Mathayo 5:43-48 “Mmesikia kwamba imenenwa,
Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni
adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye
mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye
haki na wasio haki.Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani?
Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu,
mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama
hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya
msingi mkuu wa malengo ya Mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo ilikuwa ni
kuwafanya watu wote waliomuamini kuwa wakamilifu, katika tabia na mwenendo, Kwa
bahati mbaya kanisa la Mungu katika nyakati za leo tumeacha kukazia mafundisho
yetu katika uadilifu kama ilivyokuwa kwa Yesu na Mitume na badala yake
kuwaelekeza watu katika maswala mengine!. Pamoja na kuwa agizo la Mungu ni pana
sana lakini ni muhimu vile vile tusiache kabisa kurudi katika msingi na
kuwakumbusha watu kulenga katika kukua kiroho, kimaadili na mwenendo! Hili ndio
kusudi mojawapo kubwa la kuwepo kwa kanisa.
Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa
mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa
wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya
huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia
umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata
kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”
Nadhani unaweza kupata picha
iliyo wazi kusudi la Kristo kulipa kanisa Mitume, manabii, wainjilisti,
wachungaji na walimu ni ili watu wa Mungu wajengwe kwa mafundisho na maelekezo
wakue na kukomaa na hatimaye waweze kuwa na tabia na mwenendo na sifa sawa na
zile alizokuwa nazo Kristo, hakuna gharama kubwa kama hii ya kutokuwa na
wakristo waliokomaa kiroho, wasio na ufahamu wala ujuzi wa neno na wanaoacha
kukua kiroho na kiuelewa na kubaki katika udumavu, uchanga na kutokuwa na tabia
na mwenendo unaofanana na baba yetu wa Mbinguni, tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
Maana ya
neno ukamilifu
Kipimo
cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.
Maana ya neno Ukamilifu.
Unapoyachunguza mafundisho ya
Yesu na Mitume kuhusu ukamilifu utaweza kuona kuwa kuna jambo walilolokuwa
wakililenga zaidi katika mafundisho yao, Kwa kawaida mwanadamu hawezi kuwa
mkamilifu kama Mungu, Mungu anatajwa kuwa mkamilifu na muadilifu na kuwa hakuna
uovu wowote ndani yake ona:-
Kumbukumbu 32:3-5 “Maana nitalitangaza Jina
la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana,
njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye
haki na adili. Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila
yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.”
Mwanadamu alikuwa na ukamilifu wa
uadilifu, haki na kutokuwa na uovu mara alipoumbwa na Mungu katika bustani ya
Edeni na ndio maana alikuwa na uhusiano na Mungu wa karibu kama Baba na Mwana
wake, Hata hivyo baada ya anguko la mwanadamu, Mwanadamu alipungukiwa kila
eneo la maisha yake, alipoteza haki, alipungukiwa
na uadilifu na kupoteza ushirika na Mungu wa moja kwa moja ona:-
Warumi 3:23 -24 “kwa sababu wote wamefanya
dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema
yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”
Mwanadamu aliyemuamini Yesu
Kristo na kazi yake ya ukombozi iliyofanyika pale Msalabani, kama akifunzwa
vyema katika kanisa analokuweko anaweza kuwa mkamilifu katika uadilifu kama
alivyo Mungu, ukamilifu huu ambao umetajwa katika maandiko tunaweza kujifunza
maana zake kama ifuatavyo:-
Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa
wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Neno hilo
Nanyi mtakuwa wakamilifu katika maandiko ya kiyunani yanasomeka kama “TELEIOS” neno hilo linasomeka kama “PERFECT” katika kiingereza, lakini hata
hivyo neno hilo halitoshelezi katika kuelezea ukamilifu unaokusudiwa kwa
kiyunani neno hilo teleios maana
yake ni complete or application of labor
growth, mental and moral character na
katika maana nyingine pia ni full of age, kwa hiyo ukamilifu unaozungumzwa hapo ni
kufikia kwenye uwezo wa kujitambua (Maturity),
kuacha ujinga, kukomaa kimaadili, na kitabia na kimwenendo na maandiko yanaonyesha kuwa jambo hili
linawezekana kabisa kwa kila mkristo aliyeitwa na Mungu kwa kuokolewa
1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii
msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye
aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu
wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Unaweza kuona! kumbe kama mtu
ameokolewa na amekuwa mwanafunzi waYesu na kisha bado akawa anaenenda kama kwanza
yaani kama ilivyokuwa kabla ya kuokolewa anafanya ujinga, HAJAJITAMBUA, kwa
hiyo ni lazima kila mtu aliyeokolewa afunzwe aondoke katika ujinga awe na akili
abadilike katika tabia na mwenendo na kuwa na tabia ya uungu, yaani kuwa kama
Mungu, unaona utakatifu unaozungumzwa hapo katika waraka wa Petro wayunani wanautaja kwa kutumia neno HAGIOS
ambalo pia linazungumzia Morally
Blemeless yaani kufikia ngazi ya
kutokuwa na lawama kimaadili na kujiweka
wakfu kama wafanyavyo makuhani ona
Waebrania 7:6 “Maana ilitupasa sisi tuwe na
kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa
lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu;”
Kwa namna Fulani Mungu anataka
wanafunzi wakristo, wakue wakamilike, wakomae, wakue waondoke katika maswala na
tabia za kitoto na za kijinga, kutokukua kiroho kunatupelekea kuwa na kanisa
yaani watu ambao wameokolewa kwa kumuamini Bwana Yesu lakini wakiwa na tabia
mbaya kama tu watu wa kawaida wasiomjua Mungu, watu ambao Hawajajitambua, Paulo
mtume anawaita wakristo wa namna hii kama wakristo wenye tabia ya mwilini ona
1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu,
mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na
watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo.
Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam,
hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini.
Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini
ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?”
Watu wenye tabia ya mwilini
katika kiingereza wanaitwa “CARNAL”
neno hili la kingereza linalotumika hapo katika kiyunani linatumika neno “SARKIKOS” ambalo maana yake ni tabia
za KINYAMA hii maana yake ni kuwa katika kanisa la
Korintho japo wakristo walikuwa wameokoka na kumuamini Yesu kama Bwana na
Mwokozi, bado kulikuwa na ukosefu mkubwa wa huduma ya mafundisho ya kichungaji
na kitume, kwa msingi huo wakristo wa Korintho japo walibarikiwa sana kuwa na
karama za Rohoni lakini vilevile tunaona kuwa kanisa hili lilikuwa limejaa
tabia za kinyama mfano:-
-
Kulikuwa
na Mafarakano na ushabiki wa wahubiri wa injili - kama tu ilivyo leo 1Wakorintho 3:4-9 “Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni
wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni
wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda,
Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala
atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni
wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake
mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu,
ni jengo la Mungu”
- Kulikuwa na husuda na fitina – sio jambo la kushangaza leo katika jumuiya ya Kikristo kuona watu wakiwa wamejaa fitina majungu na mafarakano, wakristo wakisingiziana mambo makubwa ya uongo bila hata kuchomwa mioyo katika dhamiri zao ona 1Wakorintho 3:3 “kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? ” wakristo katika nyakati za siku hizi wamefikia ujinga wa hata kuchomekeana mambo mabaya, kuuana, kuwekeana sumu au kutumiana watu wasiofaa kitu kufanya mauaji, na kutengeneza keshi na skendo za kuchafuana sio kiu cha ajabu
-
Kulikuwa na zinaa za kupita kawaida - yaani kulikuwa na watu waliozini mpaka na
wake za baba zao, yaani zinaa zisizokuweko hata katika mataifa ona 1Wakorintho 5:1-3 “Yakini
habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata
katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala
hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.
Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi
mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.”
Leo hii watu kuzini na wachungaji, wake za wachungaji, wazee wa kanisa na
watu wenye sifa katika kanisa limekuwa jambo la kawaida watu wanakula stori za
zinaa kama jambo la kawaida tu hofu na hali ya kumcha Mungu imeondoka na neema
ya Mungu imechukuliwa kama njia ya kujihurumia katika kuteda dhambi na
kuzihalalisha, mwenendo wetu haufanani tena na makusudi ya kuwepo kwa kanisa la
kristo duniani
-
Watu
wasiokubali kuachilia – Katika Kanisa la Kristo kule Korintho na kama
ilivyo leo kulikuwaweko watu wasiotaka kupoteza, kila wakati walitaka kuonekana
kuwa ni washindi, katika Kristo tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa
kwaajili yake, watu waliokomaa kiroho sio lazima kila kitu washinde, wakati
mwingine iko haja ya kuachia na kupoteza Korintho watu walipelekana mahakamani ona 1Wakorintho 6:1-8 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki
mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba
watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je!
Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi
si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo
ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika
kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna
hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali
mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa
upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali
kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu? Bali kinyume cha hayo
ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu
zenu.” Je katika siku za leo hujawahi ona watu wakristo
wakidhulumiana je hujawahi ona wakristo wakipelekana mahakamani? Wakisingiziana
wakitakiana mabaya maswala kama haya yanaweza kutokea tu kama watu hawatatafuta
kuwa wakamilifu kama baba wa Mbinguni, niliwahi kumsikia Mkristo mmoja
aliyekuwa anahusika na kuajiri watu mahali Fulani akitamka kuwa nitahakikisha
huyu kijana (mwajiriwa wake) ananyooka na kukimbia na kurudi kijijini, ni
matamshi hatari sana sio ya mwajiri wa kawaida wa dunia hii ni Mkristo
akihakikisha kuwa anaharibu maisha ya mtu mpaka mtu huyo akimbie mjini? Nimewahi kumsikia Mkristo mmoja akipanga
njama ya kuharibu kibali cha mtu na akiwa na nia hata ya kusambaza skendo kwa
kuhakikisha kuwa anamuandika mtu gazetini ili kumuharibia kibali chake wivu
husuda na dhuluma na masingizio leo imekuwa ni tabia ya kawaida ya Wakristo,
nataka nikuhakikishie kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na Kanisa
la watu walioharibika, waliodumaa kiroho na wasiokua kiroho na kimaadili na
wasiojitambua, wanageuka na kuwa wanyama kabisa, Mkristo anadhulumu wenzake na
anaendelea kuabudu bila wasiwasi huku akiwatishia wale aliowadhulumu, Wakristo
ambao wamedumaa kiroho na kutokukomaa na kukua ni tatizo kubwa sana na
linasumbua sana jamii ya Wakristo na makanisa tuliyonayo leo.
-
Kuweko
kwa wakristo wasio na faida – Waebrania 5:11-14 “Ambaye
tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa
mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati
mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya
Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila
mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini
chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa
kupambanua mema na mabaya.” Mwandishi wa kitabu cha waebrania
anasikitishwa na wakristo walio na miaka mingi kanisani lakini wamedumaa
hawakui Kiroho muda mwingi umepita lakini hawawezi kuwa walimu maana yake
hawajakua kufikia hata ngazi ya kuweza kuwafundisha na wengine kwa kuhudumu
katika kufundisha neno la Mungu lakini pia hata wao wenyewe kushindwa kuwa
somo, kuwa kielelezo leo tuna wakristo wana miaka mingi sana katika imani
lakini ni wabovu katika kiwango ambacho huwezi kujifunza kitu kutoka kwake,
huwezi kuona tofauti yake na watu wa duniani
na wakati mwingine hata wale wa duniani huonekana kuwa wana nafuu, changamoto
hii inatokana na kutokujali swala la kuwa wakamilifu katika mwenendo wetu yaani
kuwa na tabia ya Kristo!
-
Kuwepo
kwa karama na miujiza mingi lakini tabia mbaya – Kanisa la korintho
lilikuwa ni kanisa lililokuwa na neema ya kuwa na vipawa vingi na karama nyingi
na watu wengi sana waliokuwa wakinena kwa lugha lilijaliwa vipawa vingi sana
vya rohoni lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi za kimaadili kwa kanisa
hilo, unaona Paulo anawafundisha namna bora ya kutumia karama za rohoni lakini
vilevile akiwafundiaha njia iliyo bora ambayo ni upendo, kama ilivyokuwa kwao
nyakati za leo tuna watu wenye vipawa vingi na Mungu anawatumia sana na watu
wanawafuata lakini wana tabia mbaya hakuna uadilifu kuanzia namna wanavyofanya
huduma bila adabu, lakini wakiwa na tabia zisizovutia na wakristo wajinga waochukuliwa
na mawimbi ya watenda miujiza wakidhani kuwa kila mtenda miujiza ni wa Mungu,
Kipimo cha ukomavu wa mtu kiroho sio miujiza bali ukomavu katika uadilifu na
upendo, Kristo atawakataa wahubiri wote, na watumishi na manabii ambao kweli
kwa jina lake watafanya miujiza na kutoa unabii lakini tabia na mwenendo wao
kwa vipimo vyake hauonekani kuwa wenye kufaa.
Mathayo 7:21-23 “Si
kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali
ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku
ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa
pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri,
Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”
Kipimo halisi
cha kiroho sio mkutenda miujiza bali kuishi maisha ya utakatifu na kuzaa
matunda ya roho, mtu mmoja alisema mnadhani waislamu huenda msikitini kwaajili
ya miujiza? Wao huacha maduka yao na biashara zao na kukimbilia katika nyumba
za ibada kwaajili ya kusali na kuabudu tu, Wakristo wa leo ni kama wasipoona
muujiza kabisa wanadhani kuwa Mungu hayuko mahali hapo Yesu alikisikitishwa na
watu ambao hawawezi kumuamini hivihivi tu mpaka ziweko ishara
Yohana 4:46-48 “Basi
alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na
palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia
ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi
ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.Basi Yesu akamwambia,
Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?”
Wakristo
wasiokomaa na kukua katika uadilifu na mwenendo hukimbizana huku na huko
wakitaka kuona miujiza na ishara hawawezi kumuamini Mungu pasipo miujiza, je
unadhani ukuu wa Muhubiri ni miujiza tu hapana! Hatusomi kokote pale ambapo Yohana
mbatizaji alifanya muujiza wowote lakini Yesu alimsifika kuwa katika uzao wa
mwanamke hakuna aliye mkuu kama Yohana Mbatizaji ona
Luka 7:24-28 “Basi,
wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za
Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?
Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu
wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme.
Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya
nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso
wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale
waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo
katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”
-
Watu
wanaochukuliwa na upepo wa kila aina ya Elimu – Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii;
na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi
la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo
ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana
Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha
utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku,
na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja,
tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua
hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo” Neno la
Mungu limemaliza kila kitu kuna upepo wa kila namna wa Elimu na hila za watu na
ujanja na njia za udanganyifu hizi zipo, kukosekana kwa Elimu sahihi ya neno la
Mungu kumewafanya wakristo wa leo kuchukuliwa na hizi pepo biblia ya NIV
inatumia neno “WAVES” yaani neno la
Mungu linatambua kuweko kwa mawimbi, au
pepo katika maswala ya neno la Mungu na
kazi zake wakati mwingine hutokea amsho za aina mbalimbali za huduma au watu
wengine ni watumishi halisi wa Kristo lakini wengine huangukia katika hayo
mawimbi ambayo kimsingi huinuka na kutoweka, kama wakristo hawajaimarishwa
vizuri wakabaki wachanga kila wakati
linapotokea wimbi la aina moja utaweza kuona wakristo hao wakristo hao
wakiruka na wimbi hili na lile badala ya kukua, kukomaa na kufikia ngazi ya
kutumika kwa uaminifu katika eneo lako uliloitiwa. Kwa ujumla tunajifunza na kuona kuwa kuna hasara kubwa sana ya
kuwa na wanafunzi wa Bwana Yesu wasiokuwa na moyo wa kutafuta ukamilifu!
-
Kubadili
neema ya Mungu kuwa ufisadi – Yuda
1:4 “Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri,
watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu
wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu
Kristo.”
Moja ya
changamoto kubwa pia inayolifanya kanisa la leo kushindwa kuishi maisha ya
ukamilifu ni matumizi mabaya au tafasiri mbaya ya mafundishio kuhusu neema,
kupitia mkazo mkubwa na wa kijinga kuhusu neema ya Mungu watu wengi wamejikuta
wakiishi maisha ya dhambi na kutokubadilika kwa kisingizio tu kuwa Mungu
ametupa neema na tunaishi wakati wa neema, lakini Paulo mtume akifundisha
kuhusu Neema ya Mungu aliweka mkazo ulio wazi kuwa neema sio tiketi ya kuishi
maisha ya dhambi ona
Warumi 6:1 -2 “Tuseme
nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi
tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? ”
Neema ya Mungu
kazi yake ni kuturahisishia kuishi maisha ya haki na utauwa bila kutumia nguvu
kama wakati wa sharia, neema inasaidia kuwa kama Kristo alivyo na kama Mungu wa
mbinguni alivyo ni neema ya Mungu inayotusaidia kuwa wazuri, wenye maisha ya
kiasi na sio kuishi maisha mepesi ya dhambi. Ndani ya neema ya Mungu kuna uweza
wa kiungu wa kutuwezesha kuishi maisha ya kumpendeza Mungu nay a viwango ona
Tito 2:11-12 “Maana
neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa
ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa;”
Unaona neema
sahihi inatusaidia kukataa tama na ubaya, kukataa tamaa za kidunia, kutupa uwezo
wa kuishi maisha ya kiasi, haki na utauwa katika ulimwengu huu huu, kwa hiyo
hakuna neema inayokuelekeza kuishi maisha ya dhambi, lakini kutokana na
mafundisho mabaya kuhusu neema kanisa la leo linachukulia dhambi kama jambo poa
na lisilo la ajabu. Ni neema ya Mungu ndiyo inayotusaidia kubadilika na kuwa na
tabia kama ya baba wa Mbinguni nanyi mtakuwa wakamilifu, ukamilifu huu
hauwezekani bila neema sahihi, kama utafundishwa kuwa kuna neema na inakusaidia
kuona uko sawa dhambini hiyo itakuwa ni injili nyingine neema ya Mungu
itaachilia hukumu ndani yako itakayokuleta katika toba wala sio kuishi
dhambini, Moja ya changamoto inayowafanya wanafunzi wa Yesu leo kutokuwa
wakamilifu kama baba wa mbinguni ni mafundisho kuhusu neema iliyopitiliza,
ambayo inakufanya udumae na sio upokee mabadiliko
-
Kufilisika
kiroho - Kanisa linapopoteza
mwelekeo sahihi hususani katika fundisho la kuwa na tabia njema na mwenendo
mwema na kuwa wakamilifu na kuishi maisha ya utakatifu na tukakazia maswala
mengine yasiyo na umuhimu kama kutajirika tunaweza kujikuta
kuwa tuna changamoto nyingine mbili, jina la kuwa tajiri, lakini ni masikini
yaani kanisa limekuwa na utajiri wa mali za kawaida lakini limekuwa masikini na
limepungukiwa na kuwa na umasikini wa tabia za uungu, kanisa lina jina la kuwa
hai lakini limekufa lina mali lakini
liko uchi ona
Ufunuo 3:1 “Na
kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na
hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una
jina la kuwa hai, nawe umekufa.”
Ufunuo 3:16-17 “Basi,
kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika
kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja
ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na
kipofu, na uchi.”
Unaona hali ya
kanisa la watu wasiolenga kukamilika hubaki katika kusheherekea mafanikio ya
kimwili huku nguvu za rohoni zikiwa zimefilisika, niliwahi kumsikia askofu wa
kanisa Fulani msomi mkubwa akinieleza ya kuwa kulikuwa na wachawi kanisani
kwake na walikuwa wakikopera sadaka mpaka aliposimama na kuwakemea waache tabia
hizo? Ndipo wachawi wakapunguza kukopera sadaka, Kama kweli kanisa la Mungu
linaweza kufikia hatua ya kuweza kuwa na wachawi ndani na wakahudhuria ibada na wanaamini na kuweza kufikia ngazi ya
kukopera sadaka haiingiia akilini kuendelea kufikiri kuwa kanisa lina uhai,
afadhali kidogo kama ningesikia kuwa kuna waizi wanaiba sadaka wakati wa
kuhesabu na tumewakamata kupitia ccctv Camera kidogo ingeweza kuingia akilini
kufikiri hivyo lakini kama zinakoperwa ni wazi kuwa tunahitaji kuwa na uamsho
na kuruhusu nguvu za Mungu kutamalaki na kuweka msisitizo mkubwa wa kuweko kwa
tabia ya ukamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Bado tunaweza
kushuhudia na kuelewa kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kutokulifundisha
kanisa kuwa na tabia na mwenendo ulio mkamilifu, tungeweza kuchambua mambo
kadhaa wa kadhaa yanayodhihirisha kuwa tunamuhitaji Mungu na tunahitaji kukua
kiroho na kuwa wakamilifu lakini nadhani kwa maswala hayo machache umeweza
kuona kuwa msisitizo wa kuwa na kanisa lenye ukamilifu kama baba yetu wa
mbinguni unahitajika sana katika karne yetu. Sasa ni namna gani tunaweza
kujikwamua kutoka katika tatizo hili? Kwanza hatuna budi kujipima kama
tunakomaa kiroho, kimaadili na mwenendo.
Kipimo cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.
1.
Ni jukumu la mtu mmoja mmoja kutamani kuwa
mkamilifu kama alivyo baba wa Mbinguni – Neno la Mungu linatuonyesha kuwa
tunaweza kuwa wakamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa msingi
huo ni vema sasa kila mmoja wetu akawana na shauku ya kuwa kama Kristo ambaye
ni kiongozi mkuu wa wokovu wetu na ambaye ametuachia kielelezo tukifuate Mathao 5:6 “Heri
wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”
2.
Ni jukumu la kila mmoja kutamani kuuweza mwili
wake na hisia zake katika utakatifu 1Wathesalonike
4:3-4 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa
kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika
utakatifu na heshima;”
3.
Ni jukumu la kila mmoja kuwa na Upendo kwa
Kristo mwenyewe alisema mkinipenda mtazishika mari zangu Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri
zangu.”
4.
Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa
najijengea upendo wa kupenda maswala ya kiroho yanayochangia ukuaji wa kiroho
mfano kujisomea neno la Mungu, kuomba, kusikiliza mahubiri, kuhudhuria ibada,
kufunga, kujitoa kwa Mungu na kutimiza agizo kuu
5.
Ni jukumu la kila mmoja kutamani kukaa katika
uwepo wa Mungu na kuimarisha uhusiano wako na Yesu Kristo
6.
Kukubali kusamehe na kuachilia au kushindwa na
kupoteza haki zetu kwa faida ya ufalme wa Mungu
7.
Kukubali kuwa na maisha ya mfano na kuhubiri
kile ambacho sisi wenyewe tunakifanyia kazi 1Wakoritho 11:1 “Mnifuate mimi kama mimi
ninavyomfuata Kristo.”
8.
Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa anajaa
Roho Mtakatifu na kuwa na maisha yaliyojaa muongozo wa Roho Mtakatifu Waefeso 5:18 -20 “Tena
msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa
zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni
mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana
wetu Yesu Kristo;”
9.
Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha nya kuwa
anakubali maonyo makemeo na marekebisho kutoka kwa watu wanaoaminika kuwa
wamekomaa kiroho na kama wameona kuwa kuna jambo sahihi la kukemea katika
maisha na mafundisho yetu
10.
Ni jukumu la kila mmoja wetu kukubali
kufundishika na kukiri makosa yetu pale tunapokuwa tumekosea
11.
Ni jukumu la kila mmoja wetu kutambua na
kukubali ya kuwa hatujui kila kitu 1Wakorintho
8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno
lo lote bado, kama impasavyo kujua.”
12.
Ni jukumu la kila mmoja wetu kujilinda na kiburi
na majivuno pamoja na kuchukua utukufu wa Mungu
13.
Kukubali kujifunza kutoka kwa wengine na
kutambua huduma na ubora wa wengine katika eneo Fulani la maisha yetu
14.
Kuamini kuwa neno la Mungu ndio mamlaka ya
mwisho na ya kuwa hakuna mtu aliyejuu ya neno la Mungu
15.
Kukubali kuitambua na kuelewa na kupambanua ili
kuitii na kuifuata sauti halisi ya Roho Mtakatifu na mapenzi ya Mungu
16.
Kuwa na uhusiano ulioshiba na Roho Mtakatifu
Siku hadi siku katika maisha yetu
kama tutayatendea kazi maswala kadhaa tunayojifunza hapo juu uwezekano wa
kuishi maisha ya ukamilifu na kuwa na tabia alizosema Kristo, uwezo wa kusamehe
maadui na kuwaombea, uwezo wa kuvumilia, kuwasalimia hata wale wasiotupenda na
kadhalika, hakuna jambo zuri na la kupendeza ni kuwa kama baba yetu wa Mbinguni
alivyo.
Rev. Innocent Mkombozi Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima