Jumamosi, 22 Agosti 2026

Huduma ya wanawake Katika Kanisa!


Luka 8:1-3. “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba Kanisa lisipowatambua wanawake kama sehemu muhimu ya huduma linaweza kupoteza sehemu kubwa sana ya nguvu zake ambazo Mungu ameziweka katika mwili wa Kristo, Maandiko yanaonyesha kuwa nyakati za Biblia wanawake hawakuwa watazamaji tu wa maswala ya imani na badala yake walikuwa mstari wa mbele katika kumtumikia Mungu kwa maombi, kushuhudia, kulea, kufundisha na kuihubiri injili, lakini sio hivyo tu walimtumikia Mungu kwa huduma na kwa kutoa mali zao na kuwa sehemu muhimu na baraka kubwa sana kwa injili.

Marko 15:40-41 “Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome;hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.”

Unaona tunajifunza hapo kwamba wanawake waliookoka sio watu wanaopaswa kukaa tu kanisani bila kufanya kitu, wanawake nao wanapaswa kumtumikia Mungu na kushiriki bega kwa bega katika huduma huku wakitumia karama zao, wito, mzigo waliopewa kutimiza jukumu walilopewa katika ufalme wa Mungu, wanawake waliomwamini Yesu walianza kumtumikia mara moja hata kabla ya kuanza kwa kanisa, walishirikiana naye kwa hali na mali, na bega kwa bega kusaidia huduma, Kwa msingi huo basi leo katika maswala ya huduma tutajifunza somo hili muhimu Huduma ya wanawake Katika Kanisa! Kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu viafuatavyo:-


·         Umuhimu wa huduma ya wanawake katika Kanisa.

·         Huduma ya wanawake katika kanisa.

·         Mambo yanayoweza kufanywa na wanawake katika jamii ya kanisa.


Umuhimu wa huduma ya wanawake katika Kanisa

Huduma ya wanawake katika kanisa kwa ujumla tunazungumzia ushiriki wa mwanamke katika kulitimiza au kutekeleza agizo kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, na katika kuujenga mwili wa Kristo, wanawake ni nyenzio Muhimu katika huduma na katika kuendeleza kazi ya Mungu duniani sawasawa na karama walizopewa, wakati Yoeli anatabiri kuhusu kuachiliwa kwa Roho Mtakatifu kwaajili ya utumishi kila kundi liliguswa kama watumishi wa Mungu wakiwepo wanawake:-

Yoel 2:28-30 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu. Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.”

Kwa sababu hiyo Wanawake ni sehemu muhimu ya dunia hii, ni sehemu muhimu ya uumbaji wa Mungu na waliumbwa kwa kusudi kubwa la kipekee katika mpango wa Mungu na ni wasaidizi wa ajabu sana kwa sababu hiyo wanahusika katika kusudi na mpango wa Mungu si kama watu wa pembeni bali kama watu wanaojumuishwa kwa umuhimu wao katika jamii kumletea Mungu utukufu, uko ukweli usio wa kitafiti ya kwamba mtumishi wa Mungu awaye yote anapoanza Kanisa utaweza kuona wenye kuonyesha muitikio kwa injili kwa haraka zaidi ni wanawake na wao hufanya idadi kubwa ya washirika kanisani na kwa sababu hiyo karibu nusu na zaidi ya idadi ya washirika katika kanisa ni wanawake sasa basi tunawezaje kuwapuuzia watumishi hawa wa Mungu ambao hawabaguliwi kwa lolote katika maandiko?

Wagalatia 3:26-29 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”

Kwa msingi huu pamoja na changamoto za kiutamaduni kuhusu wanawake, ukweli unabaki wazi kuwa wao ni sehemu kubwa ya kanisa, wahudhuriaji wazuri wa ibada, wako mstari wa mbele katika kuipokea imani na hivyo inaweza kuwa hasara kubwa sana kama hatutawekeza injili na mafundisho kwao kwa sababu Mungu hajawahi kuwapuuzia katika mpango wake wa ukombozi kwa mwanadamu hata ahadi ya ukombozi wa Mwanadamu walipewa

Tito 2:1-5 “Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

Huduma ya wanawake katika jamii na kanisa inaweza kuwa na mkono mrefu zaidi katika kurahisisha huduma ya kichungaji hata kwa kuyafikia mahitaji muhumu ya kimwili na kisaokolojia ya wanawake, utafiti unathibitisha ya kuwa asilimia 73% ya mahitaji  ya kiroho na kijamii ya wanawake yanaweza kuratibiwa na kuhudumiwa na wanawake kwa kiwango kikubwa zaidi, mfano changamoto za Mimba kuharibika, kuhudumia mwanamke aliyebakwa, kuhudumia wenye ukomo wa siku za hedhi, hoja za ukatili wa majumbani, maswala ya ndoa, maswala ya kuvurugika kwa homoni, huduma za kujifungua, mfadhaiko wa wanawake, changamoto za kutokwa na damu, wakati mwingine hayawezi kutatuliwa wala kushughulikiwa vizuri na kwa ubora na watumishi wa kiume, na wanawake wenyewe pia wanaweza kujisikia aibu kujielezea vizuri kwa watumishi wanaume na hivyo mwanamke anahitajika asimame katika nafasi yake ili kusaidia kuyafikia mambo ya kike katika jamii, kwa msingi huo utakubaliana nami pia kuwa wanawake wanahitajika na wana wajibu mkubwa wa kuitikia wito wa kupata ufahamu na kutumika na kamwe tusiwabague.

Huduma ya wanawake katika kanisa

Luka 8:1-3. “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”

Katika nyakati za zamani hususani nyakati za karne ya kwanza wanawake hawakupewa kipaumbele sana katika jamii nyingi duniani ikiwepo jamii ya Kiyahudi, wanawake walikuwa na nafasi ndogo sana katika shughuli za kijamii na kielimu na hata kihuduma, hata hivyo tunaona Mungu aliwapa nafasi ya kutumika na Pia Bwana Yesu, akiwafundisha kuwahudumia, kuwaponya na hata kuwaacha wafuatane naye katika huduma huku wakifanya utumishi wao kumuhudumia Bwana Yesu. Katika andiko la Msingi wanatajwa Mariam Magdalene, Yoana, Susana na wanawake wengine wengi waliomtumikia Yesu na wanafunzi wake tena walitumia mali zao, sio hivyo tu wanawake wengi walitumiwa kwa kazi mbalimbali wakitumiwa kama Baraka katika jamii na wahusika wakuu katika imani, wako wanawake wengi lakini hapa tutaangalia wachache tu kama sehemu ya mfano:-

Debora – Moja ya waamuzi muhimu sana ambaye alikuwa wa kiroho zaidi ya waamuzi wote wanaotajwa katika maandiko, mwanamke huyu aliwamua Israel lakini pia alikuwa ni nabii aliyetambua mapenzi ya Mungu na kujua nini kinachopaswa kufanyika, alimtia moyo Baraka kupigana vita ya ukombozi dhidi ya uonevu wa watu wa Mungu ona

Waamuzi 4:4-9 “Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue. Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.”      

Esta – Anakumbukwa kama mwanamke shujaa aliyesimama mstari wa mbele katika kuwakomboa na kuhakikisha usalama wa wayahudi huko Shushani Ngomeni, alihatarisha maisha yake, alifunga na kuomba alijitia ujasiri lakini alikuwa tayari kuangamia kwaajili ya jamii ya watu wake Mungu alimtumia kama mkombozi aliyewasaidia Wayahudi

Esta 4:13-16 “Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo? Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai, Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.”

Mariam mama yake Yesu – Ni mwanamke mwenye moyo wa kishujaa, aliyekubali kubeba mimba katika mazingira ya tamaduni ngumu sana na hivyo kuhatarisha maisha yake ndoa yake na kustahimili aibu ya uanawali wake kwa sababu ya kukubali kujitoa kubeba kusudi la Mungu kwa kukubali kumbeba mwokozi wa ulimwengu huu tumboni mwake (kumbuka ilikuwa ngumu sana kueleweka kuwa ana mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu)

Luka 1:26-38 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” 

Lidia – Mwanamke wa kwanza kupokea injili kule Ulaya, yeye aliishikia injili na kuyatunza maneno ya Bwana, alikuwa mtu muelewa na aliwakaribisha wahubiri wa injili nyumbani kwake na kuruhusu kazi ya huduma ifanyike kule Makedonia

Matendo 16:13-15 “Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.”          

Prisila – Alikuwa ni mwanamke mtenda kazi pamoja na Paulo Mtume yeye na mumewe Akila na anaonekana kuwa alikuwa mwalimu mzuri sana wa neno la Mungu wao walimsaidia Apolo moja ya walimu maarufu sana wa nyakati za kanisa la Kwanza kuijua njia ya Mungu kwa usahihi zaidi hivyo kuiboresha huduma yake kwa kiwango kikubwa sana na katika jamii ya makanisa

Matendo 18:24-28 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”

Kwa ujumla tungeweza kuona wanawake wengi sana na mchango wao mkubwa katika imani na jinsi Mungu alivyowatumia kwa shughuli mbalimbali za kiimani, kubwa zaidi tunajifunza ya kuwa Mungu anawatumia wanawake katika kila kizazi bila kuwapuuzia kusimamia wajibu wa kibiblia na kihuduma katika kuifanikisha kazi hii iliyo njema ya Mungu na ufalme wake, kwa sababu hiyo kanisa halipaswi kupuuzia umahiri wa wanawake katika utumishi wa aina mbalimbali na kwa sababu hiyo tuwahimize, tuwafundishe na tuwaamini  na kutambua mchango wao katika maeneo mbali mbali ya kihuduma hata yale yasiyoonekana

Mambo yanayoweza kufanywa na wanawaje katika jamii ya kanisa

Luka 8:1-3. “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”

Wanawake ni watoaji – Moja ya utumishi mkubwa walionao wanawake na ambao wanaweza kuufanya kwa kiwango kikubwa sana kwa asili na kivitendo ni Kumuhudumia Mungu kwa mali zao, unaweza kuona katika huduma ya Bwana Yesu wanawake kadhaa wanatajwa hapo na wengine wengi na Luka anahitimisha kwa kuonyesha kuwa walikuwa wakimuhudunia Mungu kwa mali zao, hii ni ishara ya dhahiri kuwa unapozungumzia swala la utoaji unaweza kuona wanawake wanaongoza kwa utoaji makanisani na katika maandiko hata kuliko wanaume kimaumbile na kwa kadiri ya mkao wa moyo wao, Biblia imejaa mifano kadhaa ya wanawake waliojihusisha na utoaji katika Biblia wakiwemo:-

·    Mwanamke mmoja mjane – Mwanamke mmoja aliyetoa senti ndogo sana na ya mwisho katika sadaka yake wakati Yesu anafuatilia utoaji hekaluni, aliuona Moyo wa mwanamke huyu kuwa ingawa alikuwa masikini na hakuwa na kitu lakini alijitoa kwa moyo wake wote kile kidogo alichokuwa nacho kwa sababu ya upendo wake mkubwa kwa Mungu ona:-

 

Marko 12:41-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”

 

·   Mwanamke mjane wa Sarepta – Ni mwanamke ambaye hakuwa na kitu kikubwa sana lakini alikuwa na moyo wa utoaji, Moyo wa kumtolea Bwana na kuweka kipaumbele maswala ya Mtumishi wake, hakuwa na ubinafsi alimheshimu mtumishi wa Mungu Eliya, na mwanamke huyu Mungu mwenyewe alisema amemwagiza amlishe mtumishi wake utoaji wake wa kimuujiza ulimfanya mwanamke huyu asipungukiwe na kitu kwa muda mrefu

 

1Wafalme 17:8-16 “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.”

 

·      Mwanamke Mshunami – alikuwa ni mwanamke mwenye ukarimu, aliamua kumkarimu mtumishi wa Mungu Elisha na kumuhudumia kwa chakula na hata kumjengea chumba maalumu cha mapumziko awapo safarini mwanamke huyu alikuwa na imani kuwa mtu yule ni mtu wa Mungu na anastahili kukirimiwa kama Huduma.

 

2Wafalme 4:8-17 “Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula. Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo. Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala. Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake. Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe. Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.”

 

·   Mwanamke aitwaye Thabita au Dorkasi – Alijulikana sana kwa matendo yake ya ukarimu na utoaji, alitoa muda wake mwingi na nguvu zake akifanya kazi za mikono kwa kufuma ili kuwasaidia masikini na kuwavika wajane kiasi kwamba hata alipokufa msiba wake uliwagusa wengi na Mungu alifanya Muujiza wa kumfufua kupitia Petro

 

Matendo 9:36-39 “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.”

 

·    Mariam Magdalene, Yoana na Suzana - Wanatajwa na wanawake wengine kuwa walimtumikia Mungu kwa mali zao, unapoyachunguza maandiko utaweza kubaini ni kama huduma hii ya utoaji japokuwa inatuhusu wote lakini imetajwa katiika maandiko mara nyingi ikionyesha kuwa ni wanawake ndio waliongoza katika swala zima la kumtolea Mungu kwa hiyo wanawake ni watoaji wazuri sana kuliko wanaume katika ibada na utumishi

 

Luka 8:1-3. “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”

Wanawake ni waombaji – Ingawa neno la Mungu linatoa wito kwa kila mtu wa Mungu kuwa na tabia ya kuomba, na wanaume wengi katika maandiko walikuwa waombaji, hata hivyo wako wanawake ambao wanaonekana kuwa walikuwa na rekodi ya kuomba na maombi yao kuwa na matokeo makubwa sana, Neno la Mungu linaonyesha kuwa zamani nyakati za Biblia wanawake walitumiwa kama viongozi na watu wenye ujuzi wa kuomboleza wakati kunapotokea majanga na huzuni au hata misiba, wanawake waliitwa kuiongoza jamii katika maombolezo, hii ni kwa sanabu wao walikuwa na ujuzi mkubwa wa kuomboleza wakiwa na uwezo mkubwa wa kuinua sauti kulia na kuimba na kusababisha maombolezo yaliyogusa mioyo, aidha waliongoza familia nzima au taifa au mji mzima kuonyesha majonzi wakati wa vifo majanga na hukumu ya Mungu, au wakati majanga yanaikaribia jamii pia walifundisha binti zao na watu wengine jinsi ya kulia na kuomboleza wakati wa hali ngumu, Maombolezo haya yakielekezwa katika mfumo wa kimaombi yanaweza kuleta matokeo makubwa katika jamii, maombi ya wanawake kadhaa katika maandiko yalisababisha matokeo

Yeremia 9:17-19 “Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji. Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.”

·    Hana - alipitia ugumu wa kupata mtoto lakini kwa vile alikuwa mwombaji Mungu alimjibu kwa kumpa nabii Samuel ambaye alitokea kuwa Baraka kubwa sana kwa Israel, ni katika wakati wa Samuel Taifa lili imarika na kuwa na uamsho mkubwa wa kifalme kuanzia Sauli mpaka Daudi; Baraka hizi zililijia taifa kwa sababu ya maombi ya Hana.

 

1Samuel 1:10-11 “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.”            

 

·    Anna Binti Fanuel – Mwanamke wa mfano wa kuigwa ambaye inaonekana alikuwa mwombaji kuliko waombaji wote waliopata kuorodhesha katika maandiko ana alikuwa mjane  na pia alikuwa mtu mwenye umri mkubwa lakini hata hivyo maandiko yanaonyesha kuwa alikuwa mwenye uwezo mkubwa katika kufunga na kudumu katika maombi uwezo wake katika kuomba unatudhihirishia ya kuwa wanawake wanauwezo mkubwa sana kushiriki katika maombi na kusababisha matokeo, Anna Binti Fanuel  alimjua Yesu Kristo wazi wazi baada ya kuzaliwa kwake na alipowasili Yerusalem Hekaluni aliwatolea watu habari zake.

 

Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”

Wanawake ni walimu wazuri wa neno la Mungu – Maandiko yanaonyesha wazi kuwa wanawake wakiwa wacha Mungu, na wakiwa na ujuzi wa maandiko maana yake wana uwezo mkubwa sana wa kuipitisha imani hiyo kwa wengine kwa kuwafundisha na hata kuhubiri injili wanawake wamekuwa waalimu wa watoto wengi makanisani,  na nyumbani pia, lakini pia wanaweza kutumiwa kuimarisha wanawake wachanga katika maswala ya malezi na kusimamia nyumba zao vizuri, Biblia inaonyesha ujuzi wao wa kufudisha na kuhubiri katika namna mbalimbali

·       Wanaweza kuwafunza wengine namna ya kulea na kuzihudumia ndoa zao – Tito 2:3-5 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

 

·     Wanaweza kuwaelekeza wengine na kuwafundisha kukaa katika imani kwa usahihi – Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”

 

·     Wanaweza kutumiwa katika kushuhudia na kuhubiri habari njema – Yohana 4:28-39 “Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?Basi wakatoka mjini, wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule.Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.”

 

Mathayo 28:5-7. “Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa.Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.”

 

·    Wanaweza kutumiwa kuirithisha imani na ujuzi wa neno la Mungu kwa watoto wao – 2Timotheo 1:4-6 “Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.”

Wanawake wanaweza kuwa viongozi na watenda kazi pamoja nasi - Wanawake wanaweza kuwa viongozi katika kanisa na kuwa na mchango mkubwa kwa watu wengi, nyakati za kanisa la Kwanza Fibi alitambuliwa na Paulo mtume kama moja ya watumishi katika kanisa lililokuwako Kenrea na aliaminiwa na hata kutumiwa kupeleka waraka mmojawapo wa Paulo huko, tunajua katika lugha ya Kiingereza Fibi kuwa ni Mwanamke kwa sababu anatajwa kwa neno “She” badala ya “He” aidha wanawake wanaweza kutumika kama viongozi wa makanisa ya nyumbani na kadhalika katika huduma nyingine za kichungaji na kinabii.

·     Fibi - Warumi 16:1-2 “Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea; kwamba mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu; mkamsaidie katika neno lo lote atakalohitaji kwenu; kwa sababu yeye naye amekuwa msaidizi wa watu wengi, akanisaidia mimi pia.”

 

·  Lidia - Matendo 16:14-15 “Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.”

 

Wanawake wanaweza kuongoza sifa kwa asili – Maandiko yanaonyesha kuwa wanawake pia ni viongozi hodari wa kusifu, Maandiko yanaonyesha kuwa nabii mke Miriam aliongoza watu katika kumsifu Mungu  na kuimba wimbo wa ushindi mara baada ya Israel kuvuka bahari ya shamu, na pia tunamuona Deborah akiongoza sifa wakati wa waamuzi  baada ya ushindi dhidi wakanaani, akliwa na Baraka na Hana baada ya kujaliwa kuzaa mtoto Samuel alitunga shairi zuri sana la kumsifu Mungu, Na Mariam baada ya kupewa habari na malaika kuwa atamzaa mwokozi wa ulimwengu aliimba sahairi la aina yake, hawa ndio wanawake wanne wanaotajwa katika Biblia wakijihusisha na kumsifu Mungu na  waliomwimbia Bwana na kuonyesha kuwa wanawake wanaweza kufanya huduma ya kuimba sifa na kuiongoza

·   Miriam - Kutoka 15:20-21 “Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza. Miriamu akawaitikia, Mwimbieni BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.”      

 

·      Debora – Waamuzi 5 1-5 “Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema; Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana. Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli. Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji. Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli.”

·       Hanna – 1Samuel 2:1-10 “Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani. Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake.Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.”

 

·         Mariamu mama yake Yesu – Luka 2:46-45 “ Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake;Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele.”

Wanawake wanaweza kufanya kazi kubwa mbalimbali katika mwili wa Kristo – Mungu anaweza kuwatumiwa wanawake kwa karama mbalimbali, na kutoa pepo, anaweza kuwatumia kuhubiri, kufundisha kufungua makanisa, kushuhudia lakini pia wanawake wanaweza kuifanya kazi ya Mungu kwa bidi; Paulo mtume anawasalimia watendakazi kadhaa katika waraka wake kwa Warumi huku akiwataja wanawake ambao walikuwa na bidii na wenye kujitahidi sana katika kazi ya Mungu.

·  Warumi 16:6 -12 “Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu. Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana. Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu. Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika Kristo. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo. Nisalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana. Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana.”

Mungu hajamuokoa mwanamke ili awe mtazamaji katika ufalme wa Mungu, wanawake ni washiriki wenza katika kusudi na mpango wote wa Mungu, kila mwanamke anapaswa kuwajibika na kuongeza bidii katika kumtumikia Mungu, wanawake wanapaswa kujiamini, wanapaswa kuwa na ujasiri, wanapaswa kutumia vipawa na karama walizopewa na Mungu na wanapaswa kukumbuka kuwa Mungu hana upendeleo, tumia kila ulichonacho na utumishi wote na huduma zote zinazoelekezwa katika kanisa fanya huku ukiijenga famlia yako, kulihudumia kanisa na kutangaza habari njema.

Kanisa lenye wanawake waombaji ni kanisa lenye nguvu, Kanisa lenye wanawake wanaolijua neno ni kanisa imara, Kanisa lenye wanwake wanaohubiri ni kanisa linalokua kwa kasi, kanisa lenye wanawake wanaofundisha vijana ni kanisa lenye watu wenye nidhamu, kanisa lenye wanawake wahuburi ni kanisa linalosambaa, kanisa lenye wanawake wanaotoa  ni kanisa linaloweza kuisukuma kazi ya Mungu na kuwatunza watumishi vema, kanisa lenye wanawake watakatifu ni kanisa lenye ushuhuda wenye nguvu, tunataka kanisa letu liwe na wanawake imara sana katika imani

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.      

Hakuna maoni: