Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo
nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na
Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea
nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi
nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani?
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa
wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”
Utangulizi:
Je kuna watu wamewahi kukuacha na
kuondoka katika maisha yako? Je kuna watu hawakupigii simu wala hawashughuliki
tena na maisha yako? Je kuna watu mlikuwa karibu sana na siku hizi hawako
karibu kama ilivyokuwa zamani? Je unahuzunika kwaajili yao? Je unalalamika kuwa
hawakusalimii, hawatumi hata ujumbe na hawaulizi hata uko wapi na unafanya
nini?, hawashughuliki hata kukusalimu? kuna watu ulikuwa msaada mkubwa sana kwao,
lakini sasa wako mbali na wewe? Je unahuzunika kwaajili yao? Kuna watu walikuwa
faraja kubwa sana katika maisha yako, uliwapenda na wao wakakupenda,
wakakufuata lakini sasa ni kama hawako na wewe, kuna wale mlisoma nao shule
moja, darasa moja, kuna wale uliwasimamia harusi, kuna wale mlikuwa pamoja,
mlicheza pamoja, kuna wale walikaa kwenu wakasomea kwenu, kuna wale ulisoma
kwao ukakulia kwao, kuna wale ulikuwa msaada mkubwa kwao kiroho na kimwili na
sasa ni kama hawataki kutambua mchango wako je unaumia kwaajili yao? Unalia
kwaajili yao? Unasikitia kwaajili yao? Sikiliza wako watu ambao Mungu huwavuta
kwetu na kuwaleta karibu nasi kwa makusudi maalumu, wako ambao Mungu amewaleta
kwetu kama wenzi wetu, ndugu zetu, watoto wetu na ambao tunawafurahia hawa ni
furaha yetu ni damu yetu ni watiifu kwetu hawawezi kutuacha kwa sababu Mungu
alikusudia wawe nasi milele, kwa wakati mzuri na wakati mbaya, wako pamoja nasi
hawana namna ya kujitoa kwetu, wao ni familia hawawezi kutuacha wala sisi
hatuwezi kuwaacha. Lakini wako ambao Mungu huwaleta kwetu kwa sababu maalumu
kama marafiki kwa kitambo, ni watu wema kwetu na wazuri kwetu lakini uko wakati
ambao Mungu hufunga mlango na kuwaacha waende zao kwa sababu hawana shughuli
kwetu tena, lile kusudi ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwa kuwaleta kwetu
limeisha, Mlango umefungwa kwao kwaajili yetu, hawawezi tena kwenda unakoenda
kwa hiyo Mungu hufunga mlango kwaajili yao, mchango wao wa kimwili na kiroho na
kiushirika unakuwa umeishia hapo ambapo Mungu amekusudia uishie, huu ni ukweli
ulio mchungu katika maisha, lakini hatuna budi kuukubali na kuujifunza na kujua
kuwa ni mapenzi ya Mungu., Kama wana kazi nasi Mungu atawaleta tena Mara.
Muhubiri 3:1-8 “Kwa kila jambo kuna majira
yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati
wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua,
na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia,
na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa
kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa
kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na
wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza,
na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita,
na wakati wa amani.”
Leo tutachukua muda kujifunza kwa
kina na mapana na marefu kuhusiana na uhusiano uliofifia au uliokufa au
ulioondoka na faida zake katika ufalme wa Mungu, tutajifunza namna unavyoweza
kuelewa Mapenzi ya Mungu watu wanapokuacha na kuondoka zao katika maisha yako,
Utajifunza namna na jinsi unavyopaswa kutokuhuzunika na kuwa na mashaka watu
wanapokuacha na kukuona huna maana kwao, na kuona ya kuwa hawakuhitaji tena,
hupaswi kulazimisha, wala hupaswi kujikomba komba, wewe umeumbwa kwa thamani
kubwa sana na; Ni Mungu tu aliyekuumba
ndiye anayeijua thamani yako, kwa hiyo hatujifunzi kubomoa uhusiano hapa katika
somo hili lakini tunajifunza kuwaachia watu wanaojiondoa katika maisha yetu
wajiondoe, wataendelea kuwa rafiki zetu, na tutaendelea kuwapenda, lakini kama
hawajihusishi na maisha yetu hatupaswi kuumia lazima ufikie wakati ukubali
waende na ujue ya kuwa Mungu ameruhusu waende zao!, na kuna faida zake katika
hilo, kwa hiyo hupaswi kulazimisha wakae, kwani unapojaribu kulazimisha kuwa na
watu ambao wameshajiondoa katika maisha yako au Mungu amewaondoa katika maisha
yako hii maana ni nini? Maana yake yake unajaribu kung’ang’ania, na kulazimisha
kitu ambacho, Mungu ameshamalizana nacho katika maisha yako!, fahamu kuwa kila
mtu ambaye Mungu alimleta kwako alimleta yeye kwa kusudi la kukujenga na kukupa
changamoto na unapofika wakati mtu huyo au watu hao wanaondoka fahamu kuwa ni
Mungu amewaondoa kwako kwa kusudi maalumu, kwa hiyo hupaswi kushangaa,
kulalamika au kujifikiri kuwa una mapungufu na kulalamika na kuhuzunika na
kulaani hapana!
Kifungu kile cha msingi
tulichokisoma leo, ndicho ambacho kinabeba mafunuo yote ambayo Mungu amekusudia
kutufundisha katika siku ya leo kwa mfumo wa kichambuzi (an Expository
preachings) na tutakiangalia kupitia mstari kwa mstari tukizingatia vipengele
husika katika somo hili hebu tukisome tena na kisha tutakifanyia uchambuzi wake
Yohana 6:65-69 “Akasema, Kwa sababu hiyo
nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na
Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea
nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi
nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani?
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa
wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”
Tutajifunza somo hili “Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?” kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano.
·
Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.
·
Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?
Mungu ndiye mwanzilishi wa uhusiano
Yohana 6:65 “Akasema, Kwa sababu hiyo
nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na
Baba yangu.”
Katika kifungu hiki Yesu Kristo
anatufunulia jambo ambalo sio tu linatokea katika maisha yake lakini vile vile
linatokea katika maisha yetu kama watoto wa Mungu, Yesu alizungumza hili
kuhusiana na wanafunzi wake akieleza kuwa hakuna mtu awezaye kuja kwake
isipokuwa amejaliwa na baba yake wa Mbinguni, hili linatufunualia sisi nasi
kuwa Ni Mungu ndiye anayeruhusu watu watukaribie na ni Mungu ndiye anayeruhusu
watu waondoke, Marafiki zetu wanaweza
kuwa msaada mkubwa sana katika maisha yetu, wanaweza kutumiwa na Mungu kututia
moyo, kutusaidia, kutujenga na kutupa ufahamu fulani katika safari zetu za
kiroho na kimwili na kisaikolojia na kimakuzi, kwa hiyo marafiki ni neema ya
Mungu, ni kupitia mahusiano ya kirafiki Mungu huwatumia marafiki kutuonyesha
upendo, kutuonyesha namna na jinsi Mungu anavyojali, na hata kututia moyo na
wakati mwingine huwatumia kutupa changamoto, kwa hiyo kila urafiki ni lazima
utunzwe na kuchukuliwa kama zawadi ya Mungu katika maisha yetu na kuwa kupitia
wao liko kusudi la Mungu, marafiki wengine huokoa maisha yetu kutoka katika
maangamizi ya adui, wengine hutufundisha kuwa hata kama wako watu wanatuchukia
bado wako ambao wanatuthamini sana na wanathamini mchango wetu na umuhimu wetu
katika dunia hii, wengine hutusaidia kukua kiroho, na wengine tunawasaidia wao
kukua kiroho na kadhalika kwa ujumla tunahitajiana na ndio maana tunahitaji
ushirika.
1Samuel 18:1-5 “Ikawa Daudi alipokwisha
kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani
akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha
arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa
kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa
amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde
wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na
Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili
likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.”
Daudi hakukubalika sana kwa Sauli
lakini hata hivyo mwana wa mfalme Yonathan alikuwa rafiki mwenye kufaa sana kwa
Daudi, maandiko yanaeleza kuwa Yonathan alimkubali Daudi na na watu hawa
walikuwa na agano la urafiki uliodumu sana hata baada ya maisha yao, ulikuwa ni
urafiki wa kweli na wenye kufaa sana, ulikuwa ni urafiki wenye uhusiano wa kina
kama uhusiano wa ndugu, Yonathan alikuwa mwelewa kwa rafiki yake Daudi, Yonathan
aliyajua mapenzi ya Mungu yaliyokuwa juu ya Daudi, Yonathan hakuwa rafiki
mwenye wivu wala hila, Yonathan alimtia moyo Daudi, alimpa mavazi ya kifalme
aliyotumia mwenyewe, alimpa silaha, alimlinda alikuwa akimtakia mema, pamoja na
kuwa baba wa Jonathan hakumpenda Daudi, alimchukia alimkusudia mabaya lakini
haikuwa hivyo kwa Yonathan yeye alikuwa rafiki wa kweli. Na mtu ambaye
aliangalia maslahi ya Mungu kwa upana. Hakuwahi kumponda wala kumchafulia sifa
yake wala kutaka rafiki yake asipate kibali kwa mfalme, wakati wote Yonathan
alikuwa faraja kubwa
1Samuel 19:4-6 “Naye Yonathani akamsifu
Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani,
juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa
mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti,
naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo
hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo
Daudi bure?Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo
Bwana, yeye hatauawa.”
Kwa ujumla Yonathan alikuwa
rafiki wa kweli kwa Daudi, alikuwa ni zaidi ya ndugu, alilinda uhai wa Daudi,
na hakukubali maisha ya Daudi yawe hatarini wakati wote alitengeneza mazigira
mazuri, ili raiki yake akubalike kwa baba yake asionekane kuwa muhalifu,
alimtetea na kumtia Moyo na alimjulisha kuhusu hatari ambazo zingeweza
kumkabili, kama tunataka kujifunza watu waliokuwa na urafiki wa dhati basi
Daudi na Yonathani ni mfano wa kuigwa, Yonathani alikuwa ni rafiki
aliyeambatana na Daudi na mwenye kufaa sana kuliko ndugu.
Mithali 18:24 “Ajifanyiaye rafiki wengi ni
kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”
Marafiki zetu hawaji wenyewe
kwetu huwa tunaletewa na Mungu na Mungu ndiye anayewavuta watu kuja kwetu, kama
vile tu alivyowavuta wanafunzi kuja kwa Yesu Kristo, hakuna mtu awezaye kuja
kwangu, isipokuwa amejaliwa na Baba yangu, Neno hilo kujaaliwa katika kiyunani
linatumika neno “Didōmi” kimatamshi ni Did-o-mee ambalo maana yake “with the palm of hand” yaani ni tendo
la Mungu kuushika mkono na kumleta mtu moja kwa moja na kushikisha katika
kiganja cha mkono wa mwingine kama tu vile mtu anayemkabidhi bibi harusi kwa
mumewe siku ya harusi yake, kwa hiyo Ni Mungu Baba ndiye anayetushika mkono na
kutupeleka katika mikono ya Yesu, hali kadhalika ni Mungu ndiye anayewashika
mkono wale waliokusudiwa kuwa rafiki zetu na kuwaleta katika mikono yetu, Kwa
hiyo ni muhimu sana kutomchukulia kwa dharau mtu awaye yote anayetamani kuwa na
urafiki na wewe kwa sababu kila unayeletewa au anayekujia analetwa kwako na
Mungu kwa kusudi maalumu katika maisha yako na kwa ufalme wa Mungu, wakati wote
watu wanapokuwa marafiki mioyo yao inaunganishwa kuwa kitu kimoja kwaajili ya
mafanikio ya yule ambaye Mungu amemkusudia au kwa kufaidiana, na kila wakati
Mungu huhakikisha kuwa pande zote mbili zinanufaika na urafiki huo, kwa hiyo
wote mnajengana na kufaidiana kwani chuma hunoa chuma Mithali 27:17 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo
mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” Marafiki zetu huletwa kwetu na
Mungu kwa kusudi la kutusaidia na sisi kuwasaidia na wakati mwingine kwajili ya
kufaidiana, kama Barnaba na Sauli au Paulo
Matendo 9:26-28 “Na Sauli alipofika
Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote,
wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa
mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye,
na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa
pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.”
Maumivu ya kuvunjika kwa uhusiano.
Yohana 6:66 “Kwa ajili ya hayo wengi
miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.”
Hata hivyo Pamoja na kuwa Mungu
huwaleta watu karibu nasi kama tulivyojifunza kutoka kwa Bwana Yesu ni jambo la
kusikitisha kuwa, kuna wakati mwingine wengine
wataondoka kama ilivyokuwa tu kwa Yesu, watu au wanafunzi wengi siku hiyo
waliamua kuondoka tena biblia inasema wasiambatane
naye tena, hapa ni kwa sababu walishindwa kupokea mafundisho yake magumu
katika akili zao, jambo hili linatufunza ya kuwa si kila mtu anayeanza safari
pamoja nasi atakuwa pamoja nasi mpaka mwisho, na wakati huu ni wakati wa
maumivu makali sana hakuna jambo linaumiza kama kuvunjika kwa mahusiano, yawe
ya ndoa, yawe na ushirika, yawe ya kichungaji, kazini na kadhalika, lakini
Mungu huruhusu watu hao waende na huo ndio unakuwa mwisho wa stori yao katika
maisha yetu, inauma sana na inaumiza sana lakini hatuna budi kukubali, kama
ilivyokuwa kwa Yesu Kristo ambapo wanafunzi wake walimuacha na hawakuambatana
naye tena ndivyo ilivyo kwetu pia kuna kusudi kwa kila jambo katika maisha
yetu, wakati huo hakuna lolote
tunaloweza kulifanya kuwafanya wabaki, Mungu tayari amekwisha kukusudia,
wakuache wale wanaokupenda kwa dhati hawawezi kukuacha watabaki na wewe iwe jua iwe mvua lakini wale
ambao Mungu amekusudia waende wataenda tu hakua namna unaweza kulizuia hilo,
hukuwaleta wewe kumbuka kwa hiyo acha
waende zao kwa amani, Kama Mungu ndiye aliyeamua waende hakuna unaloweza
kulifanya wasiende?
Mungu ndiye mwenye funguo na
mamlaka za kufunga na akifunga hakuna afunguaye, na akifungua hakuna anayeweza
kufunga unaweza kujaribu kubembeleza na kujipendekeza kwa watu na ukajitahidi kuwapendeza
na kufanya vizuri lakini kama Bwana hajaruhusu utakuwa unajisumbua bure, kile
utakachokuwa unakitafuta ni kutafuta maumivu ya moyo tu, jaribu njia mpya na
waache waende usiumie wala usikwazike ni Mungu ameruhusu, lazima tuamini kuwa
Mungu ndiye anayedhibiti watu kuja na kuondoka katika maisha yetu na wengine
huletwa kwetu kwa majira fulani tu kisha anawaondoa, unapoendelea
kuwang’ang’ania watu ambao wamepoteza maana katika maisha yako maana yake
unazuia kusonga kwako mbele au kukua katika kiwango kingine. Rafiki mimi
ninajua uchungu wa kupoteza marafiki, ninapenda watu sana, sitaki kila ambaye
amewahi kuwa rafiki yangu aniache, lakini uko wakati unalazimika kufanya hivyo,
wako wapi uliosoma nao shule ya msingi, sekondari, vyuoni, na hata katika utumishi
huu wako wapi? Wako wapi uliofanya nao kazi zamani,? Ulifika wakati waliondoka
na Mungu aliwaficha na hukuweza kuwaona tena, kusudi la kuwepo kwao katika
maisha yako lilikwisha kutimia na sasa Mungu anataka ufungue ukurasa mpya. Ona
mfano wa maumivu yaliyomkuta Naomi:-
Ruthu 1:3-18 “Akafa Elimeleki, mumewe
Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika
wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu.
Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na
huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka,
yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya
Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi
akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili
kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa
mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama
ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. Bwana na awajalie kuona
raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao
wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.Naye
Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao
watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu,
mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama
ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa
kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume?
La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa
Bwana umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu
mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako
amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji
yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana
wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu,
Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo
nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”
Tunasoma habari za Naomi, ambaye
mumewe alifariki na kumuacha na watoto wawili ambao nao baadaye walioa, lakini
vile vile walikufa katika nchi ya Moabu, kwa hiyo Naomi alibaki peke yake yeye
na wakwe zake, Naomi aliamua kurudi kwao Yuda na aliwaeleza wakweze juu ya
maamuzi yake mmoja aliitwa Orpa na mwingine Ruthu, Ruthu aliamua kubaki naye na
Orpa aliamua kubaki katika inchi yake, wote walimpenda mkwe wao Naomi lakini
Orpa aliamua kumbusu Naomi na kuondoka, Naomi hakuanza kulalamika kuwa Orpa
anaondoka hata pamoja na wema wote aliomtendea na malezi yote aliyowapa Naomi
alielewa kuwa huu ni msimu mpya ni msimu wa mabadiliko katika maisha kwa hiyo alikuwa
na amani alipoachwa na Orpa alikubali kuwa Orpa aende na asiwe sehemu ya maisha
yake tena, Mtu aliyekomaa kiroho/na kiufahamu huwaachia watu waende, unakubali
Mungu awaondoe watu fulani katika maisha yako, Mungu ndiye anayefunga mlango au
kufungua, lakini Ruthu aliamua kubaki na Naomi kwa gharama yoyote ile, hii ndio
hali halisi, Yesu watu waliondoka na hakutikisika aliwauliza waliobaki naye je
ninyi nanyi mwataka kuondoka? Aliendelea kuacha mlango wazi kwa kila anayetaka
kumuacha, Naomi Orpa aliondoka ulikuwa wakati mgumu na wa maumivu makali sana,
ulikuwa ni wakati mgumu ulikuwa ni wakati wa machozi lakini hakuna tunachoweza
kufanya pale watu waliokuwa rafiki, waliokuwa ndugu waliokuwa jamaa zetu,
waliokuwa wenzetu waliokuwa tunashinda nao, na kuzungumza nao wanapoamua
kutuacha ni vema kukubali waende, Naomi alimbusu Orpa na kumuacha aende,
kumbuka hatuhitaji kufukuza mtu au
kumaliza nao vibaya wala kuwa na uadui nao lakini sasa wanaondoka utafanya nini
tuwaache waende zao kwa Amani huo ndio ukomavu wa kifikra na ukomavu kiroho na
ujuzi, sio wewe tu utaacha wewe pia unaweza kuachwa na watu uliowapenda lakini
wakawa hawakuhitaji tena huwezi kubadili pai isiwe 22/7 ni lazima ukubaliane na ukweli wa mambo hata
kama ni mchungu kiasi gani waache waende!
Yesu aliwahi kuwafundisha
wanafunzi wake kuwa sio kila mahali watawakubali, ziko sehemu nyingine watu
watakukataa hawatafungua mioyo yao kwako, watakukataa hawatakukaribisha unajua
unachotakiwa kukifanya ni kukung’uta mavumbi ya miguu yako kisha enenda kule
ambako watakukaribisha, hii sio kwa ugomvi ni sehemu ya kawaida kabisa katika
maisha kwamba watu watakuja kwetu na kisha wataondoka na sisi halikadhalika.
Mathayo 10:13-14 “Na nyumba ile ikistahili,
amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.Na
mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile,
au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.”
Matendo 18:6-8 “Walipopingamana naye na
kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya
vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa.
Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha
Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa
sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi
waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”
Usijisumbue na watu ambao
hawakutaki, watu ambao hawaoni thamani yako, wala usijaribu kuwashawishi,
endapo utafanya hivyo utajichelewesha na utajipatia fadhaa bure, Ni kweli Mungu
anaweza kuwabadilisha kama watatakiwa
kukuunga mkono lakini kamwe usijaribu kujilazimisha kuungana na watu
wasiotambua uthamani wako, damu ya kifalme ya Yesu Kristo inatitiririka katika
mwili wako wewe sio wa kawaida wewe ni mali ya Mungu na ndio maana Mungu
alikuokoa na amekuumba kwa sura na mfano wake kwa hiyo usiwashawishi watu
wakukubali kama mioyo yao imefungwa, Mungu ameandaa watu tayari wanaotambua
uthamani wako, inaweza kuwa inauma sana lakini ndio ukubwa achana nao waache
waende, katika maisha yetu wako Orpa wengi lakini vile vile wako Ruthu wengi
ambao wamepangiwa kutokutuacha watakaokaa nasi, na kuambatana nasi wanaoondoka
ni kuwa Mungu amemalizana nao katika kusudi lao kwako na wanaobaki ni wale
ambao Mungu anataka ushirikiane nao Baraka zako, wale walio kama Ruthu watabaki
kuwa waaminifu kwako na hawatakuacha
daima, hatupaswi kumfukuza mtu wala kumpiga teke mtu lakini acha wao watupige
teke na kutufukuza na hapo neema ya Mungu ya urafiki wetu kwao itakuwa imefikia
ukingoni inasikitisha inaumiza sana
lakini huu ndio ukweli katika maisha.
Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa
kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu
katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.Barnaba akaazimu
kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua
huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano
baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda
Kipro.Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe
neema ya Bwana.”
Paulo na Barnaba walikuwa
marafiki, waliitwa pamoja na Roho
Mtakatifu katika kazi ya huduma, waliihubiri injili kwa pamoja kimsingi Barnaba
alikuwa ni kama Mchungaji wa Paulo mtume, ni yeye ndiye aliyemtambulisha kwa
mitume na ni yeye aliye mpeleka Antiokia, walizoeana sana, waliitwa kwa pamoja
na Roho Mtakatifu kwa kazi ya umisheni, lakini ulifika wakati wakaachana
haikuwa kwa lengo baya wala kwa ugomvi, lakini ulifika wakati ambapo Mungu
alikusudia kila mmoja awe na njia yake hili ni jambo la kawaida sana katika
maisha wao tofauti yao ilikuwa ni Marko, nadhani inawezekana Marko alijisikia
vibaya maana Paulo alimuona ni mtu dhaifu, Lakini Barnaba aliona Marko
anahitaji malezi tu kwa hiyo kulitokea tofauti na kulitokea matengano, Lakini
Mungu ni mmoja, miaka mingi baadaye, Paulo aliutambua umuhimu wa Marko na
aliomba aungane naye maana anamfaa kwa huduma! Angalia:-
2Timotheo 4:10-11 “Maana Dema aliniacha,
akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda
Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae
Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”
Paulo alimkumbuka Marko na
kuagiza aletwe kwake kwa sababu ana faida nyingi sana kwa utumishi, kumbe kuna
mtu anaweza asiwe na faida kwako leo, lakini akawa na faida kwako kesho,
unaweza usimuhitaji mtu leo lakini ukamuhitaji mtu huyo kesho, Mungu ndiye
anayehusika anaweza mtu asikufae kwa jua akakufaa kwa mfua na anaweza mtu
asikufae kwa mvua akakufaa kwa jua hii ndio dunia ya Mola kwa hiyo tuheshimu
mahuisiano sana na kuyatunza isipokuwa
pale to Mungu anapoamua huyu aende kule na huyu aje hapa kwa makusudi yake mema.
Wakati mwingine mafanikio yetu
yanaweza kuwavuta watu wengi sana kwetu, na mapito yetu yanaweza kuwafanya
wengi watukimbie, unapitia upweke? Wakati wa changamoto hakuna mtu wa kukutia
moyo? Hii ilimpata Ayubu Maandiko yanasema watu wa nyumbani mwake walikuwa
wengi sana ona
Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni
kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda
wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni
mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”
Unaona tunasoma kuwa watu wa
nyumbani kwa Ayubu walikuwa wengi sana wakati wa mafanikio yake, lakini wakati
wa dhiki yake watu wote walimuacha na kundoka zao, hata hivyo wakati wa
mafanikio yake walirejea tena kwa wingi sana, hili nalo ni jambo la kawaida
katika uanadamu kwa hiyo usivunjike moyo unapopitia upweke!
Ayubu 42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea
rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo
kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana
naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia
na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote Bwana aliouleta juu yake; kila
mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja. Basi hivyo Bwana
akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo
kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake
elfu.”
Wakati mwingine watu, na marafiki
zako watakuacha kwa sababu tu unapita katika hali ngumu, lakini wanaweza
kukurudia tena hali inapokuwa nzuri hili nayo ni jambo la kawaida katika maisha
na hatuna budi kulielewa na kukubaliana nalo. Jambo kubwa la msingi ni kwamba
mahusiano yanapaswa kutunzwa na kuwa na Amani na watu woe ni swala la smingi
sana tuwapo duniani. lakini watu wanapoondolewa kwetu, tumshukuru Mungu
kwaajili yao
Je ninyi nanyi mwataka kuondoka?
Yohana 6:67-69 “Basi Yesu akawaambia wale
Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu,
Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele Nasi
tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”
Yesu anatufundisha kuwa yeye
alikuwa tayari kuwaacha watu waende zao, Kama wamechagua kwenda hakuwalazimisha
kubaki nao lakini aliwapa uhuru wa kuondoka ili wafanye maamuzi yao wenyewe,
waache waende zao kwa Amani, kama wamejisikia raha kuwa mbali na wewe wamejisikia
Amani kukuacha acha waende! Na kama wamejisikia kubaki acha wabaki na wewe
usiwalazimishe, kulazimisha watu wawe nawe wakati hawana Amani ya kuwa na wewe
kutasababisha uchungu katika maisha yako, kukosa utulivu na majuto, lakini kama
utawaacha waende watapata nafasi mpya na kujiamulia mambo yao wenyewe, wape
watu uhuru wa kuamua na Amani ya Mungu itaamua.
Na huu ndio ukomavu wa kiroho, kiufahamu na kihekima. Let them go !
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo
lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja
zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote,
itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Amini katika kusudi la Mungu
kwamba Mungu anaporuhusu watu waende zao na au wabaki na wewe ufahamu kuwa
Mungu ana mpango mkubwa na mpya na kila mmoja, inaweza kuwa ngumu kuelewa
lakini hatuna budi kuamini katika mpango wa Mungu kwa kuwa Mungu ni mwema, watu
wanapoondoka katika maisha yako iwe kwa wema au kwa ubaya bado fahamu ya kuwa
Mungu ana mpango mwema kwenu wote yeye huweza kuitumia njia yoyote ile katika kutokeza
jambo lililo jema zaidi.
Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika
mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”
Rafiki wa kweli ni yule
atakayesimama na wewe hata katika hali ngumu, Petro na wale thenashara
walichagua kubaki na Yesu, Petro alisema tuende wapi Bwana wewe una maneno ya
uzima wa milele, wako marafiki watakaa na wewe kwa muda mfupi, au watajitokeza
kwako katika wakati Fulani maalumu na kisha watakoma lakini marafiki kama Petro
kwa Yesu Kristo watamaanisha kubaki na wewe, kwa hiyo ni Muhimu kutambua
umuhimu wao na kumshukuru Mungu kwaajili yao. Wakati wote kumbuka kuwa uhusiano
wowote ule uwe wa muda au ule wa kudumu una kitu cha kutufundisha katika maisha
yetu, hatukutanishwi na watu kwa bahati mbaya, Mungu hakumuumba mwanadamu awe
peke yake, tunahitajiana, Lakini Mungu huruhusu watu waje na kuondoka katika
maisha yetu kwa kusudi maalumu, jambo
kubwa na la msingi ni sisi kuendelea kuwa waaminifu katika kila aina ya
uhusiano ambao Mungu ametupa kumbuka mahusiano yanapovunjika inaleta maumivu
makali sana lakini wale wanaoondoka waache waende na wale wanaobaki kaa nao kumbuka
kuwa ni Mungu ndiye anayewashika mkono na kuwaleta kwetu kwa hiyo amini katika
mchakato huo na utakubali ukweli huu mchungu katika maisha, wafurahie sana wale
wote ambao Mungu anawaleta katika maisha yako ukijua kuwa ni sehemu ya mpango
wa Mungu, wakubali wale wote ambao Mungu
ameruhusu waende zao mbali na wewe ukijua pia kuwa Mungu ana mpango mwema,
thamini umuhimu na msingi wa marafiki hususani wale wanaobaki kuwa waaminifu kwako
hasa wakati wa majaribu na wakati wa mambo magumu, waheshimu wote wapende
wakubali lakini usilazimishe mtu akupende au awe na wewe hii haimaanishi
uwatendee watu kikatili hapana lakini jifunze kuwa kama Yesu, Yesu aliwahoji
hata wale waliobaki je ninyi nanyi mwataka kuondoka?
Hatima yako haiko mikononi mwa
waliokuacha, wala Mungu haitaji lolote uliloliacha au chochote ulichopoteza
kupitia marafiki walioondoka, jambo kubwa la msingi uwe na Amani lakini
usilazimishe watu wakupende na kukubali au wakuamini, ukiona wamekuacha maana
yake huwahitaji tena, wao sio sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha yako tena
na Mungu ana mpango mwema na wewe na hata wale wanaokusema vibaya waache
waseme, mimi nimewahi kusikia habari za mtu anayenisema vibaya na nikaonyeshwa
sijawahi kumkataza wala kumbeleza aniseme vizuri, ninajua tu kuwa Mungu
ameruhusu wawepo watu watakaonisema vizuri na wawepo watu watakaonisema vibaya
wote wana faida katika mapenzi ya Mungu, wanaonisema vibaya wananisaidia nisiwe
na kiburi, nikumbuke kuwa mimi ni mwanadamu na nizidi kunyenyekea na wale
wanaofaidika na huduma yangu watamshukuru Mungu kwaajili yangu, sina muda wa
kumbembeleza mtu asiniseme vibaya, siumii tena na wanaosema vibaya wala siwezi
kutukuka watu wakinisifu, ninanyenyekea kwa Mungu kwa sababu mimi ni udongo tu,
sikuja duniani kusifiwa, nimekuja duniani kutimiza kile ambacho Mungu
amekikusudia katika maisha yangu na hivyo kile nitapangiwa na Mungu kukifanya
nitakifanya, Petro alitambua ya kuwa Yesu ana maneno ya uzima wa milele, na ya
kuwa ni Mtakatifu wa Mungu yaani ni Masihi.
Bwana ampe neema kila moja wetu
kuelewa makusudi ya somo hili kwa kina na mapana na marefu katika jina la Yesu
Amen!
Na. Rev Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!