Andiko la Msingi: Zaburi 16:8 “Nimemweka
Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.”
Utangulizi:
Zaburi hii ni
zaburi iliyotungwa na kuimbwa na Daudi, Ni zaburi ya kimasihi hasa kutokana na unabii
unaomuhusu Yesu Kristo moja kwa moja, hata hivyo kupitia zaburi hii bado kuna
mambo ya muhimu ya kujifunza kutokana na maisha ya Daudi, na uwezo wake
aliokuwa nao katika kumtegemea Mungu na faida zake, Daudi anatufunulia siri
mojawapo kubwa ya ushindi na mafanikio yake katika kudumisha uhusiano na Mungu,
katika mstari huu wa nane kuna maswala ya msingi matatu ya kujifunza kama
ifuatavyo:-
·
Kumuweka Bwana mbele Daima
·
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu
·
Sitaondoshwa!
Kumuweka Mungu mbele Daima.
Moja ya siri
kubwa ya ushindi katika maisha ya Daudi ilikuwa ni pamoja na kumuweka Mungu
mbele, Katika biblia ya kiingereza neno kumuweka Mungu mbele linasomeka hivi “I have set
the Lord always before me” Neno “SET” la kiingereza linalotumika hapo liko sawa na neno la kiebrabia
“SAWA” kwa msingi huo tafasiri
rahisi ya mstari wa aya hiyo katika kiingereza inaweza kusemeka hivi “I have equally set”
ambalo katika Kiswahili tunaweza kutumia neno Nimekwenda sambamba na Mungu, au
nimetembea sawasawa na Mungu, au kwenda pamoja na Mungu, au kuendenda kwa jinsi
ya Mungu lugha hii ya kibiblia ndiyo ambayo imetumika katika Mwanzo 5:22,24 “Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia
tatu, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na
sitini na mitano. Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu
alimtwaa” .ikionyesha jinsi “Henoko
akaenda pamoja na Mungu” kwa hiyo duniani kuna aina tatu za mwenendo, kwa
jinsi ya Mungu, kwa jinsi ya kishetani na kwa jinsi ya kibinadamu.
1Wakoritho
3:3 “Kwa maana
hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini, maana ikiwa kwenu kuna husuda, na
fitina Je si watu wa tabia ya mwilini; tena mnaendenda kwa jinsi ya kibinadamu”
Daudi
alidhamiria katika maisha yeke kuenenda kwa jinsi ya Mungu siku zake zote.
Hakutaka kuenenda kwa jinsi nya mwili wala ya kishetani aliamua maisha yake
yote kumuweka Mungu mbele hii ilikuwa siri ya maisha ya ushindi kwa Daudi siku
zote za maisha yake.
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu.
Mkono wa kuume
yaani mkono wa kulia kama unavyojulikana sana kwa lugha ya Kiswahili ni kuwekwa
mahali pa Heshima kubwa sana, ni sawa na kutawala pamoja, au kukaa katika meza
ya kifalme, kuamua pamoja naye, kula pamoja naye kushauriana na kufanya maamuzi
ya pamoja, hivyo mtu alipomuweka mtu mkono wake wa kuume maana yake kumuweka
mahali pa heshima kubwa unaweza kuona mfano:-
2Samuel 9:1-9,
“1. Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika
nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? 2. Palikuwa na
mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa
Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako
ndiye. 3. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli,
nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana
hata sasa, aliye na kilema cha mguu. 4. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba
akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli,
katika Lo-debari. 5. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba
ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. 6. Basi Mefiboshethi, mwana wa
Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu.
Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! 7. Daudi
akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya
Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako;
nawe utakula chakula mezani pangu daima. 8. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa
wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? 9. Ndipo mfalme akamwita Siba,
mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake
nimempa mwana wa bwana wako. 10. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na
watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula
ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu
sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini.
11. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumwa wako, nitatenda hayo yote kama
bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kwa habari za Mefiboshethi, mfalme
alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. 12. Huyo
Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote
waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumwa wa Mefiboshethi. 13. Basi Mefiboshethi
akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula sikuzote mezani pa mfalme; naye
alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.
Watu wa nyakati
za agano jipya walifahamu vizuri umuhimu wa swala hili, swala la kumuweka mtu
mkono wa kuume lilimaanisha kumuheshimu mtu huyo kwa kiwango kikubwa na cha
hali ya juu, katika serikali kumuweka mtu mkono wa kuume ni sawa na kumfanya
kuwa makamu wa rais, wana wa Zebedayo
kupitia mama yao waliwahi kumuomba Yesu wapewe nafasi hii lilikuwa ni ombi la
ajabu sana ambalo gharama yake ilikuwa ni kupitia mateso na aibu ileile
aliyoipitia Yesu Kristo Biblia inasema hivi:-
Mathayo 20:20-23 “Ndipo mama
yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba
neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili
waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme
wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe
nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywea
kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto,
sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.”
Aidha kumuweka mtu mkono wa kuume maana yake ni kumfanya kuwa msaada
wako, na ngao yako au mlinzi wako au mtetezi wako, mtu anayeketi mkono wako wa
kuume ni msaada mkubwa ni mwenzako ni
wakaribu ni mwanachama mwenzako COMRADE
Daudi kutokana
na kumtegemea kwake Mungu na kutembea naye alikuwa na uhakika kuwa Mungu yuko
mkono wake wa kuume ndiye anayemshauri, ndiye anayemlinda na ndiye
anayemtegemea na kwa sababu hiyo alikuwa na uhakika kuwa hatoondoshwa!
Sitaondoshwa!
Kutokuondoshwa
kunakotajwa mahali hapo, maana yake ni kuwa salama, kutokusumbuliwa na maadui,
kutokuogopa, kutokutikiswa, kulindwa dhidi ya maadui, kuokuingia matatani,
kutokuwamo taabuni Zaburi 10:6 “Asema moyoni
mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.”,
kudumu milele Zaburi 15:5 “Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa
amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.”,
kutokutetemeshwa Zaburi 46:5 “Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia
asubuhi na mapema.”, Hutotikisika
Kwa ufupi Daudi
anatufundisha
1.
Kumuweka Mungu mbele siku zote
za maisha yetu
2.
Kumfanya kuwa ngao yetu
3.
Kumfanya kuwa kinga yetu
4.
Kumfanya kuwa tegemeo letu
5.
Kumfanya kuwa mwangalizi wetu
6.
Kumueshimu na kutembea naye
7.
Kumtii yeye na kutafuta kwanza
ufalme wa Mungu na haki yake na mengine tutazidishiwa
Na tukiyafanya
hayo
1.
Tutakuwa na furaha
2.
Hatutatikisika milele
3.
Mungu atakuwa tegemeo letu na
ngao yetu, na mshauri wetu, na tutayafanya mapenzi yake
Taifa lolote,
chama chochote, mtu yeyote na taasisi yoyote kama tumedhamiria kumuweka Mungu
mbele katika maisha yetu mafanikio ni lazima, furaha ya Bwana ndio nguvu zetu,
amani ya Mungu ndio nguvu yetu kubwa sana, kama ukimuweka Mungu mbele, katika
mitihani, katika maisha ya kila siku, katika kazi zetu, katika ndoa zetu, katika
dua zetu na ibada na maombi yetu kila kitu mfanye Mungu kuwa mkono wako wa
kuume na utakuwa msindi na zaidi ya kushinda.
Rev. Innocent Kamote
“Mkuu wa Wajenzi mwenye hekima”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni