Jumatatu, 7 Novemba 2022

Kuupiga mateke mchokoo !


Matendo 26:12-15Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.”



Utangulizi:

Paulo mtume alikuwa ni kiongozi wa mateso ya wakristo mapema sana Kanisa likiwa katika hatua za awali, akiwakilisha mafarisayo pamoja na baraza la mahakama kuu ya kiyahudi iliyoitwa Senhedrin katika kuhakikisha kuwa wanawasambaratisha wakristo, yeye alisimamia kuuawa kwa Shemasi maarufu wa nyakati za kanisa la Kwanza aliyeitwa Stefano ona

Matendo 7:57-60 “Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.”

Baada ya mpango wake huu kufanikiwa mtu huyu aliendelea na hila za kutaka kulisambaratisha kanisa hasa kwa kuwatesa na kuwaburuza mahakamani na kuwatia gerezani  watu wa njia ile yaani wanaomuamini Bwana Yesu, na mpango wake huu ulikuwa ni tishio kubwa sana kwa kanisa  na kwa kweli maandiko yanaeleza kuwa aliliharibu kanisa kiasi ambacho waamini walitawanyika na waliobaki walikuwa ni mitume tu ona

Matendo 8:1-3 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.

Kama hilo halitoshi alipoona mpango wake umefanikiwa aliongeza mpango wa kwenda mbali nje ya Yerusalem ili nako akatekeleze mpango wake wa kuwatesa watakatifu na kuliharibu kanisa na sasa alikuwa anaelekea Dameski akiwa na kibali cha mahakama kuu ya kiyahudi kufanya hivyo, wakati huu sio akiwaza kuwafunga tu na hata kuwaua ona

Matendo 9:1-2 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.”

Ni katika mazingira kama haya ya utekelezaji wake wa nia ovu ya kusambaratisha Kanisa ndipo Yesu alipomtokea na kumkemea, vikali. Huku akimuonya kwamba aache kuupiga mateke Mchokoo!

Maana ya neno Mchokoo!

Matendo 26:12-15Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke MCHOKOO. Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.”

Neno Mchokoo katika biblia ya kiyunani linasomeka kama KENTRON ambalo kwa kiingereza ni Prick ambayo maana yake ni katikati centre au kwa lugha rahisi ni “NCHA” kali Ncha hii inaweza kuwa ya mkuki, mti wa kuchonga, au ncha ya panga au kisu,  kwa mujibu wa masimulizi ya kale wakulima wa zamani waliokuwa wanalima kwa kutumia jembe la kukokotwa na Ngo’mbe walikuwa wanaandaa fimbo ndefu yenye ncha kali na kumtegeshea mnyama kama Ngombe anapolima kama analeta ubishi au kiburi au upinzani anapopiga mateke angeweza kuumizwa nakitu hicho chenye ncha kali na hivyo angeweza kuacha mara moja tabia yake ya kushindana na mkulima, Paulo mtume alikuwa anakabiliwa na adhabu kali kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ndiye mwanzilishi wa Kanisa, Paulo mtume alikuwa akishindana na Kusudi la Mungu ambalo kwa vyovyote vile lingweza kuleta madhara makubwa sana katika maisha yake kama hangelitubu na kugeuka na kumuhubiri Kristo, kuendelea kuwaua au kuwatesa wakristo, na kuwatia gerezani ilikuwa ni kushindana na kazi au agizo la Mungu mwenyewe,  hili liwe onyo sio kwa Paulo tu lakini kwa watu wote ambao kwa kiburi na kwa ujeuri hushindana na maagizo ya Mungu, hakuna mtu anayeweza kushindana na Mpango wa Mungu na kufanikiwa

Matendo 5:34-39 “Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”

Mtu awaye yote ambaye anashindana na kupingana na kazi ya Mungu au jambo au shauri ambalo Mungu mwenyewe ni sababu kwa vyovyote vile anaupiga mateke mchokoo, Paulo alipokuwa anajaribu kulisambaratisha kanisa na kuonekana kama anafanikiwa kuwaudhi na kuwaumiza watakatifu,  alikuwa ni kama mtu anayejiumiza mwenyewe, wako watu wengi leo hii katika taasisi mbalimbali, makanisa, madhehebu na sehemu nyingine ambako adui wao wa kwanza ni wale wanaomcha Mungu, wanaweza kukutengenezea zengwe, wanaweza kukupiga vita, wanaweza kukudhukumu na kukuwekea vikwazo, wakidhani ya kuwa kwa kufanya hivyo watakukwamisha wewe lakini kwa bahati mbaya sana wanajiumiza wenyewe, Haya yalikuwa ni maonyo ya Yesu Kristo mwenyewe kumbuka kumbe Kristo yuko serious na kila aina ya binadamu anayeshindana na makusudi ya Mungu!

Kuupiga mateke mchokoo !

Ni muhimu kukumbuka kuwa makusudi ya Bwana hayawezi kuzuilika Ayubu 42:1-2 “Ndipo Ayubu akamjibu Bwana, na kusema. Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” Kila mwanadamu, mtu au awaye yote ambaye anashindana na kusudi la kiungu hapa Duniani anaupiga teke mchokoo na hatafanikiwa, kwa sababu unashindana na Mungu mwenyewe, sikiliza unaweza kusema kuwa hii sio injili kwa vile tunaishi katika agano Jipya lakini ngoja nikukumbushe kuwa maneno haya ni ya Yesu Mwenyewe akimuonya Paulo Mtume kuwa linapokuja swala la kuliudhi kanisa na kupambana ana kusudi la Mungu au hata mtu ambaye yuko katika kulitekeleza kusudi la Mungu hii iko wazi kabisa kuwa unashindana na Yesu Mwenyewe kumbuka maonyo haya ni makali Sauli Sauli mbona waniudhi? Kuna mmstari ambao ulikuwa unamfikia muhusika na kuwa ulikuwa umefikia wakati kuwa aidha aokoke au afe. Kushindana na Wakristo ni kuupiga teke mchokoo, kupamba ana kanisa ni kuupiga teke mchokoo, kushindana na watu wa Mungu ni kuupiga teke mchokoo na kushinda na mtu ambaye yuko kwenye kuyatimiza mapenzi ya Mungu ni kuupiga teke mchokoo na matokeo yake ni maumivu makali na makubwa zaidi

Madhaya ya kuupiga mateke Mchokoo!

Maandiko yananyesha wazi kuwa Mungu hawezi kuvumilia kwa namna yoyote mtu awaye yote ashindane na Kusudi lake na wote walioshindana na kusudi la Mungu aidha ndani ya mtu au taasisi zake Mungu aliwashughulikia vikali, ashukuriwe Mungu kuwa Paulo Mtume alielewa baadaye kuwa anashinda na Mapenzi ya Mungu na alitubu na kubadilika na kulitumikia shauri la Mungu, Lakini uzoefu wa kimaandiko unaonyesha kuwa Mungu hupigania mpango wake na watu wake pia, wako watu walishindana na Daniel na kumfanyia fitina ili kuathiri kusudi la Mungu ndani yake lakini badala ya Daniel kudhurika wao ndio walijikuta wako taabuni. 

Daniel 6:1-24 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku. Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.  Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.  Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao,”

 Unaona wale waliokuwa wakishindana na Daniel katika maisha yake na kusudi la Mungu lilioko ndani yake ni wenyewe ndio waliokuja kuangamia badala ya Daniel, Mungu akufanyie hivyo na kuzidi dhidi ya adui zako wanaoukuandama na kutaka kupigana na kusudi la Mungu lililoko ndani yako!, Maandiko yanaonyesha pia kuwa Mungu alikuwa amekusudia kuwarithisha Israel Nchi ya mkanaani akiwa amewabariki tangu enzi za baba yao Ibrahimu na Isaka na Yakobo, lakini mfalme wa Moabu aliyeitwa Balaki alimuita mtu mmoja aje kuilaani Israel kinyume na kusudi la Mungu huku nako ni kushindana na kusudi la Mungu ni kuupiga mateke mchokoo, Balaamu aliamua kwenda kuilaani Israel lakini mpango wake ulipingwa vikali na malaika mpaka Punda akasema naye na sio hivyo tu badala ya kulaani alijikuta anatamka Baraka ona

Hesabu 23-7-8 “Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?

Unaona Balaamu alijikuta anawabariki Israel na kuwashuindwa kuwalaani au kuwashutumu, lazima ufikie wakati ambapo maadui wa ukristo au watumishi wa Mungu au mtu awaye yote wa Mungu waache kushindana nasi kwani kufanya hivyo ni kujichimbia shimo lao wenyewe Mithali 26:27 “Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.” Kila anayeshindana nawe hatafanikiwa kila anayekupiga vita anajipiga vita mwenyewe na kila anayekushutumu shutuma hizo zitamrudia kila anayeshindana na kusudi la Mungu lililoko ndani yako anaupiga vita mchokoo na ataumia mwenyewe!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajensi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: