tena! Yesu alijua ni kwanini aliwatanguliza wanaume.

 

6.     Kuendeleza imani ya Wanaume ni kuendeleza Injili – Luka 10:1-6 “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu;na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu.”

 

Kusudi kuu la huduma ya wanaume ni kuufikia ulimwengu, Kanisa ni lazima tuwafundishe wanaume kuitafuta sauti yao, na kuieneza injili, wanaume wengi hufikiri ya kuwa wao sio chombo sahihi cha kuipeleka injili au wanadhani hawana haki ya kumzungumzia Kristo tunahitaji kuwafundisha, tunahitaji kuwajengea ujasiri na tunahitaji kuwapa silaha ili wafanye umisheni, wamtumikie Mungu, watengeneze programu mbalimbali za kuonyesha upendo wa Kristo kwa wengine, wanaume wakiamka hakuna cha kuwazuia, Yesu kama haitoshi akafundisha darasa lingine tena la wanaume 70 ukiacha wale 12 na kisha akawatuma wawili wawili kuongeza kasi ya upelekaji habari njema kwa hiyo tunajifunza hapa kuwa jinsia hii haipaswi kupuuziwa hata kidogo katika maswala mazima ya kuipeleka injili kokote duniani!

 

7.     Wanaume wanapaswa kuwasaidia wanaume vijana -  Tito 2:6-10 “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu, wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.”

 

Dunia inakwenda kwa kasi sana kama Kanisa litachelewa kimkakati kuwavuna wanaume, ni wazi kuwa pia tutachelewa kuwavuna vijana wa kiume au kizazi kijacho cha vijana wa kiume kitakosa walimu wazuri wa kuwafundisha, Paulo mtume mapema alikuwa amemuagiza Tito kuwa wanawake wazee wawafundishe wanawake vijana namna ya kuishi ona:-

 

Tito 2:3-5 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

 

Kama wazee wa kike wanaweza kuwafunza wanawake vijana je vijana wa kiume watafunzwa na nani?  Vijana wanabadilika na wanakua na dunia inaenda kasi, wakati sisi tunashindwa kuwafikia wanaume na kuwasababisha wawe walezi wazuri kwa vijana agenda ya Ibilisi lazima itaelekezwa huko na je tutakua na kizazi cha namna gani, lazima kuweko na wanaume wakomavu walioiva kimaadili waweze kuwa msaada kwa kizazi kipya  cha wanaume vijana, tusipofanya nani atatufanyia, kama tunahitaji kanisa lenye nguvu basi tusisubiri muujiza ujitokeze lazima tufanye kazi ya kuwekeza kwa wanaume ili nao wawekeze kwa wanaume vijana, mwangalie Daudi alivyomuelekeza Suleimani

 

1Wafalme  2:1-4 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema,Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.”                                           

Hitimisho!

1Timotheo 2:8 “Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.”

Kushughulika na wanaume sio program mpya ndani ya Kanisa bali ni swala la lazima kwa afya ya kanisa na usalama wa familia za Kikristo, Kama familia inaongozwa na wanaume katika mpango wa Mungu na mwanaume anafananishwa na Kristo katika itifaki ya uongozi wa Mungu je tunawezaje kuwaweka pembeni wanaume na kuwafikia wanawake kabla ya waume zao na Baba zao?  Je Mungu angelimtokea Sara na kumwambia toka wewe katika nchi yako wende katika nchi nitakayokuonyesha Je Abrahamu na Lutu, na mzee Tera nao wangelimfuata Sara?  Mwanaume ni kama sindano na mwanamke na familia ni kama uzi, pale sindano inapopita uzi utafuata, lakini ni vigumu sana kushina nguo kwa kuutanguliza uzi, Basi nataka wanaume wasalishe ni wito wa kutoa kipaumbele kwamba wanaume waokoke, wanaume wamtumikie Mungu, wanaume wakue kiroho, wanaume wawe watakatifu, wanaume wasalishe kila mahali! Wito huu ni  kwa wanaume kwamba wawe viongozi wa ibada kila mahali, waongoze maombi, waongoze ibada wasalishe, lakini sisemi kwamba wanawake hawawezi kufanya hilo, lakini mwanamke kufanya hilo ni mbadala.

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: