Jumapili, 15 Juni 2025

Huduma ya Kichungaji na Mama Mchungaji


1Timotheo 3:11 “Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.”




Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa katika mwili wa Kristo, Mchungaji ana nafasi ya muhimu sana katika kuongoza na kufundisha huku akililisha na kulichunga kundi la kondoo wa Bwana, lakini hata hivyo ni muhimu kuelewa kuwa Mchungaji sio kisiwa peke yake, anahitaji msaada wa wale walio karibu naye, na miongoni mwao ni Mama Mchungaji. Mama Mchungaji ni mwenzi wa Mchungaji na ana nafasi ya kipekee sana katika kuisaidia huduma ya mumewe kusimama au hata kudhoofika, Leo basi tutachukua muda kujifunza jinsi mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma ya kichungaji kudumu kwa mafanikio au jinsi tabia zake zinavyoweza kuathiri huduma vibaya, tutajifunza somo hili Huduma ya kichungaji na Mama Mchungaji kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Nafasi ya Mama Mchungaji katika huduma ya Kichungaji

·         Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kudhoofisha huduma. 

·         Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma kusimama.


Nafasi ya Mama Mchungaji katika huduma ya Kichungaji.

Ni muhimu kufahamu kuwa wake wa viongozi wa kiroho wanahusika moja kwa moja kwa namna moja ama nyingine na kwa njia tofauti katika kazi ya Mungu, Mwanamke anayekuwa mke wa mtumishi wa Mungu ana athari ya moja kwa moja katika huduma ya mumewe aidha kuifanya huduma hiyo kuwa na mafanikio makubwa na au kuifanya huduma hiyo kusambaratika, kwa bahati mbaya wakati mwingine watumishi wa Mugu wameandaliwa kwa muda mrefu na kwa muda wa kutosha kwaajili ya kuuhudumia mwili wa Kristo. Wakati mama wachungaji wengi hasa hapa Afrika, wameachwa wakiwa hata hawaitambui nafasi kubwa na muhimu waliyo nayo katika utumishi wao na waume zao, unapokuwa umepata nafasi ya kuolewa na Mchungaji, aidha kabla au baada ya yeye kuitwa katika huduma basi mama Mchungaji unapaswa kutambua kuwa Mungu hajamtuma mumeo peke yake na kwa sababu hiyo wote wawili mnahusika katika kumtumikia Mungu.

Luka 10:1-3 “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, AKAWATUMA WAWILI WAWILI wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu.”

Muhubiri 4:9-12 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.”

Kila mama Mchungaji anapaswa kuelewa kuwa Mungu amewaita wote wawili, hapa haimaanishi kuwa ni lazima kila mama mchungaji ajihusishe moja kwa moja na huduma ya madhabahuni hapana, lakini ufahamu wa mama Mchungaji kuhusu umuhimu wa huduma ya kichungaji na nafsi yake kama msaidizi wa mumewe una nafasi kubwa sana katika kuifanya huduma ifanikiwe, umoja wa wanandoa wenye utumishi ndani yao una mafanikio makubwa sana katika ulimwengu wa roho kuliko yanapokuwepo mafarakano kati yao, na shetani analijiua hilo vizuri, watu wawili wanapoungana na kukubaliana na kutengeneza kemia ya umoja katika ulimwengu wa roho hutokea mambo makubwa sana, Maandiko wakati wote yanaonyesha nguvu kubwa wanapohusika wawili katika utumishi ona

Kumbukumbu 32:29-30 “Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao. Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa?

Mathayo 18:19-20 “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

Kama mama Mchungaji na Mchungaji hawatakaa vizuri na kuwa kitu kimoja na kupatana, maombi yao yatazuiliwa na mafanikio yao katika huduma yataanza kudhoofika na kuathiri kazi za kichungaji

1Petro 3:6-9 “Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi Baraka

Kila mama Mchungaji awe mwenye huduma au asiye na huduma kwa maana ya wale wanaohudumu Madhabahuni na hata wale wasio na huduma ya madhabahuni, lakini kile kitendo tu cha kuwa mke wa Mchungaji kinamaanisha kuwa Mungu amekusudia jambo kwaajili yako, Mungu amekuita uwe na msaada kwa kazi ya mumeo, kwa hiyo ni muhimu ukajitambua hivyo na kusaidia wito wa Mumeo:


1. Wewe ni Msaidizi katika huduma.

 

Mwanzo 2:18 “  BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”

 

Mungu alimuumba mwanamke kama Msaidizi wa mwanaume, na hii inamaanisha ni katika kila kusudi ambalo mumeo ameitiwa wewe ni msaidizi wake, kwa hiyo kama mumeo ameitwa katika huduma wewe ni msaidizi wa huduma hiyo, kama mumeo ameitwa kwenye huduma ya kichungaji basi mke wa Mchungaji au mama mchungaji anahusika kwenye huduma hiyo moja kwa moja  na anaweza kuwa msaada mkubwa kwa Mchungaji au mume wake na kuleta faraja kubwa sana kwa ushauri, maombi, utulivu na busara, na kadhalika, kwa bahati mbaya wako baadhi ya mama wachungaji hawaungani na utumishi waliopewa waume zao na wao huishia kubweteka au kuwa mzigo wakifikiri kwamba hawana wito au hawakuitwa katika huduma hiyo na hawahusiki, na ni kazi ya mumewe na wao kuishi kama watu waendao kushoto ilihali waume zao wakienda kulia, iwapo ma Mchungaji atabweteka kiroho atakuwa mzigo na kama ilivyokuwa Eva ataleta mauti kwake na kwa mumewe na ama shetani atapitia kwa mama Mchungaji na kusababisha madhara makubwa kihuduma.

 

Mwanzo 3:6 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.”

 

1Timotheo 2:13-14 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”

 

Prisila alikuwa ni mwanamke aliyekuwa msaada mkubwa sana kwa mumewe Akila pamoja na mtume Paulo katika kazi ya injili, Yeye alishiriki moja kwa moja sambamba na mumewe na kuwa na mchango mkubwa sana katika mwili wa Kristo.

 

Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”

 

2.       Wewe ni msaidizi katika tabia na mwenendo.

 

1Timotheo 3:11 “Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.”

 

Tabia ya mama mchungaji mke wa Mchungaji inaathiri kwa kiwango kikubwa sana kazi ya huduma na injili, kila mama Mchungaji akijitambua na kujenga japo mazingira ya Amani ili kumpa mchungaji namna nzuri ya kutumika bila ya mgandamizo wa mawazo basi Mchungaji atakuwa na nguvu za kutosha kwaajili ya huduma

 

Mama Mchungaji mwenye Hekima atakuwa anajua wajibu mkubwa sana alionao mumewe na kwa sababu hiyo hata kama liko jambo atamueleza mumewe kwa hekima ya kiungu na kujitahidi kumuepushia migogoro isiyo na maana ya nyumbani kwa masalahi ya ufalme.

 

Kila mama Mchungaji ni lazima aelewe kuwa tabia na mwendo wake una maana pana sana katika huduma ya kichungaji, wajibu wa kuishi maisha ya maombi, kuwa kielelezo, kuwa mfano wa utii na utakatifu unaanzia nyumbani na mama Mchungaji anapaswa kuwa wakwanza kuigwa kwa wamama wote na hata mabinti, yeye anatakiwa kuwa kielelezo katika njia ya wokovu, na hapaswi kusema shauri zake kwani tumeitwa wote?! Mwenye huduma si ni yeye tu atajijua mwenyewe! Kushindwa kwa mama wachungaji kuwa kielelezo kikuu katika kanisa la Mungu ni kupunguza mamlaka ya kichungaji katika usimamizi wa familia na nyumba nyingi zilizoko katika kanisa lake na zile ambazo Mungu amempa ili kuwatunza.

 

1Timotheo 5:2-5. “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

 

3.       Wewe ni msaidizi katika kutia moyo

 

Wito wa kichungaji ni wito wa ajabu sana kuna wakati katika huduma za kichungaji unaweza kukutana na mambo magumu sana kuna majaribu, kuna upweke, kuna vitisho, kuna hatari, kuna kusakamwa, kuna kuchanganyikiwa, kuna kutokufurahishwa na kutokuridhika, kwa hiyo Mchungaji anahitaji kutiwa moyo na mtu aliye karibu, na mtu huyo ni mke wake, kwa kweli mtu anayeweza kuuinua moyo wa mchungaji ni mke mwenye upendo, unyenyekevu na uadilifu na mwenye uvumilivu mke wa jinsi hii anaweza kusaidia kuutimiza vema wito wa kichungaji na mama mchungaji ndiye mtu sahihi wa kufanya hayo, itakuwa inasikitisha sana kama ni mtu wa pembeni ndiye atagundua kuwa mchungaji amechoka, anahitaji kunywa maji anahitaji kupewa pole na hata kutiwa moyo, au kama tai yake imekaa vibaya, ameumizwa, na kadhalika kwa kweli hilo lilitakiwa kuwa labda jicho la tatu lakini jicho la kwanza lilitakiwa kuwa mama Mchungaji mwenyewe, Maandiko hayajawahi kueleza moja kwa moja wajibu wa mama Mchungaji wa kihuduma, lakini ukweli unabaki wazi kuwa ni mama Mchungaji ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuamua huduma ya mumewe iwe bora kwa kiwango gani na anaweza kufanya hivyo hata kwa kuwa mnyenyekevu na mtii kwa mumewe kwa sababu niliaminilo ni hili kuwa kama Mungu amemuita mume katika huduma anamuita katika ukamilifu wake yaani amemuita na mkewe hivyo utii wako kama mama mchungaji ni wa muhimu kwa mumeo na utumishi wake kwa masalahi ya ufalme wa Mungu.

 

Waefeso 5:22-24 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.”

 

4.       Wewe ni msaidizi katika maombi.

 

Kila mama Mchungaji ni anapaswa kuwa mwana maombi namba moja katika kuitia nguvu huduma ya kichungaji na kuitegemeza kwa maombi, mama Mchungaji anapaswa kuwa mwanamke wa maombi au mwanamke muombaji, kuna uwezekano wa kuwepo kwa watu wengine ambao Mungu anaweza kuwainua, kuiinua huduma ya kichungaji hata hivyo hilo sio swala la kutiliwa maanani ukilinganisha na nafasi aliyo nayo mama Mchungaji ombea huduma, mwenendo na maisha ya mumeo, lolote gumu kama likimpata wewe utakuwa mtu wa kwanza kuumia na wengine watafuata, kwa hiyo kuna umuhimu kwako kuwa muombaji.

 

Yeremia 9:17-20 “Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji. Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu. Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia

               

Waefeso 6:18 “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

 

Neno la Mungu linawatambua wanawake kama watu wenye uwezo mkubwa sana wa kulia na kuomboleza, kuliko hata wanaume na kama kuna wanawake wanapaswa kuwa waombaji ni wazi kuwa mama wachungaji wanapaswa kuwa wa kwanza, maombi yao yana uwezo mkubwa wa kuibeba huduma ya waume zao na kusababisha ufanisi mkubwa wa kihuduma.

 

5.       Wewe ni Mlinzi wa Mchungaji kwa Mungu na wanadamu.

 

Yeremia 31:22 “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.”

 

Nyakati za zamani ilikuwa ni wajibu wa Mwanaume kumlinda mkewe, na ndivyo ilivyo Mume ni mlinzi wa mkewe, Mungu alikuwa anazungumza na Israel kwa sababu yeye alikuwa mlinzi wao, alikuwa akijisikia wivu sana Israel walipokuwa wanamuacha, alikuwa hataki wamuache aliwalinda na kuwatetea lakini Mungu alisema ataumba jambo jipya yaani sasa Israel itaona wivu kuachwa na Mungu, watampenda Mungu kiasi ambacho wao ndio watakuwa walinzi wa Mungu wakiwa hawataki tena kufanya mabaya ili Mungu asije akawaacha ni katika dhana kama hii Mwanamke anawajibika kumlinda mumewe, uwe sambamba naye, usipendelee kumuacha acha, wako wanawake wengine hukosa hekima na kuwacha waume zao mara kwa mara, hawashikamani na na waume zao wala hawaambatani nao, Mumeo anapokuwa ni mtumishi wa Mungu basi ujue ya kuwa wewe una wajibu mkubwa kwa kumlinda ili awe salama kwa Mungu na kwa wanadamu, mlinde kwa kumkumbusha wajibu wake na maswala muhimu anayopaswa kuyatekeleza kwa Mungu, lakini mlinde pia dhidi ya wanadamu wanotaka kumuharibia huduma, mkumbushe mumeo wajibu wake kwa Mungu, mwamshe katika kuomba, hakikisha anakula kwa wakati, kuwa karibu naye katika huduma na wakati anapofanya ushauri wa kichungaji kama muhusika haoni shaka kujieleza chini ya uwepo wa mama Mchungaji, ambatana naye anapokwenda kutembelea washirika, hakikisha hafanyi jambo litakalopelekea apigwe na Mungu, Sipora mke wa Musa alimuokoa Musa kwa kufanya wajibu ambao Musa alikuwa ameupuuzia, Musa hakuwa amewatahiri watoto wake kwa hiyo Mungu alimkasirikia Musa na kutaka kumuua kwa kutokulishika agano la tohara, Lakini Sipora kwa haraka alijua nini kifanyike na kumuokoa Musa asiuawe na Mungu.

 

Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”

 

6.       Wewe ni mshiriki mwenza katika huduma.

 

Mama Mchungaji kama mshiriki mwenza katika huduma atashirikiana na Mchungaji katika huduma mbalimbali za kikanisa, anaweza kuwa sio muhubiri, lakini kama mchungaji anafundisha wana ndoa, au kama wanawake wanachama chao kanisani, mama Mchungaji anaweza kuhusika kwa namna fulani katika utelekezaji wa majukumu hayo aidha Ni muhimu kwa mama mchungaji kuwa mstari wa mbele katika mahudhurio ya ibada, kuwahi ibada, kusaidia usimamizi wa kanisa katika nyanja mbalimbali na maswala yahusuyo wanawake na watoto, usafi wa madhabahu na maswala mengineyo kwa kadiri ya neema ya Mungu, lakini zaidi sana kufundisha wanawake wa makundi yote kanisani na wanawake wachanga

 

Tito 2:3-5 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

 

Aidha mama Mchungaji anapaswa kuishi maisha matakatifu sawasawa na Mchungaji, kumekuwa na changamoto kwa watumishi wengi wa Mungu kuwa wa kiroho zaidi huku upande wa pili mke akiwa wa mwilini sana, matokeo yake wakati Mchungaji anashinda ofisini akiwa  na shughuli (busy) na maombi na huduma mama wachungaji wao wanabaki kuchati, na kupiga umbeya na kubadilishana mawazo na watu wasio faa, kufuatilia tamthilia, na kupeana ubuyu, hivyo kuleta tofauti kubwa  ya ukuaji wa kiroho kati ya mume na mke, wakati Adamu akiwa  anashughulika (busy) mahali Fulani, Eva alikuwa akichati na shetani na kushawishiana kula matunda aliyokataza Bwana kwa vyovyote vile kulikuwa na hitilafu Fulani wakati Eva alipokuwa anachati na shetani ni wazi kuwa Adamu huenda alikuwa mahali akichati na Bwana au kwenye huduma nyinginezo,wangelikuwa pamoja shetani angekimbia.

 

Mwanzo 3:1-4. “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,”

 

Elizabeth mama yake Yohana mbatizaji aliishi kwa haki na utauwa sawasawa na Mumewe Zekaria aliyekuwa kuhani maandiko yanawataja kuwa wote waliishi maisha ya utakatifu na ya haki, wote walishika maagizo ya Bwana na amri zake bila ya lawama je wewe mke wa Mchungaji na mumeo mnamcha Mungu kwa pamoja? Au ndio ile mmoja atwaliwa mmoja aachwa?

 

Luka 1:5-6 “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. NA WOTE WAWILI WALIKUWA WENYE HAKI MBELE ZA MUNGU, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.”

 

Mke na mume wanaweza kuishi maisha ya haki mbele za Mungu, lakini pia mke na mume wanaweza kila mtu kuishi anavyojisikia, unadhani Lutu alikuwa na mke wa namna gani? Wakati maandiko yanatueleza kuwa Lutu alikuwa mwenye haki, maandiko yanaonya kumkumbuka mkewe Lutu ambaye aligeuka nguzo ya chumvi kwa sababu aliishi maisha aliyoyataka mwenyewe

 

2Petro 2:6-7. “tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu;

 

Luka 17:28-36 “Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]

 

Unaweza kujiuliza ni kwanini mkewe Lutu aliachwa na maandiko yanamuhesabia Lutu kuwa alikuwa mwenye haki, Je mkewe hakuwa mwenye haki? Lutu alichukia ufisadi, je mkewe hakuchukia? Lutu alisema mpaka na wakwe zake lakini sikio la kufa halisikii dawa waliangamia katika moto ule na Lutu tu na wanawe walipona, mmoja atawaliwa mmoja aachwa, Familia za watumishi wa Mungu ni lazima wahakikishe wanaenda mbinguni wote                                            

Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kudhoofisha huduma

Wakati maandiko yakituonyesha wajibu wa mama mchungaji katika huduma ya kichungaji, maandiko pia hayaachi kutuonya na kutufundisha kuwa wako wanawake wa baadhi ya watumishi wa Mungu ambao walihusika kuleta aibu kubwa katika huduma za waume zao na kuwaletea usumbufu mkubwa na hata kuwafanya wawe na wakati mgumu katika shughuli zao za kimaongozi, sitaki kuamini kuwa tunaweza kuwa na wanawake wa jinsi hiyo leo lakini kama maandiko yanaonyesha kuwa walikuwepo hata leo wanaweza kuwepo wanawake wanaofanana na hao.

1.       Gomeri – Mama Mchungaji huyu aliolewa na Mchungaji Nabii Hosea lakini mama huyu alimkimbia mumewe ambaye alikuwa nabii na kwenda kujihusisha na wanaume wengine wengi, aliishi maisha ya kikimbizi na alimsababishia mumewe hasara kubwa ya fedha na kiuchumi, alijiuza kama kahaba, alisababisha madeni, alimsaliti Hosea kwa ujumla mwanamke huyu alikuwa mzinzi, Japo Hosea alimuonyesha upendo wa kweli, Lakini alimpa taabu sana Mumewe huyu, Maisha ya nabii yana mengi ya kutufundisha kuhusu uhusiano wa Israel na Mungu au kanisa na Mungu lakini leo tunajifunza kuwa Gomeri alikuwa ni mama Mchungaji lakini alikuwa Malaya na kahaba, mumewe ni nabii Mcha Mungu lakini mke anafanya mambo ya kikahaba, ni aibu sana kwa mtumishi wa Mungu kuwa na mwanamke wa aina hii, hata ingawa hatutiwi moyo kuvunja ndoa, lakini ni swala la kusikitisha kuwa leo wako mama wachungaji wanazini na wanatongoza na vijana wanajifanyia wanayotaka huku watumishi wakiwa aidha hawajui au wamemuachia Mungu, au nao wako busy na kazi ya Mungu, kila kitu kinahitaji kiasi naweza kuwafokea wachungaji lakini leo nimetumwa kusema na mama wachungaji, Mama Mchungaji aina ya Gomeri ni wengi sana nyakati za leo.

 

Hosea 1:2-3 “Hapo kwanza Bwana aliponena kwa kinywa cha Hosea, Bwana alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha Bwana. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume.”

 

2.       Mke wa Lutu – Alikuwa ni mke wa mtumishi wa Mungu Lutu, ambaye alihudumu katika miji ya dhambi ya Sodoma na Gomora, Lutu alikuwa mtu wa haki na anatajwa katika maandiko kuwa hakufurahia dhambi za Sodoma na aliumizwa na uchafu uliokuwa ukiendelea huko

 

2Petro 2:6-8 “tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria;”

               

Hata hivyo Pamoja na Lutu kuwa mtu wa haki jambo la kusikitisha ni kuwa walipoonywa waikimbie miji ya Sodoma na Gomora ili Mungu apate kuwaangamiza waovu, Yeye mke wa Lutu hakuwa miongoni mwa waliotii agizo hilo na hivyo aligeuka kuwa nguzo ya chumvi, Yeye aliachana na familia yake iliyokuwa imeokolewa na kuitamani familia ya kwao waliokuwa wakiishi maisha ya dhambi na hivyo aliangamia, Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana kama mume na watoto watakuwa wanamtii Mungu kisha akawepo ma Mchungaji ambaye yeye ni mkaidi kwa neno la Mungu huku akivutwa na dunia Yesu alionya sana kuwa na tujifunze kwa kumkumbuka mkewe Lutu

 

Luka 17:28-33 “Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya.”

 

3.       Delila – Alikuwa ni mama Mchungaji wa mchungaji mwenye nguvu nyingi sana za Mungu na upako mkubwa, lakini alisaliti kwa kukubaliana na maadui wa Samsoni akitoa siri ya asili ya nguvu zake, alijifanya kuwa anampenda sana lakini alijiunga na maadui wa Samsoni na kushiriki mpango mbaya wa kumuuza kwa sababu ya tamaa za kupata mali na ushawishi, hakujali usalama na ustawi wa mumewe, hakujali kuwa amechaguliwa na Mungu, hakuona umuhimu wa wito wa mumewe na badala yake alihatarisha mpango wa Mungu uliokuwa ukifanya kazi ndani ya Samsoni, yeye ni mfano wa mwanamke asiyejali usalama na ulinzi wa mumewe wala mpango wa Mungu juu ya mumewe hakuwa mwaminifu, alikuwa ni mwenye tamaa, alijichukulia maamuzi, alikula njama na kumuweka mumewe matatani, yeye ni mfano wa mama wachungaji wanaopoteza mwelekeo wa waume zao kihuduma na kuua huduma!

 

Waamuzi 16:18-21 “Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”        

 

4.       Mikali – Mikali Binti Sauli aliyekuwa mke wa Daudi Mchungaji wa Israel, Mchungaji alikuwa na moyo wa kupenda ibada alimpenda Mungu sana lakini Mikali alimdharau mumewe alipokuwa anajituma kuabudu, ni jambo la kusikitisha kuwa Mikali moyo wake haukuungana na mumewe katika ibada na badala yake alimsanifu mumewe na kuona kama mtu anayefanya mambo ya kipuuzi, mwanamke huyu kutokana na dharau iliyokuwa ndani yake na ya kutokumjali Mungu wala kujali ibada alipigwa na utasa siku zote za maisha yake.

 

2Samuel 6:16-23 “Ikawa, sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi, Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za Bwana; akamdharau moyoni mwake. Wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake. Ndipo Daudi akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na haya! Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za Bwana, aliyenichagua mimi juu ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa Bwana, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za Bwana. Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa. Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa na mtoto hata siku ya kufa kwake.”

 

5.       Yezebeli – alikuwa ni mwanamke aliyehusika sana kumpotosha mumewe Ahabu kwa kiwango kikubwa sana na kuharibu huduma ya Mumewe, alichangia kwa kiwango kikubwa sana ibada za sanamu, tamaa, kujipamba kulikopitiliza na kuelekeza familia nzima katika uovu, Yezebeli alijihusisha na ibada za sanamu na kueneza zinaa ya kimwili na kiroho, alikuwa ni mwanamke mpotoshaji aliyelelea manabii wengi wa uongo

 

1Wafalme 21:25-26 “(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)

 

Ufunuo 2:19-23 “Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.”

 

6.       Vashti – Anasimama kama mfano wa mama Mchungaji asiye na heshima na aliyekosa adabu na utii kwa mume wake, Mumewe alitoa amri kwa watumishi wake kwamba wamlete Vashti ili aweze kuwatambulisha watu wake mke wake (malkia) ambaye kimsingi alikuwa mzuri sana, Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida Vashti alikataa kuja kwa amri ya mfalme (Mchungaji) jambo ambalo lilimghadhibisha sana Ahasuero, Jambo hili lilipelekea mwanamke huyu kuachwa, sababu kubwa ni kuwa alikataa kumuheshimu mumewe tena mbele ya rafiki zake na watu maarufu waliokuwako, alishindwa kumstahi, alishindwa kumuheshimu, alishindwa kunyesha adabu, alishindwa kuonyesha utii, alionyesha mfano mbaya kwa taifa zima, wako mama wachungaji ambao ni mfano wa Vashti, hawana adabu kwa waume zao, hawataki kuonyesha heshima kwa waume zao hata wanapokuwa mbele za watu wengine au rafiki zake, wanawake wa jinsi hii wakati wote huwakosoa waume zao hata mbele za watu na kuwaaibisha unaweza kusikia mshaurini mwenzenu huyu, au hujifunzi kutoka kwa wenzako, anaweza hata kuwasifia wanaume wengine mbele ya mumewe au kugoma kukaa na waume zao au kuambatana nao sehemu wanakotakiwa kuwa pamoja, unaweza kushangaa kuona sehemu ambayo mchungaji alipaswa kuwepo na mkewe, mkewe hayupo na badala yake Mchungaji yuko peke yake, ni jambo baya sana kukosa hehima kwa mumeo na kumdhalilisha mbele za watu au kufanya mambo yatakayosababisha kutia aibu mbele za mume wako, kumvunjia heshima mumeo kwa hadhi yake ya kichungaji kunaweza kudhoofisha kabisa utumishi wake mbele ya jamii, Jambo alilolifanya Vashti lilikuwa ni mfano mbaya kwa nchi nzima na jamii nzima na kwa sababu hiyo wenye hekima walitoa ushauri asiitwe tena na kwa ujumla alikataliwa! Na umalkia wake alipewa mtu mwingine mwema kuliko yeye

 

Esta 1:5-21.“Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani ngomeni, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika behewa la bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawi, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu ya marumaru, mawe mekundu, na meupe, na ya manjano, na meusi. Wakawanywesha kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme; kunywa kulikuwa kama ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo. Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.”

 

7.       Mke wa Ayubu -  Ni mfano wa mama Mchungaji ambaye alisimama na mumewe wakati wote wa  mafanikio na wakati wa matukio mabaya, hata hivyo aidha kwa kujua au kwa kutokujua, kwa kuchoka au kwa kukosa uvumilivu alitoa ushauri mbaya kwa Mumewe kuwa kutokana na mateso anayoyapitia hana sababu ya kuendelea kushikamana na uadilifu wake ni afadhali amkufuru Mungu ili afe, Huu ni mfano wa mama mchungaji ambaye anaweza kutoa ushauri wa kukosa Imani, au kuangalia mambo mengine badala ya kumuangalia Mungu, wakati mwingine mtu anaweza hata akakushauri ugeukie maswala ya kishirikina ili uachane na uaminifu wako kwa Mungu huu uikuwa mojawapo ya ushauri ambao ayubu kwa msimamo wake aliuupuuzia  na kuuiona kama wa kipumbavu, kimsingi Ayubu alishangaa kuwa mkewe ameshindwa kujifunza hekima wakati wote wa kaisha yao ya pamoja na badala yake anazungumza ujinga kama wanawake wapumbavu tunajifunza kuwa wakati wa changamoto mdomo wa mama Mchungaji unaweza aidha kuleta msaada au kuleta uharibifu

 

Ayubu 2:7-10 “Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”

 

8.       Safira – Mke wa Anania ni wazi kuwa hakumshauri vema mumewe  na badala yake alikubaliana naye kwamba wadanganye kanisa na mitume kuwa wamefanya utoaji mkamilifu ilihali ziko fedha ambazo walikubaliana kuzificha walifikiri kuwa wanacheza mchezo wa kitoto kumbe walikuwa wanamdanganya Roho Mtakatifu kuhusiana na mali waliyokuwa wameuza matokeo yake waliacha watoto yatima kwa sababu Anania na mkewe walikufa kifo cha kimwili na kiroho kwa sababu walikubaliana kudanganya na yhakuna aliyekuwa na akili ya kumshauri mwenzi wake kuwa jambo hilo sio jema, kama mke wa mtumishi una haki ya kuuliza vema kama jambo hili linalofanyika ni halali au la na kumshauri mumeo kwa tahadhari na upendo ili aweze kufanya vema

 

Matendo 5:1-11 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya.”

               

9.       Eva – Mama Mchungaji wetu mkubwa kabisa kwa baba yetu Adam, alifanya makosa makubwa sana kwa kumsikiliza shetani kuliko kumsikiliza Mungu na mumewe, hakuamini kuwa yale aliyoyasema Mungu ndio yalikuwa ya kweli, hakuambatana na mumewe katika huduma, alibaki akichati na shetani  na matokeo yake alisababisha ugumu mkubwa sana katika huduma na maisha ya mumewe na kuleta mauti hata leo, na wakapotea kwenye uwepo wa Mungu Adamu alijaribu kujitetea sana na alitaka kujieleza kuwa ni mwanamke ndiye aliyesababisha Lakini hukumu ikawakuta na mabaya yakawapata wote wakaumia

 

Mwanzo 3:9-12 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”

 

Je wewe ni mama mchungaji wa aina gani? Huduma ya mume wako inatiwa nguvu? au anadhoofika kila iitwapo leo na wewe ukiwa ni sababu? Je unataka kuwa Baraka kwa kanisa la Mungu na mwili wa Kristo? au unataka kuwa laana na chanzo cha kukosesha?, andiko linatuonya kuwa Makwazo hayana budi kuja lakini ole wake yeye asababishaye, je unataka kuwa mama Mchungaji wa aina gani? Kusudi kubwa la somo hili ni wewe ujitambue na kuwa Baraka kubwa kwa huduma ya mumeo! Na usiwe mzigo na sababu ya uovu katika huduma

 

Luka 17:1-2 “Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.”

 

Mama Mchungaji anayechangia uharibifu katika huduma ya mumewe katika maandiko anafananishwa na mwanamke mpumbavu anayeiharibu nyumba yake kwa mikono yake miwili, je unataka kuwa ma Mchungaji wa namna gani mbele za Mungu atakayehukumu matendo ya kila mmoja? uwe na hekima jenga huduma yako mche Mungu. Muombe Mungu akupoe hekima yake kwani iko hekima ya Mungu na iko pia ya kibinadamu nay a shetani

 

Mithali 14:1 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.”

 

Yakobo 3:14-17 “N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima. Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”

 

Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma kusimama

Kila mama Mchungaji anaweza kuwa msaidizi mzuri sana wa mumewe katika huduma na kumsaidia Mchungaji kufanya vizuri, Mama Mchungaji unahusika na huduma na wajibu mzima wa kumtia moyo, kumuombea, kumsaidia, kutengeneza mazingira mazuri ya kiroho kwake ili aabudu, aandae neno, aombe, apumzike na maswala mengine mengi hapa kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya kusaidia huduma ya mume wako kusimama. 

1.       Maombi – Ma Mchungaji tenga muda wa kila wiki au kila siku kumuombea mumeo, kuombea huduma yake, kuombea jumbe zake, kumuombea ukuaji wake wa kiroho na kihuduma, unaweza kutengeneza mazingira ya kuomba naye na mengineyo, ziko nyumba za watumishi wengine wa Mungu mama anapiga bongo fleva na hakuna nyimbo za kwaya wala za kuabudu, nyumba inakuwa na kelele wakati wote Mchungaji akitaka kuomba ni mpaka aende porini nyumbani hakuombeki, hata kama ma Mchungaji anamuona mumewe anaandika jumbe au anahangaika kupata jumbe za kibiblia yeye na watoto ndio kwanza wako kwenye kelele, Nyumbani kwenu lazima kuwe na mazingira ya kiibada wakati wote muombee mumeo, Nyumba ya Mchungaji ni nyumba ya ibada, Nyumba ya mchungaji ni nyumba ya maombi, Nyumba ya Mchungaji ni ofisi ya dharula, Maombi yako yatamuinua sana Mchungaji na kurahisisha mambo kwenda.

 

Yakobo 5:16 “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”

 

2.       Tia moyo ukuaji wa kiroho – mtie moyo kujisomea Biblia, muulize maswali magumu ya kibiblia ili aweze kujibu kama anayefundisha, mnaweza kuwa na muda wa pamoja wa kujisomea Biblia

 

Mithali 27:17-18 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.”

 

3.       Mtie moyo kujihusisha na jamii – Mtie moyo kuandaa mazingira ya kuzifikia jamii, kujihusisha na matukio ya kihuduma, kujiunga na jamii inapokuwa na huzuni au furaha, mpe taarifa mbalimbali, mpigishe stori, jiunge naye katika shughuli mbalimbali mtie moyo kutumika kwa nguvu, epuka kumlinganisha na watu wengine acha mumeo awe nuru, usimfungie ndani, mchekeshe na mkande kande anapokuwa amechoka.

 

Mathayo 5:14-16 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

 

4.       Mpende na kumuheshimu mumeo – Moja ya wajibu mkubwa na wa msingi wa mama Mchungaji ni pamoja na kumpenda, kumlinda, kumuheshimu, kumtii na kumsaidia mumeo, mama wachungaji wana wajibu wa kuwatosheleza waume zao pia katika tendo takatifu la ndoa kesi nyingi wanazopokea watumishi wa Mungu makanisani ni pamoja na kuweko wanandoa ambao hawawajibiki kutoshelezana katika tendo la Ndoa kwa msingi huo itakuwa ni fedheha na aibu kubwa kama Mama Mchungaji ambaye anatakiwa kumsaidia mumewe kusimama imara katika huduma na utumishi kwa Mungu kisha yeye akawa mfano mbaya kwa kina mama wa kanisani kwa kushindwa kuwajibika ipaswavyo wao ndio wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwafundisha wanawake vijana wajibu wao, mama wachungaji wengi wamesababisha neno la Mungu kutukanwa kwa sababu badala ya kuwa rafiki wa waume zao wamekuwa ndio maadui wakubwa wa waume zao, na kushindwa kuwatimizia ulio wajibu wao, kufanya hivyo ni kumpa ibilisi nafasi

 

Tito 2:3-5 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

 

Waefeso 2:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.”

 

5.       Zijue fikra za Shetani – 2Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.       

 

Ni muhimu kufahamu kuwa shetani anapokuwa ameshindwa kusambaratisha huduma ya Mchungaji njia pekee na rahisi anayoweza kuitumia ni kupitia mama Mchungaji kama tu jinsi alivyopitia wanawake mbalimbali katika maandiko kuwa sababu ya anguko kubwa la waume zao na hata huduma, mwanamke asiye na akili hataelewa mbinu anazozitumia shetani, shetani atafanya mambo kadhaa ili kuua huduma, na kukumaliza na wewe, Mchungaji akipata changamoto za kihuduma wewe mama Mchungaji na familia yako pia mtaathirika hivyo usikubali kumpa shetani nafasi ya kuharibu jambo la kiungu ndani yako!

 

a.       Atachoma sindano ya migogoro ya ndoa anajua wazi kuwa kwa kupandikiza migogoro, ugomvi, kutokuelewana kiburi na ubishi kikipandwa kati ya Mchungaji na mkewe huduma itakosa Amani na moyo wa mchungaji utakosa Amani na kuchoka na maombi na dua zenu zitazuiliwa na mfumo wa ibada utaharibika  

 

1Petro 3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.

 

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”              

 

b.      Uchonganishi na washirika – Ma mchungaji anapaswa kuwa makini asitumike kama chombo cha kupanda chuki, fitina na maneno maneno ya uchonganishi kati ya mchungaji na washirika, shetani anaweza kutumia udhaifu wa kibinadamu kukufanya wewe uwe chombo cha kupeleka taarifa hata zisizo rasmi nakukuharibieni huduma

 

Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”

 

c.       Moyo wa utawala – Shetani anaweza kumuingia mama mchungaji kisha yeye akataka kuwa ndiye mdhibiti wa kila jambo na kila kitu kinachoendelea kanisani kiasi cha kufikia hatua ya kupingana na mume wake na kuleta mkanganyiko, washirika hasa wanawake wanachukizwa sana wanapoona mama mchungaji ni kama anadhibiti kila kitu au anakuwa na sauti kubwa kanisani na dhidi ya mumewe, ni vema kuwa na moyo wa unyenyekevu kama pambo kwako

 

Ufunuo 2:20 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.”

 

Mwanzo 3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”

 

Yezebeli alikuwa ni mwanamke mwenye ushawishi aliyemsukuma mumewe na watu katika dhambi, Tamaa yako itakuwa kwa mumeo ni tamaa ya utawala ambayo wanawake watajaribiwa kuwa nayo, Mama mchungaji mwenye hekima atatumika kwa unyenyekevu mkubwa na hataweza kuwa sababu na chanzo cha dhambi kwa mumewe kwa kupunguza maombi, ibada na au kumsukuma mchungaji kwenye maamuzi mabaya

 

d.    Moyo wa kuangalia nyuma -  Mama mchungaji anapaswa kukumbuka agano la ndoa na kuhakikisha kuwa anaambatana na mumewe, Neno la Mungu limeeleza kuwa mtu atamwacha babaye na mamaye ataambatana na mkewe/mumewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja, kwa bahati mbaya wako mama wachungaji ambao moyo wao hauko tayari kuambatana na mumewe na kila siku au kila mara na kila wakati moyo wake uko kwao, urafiki mkubwa hauko kwenye huduma wala kwa mumewe lakini uko kwa wazazi wao, kuwatunza na kuwajali na kuwaheshimu wazazi ni swala linaloungwa mkono kimaandiko lakini kukosa kiasi katika swala hili ni dhambi, wazazi wenye akili watamtima moyo mke wa Mchungaji na kumtaka aambatane na mumewe kwa sababu jukumu alilo nalo ni la tofauti na watu wengine kaa na mumeo wazazi msiwatenganishe wana ndoa, kama unaona kwenu ndio kwa maana zaidi kuliko huduma na ndoa yako ujue utasababisha ajali za kihuduma kwa mumeo acha kukimbia majukumu yako, kaa na mumeo mume wa agano lako mtumikieni Mungu.  

 

Mathayo 19:4-6 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”

 

Moja ya sababu ya mke wa Lutu kugeuka nyuma ni pamoja na ile hali ya kutokutaka kuambatana na mumewe na badala yake aliwaangalia wazazi wake ambao kimsingi wala hawakuwa wanamcha Mungu bali walikuwa raia wa kawaida wa Sodoma ambao walikataa ofa ya wokovu

 

Mwanzo 19:12-26 “Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametupeleka tupaharibu. Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze. Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji.Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu! Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo BWANA akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile.Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.”

 

Swala la kumfuata mume halina tofauti kabisa na swala la kumfuata Yesu, mke wa Mchungaji ni lazima amuwaze mumewe na kumjali kuliko baba yake na  mama yake na nchi yake na huko alikotoka, mke wa Mchungaji Lutu pamoja na neema kubwa aliyopewa yeye aliwaangalia ndugu zake ambao wao walikataa neema na wala hawakuwa wanajali mambo ya Mungu na hivyo aliangamia, kila mama mchungaji anapaswa kujiatafakari kwa upya anajitoa wapi na kwa kiwango gani, na wazazi ambao binti yenu anakuwa mama mchungaji basi mwacheni aende kwa mumewe na aungane na mumewe wamtumikie Mungu hivi mnadhani Ruthu hakuwa na wazazi na ndugu? Alipoamua kuambatana na Naomi?

 

Ruthu 1:16-18 “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”

 

Luka 14:26-27 “Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”

 

Kila mama Mchungaji akumbuke kuwa kumfuata mume ni sawa na kumfuata Yesu, kama unapenda sana kwenu hufai kuwa mke wa Mchungaji, wako mama wachungaji wengine huwaacha waume zao na ma - house girl au peke yao wakiwa wanataabika na njaa kisha wao huenda kufurahia maisha ya huko kwao alikotoka, kufanya hivyo ni kumpa ibilisi nafasi, kama ukipewa nafasi ya kuona yanayotokea huko nyuma ukiwa haupo nadhani ungecha mara moja kutoka na kumuacha Mchungaji akitaabika peke yake wewe ukiinjoy kwenu.

 

Waefeso 5:22-24 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.”

Kila Mama Mchungaji akumbuke kuwa ana nafasi muhimu sana ikiwa atakuwa na busara na hekima ya kiungu atakuwa Baraka kwa Mchungaji na Kanisa, lakini akiwa vinginevyo anaweza kuwa sababu ya migogoro na mafarakano, dharau na kudhoofisha kazi ya Mungu na kupoteza heshima yake binafsi ni imani yangu ya kuwa kila mama mchungaji atakayesimama katika zamu yake kwa uaminifu na kujitoa kwa kadiri ya neema ambayo Mungu amewapa na mumeo katika huduma kazi yako haitakuja iwe bure kwani imeandikwa ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii atatapata thawabu ya nabii Mungu atawabariki sana mama wachungaji watakaosimama katika zamu zao kuinua huduma ya kichungaji bila shaka mama wachungaji watakaozingatia haya watakuwa na kiti chao mbinguni. Maandiko pia yameahidi kuwa watang’aa kama mwangaza wa jua wale waongozao wengi kutenda haki, na mama mchungaji ana nafsi kubwa katika kuongoza wengi kutenda mema

Daniel 12:3 “Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.”

Mathayo 10:40-42 “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”   

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumapili, 8 Juni 2025

Maana Mungu hakutupa roho ya woga !


2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”



Utangulizi

Nyakati za Kanisa la kwanza kuwa mkristo na kuwa muhubiri wa injili maana yake ilikuwa ni pamoja na kukabiliana na mateso, maumivu, kukataliwa, kutishiwa, kuonewa, kukandamizwa na hata kuuawa, Wakristo wengi waliotawanyika duniani wakati ule waliuawa na kuteswa kwa kutupwa gerezani, kutupwa katika matundu ya simba, kuchomwa moto na kupingwa vikali kwaajili ya wokovu, kwa sababu hiyo wakristo wengi na watumishi wengi wa Mungu waliingiwa na hofu au woga, na kwa sababu hiyo maendeleo yao ya kiroho na kihuduma yalikumbwa na vikwazo kwa sababu waliingiwa na shaka na hivyo kuogopa kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwaajili ya haya wakristo wengi waliingiwa na hofu na walihitaji kutiwa moyo kujua tuko katika njia ya dhiki nyingi

Matendo 14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”

Ni katika hali kama hii Paulo mtume akiwa gerezani huko Rumi akiwa mfungwa aliyehukumiwa kama muhalifu kwaajili ya injili anaandika waraka huu kwa kusudi la kumtia moyo Mtumishi wa Mungu Timotheo ambaye kwaasili alikuwa mwoga, akimkumbusha kuwa Mungu hakutupa Roho ya woga, bali ya nguvu na upendo na moyo wa kiasi, Timotheo ni kama sisi tulivyo leo, Tunahitaji kujikumbusha kuwa Tunaye Roho wa Mungu ndani yetu ambaye anatupa nguvu katika wakati wa mahitaji yetu, bila kujali kuwa tunakutana na magumu kiasi gani, au tuko hatarini kiasi gani, tunauwezo wa kukabiliana na hali yoyote ile inayotishia maisha yetu bila kuogopa kwa sababu Roho Mtakatifu yuko juu yetu na hivyo Hatuogopi! Kwa msingi huo basi Leo wakati huu wa juma la Pentekoste tutachukua Muda kujikumbusha tena na tena umuhimu wa Roho Mtakattifu katika kutupatia ujasiri unaotusaidia kusonga mbele bila kujali kuwa ni vikwazo gani tunakutana navyo katika maisha yetu ya Ukristo katika jina la Yesu, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Mungu hakutupa roho ya woga!

·         Roho Mtakatifu ni roho wa ujasiri

·         Jinsi ya kutupilia mbali woga.

Mungu hakutupa roho ya woga!

Moja ya adui mkubwa sana wa watu waliookoka ukimuacha shetani ni woga, kwa kweli woga ni mtego mkubwa sana unaopunguza uwezo wetu wa kutenda mambo makuu pamoja na Bwana, Maendeleo yetu ya kimwili na kiroho na hata kisaikolojia yanaweza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa sana na woga, wako watu wanaogopa hata kuanza biashara, wako watu hawaoi kwa sababu wanaogopa wataoaje, wako watu hawafanikiwi kwa sababu wanaogopa kuingia gharama na kujitosa katika kufanya majaribio, woga unaleta mashaka, woga unaleta kutokujiamini, woga ni mtego unaotuzuia kufikia ndoto zetu na kuona ahadi za Mungu zikitimia katika maisha yetu, woga hutuletea kukata tamaa, woga unaweza kuchelewesha kwa kiwango kikubwa maendeleo yetu! Wana wa Israel walishindwa kuirithi inchi ya ahadi mapema kwa sababu zilizochangiwa na woga!

Hesabu 13:25-33 “Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”     

Hesabu 14:1-3 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

Woga uliwachelewesha wana wa Israel kuirithi inchi ya Kanaani kwa miaka 40,  woga ni adui mkubwa wa Imani, unapokuwa na woga ni sawa kabisa na kukosa Imani, na unapokosa Imani ni vigumu kabisa kumpendeza Mungu, huwezi kamwe kuzifurahia ahadi za Mungu na kuziona kwa uhalisi katika maisha yako, woga unaua maono, woga unachelewesha ndoto zako kutimia, Paulo mtume alifahamu kuwa kama Timotheo ataruhusu woga, kufungwa na kutiwa gerezani hata kuuawa kwaajili ya Kristo, atakuwa kikwazo kikubwa kwa injili kwake na kwa wale anaowaongoza kwa hiyo alimkumbusha kuwa Mungu hakutupa Roho ya woga, hii pia inatukumbusha na sisi leo kuwa hatukupewa Roho ya woga kwa jambo lolote lile linalotukabili, kwa kuwa Roho Mtakatifu sio Roho wa woga yeye atatupa ujasiri kuendelea mbele na injili na kusonga mbele hata kama tunakutana na magumu na vipingamizi na vitisho na hofu kamwe hatupaswi kuogopa na tusonge mbele kwa sababu hatujapewa roho ya woga

2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”

Neno woga linalotumika katika kifungu hiki, linasomeka kama “Deilia” katika lugha ya kiyunani likiwa na tafasiri ya fear au timidity ambalo tafasiri yake ni kukosa ujasiri, au kutikujiamini, au kuwa na aibu, kutishika na kuingia hofu hasa unapojilinganisha na kile unachokabiliana nacho ni kwaajili ya woga Israel walishindwa kumkabili Goliathi hata alipkuwa akiwatukana

1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.nBasi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Roho Mtakatifu ni roho wa ujasiri

Moja ya kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ndani ya mwamini, ni pamoja na kutuumbia Roho ya ujasiri, kila mwanadamu ndani yake kuna aina Fulani ya hofu au woga, tunaogopa kukosea, tunaogopa kushindwa, tunaogopa majaribio, tunaogopa kuchekwa, tunaogopa watu, lakini pia tunaogopa magonjwa, tunaogopa njaa, tunaogopa mateso na kadhalika, Lakini Roho Mtakatifu hutujengea ujasiri usiokuwa kawaida wa kuwa tayari hata kuwa mashahidi (kufa) wa Yesu Kristo kwaajili ya injili

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.

Warumi 8:15-18 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”

Roho wa Mungu ndani yetu hutupa ujasiri wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu bila kujali vikwazo vya aina yoyote tunavyokutana navyo, anatufanya tushuhudiwe ndani yetu kuwa sisi ni wana wa Mungu na kuwa hatuna kitu cha kupoteza, ndani yetu, Paulo anaona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kama ule utukufu utakaofunuliwa kwetu, kwa sababu hiyo hatuogopi wala hatupaswi kuogopa kwa sababu ndani yetu uko ujasiri kuwa sisi sio watu wa kawaida, tu wana wa Mungu na kama Yesu alivyo ndivyo tulivyo, na kama ikiwa sisi tuko kama Yesu je unaogopa nini hapa duniani?             

1Yohana 4:17-19 “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI HUMU. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.”

Tukijitambua kuwa sisi ni nani katika Kristo na kuwa hatukupewa Roho wa woga bali  ya nguvu na ya upendo, nay a kiasi hatutaogoa lolote hata ijapotetemeka nchi, ijapobadilika milima, vijapotikisa vilindi vya bahari bado hatutaogopa Roho Mtakatifu atatukumbusha kumtegemea Mungu, atatukumbusha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu msaada uonekanao tele wakati wa mateso, na sio hivyo tu anatukumbusha kuwa sisi ni wana wa Mungu na kuwa hatuna cha kupoteza duniani, hatutaweza kupoteza ujasiri kamwe ikiwa tu Roho Mtakatifu atapewa nafasi kubwa ndani yetu, Roho wa Mungu hutupilia mbali hofu na kutusaidia kukabiliana na hali yoyote ile inayotakiwa kukabiliwa ndani yetu! Na nje yetu mbele yetu na nyuma yetu!

Matendo 21:10-13 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.”          

Jinsi ya kutupilia mbali woga.

Ni muhimu kufahamu kuwa wewe sio matokeo ya mazingira wala sio matokeo ya kile watu wanachokisema wewe ni matokeo ya kile Mungu anachokisema kukuhusu, kwa msingi huo ili kutupilia mbali hofu na woga katika maisha yetu ya kila siku hatuna budi kujitazama kwa kulitazama neno la Mungu linavyosema kutuhusu  Neno la Mungu linasema:-

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.

Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.”

Yoshua 1:9 “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

Neno la Mungu linatueleza kuwa hatupaswi kuogopa wala hatupaswi kuwa na visingizio wala sababu za kibinadamu, hakuna sababu zozote za kibinadamu zinazoweza kuhalalisha sisi kutokutumiwa na Mungu kwa sababu zozote zile, wala hakuna maumbile yoyote ya kibinadamu yanayoweza kuhalalisha Mungu kuto kutimiza kusudi lake ndani yetu kwa sababu hiyo hakuna kisingizio huusani pale Mungu anapotutia Muhuri kwa Roho wake mtakatifu!

Ni kwa sababu hiyo Paulo mtume alikuwa akimtia moyo Timotheo kuweka mbali hofu na aibu ili kumshuhudia Yesu Kristo kwa ujasiri, Kila mkristo anapaswa kujiandaa na kuwa tayari kukabiliana na aina yoyote ya mateso, kukabuliana na vita vya kiroho na kufungwa nahata kuuawa, au kupigwa na changamoto nyinginezo zote kwaajili ya injili haya yote yanawezekana ikiwa tutamruhusu Roho Mtakatifu ambaye ni Roho ya ujasiri na nguvu kutawala maisha yetu na hisia zetu.

Kila mmoja wetu anamuhitaji Roho Mtakatifu katika wakati huu wa sasa ili atupe ujasiri tusione haya wala tusiogope kumshuhudia yeye kwa ujasiri hata kama kuna hatari zinayakabili maisha yetu ni nguvu za Roho Mtakatifu peke yake zinazoweza kutusaidia na kutubeba kwa neema kuendelea kuwa na nguvu hata wakati ambapo tunakabiliwa na magumu kwaajili ya injili, na kwaajili ya maisha ya kawaida Roho Mtakatifu hutusaidia kuwa imara na kutokuogopa kikwazo chochote kinachosimama mbele yetu kwani kila kitu kinawezekana alipo yeye na sio kwa akili zetu na nguvu zetu, kwa hiyo kumbuka kuwa woga na hofu sio sehemu ya maisha yetu, woga na hofu si sehemu ya mtu aliyejaa nguvu za Roho Mtakatifu badakla yake akija juu yetu hofu zote na woga wa jambo lolote hutupiliwa mbali kabisa, leo hii tunapoadhimisha sikuu ya Pentekoste kumbuka kuwa Mungu hakutupa roho ya woga! , Mwamini Mungu, kabiliana na lolote lile linalokuja mbele yako, kabiliana na lolote lile kabiliana na kila changamoto na matisho, na mateso, na uhdia, na adha, na lolote lile linaloonejkana kuwa kama kwazo au kuwa kama mlima mbele yako jua ya kuwa kwa Roho wa Bwana litasambaratishwa na kuwa tambarare na makusudi ya Bwana yatatimizwa maishani mwako!

Zekaria 4:6-7 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima! 

Jumatano, 4 Juni 2025

Kwa hiyo hatulegei!

 

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika dunia hii iliyojaa changamoto, maumivu, majaribu, mateso, uonevu, dhuluma, kukosekana kwa haki, wivu, majungu na kuumizana, maneno ya kuumiza, na vita vya kila aina ni rahisi sana kwa baadhi ya watu hususani wale walio na moyo wa unyonge kulegea na kukata tamaa, na wakati huohuo kupoteza tumaini kwa sababu ya kuwako kwa vikwazo mbalimbali katika maisha, Paulo mtume yeye anasema na kutangaza kwa ujasiri “Kwa hiyo Hatulegei” ujumbe wake Paulo mtume kwa kanisa ni ujumbe wa matumaini na ushindi na nguvu kwa kila anayemwamini Yesu Kristo Bwana wetu, kwamba sisi ni watu wa tofauti na kamwe hakuna awaye yote aliyemwamini Yesu anayeweza kukata tamaa, au kuzimia moyo “Kwa hiyo hatulegei” tunaendelea kukaza mwendo kwa kadiri tunavyokutana na changamoto na majaribu ya namna mbalimbali.

Wafilipi 3:12-14. “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

Leo basi tutachukua muda kujifunza sababu zilizopelekea Paulo mtume kuelezea “Kwa hiyo Hatulegei” na tutajifunza ujumbe huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo yafuatayo:-

·         Maana ya kutokulegea.

·         Sababu za kutokulegea.

·         Kwa hiyo hatulegei.

Maana ya kutokulegea:

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana

Neno kwa hiyo hatulegei katika Biblia ya kiyunani linasomeka “dio ekkakeō ou”  kwa hiyo neno hatulegei kwa kiyunani ni “ekkakeō”  ambalo kwa kiingereza linaweza kutafasirika to become weak, to fail, to faint, to become weary, or to fail in heart, or we do not give up. kwa hiyo kwa Kiswahili maana yake hatuwi dhaifu, hatushindwi, hatuzimii, hatuchoki, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo.

Maana yake hata pamoja na magumu kiasi gani tunayokutana nayo, hata pamoja na dhiki kubwa tunayokutana nayo, hata pamoja na changamoto kubwa tunazokutana nazo, hata pamoja na vipingamizi vikubwa tunavyokutana navyo iwe ni katika imani, iwe ni katika huduma, iwe ni ugumu katika jambo lolote unalokutana nalo, vyovyote vile visisitishe huduma yako, wokovu wako, ndoa yako biashara yako, juhudi zako katika masomo, uwezo wako wa kumtumainia na kumtegemea Mungu, utumishi wako, juhudi yako ya kupambana na umasikini, jitihada zako za kujikwamua, mpango wako wa biashara, mpango wako wa kilimo, mpango wako wa uwekezaji, mpango wako wa ufugaji, mpango wako wa maendeleo, na msimamo wako katika Bwana haupaswi kuzimia kwa sababu zozote zile kwa sababu ya ujuzi wako na maarifa yako ya kina kuhusu Mungu na kazi yake anayoifanya ndani yako! Kamwe Mungu hawezi kukuangusha! Kwa hiyo hatulegei

Hakuna jambo baya sana kama kuzimia, kukata tamaa, kuvunjika moyo, kuchoka, au kuwa dhaifu, adui mkubwa sana wa mwanaridha yoyote yule ni pamoja na kuzimia, au kulegea, kuvunjika moyo, kuogopa, wasiwasi na mashaka, na kufikiri kuwa umezidiwa, wakati wowote mwanadamu anapokata tamaa anazuia maendeleo yake, anatengeneza ugumu wa kushinda vikwazo na kutokusonga mbele mtu awaye yote aliyeokoka hapaswi kamwe kulegea, kulegea na kukata tamaa na kuzimia moyo kunaashiria kuwa uweza wako na nguvu zako ni chache, Jeshi lolote lile halina haja na Askari ambaye anazimia moyo au kukata tamaa.  Mithali 24:10 “Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.”

Kulegea kunafananishwa na mwanamke aliyebeba mimba kwa miezi tisa akipitia shida na taabu mbalimbali kisha akaanza kusikia uchungu alafu muda wa kujifungua unafika wakati anataka kujifungua mwanamke huyu anachoka kusaidia kumsukuma mtoto ili atoke huo unakuwa wakati mgumu sana, unakuwa ni wakati wa dhiki, unakuwa ni wakati wa aibu, kuwa mwanamke huyu amebeba mimba lakini ameshindwa kuzaa, mwanamke huyu atashutumiwa kuwa alipoteza ujasiri na nguvu wakati wa kujifungua, kwa hiyo ni lazima Mwanamke asukume zaidi ili aweze kujifungua kama hakuna nguvu ya kuweza kujifungua maana yake hakuna nguvu ya kushinda kwa hiyo kushindwa kunakuja, aibu inakuja, fedheha inakuja, na jambo gumu zaidi linakabili:-

Isaya 37:1-3. “Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.”

Kwa hiyo kulegea maana yake ni kuzimia, ni kukaribia kushindwa ni kukosa msaada, ni kuchoka, ni kupoteza nguvu ni uwezekano mdogo wa kushinda vikwazo na changamoto mbalimbali zinazokukabili, kwa hiyo watu wa Mungu au watu waliookoka hawalegei, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo, wala hatusitishi juhudi wakati wa mambo magumu tunasonga mbele kama askari wema na waaminifu walioko vitani na ziko sababu kadhaa za kutufanya tusilegee!

Sababu za kutokulegea.

1.       Kwa sababu tunaongezewa neema – Mst 15

 

2Wakorintho 4:15 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.”

 

Mtu wa Mungu anapopita katika changamoto za aina mbalimbali kwa kadiri ya  mateso na majaribu yanavyozidi Mungu aliyemfufua Bwana Yesu anatuongezea neema ya kupita kawaida ya kutusaidia kushinda majaribu, kwa hiyo ndani yetu moyo wa kukata tamaa unabomolewa na Neema inazidi na kutuinua juu zaidi, tunapewa neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

 

Yakobo 4:5-6 “Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

 

Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

2Wakorintho 12:8-10 “Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

 

2.       Kwa sababu mtu wa ndani hachakai        Mst 16

 

2Wakorintho 4:16 “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.”

 

Paulo mtume anasema hatulegei wala hatuishiwi nguvu wala kukata tamaa kwa sababu utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku, wakati kila mkristo anapokutana na majaribu na mateso na machungu ya aina mbalimbali utu wetu wa ndani unapata uzoefu na mabadiliko na ukuaji wa kiroho, kwa hiyo hata kama kwa nje tunaonekana kuchoka, kuugua na kuchakaa utu wetu wa ndani unafanywa upya na kuimarishwa katika imani kupitia uhusiano wetu na Mungu, Imani, maombi, neno la Mungu na uzoefu wa kiroho tunaoupata kila iitwapo leo, wakati wa majaribu unachangia kwamba akili zetu zinakuwa, ujuzi wetu unaongezeka, tunazidi kumjifunza Mungu kutoka katika pito moja kuelekea katika pito lingine  na kama ni hivyo sasa kukatatamaa kunatokea wapi, kuchoka kunatokea wapi, kupoteza nguvu kunatokea wapi, unafungwa gerezani, magereza inaachia, unapigwa mawe mpaka kufa unafufuliwa na unaendelea na injili, unapigwa bakora na kuteseka unazidi kuongezewa neema, unaviziwa getini unashushwa kwenye kikapu na injili inaendelea, utachokaje kwa mfano  unapata ujuzi unapata hekima unajengewa ujasiri na unagundua kuwa hakuna kitu kinaweza kukutenga na wewe na upendo wa Mungu

 

Warumi 8: 38-39 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

3.        Kwa sababu mateso ya sasa ni mepesi na ya muda tu. Mst 17

 

2Wakorintho 4:17 “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;”      

 

Paulo mtume anayaona mateso ya sasa na dhiki hizi ni nyepesi na za muda tu na kuwa dhiki hizi zinatutengenezea utukufu mkubwa sana na wa milele, watu waliookoka ni askari, askari ili awe na utukufu mkubwa na cheo kikubwa sana lazima akasotee katika chuo cha maafisa wa kijeshi ili kuongezewa nyota begani mwake, wakati wote dhiki huwa zinatujaribu na kutukomaza kupata ujuzi wa kiroho na kutufanya tuwe imara zaidi kwa sababu hiyo hatulegei tunapata uzoefu kutoka kwa dubu na simba ili kumpiga Goliathi.

 

Ayubu 23:10-12 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,”

 

1Petro 1: 6-7 “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

 

Paulo mtume alikuwa anaangalia hitimisho kubwa lenye utukufu mwingi baada ya dhiki hizi za muda mfupi, Kule mbinguni Mungu atamtukuza kila mmoja kwa kadiri ya neema na mapito aliyoyavumilia kwa sababu hiyo hatupaswi kuangalia hivi vinavyoonekana ambavyo ni vya muda mfupi bali tuviangalie vile vya milele, mateso na dhiki na maumivu ni vitu vinavyoonekana lakini thawabu na utukufu mkuu Mungu aliotuwekea ni kitu kisichoonekana kwa sasa lakini katika uzima wa milele kuna mambo makubwa yanakuja mbele yetu.

 

2Wakorintho 4:18 “tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.”

 

4.       Kwa sababu huduma hii tumeipata kwa rehema Mst 1

 

2Wakorintho 4:1 “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei;”

 

Mungu aliyetuita katika wokovu na kisha kutupa wito wa kumtumikia ametuheshimu sana ni rehema kwa wewe na mimi kufanywa watumishi wa Mungu, angeweza kumtumia mwingine au hata kuwatumia malaika ambao ni wajumbe wake, lakini kwa rehema kubwa ametupa sisi huduma hii  tunawezaje kulegea? Tunawezaje kukata tamaa, Mungu ametukabidhi sisi kazi ya kuieneza injili ametupenda ametuhurumia ametuheshimisha tupeleke ujumbe wa Mwanae kwa watu wote, huduma hii ni ya rehema tu si kwa saababu tunastahili kwa hiyo kwa vipi tukate tamaa, kwa vipi tuzimie, kwanini tulegee?  Kama ni Mungu ameturehemu tumtumikie ni yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa chanzo cha nguvu zetu , kwa sababu hiyo ni lazima tushinde vizuizi vyote na changamoto zote na kamwe tusizimie moyo, kazi yetu ni kazi njema na ni kazi ya Mungu kwa hiyo tusizimie, Yeye aliyetutuma ana mamlaka yote Mbinguni na duniani kwa sababu hiyo hatupaswi kamwe kuogopa!

 

Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”         

 

Kwa hiyo hatulegei.

Ni muhimu maneno haya yakawa kauli mbiu katika utumishi wetu na maisha yetu ya wokovu, kila wakati unapohisi kuchoka au kuvunjwa moyo ni lazima tukiri kuwa Hatulegei, hatuzimii moyo hatuanguki, tunasonga mbele, kutokulegea kwetu ni ishara ya kuwa tunamjua Mungu kwa kina na mapana na marefu, na tunamwamini, Paulo alipokuwa anasema kuwa hatulegei yeye alikuwa anajua hakunamtu aliyepitia mateso kama yeye lakini hakuwahi kulegea hata siku moja.

2Wakorintho 11:23-33 “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?  Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.”

Mungu hatatuacha katika mapito ya aina yoyote ile aliahidi kuwa atakuwa pamoja nasi na kwa sababu hiyo atatutia nguvu kwa hiyo hata kama tunazingirwa na mazingira magumu kiasi gani hatutaangamia, wala hatutakata tamaa, kila jaribu linao mlango wa kutokea.

2Wakorintho 4:6-10 “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo. Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.”

Kwa hiyo Hatulegei.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatano, 28 Mei 2025

Mleteni huku kwangu!


Mathayo 17:14-21 “Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]




Utangulizi:

Katika kifungu chetu cha msingi wa maandiko leo, tunakutana na kisa chenye kushangaza sana ambapo wanafunzi wa Yesu walishindwa kumsaidia kijana aliyekuwa anateswa na pepo wa kifafa, Baba wa kijana alileta mashitaka hayo kwa Yesu kwamba kijana wake amekuwa akisumbuliwa na pepo hao wa kifafa ambao wakati mwingine wamemtupa kijana wake katika maji na katika moto, na alipomleta kwa wanafunzi wake wao walishindwa kumtoa, Ndipo Yesu kwa uchungu mkubwa alitoa agizo lenye uzito “Mleteni huku Kwangu” agizo hili sio agizo la kawaida ni mamlaka ya kiroho yenye maana pana kwa kila mtu anayetafuta msaada wa kweli.

Mleteni Kwangu!

Ni muhimu kufahamu kuwa ni swala la kawaida kwamba kila mwanadamu anapopatwa na shida au changamoto zozote zile zikiwepo changamoto za kiafya huwa anatafuta msaada, na wakati mwingine wanadamu huwa na tabia ya kupeana taarifa wapi pa kwenda ili changamoto zako ziweze kutatuliwa, Baba wa kijana huyu anaonekana wazi kukosa Amani kwaajili ya afya ya mtoto wake ambaye alikuwa anasumbuliwa na Pepo wa kifafa, na huenda alihangaika sehemu nyingi sana kwaajili ya kujaribu kutatua hali ya kiafya iliyokuwa ikimkabili kijana wake, hatimaye huenda alisikia habari za Yesu, lakini wakati huu Yesu alikuwa mlimani pamoja na Petro na Yakobo na Yohana wanafunzi wengine walibaki, Mzee huyu aliwakabidhi wanafunzi wa Yesu changamoto za mwanae na wanafunzi walishindwa kushughulika nayo, Yesu alipofika baba wa kijana alitoa taarifa kwa Yesu na ndipo Yesu alipotoa amri “Mleteni huku kwangu

Kwanini aletwe kwa Yesu?

Watu wengi sana wanapopatwa na changamoto za namna mbalimbali kwa kawaida huwa hawampi Yesu nafasi ya Kwanza, na badala yake huanza kutumia akili zao za kawaida na za kibinadamu katika kutatua changamoto zinazowakabili na Yesu huwa anapewa nafasi ya mwisho, hii sio tu kwa wanadamu wa siku za leo, bali hata wakati Bwana Yesu alipokuwa duniani bado wako watu waliokuwa na changamoto mbalimbali walianza kupeleka changamoto zao kwa matabibu mbalimbali na kuingia gharama kubwa

Marko 5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake;maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule

Inawezekana umekuwa ukipitia changamoto za aina mbalimbali kama mwanadamu katika maisha yako ya kawaida, ni desturi na jambo la kawaida sana wanadamu kuomba ushauri kwa wanadamu wenzao na kuelezewa kuwa wajaribu hiki au kile, nenda hospitali hii au ile kamuone mwanasaikolojia huyu au yule, kamuone daktari huyu au yule, nenda kwa mganga huyu au yule, changamoto yako hii yuko mama mmoja huyo ni kiboko, changamoto yako hii inangekuwa kule Sumbawanga ingeshughulikiwa, tatizo lako hili lingekuwa kule Kwamsisi ni jambo dogo tu, changamoto yako hii ingekuwa kule Lamu - Mombasa sharifu angekusomea, hili tatizo lingepelekwa kule Korogwe kwa Semangube lingekuwa kama chai tu, hii kitu kuna wazee kule Kigombe Muheza inaisha na kadhalika na kadhalik wanadamu wanaweza kukupa ushauri wa kupeleka matatizo yako huku na kule na ukasumbuka sana kwaajili ya kutafuta uzima, na ikakugharimu sana, Mzee huyu ambaye alihangaika vile vile kwaajili ya kijana wake alipeleka changamoto yake huku na kule hospitali za kawaida zilishindwa, hospitali za rufaa zilishindwa na sasa akawaona wanafunzi wa Yesu ambao nao vile vile walishindwa!

·         Wanafunzi wa Yesu walishindwa – Bado walikuwa wanajifunza, Yesu alikuwa amewapa amri na mamlaka juu ya pepo, lakini walikosa namna na jinsi ya kuachilia nguvu za Mungu na kuitumia mamlaka hiyo kutoa Pepo, hii ni kwa sababu waliogopa, walishindwa kuamini na pia walikosa maisha ya kufunga na kuomba na hivyo mamlaka yao ilikuwa chini, Yesu aliwajulisha kuwa Pepo wana mamlaka za kijeshi na Pepo wa kifafa (aina hii) wana daraja la juu katika mamlaka za kipepo za kuwatesa wanadamu na kuwa wanaweza kutolewa kwa maisha ya kufunga na kuomba

 

Luka 10:17-19. “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

 

Mathayo 17:17-21 “Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

 

Maisha duni ya kufunga na kuomba, pamoja na upungufu wa Imani ya wanafunzi wa Yesu ilikuwa ni sababu ya kushindwa kwao kuwaamuru pepo hawa wa kifafa kumuachia kijana na kumuweka huru Yesu aliwajulisha baadae tatizo lililokuwako, kwa hiyo walishindwa kumsaidia, na mzazi aliwashitaki kwa Yesu.

 

·         Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanadamu – watu wengi sana wanapokuwa na changamoto za aina mbalimbali katika maisha katika akili zao kichwani kwanza huanza kuwafikiri wanadamu, wanafikiria mtu atakayewapa muunganiko “connection” mtu wa kuwaunganishia, wanaelekeza mawazo yao na kuwategemea wanadamu na kama ilivyo ada Mungu anakuwa chagua la mwisho

 

Yeremia 17:5-8 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

 

·         Yesu ndiye suluhisho – Ziko shida ambazo madaktari wa kawaida hawawezi kushughulika nazo, ziko changamoto ambazo wanadamu hawawezi, ziko changamoto ambazo huwezi kuzidhibiti kwa mifumo ya kidini na kiserikali wala kwa uzoefu wako na maarifa yako bila kumkaribia Yesu Mwenyewe!

 

Yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka yote mbinguni na duniani, hata wenye mamlaka na waliopewa mamlaka wanahitaji kumtegemea Yesu kila wakati, Yesu anapoagiza mleteni huku kwangu alikuwa anatualika wote kwamba changamoto yoyote kubwa au ndogo inayokukabili yeye anaweza kushughulika nayo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, jina lake lina kibali kila mahali, yeye ni mwisho wa matatizo zote, na kuwa kwake hakuna jambo lisilowezekana, hakuna linaloshindikana kwake, kila kitu ambacho kimeshindikana kipelekwe kwa Yesu, peleka watoto walioshindikana, peleka mke aliyeshindikana, peleka mume aliyeshindikana, peleka magonja na shida na changamoto zote zilizoshindikana kwa sababu Yesu sio wa kawaida !

 

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”

 

Ufunuo 1:8 “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

 

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

 

Hakuna mafanikio ya kweli unayoweza kuyapata nje ya Yesu Kristo, yeye ndiye mwenye mamlaka yote, yeye ndiye mwanzo na mwisho Alfa na Omega, yeye kwa jina lake kila kitu kitapiga goti kiwe cha kuzimu, duniani au mbinguni, kila kitu kimetiishwa chini yake, mapepo yametiishwa chini yake magonjwa yametiishwa chini yake roho wote wachafu, falme mamlaka wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho yametiishwa chini yake, hakuna shida ambayo yeye hawezi kuitatua, maarifa yako yanaweza kushindwa wagaganga wako wanaweza kushindwa, washauri wako wanaweza kukwama, dini yako inaweza kukwama, wanasaikolojia wako wanaweza kushindwa kukukwamua Lakini Yesu anasema na kutoa mwaliko leo Mleteni huku kwangu, Yako mambo katika maisha yako huwezi kuyashughulikia, unahangaika kwa sababu hujawahi kujaribu kwa Yesu, sikiliza mwito wa Mwana wa Mungu yeye anasema Mleteni huku kwangu, ni mke aliyeshindikana kwa ukorofi, mleteni huku kwangu, ni mtoto aliyeshindikana kwa ukorofi mleteni huku kwangu, ni mume aliyetekwa na makahaba mleteni huku kwangu, ni mlevi aliyepindukia kila mtu amemkataa mleteni huku kwangu, ni huduma yako haieleweki, mleteni huku Kwangu, ni magonjwa madakatari wameshindwa mleteni huku kwangu, ni mwenye nyumba mkorofi mleteni huku kwangu, ni bosi mwenye gubu mleteni huku kwangu, ni shida ya aina yoyote imekushika kooni Yesu anatoa mwaliko mleteni huku kwangu  Yesu habadiliki uwezo wake wa kutoa msaada bado uko pale pale yeye ni yeye yule jana leo na hata milele na hakuna jambo lililo gumu la kumshinda yeye.Hebu twende mbele za Bwana na kupeleka mahitaji yetu yote yaliyoshindikana kwake yeye ni mwema atatusaidia.

 

Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.” Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”

 

Fanya uamuzi leo, wa kumkabidhi Yesu lolote linalokusibu na lolote libnalokusumbua katika maisha yako

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumanne, 20 Mei 2025

Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari!


Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini.Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue. Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa muujiza wa Bwana Yesu kutembea juu ya mawimbi ya bahari ya Galilaya haukuwa muujiza wa kawaida kama wengi tunavyodhani, muujiza huu wa aina yake kati ya miujiza mingi aliyoifanya Bwana Yesu huu umerokodiwa na injili tatu zisizo fanana kwa kusudi maalumu


Mathayo 14:22-33 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”


Marko 6:45-52 “Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.”


Yohana 6:16-21 “Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa.Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.”


Muujiza huu wa Yesu Kutembea juu ya mawimbi ya bahari kimsingi ulikuwa ni muujiza maalumu wa kujifunua kwa wanafunzi wake mamlaka kubwa aliyokuwa nayo Yesu dhidi ya majanga ya asili na uweza wake wa kiungu, na ndio maana muujiza huu haukufanyika mbele ya watu wote isipokuwa wanafunzi wake peke yao kimsingi muujiza huu ulikuwa unamfunua Yesu kwa wanafunzi wake kwamba yeye ana upekee wa aina yake!


1.       Uwezo wake wa kiungu – Wanafunzi wake wote waliorekodi muujiza huu hawakuacha kutaja neno “NI MIMI” Msiogope, Yesu Kristo alitumia mara kadhaa neno NI MIMI au mimi ndimi moja kwa moja akijifunua kwa mamlaka na uweza wa kiungu sawa na mwokozi aliyemtokea Musa tayari kwa wokovu wa wana wa Israel kutoka utumwani kule Misri neno NI MIMI lilitumiwa na Mungu kujitambulisha yeye ni  nani wakati Musa alipopata wasi wasi kuhusu wovovu wa wana wa Israel mbele za Farao.


Kutoka 3:13-15 “Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.”

 

Kwa kujitambulisha hivyo kwa wanafunzi wake Yesu ni sawa tu na anarudia namna Mungu alivyojitambulisha kwa Musa MIMI NDIMI, NI MIMI “I AM WHO I AM” jina hilo tafasiri yake ndio YHWH au Yahweh ambalo maana yake ni Mungu mwenye kujitosheleza na wa milele ni mwokozi kwa hiyo Yesu aliposema NI MIMI msiogope alikuwa anafunua mamlaka yake kamili ya uungu kwa wanafunzi wake

 

Kuna nguvu kubwa ya kupita kawaida nguvu ya uungu yenye uwezo zaidi ya wanadamu wa kawaida Yesu alipojitambulisha NI MIMI au MIMI NDIMI mwanafunzi wa Yesu Yohana katika injili yake anaonyesha jinsi majeshi ya wakamataji, yaani kikosi kilichotumwa kumkamata Yesu kilivyopata misuko suko mkubwa wakati Yesu alipojitambulisha kwao kwa usemi huo

 

Yohana 18:4-6 “Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.”

 

2.       Uweza wake juu ya maswala ya asili – Kristo Yesu alijifunua kupitia muujiza huu kuwa yeye anazo nguvu juu ya uumbaji na maswala yote ya asili, (Power over nature) kila janga la asili iwe ni matetemeko, iwe ni radi, iwe ni dhuruba, uwe ni upepo au bahari iliyochafuka Yesu ana uweza juu ya majanga ya asili, anauwezo wa kufanya yale yasiyowezekana kibinadamu ama yale yasiyofikirika injili zinaelezea kuwa mara Yesu alipopanda chomboni upepo na dhruruba vilikoma.

 

Mathayo 14:32-33 “Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”

 

Marko 6:49-51 “Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao;”

 

3.       Kutimiza unabii na kufunua uungu wake – Ayubu aliwahi kutabiri miaka 2,000 kabla ya Yesu kuwa ni Mungu peke yake mwenye kuzitandaza mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo kimsingi Yesu Kristo alikuwa anaufanya muujiza huu na maalumu alikuwa akitimiza unabii huu, kitabu cha Ayubu kiliandikwa yapata miaka 1000 kabla ya Yesu  na Yesu aliishi mnamo karne ya kwanza na kwa sababu hiyo kutoka Ayubu mpaka kuzaliwa kwa Yesu Kristo ilikuwa ni zaidi ya miaka 2,000. wanafunzi wa Yesu na watu wengine bila shaka walikuwa wamewahi kuyasoma maneno ya Ayubu na hivyo Kristo alipofanya muujiza huu walishangazwa sana na kujiuliza kuwa huyu ni mtu wa namna gani? Hata Pepo na bahari zamtii?

 

Mathayo 8:26-27 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?                 

 

Ayubu 9:8-12 “Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari. Yeye afanyaye hizo nyota za Dubu, na Orioni, na hicho Kilimia, Na makundi ya nyota ya kusini. Atendaye mambo makuu yasiyotafutikana; Naam, mambo ya ajabu yasiyohesabika. Tazama, yuaenenda karibu nami, nisimwone; Tena yuapita kwenda mbele, nisimtambue.Tazama, yuakamata, ni nani awezaye kumzuia? Ni nani awezaye kumwuliza, Wafanya nini?

 

Andiko hilo linafunua kuwa ni Mungu peke yake azitandaye mbingu na kukanyaga mawimbi ya bahari, kwa hiyo ni Dhahiri na ni wazi kuwa kitendo cha Yesu Kristo kutembea juu ya maji kwa kuyakanyaga mawimbi ya bahari alikuwa akiutimiza unabii huu, kwa hiyo muujiza unatufunulia ya kuwa Yesu hakuwa wa kawaida tu bali alikuwa na mamlaka ya uungu ndani yake, Bahari ilimtii, kanuni za kisayansi zilivunjika na Yesu alitembea juu ya maji, alikemea upepo na bahari na zikamtii.


Mambo ya Msingi ya kujifunza:

Kwanini Kristo anajifunua hivi kwa wanafunzi wake na kwa watu wote leo? Yesu hajifunui hivi kwa faida yake tu kwamba awe na sifa za uungu, Yesu anajifunua hivi kwetu leo ili kwamba wote tupate kumuamini kuwa yeye yuko pamoja nasi katika aina yoyote ya dhuruba, unapomuamini Yesu kwa kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako kumbuka muujiza huu haukuwa wa watu wote huu ulikuwa ni maalumu kwa wanafunzi wake ni muujiza maalumu kwa wale wanaomuamini yeye  kwa hiyo kwanza tunafunuliwa ya kuwa hatuko peke yetu, Wakati wanafunzi walipokuwa wakisumbuliwa na dhuruba na kujifikiri ya kuwa wako peke yao Yesu Kristo aliwatokea na kuingilia kati masumbufu yao, mashaka yao na wasiwasi wao, Leo tunajifunza ya kuwa muumba ulimwengu, mwenye nguvu juu ya majanga yote ya asili yeye ambaye Peke yake anaweza kukanyaga mawimbi ya bahari yuko pamoja nasi na atatutokea na atatuliza dhoruba zote zinazotukabili katika maisha yetu katika namna iliyo nyepesi sana na ya kushangaza, kwa hiyo hatuwezi kuogopa linapotokea janga la aina yoyote yeye ni kimbilio letu na nguvu zetu ona:-

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Tunajifunza kuwa tunapaswa kumwangalia yeye kwa imani bila kuona shaka, Petro alipomtambua Yesu aliyekuwa anatembea juu ya dhuruba na kuomba atembee juu ya dhuruba Bwana alimpa kibali na aliweza, lakini pale alipoona shaka na kuanza kuangalia dhuruba mara alianza kuzama, tunajikumbusha au kukumbushwa kuwa wakati wa changamoto zozote za maisha ni lazima tuendelee kumtazama Yesu, Ni lazima tumwamini na kutambua ya kuwa yeye peke yake anaweza kutusaidia na kuwa tunapoliitia jina lake atatushika mkono

Waebrania 12:2- “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Tunapomtazama Yesu ni muhimu kufahamu kuwa hakuna kuzimia na hakuna kuchoka wala kukata tamaa au kuingia mashaka, tunajifunza uweza mkubwa na mamlaka kubwa ya Yesu Kristo ili kwamba tupate kuamini na tukiisha kumwamini hakuna mtu awaye yote atakayetahayarika, Kama  Bwana wetu Yesu Kristo aliweza kupita sehemu hatarishi na akavuka salama tunajifunza kuwa sisi nasi tukimwangalia yeye tutapita sehemu hatarishi pamoja naye na tutavuka salama, maji na radi na vilindi vya bahari na dhuruba za kila namna vyote vina muogopa Mungu na kwa sababu hiyo hakuna jaribu liltakaloweza kusimama mbele yako lisishughulikiwe kwa jina la Yesu Kristo aliye hai.

Zaburi 77:16-20 “Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka, Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa. Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika; Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana. Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.”

Hitimisho!

Leo nakutangazia kuwa  haijalishi unapitia changamoto ya aina gani, dhuruba ya aina gani, upepo wa aina gani, haijalishi madaktari wamekuambia nini, haijalishi kuwa una rufaa mkononi kwenda hospitali kubwa, haijalishi mapigo yako ya moyo yako juu au chini, haijalishi umevamiwa na virusi vya korona, au ukimwi, haijalishi vipimo vikubwa vimekuja na matokeo magumu kiasi gani, haijalishi una maadui waliojipanga kwa kiwango cha kukutishia, haijalishi unaogopa nini,  haijalishi una madeni ya kausha damu, na mikopo umiza, haijalishi wamekodi mganga gani akuroge, haijalishi kuna vikao gani vya majungu vimekukalia, haijalishi fitina na majungu, na mizengwe unayowekewa nakutangazia ya kuwa yuko yeye akanyagaye mawimbi, kila aina ya wimbi katika maisha yako litakanyagwa na kutulia tuli katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, usiogope, usione shaka, usitikisike, usisitesite, usitetemeke, usikate tamaa, usilie, usiogope na kuwaza itakuwaje nakutangazia ya kuwa yuko akanyagae mawimbi ya bahari kila wimbi linalopita katika maisha yako Yesu atalikanyaga na litatulia kimya kwake yeye aliyezifanya mbingu na nchi katika jina la Yesu. 

“Kumbuka ni Yeye peke yake akanyagaye mawimbi ya bahari! Wokovu una yeye Mungu wetu!”

Tufani inapovuma

sana moyoni mwangu!

Huona pa kujificha 

Mkononi mwa Mungu.

 

Hunificha, hinificha, Adui hatanipata, Hunificha, hunificha mkononi mwake

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.