Jumapili, 9 Agosti 2026

JINSI YA KUANZISHA KANISA LA NYUMBANI


Mathayo 18:18-20 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”




Utangulizi:

Tumejifunza huduma ya makanisa ya nyumbani na tumeona faida zake kwamba Mungu anaheshimu makusanyiko yetu yanayojenga umoja upendo na ushirikiano, Lakini sasa hatuna budi kwenda ndani zaidi na kujifunza kivitendo sasa namna ya kustawisha Kanisa la nyumbani, sasa tunaweza je kuanza Kanisa la nyumbani

1.       Ni lazima kumuomba Mungu – Kila kitu katika ulimwengu wa roho kinaweza kupata ufunguzi endapo kitaanza na maombi, Nyakati za kanisa la kwanza Paulo mtume na wengineo watenda kazi pamoja naye waliweza kuifanya kazi kubwa ya Mungu ambayo kimsingi ilianzia katika maombi, kila kitu cha kiroho ni matokeo ya maombi kwa hivyo tunapotaka kuanzisha kanisa la nyumbani ni lazima tumuombe Mungu na Mungu atatoa muongozo na kutupa neema na mpenyo wa jinsi ya kunzisha makanisa hayo.

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

Mathayo 9:36-38 “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

 

2.        Kufanya utafiti wa mitaa na kubainisha vigezo – ili tuweze kuufikia mji kimkakati na kihuduma hatuna budi kufanya utafiti, wa kina kuhusu mitaa ambayo tunalenga kufungua kanisa la nyumbani na kubainisha vigezo vitakavyotusaidia kuweka makanisa ya nyumbani, katika maandiko tunaona kwamba Israel walipotaka kuirithi nchi ya kanaani walituma wapelelezi kuangalia nchi, kwa hiyo ni muhimu kufanya survey (ulinganifu na utafiti) wa kujua wapi tunaweka nini na nani anaweza kufika eneo Fulani na kanisa linaweza kuwa wapi, kwa mfano kama eneo husika ni wanajeshi, au askari ni nani anaweza kutuwakilisha katika eneo hilo, ama kuna chuo kikuu ni nani anaweza kutuwakilisha katika eneo hilo au ni uzunguni, uswahilini na kadhalika ni muhimu kujua ni watu gani tunawafikia ili tuweze kukidhi vigezo vyao, kwa mfano kama eneo ni la wasomi wa vyuo vikuu na likawako kanisa la nyumbani huko, mtendakazi atakayepelekwa kusimamia atakuwa ni yule anayeendana na vigezo vya eneo husika, Kanisa lazima tufanye mambo kwa kutumia busara na akili, tujue idadi ya watu  hasa washirika wetu na ile jamii ya wale tunaotaka kuwafikia ni wa aina gani !

 

Hesabu 13:17-20 “Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi;na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome;”

 

Yoshua 2:1-2 “Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko. Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi.

 

Yoshua 7:2-3 “Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu.”

                       

3.       Tutambue nyumba na mwenyeji wetu – Kanisa la nyumbani linaitwa la nyumbani kwa sababu linafanyia ibada zake katika sebule za watu, kila mtu anaustaarabu wake na anaipenda sebule yake, kwa hiyo kukaribisha watu katika sebule yako ili kufanyike ibada ni kujitoa katika hali ya juu sana sio swala jepesi, lakini jambo hili Mungu analiheshimu na kusababisha Baraka, utoaji wa nyumba au mahali kwaajili ya kuabudia linapaswa kuwa jambo la hiyari na sio la kulazimishwa, mtu anayejitoa nyumba yake sio lazima iwe nzuri au kamili bali anaitoa kwaajili ya Bwana mtu huyu Mungu atamheshimu sana na kumbariki mno, Mungu aliibariki nyumba ya Oded-Edom kwa sababu alikubali Sanduku la Agano la Bwana Mungu wa Israel likae nyumbani mwake, Mtu anayekubali nyumba yake iwe sehemu ya kufanyia ibada hana tofauti na Obedi- Edom

 

Luka 10:5-7 “Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii.”

 

2Samuel 6:10-12. “Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, Bwana ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.”

 

4.       Weka viongozi waliopitia shule ya huduma – Baada ya kuwa tumepata haya yote tunaweka viongozi wetu ambao wamejifunza kutoka kwetu wana mafundisho yetu yaliyo sahihi, walio waaminifu kwetu, wanaotii uongozi, wanaojua kuhudumia watu wenye Imani yetu, viongozi hao ni viongozi watumisi na sio wachungaji wenye mamlaka kamili ya kichungaji

 

Matendo 14:21-23 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.”

 

Mfumo wa ibada katika makanisa ya nyumbani haupaswi kuzidi saa moja

  1. Utafungua kwa maombi.
  2. Itafanyika ibada ya kusifu na kuabudu kwa ufupi.
  3. litahubiriwa neno la Mungu la kibiblia na sio maoni ya mtu (sawa na mafundishio katika kanisa letu) tunakuwa na mafundisho maalumu na tutayagawa kwa walimu wa makanisa ya nyumbani na watafundisha kwa kadiri watakavyokuwa wanapangiwa na kiongozi husika.
  4. Ushirika, maswali, maombi na maombezi, na taarifa za ufuatiliaji.
  5. Kufunga kwa maombi.  

 

Hakuna kanisa la nyumbani linalotakiwa kujiendesha kinyume na utaratibu uliowekwa na kanisa mama ambalo ndilo lenye mamlaka ya mwisho.

Kama kanisa la nyumbani litakapokuwa kubwa taarifa itatolewa na litalazimika kugawanywa na kuwa na kiongozi mwingine aliyepitia shule ya huduma

Kiongozi wa kanisa la nyumbani jihadhari na mafundisho potofu. Jilinde na uasi au kulikata kundi, jihadhari kuligeuza kanisa kuwa klabu ya maswala ya kijamii na michango ya upatu kila kitu kifanyike kwakufuata utaratibu usafi na ushuhuda mwema wa Kirsto

Kanisa la nyumbani sio mfumo au wazo jipya ni mpango wa Mungu wa kibiblia tangu zamani za mitume na kwa kufanya hivi waliupindua ulimwengu

Kama ilivyo kwa watenda kazi kiongozi wa kanisa la nyumbani atawajibika kutoa taarifa katika mfumo utakaowekwa na kanisa kuu.

1Wakorintho 14:40 “Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.”

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: