Jumatano, 12 Agosti 2026

HUDUMA KATIKA VITUO VYA KUZALISHA NGUVU (POWER HOUSE)


Matendo 4:31-33 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.”




Utangulizi:

Neno la Mungu linatuonyesha ya kuwa nyakati za kanisa la kwanza Mitume walikuwa na kundi la watu waliokuwa wanawaombea, wao walikuwa kama askari wa mstari wa mbele katika kuihubiri injili na walipopata mashambulizi walitoa taarifa kwa kanisa na Kanisa liliwaombea kulingana na mashambulizi waliyoyasikia au kuyapata ona kwa mfano katika mistari hii ya Biblia utangundua kuwa kazi ya Mungu na watumishi wa Mungu wanapaswa kuombewa

Matendo 4:18-33 “Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.”                

 

Matendo 12:1-5 “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.”

Maombi ndio asili ya nguvu ya maswala yote ya kiroho katika kanisa la Mungu, na kwa sababu hiyo kila kanisa linalotaka kuwa na mafanikio katika kazi ya kuhubiri injili linapaswa kuwa na kiwanda cha kuzalisha maombi, kiwanda hiki ni nyumba ya kuzalisha nguvu yaani Power house, Katika dunia ya maendeleo ya viwanda na uchumi mwenye nguvu ni yule mwenye kuzalisha umeme wa uhakika, kwa hiyo kanisa ni lazima tuwe na viwanda vya kutosha kuzalisha umeme au nguvu na viwanda hivyo au kiwanda hicho ni katika dunia ya kawaida vinaitwa Power House, Power house ni kituo cha kuzalisha nguvu ya nishati ya umeme na kusambaza katika maeneo mengine na kusababishwa mwanga, uhai, na harakati nyinginezo sasa kanisa linapaswa kuwa na Power House. Kwa msingi huo tunajifunza somo hili sasa Huduma katika vituo vya kuzalisha Nguvu (Power House) Kwa kuzingatia vipengele vitatu

·         Maana ya kiroho ya Nyumba za kuzalisha nguvu (Power House)

·         Umuhimu wa kuwa na Nyumba za kuzalisha nguvu (Power house)

·         Huduma katika vituo vya kuzalisha nguvu (Power House)

Maana ya kiroho ya Nyumba za kuzalisha nguvu (Power House)

Kama tulivyojifunza katika utangulizi kuwa neno Power House au nyumba ya kuzalisha nguvu ni kituo kinachohusika na uzalishaji wa umeme unaoingizwa katika gridi ya taifa kwaajili ya kuleta Nuru, nguvu na kusababisha michakato ya maendeleo endelevu kuchukua nafsi yake katika inchi, katika msingi kama huo, kanisa likiwa na vituo vya maombi ni sawa na taifa kuwa na vituio vya kuzalisha nguvu ya nishati ya umeme, Kituo cha maombi huzalisha nguvu za Mungu kutoka mbinguni na kusababisha mwenendo na utendaji mzima wa kanisa kufanya kazi kwa mpenyo na kwa njia rahisi, kanisa ni matokeo ya chumba cha maombi

Matendo 1:12-14. “Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”

Unaweza kuona kuwa kanisa lilizaliwa kama matokeo ya Maombi, wakati watu hawa wakiomba katika chumba cha juu, hapo ndipo mahali ambapo Nguvu za Mungu ziliachiliwa na watu wakajazwa Roho Mtakatifu na kazi ya Mungu ikaanza kuenea duniani tangu wakati ule hata leo,

Matendo 2:1-4 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”            

Wakati wote tumeona kuwa Mungu alianzisha jambo wakati ambapo alikuwepo mtu anaomba, Petro alipokuwa anaomba na Kornelio naye alipokuwa katika kuomba Mungu aliweka mfumo wa kuwakutanisha watu hawa na watu wa Kornelio wakajazwa Roho Mtakatifu, kazi ya Mungu ikazidi kuenea haya yote yalisababishwa na mtu Fulani kujichimbia katika chumba cha maombi na kutoa muda wake au hata kuacha kula na kuruhusu utendaji wa Mungu Roho Mtakatifu katika kazi yake ambaye kimsingi ndiye Bwana wa Mavuno!

Matendo 10:1-6 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.”

Matendo 10:9-13 “Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.”

Matendo 10:44-48 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.”

Watu wa Mungu wanapojichimbia mahali Fulani kuomba kwa bidii, Mungu husababisha matukio makubwa sana ya kushangaza, hufumua nguvu za utendaji na nguvu za Roho wake Mtakatifu na kusababisha uamsho mkubwa au kuleta muelekeo au kufungua mlango wa injili au kusababisha usikivu wa kiungu na kutoa melekezo na kusababisha mfumuko mkubwa sana wa kazi ya Mungu duniani, lakini haya yote husababishwa na watu wanaoomba yaani watu wanapojifungia katika chumba cha maombi na kuomba kwa bidii

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

Kwa hiyo pamoja na kanisa kuwa na mfumo wa huduma ya makanisa ya nyumbani ambayo kimsingi yanaweza kuwa yanakutana labda siku ya jumamosi (kulingana na makubaliano ya kanisa) na itakuwa vema basi siku kama alhamisi ikawa ni siku ya maombi kwaajili ya huduma zote za kanisa (Power House) huku jumatono ikiwa ni siku ya mafundisho na ijumaa ikiwa siku ya maombi na maombezi na jumapili ikiwa ni siku ya Bwana vyovyote kwa kadiri ya neema ya kila kanisa lakini nilisisitizalo mimi ni uwepo wa Nyumba za kuzalisha nguvu (Power Houses) na viongozi. Kanisa lolote lile linalotaka maendeleo bila ya kuwa na Power House haliwezi kuwa na mwanga, wala haliwei kuwa na uhai, wala hakutakuwa na harakati, na mpango kazi na mkakati wa kanisa itageuka kuwa mipango ya kawaida tu ya kibinadamu, kama unamtaka Bwana na nguvu zake basi anapatikana katika nyumba za maombi.(Power Houses)

Umuhimu wa kuwa na Nyumba za kuzalisha nguvu (Power house)

Mpaka hapo umeanza kupata picha kwamba ni muhimu kwa kanisa kuwa na vituo vya maombi, hata kama maombi hayo hufanyika ndani ya saa moja tu kati ya saa kumi na moja jioni hata saa kumi na mbili jioni, Lakini tunatambua sasa uhai wa kanisa lolote lile ni maombi, uamsho wa aina yoyote hauwezi kuendelea pasipo maombi, nguvu za Mungu na utendaji wa Mungu hauwezi kuendelea kuwepo katika kanisa bila ya maombi, hamna kitu kwa sababu hamwombi, lolote tunalilitaka lifanyike katika kanisa lazima kuwe na watu wanaooomba, maombi, maombi maombi.

·         Power House hufungua mbingu – Neno la Mungu linaonyesha kuwa Mungu huwa anafunga mbingu, habari ya kuzifunga mbingu ilikuwa inajulikana tangu zamani za kale nyakati za Biblia kuwa Mungu anaweza kuzifanya mbingu kuwa ngumu, anaweza kuzifunga wakati mwingine kama matokeo ya watu kutokutii lakini kupitia maombi inaonekana wazi kuwa Mungu anaweza kuzifungua mbingu:-

 

1Wafalme 8:35-39 “Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa; basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao; au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote; maombi yo yote au dua yo yote ikifanywa na mtu awaye yote, au na watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu maradhi ya moyo wake, na kuikunjua mikono yake kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote);”

 

Kumbukumbu 28:23-25 “Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma. Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie. Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.”

 

2Nyakati 7:13-15 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”

 

Neno la Mungu linaonyesha kuna wakati Mungu huzifunga mbingu, na hii maana yake sio kwaajili ya mvua tu lakini Mungu anaweza hata kuzifunga mbingu za mtu mmoja mmoja na hata mbingu za kanisa Fulani na kama tunataka kuona mkono wa Mungu ukitusaidia basi “Power houses” zinaweza kuwa sababu ya kufunguliwa kwa milango hii ambayo imefungwa, kwa nguvu za Maombi Mungu huzifungulia mbingu

 

Luka 3:21-22 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

 

·         Power House ni Chanzo cha nguvu za utumishi – Tumetumwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu hatari, ni kauli inayoonyesha kuwa watu wa Mungu wana maadui wasioonekna na wanaoonekana, kwa sababu hiyo kila aliyetumwa na Mungu alipewa nguvu kwaajili ya kukabiliana na upinzani tunaita Power encounter, shetani ni mpinzani wa injili, wachawi na kadhalika hatuwezi kwenda bila nguvu za Mungu na tunazihitaji nguvu za Mungu wakati wote na ni wapi tunaweza kupata/au kuzalisha nguvu kwaajili ya utumishi huu ni katika nyumba  za mombi “Power houses” ni chumba cha maombi ndicho kinachoweza kutupa nguvu na ujasiri wa kukabiliana na aina yoyote ile ya upinzani wa kiinjili na maendeleo endelevu ua utumishi tuliopewa

 

Luka 4:1-2 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.”

 

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

 

Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 

Mafundisho yetu ili yaweze kubadilisha maisha ya watu ni lazima yaombewe na kinyume cha hapo yatakuwa nadharia tu, huduma yetu ili iendelee kuleta matokeo chanya inapaswa kujaziwa na maombi, huduma ikifanyika bila ya maombi ya kutosha mwili tu ndio utakaokuwa umefanya kazi yake tunahitaji nyumba ya uzalishaji wa nguvu za Mungu katika maisha yetu ya kiroho ili mambo yaende!

 

·         Power House ni ulinzi wa Kanisa -  Ni muhimu kufahamu kuwa maombi pia hufanya kazi ya kuweka ulinzi wa rohoni, hutulinda na yule muovu, hutuepucha na majaribu, huzuia mashambulizi ya adui, hufunika wahudumu, watendakazi, wachungaji na familia zao na mali zao kwa hiyo tunayahitaji maombi kama tunavyohitaji maji ya kunywa , Lazima watu waombe na kusimama katika zamu yao kama walinzi wa rohoni

 

Matendo 12:5-7 “Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.”

 

Mathayo 6:13 “ Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]

 

Mathayo 26:40-41 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”

 

Habakuki 2:1-3 “Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.”       

 

·         Power House huvunja minyororo – Maombi ni silaha ya kiroho inayovunja vunja nira yaani vifungo na minyororo ya aina mbalimbali, maombi huwatoa watu utumwani na kuwaweka huru walikandamizwa, yanaondoa mizigo mizito na kuwapa watu uhuru na raha ya kiungu, yanavunja laana ya kizazi na kizazi, kurejesha uhuru wa kiroho, upako huo wa kuvunja nira unapatikana kwa njia ya maombi, maombi yanaweza kufungua mpaka magereza za kawaida  na kuvunja hata nira za chuma

 

Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.”

 

Isaya 58:6 “.Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

 

Matendo 16:25-31 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”             

 

·         Power House ni nguvu ya kupokea maelekezo na muelekeo – hatuwezi kwenda wenyewe, hatuwezi kwenda peke yetu, tunamuhitaji Mungu atupe muelekeo na maelekezo katika kazi yake ni katika wakati wa kuomba mbele zake na utulivu ndipo ambapo Mungu hutupa muelekeo na maelekezo, kwa hiyo kanisa ni muhimu kwetu kuwa na vituo vya kuzalisha nguvu yaani Power House ili tusiongozwe na mawazo yetu bali tuongozwe na Roho Mtakatifu ili tuweze kuifanya kazi yake kwa usahihi, kanisa lisilo na power house huongozwa na mawazo ya wanadamu na kanisa lenye power House huongozwa na Roho Mtakatifu

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

Matendo 16:6-10 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.”                

Huduma katika vituo vya kuzalisha nguvu (Power House)

Watenda kazi wetu, wahudumu, wanafunzi na wenye hekima wote wanapaswa kusimamia kwa uaminifu vituo vya maombi ya kuzalisha nguvu kokote viliko, ni afadhali kitu kingine kisimame lakini sio maombi Kanisa hatuna budi kuhakikisha kuwa maombi yetu yanakuwa endelevu, na tuone kusimama kwa maombi kama kusimama kwa moyo katika mwili wa mwanadamu ndio maana maombi yanapaswa kuendelea “Ombeni bila kukoma”, watu wote waombaji wanapaswa kuwa watu wa toba, wenye kujitia nidhamu kwaajili ya kuomba, wanaopenda kusihi maisha matakatifu, wenye tabia ya unyenyekevu na wanaojua kukaa kimya mbele za Mungu, aidha waombaji hawapaswi kuwa na midomo michafu kwa sababu midomo hiyo hiyo ndio inayotumika kuomba hivyo haifai kutumika kwenye mambo mengine hasa yasiyofaa katika mapenzi ya Mungu.

Yakobo 3:10-12 “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu.”

Watendakazi wetu walioandaliwa katika shule za uongozi na huduma ndio watakaohusika na kituo cha kuongoza maombi ya Power house maombi haya yataongozwa kila wakati katika siku na muda utakaokuwa umepangwa na kanisa

1.       Toba litakuwa jambo  la kwanza na la muhimu katika maombi

2.       Kurekebisha Mahusiano kutakuwa ni jambo muhimu katika hatua za maombi

3.       Kufunga itakuwa ni sehemu mojawapo ya muhimu katika maombi yetu

4.       Shukurani itakuwa ni sehemu muhimu ya maombi

5.       Toba za kila mtu binafsi, kwa niaba ya kanisa na kwaniaba ya taifa itahusika

6.  Tutaomba uwepo wa Mungu, Nguvu zake, huduma na kuombea wachungaji watumishi wote na watendakazi, Mungu awalinde awatumie na kuwapa afya njema

7.       Tutakemea na kuvunja nguvu za giza, kukemea mapepo na kutangaza ushindi

8.    Tutaombea kanisa, miji yetu na taifa, tutamuomba Mungu aponye wanaoteseka na kufanya ishara na miujiza akichochea karama za Roho, aokoe na kuponya na kurahisisha kazi yake kotekote

9.       Tutamsikiliza Mungu na kukaa kimya kusubiri maelekezo yake   

Power house ni tofauti na kikundi maalumu cha maombi, hii ni kiungo au kiwanda cha kuzalisha waombaji katika kanisa hivyo inapaswa kulishirikisha kanisa zima katika mfumo kama ule wa makanisa ya nyumbani,  Neno la Mungu linapaswa kuwa muongozo wa maombi haya, “Power house” sio mashindano ya kuomba, wala sio sehemu ya kujitukuza na kuonyesha uhodari wa kuomba, wala sio sababu ya kutokutii uongozi wa kanisa, ni kituo cha nidhamu kinachoomba kwaajili ya maswala mbalimbali ya kazi ya Mungu, hakipaswi kuwa chanzo cha machafuko, ni sehemu ya upendo kwa Mungu na kwa kazi yake, ni ushirika wa maombi ya washirika wote na wageni wanaopenda kujiunga kuomba nasi, Bwana ampe neema kila mtenda kazi kulijua hili na kulifanyia kazi katika jina la Yesu Ameen

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: