Jumatano, 16 Novemba 2022

Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu!


Luka 16: 9 - 12Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.


Utangulizi:

Mojawapo ya kifungu kigumu katika tafasiri za mafundisho ya Yesu ni pamoja na maneno haya ambayo Yesu aliyasema kama sehemu ya Hitimisho ya mfano tajiri na wakili wake, katika Luka 16:1-8 ambako kimsingi Yesu Kristo alikuwa anatufundisha wazi namna ya kutumia fedha na mali tulizopewa na Mungu na ujuzi ya kuwa hatuna tunachomiliki duniani, na kuwa tunwajibika namna tunavyotumia mali na fedha na kwamba tutatoa hesabu ya kila alichotupa Mungu. Baada ya fundisho hilo Muhimu ndipo sa Yesu alianza kuweka mikazo ya maneno haya tunayojifunza leo JIFANYIENI RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU! Kimsingi Yesu alikuwa anafundisha namna ya kujipatia utajiri wa kweli. Yesu qanawataka wanafunzi wake kutumia fedha na mali za ulimwengu huu walizonazo kujipatia thawabu za kudumu katika ufalme wa Mungu. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

Ø  Tafasiri ya Mali, fedha, Utajiri na udhalimu wakati wa Yesu Mst9-11

Ø  Jifanyieni rafiki kwa mali ya Udhalimu Msta 9-12

Ø  Jinsi ya kumtumikia Mungu na Mali Mst 13

Tafasiri ya Mali, fedha, Utajiri na udhalimu wakati wa Yesu (Mst9)

Luka 16:9-11 “Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.  Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.  Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?”

Ni muhimu kufahamu kuwa wakati wa Yesu Kristo katika mwili Duniani falsafa kuhusu Mali utajiri na fedha ilikuwa na mitazamo mikubwa mwiwili, hasa katika jamii ya mafarisayo na watu wa ulimwengu wa wakati ule Katika mtazamo wa kwanza wa Mafarisayo hasa katika lugha ya KIARAMU, kuwa na Mali, fedha na utajiri kulihusishwa moja kwa moja na dhuluma (UDHALIMU). Kwa kiyunani ni “ADIKOS”- Wicked, treacherous, unjust au unrighteousness,  Matajiri walikuwa wanafikiriwa kuwa ni watu dhalimu na kuwa walivyonavyo wamevipata kwa kudhulumu au kwa njia zisizofaa kwa hiyo walivipata kwa kufanya dhambi, kwa njia za uovu, kudhulumu watu  kwa hila, au isivyo sawasawa na pia walivitumia kwa anasa na ubinafsi mkubwa ona 

Yakobo 5:1-6 “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.”

Kwa hiyo fedha na mali na utajiri ulifikiriwa na kuhusishwa na choyo na dhambi katika mtazamo wa kwanza, lakini vilevile katika mtazamo mwingine au falsafa ya pili fedha ilifikiriwa kuwa ni Baraka kutoka kwa Mungu kama mmiliki alikuwa amezipata kwa haki huku akiwa anamcha Mungu,

Marko 10:17-23 “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!

Hata hivyo Matajiri wote wale waliofikiriwa ni wadhuluma na wale wa haki wote walikuwa na matatizo wote walikuwa wanakabiliwa na choyo na ubinafsi, na hivyo Yesu yeye alizuiona fedha mali na utajiri wa dunia hii kama havitatumika kwa usahihi madamu ni mali za duniani zote aliziita mali za udhalimu, kwa nini kwa sababu haziwezi kuwapa wanadamu manufaa ya kudumu katika ulimwengu wa ufalme wa Mungu.

Jifanyieni rafiki kwa mali ya Udhalimu Msta 9-12

Kama tulivyojifunza hapo awali ya kuwa Yesu aliona matumizi yote ya fedha kwa watu wa dunia hii bila kujali mali zao wamezipataje mali zao zingeliweza kuwapa manufaa ya kudumu kama watakosa akili na ufahamu wa kutosa katika kuzitumia, akiendelea kukazia mfano wa wakili dhalimu alioutoa katika Luka 16:1-8 Kwamba pamoja na kuwa wakili yule alikuwa afukuzwe kazi, alikumbuka kuwa kuna maisha baaya ya kufukuzwa kazi na hivyo alikumbuka kujiandalia marafiki kwa mali yake ya udhalimu ilia je kunufaika baadaye, aidha matajiri wa dunia hii vilevile  wakati ule waliweza kutumia fedha kujipatia marafiki na hata kujiongezea umaarufu duniani na ilikuwa rahisi kukubalika kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kifedha waliokua nao

Mfano hata leo kama utahitaji kugombea ubunge na vyeo vinginevyo vya kikampeni, utaweza kuona kwamba ni lazima uwe na fedha za kutosha kuweza kuongeza ushawishi kujipatia nafasi uitakayo wazo hili hili alilokuwa nalowakili dhalimu kuhusu kesho yake lingeweza vilevile kutumiwa na wanafunzi wa Yesu kuwa na ujuzi na hekima na akili ya kujitengenezea maisha ya baadaye kwa kuwekeza katika Mungu, tunaweza kutumia fedha mali na utajiri  kwa makusudi mema, tunaweza kuzitumia mali fedha  na utajiri wao (Kwa Mtazamo wa Kiaramu Mali ya Udhalimu) kwa lengo zuri la kuujenga ufalme wa Mungu, badala ya kutumia fedha na mali na utajiri wetu kujifurahisha, kwa choyo na ubinafsi, tunaweza kuitumia kujijengea jina kwa kuwekeza kwa Mungu na kuwatendea mema wengine jambo litakalotufanya tuwe matajiri katika kazi njema kwa msingi huo   Agizo hili la Kristo linaweza kutafasiriwa sambamba na,

1Timotheo 6:17-18 “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo;”  

kwa hiyo kama hatutakuwa waaminifu kuitumia mali, fedha na utajiri huu wa duniani (Wa Kidhalimu) kwa Mungu wetu, Mungu naye hatatatutumia au kutuamini katika mambo Halisi ya kweli ya ufalme wa Mbinguni, huko tutakuwa na hazina isiyoharibika,  Kimsingi Yesu hakuwa anamaanisha kuwa na fedha ni jambo baya wala hakuwa anatia moyo kuwa watu wajitafutie fedha kwa nia mbaya au kwa njia zisizofaa, lakini kama waili yule muovu alikuwa na uwezo wa kufikiri kuhusu maswala yajayo kwanini matajiri wa kawaida wawe wachoyo  na kushindwa kuutumia utajiri wao ambao kimsingi utawanufaisha tu hapa duniani kisha wasahau kujiwekeza katika ufalme wa Mbinguni. Aidha tunaweza kuzitumia fedha zetu sio kwaajili ya kutafuta umaarufu lakini kuwasaidia wengine wenye uhitaji jambo ambalo pia linatupa thawabu Mbinguni, Mungu anapotumilikisha fedha mali na utajiri maana yake ametuamini kuwa tunaweza kutunza kwaajili ya wote na sio kwaajili yetu, hivuo kila Mkristo anapaswa kuwa mwaminifu katika kutumia rasilimali ambazo Mungu ametupa kwa faida ya ufalme wake!

“Luka 6:11 Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu (mali fedha na utajiri wa Duniani), ni nani atakayewapa amana mali ya kweli (ya ufalme wa Mungu, na umilele)”?

Jinsi ya kumtumikia Mungu na Mali Mst 13

Kimsingi Bwana wetu Yesu Kristo anauona mlango ni mdogo sana kwa wenye utajiri kuingia katika ufalme wa Mungu kwa sababu ya ubinafsi na choyo, Wakristo ni lazima waende mbele zaidi na kujifunza kumpa Mungu kipaumbele kikubwa zaidi na jamii,  Mungu anapokuwa ametubarikia wingi wa mali, fedha na utajiri vilevile anataka tuvutumie kwa utkufu wake na kumuabudu yeye 

Kutoka 10:8-11 “Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda? Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.”

Mungu anapotuita Kumuabudu yeye na kumfanyia ibada hatuiti nusu  nusu anakuwa ametuita sisi  na kila tulichonacho, kama sisis ni watumishi wake basi kila tunachomiliki ni kwaajili ya utumishi ulioko mbele yetu, sisis ni mawakili tu ambao tumeaminiwa na Mungu,  na tunawezaje kuonyesha imani yetu kwa Mungu ni pamoja na kumuabudu Mungu na kila tunachokitaka! Tunaweza kuonyesha imani yetu kwa Kristo kwa kumtumikia pamoja na mali zetu, katika kila jambo lazima tumpe Mungu kipaumbele na kuonyesha ya kuwa ni yeye anayetawala na wala sio mali zinazotutawala, kutawaliwa na fedha kuliko kutawaliwa na Mungu ni kosa la kiufundi katika maswala ya kiroho, lazima Bwana awe juu ya kila kitu na kila kitu kitiishwe chini yake

Luka 16:13 “Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali

1Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”

Unaona kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kuwa je ni

1.       Mungu anayemiliki kila kitu katika maisha yake?

2.       Je una moyo wa ukarimu au kuna hali ya choyo katika maisha yako?

3.       Je unatenga fungu la kumtolea Mungu katika maisha yako?

4.       Je unahofu ya kuwa utapungukiwa?

Mafarisayo ambao kwa kweli walikuwa wamekwisha zama katika mtego wa kupenda fedha walijikwaa kwa mafundisho ya Kirsto na kumpuuzia kwa sababu choyo kilikuwa ikmetawala nia zao na mioyo yao ili hali wakati huo huo wakijikinai kuwa ni watumishi wa Haki. ona

Luka 16:14 -15 “Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki. Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.”

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Maoni 1 :

Raymond alisema ...

Asante kwa mafundisho, barikiwa sana