2Samuel 3:33-34 “Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje
Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa
pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote
wakaongeza kumlilia.”
Utangulizi:
Abner alikuwa ni binamu na mkuu
wa majeshi ya ulinzi wa Jeshi la Mfalme Sauli, Jina lake limejitokeza katika
maandiko vilevile kama Abner mwana wa
Ner jina lake maana yake baba yangu ni Ner na neno Ner
maana yake ni Mwanga au Nuru!, Mkuu
huyu wa majeshi alitumika na Sauli na Jonathan na hata baada ya kifo chake
alikuwa mwaminifu kwa Mtoto wa Sauli aliyeitwa Ishboshethi hivyo tunapata picha
ya kuwa wakati wote wa vita vya Sauli na Daudi Abner ndiye aliyekuwa akiongoza
mapambano hayo lakini kwa neema ya Mungu siku hadi siku Nyumba ya Sauli ilizidi
kudhoofika dhidi ya Nyumba ya Daudi kama yanenavyo maandiko.
2Wafalme 3:1 “Basi kulikuwa na vita siku
nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi,
lakini nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika.”
Hata hivyo kutokana na kutambua
mapenzi ya Mungu, Abner alitambua wazi kuwa Mungu alikuwa amekusudia Daudi awe
mfalme tangu miaka mingi alipopakwa mafuta na Samuel Nabii, lakini kibishibishi
upande wa Sauli walikuwa wanachelewesha au kushindana na makusudi ya Mungu,
hatimaye Abner aliamua kuwa atasaidia kumkabidhi Daudi ufalme baada ya kugombea
mwanamke kati yake na Ishboshethi mwana wa Sauli.
2Wafalme 3:6-9 “Ikawa, wakati vilipokuwapo
vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri akajipatia nguvu
nyumbani kwa Sauli. Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake akiitwa Rispa, binti
Aya; Ishboshethi akamwuliza Abneri, Kwa nini umeingia kwa suria ya babangu? Basi
Abneri akakasirika kwa maneno ya Ishboshethi, akasema, Je! Mimi ni kichwa cha
mbwa, aliye wa Yuda? Hata leo hivi nawafanyia fadhili nyumba ya Sauli babako,
na ndugu zake, na rafiki zake, nisikutie wewe mkononi mwa Daudi; nawe hata
hivyo wanitia hatiani leo kwa mwanamke huyu. Mungu amfanyie Abneri vivyo, na
kuzidi, nisipomtendea Daudi kama vile Bwana alivyomwapia;”
Kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa kwa kiwango fulani kikubwa Abner
alikuwa ni kikwazo kikubwa kwa mapenzi ya Mungu kwa Daudi kutimia akitetea upande
wa Sauli na watoto wake na pia kumbe alijua mapenzi ya Mungu kuwa Mungu
alimuapia Daudi Ufalme lakini kwa makusudi alikuwa akipingana na mapenzi ya
Mungu na kuchelewesha kusudi la Mungu juu ya Daudi ashukuriwe Mungu kuwa
makusudi yake hayawezi kuzuilika, Mungu aliutumia ugomvi wao na Ishbotheth
kutimiza Mpango wake na Abner sasa alikuwa katika njia ya Mungu akijua wazi
kuwa anatimiza mapenzi ya Mungu.
Abner na mapenzi ya Mungu.
Abner alifahamu kuwa kama
amekosana na Ishbotheth mwana wa Sauli na kujipa nguvu yeye mwenyewe kwa
vyovyote vile atakayepambana na Daudi angekuwa yeye, uso kwa uso, kwa ujumla Jemedari
huyu alikuwa na tatizo la kiburi moyoni mwake maandiko yanaposema alijipatia
nguvu katika nyumba ya Sauli maana yake alijiinua yeye mwenyewe
2Wafalme 3:6-7 “Ikawa, wakati vilipokuwapo
vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri akajipatia nguvu
nyumbani kwa Sauli. Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake akiitwa Rispa, binti
Aya; Ishboshethi akamwuliza Abneri, Kwa nini umeingia kwa suria ya babangu? ”
Unaona akajipatia nguvu nyumbani
mwa Sauli hii maana yake kibiblia alianza kujiinua alianza kuwa na kiburi,
kuchukua mke au suria katika mila za kifalme kulikuwa hakuna tofauti na
kujifanya mfalme au kutaka ufalme ona, 1Wafalme
2:13-23 “Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa
Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akajibu,
Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia,
Sema. Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote
wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa
wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa Bwana. Basi sasa nina haja
moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema. Akasema, Nena,
nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze
Abishagi, Mshunami. Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili
yako. Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya
Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti
chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye
akaketi mkono wake wa kuume. Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba;
usinikataze. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukataza neno. Naye
akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami. Akajibu mfalme
Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami?
Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye,
na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya. Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa
Bwana, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno
hili juu ya uhai wake mwenyewe.” hivyo ili Daudi atawale ilikuwa
lazima Abner ashughulikiwe, naye akijua yatakayompata baada ya kuasi nyumba ya
Sauli sasa anakuja na mpango wa kukabidhi mamlaka ya kifalme kwa Daudi,
lilikuwa wazo jema na mapenzi ya Mungu, lakini ni yeye ndiye aliyekuwa anachelewesha
kusudi la Mungu, sasa anataka kurudisha mamlaka kwa Daudi.
2Wafalme 3:9-10 “Mungu amfanyie Abneri
vivyo, na kuzidi, nisipomtendea Daudi kama vile Bwana alivyomwapia; kuupitisha
ufalme toka nyumba ya Sauli, na kukisimamisha kiti cha Daudi juu ya Israeli, na
juu ya Yuda, toka Dani mpaka Beer-sheba.”
Abner alikuwa mtu mwenye
kujiamini kupita kawaida yeye alijifanya kuwa ni Mungu, pamoja na kuwa aliapa
kwa Mungu lakini anapotumia neno
KUUPITISHA UFALME TOKA NYUMBA YA SAULI NA KUKISIMAMISHA KITI CHA DAUDI JUU YA
ISRAEL NA JUU YA YUDA hii ilikuwa ni kazi ambayo haifanyiki kibinadamu neno
kupitisha Katika kiingereza linasomeka kama “To translate” ambalo katika kiebrania maana yake ni Abar likisomeka kama AW-BAR ambalo maana yake ni ni sawa na
kutenga au kusababisha au kuweka wakfu au kuhamisha
kimsingi hayo yanaweza kufanywa na Mungu tu ona Wakolosai 1:13 “Naye alituokoa katika nguvu
za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;”
unaweza kuona Lugha hiyo pia katika Waebrania 11:5 “Kwa
imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu
Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba
amempendeza Mungu.” Kwa hiyo kumamisha au kupitisha ni kumtoa mtu
katika hali moja na kumpeleka katika hali nyingine hii ni kazi ya Mungu na sio
ya Mwanadamu. Ni wazi kuwa kamanda huyu alikuwa na kiburi.
Abner vilevile alikuwa ni mtu
hatia ya damu ya shujaa anayeitwa Asahel, Huyu alikuwa moja ya watu mashujaa
aliyekuwa na mbio za kufukuzia maadui kama mbio za kulungu, katika mashujaa
watatu waliotoka kwa Seruya waliojulikana kama wana wa Seruya Asahel alikuwa ni
hodari lakini zaidi sana aliyekuwa na uwezo wa kukimbiza adui, Asahel alikuwa
akimkimbiza Abner na kwaajili ya kujihami Abneri alimshihi sana aache
kumfuatilia lakini Asahel alikaza na kwa sababu hiyo yeye alimuua ona
2Samuel 18-28 “Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na
Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu. Naye
Asaheli akamfuatia Abneri; na katika kwenda kwake hakugeuka kwenda mkono wa
kuume wala mkono wa kushoto katika kumfuatia Abneri. Basi Abneri akatazama
nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi. Basi Abneri
akamwambia, Geuka mkono wa kuume au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa
vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha
kumfuata. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi;
kwa nini nikupige hata chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu,
ndugu yako? Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha
ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo,
akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa,
wakasimama. Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo
walipoufikilia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni. Nao
wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja,
wakasimama juu ya mlima. Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga
uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi
itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao? Naye
Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao,
wasiwafuatie kila mtu ndugu yake. Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote
wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena.” Mtu
aliyeua mtu mwingine alipaswa kusalimisha maisha yake katika mojawapo ya miji
sita ya makimbilio ili mwenye kujilipiza kisasi kwaajili ya nduguye aije
akamuua, Hata hivyo Abneri hakuweza kujali maelekezo hayo ya torati kwa vile
alikuwa akijiamini kutokana na umahiri wake katika vita
Agano la Abner na Daudi.
Pamoja na madhaifu makubwa
aliyokuwa nayo Abner, huyu pia alikuwa ni jemadari wa vita, alikuwa ni mzoefu
wa vita shujaa na kamanda mwenye nguvu sana lakini pia alikuwa mpenda amani na
mwangalifu mno, katika uwezo wa kujihami,
ulifika wakati akaona pia kuwa sasa Israel wanahitaji amani.
2Samuel 3:12-16 “Basi Abneri akatuma
wajumbe kwa Daudi mahali alipokuwapo, akisema, Nchi hii ni ya nani? Fanya agano
nami, na tazama, mkono wangu utakuwa pamoja nawe, ili kuwaleta Israeli wote
kwako. Daudi akasema, Vema, nitafanya agano nawe, lakini nina sharti moja
nitakalo kwako, nalo ni hili; Hutaniona uso wangu, isipokuwa uniletee Mikali,
binti Sauli, hapo ujapo kuniona uso wangu. Basi Daudi akatuma wajumbe kwa
Ishboshethi, mwana wa Sauli, kusema, Nipe mke wangu Mikali, niliyemposa kwa
govi mia za Wafilisti. Basi Ishboshethi akatuma watu, akamnyang'anya Paltieli,
mwana wa Laishi, mumewe, mwanamke huyo. Huyo mumewe akafuatana naye, akiendelea
na kulia, akamfuata mpaka Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia, Haya, rudi. Naye
akarudi.”
Kwa kuwa ilikuwa ni desturi ya
Israel mtu anapofanya agano lazima wawekeana masharti Daudi aliitumia nafasi
hiyo kumdai Abner ili aweze kumona uso wake amletee mke wa ujana wake aliyemuoa
kwa gharama ya givi za wafilisti 100 lakini yeye aliua 200 ambaye alikuwa ni
mikali Binti wa Sauli jambo ambalo Abner alilitii, hii ilikuwa picha halisi ya kuwa Abner kweli
alikuwa anataka amani Jambo hili lilimpendeza Daudi, hata hivyo Daudi hakuwa
anahitaji sana Nguvu ya Abner kwani vijana wa Daudi walikuwa wameshaonyesha
uwezo mkubwa sana kivita kumzidi yeye ona
2Samuel2:14-17 “Abneri akamwambia Yoabu,
Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya!
Na waondoke. Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi
na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na
wawili wa watumishi wa Daudi. Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa
chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata
mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni. Vita vile
vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli,
mbele ya watumishi wa Daudi.”
Hata hivyo swala la kuwa na amani
ya pamoja lilikuwa ni wazo zuri na mapenzi ya Mungu hivyo Daudi alilikubali na
alimkubali Abneri kama mtu mwenye akili na mwema na aliyekubali kushindwa na
kukubali mpango wa Mungu.
Kufa afavyo Mpumbavu!
Abneri alikuja Hebron ili aweze
kuonana na Daudi na kufanya patano naye 2
Samuel 3:20-23 “Basi Abneri akamwendea Daudi huko
Hebroni, na watu ishirini pamoja naye. Daudi akamfanyia karamu Abneri, na watu
wote waliokuwa pamoja naye. Kisha Abneri akamwambia Daudi, Nitaondoka, niende
zangu; nami nitamkusanyia bwana wangu mfalme Israeli wote, ili wafanye agano
nawe, ukamiliki juu ya wote inaowatamani roho yako. Basi Daudi akamruhusu
Abneri; naye akaenda zake kwa amani. Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na
Yoabu walitoka jeshini, wakaleta mateka mengi pamoja nao; lakini Abneri
hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda
zake kwa amani. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika,
watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme,
naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani.”
Daudi aliamini kuwa yalikuwa ni
mapatano ya kweli na kuwa Abneri sasa anakwenda kuwakusanya watu kwaajili ya
Daudi ili wafanye patano naye na kumfanya mfalme kwa njia ya amani, Hata hivyo
Kamanda mkuu wa majeshi ya Daudi alikuwa hayuko wakati hilo likifanyika na kwa
medani za kivita Yoabu hakuamini kuwa Abneri alikuwa na nia ya dhati ya kufanya
hivyo yeye alikumbuka kuwa huyu ndiye alikuwa mpinzani mkubwa wa kuzuia kusudi
la Mungu na iweje leo aweze kuwa mwema aidha Yoabu alikuwa na ufahamu kuwa
Abneri pia alikuwa na kisasi cha damu ya kumuua Asaheli Ndugu yake, Yoabu
alisikitika kuwa ni kwanini Abneri amekuja na Daudi anamuachia aende zake kwa
amani inawezekanaje mtu mwenye nia ovu kesho akawa na nia njema? Hivyo Yoabu
aliagiza kuwa Abneri arudi akidhani ya kuwa ameitwa tena na Daudi kumbe Yoabu
alitaka kujilipizia kisasi kwaajili ya Ndugu yake ona
2Samuel 3:24-27 “Basi Yoabu akamwendea
mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu,
naye amekwisha kwenda zake? Wewe wamjua
Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako,
na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi,
akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini
Daudi alikuwa hana habari. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu
akamchukua kando hata katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga
mkuki wa tumbo huko, hata akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake.”
Tukio hili lilimsikitisha sana
Daudi, kwani lingeweza kuhesabika ya kuwa amechukua ufalme kwa upanga, hata
hivyo Daudi alifahamu kuwa Abneri hakuwa na nia ya uovu, hivyo alilaani vikali
tukio la Yoabu. Na kumlaani Yoabu pamona na nyumba yake kwa kumuua mtu ambaye
alikuwa anataka amani, Daudi aliitisha mbiu ya maombolezo lilikuwa ni tukio la
kusikitisha sana Hata hivyo katika maombolezo hayo Daudi hakumlaumu yeyote bali
alimlaumu Abneri mwenyewe kwa kufa kipumbavu ona
2Samuel 3:28-34 “Hata baadaye Daudi
aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za Bwana,
kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri; na imwangukie Yoabu kichwani pake,
na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye
kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka
kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula. Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua
Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni.
Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo
zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata
jeneza. Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia
kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia. Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri,
akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu? Mikono yako haikufungwa, Wala
miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo
ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia.”
Kwa nini Daudi amsikitikie Abneri
kuwa amekufa kipumbavu? Hii ni kwa
sababu Abneri aliuawa pembeni kidogo tu ya lango la mji wa Hebroni, Mji wa Hebroni ulikuwa ni mji wa makimbilio, miji ya
makimbilio ilikuwa ni miji maalumu iliyotengwa kwaajili ya kutunza uhai wa mtu
aliyeua kwa bahati mbaya, Abneri alikuwa amemuua Asaheli hivyo ilikuwa rahisi
kwa mtu mwenye kutaka kisasi cha damu ya ndugu yake kumuua na mahali sahihi na
salama ni kwenye moja ya miji ya makimbilio na Hebron ulikuwa ni mojawapo ya
miji hiyo, hii ni miji ambayo muuaji angekimbilia humo angekula angevaa na
kuishi salama miji hii iliwekwa na Mungu kwa sababu hiyo!
Hesabu 35:9-16 “Kisha Bwana akanena na
Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa
Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya
makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia
kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio,
kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata
atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa
kwenu ni miji sita ya makimbilio. Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya
Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni
miji ya makimbilio. Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana
wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali
ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika
yake atauawa.”
·
Ni miji iliyowekwa na Mungu kwaajili ya usalama
wa kila mtu.
·
Ni miji iliyowekwa na Mungu kwaajili ya kupate
neema ya kutokuuawa
·
Ni miji iliyowekwa na Mungu ikiwa na mamlaka ya
kuokoa
·
Ni miji iliyowekwa na Mungu kwa makusudi ya
kutunza uhai
·
Ni miji Iliyokuwa maarufu na iliyojulikana sana
na kila mtu aliijua
·
Ni miji iliyowekwa na Mungu kutoa mahitaji ya
kutosha kwa kila anayekimbilia
·
Ni miji iliyokuwa imeandaliwa kwa maelekezo ya
Mungu
·
Ni miji ambayo njia zake hazikufungwa
·
Miji hii ilikuwa sita tu katika nchi nzima ya
Israel
1. Kadesh – maana yake Haki
2. Shekemu – mabega maana yake nguvu za Mungu
3. Hebron -
maana yake Ushirika
4. Bezeri – maana yake Ngome
5. Ramoth – maana yake juu
6. Na Golan – Maana yake Furaha
Kwa hiyo ilihitajika hatua moja
tu kujikinga ndani ya mji wa Hebron, kwa mtu aliyekuwa shujaa, aliyepigana vita
vingi sana, jemadari, anakujaje kufa wakati wa amani tena hatua chache tu
kutoka lango la mji unaoweza kuokoa, tena akiwa na silaha zake, tena akiwa
hajatiwa pingu, tena akiwa hajafungwa miguu wala mikono, tena akiwa hajachukua
tahadhari ya aina yoyote, Komandoo
anawezaje kufa kirahisi namna ile, kimsingi yako mambo ambayo yako katika uwezo
wetu ambayo tulitakiwa kuchukua hatua moja tu na hiyo ingetuweka mahali salama,
Mungu ametupa Mwokozi, ametupa Yesu Kristo aliye haki yetu, aliye na nguvu za
kiungu za kutusaidia ambaye anahitaji ushirika na kila mtu, ambaye ni ngome
imara, ambaye yuko mkono wa kuume wa Mungu mbinguni ambaye ni furaha yetu, yuko
tayari kutoa neema kwa kila mtu, yuko tayari kuokoa, yuko tayari kutuhifadhi na
kutunza uhai wetu, anatoa kila kitu ni msaada ulio karibu, yuko tayari
kumsaidia kila mtu hata bila kujali umefanya dhambi kiasi gani yuko tayari kusamehe
na kukuhifadhi ni kifo cha kujitakia kufa bila kumpokea Yesu, ni aibu kukaa
karibu na injili na kushindwa kuchukua hatua moja tu itakayostawisha usalama
wako milele, ndani ya mji yuko mfalme ambaye anataka amani na wewe anakuamini
hata kama watu hawakuamini, iweje leo ushindwe kuchukua hatua, ndugu yangu ni
aibu ni kufa kipumbavu kama tutashindwa kumtumia Yesu aliyetupa kila kitu
katika maisha yetu, ni hatua moja tu ya maombi, ni hatua moja tu ya kufunga, ni
hatua moja tu ya kukumbuka kuwa liko lango la Hebron ni kuingia tu hakuna wa
kukuzuia hupaswi kufa kipumbavu! Na
huwezi kuwa salama nje ya mji wa makimbilio! Kamanda mwenye akili na mwenye
kujua mapenzi ya Mungu na mtu ambaye aklikuwa na nguvu na mzoezu wa vita
ilikuwaje akafa kipumbavu, leo hii yako magonjwa mengine kama yakituua ni kwa
sababu tumejitakia, maandiko yanasema kila atakayeliitia jina la Bwana
ataokoka, tena yanasema nimekukimbilia wewe bwana nisiabike milele, mtu mweye
akili na hekima kama wewe huwezi kuangamia ilihali unajua ya kuwa Yesu ni
kimbilio na msaada wetu, heri leo kama utayatoa maisha yako kwake na kukubali
msaada mkubwa utokao kwake !
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni