Jumanne, 20 Julai 2021

Moyo wa ushujaa!

Kumbukumbu la Torati 31: 6 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”


Utangulizi:

Neno la Mungu linamtaka kila mmoja wetu kuwa na moyo wa ushujaa, na kwamba tuwe hodari na kamwe tusiogope, na zaidi ya yote linatuhakikishia kuwa Mungu wetu atakuwa pamoja nasi katika yote tunayokabiliana nayo iwe jua iwe mvua neema ya Mungu inatosha kabisa katika kutufikisha katika mafanikio yote ya kimwili na kiroho tunayoyahitaji. Mungu huyu huyu aliyekuwa na wana wa Israel Jangwani kumbuka yuko pamoja nasi hata ukamIlifu wa dahari, Yuko pamoja nasi na zaidi ya yote amemuachilia Roho wake Mtakatifu mno eti akae ndani yetu, na kutuongoza na kutufariji na kutupa nguvu wakati wa mahitaji, kwa msingi huo hatupaswi kusitasita wala kuhofia au kuogopa jambo lolote zaidi ya kuwa na Moyo wa ushujaa! Biblia ya Septuajint version maneno moyo wa ushujaa yanasomeka hivi “Play the men and be strong”    au “Prove yourself a man” ambalo kwa tafasiri nzuri lingeweza kusomeka hivi “fanyeni kiume iweni na moyo wa ushujaa” unaweza kuona mfano katika 


1Wakoritho 16:13Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari.”  Ni sawa na maneno ambayo Daudi alimuusia mwanaye Suleimani katika 1Wafalme 2:2-3 “Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;” 


Hatuwezi kuwa na mafanikio yoyote yale katika mwili na katika roho kama hatutakuwa na Moyo wa ushujaa. Maneno ya Mungu kupitia Musa mtumishi wake kwa wana wa Israel yalikuwa iweni na moyo wa ushujaa, simameni kiume, sina shaka kama jinsi ambavyo watu wote hawana shaka kuwa Mungu akisema yuko pamoja nasi basi yuko pamoja nasi kweli kweli, yeye sio kama rafiki zetu ambao wanaweza kukuambia tuko pamoja mzee lakini zinapotokea changamoto katika maisha yetu wanayeyuka, Mungu yuko Pamoja nasi kweli kweli, Lakini kama Mungu yuko pamoja nasi na anaendelea kuwa pamoja nasi, kwanini niwe au tuwe na moyo wa ushujaa?, kwanini maandiko yanatutaka tuwe na moyo wa ushujaa? Bila shaka hapa ndio kuliko na siri ya ushindi.


Israel walikuwa wanakaribia kabisa nchi ya kanaani, ilikuwa nchi njema kama Mungu alivyowaaminisha, Hata kama Israel ni jangwa kwa sehemu kubwa lakini ni nchi ambayo Mungu aliichagua ili aliweke jina lake na kutukuzwa kutoka hapo kwa dunia nzima kwa hiyo popote ambapo Mungu anasema ni pazuri ni pazuri, nchi hii ilikuwa njema, ilikuwa imejaa maziwa na asali, mizabibu na tini tende, na kadhalika na eneo zuri kwa malisho ya wanyama, lakini ilikuwa inakaliwa na wakanaani, na wakaani walikuwa hodari, walionekana kuwa majitu, na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye maendeleo makubwa sana ikiwa imezungukwa na ngome zenye kutisha, walikuwa na utaratibu maalumu wa kiserikali walikuwa na wafalme na majeshi, walikuwa wameendelea kitaaluma kwa hiyo ni wazi kuwa Israeli walikuwa wakijilinganisha kwa namna yoyote ile na wakanaani, walijiona sio kitu, Lakini Mungu Yehova alikuwa amewaahidi kuwa atakuwa pamoja nao na kuwa wasiogope na kuwa hatawapungukia wala hatawaacha lakini jambo kubwa ilikuwa wawe na moyo wa ushujaa! Hilo tu ili kumiliki yale tunayopaswa kuyamiliki katika ulimwengu huu tunahitaji tu kuwa na moyo wa ushujaa ona 


Yoshua 1:6- 7 na 9 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. 9Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”


Maana ya moyo wa ushujaa!

Kuwa na moyo wa ushujaa katika lugha ya kiibrania kulikuwa na maana ya kusimama kiume, au kuonyesha uanaume kweli kweli kwa kiingereza “Courage” ability to do something that which is frightens; bravery ambalo maana yake ni uwezo wa kufanya jambo lenye kutisha kwa werevu. Au kwa weledi, au nguvu ya kukabiliana na jambo lenye kutisha au kuogopesha au hatarishi kwa ushujaa mkubwa, ni uwezo wa kuamua kupambana na maumivu, tishio, mateso, hatari, au jambo lenye kutisha bila woga wowote, wala hofu yoyote, Ni uwezo wa kuthubutu kufanya au kukabiliana na jambo ambalo kwa akili za kibinadamu linaonekana kuwa gumu kwa imani kuwa utalifanikisha iwe mvua ama jua, kibiblia ushujaa huu unaambatana na kumuamini Mungu, ndio maana Mungu ameambatanisha na kuwa pamoja nasi, na ili kuiifikia ile ndoto, au lile tumaini au ile ahadi Waebrania 10:35-36 “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.” Kwa hiyo tunapokuwa na moyo wa ushujaa ndipo tunapoweza kupokea thawabu kuu na kutimiza mapenzi ya Mungu na kuifikia ile ahadi au ile ndoto au lile lengo tulilolonalo ambalo ni mapenzi ya Mungu, Katika ulimwengu huu vilevile ili tuweze kufikia malengo yetu ya kawaida hatuna budi kuhakikisha kuwa tunavaa moyo huu wa kijasiri, nina mshirika wangu mmoja anaishi maisha duni na yakawaida kabisa lakini ananiambia mchungaji mimi sitaki kuomba kwangu kuomba ni aibu kubwa hivyo napambana katika maisha, yeye anapambana kwa kuzunguka mitaani na kuuza mahindi ya kuchemsha na anapozunguka hazunguki kimya kimya anapiga kelele aiiiiimahindi ya kuchemshaaa kwa hivyo mimi nilimuhurumia lakini sikuwa na namna ya kumsaidia nilimnunuza mahindi matano ya kuchemsha na niliyagawa kwa watu waliokuwa mtaani ili wale nami nilikula moja tu, lakini nilitaka kumtia moyo kwa kununua mahindi yake kwa sababu nilifuarahia ujasiri alio nao, anapata ridhiki yake kwa sababu haoni aibu, ni mwanamke mzuri wa makamo hivi, ni mzuri, uzuri wake na biashara anayoifanya ni kama haviendani hivi, Lakini ndio njia ambayo Mungu amempa kupata ridhiki yake, yako mambo duniani ambayo ili tuweze kutoka katika hayo hatuna budi kuwa na moyo huu na kutokuogopa lolote hata kama ni kuangamia lakini tukiwa na kusudi la kukaa na kutimiza mapenzi ya Mungu, tunahitaji Moyo huu, ni moyo huu ndio unaoweza kutufanya tukasimama sokoni, viwanjani na kumuhubiri Yesu, ni moyo wa aina hii unaoweza kumfanya mtu akakubali kuwa Kondakta wa basi na kupata ridhiki yake, kuhutubia watu na kila jambo, kusoma, kujifunza na kufundisha kote kunahitaji moyo wa ushujaa, bila moyo huo ni vigumu kuyafikia malengo yetu na mapenzi ya Mungu, sasa tunawezaje kujifunza kuwa na moyo wa ushujaa? Hilo sasa linatuleta sasa katika kutafakari kipengele muhimu jinsi ya kuwa na moyo wa ushujaa:-


Jinsi ya kuwa na Moyo wa ushujaa!

Kuwa na moyo wa ushujaa ni swala la kujizoeza, na ndio maana maandiko yanatuamuru tuwe na moyo wa ushujaa,ushujaa hautoki kwa Mungu unatoka mioyoni mwetu pale tunapomuamini na kumtegemea Mungu, hivyo ni lazima kuamua kutoka moyoni ili kukabiliana na kile ambacho tunataka kukabiliana nacho, lakini tunawezaje kujua au kujipima au kujizoeza kuwa na moyo wa ushujaa yafuatayo ni maswala ya msingi sana yanayoweza kutusaidia kuwa na moyo wa ushujaa na kwa ufupi ukiwa na mambo haya na kuyafanyia kazi katika maisha yako utakuwa na moyo wa ushujaa;-


1.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kujihurumia -  Moyo wa ushujaa na mafanikio yake hauwezi kuwepo kwa mtu anayejihurumia, wengi tumeweza kuangamiza nafsi zetu kwa sababu ya kujihurumia, tumeshindwa wakati mwingine kufikia ndoto kadhaa kwa sababu tuna tabia ya kujihurumia, mtu anapojiandikisha kuwa askari ni kama mtu anayejiandikisha kuangamiza nafsi yake kwaajili ya nchi yake,kujiandikisha kuwa askari ni kujiandikisha kufa! huwezi kuwa mpiganani mzuri kama unajionea huruma, wala huwezi kuwa mwanafunzi mwema wa Yesu Kristo kama unajihurumia, wala huwezi kutoboa katika maswala kadhaa wa kadhaa ya maisha kama utajihurumia Mathayo 16:24-25 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.” Kwa hiyo kuwa mwanafunzi wa Yesu lazima uwe kama mtu unayepoteza maisha, unayekubali kuangamia, unayekataa nafsi yako kujifurahisha, watu wanaojihurumia hawawezi kamwe kuwa wanafunzi wa Yesu, lakini sio hivyo tu watu wanaojihurumia hawawezi kutoboa katika maisha haya!  Nyakati za torati katika agano la kale wanajeshi wote waliokuwa wameoa hivi karibuni au mtu aliyenunua shamba jipya na kadhalika Mungu aliagiza wasiende vitani, kwa sababu mawazo yao hayatakuwa tayari kuangamia na kuacha mke mpya nyumbani hivyo watu wote waliokuwa na mioyo ya hofu na sababu zinazoweza kuwafanya wasijikane nafsi walipaswa kuchujwa ili wasiende vitani ona Kumbukumbu la Torati 24 :5 “Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa.” Au wale waliokuwa na hofu au woga walipaswa kurudi nyumbani Waamuzi 7:3 “Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi.” Unaona Mungu hakuhitaji watu wenye hofu au wanaotetemeka wanaoogopa vita wanaojihurumia wenye ndoa mpya hawa walitakiwa kurudi nyumbani, awaye yote ambaye anataka kufanikiwa lazima avae moyo wa ushujaa asijihurumie kamwe apambane kiume awe na moyo wa ushujaa #

 

2.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuchoka – ili tufanikiwe katika maisha yetu lazima tuwe na mioyo migumu, hatupaswi kuchoka, Biblia inamtaja punda milia au punda mwitu kama mnyama asiyechoka, aliyeizoelea nyika na ukijaribu kumtafuta utachoka wewe na hutaweza kumkamata au kumgeuza ona Yeremia 2:24 “punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona.” Mtu mwenye moyo wa ushujaa moyo wake hauchoki haukati tamaa, unaendelea mbele hata kutokee vihunzi vya namna gani moyo unaendelea tena na tena katika kuyafikia malengo yake, watu wote mashujaa katika maandiko waliofanikiwa katika Nyanja mbalimbali walikuwa watu wasiochoka, watu wengi ambao wanachoka wanakata tamaa na kuishia njiani, kwa msingi huo hatupaswi kuchoka katika kutia bidii kwenye kila kitu tunachokifanya kwaajili ya utukufu wa Mungu, tusichoke katika kutenda mema na pia tusichoke katiika kumgojea bwana naye atatutokea na kututia nguvu Wagalatia 6:9 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho”. Isaya 40:31 “bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”  Watu wengi wenye mafanikio katika Nyanja mbalimbali ni wale wasiokuwa na moyo wenye kuchoka, maisha ya kwenda mbinguni na maisha ya kumngojea bwana yanawezwa na wale wasiochoka, Lakini vilevile tukitaka mafanikio ya aina mbalimbali basi hatupaswi kuchoka. #

 

3.        Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuogopa kubaki peke yake -   Moja ya mambo ambayo yanaweza kumvunja mtu moyo ni pamoja na kuachwa peke yako, watu wengi sana hukata tamaa wanapobaki wenyewe, mtu mwenye moyo wa ushujaa wakati wote anakuwa tayari kupambana hata anapobaki peke yake, hayuko tayari kwenda kwa mkumbo au kufuata mkumbo, Hesabu 14:6-10 “Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote”. Yoshua 24:15Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.” Yoshua ni moja ya viongozi walioambiwa na Mungu moja kwa moja wawe na moyo wa ushujaa, wawe hodari na wasiogope, katika maisha yake anadhihirisha kuwa yuko tayari kusimama na jambo lililo jema na katika mapenzi ya Mungu hata kama atabaki yeye mwenyewe na nyumba yake, ukiisha kuyajua mapenzi ya Mungu na kujua lile kusudi lililoko kwako kamwe usikubali kufuata mkumbo katika kufanya ujinga wewe lenga katika kuyafanya mapenzi ya Mungu, hata kama inatokea migomo mashuleni vyuoni na kadhalika, wewe kama unajua kuwa mgomo huo hauna maslahi kwako na kwa Mungu simama mwenyewe ni wewe peke yako unayeweza kumdhihirisha Mungu wa kweli, Mungu sio mwanademokrasia kwamba anaangalia wengi wape yeye ni mwanatheocracia anaangalia wanaosimama upande wake, Nuhu alisimama na Mungu wakati mkumbo wa ulimwengu wa nyakati zake watu waliishi kwa anasa na kutokujali, Lutu aliishi kwa kumtii Mungu wakati watu wa miji ya Sodoma na Gomora  walipokuwa wakiendekeza dhuluma uovu uozo na mapenzi ya jinsia moja, Eliya alisimama mwenyewe wakati Israel walipokuwa wakimtumikia baali na yeye pekee nabii wa Bwana alisimama ona 1Wafalme 18:22-39 “ Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.  Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.” Mungu hupendezwa na mtu anayejitambua na kutambua mapenzi ya Mungu, ili uweze kufabnikiwa huna budi kusimama mwenyewe, katika kutimiza kusudi lile ambalo Mungu amekuitia Biblia inasema usiandamane na mkutano kutenda uovu, maana yake usikubali kufuata wingi wa watu hususani kama watu hao wamepotea na kupotoka, kanuni hii inafanya kazi sio katika mazingira ya uovu tu na kumcha Mungu lakini inafanya kazi katika kuyafikia mafanikio ambayo lengo lake Mungu ameweka moyoni mwako kwa kuwa wewe ndiwe unayelitambua kusudi hilo simama mwenyewe, usikubali kufuata mkumbo, hata kama dunia itakuacha peke yako Kutoka 23:2 “Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;

 

4.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kupoteza nguvu zake – Kumbuka kuwa tunazungumzia Moyo wa ushujaa na hivyo hapa hatuzungumzii kamwe nguvu za kimwili, shetani anajua kuwa ili aweze kutukwamisha anajua wazi kuwa anapaswa kuujeruhi moyo, moyo wako ukiisha kukubali kujeruhika basi umepoteza nguvu zako, hata kama mtu ana miguvu kiasi gani ushindi wa mtu hatokanani na muonekano wake wa kimwili bali mtazamo wake wa moyoni, yako mambo ambayo ibilisi anaweza kuyatumia kujeruhi mioyo yetu ili tupoteze nguvu zetu watu wenye moyo wa ushujaa hawapaswi kupoteza nguvu zao!huwezi kuwa na nguvu kama utakubali shetani na watu waudhibiti moyo wako, na hisia zake mtu akifanikiwa kuudhibiti moyo wako na hisia zako amekupunguzia nguvu ya moyo wenye ushujaa, unajua ni kwanini maandiko yanatuasa kusamehe au kuwa na subira kwa sababu mtu asiyesamehe anapoteza nguvu unapoteza muda kumfikiri mtu anayekukwaza kuliko kufikiri unachopaswa kukifanya Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.  Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata, akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.” Kumbe kutokuachia ni kutokujiachilia, hatupaswi kukaa chini na kuwafikiri wale waliotuumiza kwa vile watachelewesha kusonga kwetu mbele, sisi hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaachilia kutokuachilia kutatufanya tupoteze nguvu, kuachilia ni nguvu kubwa katika maisha yetu.

 

·         Mfano umeumizwa na unakaa chini kusikilizia maumivu yale badala ya kusamehe na kusonga mbele

·         Watu wanakusema vibaya au wanakosoa vikali kile unachokifanya unakaa kusikiliza maneno yao

·         Umedhulumiwa usipoteze muda kutafuta kurudishiwa tafuta njia mpya ya kupata kilichopotea mara dufu zaidi,

·         Mtu anafanya mambo ya kuumiza moyo wako nawe unasikilizia badala ya kupuuza, unabadili mtazamo wako na malengo yako kwa sababu ya maneno ya watu au vitisho, hakikisha unasahau unaachilia na kusonga mbele ukijihakikishia furaha katika maisha yako

·         Unapoteza muda kukaa chini na kulalamikia watu au mazingira kuwa ndio sababu ya kushindwa kwako,

·         Unasikitikia mambo yote uliyoshindwa kuyatimiza katika mipango yako, au unaketi chini kukumbuka mambio ya kushindwa kwako yaliyopita

Mtu wa Mungu unapokaa chini na kuanza kufikiria kile watu wanasema au wanakufanyia hutaweza kutoboa kumbuka kuwa hao wanakupotezea nguvu zako, unachotakiwa kukifanya ni kusonga mbele na kutokupoteza nguvu zako, wakati mwingine huhitaji hata kuwajibu wanaokushambulia Nehemia 4:1-3 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.”Wakati wote usikubali kukaa katika mambo ambayo yatakupotezea nguvu hakikisha kuwa unasonga mbele, usikubali kitu au jambo likukalishe chini, unapokuwa unakubali watu au mtu Fulani aushike moyo wako maana yake utahitaji watu wa kukutia moyo, wa kukusiafia ili ujisikie vizuri, utashindwa kukabiliana na wajibu muhimu ulioko mbele yako na mazingira yatakutawala na kukukalisha chini na kukuchelewesha, inuka songe mbele, usipoteze nguvu zako, acha kazi zako zijibu hoja za wapinzani wako!

5.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuangalia nyuma – Marrianne Williamsone aliwahi kusema hivi nanukuu  “we do not heal the past by dwelling there, we heal the past by living fully in the present” kwa tafasiri isiyo rasmi ni kama anasema hivi hatuwezi kujiponya na mambo ya nyuma kwa kukaa na kuyakumbuka tunaweza kujiponya na mambo ya nyuma kwa kuishi sasa, kwa lugha nyepesi wakati wote tunapaswa kuyasahau yaliyo nyuma na kuyaangalia yaliyo mbele Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” Mtu mwenye moyo wa ushujaa wakati wote ataangalia mbele, hatupaswi kuangalia nyuma aidha kulikuwa na mafanikio au tulishindwa, wakati wote tuwaze kufikia malengo makubwa na kuyatimiza kwa ubora zaidi,  wachungaji wengi wakifikisha kanisa lina watu 200 tayari wanadhani wamefikia mahali pa kupumzika, mwanafunzi ana maksi tisini au themanini amepitisha kiwango cha matokeo yaliyowekwa na shule anaridhika, Mwalimu amefaulisha au shule na imashika nafasi Fulani njema mtu anadhani amefika, hatuna budi wakati wote kuhakikisha kuwa haturidhishwi na mafanikio madogo tunayoyapata ilihali tunaweza kwenda zaidi ya vile  kwaajili ya hayo ndugu zangu ni muhimu sana kuhakikisha kuwa tunaangaluia mbele, Mtume Paulo alikuwa ni mtume aliyefanya kazi kubwa kuliko wote, alikuwa muombaji na mwenye uwezo mkubwa sana wa kunena kwa lugha kuliko watu wote, alihubiri injili na kuupindua ulimwengu wa wakati wake. Aliishi maisha matakatifu na kuwa kielelezo, hata cha kuwataka watu wanfuate yeye kama anavyomfuata Kristo, alipewa mafunuo makubwa sana lakini anasema anasahau yaliyo nyuma na anayachuchumilia yaliyo mbele, kila wakati tuhakikishe kuwa tunaongeza viwango na kuachana na mafanikio madogo ya nyuma.

 

6.       Mwenye moyo wa uhujaa hapaswi kuwaogopa wanadamu inasemekana kuwa mwanadamu ndiye mnyama anayetisha zaidi kuliko wanyama wote, ili uwe na moyo wa ushujaa ni lazima ujifunze kutokuwaogopa wanadamu, wao ndio viumbe tunaoshindana nao katika mambo yote ndio wanaoweza kutumiwa na Mungu kwa mafanikio yako lakini vilevile ndio wanaoweza kutumiwa na ibilisi wakasimama kama vikwazo ili uweze kutoboa katika maisha yako usiwaogope wanadamu Kumbukumbu la torati 3:21-22 “Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda Bwana, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda Bwana kila ufalme huko uvukiako. Msiwache, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.” Ili uwe shujaa Mungu anataka kuona ukimuogopa yeye tu peke yake wale tunaoshindana nao ni wanadamu tu kama sisi, kwa msingi huo hatupaswi kwa namna yoyote kuwaogopa kwa kuwa wewe unapiganiwa na Mungu wako, Mungu akiisha kusema nawe na akiisha kukupa wazo la kufanya katika Nyanja yoyote lifanye maana Mungu yuko pamoja nawe na amekupa watu kwa msingi huo usiwaogope watu Yoshua 8:1 “Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake;” kwa kawaida Mungu anakupa ushindi wa vita hata kabla hujaingia katika vita vyenyewe, na kwa sababu hiyo haitakuwa vema kabisa kuogopa, unapoogopa watu  na kufadhaika unaondoa uwepo wa Mungu maana yake unashindwa kumfanya Mungu atende kazi na wewe na kwa sababu hiyo utaleta kushindwa,  Zaburi 56:11 “Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?” Mwandishi wa zaburi hii ana ushahidi wa kushangaza yeye nguvu zake ziko katika kumtegemea Mungu kiasi ambacho  anajua kabisa kuwa akama ukiweka tumaini lako kwa Mungu ni dhahiri hofu taondoaka na hautaogopa chochote, kujifanya tu uko vizuri huku humtegemei Mungu ni kiburi,  Lakini kuweka tumaini kwa Mungu kunakupa ujasiri sio kusema tu humuogopi mwanadamu lakini hata majeshi yakijipanga kwa mtu anayemtegemea Mungu bado hawezi kuogopa ona Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.Kama utajifunza kutokuwaogopa wanadamu na kuangalia imani yako na kuweka tegemeo lako na tumaini lako kwa Mungu lazima ukumbuke kuwa ni Mungu ndiye atakayekupigania na kukusaidia na kukushuindia hivyo hupoaswi kuoopa changamoto ya aina yoyote ile na hupaswi kuwa na moyo wa unyonge, wewe utamwangalia Mungu tu.

 

7.       Mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuogopa mabadiliko -  Tunaishi katika ulimwengu ambao mambo yanabadilika kwa haraka sana kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknoliojia, lakini moja ya maswala ambayo yanawatishia watu ni pamoja na mabadiliko watu wengi wanaogopa mabadiliko, kwa sababu hiyo wanapingana nayo, kwa mfano moja ya jambo ambalo watu wengi wanaliogopa katika taifa letu ni pamoja na mabadiliko ya katiba, watu wanaogopa sana lakini mabadiliko ya katiba hayaogopeshi kama yalivyo mabadiliko ya viongozi, kama tunaweza kubadili viongozi wetu kwa amani basi vilevile tunaweza kuibadilisha katiba yetu kwa amani, jambo la msingi tu ni kwa wale wanaoona hitaji la katiba mpya watoe Elimu ya kutosha kuinyesha kwanini sasa tunahitaji mabadiliko ya katiba, ili waoogopa wajue kwanini tunahitaji katiba mpya, dhambi ni kushinikiza tu kuwa ni lazima tuwe na katiba mpya huku hata wapiga kura wakiwa hawajui kwanini tuwe na kaiba mpya, tukiipata itatunufaisha nini ina manufaa gani, hakuna sababu ya kuogopa, kwa msingi huohuo watu wanaoweza kuleta mabadiliko na kutoboa ni wale ambao kwa namna Fulani hawaogopi kubadilika kwa mambo, ukiogopa mabadiliko utapoteza nafasi nyingi za muhimu ambazo zingekujilia kuliko kuogopa Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”  Unaona mwandishi wa zaburi hii aonyesha kuwa haogopi mabadiliko, lazima akili ya mtu shujaa ijiandae kwa mabadiliko, na kukubaliana nayo, kama tumemtegemea Mungu tujue tu katika maisha yetu pia kwamba kuna kupanda na kushuka, kuna wakati kwa kila jambo, kuna kudhiliwa, kuna wakati wa magumu na kwa vyovyote vile hali yoyote ya mabadiliko haipaswi kuwa sababu ya kuondoa ujasiri katika maisha yetu Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”Mwandishi anaonyesha kuwa hakuna kitu maana yake hakuna aina ya mabadiliko ya maisha itakayomtenganisha na Yesu Kristo, iwe dhiki, au shida, au njaa, au uchi au hatari au upanga hata kama tunauawa iwe jua iwe mvua atabaki katika imani bila kujali hali ikoje? Wako watu wengine haki yao ya wokovu inategemeana na hali ya hewa, hali yao ya kumuamini Mungu, inategemeana na hali ya hewa na mazingira kukiwa na shida anamuacha Yesu, hawa ni watu wanaoogopa mabadiliko, unasikia watu wanasema wokovu wa siku hizi, kumbe kuna wokovu wa zamani, wa siku hizi je wa siku zijazo utakuwaje maandiko yanatuambia kuwa Yesu ni yeye yule jana leo na hata milele, Neno la Mungu linatuonyesha kuwa watru wenye moyo wa ushujaa wanaendelea kubaki vilevile bila kujali kuwa mazingira yakoje hawaogopeshwi na mabadiliko, wakati wote huyatumia mabadiliko kama wimbi la kuelekea katika Nyanja nyingine, nimeona kuna wanafunzi wanaogopa mabadiliko, Mwalimu fulani hayuko sijui itakuwaje, fomart ya mitihani imebadilika sijui itakuwaje, syllabus imebadilika sijui itakuwaje, bei ya hiki na kile imepanda sijui itakuwaje kwani ilipokuwa nafuu ulifanya nini? Ndugu zangu mwenye moyo wa ujasiri haogopi mabadiliko!.

 

8.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuogopa Kushindwa! – Kushindwa ni sehemu ya maisha tunajifunza mengi mazuri kwa watu waluioshindwa kuliko hata washindi, Biblia imejaa mifano ya watu wengi wanaoitwa mashujaa wa imani ambao maisha yao yamejaa ushindi kwa msaada wa Mungu hata hivyo Roho Mtakatifu hajaacha kuonyesha kushindwa kwa watu hao, tunawaonaga wachezaji wakikatwa mtama na kutibiwa na hatuimaye kuinuka tena na kuendelea na kucheza hawakati tamaa kwa sababu wameshindwa, shule za Private zamani zilikuwa ni shule za watu walioshindwa ndio wanachukuliwa na kuandaliwa na kufanywa washindi tena!, kushindwa ni moja ya changamoto kubwa sana katika maisha ya wanadamu na inaogopewa na watu wengi sana wengine hawataki hata kujaribu kwa sababu wanafikiri watashindwa! Kama ingekuwa unaweza kuchagua aina za washirika wa kuchunga kama mchungaji mimi ningetamani sana kuchunga watu walioshindikana, walioanguka, wenye madeni, wanyonge hao ndio ningetamani wanijie alafu nionyeshe uwezo wangu wa kichungaji na niwawezeshe wao kuonyesha uwezo wao na uzoefu wao wa kushindwa ulivyo wa muhimu sana na unavyoweza kuwaletea ushindi dhidi ya wale wanaofikiri wanaweza!  1Wakoritho 1:26-31 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.” Mungu huwa haogopi kushindwa kwa hiyo ana chagua vitu au watu dhaifu kisha anawatumia kwa utukufu wake, kushindwa kwetu katika maeneo mbalimbali hakukufanyi wewe uwe dhaifu bali kunakufanya wewe ujue ni changamoto gani unaweza kuziepuka na ukaleta ushindi, kwa hiyo lazima tujaribu tena na tena, Daudi jeshi lake lilikuwa na watu hodari sana lakini wengi waliomwendea na kujiunga naye walikuwa watu duni ona  1Samuel 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.” Inashangaza sana kuona kwamba Daudi alikuwa jemedari yaani ni mkuu wa majeshi lakini tunaambiwa jeshi lake liliundwa na watu duni, watu waliokuwa na dhiki, waliokuwa na madeni tena wameshindwa kuyalipa huko watu waliojaribu maisha wakashindwa hao ndio wanaunda jeshi la Daudi unaweza kuona, lakini katika namna ya kushangaza sana hawa ndio waliotumiwa na Mungu na kuleta ushindi mkubwa, hawaogopi kushindwa kwa sababu inaonekana walishashindwa mara nyingi, Waamuzi 11:1-3 “Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha.Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye.” Ni katika hali kama hiyo Yeftha pia tunaelezwa kuwa alikuwa mtu shujaa yaani jemadari na jeshi lake liliundwa na watu mabaradhuli, hii ni jamii ya watu walioshindwa maisha lakini baadaye walileta ushindi mkubwa, mtu anayeogopa kushindwa hawezi hajta kujaribu, tunaweza kukwepa mambo kadhaa wa kadhaa na hatimaye tukakosa mambo ya msingi na ya muhimu kwa sababu tu tunaogopa kujaribu kwa sababu ya kuogopa kushindwa! Kumbe kushindwa kunaweza kutupa uzoefu utakaotuletea ushindi wa kweli, tunajifunza vitu vingi kwa namna ya kushindwa, watoto kusimamam na kutembea na kujua mambo mengi kwa kujaribu na kushindwa, baiskeli kwa namna ya kuanguka na kuumia, lugha kwa namna ya kuanguka na kuumia, na hali ya kiroho wakati mwingine kwa kuanguka na kuinuka tena hatimeye kusimama

 

9.       Mtu mwenye moyo wa ushujaa haogopi kukataliwa -  watu wengi sana wanajiepusha na mambo Fulani kwa sababu wanaogopa kukataliwa, mtu anaweza kuona binti mzuri na akampenda lakini akashindwa kusema chochote kwa sababu anaogopa kukataliwa, hata wanandoa mtu anaweza kuogopa kuomba jambo Fulani kwa mwenzi wake kwa kudhani kuwa atakataliwa, kwa sababu ya kuogopa kukataliwa wakati mwingine katika maisha yetu tunabakia palepale na hatusiongi mbele Biblia imejaa ushahidi wa watu wengi ambao walikuja kufanya vizuri katika nafasi zao lakini mwanzoni walikataliwa Mwanzo 37:18-20 “Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.” Yusufu alikuwa na ndoto ambayo ingekuja kuwafaa ndugu zake lakini alipowasimulia hawakufurahi, walikusudia kumuangamiza ili waone ndoto zake zitakuwaje mkono wa mungu ulikuwa pamoja naye na akatoboa Matendo 7:9-10 “Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote.” Unapokataliwa huo sio mwisho wa maisha Oprah Winfrey alikuwa ni mtangazaji wa taarifa za habari jioni katika televisheni Fulani na alifukuzwa kazi kwa sababu hakuweza kuzuia hisia zake wakati akitoa habari, kwa hiyo alitimuliwa kama mtanzagaji asiyefaa, alianzisha kipindi chake kiitwacho Oprah Winfrey show na kuwa mtu maarufu sana na baadaye kuwa tajiri mkubwa na mtu mwenye kibali ambaye unaweza kusimama naye wakati wa kampeni za kisiasa, sasa ni moja ya watu wenye ushawishi mkubwa nchini Marekani, Msanii Harmonize ambaye alitokea WCB au wasafi hapa Tanzania unapomuona anaonekana kama kituko flani hivi na ndio hali halisi, lakini wakati anaanza sanaa alikataliwa na watu wanaohusika na kuinua vipaji katika mashindano maarufu yajulikanayo kama Bongo Star search, kwamba hafai na ajaribi fani nyingine, leo hii Harmonize ni moto wa kuotea mbali, hakujali kukataliwa, hakukata tamaa, alipambana kupigania ndoto zake kwa nguvu zake zote leo hii Harmonize ni next level  kwa hiyo neno la Mungu, kwa msingi huo mtu kukuambia haufai au kukukataa haimaniishi kuwa huwezi kuachieve au kufikia kile unachotaka kukifikia, hakikisha wakati wote unapambana kuifikia ndoto yako Yefta alikataliwa na ndugu zake lakini walipoozidiwa walienda kumuomba yeye awe mwamuzi juu yao Waamuzi 11:1-2Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine.” Unaona hapa Yefta anakataliwa laiki mtu huyu alikuwa ni shujaa mno na baadaye wale walimkataa yalipowakuta walienda kumuomba aje awasaidie na akakubali kurudi na kuwasaidia watu wake ona Waamuzi 11:4-11 “Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?  Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu? Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye Bwana atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya Bwana huko Mispa.”

 

10.    Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuwa na mashaka – ni ukweli ulio wazi kuwa watu wengi huogopa kujaribu mambo kwa sababu wanaona shaka, watu wana mashaka ya kujaribu kitu kingine, wanaogopa kuwa labda kujaribu kitu kingine kunaweza kusiwaletee maisha mazuri, lakini kukaa tu bila kujaribu kwa sababu ya mashaka kutakufanya udumae na Yesu aliwakemea wanafunzi wake mara kadhaa kutikana na kuwa na mashaka Mathayo 14:25-31 “Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.  Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? ” Yesu anatuonyesha wazi kuwa hakuna lisuilowezekana kwa mtu anayeondoa shaka ukiweka mashaka utashindwa lakini ukiondoa shaka utashinda angalia Marko 11:23-24 “Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Mashaka yatakuondoa kwenye malengo, mashaka yatakuondoa kwenye imani, amshaka yatakutupa nje ya mpango wa Mungu, mashaka yatakufungia mafanikio yako Yakobo 1:5-7 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.”

 

11.   Mtu mwenye moyo wa ushujaa hapaswi kuogopa kukosolewa “Critics” -  kwa kawaida kukosolewa na au kuhukumiwa na wanadamu katika mambo tunayoyafanya, kukosolewa au kuhukumiwa na wanadamu katima maswala tuyafanyayo ni jambo la Muhimu sana, nani kawaiada  hivyo hatupaswi kuogopa kukosolewa wala kuhukumiwa wala, ukweli ni kuwa watu watakuhukumu na wakati mwingine kwa maneno makali, lakini ukiwa na moyo wa ushujaa utaishi sawa na thamani ya vile ulivyo, na hiyio ndio njia ya mafanikio ya kufanikiwa kwako, unaposoama sana ni rahisi wenzako kukuambia umetumwa na kijiji, unapojituma sana ni rahisi kuambiwa na wenzako unajipendekeza, Yesu alikosolewa katika kila anachokifanya na hata alipotoa Pepo walisema anatumia nguvu za giza za mkuu wa pepo Belizebul Mathayo 12: 22-24 “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.” Paulo mtume alihakikisha kuwa wakati wote anakubali kila aina ya udhaifu, dharau, taabu udhalimu na mateso kwaajili ya Kristo Yeye alikuwa mtu mkubwa sana katia ulimwengu war oho alipata mafunuo makubwa sana kuliko mtu awaye yote lakini hakuwahi kujisifu, na alikubali kukosolewa wala hakukumtisha kwa sababu alimuweka Kristo mbele 2Wakoritho 12:1-10 “Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana.Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua);ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene. Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu. Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu. Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” Lengo lake yeye ilikuwa Yesu atukuzwe katika mazingira yote, kwa msingio huo basi hatuna budi kuhakikisha kuwa tunakabiliana na kutikuogopa aina yoyote ya kukosolewa tukijua ya kuwa kuna lengo tunakusudia kulifikia     .

12.   Watu wenye moyo wa ushujaa hawaogopi kupoteza maslahi yao – Kupoteza maslahi ni moja ya hofu inayowakumba watu wengi sana, kwa mfano kutokana na kujiunga na chama Fulani cha kisiasa na kupoinzana na kingine unaweza kujikuta unapoteza maslahi, kumfuata Yesu na kuacha dini nyingine inaweza kukufanya upoteze maslahi, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoteza nafasi ya kuwa Mwalimu wakati wa ukoloni alipoanzisha TANU ili kuwaunganisha watanganyika wapiganie uhuru, kwa hiyo ni wazi kuwa wakati mwingine ili uelekee katika manufaa Fulani huna budi kukubali kupoteza maslahi yako, Wafilipi 3:7-11 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;  ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.” Watu wanaowekeza katika biashara, na maswala mengine mara nyingi ni risk takers wako tayari kujilipua, lakini wakati mwingine tunaweza kuchukua hasara kwaajili ya kuwatetea wengine.

Hili ndilo jambo la msingi zaidi ambalo mwanadamu anaweza kulifanya ili Mungu awe pamoja na kumfanikisha katika kila jambo ni kuwa na moyo wa ushujaa, bila moyo wa haina hii huwezi kuitomboa katika Nyanja ya aina yoyote ile

 

Ujumbe: Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 13 Juni 2021

Hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena Milele !


Msatri wa Msingi: Kutoka 14:14-14Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”




Utangulizi:


Siku moja Bwana Mungu aliviita viungo vyote katika mwili wa mwanadamu na akataka kuwauliza ili kujua wanafanyaje kazi? Kichwa kilielezea yote, Moyo, mikono miguu na kila kiuongo kwa jinsi yake, Lakini kiungo kimoja kilikuwa na malalamiko dhidi ya kiungo kingine, kiungo kilichokuwa na malalamiko kilikuwa ni *Ulimi* na mlalamikiwa alikuwa ni *Meno*, Kesi iliposikilizwa, ulimi ulisema kuwa mimi ni laini sana Mzee na umeniweka na Meno ambaye kwaasili yeye ni mgumu, tunapokuwa katika kazi ya kulainisha chakula mara kwa mara Meno huning’ata na kuniumiza na hivyo nachukua siku kadhaa kupona na kuendelea na kazi zangu, Mungu alimwambia ulimi usilalamike, ulaini wako haumaanishi kuwa wewe ni dhaifu kuliko meno, wewe ni mgumu sana, kuliko unavyojifikiri utaumizwa na utapona, na utaendelea kuwepo,  lakini sivyo ilivyo kwa meno ambaye anaonekana kuwa mgumulakini ukweli yeye ni dhaifu, baada ya miaka kadhaa utahesabia meno na utakubaliana nami kuwa mengine yataliwa na wadudu na hutayaona tena na yatang’olewa, lakini wewe ulimi utadumu hata mwisho wa dahari, ni kweli ulimi ulivumilia na kutoa muda kwa meno na wakati wa uzee, ni ulimi pekee aliyeonekana kudumu na kutokuchoka tena ukiwa na nguvu zake vilevile!


Lolote lile linalokusumbua katika maisha yako, na kukuumiza lipe muda tu, iko siku litang’oka, Wamisri waliwaonea wana wa Israel na kuwatumikisha kama watumwa kwa miaka mia nne na thelathini, Lakini siku moja wakati Israel wakiivuka bahari ya shamu, Musa alitabiri kuwa hawa wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele, unabii huu ulidumu kwa muda mfupi tu, kwani hata Musa aliusema akiwa kama kiongozi na mwenye kuwatia moyo watu wake kama mchungaji, lakini yeye mwenyewe alimlilia Mungu kwa hali aliyokuwa anaiona, Mkono wa Mungu ulikuwa mwema kwani aliwafutilia mbali Wamisri wale waliokuwa wakiwaandama wana wa Israel ili kuwaonea.


Leo nakutangazia kwa jina la Yesu, Magumu yote yanayokukabili na changamoto zote unazozipitia hautakuja uzione tena milele, Bwana atakupigania nawe hutanung’unika milele, Bwana atakustarehesha, Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya, kila changamoto unayokutana nayo katika maisha yako na inayoonekana kuwa ngumu au tishio kwako, hayo ni kama magego tu na wewe ni kama ulimi wewe ni imara zaidi kuliko wao na kuliko changamoto zako, Mungu anayejua kuwa uko katikati ya magumu atakutetea, Changamoto hizo kwa mamlaka niliyopewa kama mtumishi wake natangaza  leo ziwe mwisho na usizione tena katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, Natangaza kuwa changamoto zinazokukabili hautaziona tena, sema amina

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Alhamisi, 3 Juni 2021

Ni mizuri kama nini miguu yao, wahubirio habari ya mema!


Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!



Utangulizi:

Ujumbe huu wa Nabii Isaya ulikuwa ni ujumbe wa maono ya siku ya ukombozi wa Yerusalem ambao vilevile huitwa sayuni, Ni ujumbe unaohusiana na Israel (Wayahudi) kuletewa ujumbe wa amani kutoka kwa mfalme Koreshi ya kwamba Mungu amemtuma awatangazie uhuru wayahudi waliokuwa utumwani huko Babel kwamba warejee kwao na kuujenga tena mji wao na Hekalu la Mungu wao baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi, Nabii anaona maono ya ukombozi anawaona wajumbe juu ya milima ya Yudea wakiiletea Yerusalem habari za kufunguliwa kwake! Ona


Isaya 40:9-11 “Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope; Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Nabii Isaya hakupata nafasi ya kuona kile kilichowapata wana wa Israel (Wayahudi) waliochukuliwa utumwani wakati wa Mfalme Nebukadreza, lakini aliweza kuona na kutabiri katika ulimwengu wa kiroho na kuwaona wayahudi wakipelekwa utumwani lakini vilevile wakirejea, Unabii wake huu hasa unatoa matumaini kwa Wayahudi ambao wangechukuliwa utumwani na kuwatia moyo ya Kwamba Mungu angewatokea tena na kuwarejeza.

Wayahudi walichukuliwa utumwani na Mfalme aliyeitwa Nabukadreza kimsingi mfalme huyu wa wakaldayo, alikuwa ni mwana wa Nabopolassar na alipata utawala mwaka wa 604 Kabla ya Kristo baada ya kuanguka kwa utawala wa waashuru, Jina lake kamili hasa linaandikwa na kutamkwa kama Nebuchadrezzar ambalo kwaasili ni “Nabu-Kudurri-usur” ambalo maana yake ni Nebo linda mipaka yangu (Nebo ni mungu wa wakaldayo) Mfalme huyu aliyekuwa katili sana na aliyekuwa dikteta mkubwa mno ametajwa zaidi ya mara tisini katika agano la kale.

Wayahudi wanamkumbuka Mfalme huyu kama moja ya wafalme katili sana ambaye wao wanamuhesabu kuwa aliwafanya wayahudi kama moja ya wanyama, alipopata utawala alikuwa na kampeni ya kupanua mipaka yake ya kuitawala Dunia mpaka Misri na kuhakikisha kuwa kila mfalme anamtii yeye na akawa mfalme wa wafalme, Wayahudi pia walitawaliwa na mfalme huyu, na Yehoyakimu mfalme wa wayahudi alitakiwa kujinyenyekesha chini yake na alipoasi jamaa alimuharibu ona

2Wafalme 24:1-3 “Katika siku zake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu;kisha, akageuka,akamwasi.Naye Bwana akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii. Hakika kwa amri ya Bwana mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;


Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Nebukadreza vilevile aliliharibu Hekalu la Yerusalem na kuchukua vyombo vitakatifu na kuvipeleka katika hekalu lake huko Babeli wakati wa mfalme Yehoyakimu

2Nyakati 36:5-7 “Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake. Juu yake akakwea Nebukadreza, Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya Bwana mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.”
Aidha alimuua mfalme wa wayahudi na kuutupa mwili wake bila kuuzika sawa na alivyotabiri nabii Yeremia ona

Yeremia 22:18-19 “Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.” Ona pia

Yeremia 36:30-32 “Basi, Bwana aseme hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi. Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza. Ndipo Yeremia akatwaa gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.
Licha ya kumuua mfalme wa wayahudi na kumtupa bila kuzikwa, Nebukadreza pia alichukua utumwani kundi la wayahudi wapatao 4,600 ona

Yeremiah 52:27-30 “Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake. Watu hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu; katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili;katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita.” 

Mfalme huyu ambaye hakuwa na huruma aliamuru mateka watembee moja kwa moja bila mapumziko mpaka Ukaldayo bila kupumzika hata hatua moja, akiamini kuwa wayahudi wakipewa nafasi tu watapata muda wa kusali na kuomba na kutubu kwa Mungu wao na wanaweza kupata rehema, hivyo ili wakose pumzi ya kupata kanafasi ka toba na kusababisha Mungu wao kubadili mawazo alihakikisha kuwa wanakula kibano sawia, alipofika ukaldayo alifanya sherehe kubwa sana ya kufurahia ushindi wake na kuwalazimisha wayahudi waimbe nyimbo za Sayuni kwa miungu yake huko


Zaburi 137:1-3 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.”


Vijana wazuri wenye nguvu na hekima walihasiwa ili wawe watumishi wa mfalme yaani walifanywa kuwa matowashi, akiwepo Daniel, Hanania, Mishael na Azaria, walikuja kujulikana baadaye kama Shedrack, Meshak na Abednego ona Daniel 1:1-4 “Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.”                

Licha ya mateso haya ya kiutu na kisaikolojia Mateka wengi waliachwa na njaa, walipigwa na jua kali, walitembezwa wakiwa uchi mpaka wakawa weusi, njaa ilisumbua watu wazima mpaka vitoto vichanga, ilifikia  hatua hata wanawake waliokuwa na huruma walikula watoto wao kwa zamu Maombolezo 4:8-10 “Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti. Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba. Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.” Kuna maswala mengi sana ya kikatili yaliyofanywa na Mfalme huyu mkubwa sana na dikteta wa hali ya juu aliyekuwa amejaa kiburi mpaka aliponyenyekeshwa na Mungu, ukweli ni kuwa hata wayahudi walipofika utumwani hawakuwa na maisha salama waliendelea kutumikishwa katika shughuli ngumu na kali na mateso. Aidha kiimani walilazimishwa kuabudu na kuitumikia miungu migeni ya Ukaldayo kwa ujumla waliishi Maisha ya wasiwasi na kutokuelewa kuwa kesho yao itakuwaje jambo hili liliwafanya waikumbuke Sayuni, wakumbuke Yerusalem wawe na tamaa ya kurudi kwao, Kwa hiyo nabii Isaya licha ya kuona mateso haya kinabii vilevile alitabiri kuwa anawaona malaika wa Bwana wanashuka juu ya milima ya uyahudi wakitangaza habari njema, ni habari ya kuwekwa huru, ni habari ya kuamuriwa kurudi Yerusalem, ni habari ya kurudi nyumbani, ni habari ya kwenda kuwa na ushirika na Mungu wao ni habari ya kwenda sehemu ambako unabii wa kuja kwa masihi ungetimizwa ni habari ya kurejeshewa kwa matumaini yao, ni habari ya kuelezewa ya kuwa mambo yatakuwa mazuri, Nabii isaya anasema ni Mizuri kama nini Miguu yao juu ya milima ya uyahudi waletao habari za amani, waenezao habari njema wasemao habari za wokovu waambiao watu Mungu ndiye anayetawala yaani ufalme wa Mungu u karibu  hii ilikuwa ni kauli ya furaha kwa watu waliokata tamaa, kila mmoja anaweza akawa yuko katika hali ya mateso na hali isiyofurahisha wala kuridhisha kila mmoja anahitaji ukombozi, anahitaji kusikia habari njema Baada ya kutimizwa kwa unabii huu wa Isaya Mungu alimuinua mfalme mkuu Koreshi wa uajemi ambaye alitoa habari njema kwa kuwaruhusu Wayahudi warejee Yerusalem ili kulijenga tena hekalu na vilevile kukomesha utumwa wa wana wa Israel na mateso yao ona Isaya 44:28 “nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.” Isaya 45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;” Unabii Isaya wa isaya ulitimizwa miaka 180 baadaye Isaya alikuwa na maono ya ajabu sana mpaka ya kutaja jina la Mfalme huyo mabaye Mungu alimuita Mtumishi wake na mpakwa mafuta waka na Mchungaji wake, hii ni wazi kuwa mtumishi awaye yote wa Mungu atakayetenda mapenzi halisi ya Mungu ni yule mwenye miguu mizuri anayetangaza habari njema na za amani na za wokovu na za kuwaweka watu huru, katika namna nyembamba kiongozi huyo ni Koreshi bali katika namna pana Kiongozi huyo ni Yesu Kristo, lakini wale wanaoihubiri habari njema yaani injili pia wanaitwa ni wenye miguu mizuri kwa sababu wanafanya yale mapenzi ya Mungu kwa watu wake.

Paulo anaitumia kauli hii ya Nabii Isaya katika Warumi 10:15b “Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya memaWahubiri katika agano jipya wanapaswa kuwatangazia watu habari njema za matumaini ya Kwamba Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai ndiye aliyekuwa anatabiriwa kutuletea habari njema ya ukombozi ya kuwekwa huru sio tu kwa Israel bali na kwa mataifa mengine, watu wameteseka vya kutosha chini ya utawala wa mfalme asiyekuwa katika mikono ya Mungu, shetani ni mfalme wa wafalme aliye katili sana mwenye kuwatesa watu na kutokuwapoa pumzi ya uhuru wala nafasi ya toba, Lakini Yesu ni Mfalme wa wa falme mwenye rehema, Wahubiri katika agano jipya hawapaswi kuwatisha watu, wala kuwabebesha watu mizigo, bali wanapaswa kuwafungua watu kutoka katika vifungo vyao, watu wa Mungu wana mahitaji ya aina mbalimbali na wanahitaji ukombozi wa kweli wala sio vitisho na migandamizo kutoka kwa watu waovu wanajipa mamlaka kubwa na kusahau kuwa yuko Mungu wa mbinguni na kuwa Mungu huyo ndiye anayetawala, Mungu anachokitaka kwa watu wake ni kuwatangazia habari njema huu ndio mpango wake Israel wote walikuwa wakiusubiri mpango huu ona Isaya 58:6 “ Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?       

Mungu anapenda watu wake wasamehewe, walegezewe mizigo yao inayowaelemea, wajisikie huru kutika kila aina ya uonevu na kila aina ya magereza inayowatesa hata kama ina nguvu kiasi gani nira yake ivunjwe mtu anayefanya hayo ndiye mwenye kuleta habari njema ndiye ambaye miguu yake ni mizuri kama nini, ndiye anayetangaza habari za kweli za wokovu, ni ujumbe kama huu ndio tunayaita maneno ya neema na nitangazo la namna hii ndio Yesu Kristo alikuja kulitimiza na kulifanya Luka 4;16-22 16. “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? unaona Masihi Yesu Kristo mwenyewe alipoianza kazi ya kuhubiri injili yaani habari njema alitangaza kufunguliwa kwa watu na jamii ya watu wa kwao WALISTAAJABIA MANENO YA NEEMA YALIYOTOKA KINYWANI MWAKE. Huyu ndiye ambaye kila mtu alikuwa anamgoja anayetangaza habari ya mema, habari za amani habari za kuwaweka huru waliosetwa, habari za kuwafungua waliofungwa, habari za vipofu kuona habari ya kutangaza jubilii yaani mwaka wa bwana wa neema, Mtu wa namna hii ndiye ambaye tunasema ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari njema, kutana sasa na wale wasiotangaza habari njema miguu yao ni mibaya utasikia Leo tunamtangaza dada fulani au kaka fulani kuwa tumemkabidhi kwa shetani, leo natangaza kumtega fulani, leo namfukuza fulani kutoka katika kanisa letu, leo tunaanza mfungo wa siku miamoja, leo ni siku ya kumtolea Bwana Isaka wako, leo ameondoka katika kanisa hili habari zake ndio kwishinei, leo nalaani wanaopingana nami, dhehebu hili ndilo bora kuliko lile, muhubiri yule anahubiri mafundisho potofu na yasiyofaa, yule ndio mzinzi namba moja, huyu jamaa si aliwahi kufumaniwa, yule hanizidi mimi kwa maombi,  sisi ndio waanzilishi wa imani, sisi tunauzoefu, mimi sibabaishwi na hiki ama kile, mimi nimetembea sana nimezunguka nchi nyingi sana duniani, mimi utaniambia nini, mimi nina miaka mingi sana katika wokovu au nimekutangulia sana katikla huduma na kadhalika nisikilize, watu hawahitaji kujua umezunguka nchi ngapi, hawahitaji kujua umesoma kiasi gani watu wanahitaji kustaajabia maneno ya neema yanayotoka kinywani mwako, watu wanahitaji kutangaziwa msamaha wa dhambi,  wanahitaji wokovu, wanahitaji utawala na ufalme wa Mungu, wanahitaji kufundishwa na kuwekwa huru kutoka katika vifungo mbalimbali, wanahitaji kuelekezwa kwa masihi ili awaponye na kuwaweka huru, watu wanaotangaza habari za namna hii ni adimu sana kuwapata siku hizi, watu watamleta Isaka wao na hata Yakobo kama tu watahudumiwa vema na kutangaziwa utawala na malamaka ya kiungu hawa ndio Isaya anawatabiri kuwa ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari njema, wanaoleta habari njema wanaotangaza amani, wanaotangaza mambo mema, wanaotangaza wokovu na kuwaambia watu uko ufalme wa Mungu na kuwaelekeza watu kwa Yesu!

Ni Mizuri kama nini miguu yao, wahubirio habari ya mema!

Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 24 Mei 2021

Jinsi ya kutupilia mbali aibu!!


Isaya 54:4 “Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.”



Utangulizi:

Moja ya changamoto kubwa inayotukumba wanadamu tangu anguko la mwanadamu kutokea  katika bustani ya Edeni ni pamoja na changamoto ya aibu, au kuona aibu, au kutahayari. Aibu ni moja ya fedheha kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, Hakuna mtu awaye yote anayependa kuaibishwa, Mpango wa shetani wakati wote ni kutuleta katika aibu, na kwa sababu hiyo kuna changamoto nyingi sana ambazo ibilisi huzifanya ili kutuleta katika aibu!, moja ya changamoto inayotuleta katika kuona/Kupata aibu ni pamoja na dhambi kama maandiko yasemavyo ona


Mwanzo 3:9-10 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.”


Adamu na Eva wazazi wetu wakubwa sana waliokuwa karibu sana na Mungu walipofanya dhambi, walijisikia aibu, kule kujiona kuwa wako uchi na kujificha ilikuwa ni ishara ya aibu kwao kwamba wamevunja sheria ya Mungu wao, ni ukweli usiopingika kuwa dhambi ni aibu ya watu wote ona


Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.”tunapofanya maovu kwa njia ya siri tunaweza kujifikiri kuwa ni wajanja na washindi, lakini dhambi zetu zinapofuniliwa na wengine wakazijua kwetu linaweza kuwa jambo la aibu, kwa msingi huo ni wazi kuwa aibu inaleta fadhaaa kubwa!. Na hakuna mwanadamu anayependa kuaibishwa!


Aibu hasa ni nini? Aibu ni tatizo la kisaikolojia na kisosholojia (Kijamii)- (Psychosocial-Problem) linaloendeshwa na hisia, hasi zinazotokana na dhamiri ya mwanadamu kujihuhukumu kuwa hajaenenda sawa na jinsi alivyopaswa kuenenda, ni hali ya kujitathimini kihisia na kujithaminisha katika hali ya chini na hivyo kupelekea kujitoa, kujificha, kujihukumu, kukosa furaha, kutokujitokeza, kutokujiamini, kukosa nguvu na kujiona hufai! Ni hofu ya kuogopa kuwekwa wazi kwa mambo yetu yasiyofaa tuliyoyafanya sirini, na wakati mwingine hutupelekea kuwashutumu wengine kwa kusudi la kuficha mambo yetu! Neno aibu kwa kiyunani ni Aischuno ambalo maana yake ni kuvuliwa nguo hadharani Yesu analishughulikia swala hilo la mtu kuvuliwa nguo kwa kutoa ushauri wa kutoa mavazi yatakayo ficha aibu hiyo ya kuwa uchi ona “Ufunuo 3:18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.” Hakuna mwanadamu awaye yote mwenye akili kamili na timamu ambaye atafurahia kuwekwa uchi hadharani, jambo kama hili ni aibu kwetu na kwa kila mwanadamu mwenye akili timamu.


Aibu ni moja ya tatizo linalohitaji kutatuliwa kiroho, Mungu katika Hekima yake na mpango wake wa ukombozi alikusudia pia kutukomboa kutoka katika aibu.  Yeye kama Muumba wa Mbingu na sisi anatujua vema namna na jinsi tunavyoteswa na aibu na hivyo aliwasaidia wazazi wetu wa kwanza kuwa mbali na aibu kwa kumwaga damu ya Mnyama ili awatengenezee mavazi ya ngozi na kuwavika hii ilikuwa ni ishara ya kinabii ya kuvikwa vazi la kutuondolea aibu yetu ona Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.Kwaajili ya hayo nabii Isaya anatupa ujumbe kwamba tusifadhaike wala tusiogope na kwamba hatutatahayari wala kuaibishwa na kuwa Mungu mwenyewe ataifutilia mbali aibu yetu, hakuna wa kutushutumu wala hatutakumbuka tena aibu! Milele! Kwa hivyo ni ahadi ya Mungu kutuondolea Mauti, ni ahadi ya Mungu kutufuta machozi lakini vilevile ni ahadi ya Mungu kuiondoa aibu ya watu wake milele angalia Isaya 25:8-9 “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.”  

             

Yesu alikuja kuiondoa aibu yetu!

Moja ya majukumu makubwa ya waamuzi,wafalme na manabii nyakati za agano la kale ilikuwa ni pamoja na kuwaondolea watu aibu, kuna aibu za aina nyingi sana, kushindwa vita ni aibu, kufungwa magoli mengi ni aibu, kufeli ni aibu, ndoa kuvunjika ni aibu, kuziniwa mkeo au mumeo ni aibu, kufukuzwa kazi ni aibu, kufanya uzembe ni aibu, kuomba omba ni aibu, kufumaniwa ni aibu, kuugua magonjwa mabaya ni aibu, kufiwa na mtu mnayemtegemea sana ni aibu, kusemwa vibaya ni aibu, kuvuliwa nguo ni aibu, kusutwa ni aibu, kudhalilishwa ni aibu, kufanyiwa ukatili wa kijinsia ni aibu, kushindwa vita ni aibu, kutengwa kanisani ni aibu na maswala mengi kadhaa wa kadhaa yenye kuumiza moyo, kwa ujumla hakuna mwanadamu anayependa aibu, Na ndio maana watakatifu waliotutangulia nyakati za agano la kale walimkimbilia Mungu ili wasiabike milele Zaburi 31:1 “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,” Tunapokuwa tumefunikwa na aibu tunakosa ujasiri wa kufanya mambo kwa ufasaha hata katika kumtumikia Mungu, vijana wengi sana hunifuata kwa siri na kwa kuwa mimi pia ni mkuu wa shule na mchungaji, hivyo wanafunzi wengi wa kiume hunifuata na kunieleza wazi wazi, kuwa mchungaji mimi napenda sana kumtumikia Mungu na ni kweli unaweza kuona ni vijana wenye vipawa mbalimbali vya utumishi na lakini unaweza kuwaona wanakwepa kufanya huduma zao walizopewa na Mungu nao huniambia tunasumbuliwa na tatizo la kupiga punyeto na ingawa tatizo hili linafanyika kwa siri lakini dhamiri zao zinawafanya wajisikie aibu na kukosa ujasiri wa kutumika ipwaswavyo, nami huwa ninawajibu na kuwasaidia katika namna na hekima ile ambayo Mungu hunipa niwahudumie, lakini Napata jibu kuwa kama tuna mambo ya aibu hata kama watu hawajayajua, ni ya sirini yanapunguza ufanisi wetu kwa kiwango kikubwa, kuna changamoto nyingi mno zinazofanana na hizo ambazo huwanyima watu kuutumia uwezo waliopewa na Mungu kwa kuwa ndani ya mioyo yao wana hisia za aibu, na zinakuwa mbaya zaidi zinapofunuliwa katika jamii na hivyo wengi wanashindwa kujiamini, Habari njema ni kwamba Yesu ndiye mwamuzi mkuu, ndiye nabii, mkuu na ndiye mfalme mkuu, Yeye ukiacha kushughulika na maswala mengine pia alikuja kwaajili ya kutuondolea aibu, tunapokuwa na aibu tunashindwa kufanya mambo lakini tunapokuwa na ujasiri tunaweza kufanya mambo makubwa sana, Nisikilize Mungu anataka tumuone Bwana wetu Yesu Kristo kama sababu ya ujasiri wetu, wakati mwingine vilevile tunaogopa kukosea, tunatetemeka hatujiamini kwa sababu ya mambo ya aibu ya sirini au kwa sababu tunaogopa kuwamba tutakosea hatutafanya kwa ufasaha na kusababisha aibu hivyo tunaona aibu hata kabla hatujajaribu, huu ni uonevu wa ibilisi kwetu, Biblia inatuita kwamba tunapokuwa na hali kama hiyo na 

unapolemewa na aibu Mtazame Yesu –  Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”


Unapolemewa na aibu Kisogelee kiti cha rehema  - Waebrania 4;15-16 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”


Ujasiri wetu ni katika kumtumainia Kristo – Waefeso 3:11-12 “kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.”


Kumbuka kuwa sisi wenyewe hatutoshi – 2Wakoritho 3:4-6 “Na tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu. Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”   

     

Mtumaini Bwana – Warumi 5:3-4 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” Tunapoweka tumaini letu kwake Mungu wetu hatatuacha tuaibike wala hatawaacha adui zetu wafurahi Zaburi 25: 1-3 “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.”


Tumuombe yeye atufunike – Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.Mungu anaijua aibu yetu anaelewa kioa kitu tuko wazi mbele zake hatuwezi kujificha Adam hata kabla hajaomba Mungu alijua fedhea ya Adamu alieleza wazi kuwa amejificha waliposikia sauti ya Mungu kwa sababu yuko uchi, Mungu alifanya mavazi kwaajili ya Adamu na mkewe akawavika, Yesu kama mwokozi anajua kwamba anawajibika kutufunika , tukimwamini hatutaaibika kamwe Warumi 10:11 “Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.” Yaani kila amwaminiye hataaibika unaona


Tumtumikie yeye wala tusiache yeye atatusitiri – Zaburi 91:1-4 “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.” na Zaburi 27:4-5 “Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”


Hakuna wa kukushitaki Yesu ndiye mtetezi wetu – Zakaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”    

          

Jinsi Yesu alivyoiondoa aibu yetu!

Maandiko kadhaaa hapo yametutia moyo kwamba hatupaswimkuogopa, na kuwa tunapaswa kuwa na ujasiri, kwa nini kwa sababu Kama Mungu alivyoshughulika na aibu ya adam na Eva na vilevile malaika wa bwana alivyoshughulika na aibu ya Yoshua kuhani mkuu ni ufunuo wa kimaandiko ulio wazi kuwa Yesu Kristo anashughulika na mambo yetu yote ya aibu na dhambi, Yeye alipoishughulikia dhambi pale msalabani na kuaibishwa aliaibihwa kwa niaba yetu, na kwa mateso yake akaimwaga damu yake pale msalabani ni wazi kuwa damu yake inafunika dhambi zetu na sio kufunika tu inaziondilea mbali kabisa, Yesu aliwaendea watu waliokuwa ni aibu kabisa katika jamii, wasio na matumaini wala kufikiri mkwamba itakuja itokee siku kuna mtu atawajali lakini wote aliwavuta kwake na kuwaingiza katiia mpango wake wa ukombozi, tunapozungumza wiokovu wetu ni pamoja na kufutiwa aibu yetu, hatupaswi mkuogopa wala kujidharau na kufikiri kuwa sisi hatufai hata kidogo, wala hatupaswi kuwalaumu watu, tunaye Mungu ambaye anajua kushughulika na aibu zetu kwa huruma zake na rehema zake atatufunika tunachotakiwa ni kumjia na kumueleza kuwa Bwana Yesu mimi sifai hata kidogo, nisamehe nisafishe kwa damu yako na kwa kazi yako uliyoifanya pale msalabani, na kwa njia rahisi sana weka imani kuwa amekusamehe na kukuelewa Mungu anatuelewa vizuri kuliko kiongozi yeyote wa kidini, hatupaswi kujificha, hupaswi mkuaxcha kuimba, hupaswi mkuacha kuhudhuria ibada na kumtumikia Mungu, Mwambie Bwana Yesu afanye kazi na wewe kwa utukufu wake akufiche chini ya ushindi wake akufunike kwa neema yake, usitishiwe na mtu yeyote kwa sababu wote biblia imesema wote ni wenye dhambi, wote tunaokolewa bure kwa neema kwa njia ya imani, asikutishe mtu kazi ya ukombozi sio mya mwanadamu wala haifanywi kwa vitisho vya kidini na viongozi wa kidini, wala kwa kukutenga imefanywa na Yesu pale msalabani nani yeye ndiye anayeweza kutuhukumu na kutuhesabia haki na sio mwingine, hakuna mamlaka yoyote inayoweza kukutenga na upendo wa Kristo, hata malaika hawawezi, viongozi wa dini hawawezi,  wako watu wanajipa mamlaka hata za kutenga au kukabidhi mtu kwa shetani, ni wajinga tu mwana akiwaweka huru mnakuwa huru kwelikweli watafunga hewa watatenga hewa mimi na Yesu tunaendelea kuwasiliana milele anaendelea kunibariki anaendelea kunitumia na wataisoma namba viongozi vipofu wa vipofu,  majoka wana wa majoka kuta zilizopakwa chokaa hakuna mtu wa kututenga na upendo wa Kristo, hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, ni watu waliojaa kiburi na jeusi wanaochukua nafasi ya Mungu tu wanaoweza kujifanya wana mamlaka ya kufunga lolote au kufungua lolote, nataka ujue ya kuwa mamlaka hiyo umepewa wewe na mimi, wakifunga nafungua mwenyewe wakifungua nafunga mwenyewe, wakikufukuza kwenye dhehebu lao na kuweka zengwe nenda linguine, wakikukataa anzisha la kwako liite hata kwa jina lako Muhubiri Yesu anza hata na mkeo na mwanao ahaaaaa, mpaka walalamike kuwa madhebu yamezidi utawajibu na vilabu vimezidi, acha kusikitika wanapokuaibisha kata aibu Yesu yuko kutupilia mbali uonevu Warumi 8:33 -35 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? ” kisha 38-19 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !    

Mtu wa kumwangali


Zaburi 37:37 “Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.

 

Utangulizi:

 

Moja ya njia ya kujihakikishia kuwa tunasonga mbele katika safari ya imani, ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunasahau yaliyo nyuma na kuyachuchumilia yaliyo mbele, Hii ilikuwa njia mojawapo ya mafanikio kwa Mtume Paulo ona

 

Wafilipi 3:12-13 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;”

 

ukimuuliza mtu ni nani anaweza kuwa mtu wako wa mfano au shujaa wako, kila mmoja anaweza kuwa na watu kadhaa ambao anavutiwa nao na anawaiga kiimani, Binafsi katika maswala ya imani navutiwa sana na Bishop Zachary Kakobe kwa kuwa ndiye aliyekuwa Mchungaji wangu wa kwanza mara baada ya kuokoka niliokokea katika kanisa lake nilipoikuwa nasima Makongo Secondary Jijini Dar, Lakini pia navutiwa sana na mafundisho ya Muhubiri Mwalimu kutoka Ghana anayeitwa Mensa Otabil napenda anavyofundisha neno la Mungu, naweza kuwa na watu wa mifano katika siasa, uongozi, watumishi na kadhalika Katika Biblia ukimuacha Yesu Kristo navutiwa sana na Paulo Mtume katika agano jipya na Daudi katika agano la kale, watu tunaowafanya kuwa mfano wetu wa kuigwa, huwa tunawaiga imani zao na kuwafuata kama vile wanavyomfuata Yesu Kristo, kuwakumbuka wale waliotuongoza, waliotuambie neon la Mungu ni agizo la kibiblia ona

 

Waebrania 13:7 “Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.”    

 

Hata hivyo maandiko yanatuasa pia kuwafuata wao na kuwaiga wao kama vile wanavyomfuata Kristo kwa sababu wao ni wanadamu

 

1Wakoritho 11:1Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” Wanadamu wote katika maandiko ambao tunaweza kuvutiwa nao na wakawa mifano kwetu walikuwa na mambo mengi na sifa nyingi njema lakini vilevile walikuwa na madhaifu ya aina mbalimbali ya kibinadamu kwa mfano:-

 

1.       Adamu na Eva – Ndio wazazi wetu wa kwanza, hawakuzaliwa waliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, walikuwa na ushirika wa karibu na Mungu wakizungumza naye usokwa uso, Mungu alikuwa muumba kwao na baba kwao, aliwadekeza na kuwamilikisha kila walichokitaka. Walipewa mamlaka mna utawqala dhidi ya kila kitu Duniani, wanyama waliwaogopa, hata hivyo walimkaidi Mungu na kumuasi kwa kula matunda waliokatazwa na Mungu,  wakawa sababu ya kuleta kifo na mauti duniani, leo hii wote tunapata tatizo la kifo kwa sababu yao ona:-

 

Mwanzo 3:11-13 “Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.

 

2.       Nuhu aliyetajwa kuwa mtu wa haki mkamilifu katika vizazi vyake na kwamba alikwenda au kutembea pamoja na Mungu na katika ulimwengu uliokuwa umeoza kwa uovu yeye pekee na familia yake walipata neema Machoni pa Bwana ona

 

Mwanzo 6:8-9Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu.Pamoja na ukamilifu wake wote baadaye maandiko yanatutaarifu kuwa ndiye mgunduzi wa kwanza wa Pombe na ndiye mtu wa kwanza kujihushisha na ulevi na sio hivyo tu alikunywa divai akalewa  na kusababisha aibu kubwa

 

Mwanzo 9:20-22 “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.”

 

3.       Ibrahimu anayetajwa kuwa baba wa imani na rafiki wa Mungu, Baada ya miaka mingi sana ya ukimya tangu Mungu alipozungumza na Nuhu, hakuwa amezungumza na mwanadamu awaye yote kwa Karne nyingi sana mpaka alipozungumza na Abrahamu na kufanya maaganio naye Ibrahimu anaitwa mtu wa kwanza kuwa na uhusiano na Mungu aliye hai baada ya karne nyingi, Ni baba wa imani kwelikweli Imani ya kiyahudi na Kikristo na Uislamu zinaitwa Abrahamic Religions yaani ni imani ambazo mizizi yake imeanzia kwa Ibrahimu Warumi 4;16 “Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; Mungu alikuwa na urafiki wa Karibu na Ibrahimu kwatika ushirika wa ajabu sana kiasi cha kumuita rafiki yake ona Isaya 41:8 “Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu;” Lakini hata hivyo maandiko yanatutaarifu kuwa yeye alisema uongo zaidi ya mara moja, kwa sababu ya woga na kutokumuamini Mungu kwaajili ya ulinzi wake,

 

Mwanzo 12:18-19 “Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako.”

 

Mwanzo 20:1-5 “Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. 


Isaka na Yakobo wanaotajwa na Mungu pale anaposema mimi ni Mungu wa Ibrahimu Isaka na Yakobo 


Kutoka 3:15-16 “Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri; wote tunafahamu kuwa Isaka alisema uongo vilevile Mwanzo 26:6-7 “Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.Yakobo ndiye aliyekuwa muongo zaidi na mwenye hila zaidi akijifanya kuwa ni Esau na wanawe pia walimdanganya kuhusiana na habari za Yusufu kuwa aliuawa na mnyama ilhali walimuuza kwa hiyo hawa wote walikuwa ni wanadamu na walikuwa na udhaifu wao!

               

4.       Musa anayetajwa kuwa mpole au mnyenyekevu kuliko watu woote wakaao juu ya uso wa nchi Ona katika Hesabu 12;3 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” Biblia inatuambia kuwa Musa ndiye aliyekuwa mtu mpole, myenyekevu kuliko watu wiote wakliokuwa juu ya uso wanchiyeye naye kuna wakati alikasirika sana na kunena Maneno yasiyotegemewa na hata hatimaye kushindwa kumstahi Mungu pale Meriba jambo lililomkosesha kuingia katika nchi ya Kanaani, Hesabu 20:10 “Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?             

 

 Kumbukumbu 3;23-26 “Nikamnyenyekea Bwana wakati huo, nikamwambia, Ee Bwana Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu? Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng'ambo ya Jordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni. Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili.”      

5.       Daudi mtu anayetajwa na Mungu kuwa ni mtu aliyeupendeza moyo wake, Matendo 13;21-22 “Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.” Wote tunafahamu ushujaa wa Daudi, mtu aiyependa uonevu, mtu mwenye kumcha Mungu, kiongozi mkuu sana wa ibada lakini maandiko nayo yanasema yeye naye alifanya dhambi ya zinaa na mke wa Uria, alimpa na mimba, alimuua na mumewe kisha akajioza yeye mke huyu wa uria ona 2Samuel 11;2-5 “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito., 


    2Samuel 14-27Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe. Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa. Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita; akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita, itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani? Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye. Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu. Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni. Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye. Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo. Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe. Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza Bwana.”  

6.       Suleimani alikuwa mwenye Hekima kuliko watu wote, aliwaonya watu wajiepushe na maswala mbalimbali ya uovu katika kitabu cha mithali, lakini pia aliwataka watu wamkumbuke Mungu tangu siku za ujana wao, Mungu alizungumza na Suleimani wazi wazi, na kumtaka aombe lolote, alikuwa mtoaji kwa rekodi ambazo hazijawahi kuvunjwa 1Falme 4;29-34 “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki. Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.” lakini aliangukia katika tamaa ya wanawake iliyokuwa ya kutisha sana akaoa wanawake wengi sana na wanawake zake wakamgeuza moyo akaabudu miungu ona 1Wafalme 11;1-4Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti,na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake              

7.       Mtume Petro alikuwa mtu wa kwanza kudai kuwa yuko tayari kwenda na Bwana Yesu gerezani na aliapa luwa hatamkana Yesu kamwe! Mathayo 26:31-33 “Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.” Petro aliahidi mbele za Yesu kuwa yeye atakuwa tayari hata kwenda naye gerezani lakini wakati wa majaribu Petro alimkana Yesu mara tatu ona Mathayo 26:69-75 “Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu.Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo.Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.

 

Nini cha kujifunza?

 

Sisi wote ni wanadamu tu, manabii na mitume nao ni wanadamu, wachungaji walimu , wazee mashemasi na washirika wote ni wanadamu tu, katika namna fulanifulani za uanadamu wetu tunajikwaa Yakobo ambaye alikuwa mtume na askofu mkuu wa kanisa lililokuwako Yerusalem Ndugu yake Yesu wa kunyonya aliyeitwa James the Just alikuwa muombaji na mtu wa haki alisema katika Yakobo 3:2 “Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. Sisi sote kama binadamu tunajikwaa katika mambo mengi hakuna mwanadamu aliyemkamilifu, Mungu hututumia kwa sababu ya mambo mazuri ya upande wa jambo zuri analotaka kulitimiza kwetulakini kama Mungu angelikuwa anaangalia ukamilifu wetu hakuna amabaye angeweza kusimama mbele zake sio Musa wewe wala mimi, tunapoona madhaifu kadhaa wa kadhaa kwa viongozi wa kidini, tunapaswa kukumbuka kuwa wao sio kielelezo chetu, wao ni binadamu tu, udhaifu wao hauondoi ukweli kuwa wokovu upo, Mungu anaokoa, na kielelezo chetu ntulichopewa kukifuata ni Yesu Kristo pekee, wao walitolewa ili kutumia vipawa walivyopewa na Mungu kutuelekeza kwa Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye CHEO CHA KIMO CHA UTIMILIFU WA KRISTO;” Yesu Kristo ndiye Mwanzilishi wa imani yetu, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamfuata yeye katika mwenendo wetu wote Waebrania 12:2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.” Maandiko yanatutaka tumtazame yeye kwa sababu yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote bila kufanya dhambi ona Waebrania 4:15 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.” Imani yetu haisimami kwa mtu inasimama katika Kristo Yesu, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaacha kuwaangalia wanadamu na kumtazama mtu mkamilifu ambaye mwisho wake utatupa amani, Ni Yesu pekeee aliye mkamilifum, ni Yesu pekee aliye kielelezo chetu, tutawafuata wengine na kujifunza kutoka kwao kama vile wanavyomfuata Yesu lakini wakikengeuka haiwi sababu ya sisi kulaumu, au kuacha wokovu au kurudi nyuma kwa sababu Yesu hajawahi kurudi nyuma, acha kuwatazama wanadamu mtazame Yesu, mtazame Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai acha kuwashutumu wanadamu, acha kuwaangalia wao, wao ni watu tu tunaye kuhani mkuu aliyejaribiwa katika mambo yote bila kufanya dhambi, Baba mtakatifu he is not our hero he is not our rolemode, askofu mkuu, wa jimbo waangalizia, mapadri na mashemasi na kdahalika wao sio kielelelzo chetu Yesu Kristo pekeee ndio kielelezo chetu kikuuu, yeye ndiye aliyetuita tumfuate 1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Never compromise becase someone somewhere sheor he has compromise he/she is not our example our real example is Jesus Christ the son of the living God!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!.