Mathayo 5:39-41 “Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini
mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na
kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa
maili moja, nenda naye mbili.”
Utangulizi:
Mathayo 5:38-42 ni mojawapo
ya sehemu muhimu sana katika hotuba ya Yesu Kristo ya Mlimani ambapo Yesu
anafundisha namna ya kuonyesha muitikio wakati mtu anapokudhalilisha au kukutesa,
wakati kanuni za msingi wa agano la kale zilikuwa zinakazia usawa na malipo ya
jino kwa jino au jicho kwa jicho zikimaanisha kwamba mtu akikufanyia kosa
Fulani alipaswa kulipizwa sawasawa na ukubwa wa kosa hilo, yaani kimahakama mtu
apewe adhabu inayolingana na makosa yake, Lakini Kristo anakuja na mtazamo
tofauti mno wakati mtu anapotendewa mambo yasiyo ya haki, Yesu anawataka
wakristo kuonyesha uvumilivu mkubwa sana bila kulipiza kisasi, badala yake
kuwapenda maadui na hata kuwatendea mema
yaliyopitiliza!
Akikulazimisha maili
moja nenda naye mbili !
Nyakati za Biblia wakati wa Yesu
Kristo, Israel pamoja na mataifa mengine yalikuwa chini ya utawala wa kikoloni
wa warumi, Wakoloni wa kirumi hata hivyo kuna wakati hawakuweza kuwatendea haki
raia wa kawaida na hasa raia wa kiyahudi, waliwaburuza barabarani na pia
kuwalazimisha kubeba mizigo mizito kama watumwa
hali hii ilipelekea wakati mwingine kuamsha gahadhabu na kuchochea watu
kutaka kujilipizia kisasi, kitamaduni ilikuwa inawasukuma sana wayahudi kutaka
kujilipizia kisasi na kujitangazia uhuru na utawala
Baadhi ya wale waliokuwa
wakimfuata Yesu, kwa kuwa walitambua kuwa ndiye Masihi walikuwa na fikra kuwa
ataushimamisha ufalme wa Mungu kwa kuuondoa utawala wa Warumi hata hivyo amri
ya Yesu Kristo na fundisho lake lilikuwa kinyume na matarajio yao na
liliwashangaza sana yeye aliwafundisha
kuwa wakubaliane na mateso yale hata ikiwezekana zaidi ya kile walichokuwa
wakifanyiwa, Yesu alisisitiza kuwa wakilazimishwa maili moja na waende nao
mbili.
Kimsingi Yesu hakuwa anafundisha
wanafunzi wake kuwa dhaifu kama wengi wanavyoweza kudhani, badala yake Yesu
alikuwa anamaanisha kuwa hakuna mtu dhaifu duniani, Yesu alikuwa anatufundisha
kuwa watu Hodari na wavumilivu kiasi cha kuweza kuvumilia watu waovu na kuwapa
maadui zaidi ya kile wanachokitarajia, Kristo hakutaka wakristo washindwe na
ubaya badala yake alikuwa akitutaka tuushinde uovu kwa wema
Warumi 12:19-21 “Wapenzi, msijilipize
kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu
mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe;
akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani
pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”
Yesu anawataka wafuasi wake watoe
zaidi ya kile ambacho ulimwengu unaweza kutoa, Yesu hataki tuwe dhaifu lakini
anataka tuwe wavumilivu kwa wanadamu ambao ni wadhaifu sana, wakristo wanapaswa
kuwa hodari na wenye nguvu kiasi cha kuzalisha mambo bora wakati wengine
wakizalisha uovu, hatuwezi kuwa sawa na wana wa ibilisi, sisi ji lazima mtuwe
wakamilifu kama baba yetu wa Mbinguni alivyo mkamilifu, Ubaya wa watu waovu kamwe haupaswi kuwa sababu
ya kuvunjika moyo kwa wakristo na badala yake lazima sisi tuzalishe jamno
lililobora ili kuonyesha kuwa wao ni wapuuzi.
Maandiko yanamsifia mtu
anayejitawala kuwa bora kuliko shujaa, mtu anayeweza kujizuia nafi yake
asikasirike ni mwema sana kuliko hata mtu mwenye uwezo wa kuteka mji, Wakristo
waliokomaa kiroho hawasukumwi kamwe na misukumo ya kihisia bali wanakuwa wenye
nguvu ndani kwa kuonyesha kuwa wanaweza kujizuia hata pale mtu anapotaka
wakasirike
Mithali 16:32 “Asiye mwepesi wa hasira ni
mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.”
Mtu mwenye ukomavu wa hali ya juu
ni yule ambaye anaweza kuwasamehe adui zake na kuwapenda, Daudi ni moja ya
Mfano wa watu waliokuwa wanaweza kuushinda ubaya kwa wema hakuwahi kufurahia
hata kufa kwa adui zake kabisa
2Wafalme 19:4-6 “Mfalme akajifunika uso; na
mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu!
Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso
za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za
binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako; kwa kuwa unawapenda
wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na
watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu
angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako.”
Luka 6:27-30 “Lakini nawaambia ninyi
mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi,
wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.
Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie
na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake
akurudishie.”
Mitume wa Bwana adiha
walisisitiza pia fundisho hili la bwana na kuwataka wakristo kutokuwa watu wa
kulipa baya kwa baya, wala laumu kwa laumu na wanatakiwa kubariki hata watu
wanaowafanyia maovu kwa kufanya hivi
inaashirikia ukomavu mkubwa na unaonyesha kuwa sisi kweli tumekuwa wanafunzi wa
Yesu kweli kweli jambo hili linapaleka habari njema kwa maadui wa Ukristo na
kuwafanya wamkubali Kristo!
1Petro 3:9 “Neno la mwisho ni hili; mwe na
nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu,
wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye
kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.”
Hitimisho:
Aina hii ya muiikio ndio
utakaosababisha watu wauone uzuri wa Mungu hata katika maisha ya wale
wanaowashutumu, kuwaonea na kuwatesa, aidha hii itamfanya mtu muovu akome
kuutumia uovu wake kukomoa wakristo, kwa hiyo mateso na nia ovu za watu wabaya
hazitakuja zishinde nguvu ya Mungu na uwepo wa utendaji nwa Kristo katika
maisha yetu siku zote za maisha yetu. Nabii Elisha aliwahi kuitumia njia hii na
washamu wakaacha kuwafuatia Israel kwa muda mrefu ona
2 Wafalme 6:19-23 “Elisha akawaambia, Njia
hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule
mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha
akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. Bwana akawafumbua macho
wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli
alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? Akamjibu,
Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na
uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa
bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa,
akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika
nchi ya Israeli.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni