2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika
njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao
waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la
Ahithofeli liwe ubatili”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa unapokuwa
kiongozi wa ngazi yoyote ile, iwe kisiasa au kiimani, huwezi kupendwa na kila
mtu, sio viongozi tu lakini hata katika maisha haya ya kawaida, wanakuwepo watu
wanaotukubali sana na vilevile wako watu ambao hawawezi kutukubali, hili ni
jambo la kawaida sana, hatuwezi kuwapendeza watu wote, sisi sio wema sana kama
Masihi Yesu Kristo yeye alikuwa mwema mno kuliko mtu awaye yote lakini watu
walimchukia na kufikia ngazi ya kumsulubisha Luka 15:18-20 “Iwapo ulimwengu
ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama
mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi
si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo
ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa
kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika
neno langu watalishika na lenu.” Unaona Yesu hapa alikuwa
anawafundisha viongozi, yaani hawa ni wale wanafunzi 12 wa Yesu ambao walikuwa
kimsingi wanaandaliwa kuwa viongozi wa kanisa, si unakumbuka Yesu alikuwa na
wanafunzi wengi? Ila wachache waliandaliwa kuwa viongozi, sasa kaka kiongozi
kama Yesu aliongoza vizuri na wakamfanyia mabaya wakamuasi ni wazi kuwa sisi
tutafanyiwa mabaya makubwa zaidi Luka
23:31 “Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika
mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” kulijua jambo hili mapema ni
muhimu kwa sababu biblia inatufundisha vilevile namna ya kukabiliana na
changamoto za aina hii na namna tunavyoweza kumuomba Mungu yanapotokea maswala
magumu katika maisha yetu!, Leo tunachukua muda tena kujifunza kwa undani
kuhusiana na jinsi Mungu alivyomtetea mtumishi wake Daudi alipokuwa kiongozi na
alipokuwa akitimiza majukumu yake kwa Mungu! Namna na jinsi alivyomuomba Mungu
kwa hekima na Mungu akamsikia.
2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika
njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao
waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la
Ahithofeli liwe ubatili”
Katika mstari wetu wa msingi leo,
tunajifunza mojawapo ya tukio gumu sana lililopata kumtokea Mfalme Daudi akiwa
madarakani, Daudi alipata jaribu la kupinduliwa madarakani na kijana wake wa
kumzaa aliyeitwa Absalom, hata hivyo uasi wake haukuwa na nguvu sana mpaka pale
mtu mmoja muhimu mno katika utawala wa Daudi aliyeitwa Ahithofeli, alipoungana
na upande wa uasi, Mtu huyu alikuwa ndiye mshauri mkuu wa Mfalme Daudi na
alikuwa na sifa kubwa muhimu mno Maandiko yanasema uwezo wake wa kushauri
ulikuwa sawasawa na Mtu anapouliza kwa Mungu ona.
2Samuel 16:23 “Na shauri lake Ahithofeli,
alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu;
ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.”
Unaweza kuona kwamba mtu huyu
alikuwa na nafasi muhimu sana kwa mfalme na nafasi yake kama mshauri wa mfalme
ilikuwa nafasi muhimu sana, Licha ya kuna na nafasi hii inasemekana pia
Ahithopheli alikuwa na kijana wake ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa maakida
yaani makomandoo au mashujaa wanaotajwa
kuwa waliokuwa mstari wa mbele katika majeshi ya Daudi Mfalme ona
2Samuel 23:34 “na Elifeleti, mwana wa
Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;”
Unaona huyo Eliamu alikuwa ni
kijana wa Ahithofeli kwa msingi hio kwa vyovyote vile lazima ieleweke wazi kuwa
Ahithofeli alikuwa mtu muhimu na hakuwa mtu wa kawaida na katika mashauri na
hekima alikuwa mtu muhimu kwa mfalme kwa miaka Mingi.
Hekima ya Ahithofeli
Wengi tunajiuliza ni nini
kilimpata Ahithofeli kwanini alimchagua Absalom aliyeasi badala ya Daudi?
Kwanini mtu huyu aliyekuwa na ujuzi wa kushauri na hekima ambayo inatajwa kuwa
alikuwa akishauri, ushauri wake ulikuwa sawa na mtu kutafuta ushauri kwa Mungu?
Nini kilimpa sifa kuwa anavyoshauri ni kama mtu akiuliza kutoka kwa Mungu? Watu
wengi wanasema kuwa huenda ushauri wake kumwambia Absalom azini na wake za baba
yake ulikuwa ushauri mbaya na usio wa kiungu, Binafsi ninakataa ushauri wake
Ahithofeli ni kweli kabisa ulikuwa kama ushauri utokao kwa Mungu, Mapema sana
Daudi alipofanya dhambi na kumtwaa mke wa Uria na kisha kufanya njama za kumuua
Uria, Nabii Nathan alitumwa na Mungu kuja kumuonya Daudi dhidi ya dhambi zake
na adhabu ambazo angepewa ona
2Samuel 12:1-13 “Ndipo Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye
akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa
tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali
yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na
kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake,
na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata
msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake
mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri
aliyemfikilia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia
yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule;
akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake
astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu
ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia
Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia
mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa
nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya
Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo
kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya
machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke
wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga
hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti,
kuwa mke wako. Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba
yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye
atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa
siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi
akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana
naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.”
Uko uwezekano ulio wazi kabisa
kwamba maelekezo haya yaliyotolewa na Nabii Nathani ambayo yalikuwa yanatoka
kwa Mungu wakati yanatolewa Ahithofeli hakuwepo kabisa na mwandishi wa Kitabu
anamuona Ahithofeli kama mshauri ambaye ushauri wake anapoutoa ni kama mtu
anayeuliza kutoka kwa Mungu, kwanini kwa sababu ukiiangalia adhabu hii ambayo
Mungu alikuwa ameitangaza Nathan Nabii kwa Daudi na ushauri aliokuwa anautoa
Ahithofeli ilikuwa ni kama mtu anayetaka kulitimiza neno lililotoka kinywani
mwa Bwana kupitia nabii wake
2Samuel 16:20-23 “Kisha Absalomu akamwambia
Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje. Naye Ahithofeli akamwambia
Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza
nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako;
ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. Basi wakamtandikia
Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya
babaye machoni pa Israeli wote. Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa
siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa
mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.”
Unaweza kuona namna na jinsi
Ahithofeli alivyokuwa na Hekima ya ajabu, na uwezo mkubwa wa kushauri sawa na
mapenzi ya Mungu, Ahithofeli alikuwa na hekima na busara kubwa na alijua namna
ya kuishawishi jamii, kitendo cha kumshauri Absalom alale na masuria wa baba
yake hadharani kiliifanya kambi ya Absalom kupata nguvu kwani kiliwaaminisha
kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa kijana amemchukia baba yake waziwazi hivyo
waliweza kuiteka mioyo ya watu, kiuadilifu ushuri huu haukuwa mwema lakini
kinabii Ahithofeli alisaidia kutimia kwa unabii wa Nathan na ahadi ya Mungu ya
kumuadhibu Daudi, na ndio maana mapema sana Absalom alipoasi alimuhitaji mtu
huyu aliyekuwa Mshauri hodari, mwenye hekima na sio tu kuwa alikuwa mwenye
hekima lakini vilevile alikuwa shujaa yaani alikuwa na ujuzi wa kivita kwa
hivyo uasi wa Absalom ulipata nguvu kubwa sana alipompata Aithofeli, vita hiii
ilikuwa moja ya vita ngumu sana kwa Daudi na uwezekano wa kushinda ulikuwa ni
mdogo kama sio rehema za Mungu ona
2Samuel 15:10-13. “Lakini Absalomu
akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia
sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamiliki huko Hebroni. Na watu
mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika
ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli
Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa
akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na
Absalomu wakazidi kuwa wengi. Mjumbe akamfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu
wa Israeli inashikamana na Absalomu.”
Kwa namna na jinsi Daudi
alivyofahamu uwezo wa Ahithofeli alijua wazi kabisa kuwa vita imekwisha kuwa
kali sana na kutoboa kwake kuko katika mazingira magumu mno, Daudi alitoroka
ikulu akiwa miguu peku na akajitanda nguo kichwani akiwa analia kwani alihitaji
rehema za Mungu tu, kumuokoa katika vita ile kali
2Samuel 15:30 “Daudi akapanda akishika njia
ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda.”
Swali kubwa la kujiuliza ni
kwanini Ahithofeli aliyekuwa na hekima namna hii, Hekima yake haikumuongoza
kuungana na Daudi? Kulikuwa na dhida katika maisha ya Ahithofeli, Hekima yake
ilimezwa na uchungu na moyo wake wa kutokusamehe na kuachilia! Na roho mbaya
Hekima imemezwa kwa uchungu!
Ahithofeli Pamoja na kuwa alikuwa
mtu muhimu na kuwa yeye na mwanaye wote kwa Pamoja walimtumikia Daudi katika
kulitimiza shauri la Mungu, Na kuwa mtu mwenye hekima ya kupita kawaida
tunaposoma maandiko mwanaye anatajwa kuwa ni Eliam
2Samuel 23:34 “na Elifeleti, mwana wa Ahasbai,
na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;”
unapofanya uchunguzi wa
kimaandiko inaonekana kuwa binti wa Eliam kijana wa Aithofeli ndiye Bathsheba ona vizuri katika maandiko
haya
2Samuel 11:2-3 “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani,
akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona
mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.
Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je!
Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? ”
kwa maana hiyo sasa Ahithofeli
alikuwa ni babu wa Bath-sheba, binti wa kijana wake Eliamu, kwa msingi huo basi
Ahithofeli alitunza uchungu moyoni kwa kitendo alichofanyiwa mjukuu wake
aliutunza uchungu huo kwa miaka mingi, hivyo alikuwa akimtumikia mfalme kwa
unafiki, hivyo ndivyo uchungu ulivyoharibu maisha ya mtu mwenye hekima ya
ajabu, uchungu uliweza kuharibu sio hekima yake tu hata maisha yake baadaye,
uchungu huu ulifunuliwa sio tu kwa kuungana na Absalom lakini inaonekana katika
ushauri wake alikuwa na nia ya dhati ya kumshambulia Daudi, sio tu akitumia
Hekima yake lakini alikuwa tayari hata kumshambulia kwa mikono yake na kumuua ona
shina la uchungu linapunguza neema ya Mungu kwetu na kutufanya tufanye
mambo ya hovyo,
Waebrania 12: 14-15 “Tafuteni kwa bidii
kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona
Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la
uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa
hilo.”
Kutokana na kutunza uchungu kwa
Muda mrefu Aithofeli sasa anapanga kumuua Daudi kwa mikono yake mwenyewe,
anajiamini kuwa hakuna sababu ya kusumbua watu wala kumwaga damu ya watu wengi
hapa ni kummaliza Daudi pekee na kazi imekwisha,
2Samuel17: 1-4 “Zaidi ya hayo Ahithofeli
akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka
na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka,
na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja
naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza
kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote
watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni
pa wazee wote wa Israeli.”
Unaweza kuona Ahithofeli alikuwa
anajiamini sana hii ni wazi kuwa mtu huyu licha ya kuwa Mshauri na mtu mwenye
hekima vilevile alikuwa anajua kupigana, kama kijana wake Eliamu alikuwa moja
ya mashujaa wakubwa katika makomandoo wa Daudi ni wazi kuwa Ahithofeli alikuwa
na uwezo mkubwa na mbinu kali za kivita alihitaji watu 12 elfu tu na angemuua
Daudi tu na kazi ingekuwa imekwisha, ni wazi kabisa kumbe uchungu unapotunzwa
moyoni watu wanatunza mauti,
Mathayo 5:21-22 “Mmesikia watu wa kale
walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni,
Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake,
itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.”
Ni wazi kuwa uchungu na kisasi
kinaweza kuharibu Hekima ile Mungu anayoikusudia kwetu maisha ya Aithofeli na
maneno yake na mpango wake ulionyesha wazi kuwa ana uchungu mkubwa na Daudi na,
Daudi ni kweli alikuwa amefanya dhambi na alikuwa kweli amejutia dhambi yake
alitubu mbele ya Nathani Nabii na alikuwa ametamkiwa msamaha na kukubali adhabu
zote ambazo Mungu alikuwa amezikusudia, hata hivyo kwa upande wa Pili
Ahithofeli alikuwa hazijui njia za Mungu yeye aliendelea kuitegemea akili yake
mwenyewe na kusahahu kuwa ziko njia za kiungu
Mithali 3:5-8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana,
ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.”
Unaona Ahithofeli alikuwa ameacha
kumtegemea Mungu wala hakumtumaini kwa lolote alizitegemea akili zake alikuwa
mwenye hekima machoni pake mwenyewe, alichukulia poa kile kitendo cha
kukubalika katika Israel na kusifiwa na wazee, hakumcha Mungu na kwa sababu
hiyo hakujua kuwa uovu ulikuwa unammendea, uchungu ukamuharibu mtu mwenye
hekima moyo wake ukajaa kulipiza kisasi na kutaka kuua mtu asiye na hatia kwa
Mungu, Daudi alitambua njia za Mungu, alifahamu kuwa Mungu atamhurumia na kumpa
rehema alimuomba Mungu na kumtegemea yeye, hata kabla ya kupanga vita na
kupigana yeye alimuomba Mungu, Daudi alikuwa tayari hata kuwasamehe watu
waliomtukana
2Samuel 16:5-12 “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka
huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera;
alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi
wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume
na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda
zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! Bwana amerudisha juu yako damu yote ya
nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika
mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako
mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya,
akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke,
nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana
wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani
Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? Daudi akamwambia
Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu,
anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa
sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata,
naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo.” Daudi
alizifahamu njia za Mungu, alisamehe hata waliomlaani, akijua wazi kuwa Mungu
atazigeuza laana zao kuwa Baraka!, Daudi alimtegemea Mungu kwa asilimia 100 na
hakuzitegemea akili zake tu, Daudi alimlilia Mungu!
Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili
Daudi alitumia njia ya kiungu,
Yeye mwenyewe alikuwa shujaa wa vita, lakini alikuwa na uzoefu kuwa hakuna vita
ambayo alipigana peke yake, alijua kuwa siri kubwa ya ushindi wa vita yake ni
Bwana, tangu ujana wake alipompiga Goliathi alimpiga kwa jina la Bwana wa majeshi
ya Israel, na kila wakati alihitahi fadhili za Mungu ziweze kumpigania na
alihitaji kujua kuwa bwana yuko upande gani, kumbuka Daudi alikimbia ikulu
akiwa analia alipaza Sauti yake juu akilia kwa uchungu na kurusha mavumbi juu
alikuwa akimlilia Mungu aweze kuingilia kati
2Samuel 15:30 “Daudi akapanda akishika njia
ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda.”
Akiwa katika hali hii ya
kuomba Daudi alielezwa kuwa Mshauri wake muhimu sana wa kutegemewa alikuwa
amejiunga na uasi wa Absalom, huyu ndiye Ahithofeli alikuwa sasa amemsaliti alikuwa
ni mtu wa karibu sana kwa Daudi lakini amemgeuka,Huenda hii ndio sababu ya
Daudi kuimba zaburi hii
Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena
niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.”
Pamoja na mambo mengine Daudi
alimuomba Mungu dua muhimu sana iliyoleta ushindi katika maisha yake Daudi
alisema maneno haya
2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika
njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa
amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja
naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia
walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao
waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, EE BWANA, NAKUSIHI, ULIGEUZE SHAURI LA
AHITHOFELI LIWE UBATILI”
Daudi aliyalaani maarifa na
hekima ya Ahithofeli tangu wakati ule iwe ubatili, aliibatilisha hekima yake
haithofeli ikapate kuwa ubatili, na Maarifa yake yawe ujinga, hii ilikuwa duwa
Muhimu sana inayoweza kutupa ushuindi katika maisha yetu hata katika wakati huu
tulio nao, tunapokuwa na vita zozote za kiroho, tunapokabiliwa na majanga
mazito na maadui wanaotafuta kutuua au kutuangamiza au kutuumiza au kutujeruhi,
maombi pekee tunayoweza kumuomba Mungu ni kuifanya hekima yao maadui zetu kuwa
ubatili ma maarifa yaio kuwa ujinga Daudi alikuwa anajua kuwa Mungu wa Mbinguni
ana uwezo wa kutangua mashaurui ya watu wabaya, anauwezo wa kuharibu mikono ya
watu waovu isitimize makudui yao na kuzinasaa hekima zao kuwa hila na mashauri
yao kuharibika kwa haraka
Ayubu 5:12-13 “Yeye huyatangua mashauri ya
wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. Yeye huwanasa wenye
hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.”
Ni tabia ya Mungu kugeuza
mashauri ya wanaojidhani kuwa wana hekima, au maarifa ni kazi yake kuwatia
wazimu, kuwarudisha nyuma na kuyafanya maarifa yao kuwa ujinga
Isaya 44:24-25. “Bwana, mkombozi wako, yeye
aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote;
nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami? Nizitanguaye
ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima,
na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;”
Watu wasiotembea katika njia za
Mungu wamejaa chuki, hawana upendo, wamejaa kisasi, kila wakati wanatafuta
mabaya watu hao hawatoboi, Mungu anaigeuza Hekima yao kuwa upumbavu
Warumi 1:21-22. “kwa sababu, walipomjua
Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika
uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye
hekima walipumbazika;”
Mungu yuko tayari kuiharibu
hekima ya watu wenye hila hekima ya dunia hii na amaeahidi katika neno lake
kuwa ataiharibu hekima yao wanaojidhani kuwa wana hekima na atazikataa akili
zao wanaojidhania kuwa wana akili na hekima ya kidunia itafanywa kuwa upumbavu
1Wakoritho 1:19-20. “Kwa kuwa imeandikwa,
Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu
wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je!
Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?”
Aithofeli alikuwa amemezwa na
uchungu, hivyo Hekima na akili yake ilikuwa sio ya kungu bali ilikuwa ya dunia
hii hekima iliyojaa ugomvi na kuondoa amani hii ndiyo Mungu anaibatilisha
Yakobo 3:14-18. “Lakini, mkiwa na wivu
wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya
kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya
kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo
machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena
ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na
matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika
amani na wale wafanyao amani.”
Mungu aliishikia Maombi ya Daudi
Katika namna ya kushangaza sana
Daudi alimtuma mshauri wake mwingine rafiki yake wa karibu aliyeitwa Hushai
kwamba aende kwenye kambi ya maadui, awe miongoni mwa washauri wa Absalom na
atumike kutangua ushauri wa Aithofeli, kwa kuwa tayari Ahithofeli alikuwa
amejawa na uchungu na moyo wa kisasi na kutokusamehe, lakini zaidi sana kuwa na
chuki dhidi ya mpakwa mafuta wa Bwana na hata kukusudia kumuua , Mungu
aliutumia ushauri wa Hushai na kwa mara ya kwanza ushauri wa Aithofeli
ulikataliwa na hapo ndipo mtu huyu mwenye kiburi alipokimbia nyumbani na kwenda
kujiua mwenyewe
2Samuel 17:1-14 .”Zaidi ya hayo Ahithofeli
akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka
na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka,
na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja
naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza
kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote
watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni
pa wazee wote wa Israeli. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki,
naye, tukasikie atakayosema yeye pia. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu,
Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama
alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Shauri
hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.Hushai akafuliza kusema, Wamjua
baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika
mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni
mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.Angalia, amefichwa sasa katika shimo,
au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu
atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi
hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana
Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio
pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka
Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na
wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na
kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja
wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao
wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota
mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye
Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema
kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja
shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.”
Unaona hivi ndivyo Mungu alivyomtetea Mtumishi wake Daudi na kubatilisha shauri
la Aithofeli hebu na tuone yaliyomkuta sasa
2Samuel 17:23“Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake
halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini
mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa
babaye.”
Ahithofeli anamwakilisha Yuda,
kama jinsi ambavyo Yuda alimsaliti Yesu na kisha alipopata uchungu alikwenda
akajiua yeye mwenyewe, Hekima yake ya kumuza Yesu iliishia kuwa mauti, hatuna
budi kuhakikisha kuwa wakati wote tunafanya mambo katika hekima ya kiungu,
tunapamba kwa kutumia hekima ya Mungu na tujue namna ya kumuo,ba Mungu katika
maisha yetu abatilishe kila makusudi mabaya ya adui zetu ama wale wanaotutakia
mabaya na wale wenye hekima za dunia hii zilizojaa hila na uchungu tujifunze
kumtegemea Mungu katika mambo yote wala tusizitumainie akili zetu wenyewe,
Bwana atupe neema yake ili tuweze kuzijua njia zake na Mungu wangu na bwana
wangu na aifanye hekima ya adui zetu kuwa ubatili na maarifa yao kuwa upumbavu
katika jina la yesu Kristo Amen
Rev. Innocent Samuel
Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye hekima!
#0718990796#