Jumanne, 11 Aprili 2023

Baba Mikononi mwako Naiweka Roho yangu!


Luka 23:44-46 “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.”

Utangulizi:

Tunaendelea kujifunza kuhusu maneno ya Yesu aliyoyasema pale msalabani, ambayo yana maana pana sana kama utapata nafasi ya kujifundisha moja baada ya jingine, Leo nataka kuzungumzia kuhusu maneno ya mwisho miongoni mwa maneno saba aliyoyazungumza Yesu pale msalabani ambalo ni BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU!, Maneno haya ni sehemu ya maombi aliyokuwa akiyaomba Bwana Yesu Pale msalabani kwa kutumia Zaburi, yeye alipaza sauti kubwa sana na kuyasema maneno haya na kisha akakata roho, watu wengi sana huyaogopa maneno haya wakidhani ya kuwa ukiyasema basi utakuwa unajitakia kifo, au unaweza ukayasema inapofika saa yako ya mwisho, lakini maneno haya yana maana tofauti kabisa na namna ambavyo wengi wetu tumefikiri kwa siku nyingi, hata hivyo kabla ya kuyafanyia uchambuzi na upembuzi yakinifu ni vema kwanza tukajikumbusha tena maneno mengine katika maneno yote saba aliyoyasema Bwana Yesu Pale msalabani, maneno hayo ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Baba mikononi mwako naiweka roho yangu

Kama tulivyoona ya kwamba maneno haya BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU Yalizungumzwa na Bwana Yesu kama maneno ya mwisho pale msalabani na kisha Yesu akakata roho na matukio mengi ya kushangaza yakajitokeza wakati mwana wa Mungu akikata roho, Maandiko haya ya msingi yanatuambia hivi tuone tena:-

 Luka 23:46 “Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu

kimsingi maneno haya yana asili ya Lugha ya kiibrania na yanatoka moja kwa moja katika Zaburi ya 31:5 thelathini na moja, mstari wa tano, Na hivyo kimsingi Mwandishi au waandishi wa agano jipya waliruka maneno muhimu kutoka katika zaburi hii ambayo yana maana pana sana nay a muhimu  linapokuja swala la kufufuka kwa Yesu na sikukuu ya Pasaka, labda waandishi walikuwa na dhana kama yetu ya kufikiri kuwa Yesu alikuwa amevuta pumzi yake ya mwisho ya uhai na kuamua kufa kwa kukabidhi roho yake kwa baba yake, basi. Lakini maneno haya yanasomeka namna hii katika Zaburi yenyewe ya asili ambayo Yesu alikuwa akiinukuu kama maombi pale msalabani  ona -

Zaburi ya 31:5 “Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.”

Aidha ili ieleweke vema pia zaburi hii katika kiingereza inasiomeka namna hii hasa kwa tafasiri ya Biblia ya kiingereza ya ESV yaani “English Standard Version” yanasomeka hivi Psalm 31:5 “Into your hand I commit my spirit; you have redeemed me, O LORD, Faithful God”, Kwa msingi huo pale msalabani Yesu alikuwa anasali kwa kunukuu Zaburi ya 31:5 akiwa katika hali ya mateso makali mno wakati akiwa katika hali yake ya mwilini duniani akiteseka maneno aliyoyasema Yesu kwa tafasiri ya ESV yalitakiwa kusomeka hivi MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU,UMENIKOMBOA EE BWANA, MUNGU MWAMINIFU, Kwa hiyo utakubaliana nami kuwa kuna maneno ya msingi yalirukwa au yalipoteza maana wakati wa kufanya tafasiri katika lugha mbalimbali, nataka sasa nikuchukue taratibu ili iweze kujua kwa uwazi maneno haya na maana yake namna yalivyo na nguvu kuliko tunavyoweza kufikiri utanielewa tu, kwanza tuangalia neno NAIWEKA kwa undani kisha tuunganishe na maneno yaliyorukwa katika Luka 23:46 na kuyaona kwa uhalisia wake katika Zaburi 31:5

Usemi huo unakubaliana wazi kabisa na Lugha za kiibrania na kiyunani ambapo neno NAIWEKA ROHO YANGU kwa kiingereza “I COMMIT” katika lugha ya Kiibrania linatumika neno “AFKID” na kiyunani neno “DIAPRATO”, Neno la kiibrania AFKID kwa kiingereza linasomeka kama “I DEPOSIT” ambalo Kiswahili chake ni kuweka amana au kuacha kitu cha thamani kubwa mfano fedha kwa mtu au taasisi unayoiamini kwa kusudi la kuja kuchukua kitu hicho baadaye, mfano ni kama vile tunavyoweka fedha zetu bank na kisha tunakuwa na haki au uhakika wa kuzichukua wakati wowote unaona!, na neno la kiyunani “DIAPRATO” kwa kiingereza “ENTRUST” ambalo maana yake kukabidhi jukumu Fulani muhimu kwa mtu unayemuamini kuwa atalifanya, atalinda na kukuwakuilisha salama, Hatakuangusha. Kama Neema ya Mungu itakuwa imefunuliwa kwako sasa utakuwa umefahamu kuwa  Yesu aliposema BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU, kama alinukuu Zaburi 31:5 Basi Yesu alikuwa akisema maneno haya “BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA AMANA ROHO YANGU, UMENIKOMBOA EE BWANA, MUNGU MWAMINIFU.

Hii maana yake ni nini maana yake Yesu alipaza Sauti yake kwa imani pasipo shaka akatamka kwa uhakika kuwa anaiweka Roho yake amana kwa Mungu mwaminifu na ambaye anaweza kumrejeshea na sio anaweza kukaa nayo jumla jumla, Yesu aliamini katika uweza wa baba yake ya kuwa anauweza wa kuirejesha Roho yake tena na sio hivyo tu yeye mwenyewe anauwezo wa kuichukua atakapokua anaitaka kama wewe unavyoweza kuchukua fedha zako kutoka katika bank wakati unapotaka, Hii maana yeke ni kuwa Yesu kristo aliutoa uhai wake yeye mwenyewe  na hakuna mtu anayeweza kumuondolea uhai, lakini licha ya kuutoa mwenyewe yeye pia anauwezo wa kuutwaa tena uhai wake au roho yake, Aidha tunajifunza kuwa maneno yale yalikuwa na maana ya kuiweka roho yake kwa muda tu, na kisha ataichukua tena, kwa hiyo kukata roho kwa Yesu kulikuwa ni kwa muda na kuwa angafufuka tena !

Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”

Kwa msingi huo Yesu alimaanisha kuwa hakuna anayeweza kuuondoa uhai wake hapa inajumuisha kila kitu mbinguni na duniani hakuna anayeweza kuiondoa uhai wake, kifo cha Msalabani ilikuwa ni hiyari yake mwenyewe kwaajili ya kuwakomboa wanadamu na ndio maana anapendwa na baba  kwa sababu hakuna aliyemshurutisha, Yesu anayo mamlaka ya kuyatoa maisha yake na anayo mamlaka ya kuyachukua tena, hivyo ni kwa hiyari yake mwenyewe kwa kawaida yeye humuheshimu baba yake, na hafanyi neno Bila kuagizwa na baba hasa alipokuwa Duniani neno linasema:-

Yohana 5;19  Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.”

Yesu anazungumza hii katika hali ya ubinadamu wake hali ya kumtegemea baba yake akiwa duniani, hali ya kujinyenyekeza, lakini neno lake baba mikononi mwako naiweka roho yangu linatufungulia akili kujua uweza na mamlaka kubwa aliyonayo Yesu Kristo, lakini linatuthibitishia kuwa alikuwa na uhakika wa kufufuka!

Yesu hakufa kama afavyo mchuuzi, ulikuwa ni mpango wake kamili wa kumuokoa mwanadamu, mpango ambao baba wa mbinguni alifurahishwa nao, kwa mamlaka hii, tunaweza kukabidhi chochote kwake, na anauwezo wa kuturejeshea, kama kuna vitu tulipokonywa au kuumizwa au kuibiwa au kudhulumiwa vyovyote iwavyo tunaye Yesu mwenye uwezo wa kuturejeshea maradufu yeye anauwezo wa kufisha na kuuhisha, anajeruhi na anaponya, nani yeye mwenye uwezo wa kuokoa hivyo kama kuna kitu kimepotea katika maisha yetu iwe amani, furaha na kadhalika Huyu Yesu anauwezo mkubwa ana mamlaka kubwa yeye ni Mungu na anajitambulisha kuwa hakuuawa isipokuwa ilikuwa kwa hiyari yake ni sadaka aliyojitoa yeye anauwezo wa kuutoa uhai wake na kuuchukua tena na anaweza kufanya hivyo na lolote kwa yeyote akimtumainia yeye, Maandiko yanasema!  

Kumbukumbu 32:39 “Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,”

Hakuna jambo la Msingi kama kukabidhi maisha yetu, mali zetu, ndoa zetu, kazi zetu, watoto wetu, waume zetu, wake zetu, mashamba yetu, magari yetu, afya zetu, na lolote lila katika mikono salama ya baba wa mbinguni ambaye tunajua anaweza kulinda kile tunachiomkabidhi, hakikisha kuwa katika maisha yako unamkabidhi Mungu mwaminifu maisha yako kwa sababu yeye anauwezo wa kutunza, kulinda na kukurejeshea kila kinachopotea ni kwa Mungu pekee ndipo tunapokuwa na uhakika wa kurejezewa kila kilichopotea endapo kweli katika maisha yetu tulimkabidhi yeye, watu wengi wamekabidhi maisha yao na mali zao kwa watu mabaradhuli na wakapoteza Yesu anatukumbusha kuwa ukijikabidhi kwa Mungu mwaminifu hakuna cha kupoteza ! ni muhimu wakati huu wa msimu wa Pasaka kukabidhi maisha yetu kwa Mungu mwaminifu yeye atayarejesha tena yatakapopotea kwa sababu yoyote ile, tukiamini kazi aliyoifanye Yesu Msalabani hakika yeye naye atatufufua siku ya mwisho

Yohana 6:53-54 “Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”

Na Rev Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!



Imekwisha !


Yohana 19:28-30Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.




Utangulizi:

Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa sita wenye Neno IMEKWISHA  ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Maana ya neno IMEKWISHA

Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza linasomeka “IT IS FINISHED  katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki linasomeka kama “TETELESTAI  Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au gari, au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.

Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili IMEKWISHA liko katika wakati uliopita kwa namna linavyoonekana hapa  lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai 2:14-15 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.

Umuhimu wa neno IMEKWISHA.

Yesu alipolia kwa sauti kuu IMEKWISHA alimaanisha katika wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-

1.       Alikamilisha kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.

2.       Alikamilisha kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

3.       Alikamilisha kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka 1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,

4.       Alikamilisha unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara, alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53

Kwa msingi huo hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote, Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni, tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha, Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na kukumbuka kuwa imekwisha

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Naona Kiu - Nina kiu!

 

Yohana 19:28-30 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, NAONA KIU. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.”


Utangulizi

Hivi karibuni Wakristo wote duniani tunaingia katika moja ya Majuma muhimu sana katika kukumbuka mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye aliteseka na kufa kwaajili yatu pale msalabani, Katika wakati huu moja ya maswala ya msingi ambayo huwa tunayakumbuka kwa Pamoja ni pamoja na maneno ya Yesu Kristo pale Msalabani wakati alipokuwa anateseka, kwa ujumla katika injili zote nne unapokusanya maneno yote aliyoyatamka Yesu kabla kidogo ya kukata roho ni Pamoja na maneno haya saba ya mwisho ambayo wakristo huyachukulia kwa uzito mkubwa, Moja ya maneno ambayo tutayatafakari kwa pamoja leo ni pamoja na neno Naona kiu, au Nina kiu,ambalo ni neno la tano katika manenio hayo muhimu, Pamoja na neno hili, lakini maneno yote saba aliyozungumza Kristo ni Pamoja na :-

1.       Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

2.       Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

3.       Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

4.       Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

5.       Naona kiu au Nina kiu Yohana 19:28

6.       Imekwisha Yohana 19:30

7.       Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Tutajifunza somo hili Naona kiu au Nina kiu kwa kuzingatia maswala mawili ya msingi yafuatayo:-

·         Maana ya neno KIU

·         Naona kiu

Maana ya neno Kiu.

Neno kiu kwa kiingereza THIRST ni hali ya  kuhisi au kutaka kunywa kitu Fulani na hasa maji, ni Hali yenye msukumo wenye nguvu wa kutaka kutimiza kitu au jambo Fulani, hali hii wakati mwingine kama ni katika mwili wa mwanadamu inatokana na umuhimu wa mwili kuhitaji maji, kutokana na umuhimu wake na pia kutokana na joto au ukavu Fulani unaojitokeza katika mwili, Neno hilo Kiu katika biblia ya kiyunani linasomeka kama “DIPSAO” kimatamshi  “DIP – SAH – O” Ambalo maana yake kiu halisi au kiu ya jambo Fulani  (to thirst for LITERALLY or FIGURATIVELY) Kwa hiyo Yesu alipozungumza kuhusu kiu kimsingi inaweza kuwa ilikuwa kiu halisi ya kutaka kunywa maji au kiu ya kutaka kuyatimiza mapenzi ya Mungu, nani wazi kuwa kiu aliyokuwa nayo Yesu haikuweza kutimizwa na dunia kwani badala ya kumpa maji wao walimpa divai, na sifongo jambo lililopeleka Yesu kutokunywa, kwa kuwa hiyo haikuwa kiu yake sahihi, Leo tunapotafakari kiu aliyokuwa nayo Yesu Msalabani ni Muhimu kula mmoja wetu kujihoji ana kiu  ya namna gani na je kiu yake inaweza kutimizwa na dunia au inaweza kutimizwa na Mungu? Kiu ya Yesu ilitimizwa na Mungu na haikuweza kutimizwa na wanadamu! Marko 15:23 “Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.” Kile alichokitamani Kristo katika shauku na kiu yake hakikuwa kile ambacho dunia imempa, Mungu atupe neema ya kuweza kutimiza kiu sahihi tuwapo ulimwenguni katika jina la Yesu!

Naona kiu!

Yohana 19:28 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.”   

Moja ya namna ya kuadhimisha Pasaka ni pamoja na kukumbuka Mateso na siku ya mateso ya Bwana wetu Yesu ambayo yametuletea ukombozi, katika siku ile ya mateso Kristo alizungumza maneno Saba muhimu sana katika maisha ya kila Mwanadamu, Katika maneno hayo saba Neno Noana kiu ndio neno la Msingi sana na kiini kikubwa sana cha Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na katika uhitaji wa Mwanadamu wakati tunapopitia mateso kutoka kwa wanadamu wenzetu huku tukiwa na lengo la kudumisha uhusiano wetu na Mungu!, Hapo ndipo Kiu ya kila jambo tulilonalo inapokutana na shida na changamoto mbalimbali,  maneno yote sana yana umuhimu wake na kila moja lina ujumbe wake ingawa leo tutalipa uzito neno la Tano NAONA KIU ;-  bila kupuuzia jumbe katika maneno mengine:-

1.       NENO LA MSAMAHA – Tunapopitia katika wakati Mgumu hasa unaosababishwa na wanadamu wenzetu hatuna budi kufahamu kuwa wakati huo wao wanaona kuwa wako sahihi katika lile wanalokufanyia nan i wewe ndio unaonekana kuwa mkosaji, wakati hio wao huwa dhaifu sana na wewe unayepelekwa matesoni ndio unapaswa kuonyesha ukomavu hivyo kwaajili ya mafanikio Yako samahe – Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo

2.       NENO LA UHAKIKA – Wakati tunapopitia mateso tunapaswa kukumbua ya kuwa wako watu wanaoona umuhimu wetu, na bado wanatutegemea wana wanapaswa kuhakikishiwa kuwa wanakuwa na wakati mzuri hata pamoja na kuteseka kwetu au kuteseka pamoja nao, wahakikishie ya kuwa Mateso ni njia ya kutupeleka katika hali iliyo bora zaidi – Leo hii utakuwa pamoja nani peponi

3.       NENO LA HESHIMA – Wako wale wanaodhalilika unapodhalilika, wako wanaoteseka unapoteseka wako wanaokutegemea ni muhimu kwetu kufahamu kuwa Yesu alikuwa anategemewaa na Ndugu zake na wazazi wake, wakati akiwa katika mateso alitaka kuhakikisha kuwa wazazi wake wanakuwa salama na hivyo alikabidhi Majukumu ya usimamizi wa familia kwa mwanafunzi aliyeaminika kuwa anaweza kumsaidia – Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako

4.       HALI YA UPWEKE – Kila mwanadamu anahitaji kuwa na watu wa kumtia moyo, upweke ni moja ya changamoto kubwa sana kwa mwanadamu hasa anapokuwa mtu mzima lakini zaidi sana tunapopitia katika mateso, wanadamu kwa kawaida hudhani ya kuwa Mungu amemuacha  hsusani anapopita katika magumu au anapokuwa amelemewa na dhambi, - Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha

5.       NAONA KIU – kiu inawakilisha kiini kikuu cha mateso, kila mwanadamu anateseka kwa sababu ya kiu, kila mwanadamu ana kiu anayotaka kuiona inatimizwa katika maisha yake, Kwa bahati mbaya wakati mwingine kiu zetu huharibiwa na watu wenye nia mbaya ambao wanataka kuona kiu yetu ikitimizwa kwa mlango mwingine, Yesu Kristo katikati ya mateso na katika kilelel cha mateso alijisikia kiu bila shaka ilikuwa ni kiu nzuri kiu ya maji safi lakini tunaambiwa watesi walimpa siki badala ya maji, jambo lililopelekea yeye kukataa kunywa Mathayo 27:33-34 “Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa.” Dunia haita kubali utimize kiu yako, na wakati mwingine utapewa  kitu mbadala kinyume na kiu yako, na kama kiu yako imetoka katika kwa Mungu ni dhahiri kuwa dunia haitakubali uitimize kiu hiyo na badala yake watataka unywe kitu kingine Kiu ya Kristo ilikuwa ni kuwakomboa wanadamu na kuona kuwa watu wote wanaishi kwa amani huku yeye akiwa ni mfalme wa amani, lakini badala yake Dunia ilimfanyia mambo mengine, katika wakati huu tulio nao ni lazima tuwe wakali ili kwamba kiu yetu sisitimizwe kwa njia nyingine, Mapenzi ya Mungu yasikataliwe, Baraka za Mungu zisigeuzwe kuwa laana,

-          Wengi walikuwa na kiu ya kuolewa na kuoa ili wawe na amani katika ndoa zao lakini dunia imewapa machungu badala ya amani

-          Mungu alikusudia tuishi kwa furaha na amani lakini leo hii dunia imewapa vilio na mateso kiu yao ya kuwa na furaha duniani imeharibiwa badala ya maji wamepewa sifongo

-          Wengi wamelima na kupanda wakitarajia mvua itanyesha wapate mazao, lakini dunia imewanyima mvua na imawapa ukame na hali ya uchumi imakuwa sio

-          Mungu alikusudia dunia iwe kama paradiso ka ma watu wangeitunza lakini watu wameharibu mazingira  na hatimaye leo dunia inashuhudia mabadiliko mabaya ya hali ya hewa na ukiharibika kwa anga linalozuia miali mikali ya jua kutufikia moja kwa moja Ozone layer, kuongezeka kwa hewa ya ukaa na hali joto ma mabadiliko makubwa

-          Dunia ilitarajiwa iwe ni sehemu ya ustaarabu, uadilifu na yenye kutunza utamaduni lakini leo tunashuhudia uharibifu mkubwa wa ustaarabu na mmomonyoko mkubwa wa uadilifu, kuharibika kwa tamaduni zenye manufaa na badala yake dunia leo inataka kuwe na ndoa za jinsi moja na kuzalishwa kw agenda ya tatu isiyo ya kiume wala ya kike, Haya pamoja na mambo mengine ni uharibifu wa kiu ya Yesu Kristo unaofanywa na wanadamu

-          Mungu alikuwa na kiu ya kuona haki ikitendeka na dunia ikifanikiwa kila mahali, maana haki huinua taifa lakini dhambi ni aibu ya taifa zima, leo hii wote tunashuhudia haki ikipindishwa kwa rushwa na upendeleo na hukumu zikipotoshwa huo nao ni uharibifu wa kiu ya Mungu

-          Wewe una kiu gani na dunia imekupa maji ya namna gani? Hatuna bhudi kujiweka katika neema ya Mungu na kumuomba Mungu atufanikishe ili kiu yetu na kiu yake isiharibiwe katika maisha yetu tuwapo duniani

6.       KILIO CHA USHINDI – Imekwisha, Yesu alitimiza majukumu yake yote duniani kwa ushindi mkubwa TETELESTAI  Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, kila mmoja wetu analo jukumu la kutimiza awapo duniani

7.       KILIO CHA UTII – baba mikononi mwako naiweka roho yangu, Yesu alitii mambo yote ambayo Mungu alikuwa amemuagiza ayatende, usikubali kuondoka duniani bila kutimiza ndoto ambazo Mungu amekukabdihi uzitimilize

Hitimisho!

Kwa hiyo unapoangalia maneno haya saba ya Bwana wetu Yesu Krist utagundua kuwa yote yana umuhimu mkubwa sana lakini neno la tano lina umuhimu mkubwa sana katika swala zima la matarajio ya mwanadamu na kile ambacho dunia inatupa kwa msingi huo basi usalama wetu na kutimia kwa kiu yetu vinaweza kupatikana kwa Mungu mwenyewe

-          Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa” Kama kiu yetu itakuwa ni ya haki na bila shaka hii ni kiu yenye kutaka kuyatimiza mapenzi ya Mungu basi kiu hiyo itatimizwa

-          Yohana 7: 37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.”  Yesu anatoa mwaliko wa kila mtu mwenye kiu aje kwake anywe unaona ni dhahiri kama kiu aliyoisema Yesu ingekuwa kiu HALISI literal Maandiko yasingeweza kuzungumza katika hali kama hii haba ni uhitaji wote wa kimwili na Kiroho Dunia haiwezi kututimizia kiu halisi tuliyo nayo Lakini Yesu anaweza na ametyuahidi kuwa atatimiza hivyo kiu yetu atatupa maji halisi tunywe

Ni maombi yangu kwako katikka pasaka hii kuwa Mungu akutane na kiu yako hamu yako na shauku yako inaweza kutimizwa na Yesu aliyegharimika kufa kwaajili yako pale Msalabani

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!


Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

 

Mathayo 27:46 - 49. “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.”


Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani mojawapo ya maneno Muhimu katika maneno yaliyosemwa na Yesu Kristo wakati wa Mateso yake pale msalabani MUNGU WANGU MUNGU WANGU MBONA UMENIACHA, tunataka kujifunza maana ya maneno haya kwa kina na kuangalia uhalisia wa ubinadamu hususani wakati wanadamu wanapopitia mateso, Pamoja na menono haya muhimu, tutakayoangalia leo maneno mengine kwa mfululizo katika maneno saba aliyozungumza Kristo pale msalabani kwa mujibu wa injili zote nne ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Maana ya Maneno Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?

Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Ni muhimu kufahamu kuwa Mwandishi wa kitabu cha Mathayo anajaribu tu kufupisha kile ambacho Yesu Kristo alikisema na pia anajaribu kutafasiri lugha kiaramu ambayo Yesu aliitumia wakati anazungumza maneno hayo. Maneno hayo Eloi, Eloi, Lamasabakthan, katika lugha ya asili yanasomeka kama Eli, Eli, Lama Sabachthan ni sehemu ya maneno kamili ambayo Yesu aliyazungumza ka lugha ya kiaramu, maneno hayo yanatafasirika hivi Eli, (Adonai) Eli (Adonai) Lama (Why?) kwanini ?, mbona? Sabachthani (You have left, Abandoned) me) Umeniacha.  Kimsingi ni kuwa katika kini cha mateso yake Yesu Kristo alikuwa anatimiza na kumuomba Mungu sawa na Zaburi ya 22:1-22 ambapo katika Zaburi hii Daudi ambaye alipendwa sana na Mungu alikuwa akimuomba Mungu kutokana na Mapito aliyokuwa akiyapitia ambayo kimsingi pia yalikuwa ni mapito ya kinabii yaliyohusiana na Yesu Kristo Mwenyewe Mwana wa Daudi, Kumbuka kuwa Yesu alikuja kutimiza maandiko ambayo torati na manabii na maandiko yote yaliweka bayana kuwa Masihi hana budi kuteseka 

Luka 23:13- 27 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.”

Unaona kimsingi Yesu alikuwa ameandikiwa kila atakalokuja kulitenda na kulinena katika Torati, Manabii na Zaburi au maandiko hivyo Neno Mungu wangu Mungu wangu ilikuwa ni nukuu ya Zaburi ya 22 ambayo ina mukhtasari wa Mateso ya Bwana Yesu yaliyotabiriwa na Daudi katika zaburi hiyo hebu tuyaangalie tuweze kuona 

Zaburi 22:1-20 “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.  Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma. Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.”

Kimsingi maombi ya Daudi na Maombi ya Yesu Kristo yanafanana na hatujawahi kuona wakati wowote Mungu akimuacha Daudi au akimuacha Yesu Kristo lakini kwanini walilia maneno hayo na kuomba dua hizo wakati wa mateso yao ilihali wote tunajua kuwa maandiko yanamsifia Daudi kama mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu ona

Matendo 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.”

Aidha katika namna kama hiyo Mungu katika neno lake vilevile anajivunia Kristo Yesu mwanae kama mtu aliyeupendeza moyo wake ona

Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

Inawezekanaje Mungu kuwaacha awapendao? Mungu anatujali sana katika kiwango ambacho hata mama anaweza kumsahau mtoto wake lakini sio Mungu wetu ona

Isaya 49:15-16 15. “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima. Kimsingi kila mwanadamu anapokuwa na mafanikio watu”               

Mungu wetu anatujali mmno lakini katika hali ya kawaida kila mwanadmu anapopitia mateso na changamoto za aina mbalimbali kwa kawaida wanadamu wana tabia ya kuwa mbali nawe wanatabia ya kukuacha ubaki peke yako na wakati huu Mungu hukaa kimya ili mateso yale yaweze kuleta somo linalokusudiwa kwako hivuo kibinadamu zinakuweko fikra ya kuwa huenda Mungu amekuacha, Ayubu alipokuwa na mafanikio makubwa sana tunaambiwa watu wengi sana walimwendea na nyumba yake ilijaa watu wa kila aina maandiko yanasema na watu wa nyumbani wengi sana ona

Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”

Tunaambiwa kuwa wakati wa mateso yake Ayubu watu wote waliokuwa nyumbani mwake walimkimbia mpaka pale Ayubu alipobarikiwa tena ndio tunaelezwa kuwa watu wote wakamwendea ona

Ayubu 42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”

Ni swala la kawaida kwamba wakati wa mateso watu wanakukimbia na mara kadhaa inadhaniwa kuwa Mungu amekuacha nani kilio cha kawaida Pale mtu anapopita katika magumu kufikiri mkuwa ni Mungu ndiye aliyemtendea hayo, Ndio maana Daudi alilia katika Zaburi ya 22 japo ilikuwa pia ni unabii kw Mwanaye Yesu Masihi ambaye naye alilia akijua ya kuwa anaitimiza Zaburi ya 22 yote alitioandikiwa humo yalitokea siku ya mateso yake maneno mabaya , kugawanywa kwa nguo zake kwa kuzipigia kura, kugomelewa mikono yake na miguu yake msalabani, kudharauliwa na kuwekwa katika mikono ya watu wabaya wapate kumdhihaki, na kumdhalilisha, Kifo cha Msalabani hakikuwa kifo cha kawaida kilikuwa ni kifo cha maumivu ya kila aina kisaikolojia na nafsi na mwili Yesu ni kama alikuwa amabaki pake yake msalabani, saa ya kujaribiwa huwa ni kama tunabaki peke yetu, kundi kubwa la watu waliofaidika na huduma yake hakuna hata mmoja aliyeweza kusogea na kufanya utetezi wakati Masihi alipokuwa anateseka Msalabani na ndio maana akaisema zaburi ya 22 ambayo hutambulika zaidi kwa Mstari wake wa kwanza Mungu wangu Mungu wangu mbiona umeniacha!

Msalabani Yesu hakuwa ametundikwa kwa sababu nya dhambi yake ilikuwa ni kwaajili ya dhambi zetu mimi na wewe, nani mimi na wewe ndio ambao tulipaswa kuyabeba maumivu yale, lakini Mwokozi alibeba kwa niaba yetu na kilio kilikuwa kwa ajili yetu na ubinadamu wetu, alilia kuonyesha kuwa wanadamu wakati wote tunahitaji msaada wa Mungu na kuwa peke yetu hatuwezi, adui yetu yu aweza kufanya jambo lolote la kutuumiza sana kama tutabaki bila msaada wa Mungu, Mtu mmoja aliimba wimbo unasema nafikiria ukiniacha roho yangu itakuwaje Bwana ? itakuwa ni mawindo ya adui kwa wepesi sana… wakati wote tunapokuwa na maisha yetu bila ya Mungu tunajiweka katima hatari ya kushambuliwa na kuumizwa na ibilisi, magonjwa matesi na dhiki za dunia hii, lakini ashukuriwe Mungu kuwa pale msalabani Yesu Kristo alikuwa anateseka kwaajili yatu na kwaajili ya ukombozi wetu ili kuukaribisha uwepo wa Mungu katika maisha yetu

Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Mama tazama mwanao


Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”


Utangulizi

Moja ya maneno saba aliyoasema Bwana Yesu pale msalabani ni Pamoja na Maneno haya Mama tazama mwanao, neno hili ni moja ya neno Muhimu sana linalotukumbusha wajibu wetu Muhimu sana wa kuhakikisha kuwa wazazi wetu na jamii yetu na familia zetu zinajengewe uhakika wa maisha ya baadaye hata pale wakati sisi tunapokuwa hatupo, leo tutachukua muda kujifunza kwa undani kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na maana ya maneno haya, hata hivyo ni muhimu kama ilivyo kwa masomo yote ya mfululizo wa maneno saba ya Kristo pale Msalabani kujikumbusha maneno yote sana kwa mfululizo wake kisha tutaendelea na uchambuzi wa neno husika leo, Maneno yote sana ya Msalabani ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Tutajifunza somo hili, Mama tazama mwanao kwa kuzingatia maeneo makuu matatu yafuatayo:-

*      Utata kuhusu Ndugu wa Yesu Kristo

*      Kwa nini Mariam mikononi mwa Yohana ?

*      Mama tazama mwanao

Utata kuhusu Ndugu wa Yesu Kristo.

Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”

Kabla ya kuzungumzia umuhimu na maana ya maneno ya Bwana Yesu ya awamu ya tatu Mama tazama mwanao… Ni muhimu kwanza tukaondoa utata wa kitheolojia unaotoka na msimamo wa kanisa katoliki na msimamo wa makanisa ya kipentekoste kuhusu Maana ya mstari huu!

Katika mtazamo wa kikatoliki wao wanajenga hoja ya kuwa mstari huu wa Yesu akiwa msalabani kumwambia Mama tazama mwanao Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama mama yako, Na tangu saa ile Mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake, ni suhahidi wazi kuwa Mariamu hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu, wakatoliki wanajenga hoja kuwa ni jambo la kushangaza kumuona Yesu akimkabidhi mama yake kwa Mtu mwingine mbali na watoto wake mariamu kama mama huyo angelikuwa na watoto wengine kwa hiyo kwao mstari huu ni ushidi ulio wazi kuwa Mariamu hakuwa na watoto wengine tofauti na wapentekoste wanavyodai!

Katika mtazamo wa kipentekoste ni wazi na dhahiri kuwa kulikuwepo sababu maalumu za Yesu kumkabidhi mama yake Kwa mwanafunzi aliyempenda sana ambaye kiushahidi mwanafunzi huyu ni Yohana, ukweli wa kuweko ndugu za Yesu kristo sio ukweli na mtazamo wa kipentekoste bali ni ukweli na mtazamo wa Biblia yenyewe Maandiko yanaionyesha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu zake wa kuzaliwa mara baada ya yeye kuzaliwa nao walikuwa ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda pamoja na dada zake wawili ona :-

Mathayo 13:53-56 “Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?

Biblia imeweka wazi kuwa Yesu Kristo alikuwa na ndugu zake na imetueleza kuwa mwanzoni nduguze walikuwa bado hawajamuamini, na pia mara kwa mara walimtembelea kutaka kumuona hata wakati akiwa anawahudumia watu ona

Mathayo 12:46-47 “Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe.”

Marko 3:31-32 “Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

Luka 8:19-20 “Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.”

Yohana 7:1-10 “Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. Kweeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa haujatimia wakati wangu. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.”

Matendo 1:13-14 “Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”

Wagalatia 1:18-19 “Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.    

Kwa hiyo tunapoyachunguza maandiko unaweza kuona kuwa yanabainisha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu wa kibailojia ndugu wa damu ndugu wa kuzaliwa mara baada yaye ye kuzaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kwa msingi huo ni dhahiri ya kuwa Yesu alikuwa na ndugu,  na ndio maana utaweza kuona kwa asili wanapotajwa wanatajwa wakiwa pamoja na mama yao, wakatio mwingine wakatoliki wamefikiri kuwa ndugu hao wa Yesu ni binamu zake lakini iko wazi kuwa hao hawakuwa binamu zake Neno la asili la kiyunani linalotumika katika maandiko kuelezea maana ya Ndugu ni Adelphos au Delphus ambalo maana yake connective particle au Morphological ties Neno hilo Ndugu limetumika mara 346 katika Biblia likimaanisha Ndugu wa damu au ndugu wa tumbo Moja wakati ndugu wa kiimani limetumika mara 226 kwa msingi huo Yesu alikuwa na ndugu wa damu na wa kuzaliwa baada ya kuzaliwa yeye kwa muujiza nduguze wa karibu walizaliwa Nduhu hao wa Yesu wanatajwa katika maandiko baada ya Yesu kuzaliwa na sio kabla kwa kuwa wangeweza kutajwa wakati Yusufu alipoenda Bethelehemu au walipokimbilia Misri au wakati wa kurudi Nazarethi kwa msingi huo Maandiko yanabainisha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu zake wa damu na wa kuzaliwa mwenye sikio la kusikia na alisikie neno hili.

*      Kwa nini Mariam mikononi mwa Yohana ?

Swali kubwa wanalouliza wengi ni kuwa kama Yesu alikuwa na ndugu zake iweje Yesu amkabidhi Mariama kwa Mwanafunzi wake aliyempenda aitwaye Yohana? Jibu ni rahisi sana Yohana ndiye mwanafunzi pekee aliyekuwa karibu sana na Msalaba pamoja na Mariamu mama yake Yesu wakati wanafunzi wengine walikimbia au walikuwa wakiangalia kwa mbali sana

Mathayo 26:58 “Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.”

Mathayo 27:55-56 “Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.”

Marko 15:40-41 “Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.”

Luka 23:49 “Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.”

Wakati injili zote zikithibitisha kuwa watu wote walikuwa mbali sana na Yesu wakati wa mateso yake habari njema ni kuwa waliokuwako karibu kabisa na msalaba kiasi cha kusikia maneno ya Yesu akizungumza ni Mariamu mama yake Yesu na Yohana mwanafunzi mpendwa wa Yesu Kristo  ona

 Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”

Yesu alipokuwa msalabani aliweza kumuona mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu unaona jukumu la kumuangalia Mariamu mama yake Yesu alipewa Yohana na Jukumu la Mama kumuona Yohana kama mwanae walipewa kwa sababu ndio waliokuwa karibu na Yesu na sio vinginevyo, wakati wa mateso  na majaribu watu muhimu ni wale wanaokuwa karibu na wewe na sio wale wanaokuwa mbali na wewe

*      Mama tazama mwanao

Ukiacha sababu ya Yesu kumuona Yohana na mama yake kuwa karibu kiasi cha kuweza kuzungumza nao na kuwapa majukumu ya kutunzana maneno haya mama tazama mwanao na mwana tazama mama yako, ni fundisho lililowazi kuwa Yesu pamoja na mambi mengine alikuwa anaijali famlia yake, Historia ya kimasimulizi ya kale inaona wazi kuwa huenda Yusufu baba mlezi wa Yesu Kristio na baba mzazi wa ndugu zake Yesu huenda atakuwa alifariki kitambo kidogo kabla ya kusulubiwa kwa Yesu na huenda kuwa ni kwa muda Fulani Yesu alikuwa ndio nguzo ya Familia na ndio maana utaweza kuona ndugu zake na mama yake mara kadhaa walikuwa wakimuendea, Sasa Yesu Yuko Msalabani alimkabidhi mama yake kwa Yohana na kumtaka amuangalie na pia alimkabidhi Mariamu kwa Yohana ili wawe na ushirika naye

Agizo hili linatukumbusha wote majukumu yetu ya kuwaangalia wanafamilia wote na kuhakikisha tunawatunza,  kukabidhiwa kwa Mariamu kwa Yohana ni sawa na kukabidhiwa kwa wanafunzi wote na Yesu angeagiza hivyuo kwa owte kanma wote wangekuwa karibu naye Mungu hana upendeleo, baadaye tunamuona Yesu akiwaoa wanafunzi wake majukumu kadhaa akionyesha kuwa amewaamini, mfano alimwambia Petro Lisha kondoo zangu lakini pia aliwaambia wanafunzi wote waihubiri injili na kuwa anagekuwa pamoja nao zaidi ya yote tunawaona wanafunzi wote baadaye wakiwa na Mariamu mama yake Yesu na nduguze wakiwa na ushirika mmoja wote kwa pamoja, 

Matendo 1:13-14 “Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”

Unaona Katika majira ya Pasaka ni muhimu kila mmoja kukumbuka kuwa karibu na familia na kuangaliana na kutunzana lakini ni wakati wa kujikumbusha umuhimu wa kuwa karibu na wale wanaopitia changamoto za aina mbalimbali, na wakati wote kuhakikisha kuwa tunawakumbuka wazazi wetu na kuwapa msaada wa karibu unaowezekana heshima hii ni ya Muhimu wakati wote tunapokuwa hai.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima