Jumatano, 16 Novemba 2022

Wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia

 

Mathayo 23:23-28. “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”



Utangulizi:

Katika Mathayo 23:13-36, kuna mahubiri makali ya maonyo kutoka kwa Yesu Kristo kuelekea kwa mafarisayo na viongozi wa dini waliokuweko katia nyakati hizo, Neno ole ni sawa na onyo la kulaani au kuonya juu ya hukumu kubwa ya Mungu kwa watu ambao maonyo hayo yanaelekezwa kwao,Krito alikemea vikali kwa maneno mazito hata wakati mwingine akitumia neno vipofu na wanafaiki, Sababu kubwa ni kuwa watu hawa walikuwa wakiwashawishi watu wafuate imani zao na matiokeo yake ilikuwa ni kama kuwapeleka Jehanamu, wakikazia katika mafundisho yao maswala yasiyo ya msingi wa Neno la Mungu na kuwaelekeza katika mapokeo ya kibinadamu zaidi, huku wakipuuzia msingi wa sharia ya Mungu ambayo ni ADILI, REHEMA na IMANI

Kwa maana nyingine Kristo alikasirishwa na Jinsi ambavyo viongozi wa kidini walishindwa kuwatafasiria watu kile ambacho sheria ya Mungu inakipa kipaumbele na badala yake wakaanza kukazia sharia za kidini zinazotokana na mapokeo, mikazo hiyo haikuwa dhambi hata hivyo lakini ilikuwa si Muhimu, tabia mbaya waliyokuwa nayo Mafarisayo ilikuwa ni mkazo wa utoaji wa zaka hususani kutoka katika mazao ambao kimsingi ulikuwa ni urithi wa watumishi wa Mungu yaani walawi kwa wakati ule

Hesabu 18:20-24 “ Kisha Bwana akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli. Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.  Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa. Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi. Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote.”

Kumbukumbu la torati 14:24-29 “Na njia ikiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia Bwana, Mungu wako; ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako; na zile fedha zitumie kwa cho chote itakachotamani roho yako, ng'ombe, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako cho chote; nawe utakula huko mbele za Bwana, Mungu wako; tena furahi, wewe na nyumba yako; na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe. Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.”                       

Unaweza kuona Mafarisayo na viongozi wa dini walikazia sana kuhusiana na vifungu vinavyokazia kuhusu utoaji wa zaka na kwa kweli kutokana na uroho walikazia utoaji wa zaka mpaka ya mnanaa, Bizari na jira kwa faida zao, Mnanaa ni mmea wenye majani madogo madogo ya kijani kwa kiingereza unaitwa Mint mmea huu unatumika kutibu magonjwa mbalimbali kama Aleji, kuvimbiwa, maumivu ya tumbo na kutibu magonjwa mengine kama kisonono, bawasiri na maumivu katika njia ya mkojo, mmea huu ulitumika kama tiba kwa miaka elfu nyingi sana duniani,

Bizari kwa kiingereza Dill ni kiungo cha manjano BINZARI ambacho tutumika kuweka rangi ya mchuzi na kuifanya iwe wa manjano au mwekundu na shughuli nyinmginezo za kimapishi na ladha au harufu nzuri kwenye chakula pia hutumika kama tiba ya magonjwa

Jira kwa kiingereza cummin ni vijijani vyenye vitunda vidogo vidogo sana vya kijana ambavyo vikianikwa huwa na rangi ya kijivu hivi ni viungo ambavyo huchanganywa na viungo vingine na kuleta ladha maalumu katika kama pilau na mchuzi na kadhalika, jira ina uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali ikiwepo, kusaidia kupunguza uzito, kuondoa msongo wa mawazo, kuyeyusha mafuta hatarishi mwilini, kisukari, na magonjwa mengineyo. Kwa ujumla vitu hivi vilikuwa vinahusiana na UPONYAJI, UZURI NA UNONO. Mafarisayo walisisitiza sana utoaji wa zaka hata wa vimimea hivi vidogo vidogo kwa mkazo mkubwa sana kwa makusudi tu wakuu wa dini wanufaike na utamu wa vyakula vyao na afya nzuri, Yesu hakuhukumu utoaji wala utoaji wa zaka lakini kuna kitu nyuma ya mkazo wa viongozi wa dini ambacho Kristo alikuwa anakikemea huku akiwakemea kwa kuacha kusisitiza maswala ya msingi na ya muhimu

Mafarisayo waliacha kuweka mkazo katika maswala makubwa ya msingi ya kiroho ambayo yangekuwa na faida kubwa kwa watu kuliko yale ambayo yangekuwa na faida kubwa kwao  waliacha maswala ya ADILI – Maswala ya kuhukumu kwa haki linapokuja swala la Mtu Fulani amekosea, REHEMA – Kushindwa kuwahurumia watu waliokosea na wale wanaohitaji msaada wa kibinadamu au walio kwenye mateso, IMANI -  Biblia ya kiingereza inatumia neno FAITHFULNESS ambalo linahusiana na UAMINIFU

Kuchuja mbu na kumeza ngamia

Wakati mwingine unaweza kudhani kuwa shida hii ilikuwa ya mafarisayo pekee wakati wa Yesu Kristo la hasha hata sasa ziko tabia Fulani zinazoweza kukemewa katika mtindo kama huu wa Masihi, Leo hii pia wako watu wameacha mambo ya msingi na kukazia mambio ya siyio ya msingi, kwa mfano sio vipaya kuhubiri uponyaji na mafanikio kwa vile ni wazi kuwa watu wanahitaji mafanikio na uponyaji na hakuna jambo baya kama umasikini, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa injili inahitaji balansi, lazima wahubiri wasisahau kuwa tunapaswa kuhubiri injili kamili, mara kadhaa unaweza kukuta wahubiri wansisitiza juu ya utoaji lakini sababu kubwa ni kwaajili ya mahitaji makubwa waliyo nayo,  na wakati mwingine kwaajili ya ubinafsi na kujinufaisha, tunaweza kuhubiri kuhusu uponyaji lakini tusisahahu kuwa watu wanapaswa pia kuishi maisha matakatifu na kukumbushwa kuhusu toba na kusamehewa dhambi na sio uponyaji pake yake

Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,” unaona wakati tunasisitiza kuhusu Uponyaji ni lazima vile vile tukumbuke kusisitiza toba na msamaha wa dhambi, itajkuwa ni hasara kubwa sana kama mtu ataponywa magonjwa yake yote lakini hajawahi kuambia atubu dhambi au aishi maisha matakatifu, na sio sahihi vilevile kuhubiri mafanikio na afya njema bila kusahau kuwa afya halisi inapaswa kuanzia rohoni

3Yohana 1:3 “Mpenzi naomba ufanikiĆ„e katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo

lakini vilevile inaweza kuwa makosa sana kuwahukumu watu kutokana na muonekano wao, au hali yao ya kifedha au cheo chao na kuacha kuweka uthamani wa mtu katika mizani ya kiroho, aidha kumekuweko na upendeleo katika utoaji wa haki, wako watu kwa sababu ya utajiri wao wanaweza kupewa heshima Fulani na hata wakifanya dhambi wanaweza kuhifadhiwa lakini wewe ambaye huna kitu ukadhalilishwa

Yakobo 2:1-5 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?

 Unaona watu hawajali umuhimu thamani ya nasfi na roho ambayo ni moja bali wanaangalia muonekano, wako watu ambao wanaweza kuhukumu mambo pia kwa sababu tu wamesikia umbeya na uongo bila hata kujithibitishia uhalisia wa mambo,  Pamoja na mahitaji ya watu wenye njaa, wenye uhitaji lazima tuonyeshe rahema kwa watu kwa kuwasaidia kukutana na mahitaji yao. Mtu anaweza akaonekana anahudhuria ibada na kutii kila kinachoamuriwa kanisani lakini maisha yake binafsi yakawa na uchafu wa kila aina, je tunaishi vipi na waume, zetu, wake zetu, watoto wetu, na je akilini tunawaza nini?  Wako watu wanahukumu wengine lakini akilini mwao ni waongo,  wana hasira, wachonganishi wamejaa fitina majungu na uzushi, kutaka sifa na kujitwalia utukufu, Yesu anachokitaka ni tuwe wakamilifu pande zote hatupaswi kuchagua kipi cha kutii na kipi sio cha kutii

Mathayo 23:23-24 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.”

Yesu anacho kitaka wetu ni kuwa pamoja na mambo mengine tusiache kukazia maswala ya muhimu na kuyapa kipaumbele, kama tunahubiri injili na kuichukia dhambi basi tuhakikishe kuwa tunapambana na kile kitu, ukikataza ulevi kataza na tamaa, ukikataza uzinzi kataza na hasira, haki haki, rehema rehema na adili ni adili, hatuwezi kuhubiri uaminifu katika eneo Fulani na wakati huo huo eneo lingine tukawa tumelilegezea, huko ni kuchuja mbu na kumeza ngamia, nusu utii ni sawa na kutokutii haya ni machukizo sawa na namna Mungu alivyochukizwa na Sauli alipomwambia aangamize kila kitu cha amaleki yeye akabakiza  nab ado akawa anasisitiza kuwa ametii

1Samuel 15:1-23Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya Bwana. Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri. Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda. Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu. Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni. Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki. Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri. Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga. Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa. Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha. Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali. Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana, nimeitimiza amri ya Bwana. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia? Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana? Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali. Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”

Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda!

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: