Jumamosi, 24 Juni 2017

Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume:



1Timotheo 2: 12Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.”
 
Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Agano jipya liko wazi kabisa katika mafundisho yake kuhusu nafasi ya mwanamke, kama ilivyo ya mwanamume katika utumishi wake kwa Mungu, wanawake wamepewa Karama za rohoni kama ilivyo kwa wanaume 1Wakoritho 12:7-11, wote wanatumiwa na Mungu katika kuujenga mwili wa Kristo 1Petro 4:10, Huduma za wanawake ni muhimu katika kanisa kama na zina mchangoi mkubwa katika ujenzi wa mwili wa Kristo na hilo halina shaka yoyote, 1.Wakoritho 12:12-26, Kuna mifano mingi sana katika Agano jipya jinsi Mungu alivyowakirimia wanawake na kuwatumia katika kumtumikia Mungu.

Je lakini agano jipya limewakataza wanawake kuwa makasisi yaani kuwa wachungaji? Hili linawezekana lakini litakuwa fundisho lenye utata mkubwa, kutokana na mitazamo mbalimbali ya wanatheolojia, kwa mfano Makanisa makubwa ya zamani, likiwemo kanisa la Orthodox wamekataa na kupinga wanawake kuwa wachungaji kutokana na sababu ya tafasiri ya 1Timotheo 2:8-15, Katika mistari hiyo Biblia inasema hivi;- “Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano. Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu. Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.  Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.  Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi”.

Swala kubwa katika mabishano ya kitheolojia ni je Mwanamke anaweza kuwa Mchungaji? Au Mwanamke anaweza kuwa Kuhani kwa wayahudi, au mwanamke aweza kuwa Rabbi kwa wayahudi na je mwanamke aweza kuwa sheihk kwa waislam? Maswali hayo yote yakijibiwa kwa ufasaha yanaweza kuleta jibu muafaka kama wanawake wanaweza kuzishika nafasi hizo nyeti katika imani, licha ya kuwa Mungu anaweza kuwakarimia karama zilezile ambazo wanaume wanaweza kuwa nazo bila upendeleo.

Swala la wanawake kuwa makuhani Priest ni lenye utata hata katika jamii ya kiyahudi na ni swala la kihistoria ambalo ni vigumu kulitolea maamuzi thabiti kwa sasa na katika mada fupi kama hii



Pichani mwanamke wa Kiyahudi anayefanya kazi za kikuhani, jambo hili limewagawa Wayahudi kwamba wako wanaopinga na wako wanaokubaliana 

Ujumbe:
1Timotheo 2: 12Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.

Tunaporejea katika ujumbe wangu wa leo Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume Mimi kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima nataka kuzungumzia mada tofauti na ile ambayo nimeigusia katika utangulizi wangu, mimi nataka kutafasiri andiko hilo hapo juu na kisha kuleta fundisho ambalo linaweza kuleta unafuu katika ndoa zetu na kutupa amani
Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Katima mstari huu ukiacha mjadala wa mwanamke anaweza kuwa kasisi au la, kuna jambo la msingi linalofunuliwa na andiko hili katika uhusiano wa wanandoa, mstari huu katika lugha ya kiingereza unasomeka namna hii katika matoleo tofauti ya biblia mfano

 KJV inasema “But I suffer not a woman to teach, nor to usurp authority over the man, but to be in silence” NIV inasema “I do not Permit a woman to teach or to have authority over a man; She must be silent. Maneno teach na neno Authority au Usurp yote yanabeba maana moja katika biblia ya kiyunani neno linalotumika hapo ni kama to have authority au to usurp ni neno “authentein”ambalo maana yake ni to take position au to have a power without the right to do that au to have control au Dominate. 

Katika lugha yetu ya Kiswahili neno “Kufundisha na kumtawala”katima maana ya kibiblia hapo yana maana moja ambayo ni kutawala, au kushikisha adabu au kuwa na nafasi ya juu kuliko mwanaume katika madaraka ya nyumba na kanisa, fundisho langu kuu leo linalalia katika kutawala mume kwa maana ya madaraka au mamlaka katika ndoa.

Katika nyakati hizi za kidigital wanawakwe wengi na hata wanaume wamekuwa wakisahau wajibu wao katika ndoa na hivyo kusababisha madhara makubwa na mafarakano na hata kuweko kwa talaka, moja ya tatizo kubwa ambalo ndio ningependa kulizungumzia leo ni wanawake kuwatawala waume zao, jambo hili inawezekana umewahi kulishuhudia, au linakutokea au umewahi kuwasikia watu wakisema na wakati mwingine hata wanawake wenyewe wakijisifu kuwa wamewaweka kiganjani waume zao je jambo hili lina mustakabali gani kibiblia?

·         Kwa nini wanawake wanataka kuwatawala wanaume?
·         Kwanini baadhi ya wanawame tayari wanawatawala waume zao?
·         Kwanini kweli wako wanaume wanatawaliwa na wake zao na hawawezi kukohoa au nkusema lolote mbele zao?
·         Kwa nini wanwake ndio wamekuwa mabwana na watawala wa waume zao?

Ni imani yangu kuwa utakuwa umelishuhudia hili katika ulimwengu huu tulio nao duniani, utakuwa umeshuhudia kwa kiwango kikubwa kuwako kwa hamasa kubwa ya wanawake kuwatawala wanaume na kuwaweka chini ya udhibiti wao, wanawake leo wanafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha wanawatawala waume zao, na kuwa ndani ya nyumba hakuna anayekohoa isipokuwa mwanamke, leo nataka kutoa jibu au majibu ya sanbabu hii ya changamoto kubwa inayojitokeza na kuharibu jamii.

Nataka kama mkuu wa wajenzi kujibu kwanini wanawake wanataka kuwatawala wanaume?

1.      Ni mpango wa shetani mwanamke kumtawala mwanamume.

Ni muhimu kwanza tukajenga msingi wa kiroho wa kuona kilichompelekea Paulo mtume kuzungumza swala hili angalia 1Timotheo 2: 12-15 biblia inasema;-
Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi”. 

Paulo mtume anatoa sababu za katazo lale kwa nini hataki mwanamke kumtawala mwanamume anaweka wazi sababu za kimaumbile kwanza akisisitiza kuwa Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza na Hawa baadaye, hii inamaanisha kimaumbile tu mwanamume ni kiongozi, yeye ndiye aliyeumbwa kwanza na Hawa alifuata baadaye, katika bustani ya Edeni aliyepokea maelekezo ya kwanza ya kutokula mti wa matunda yaliyokatazwa alikuwa mwanaume, na mwanaume hakudanganywa kwanza maana yake mwanaume alikuwa na msimamo, ndiye kiongozi ndiye mzaliwa wa kwanza kisha mwanamke aliumbwa baadaye.

Pili Paulo mtume anaeleza habari za utendaji wa kazi wa shetani, kwamba shetani hakumfuata kwanza mwanamume, alimfuata mwanamke, shetani alijua udhaifu aliokuwa nao mwanamke, aliutumia kumdanganya na kwa kuanza nayeye alileta uharibifu kwa familia nzima na aina binadamu wote leo ulimwenguni, kwa mtindo huo huo shetani ataendelea kuwatumia wanawake duniani kupitia udhaifu wao kuleta maanagmizi katika familia na kanisa kwa ujumla.

Mungu aliona katika mpango wake kuwa ili mwanamke awe salama anapaswa kuwa chini ya mumewe anapaswa kujinyenyekesha chini ya mumewe angalia Mwanzo 3:16Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”

Katika maandiko hayo Mungu alitangaza adhabu atakayokuwa nayo mwanamke kutokana na anguko na moja ilikuwa ni kuzidishiwa kwa uchungu wake, na  pili kwa utungu utazaa watoto na tatu tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.

Katika mgogoro huu uliotangazwa na Mungu ni muhimu kukumbuka kuwa ni mgogoro wa milele ambapo kila saa na kila wakati wanwake watajaribu kuwatawala wanaume moja kwa moja au kwa namna nyingine kama tutakavyoona katika vipengele vingine.

KJV inasema ;-

Unto the woman he said, I will greatly multiply thy sorrow and thy conception; in sorrow thou shalt bring forth children; and thy desire shall be to thy husband, and he shall rule over thee
. 
Kutokana na mwanamke kudanganywa na ibilisi, biblia inaonyesha kuwa Mungu ataongeza uchungu wa mwanamke, yaani huzuni, lakini vilevile uchungu wakati wa kuzaa na zaidi tamaa yake itakuwa kwa mumewe na mumewe atamtawala

“Tamaa yako itakuwa kwa mumeo na mumeo atakutawala” katika maneno haya Mungu yu aonyesha kuwa wanawake watakuwa na tamaa ni tamaa gani hii sio tamaa ya ngono ni tamaa ya kuwatawala wanaume lakini matokeo yake mumewe atamtawala Mungu alitangaza mgogoro hapa kuwa mwanamke atashawishika kutaka kumtawala mwanaume na matokeo yake yatakuwa mabaya kwa sababu Mungu ameandaa utawala kwa mwanaume, kwa sabubu hiyo kiu nya wanawake kutaka kuwatawala wanaume inachochewa na shetani kuiinua nia iliyoko ndani yao Mungu alikuwa anaonyesha njia ya amani kwa mwanamke ni kunyenyekea na kukubali kutawaliwa na mumewe
Mara zote chanzi kikubwa cha migogoro hutokea pale nyumba inapokuwa na mwanamke mtawala, wanawake wengi hupigwa na hata kupewa talaka kwa sababu ya kutaka kutawala waume zao, pale wanapojaribu tu kuwa juu ya waume zao, mgomgoro unaibuka na kuanza, Mungu katika hekima yake alitaka kuwasaidia wanawake wapate kutambua kuwa njia pekee ya wao kuwa na mafanikio katika ndoa zao ni kuwa wanyenyekevu. 1Petro 3:1aKadhalika ninyi wake, watiini waume zenu;” mwanamke awaye yote anayetaka kuheshimika na kupendwa na kuthaminiwa katika ndoa yake ni muhimu akakubali muongozo huu wa upenndo wa kiungu.

2.      Ni kwa sababu ya malezi toka kwa mama yake.

Nyani hujifunza kuogopa nyoka pala wanapoona nyani wengine wakiogopa nyoka na kutetemeka, wanadamu pia hujifunza kutoka kwa wanadamu wengine, kama mwanamke amekulia katika mazingira ambayo mama ni mtawala wa mumewe hali kadhalika binti  yake au zake wanauwezo wa kukua katika tabia na mwenedno huo huo Biblia inaonyesha hivyo wazi katika Ezekiel 16:44-45Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.  Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.”  Kama mama atakuwa mwanamke mtawala na binti yake atakua akiwa na mtazamo huo na hapo ndipo mafanikio huweza kuwa hatarini katika nyumba na familia za aina hii 
      
3.      Kutokana na kutokujiamini.

Hili ni tatizo la kiroho na kisaikolojia kama mwanamke hajiamini huanza kuwadibiti wengine yaani kuwatawala ili kwamba ajisikia yuko salama kitaalamu ningesema “when someone feels insecure he might start to control others in order to feel in control once again” Saikolojia sio kama 1+1=2, kwa hiyo hapa simaanshi kila mwanamke mtawala anakuwa na tatizo la kutokujiamini HAPANA lakini  mara nyingi wanawake wasiojiamini watajaribu kujiweka huru na salama kwa kujaribu kudhibiti mazingira yanayomzunguka na ikiwezekana atamjumuisha na mumewe.

4.      Kujichukia au kuchukia jinsia yake.

Tatizo hili ni tatizo la kisaikolojia na linatokea pale ambapo mwanamke najichukia kuzaliwa manamke kwa kudhani kwamba kuwa mwanamke ni kuwa wa ngazi ya chini na matokeo yake huanza kutumia nguvu za kiutawala kutawala watu na mumewe ili kufidia au akifikiri kuwa yuko katika nafasi salama kama ya wanaume, Katika saikolojia jambo hili huitwa Masculine protest ambayo maana yake kwa lugha ya kigeni ni
Masculine protest is a tendency attributed especially to the human female in the psychology of Alfred Adler to escape from the female role by assuming a masculine role and by dominating others; broadly: any tendency to compensate for feelings of inferiority or inadequacy by exaggerated overt aggressive behavior.

5.      Mwanamke mtawala huchagua mwanamme dhaifu.

Kutokana na maswala ya kisaikolojia na kiroho pia utaweza kuona ile tamaa ya kiutawala ndani ya mwanamke itakuwa inatafuta mwanamume dhaifu ambaye anatawalika kwa njia rahisi sana bila kutumia nguvu nyingi, hii maana yake mwanamke mwenye tamaa hii ya kutawala haraka sana anavutiwa na mwanamume ambaye ni rahisi kutawalika, Endapo atagundua kuwa hutawaliki wakati wa migogoro ya kiutawala atahitimisha kwa kusema kuwa umekuwa na kiburi siku hizi, anaweza kusingizia uwezo ulio nao cheo na hata fedha kuwa zimekubadilisha.

Njia mbadala wanazotumia wanawake kuwatawala wanaume!

Katika mgogoro huu uliotangazwa na Mungu ni muhimu kukumbuka kuwa ni mgogoro wa milele ambapo kila saa na kila wakati wanwake watajaribu kuwatawala wanaume moja kwa moja au kwa namna nyingine.

Ni muhimu kufahamu kuwa huu ni mgogoro wa asili uliotokana na anguko la mwanadamu hivyo ni muhimu kukumbuka kuwa wanawake watafanya hivyo kwa kusudi au hata bila kukusudia ili mradi wajisikie salama kutawala, Hapo juu tumechambua njia ambazo wanawake huzitumia kuwatawala wanaume moja kwa moja lakini sasa nataka kufunua njia nyingine ambazo sio za moja kwa moja namna wanawake wanavyotafuta kutawala ndoa zao au waume zao au nyumba zao, njia hizi huzitumia kutawala hata kama hawajawa au hawajafanikiwa kushika madaraka hayo

1.      Kulitumia tendo la ndoa kama njia ya kutawala.

Wanawake hutumia njia ya kunyima tendo la ndoa kama njia ya kuwafanya waume zao watimize matakwa yao, mwanzoni nilipokuwa nimeoa moja ya mgogoro mkubwa niliokutana nao ulikuwa ni huu wa kunyimwa unyumba sikufahamu sana sababu zilikuwa ni nini lakini nilikonda na kuwa mnyonge sana kwa sababu namcha Mungu na hakuna mahali pengine ningeweza labda kupata tendo hilo, nilimuuliza Mchungaji wangu mmoja kuhusu hili na alinijibu kwa ufupi tu “Ukiona mwanamke anakunyima unyumba ujue anataka kukutawala” full stop mchungaji hakunifafanulia kwa undani jambo hili lilikuwa lina maana gani, inawezekana ni kutokana na ufahamu wake aliokuwa nao wakati huo na mimi sikuuliza maswali mengi pia kutokana na ufahamu wangu niliokuwa nao wakati huo. Lakini sasa nafahamu kuwa hakuna jambo baya duniani kama kunyimana unyumba na dawa ya jambo hili inaweza kuwa mbaya hata kuielezea hapa, Lakini mjenzi mwenye hekima mwenzangu alisema tu shetani asije akapata nafasi msinyimane.

1Wakoritho 7:2-5Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu

Mwanamke mpumbavu huweza kuibomoa nyumba yake kwa mikono yake miwili, kama mwanamke atalitumia tendo la ndoa kwa matakwa yeke tu na kwa kusudi la kumtawala mumewe biblia iko wazi tu kwamba shetani atafanikiwa kuwajaribu, na zinaa itatokea na anguko lilelile kama lililomtokea Adamu  na Hawa linaweza kuwatokea na ninyi katika namna hii ambayo Mwanamke anatafuta utawala na ndio maana hakuna jambo la msingi na maana sana duniani kama mwanamke kuwa mnyenyekevu, wabarikiwe sana makabila yote ambayo wanawake wamefunzwa kuwapigia goti wanaume mpaka chini na kuwaheshimu waume zao kama watawala na mabwana kwa kufanya hivi hawapungukiwi na kitu lakini wataongeza kupendwa zaidi na waume zao na kuaminiwa.

Malaki 2:16Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.”

Pia kutokana na wanawake kufanya hayo kuachana kunaweza kutokea jambo ambalo linamuudhi sana Mungu na sio hivyo tu Mungu anachukizwa na “naye aifunikaye nguo yake kwa udhalimu”kunaweza kuwa na tafasiri mbili tu katika kimstari hicho yeye nafanyaye zinaa lakini zaidi sana yeye anayenyima unyumba, kufunika nguo yako kwa udhalimu ni kukataa kuwa tayari kwa tendo la ndoa, wanawake wa jinsi hii hupanda kitandani wakiwa na magwanda, hawatoi ushirikiano wa kutosha katika tendo la ndoa, na tendo la ndoa hupewa mwanaume kama vile mtoto anapohitaji kunyonya tu na sio kwaajili ya kuhakikisha nyumba inasimama
Kwa nini wanawake hunyima tendo la ndoa makusudi wapate kutawala na tabia hii hufanywa zaidi na wanawake waoajiita kuwa wacha Mungu, waliobarikiwa kuwa na Mume mmoja mcha Mungu na mwaminifu na hatima ya jambo hili huwa mbaya

2.      Hutumia Machozi kama njia ya kutawala.

Baadhi ya wanawake huwatawala wanaume kwa kutumia machozi, yaani hutumia njia ya kukimbilia kulia machozi pale wanapokutana na vikwazo kuhusu jambo Fulani katika ndoa zao hii hutokea endapo mwanamke ana mahitaji yake au madai yake ya aina Fulani, ama amefanya jambo ambalo anajua kama mume utachukua hatua kali, kumdibiti hapo mwanamke hukimbilia kulia kama kinga na njia yaw ewe kukubaliana naye au ushindwe kuchukua hatua stahiki.

3.      Hutumia njia za kuaibisha au kusemelea.

Mwanamke anayetaka kutawala hutumia njia ya kuaibisha yaani anaweza kutishiakuondoka akiwa amefungasha mizigo yake yote, au baadhi ya nguo, hii itakuogopesha kwamba watu watajua kuwa mmegombana na hivyo, utambembeleza, au kwamba unawaogopa wakwe zako na unawaheshimu hivyo hutaki kuonekana mbaya na hivyo utanyenyekea mwanamke wako na kutimiza matakwa yake aidha wanawake hao pia hukimbilia kwa watu unaowaheshimu na kueleza mambo yenu ili kukuitisha vikao na kutafuta suluhu, haya yote yatakufanya uogope kumfanya lolote ukijua kuwa utaaibika na hapo ndipo wanapopata nafasi ya kutawala kama mwanaume hutakuwa na ufahamu wa kukutosha kuhusu viumbe hao.

Ni kwasababu nkama hizo na nyinginezo zisizoorodheshwa hapa shetani huzitumia kupitia wanawake ili kuwatawala wanaume na ni kwaajili ya hayo Paulo mtume anakataza kutoa nafasi hii kwa wanawake kuwatawala wanaume na kutokuheshimu nafasi ya mwanamume katika ndoa na katika kanisa

Dawa ya mwanamke mtawala.

Kama wewe ni mume au mwanaume unayepitia mateso ya kuwa na mwanamke mtawala ujue una njia moja au mbili tu za kusuluhisha tatizo lako moja kumsaidia kwa kumfundisha ili kwamba atambue wajibu wake na mahitaji yake ya kisaikolojia na nafasi yake kiroho na kimaandiko na njia ya pili ni kukubaliana naye kwa kumfanya ajione kama mtawala na kutafuta namna unavyoweza kumtawala.

Njia ya kwanza sio rahisi kama unavyodhani, mwanamke mtawala hawezi kukubali hilo na atahakikisha kuwa anajisaidia vyovyote iwavyo ashike mpini, na hapo ndipo kosa linapotokea kwani sasa mwanaume anaweza kujikuta akitumia nguvu na migogoro mingi hutokea magomvi, vipigo, kunyimana unyumba, zinaa na talaka pia, hakuna mtu hasa mwanaume anayeweza kukubali kukaa katika nyumba isiyo na amani.

Mfalme Sulemani alisema manen magumu sana kuhusu kuwa na mwanamke mtawala Mitahli 21:9 Biblia inasema “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi” pia Sulemani akarudia tena Mithali 21:19Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.” Je wadhani Mfalme mwenye hekima anazungumzia mwanamke mgomvi au mchokozi anamaanisha nini ni wanawake watawala.

Ugomzi utajitokeza na kama ukitumia nguvu uhusiano utavunjika na kuachana kutatokea, ni muhimu kuwafunza wanawake kutambua nafasi zao na kujinyenyekesha kwa waume zao, mfano mwema biblia inamtaja Sarah alikuwa ni mwanamke wa kipekee sana aliyejali hisia za mumewe na kumuheshimu sana kiasi ya kumuita BWANA 1Petro 3:1-6Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu. Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote

Unaona Sarah anatajwa kama mfano wa wanawake watii waliowaheshimu waume zao Sara alimuheshimu sana Abraham, na kwa sababu hiyo Abrahamu alimsikiliza sana Sarah kila mwanamke mcha Mungu anapaswa kuiga mfano wa Sarah wa utii na unyenyekevu na heshima kwa mumewe kwa faida ya nyumba yake na familia yake hutakuwa mjinga mwanamke ukijinyenyekeza lakini utakuwa mpumbavu ukitafuta utawala.

Biblia inamtaka mwanamume kutumia akili 

1Petro 3:7  Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”

Biblia inamtaka mwanaume kuitumia kili yake ipaswavyo katika kuishi naye mapambano yote ya mwanamke ya kutaka kutawala yakiachiwa hivihivi ni hatari, mwanamke akifanikiwa kukutawala atatawala kwa uangamivu wa nyumba yako yote nao wanapolenga kutawala wanalenga kutawala Tendo la Ndoa, Fedha, kujaliwa na Muda wako kwa msingi huo ili umtawale mwanamke ni lazima maswala hayo manne yawe yamakaa vema na uwe na ujuzi nao na utaalamu nayo, Hakikisha una ujuzi wa kutosha katika Tendo la ndoa na unampatia haki yake kana inavyopaswam hakikisha unaitunza familia yako na kuipatia mahitaji yake yote na ukifanikiwa nay a ziada, hakikisha kuwa unamjali kiasi ambacho anaweza kujifikiri kuwa yeye ndiye anayetawala na hakikisha unampa muda wa kutosha, kama hutajali hayo utajikuta unaingia katika wakati mgumu sana wanaume wengi hudharaulika kwa sababu ya kuwa dhaifu katika eneo moja wapo kati ya hayo, mwanamke akiwa mpweke anaweza kufanya jambo lolote, mwanamke akikosa tendo la ndoa anaweza kushiriki na yeyote hata mnayama, mwanamke asipojaliwa anaweza kutoa muda wake hata kwa house boy, mwanamke kama hana matuzo au yeye ndiye anakutunza unapoteza maana katika ndoa, aidha nitoe tahadhari kwa watumishi wa Mungu wanaotoa muda mwingi sana katika kuomba bila ya wake zao, hili ni kosa maombi yako hayatazuia mkeo kushughulikiwa na watu wa ajabu ajabu wanaweza kuwa wauza mchele tu, au madereva nk.  kama hutampa mahitaji muhimu na kuishi naye kwa akili, kla kitu kifanyika kwa kiasi, Mungu yu ajua kuwa tuko ulimwenguni hivyo usihamie kwenye ulimwengu wa roho tu na kuacha ulimwengu wa akili ukitoa muda kwa mkeo na familia yako.

Ni matumaini yangu kuwa wanawake kwa wanaume mmefaidika na mafundisho haya yenye Baraka, tafadhali kama somo hili limekusaidia wewe Mwanamume na wewe mwanamke acha maoni yako hapa, ili nimtukuze Mungu kwa somo hili au nitumie ujumbe au kunipigia kwa namba zifuatazo.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Rev. Innocent Kamote
0718 990 796 call any time
0784 394 550 call any time
0626 606 608 sms only
E mail ikamote @yahoo.com

Jumapili, 18 Juni 2017

Nendeni Mkwamwambie Yule Mbweha!


Andiko La msingi: Luka 13:32 “Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.”


Wengi wetu tutakuwa tunafahamu, jinsi Mafarisayo walivyokua wapinzani wakubwa sana wa Bwana Yesu katika huduma yake na kazi zake, Katika kifungu hicho hapo juu hatuna uhakika kama Mafarisayo walikuwa wametumwa na Herode kweli, au walitunga uongo wao wenyewe ili kumtoa Yesu katika KUSUDI kuu la kazi yake ambalo lilikuwa ni kuutangaza Ufalme wa Mbinguni. Tunasoma hivi katika Mukhtadha mzima wa habari hii:-…



Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.  Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.  Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”

Yesu alikuwa katika mipaka ya galilaya wakati huu, Mafarisayo walimjia wakijifanya kama wanaurafiki na Yesu na kuwa wanamtakia mema, wanataka kuokoa maisha yake wana uchungu na maisha yake, walijifanya wana habari hizi kutoka kwa Herode kwamba Herode anataka kukuua hivyo uondoke, Yesu alitaka kuwaonyesha Mafarisayo hawa kuwa kama wamekubali kuwa wajumbe wa Herode yeye anawarejesha tena kwa Herode, na anawatuma waende wapeleke taarifa hii maana wamekubali kutumiwa kama wambeya sasa wamweleze wazi Herode na Yesu anatumia neno gumu

Nendeni Mkamwambie yule Mbweha!
Mbweha ni kijimnyama dhaifu sana  na kioga ambacho kinafanana na Mbwa, ni vinjinyama vinavyoishi mwituni vina uwezo wa kubweka lakini ni vioga, viongo na vichafu na vimejaa hila,huwinda wanyama wengine ni mnyama asiye na Heshima wala umaarufu na ni mnyama anayedharauliwa sana!

Yesu Kristo aliifahamu sheria kuwa imeandikwa usimnenee mabaya mkuu wa watu wako, Hivyo Yesu kimsingi hakuwa anamtukana Herode au kumnenea mabaya, Lakini alimuita mbweha kwa sababu  Yesu alikuwa anatambua roho ya ukatili aliyokuwa nayo Herode alikuwa anafahamu jinsi Herode alivyosumbua wengi kwa ukatili wake, alitambua kuwa Herode alikuwa amepoteza umaarufu kwa wayahudi na tena alikuwa ni kibaraka tu wa warumi na Kaisari, alikuwa muoga na mwenye hila na aliyepoteza umaarufu kabisa, 

 Yesu alikuwa anajua kuwa Herode hataki yeye awepo katika mipaka yake, na hivyo anataka kumtisha ili Yesu akimbilie mji mwingine, Majibu ya Bwana Yesu yalikuwa ya kumuondoa wasiwasi huyu Mbweha kuhusu huduma anayoifanya,

 Yesu alikuwa anajua kusudi la kuwepo kwake na hata saa ya kufa kwake, alikuwa anajua kusudi la Mungu katika maisha yake na hivyo mbwembwe  za Herode hazikuwa tishio kwake, watu wengi walimuogopa Herode kama Simba lakini Yesu alimuona Herode kama mbweha tu, Hivyo Yesu alitaka kumhakikishia Herode kuwa Yeye yupo kwa mapenzi ya Mungu katika ardhi ya Mungu na kuwa anatimiza kazi ya baba yake tu, na kuwa haogopi lolote! Aidha katika wakati huu Yesu alikuwa amepata umaarufu mkubwa sana na watu wengi walikuwa wamemuamini na kwa vile Yesu ni wa ukoo wa Daudi watu wengi walikuwa wameanza kujenga imani ya kuwa Yesu ndiye mfalme ajaye na mwokozi wa Israel Yesu alitambua wazi kuwa Yeye hakuzaliwa kwa kusudi la kutawala serikali ya wakti ule, Yeye alikuwa amekuja kufanya kazi ya ukombozi wa Mwanadamu kwa kufa na kufufuka kwake na hivyo alitambua kusudi la kuweko kwake!

Natoa Pepo na Kuponya wagonjwa!
Aidha Yesu alimtangazia Herode kupitia wajumbe wake ukweli kuwa anaendelea kufanya kazi ya Mungu katika mipaka ya Herode na kuwa ataendelea kufanya kazi ya Mungu, Ni kama Yesu alikuwa anamwambia Herode kuwa Haogopi wala hana hofu yoyote ya njama za Herode, Badala yake naendelea kutimiza kusudi la Mungu kwa kuwa yuko ndani ya majira na saa ya Mungu na haogopi vitisho, aidha Herode hapaswi kuogopa kwa kuwa Yesu anafanya kazi ya Mungu kwa muda mfupi tu,
Yesu Kristo ni kama alikuwa alikuwa akimjibu Herode kuwa kutoa Pepo na kuponya wagonjwa na kuhubiri injili leo na kesho tu (Kwa maana ya muda mfupi tu) kulikuwa na maana ya kuwa hakuwa anavunja sheria, hakuna ubaya wowote ambao Yesu alikuwa akiutenda, kutoa pepo na kuponya wagonjwa kwa siku chache tu, na kuwa Yesu baadaye angeondoka katika Mipaka yake kwa wakati wa Mungu na sio wa Herode.

Siku ya tatu nakamilika
Yesu alikuwa akitoa Muda tu wa kinabii kuwa siku ya tatu anakamilika, hii haikuwa na maana ya siku tatu katika jimbo la Galilaya, hii ilikuwa na maana ya siku tatu katika mpango wa Mungu na Muda wa Mungu, Yesu alikuwa anafahamu kuwa hakuna wa kumuua wala wa kumuondoa mpaka Muda wa Mungu utakapowadia, Yesu alikuwa na ujuzi kuwa atakwenda Yerusalem na huko ndiko atakakofia na kufufuka na kurudi katika enzi yake Mbinguni.

Ndugu Momaji wangu Jambo lolote lile linalokuja katika maisha yako, kukutisha na kukudhoofisha na kukutia woga na kukuvunja moyo na kukukatisha tamaa ni MBWEHA!  

Kama unaifanya kazi ya Mungu wewe ni mtumishi au nabii mamlaka uliyo nayo kwa Mungu ni kubwa kuliko ya watawala wa kisiasa, timiza kusudi la kazi uliyoitiwa bila kuogopa vitisho
Ndoto yako na maono yake yasitishwe na mtu awaye yote.

Hatuishi duniani kwa kubahatisha wala hatutimizi kusudi la kuweko kwetu kijinga, Mungu ndiye alpha na omega, hatima ya maisha yetu haiku mikononi mwa mtu Fulani au kiongozi Fulani iko mikononi mwa Mungu.

Wachawi ni Mbweha tu hawana hatima ya maisha yetu, waganga ni mbweha tu, wambea ni mbweha tu, wazushi ni mbweha tu, wafitinini mbweah tu, Kaaa katika kusudi la Mungu mtu awaye yote asikutishe, Usiondoke katika kusudi lako la Utumishi, kusoma, kufanya biashara, wokovu, malengo na mipango yako muhimu, ndoa yako na kadhalika, Kumbuka lolote linalotaka kukutoa katika mpango wa Mungu ni Mbweha tu!

Ujumbe: Na Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
kwa Mawasiliano, Maoni, ushauri na shukrani wasiliana nami:-
 
0718990796
0784394550
0626606608 SMS only
ikamote@yahoo.com

Jumatatu, 15 Mei 2017

Je Hapana Zeri Katika Gileadi? (Zeri ya Gilead)

Mstari wa Msingi: Yeremia 8: 22 “Je Hapana Zeri katika Gilead? Huko Hakuna tabibu? Mbona basi haijarejea afya ya Binti ya watu wangu?

 Mmea aina ya zeri kama unavyoonekana katika Picha

Ni muhimu kufahamu kwamba hapa duniani hakuna jambo lolote Gumu lisilo na majibu, kila jambo na kila tatizo lina majibu yake na ufumbuzi wake, Magonjwa hali kadhalika yanaweza kutibiwa kwa tiba za aina mbali mbali, Mungu aliwapa wanadamu mimea ambayo ndani yake aliweka nguvu za uponyaji kwaajili ya matibabu ya aina mbali mbali.

Nyakati za Biblia watu walitumia pia madawa yatokanayo na mimea kutibu magonjwa na mateso ya aina mbalimbali, kulikuwa na miti mingi sana iliyotumika kama tiba, kabla ya kuanza kutumia zaidi kemikali ambazo nyingi zina uharibifu mkubwa katika mwili wa wanadamu na hivyo kuchangia udhaifu mkubwa wa aina binadamu walioko leo juu ya uso wa nchi. Moja ya miti maarufu sana iliyotumika kwa tiba katika Israel na mashariki ya kati ulikuwa ni mmea ujulikanao kama Zeri ambao ulikuwa unapatikana kanaani na katika mji wa Gilead.

Zeri ni nini hasa?

Zeri kwa kiingereza (BALM) ulikuwa ni mmea ambao ulikuwa maarufu sana nyakati za Biblia mmea huu ulipatikana katika nchi ya milimamilima iliyokuwa nga’mbo ya Jordan iliyojulikana kama milima ya Gilead, mmea huu uliuzwa kwa bei kubwa sana na wafanya biashara wa zamani waliokuwa matajiri walitajirika kwa kuuza zeri, 

Mwanzo 37:25 “Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na ZERI na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri.” 

Unaweza kuona aidha katika nyakati za Biblia kama mtu anakupenda sana na kukuheshimu sana moja ya zawadi ya ngazi ya juu kabisa ambayo mtu anageweza kukupatia ilikuwa ni pamoja na ZERI angalia
Mwanzo 43:11 “Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, ZERI kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi”.

Kwa nini Zeri ilikuwa bidhaa ya thamani na zawadi kubwa sana, Zeri ilikuwa na sifa ya kuponya majeraha yote ya mwili “recovering” na vidonda mbalimbali pia vikiwemo vidonda vya kuumwa na nyoka, aidha watu pia waliitumia zeri katika kuhifadhia mwili wa mwanadamu aliyekufa usioze, Hivyo kama dawa nyingine zote zingeshindwa kutibu jeraha la mtu ndipo sasa ili kuokoa maisha yake ilipaswa kuitafuta Zeri kwa vile hii ilijulikana kama dawa isiyoshindwa hata hivyo dawa hii ilikuwa ghali sana ingekugharimu kuuza vyote ulivyo navyo ili kutibiwa na wataalamu wa Gilead upate kupona. Dawa hii likuwa haishindwi kutibu jambo kama mtu anetibiwa na dawa zote na ikashindikana watu walimshauri aende Gilead kwa wataalamu kataumie Zer.

Yeremia 46:11Panda uende Gileadi, ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati kupona kamwe.” 

Ni wazi kuwa kama mtu angetumia dawa bila mafanikio dawa ya mwisho ingekuwa Zeri ni zeri tu ndiyo ambayo ingeweza kutibu maumivu aliyoyapata mtu".

Yeremia 51:8Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa

Katika namna ya kushangaza sana hata hivyo yalikuweko magonjwa ambayo yalikuwa ahayasikii dawa yaani magonjwa sugu, ilipotokea kuwa mgonjwa haonyeshi badiliko, kila mara alionekana yuko vilevile hapati kugangwa lilikuwa ni jambo la kushangaza sana kusikia Zeri imeshindwa au wataalamu wa Gilead wameshindwa, katika mstari wa Msingi Yeremia alikuwa anazungumzia tatizo la kiroho na tabia ya wana wa Israel ambao walishindwa kutubu na kubadilika kiasi cha kufikia ngazi ya kuhukumiwa na Mungu, Nabii alikuwa akiomboleza na kujiuliza kuwa dawa isiyoshindwa imekosekana? Matabibu wa Gilead hawako, Yeremia alikuwa anamaanisha kuweko kwa toba na manabii, Israel walishindwa kuwasikiliza manabii na pia walikosa moyo wa toba nJe hapana zeri katika Gilead? Na Matabibu maana naona afya ya watu wangu haijarejea?

Kimsingi zeri ya Gilead ilikuwa ghali sana na hata hivyo haikuweza kuponya majeraha mengine yaliyowasibu watu.

Marko 5:25-28Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya, aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona

Zeri ulikuwa ni mti halisi lakini vilevile ulikuwa ni picha ya Yesu Kristo, katika muujiza huu alioufanya Yesu ni dhahiri biblia inatuonyesha zeri kutoka mbinguni, inatuonyesha mwanaume mwenye uwezo wa kumfanya mtu akawa recovered akapona akawa kamili, unaweza kuhangaika huko na kule kwaajili ya mahitaji yako, kwaajili ya afya yako ya kimwili na kiroho, kwaajili ya majeraha ya moyo wako, kwaajili ya majeraha ya adui zako, kwaajili ya majeraha ya ndoa na kazini na shuleni na hata kanisani, unaweza kuangaika huku na kule kwaajili ya mahitaji yako ya aina mbalimbali lakini lao ninakutangazia kuwa iko dawa isiyoshindwa Dawa hii ni Yesu Kristo peke yake yeye anaweza yote kwake hakuna linaloshindikana ni dawa ya waliokata tamaa, dawa ya waliojeruhiwa na kudharaulika, ni dawa ya maisha yetu, feature yetu haiku mikononi mwa wanadamu, iko mikononi mwa Yesu tu, huyu ndio wa kumkimbilia, huyu ndio wa kumpapatikia, huyu ndio wa kumtazama kwa kila unalokaboliana nalo katika maisha katika masomo, katika ndoa, kazini nk. Mwangalie Yesu na utafanikiwa yeye ni zaidi ya zeri ya Gilead ni Zawadi ya upendo wa hali ya juu kutoka kwa Mungu baba 

Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa Pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.

Na. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima

Ijumaa, 5 Mei 2017

Kama Mlivyonena Ndivyo nitakavyowafanyia!


Katika maandiko haya,(HESABU 13:25-33; 14:1-12,26-32),

Hesabu 14:26-32 “Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,  Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo.  Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;”

Hesabu 13:25-33 “Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. . Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi.  Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.  Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.  Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.  Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.    Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.  Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Hesabu 14:1-12 “1. Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.  Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.  Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.  Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao.  


Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa ulimi wa Mwanadamu una nguvu ya kusababisha madhara makubwa na pia kuleta uponyaji mkubwa, kwa kuwa wanadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mungu aliuumba ulimwengu kwa Neno tu alitamka na ikawa, wakati wote utendaji wetu na matukio yetu katika maisha yanatokana nay ale tunayoyazungumza Mithali 18:20-21Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”Kama hivi ndivyo ni jambo la msingi sana kujichunga ni kitu gani tunakizungumza na kukitamka kwa vile tunaweza kuumba jambo hilo.

Kumbuka hata wokovu wetu unapatikana kwa kumuamini Yesu moyoni na kwa kumkiri kwa kinywa na ni kwa kinywa tu tunaweza kuliitia jina la Bwana na kupata msaada Warumi 10:9-13  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.  Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.  Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

Kwa msingi huo kama tunataka kuwa mbali na mauti na kama tunataka kuleta uzima katika maisha yetu ni lazima tuwe na semi zilizo na manufaa katika maisha yetu na hata ya wengine

Jambo la kujifunza:
Wana wa Israeli wanatumia ulimi kuzungumza maneno kama haya "AHERI TUNGALIKUFA KATIKA JANGWA HILI" na maneno kama "HATUWEZI".Mungu akasema atawafanyia hivyo walivyosema na kweli walikufa katika jangwa hilo.

Kalebu Mwana wa Yefune na Yoshua Mwana wa Nuni walisema maneno ya ushindi kama haya "TWAWEZA KUSHINDA BILA SHAKA na BWANA YU PAMOJA NASI".

Tunajifunza juu ya makundi mawili.Kundi la kwanza ambao ndio wengi wanazungumza maneno HASI NA YA KUSHINDWA na kweli walishindwa.

Kundi la pili ambao ni wachache sana wanazungumza maneno ya CHANYA YA KUSHINDA na kweli walishinda na kuingia nchi ya ahadi.

Watu wa Mungu ikiwa Mungu anatufanyia jambo sawa na ukiri wetu, ikiwa uzima na mauti uko katika uwezo wa ulimi wetu, ikiwa kwa ulimi tunaweza kukiri na hata kupata wokovu ni muhimu kwetu ,KWA KILA JAMBO TUZUNGUMZE MANENO CHANYA  YA KUSHINDA sawasawa na Neno la Mungu,NA BWANA mwenye kutushindia atakuwa pamoja nasi kufanikisha yote kiroho na kimwili.

MANENO TUNAYOSEMA NDIYO BWANA ANAYOTUFANYIA YAWE MEMA AU MABAYA!Maana anasema CHAGUENI HIVI LEO!(YOSHUA 24:14-15;WAFILIPI 2:13;WARUMI 8:31-32,37-39;WAFILIPI 4:13).Mungu aweke mlinzi vinywani mwetu ili sikuzote tuzungumze maneno ya kuumba ushindi katika Jina la Yesu Kristo.(ZABURI 141:1-3)

Ni imani yangu kuwa Tangu sasa utatumia kinywa chako vema na kujizungumzia ushindi, acha kujizungumzia kukata tamaa, jizungumzie mambo mema wazungumzie wengine mema  Na mungu atatubariki sawasawa na ukiri wetu.

Sources. Rev.George Swenya Full Gospel Bible Fellowship Church Tanga.

Ukarabati: Rev. Innocent Kamote Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Ijumaa, 28 Aprili 2017

Kazi za Roho Mtakatifu katika Kanisa!


Andiko la Msingi: Matendo 1:8Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”


 Hii hapo juu ni picha (symbol) ya Roho Mtakatifu na sio Roho Mtakatifu

Utangulizi.

Hali ya kanisa la leo imekuwa dhaifu kuliko Nyakati za kanisa la Kwanza, Kanisa lilikusudiwa na Mungu kuwa Chombo kikuuu cha ukombozi wa wanadamu Baada ya kazi njema iliyofanywa na Yesu Msalabani, Mungu analitegemea kanisa kuwa kama Waamuzi, watetezi, wakombozi, makuhani, wafalme na askari wa mstari wa mbele katika kuwatetea wanyonge, walioonewa na waliosetwa katika vifungo vya Ibilisi, na kukemea uovu, kuikosoa serikali na kuonyesha njia kwa ulimwengu!

Luka 4: 18-19Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Kanisa lilipaswa kufanya kazi hizo alkizozitaja Yesu na kuzitabiri Isaya hapo Juu, ikiwa Roho wa Mungu yuko juu yetu, ikiwa ametupaka Mafuta, lakini jiulize leo hii je kazi zinazofanywa na kanisa ndizo hizo hapo juu? Leo kanisa limejaa watu wengi wenye Stresses yaani migandamizo, lina watu wengi wasio waaminifu bila kujali kuwa wako ngazi gani za kiroho, yale ambayo zamani tulikuwa tunayaona na kuyashuhudia yakifanywa na watu tuliowaita Mataifa watu wasiomjua Mungu, tuliokuwa tukiwalilia waokolewe, wamjue Mungu wamgeukie Mungu sasa ndio yanafanywa na Kanisa, Je ni mara ngapi kanisa limekaa kimya watu wanapoonewa, Mauaji yanapotokea Duniani, vita vinavyoendelea, matishio ya umwagikaji wa damu na dhuluma za kila aina je leo ni nani anaifanya kazi hii? Nani anasimamia haki za binadamu zinazoendana sawa na Neno la Mungu? Kwa nini tumefikia hapa tulipofikia? Kuna na mambo mengi sana sitaki kuyazungumza hapa lakini wewe unayajua kuhusu hali ya kanisa la leo! Ni ya kushangaza, ni kweli ziko huduma za kinabii na mitume na miujiza ambayo inatendeka na najua inatendeka kwa nguvu za Roho Mtakatifu, lakini je uadilifu? Uko? Je Hakuna ulevi, uongo, picha za ngono, chuki, uadui, uchawi, ushirikina, masengenyo, uasherati na zinaa, je hatutoi muda mwingi kwa simu zetu, tablets, na laptop, zaidi kuliko kwa Mungu na familia zetu, hali ni mbaya mno sasa, Turudi kukazia kazi za Roho Mtakatifu ndani ya kanisa, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

1.       Roho Mtakatifu ni Nani?

2.       Kazi za Roho Mtakatifu Katika ya Kanisa

Roho Mtakatifu Ni nani?

Katika Maandiko Roho Mtakatifu anaelezewa vema kama Nafsi kamili  inayojitegemea yeye ni BWANA yaani ni Mungu 2Wakoritho 3:17-18 17. Basi 'Bwana' ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, Waebrania  9:14 Roho Mtakatifu ni wa Milele tunaelezwa katika maandiko “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” kuwepo milele ni sifa ya uungu, 1Petro 1:2, Roho Mtakatifu ni Mungu kama ilivyo kwa Baba na Mwana kwa msingi huo hatupaswi kumfikiri Roho mtakatifu kama nguvu tu au hamasa Fulani, ana sifa za nafsi anafikiri, Warumi 8:27 ana hisia Warumi 15:30 ana maamuzi 1Wakoritho 12:11 na ana uwezowa kupenda na kufurahia ushirika , alitumwa na Mungu Baba kuleta uwepo wa kiungu kwa washirika ili tufurahie ushirika wetu na Kristo Yohana 14:16-18,26, kwaajili ya hayo Kanisa linapaswa kukumbuka kuwa Roho ni Mungu na ni nafsi na nilazima tuhakikisha anaunganishwa mioyoni mwetu, na kuwa anastahili kuabudiwa kupendwa na kusikilizwa Marko 1:11

Kazi za Roho Mtakatifu katika Kanisa.

1.       Yeye ndio njia ya wokovu anayetushawishi kwa habari ya haki dhambi na hukumu Yohana 16:7-8 Sasa basi ni vigumu kwa kanisa kujisikia hukumu na kufa kwa dhamiri kama Roho Mtakatifu hapewi nafasi ya kutosha katika kuifanya kazi ya kutuhukumu kwa habari ya dhambi, kutuonyesha kuna hukumu kubwa ijayo endapo hatutatubu na kutushuhudia namna ya kutenda haki.
2.       Anafunua kweli kuhusu Kristo Yohana 14:16,26,
3.       Anatuzaa kwa upya Yohana 3:3-6
4.       Anatufanya washirika wa mwili wa Kristo 1Wakoritho 12:13
5.       Anatutakasa  Warumi 8:9, IWakoritho 6:19
6.       Anatuthibitishia kuwa sisi ni wana wa Mungu Warumi 8:16
7.       Anatusaidia katika kuabudu Matendo 8:26-27
8.       Anatufanya tumtukuze Yesu Kristo Wagalatia 5:22-23,1Petro
9.       Anazalisha neema ya Kristo inayotufanya tuwe na sifa zinazomtukuza Kristo Wagalatia 5:22-23, 1Petro 1:2
10.   Ni Mwalimu  na hutuongoza katika kweli yote  Yohana 16: 13, 14:26, 1Wakoritho 2:9-16
11.   Aanamfunua Yesu kwetu na kutuongoza katika kuwa na ushirika na Yeye Yohana 14:16-18,16:14
12.   Anapanda upendo wa Mungu siku zote ndani yetu  Warumi 5:5
13.   Anatupa Furaha faraja na msaada Yohana 14:16, 1Thesalonike 1:6
14.   Ni njia ya huduma na hututia nguvu kwaajili ya huduma, shuhuda na utangazaji wa Neno la Mungu Matendo 1:8, 4:31 na hutenda miujiza Matendo 2:43;3:2-8, 5:15, 6:8, 10:38
15.   Anatoa Karama za Roho kwa kusudi la kulijenga Kanisa 1Wakoritho 12-14
16.   Analijenga Kanisa Waefeso 2:22, anatia moyo kuabudu Wafilipi 3:3
17.   Anaongoza katika Umisheni Matendo 13:2, anateua waamini Matendo 20:28
18.   Anapaka Mafuta watumishi Matendo 2:4 1Wakoritho 2:4
 
Hitimisho!
Kama ikiwa Roho wa Mungu hufanya kazi hizo zote kanisa halipaswi kumdharau, upungufu mkubwa unaolikumba kanisa la leo unatokana na sababu tu za kumzimisha Roho Mtakatifu, Ni lazima kanisa limpe Roho Mtakatifu kipaumbele kama linataka kuwa hai nnapozungumza kanisa namaanisha kila mtu aliyeokolewa anayemwamini Yesu anapaswa kuzingatia haya ili Kazi za Mungu ziweze kufanyikakatika kiwango ambacho Mungu amekikusudia na sio chini ya kiwango.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote. 0718990796