Jumatatu, 30 Agosti 2021

Si kumwamini tu ila na kuteswa kwaajili yake!


Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa mojawapo ya masomo ya msingi sana mara baada ya mtu kumuamini Yesu, ni pamoja na uelewa mpana ya kwamba kumfuata Yesu sio jambo jepesi kama wengi wanavyokudhani, Lakini kumuamini Yesu, vilevile kutaambatana na changamoto kadhaa ikiwemo mateso, Wahubiri wengi wa nyakati za leo wameacha kuwakumbusha watu wa Mungu kwamba mateso, dhiki na udhia ni sehemu ya injili, kuhubiri upande mmoja tu wa mafanikio bila kuisema kweli hii ni sawa na kuhubiri injili ya mafanikio “Prosperity Gospel” kufanya hivyo ni kushindwa kutoa mlo kamili (The balance diet) wakati wa kuwapikia watu neno la Mungu, Lakini kutokuwatahadharisha watu ya kuwa kuna dhiki na udhia na mateso na hata kuuawa kwaajili ya injili ni kuwa kinyume na mafundisho ya Yesu na Mitume pia ambao wao kwa uwazi walikaza kuwa ni lazima watu wanaomuamini wajikane nafsi na kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nayingi na hivyo wasine kuwa ni ajabu wanapopita katika majaribu ya aina mbalimbali ona   

Mathayo 16:24-25 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

Unaona? Kwa bahati mbaya nyakati za leo wahubiri wengi wa kisasa wanashindwa kuweka uwiano wa kuwaelezea watu ukweli huu kuwa kumfuata Yesu sio lele mama, kwa kadiri tunaposonga mbele katika imani utagundua wazi kuwa wokovu sio kitu chepesi na wala sio lele mama, tunahitaji sio tu kujikana nafsi lakini na neema izidiyo ili tuweze kustahimili, Nyakati za kanisa la kwanza somo kuhusu Mateso lilikuwa ni moja ya somo la kwanza la muhimu katika kuwaimarisha wanafunzi wa Yesu ona

Matendo 14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”        

Kumfuata Yesu kuna mchanganyiko wa mambo mazuri, furaha na amani, na mafanikio mengi sana  lakini vilevile kuna udhia yaani iko dhiki ambayo waliomuamini Yesu watakumbana nayo, Yesu aliweka wazi swala hili mapema wakati Petro alipouliza swali kuwa sisi tumeacha vyote tutapata nini kwa kufuata wewe? ona

Marko 10:28-30. “Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.”

Kwa msingi huo ni lazima ieleweke wazi kwamba kila mtu anayemuamini Yesu, sio tu kuwa kumuamini Yesu kutatufanya tusijaribiwe na au kupitia dhiki za namna mbalimbali hapana tutapitia dhiki na mateso ya aina mbalimbali Petro aliwaambia wakristo wa nyakati za kanisa la kwanza kuwa imani yao itajaribiwa kama dhahabu inapopitishwa katika moto

1Petro 1:6-7 “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

1Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.   

Unaona kupitia mateso, au misiba kwa mtu aliyemuamini Yesu halipaswi kuonekana kuwa ni jambo geni, maana yake ni jambo la kawaida kwa sababu nasi tunashiriki mateso pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo kwa msingi huo ni kawaida na tunapaswa kuwa na subira katika mapito haya, na kwa kadiri mtu anavyopenda kuishi maisha ya utauwa yaani maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu ndio anaudhiwa zaidi ona:-

2Timotheo 3:12 “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.”

Kwa msingi huo kuna  muhimu kuwaelimisha watu wa Mungu mapema wakaelewa kuwa kuwa kuwa katika mpango wa Mungu hakukufanyi wakati wote uwe na raha tu, Yesu alisema ulimwenguni mnayo dhiki lakini jipeni moyo mimi nimeushinda ulimwengu, watu wengi sana hudhani pia labda mtu unapopitia changamoto za aina mbalimbali labda uko nje ya mapenzi  ya Mungu, au hauko sehemu sahihi hapana uko sehemu sahihi na Yesu yuko pamoja nawe lakini hii haimaanishi kuwa dhoruba utazikwepa kwa msingi huo ni lazima upambane na kuendelea kumtegemea Yesu kwani hako mbali atashughulika na changamoto yako ona jinsi Yesu alivyowafundisha jambo hili wanafunzi wake kwa maneno na kwa vitendo:-

Marko 4:35-41 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.  Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?  Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Ilikuwa ni jambo la kushangaza kuwa ni Bwana mwenye aliyewaahidi wanafunzi wake wavuke ng’ambo, na Yeye mwenyewe alikuwemo chomboni, lakini ni jambo lenye kushangaza kuwa dhoruba kubwa ilitokea na kuwatisha sana wanafunzi wake hata wakashangaa kwanini Yesu amerelax na kulala usingizi wala hana hofu wakati wao wanakaribia kuangamia, lakini kwa wakati wake walipomwamsha akaukemea upepo, na kuwakemea na wao kwa kuwa hawakuwa na imani kwamba Mungu yuko Pamoja nao,

Jambo kubwa la msingi na la kulielewa ni kuwa majaribu hayo na mateso hayo hayatakumaliza, Mungu hajamaanisha katika neno lake kuwa hatutapitia changamoto bali anataka tuendelee kutambua hata ndani ya changamoto hizo yeye yupo na analo kusudi ndani yake kwa msingi huo hatuna budi kutamka maneno ya ushindi kwamba hata kupitia changamoto za aina gani yeye yuko pamoja nasi na ametushika kwa mkono wake hakuna changamoto itakayokumeza hususani pale Yesu anapokuwa ametuahidi kuwa atakuwa pamoja nasi, na kama ametukomboa na ametuelekeza lolote katika neno lake basi hatupaswimkuogopa na kudhani au kufikiri kuwa tutazama, Muujiza huu alioufanya Yesu una mafundishi wazi kuwa tunaweza kuwa katika mapenzi ya Mungu na tunaweza kuwa na Mungu mwenyewe na wakati huohuo dhuruba zikatupata hii haina maana ya kuwa neno la Mungu sio kweli, wala haina maana kuwa uwepoo wake umepungua hapana, Yuko pamoja nasi, anatupenda na ahadi zake kwetu ni ndio na kweli na tutapitia changamoto kadhaa lakini hiyo haimaanishi kuwa Mungu ametuacha yeye hatimaye ataikemea ile hali somo kama hili lilikuwa wazi pia hata kwa nyakati za watakatifu wa agano la kale ona :-

 Isaya 43:1-2 “ Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. ”   

Ni  imani yangu kwamba safari ya imani ina mawimbi, ina hofu,ina huzuni, ina mateso, lakini Kristo Yesu atatufikisha ng’ambo salama, Mashaka na hofu zinazotusonga  na dhoruba zitatusumbua lakini kama Yesu atakuwa pamoja nasi ni yeye aliyetuita kwa neno lake kwa hiyo hatupaswi kuogopa  tunapozidiwa kumbuka kuomba au kuimba kama Marehemu Fanuel Sedekia aliyeimba Nishike mkono na Bwana  naye Mungu Yule tunayemtegemea atakushika Mkono na hatatuacha tuzame na atatukomboa:-

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima  

Nishike Mkono

Fanuel Sedekia

Safari ya imani, nakutazama Yesu
Nataka nifike ng'ambo salama
Lakini njiani mawimbi ni mengi
Mashaka yanisonga kuniangamiza

Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe
Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe

Mawimbi ni makali nahitaji msaada
Nishike Mwokozi niwe salama
Wewe ulieniita nakuja kwa neno lako
Napata kutembea kwa neno lako

Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe
Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe

Safari ya imani, natembea kwa imani
Zambi isinishinde, nisaidie
Katika majaribu makali kama moto
Najua nitatoka kama dhahabu

Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe
Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe

Oh, oh, oh, nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe
Nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe

Nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe
Nishike mkono nisizame
Mawimbi ni mengi, niokoe

Hakuna maoni: