Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina
lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa
hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa
kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi
habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri
katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao,
wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”
Utangulizi:
Mojawapo ya wahubiri wakubwa sana
waliokuwa na mvuto wa kipekee katika nyakati za Kanisa la Kwanza sambamba na
Petro (Kefa) na Paulo Mtume alikuwa
ni Apolo, Muhubiri huyu wa injili na Mwalimu mbobevu aliyekuwa na mchango mkubwa
sana katika kanisa alikuwa na uweza wa kipekee kiasi cha kuwekwa katika kiwango
kimoja na Mtume Petro na Paulo katika kanisa la Korintho huku akisifiwa kama
mtu aliyemwagilia maji mbegu iliypandwa na Paulo katika kanisa la Korintho, sio
hivyo tu watu walijivunia na kujisifia muhubiri huyu katika makundi
1Wakorintho 3:21-23 “Basi, mtu ye yote na
asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au
Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile
vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.”
Biblia inamuelezea Apolo kama
moja ya wahubiri aliyekuwa na neema ya juu katika ufundishaji na kwamba alikuwa
ni Myahudi kutoka Alexandria nchini Misri, aliyekuwa na uwezo mkubwa sana
katika kunena, Hodari wa maandiko, mwenye ujuzi wa kina katika Agano jipya anatajwa
kuwa muhubiri maarufu na mwalimu aliyebobea ambaye ana mchango mkubwa katika
kanisa la karne ya kwanza, akitajwa kama mtu wa Elimu yaani msomi mtu huyu leo
ana kitu ambacho tunaweza kujiufunza kutoka kwake na tutajifunza kwa kuzingatia
vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Apolo Aliyekuwa Hodari katika maandiko.
·
Mchango wa Apolo katika Kanisa la kwanza.
· Mambo ya kujifunza kutoka kwa Apolo.
Apolo Aliyekuwa Hodari katika maandiko.
Apolo ni mojawapo ya wahubiri
mashuhuri wa nyakati za kanisa la Kwanza ambaye mwandishi wa Injili na Historia
wa nyakati za Kanisa la Kwanza Luka anashindwa kuacha kuzungumza habari zake,
Muhubiri huyu na Mwalimu mashuhuri anatajwa katika kiwango cha juu pamoja na
Paulo, Petro na yeye mwenyewe, hii inaonyesha wazi kabisa kuwa hakuwa mtu wa
kuchukuliwa poa, kumbuka kuwa yeye hakuwa wala hakuwahi kuwa miongoni mwa
wanafunzi kumi na mbili wa Yesu waitwao mitume, na wala hakuwahi kuwa na Petro
wala kuambatana na Paulo, na huenda hakuwahi kuwa miongoni mwa wanafunzi
waliopata kumjua Yesu Kristo wakati wa huduma yake duniani, lakini anaelezewa
katika maandiko kuwa hakuwa mtu wa kawaida, pamoja na kuwa hatupaswi kuwa
washabiki wa wahubiri lakini uwezo wake na umahiri wake katika injili
uliwafanya Wakorintho kutokumuacha pembeni katika makundi ya kishabiki
yaliyojitokeza mwanzoni mwa huduma kwa kanisa hilo mpaka pale Paulo alipokemea
makundi hayo kwa waraka wake na
kuwaelimisha wakorintho kwamba kila mmoja ana karama yake huyu hivi na huyu
hivi:-
1Wakorintho 1:10-13 “Basi ndugu, nawasihi,
kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe
kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu
zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba
iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema,
Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa
Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je!
Mlibatizwa kwa jina la Paulo?”
Kugawanyika kwa kanisa katika
makundi ya kuwashabikia walimu wa neno la Mungu katika kanisa la Korintho
halikuwa jambo jema na la busara lakini hata hivyo limetokea kutufunulia kitu
kuwa kama Apolo aliwekwa katika kiwango kimoja au kuwa na kundi kati ya Paulo
na Petro ni Dhahiri kuwa mtu huyu hakuwa wa kawaida na hapa tunataka kujifunza
nini siri ya uwezo wake na ushawishi wake mkubwa katika jumuiya ya wanafunzi wa
Yesu Pale Korintho? Apolo ni nani hasa?
-
Biblia
inamuelezea Apolo kuwa alikuwa Myahudi, sawa na tu na alivyokuwa Petro na
Apolo, lakini huyu alikulia katika jiji la Alexandria ambao ulikuwa moja ya
miji ya kale na iliyokuwa maarufu sana kwa Elimu kule Misri ya kale, Mji huu
ulianzishwa na mfalme wa Kigiriki aliyekuwa na umaarufu mkubwa Alexander the
Great mwaka 331 Kabla ya Yesu Kristo, Mji huu ulikuwa ni moja ya mji uliokuwa
kituo kikubwa sana cha Elimu na utamaduni katika ulimwengu wa Mediteranian kwa
hiyo Apolo alikulia huko na alitokea huko
Matendo 18:24 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa
Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.”
Kwa msingi huo ni wazi kuwa Apolo alilelewa na kusomea katika jiji hilo lililokuwa na
ujuzi katika maswala ya Elimu, Falsafa, uwezo mkubwa wa mijadala, kujenga hoja
na kujibu, utaalamu wa lugha, sheria, utamaduni na uwezo wa kujitambua na
kutafasiri maandiko, Jiji la Alexandria pia lilikuwa jiji lenye vyuo vikuu
vingi vya taaluma
-
Jina lake Apolo
kimsingi ni jina la Kiyunani (Greek) “Apollōs” ambalo pia linahusishwa na jina
la mungu wa kigiriki aliyeitwa “Apollo”
au “Apaella” ambalo maana yake kwa kiingereza ni “Sheepfold” ambaye wajibu wake ulikuwa ni ulinzi wa
kondoo na mifugo Protector of flocks and herds kwa hiyo jina Apollo maana yake
ni Mlinzi wa Kondoo na wanyama wa kufugwa, hata hivyo Biblia haijasema kitu
kuhusu uhusiano wa jina lake na miungu ya Kigiriki lakini tunaweza kupata picha
ya kile ambacho jina lake linaakisi,
huyu alikuwa mtumishi wa Mungu na alikuwa muhubiri na Mwalimu mbobevu
aliyekuwa akifundisha habari za Yesu. Kweli aliwalinda kondoo!
-
Mwenye
uwezo mkubwa wa kuwasilisha kwa usahihi – Neno la Mungu linamuelezea Apolo
kama mtu aliyekuwa na uhodari na mtu anayeweza kuwasilisha kwa usahihi habari
za Kristo
Matendo 18:25 “Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa
roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za
Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.”
Kunena na kufundisha kwa usahihi kunamaanisha kuwa
alikuwa anawasilisha kwa ufasaha ujuzi
aliokuwa nao kuhusu Kristo kupitia maandiko ya Torati, mtu huyu alikuwa na
ujuzi wa maneno, elimu na uwezo mkubwa wa kujieleza kwa Kiyunani ni “Logios” kwa hiyo hakuwa mtu tu mwenye
maarifa kichwani lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwasilisha kile alichokuwa
anakijua, mtu anaweza kuwa ni Profesa au daktari wa falsafa wa jambo fulani au
hata theolojia lakini akawa hana uwezo
wa kufundisha, Mtu anaweza kuwa na maarifa mengi sana kichwani lakini
uwasilishaji wake ukawa unamfanya asieleweke kwa Apolo mambo yalikuwa tofauti
alikuwa ni mtu aliyebobea katika kujifunza, mwenye maarifa, mwenye uelewa na
anayeweza kuelezea kwa kina na sio hivyo tu alikuwa na nguvu ya ushawishi na
uwezo wa kupata kibali, jambo hili lilimfanya kuwa Mwalimu mzuri, akikubalika,
Uwezo wake mkubwa katika kufundisha unaonyesha umahiri wake mkubwa katika
kijifunza pia
-
Mwenye
kufundishika, Apolo pamoja na ujuzi mkubwa na sifa kubwa alizokuwa nazo pia
alikuwa sio mtu mwenye kiburi na majivuno, alikuwa ni mtu anayeweza kuwekeka
chini na kufundishika, wasomi wengi tulionao leo duniani ni “unteachable” wasiofundishika, Sivyo
ilivyokuwa kwa Apolo yeye kama msomi alikuwa na ufahamu kuwa huwezi kujua mambo
yote na kwa sababu hiyo elimu aliyokuwa nayo haikumpa kujivuna na unyenyekevu
aliokuwa nao ulimfanya awe tayari kupokea darasa zaidi kutoka kwa Priscilla na
Akila ambao walikuwa ni watenda kazi pamoja na Paulo mtume hawa walimualika na
kumfundisha njia ya Bwana kwa usahihi zaidi na hivyo kumfanya asaidike maradufu,
ujuzi haukumfanya ajivune! Na aliendelea kuwa Mwalimu bora zaidi
Matendo 18:25-26
“Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa
kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi
habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri
katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao,
wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”
1Wakorintho 8:1-2
“Na kwa habari ya vitu vilivyotolewa sadaka kwa
sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo
hujenga. Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama
impasavyo kujua.”
Pamoja na kuwa muhubiri mzuri na mtu mwenye elimu,
mnenaji hodari, na mwenye uhodari katika maandiko Lakini alipoalikwa na
Pricilla na Akila na kufundishwa njia ya Bwana kwa usahihi zaidi alisikiliza na
kufundishika hii ni dalili inayoonyesha
kuwa Apolo alikuwa mnyenyekevu na ujuzi haukumletea majivuno alikuwa ni mwenye
kufundishika hakusema mimi ni Muhubiri mkubwa, mimi nasimama mbele ya watu
wengi na ninasikilizwa, mimi ni msomi lakini alikubali ushauri na kuwasikiliza
wengine hii ilikuwa ni hekima kubwa kwa mtumishi huyu wa Mungu. Jambo
lililofungua mlango wa kupokea neema kubwa zaidi na kumfanya kuwa Mwalimu
aliyekubalika!
-
Apolo
alikuwa ni mtu mwenye bidii – Kadiri tunavyojifunza kuhusu Apolo unaweza
kupata picha kubwa ya aina ya mtu huyu wa kipekee inaonekana wazi kuwa alikuwa
na elimu, alikuwa na ujuzi wa maandiko, alikuwa mnenaji hodari, alikuwa na
uwezo wa kuwakilisha, alikuwa na ujuzi wa mawasiliano, alikuwa na moyo wa
huduma alikuwa anafundishika, alikuwa mnyenyekevu, alikuwa na kipawa lakini juu
ya yote hayo alikuwa na bidii, jambo lililomfanya awe muhubiri na mwalimu
mwenye matokeo, tunajifunza kuwa pamoja na kumuamini Mungu na kujifunza na
kumtumikia Mungu bado tunapaswa kuwa na bidii katika maswala yote ya kiroho
Apolo alikuwa mwenye bidii, kila mtu wa Mungu anapaswa kuwa na bidii katika
Nyanja mbalimbali za kiroho, na kimwili ili kujiongeza na ili tuweze kuwa
msaada kwa wengi, lakini zaidi sana tuweze kuwa na ufanisi katika wito
Matendo
18:24-28 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo,
mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika
maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake
ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye
alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata
Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa
usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza,
wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale
waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa
kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni
Kristo.”
-
Apolo
alikuwa Mwalimu mwenye uwezo wa kuwajenga wengine – Neno la Mungu
linaonyesha kuwa neema iliyokuwa juu yake ilimsaidia kuwajenga na wengine,
maarifa na ujuzi mkubwa aliokuwa nao haukuwa kwa manufaa yake mwenyewe lakini
alitumia kila alichokuwa nacho kuwajenga wengine jambo hili linaonyesha kuwa
kweli mtu huyu alikuwa mtu wa Mungu na alikuwa na ujuzi wa kuyatumia maarifa
aliyo nayo kwaajili ya mwili wa Kristo, kila mara sisi kama watu wa Mungu kuna
umuhimu wa kuhakikisha kuwa wengine wanafaidika na kile Mungu ametupa badala ya
kujawa na hila na wivu na umimi na kuyatumia maarifa yetu na akili zetu na
nafasi zetu kuwakwamisha wengine kwa hila na husuda, Kila mtumishi wa Mungu
mwenye afya nzuri ya kiroho anapokutana na wengine anapaswa kuwaachia athari ya
imani zaidi, maarifa zaidi, ujasiri zaidi, utakatifu zaidi, wepesi zaidi, ujuzi
zaidi, na uwezo mkuu wa kumtumikia Mungu zaidi, Apolo alikuwa ni mjenzi alipokwenda makanisani aliwasaidia sana wale
waliokwisha kuamini kwa neema, wewe umesaidia wangapi? Umeumiza wangapi?
Umekwaza wangapi?, umebomoa wangapi? Apolo aliwasaidia sana wale waliokwisha
kuamini.
Matendo 18:27.
“Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya,
ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika
akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu.”
-
Apolo alikuwa
ni mtetezi mkubwa wa imani – Moja ya wajibu wetu mkubwa tulio nao ni pamoja
na kuilinda imani na kuitetea Apolo licha ya kuwa msomi, alikuwa na mnenaji
hodari na mtaalamu wa maandiko aliutumia ujuzi wake alionao kuitetea imani na
kumuhubiri Kristo, hii ilikuwa ni kama kilele cha mukhtasari wa imani yake
alitumia mandiko kuwaelekeza watu kwa Yesu Kristo, huduma ya kweli ya kila
mtumishi wa Mungu ni kuwapeleka kwatu kwa Yesu, ni kumfunua Yesu Kristo kwa
jamii ya watu wote na kuilinda imani, ujuzi wa maandiko bila kumfunua Yesu
Kristo inakuwa ni ujuzi wa maarifa tu, lakini neno la Mungu linapomfunua Yesu
Kristo watu wanapata ujumbe kamili uliokusudiwa na Yesu na huu ndio wokovu
wenyewe, Apolo alitumia ujuzi wake
wa neno la Mungu kuwaelekeza watu kwa Yesu Kristo, na ndio ukweli kuwa maandiko
yanamfunua Yesu tu
Matendo 18:28 “Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya
watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
Yohana 5:38-40
“Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa
kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mwayachunguza maandiko, kwa
sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo
yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.”
-
Alikuwa
hodari katika maandiko – Moja ya sifa yenye nguvu na mvuto Mkubwa ambayo
Luka mwandishi wa injili na kitabu cha matendo ya mitume anaielezea kuhusu
uwezo na nguvu za Apolo ni kuwa mtu huyu alikuwa hodari katika maandiko! Ona
Matendo 18:24 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa
Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.”
Kama kuna sifa ambayo natamani kila mtumishi wa Mungu
awe nayo na tuachane na ubishi ni kuwa na ujuzi au uhodari katika maandiko kama
alivyokuwa Apolo, Luka haandiki habari za Apolo kama jambo la kushitukiza na au
la bahati mbaya Luka na timu yote ya umisheni ya Paulo walikuwa wamebaini uwezo
mkubwa sana wa Apolo na ambao una faida kubwa sana katika mwili wa Kristo. “Naye alikuwa Hodari katika maandiko” neno
Hodari linalotumika hapo katika kiyunani linatajwa kama neno “Dynatos”
ambalo kwa kiingereza ni
sawa na neno Powerful, Mighty, Strong,
au Possible likimaanisha kuwa mtu huyu alikuwa ni mwenye Nguvu, Uwezo, Mamlaka na ujuzi mkubwa katika maandiko, Apolo sio tu
alikuwa msomaji wa kawaida wa maandiko yaani Biblia, lakini alikuwa na uweza
mkubwa katika maandiko, alifahamu sana Agano la kale na alikuwa na ujuzi wa
kulifafanua kuwa linasema nini kuhusu Kristo wote tunafahamu kuwa maandiko yote
yanamtaja Yesu Kristo na kueleza habari zake kuanzia torati na manabii vitabu
vyote vinaeleza kuhusu Yesu ona
Luka 24:13-27
“Na tazama,
siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina
lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao
walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa
katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.
Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana
hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa,
akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui
yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu
wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele
za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia
katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye
ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu
yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu
walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake;
wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na
wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale
wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye
mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata
mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii
wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.”
Ujuzi huu na uweza huo na mamlaka na ufahamu katika neno la
Mungu aliokuwa nao Apolo ulimfanya awe muhubiri mwenye matokeo kokote
alikokwenda na alikohudumu na kufundisha kimsingi alikuwa ni kama Mwalimu
ambaye wakati Paulo amepanda yeye alikuja kutia maji, na kusababisha ustawi,
uweza wake katika Bwana na neno lake kulileta ustawi mkubwa sana katika mwili
wa Kristo kama watu watayajua maandiko,
na malengo yake watakuwa na msaada mkubwa kama aliokuwa nao Apolo, ujuzi
katika maandiko unasaidia katika ukuaji wa Kiroho, unasaidia kuweka muongozo wa
maisha ya kila siku, unawasaidia watu kufanya maamuzi sahihi, unawasaidia watu
kujua kwa kina na mapana na marefu ufahamu wa kina na wa ndani kuhusu Mungu,
unawatia moyo watu wakati wa mambo magumu, unawajenga watu kwa hekima,
unawafundisha watu uadilifu na maarifa unawaunganisha watu karibu na Mungu unawajengea
watu mahusiano mema, unawapa watu na kuwajengea imani, unawazamisha watu katika
kujua ahadi za Mungu, unawatia watu nguvu na kuwajenga kiroho katika maisha ya
kila siku, unawapa watu hekima na jinsi ya kufanya maamuzi sahihi,
unawafundisha watu njia za Mungu na utajiri mkuu wa upendo wake na heshima kwa
wengine, unawajengea watu matumaini wanapokuwa na hofu, huzuni na woga,
inawapunguzia watu hofu na kuwakumbusha uweza wa kiungu wa kuwalinda, unatoa
msaada wa ndani na kuleta utulivu wakati wa Magumu, kwa hiyo hii ina maana ya
kuwa mtu anayejua maandiko na namna ya kuyatumia katika maeneo hayo yote huyo
sio wa kawaida na anaweza kumsaidia mtu wa aina yoyote ile na kuwaongoza watu katika kweli huu ndio uwezo
mkubwa na wa juu zaidi wa Apolo aliokuwa nao na kwa sababu hiyo alikuwa Mwalimu
kweli kweli anayefaa kwa nyakati zote! Mungu atupe kina Apolo wengi leo
Mchango wa Apolo katika Kanisa la kwanza.
Kama tulivyotangulia kuona habari
za Apolo na uhodari wake katika maandiko jinsi ulivyo na maana, utaweza kwa
jicho la haraka kugundua pia mchango wake mkubwa ulivyokuwa nyakati za Kanisa
la kwanza ujuzi wake katika maandiko ulimfanya Apolo awe mtu mwenye mchango
mkubwa sana katika nyakati za Kanisa la kwanza
1. Aliimarisha sana wale walioamini – Matendo
18:27-28 “Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka
Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye
alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa
maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa
maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
Apolo alitumiwa na Mungu kwa neema kama mtu aliyewaimarisha sana waamini alivuka
bahari na kwenda mpaka Akaya bila shaka Macedonia kule ulaya Ugiriki na
alikaribishwa huko kwa barua na kuwa Msaada mkubwa kwa waamini, Mungu anamtumia
Apolo sio kama Mwanzilishi wa makanisa bali anamtumia kama mtu anayeimarisha kile
kilichoanzishwa Paulo mtu anaifananisha huduma ya Apolo kama mtu anayemwagilia
huku yeye akiwa kama mtu aliyepanda kwa hiyo alikuwa ni Mwalimu mwenye kujenga
umahiri wa waamini “Strengthener of the belivers”
mwenye kuwatia nguvu waamini, mwenye kuimarisha waamini!
1Wakorintho
3:5-7 “Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu
ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo
akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye
maji, bali Mungu akuzaye.”
2. Alimuhubiri Kristo - Matendo 18:27-28 “Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu
wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika
akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana
aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya
maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
Kutokana na ujuzi wake katiika maandiko aliweza
kuonyesha kupitia maandiko na kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo kwa hiyo
kitaalamu Apolo pia alikuwa au anajulikana kama Apologetic Preacher, Mwalimu aliyekuwa na uwezo wa kuitetea imani
na kuithibitisha imani kwa kutumia maandiko na kuwasaidia watu katika kumjua
Bwana na Mwokozi wetu, hili ni la Muhimu kwetu tuwaelekee watu kwa Yesu na sio
kwetu watu wamjue Yesu zaidi
3. Alitambuliwa na Paulo kama mtumishi
mwenzake – Utambuzi wa Paulo mtume kuhusu Apolo unatufundisha kuwa Muhubiri
mzuri sio wewe peke yako, inatukumbusha kuwa Mungu anaweza kuinua wengine
katika kiwango kama chako na kuzidi, na hatupaswi kuoneleana wivu, badala yake
ni lazima tukubali kuwa kila mmoja ana majukumu yake ya kutekeleza katika mwili
wa Kristo, Paulo anatambua hilo kuhusu Apolo na anasema kuwa sisi sote ni
wahudumu ambao ninyi mliamini mmoja alipanda na mwingine akatia maji na mwenye
kukuza ni Mungu, hivyo Kanisa halijengwi na mtu mmoja, Mungu huweza kumtumia
huyu hivi na mwingine akatumiwa vile kwa utukufu wa Mungu, huyu anaweza kuwa
mtume mwingine Mwalimu mwingine muhubiri na kadhalika
1Wakorintho
3:5-7 “Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni
wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda,
Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala
atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”
Paulo anasema kuwa wao ni wafanyakazi katika shamba au
jengo la Mungu na hakuna mtu mwenye kanisa
lake, au watu wake wala hakuna anayeweza kusema mimi ndiye mwanzilishi, au watu
hawa ni wangu kila mmoja ana kazi yake katika mwili wa Kristo mmoja alipanda na
mwingine akatia maji, leo hii watu wanamiliki makanisa makanisa ni mali yao na
sio mali ya Kristo wanabaguana kuwa huyu alikuwa nje ya mfumo, huyu hajaitwa
sawasawa huyu hapa ana dosari hii au ile, Paulo alimtambua Apolo na uwezo wake
na hakumpiga vita kwa sababu alikuwa na mchango mkubwa katika kanisa la Mungu,
4. Aliimarisha makanisa – Apolo alikuwa na
huduma ya Ualimu, Huduma hii ina umuhimu mkubwa sana katika kanisa la Mungu,
kwa sababu inajenga watu na kuwaimarisha na kuwafanya waamini kuwa imara,
inawalinda watu na mafundisho potofu, inawasaidia watu kumjua na kumtii Yesu
Kristo, na zaidi sana inawabadilisha waamini wachanga na kuwapa ukomavu huku ikiwaelekeza
kumtumikia Mungu na kuielewa Biblia zaidi ya yote inaandaa viongozi wa kanisa
wa baadae na kulifanya neno la Mungu liwe halisi katika maisha kutokana na
umuhimu wake alitembelea makanisa mbalimbali na kote huko aliyaimarisha na
kuwatia moyo waamini ona:-
Matendo
18:27-28 “Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka
Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye
alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa
maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa
maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
1Wakorintho
3:5-7 “Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni
wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda,
Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala
atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”
Tito 3:12-14. “Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi
kuja kwangu huku Nikopoli; kwa maana huku nimekusudia kukaa wakati wa baridi.
Zena, yule mwana-sheria, na Apolo, uwasafirishe kwa bidii, wasipungukiwe na cho
chote. Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo
lazima, ili wasiwe hawana matunda.”
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Apolo
Kuna maswala kadhaa ya kujifunza
kutoka kwa Apolo ambayo yanaweza kutuimarisha na kutujenga wahubiri wa kizazi
hiki, Apolo alikuwa msomi asiye na majivuo na mtu aliyejua kuitumia elimu yake
kwa maslahi ya ufalme wa Mungu, aidha alikuwa mtu anayefundishika na
anayekubali kuongezewa kitu na unyenyekevu wake mkubwa uliweza kumbeba niseme
katika kiwango sawa na Petro na Paulo kutajwa kwake na Luka japo kwa muktasari
lakini maelezo yake yameweza kubeba kitu kikubwa sana ambacho kinatuhakikishia
kuwa tuna kitu cha kujifunza kutoka kwake
1. Kuwa hodari katika maandiko – Apolo alikuwa
ni mwenye Nguvu, Uwezo, Mamlaka na ujuzi mkubwa katika maandiko na inaelezwa
kuwa hii ilitokana na bidii aliyokuwa nayo, kwa hiyo pamoja na mambo mengine
kila Mtumishi wa Mungu anapaswa kujifunza kutoka kwa Apolo kwamba tunapaswa
kuweka Bidii katika kujifunza Neno la Mungu ili tuweze kuwafaa na wengine, watu
wa Mungu hatupaswi kuwa wavivu katika kujifunza maneno ya Mungu badala ya
kuzurula na kusoma magazeti ya udaku tunapaswa kutulia na kuwa na bidii katika
kulihudumia neno na maombi, mtumishi wa Mungu usiwe mvivu katika kujifunza
Neno.
Matendo 6:3-4 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu,
walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya
jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno”
2Timotheo 2:15
“Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu,
mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.”
2. Kufundisha neno la Mungu kwa Usahihi –
Apolo alikuwa na juhudi na alitumia ujuzi wake na elimu yake kufundisha kwa
usahihi neno la Mungu, na tumeona pia alikubali kujifunza kutoka kwa wengine,
ni jambo la kusikitisha sana kuwa katika karne hii kuna watu wanaona kusoma
chuo cha Biblia ni ujinga, kimsingi wanamuaibisha Roho Mtakatifu kwa sababu yeye
ndiye mwanzilishi wa elimu, kuna watu hata leo wanaona kwenda vyo vya Biblia ni
kupoteza Muda, ni kupoteza upako na dhana nyingine nyingi za kipuuzi,
kufundisha kweli ya Mungu kwa usahihi kunahitaji uwe na ujuzi wa kutosha namna
ya kulifasiri neno la Mungu na sio kujitafasiria kama upendavyo tu ziko kanuni
za kuzingatia ili uweze kufasiri kwa usahihi na zinahitaji ukae chini
2Petro 1:20-21
“Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii
katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii
haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka
kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”
3. Alitumia kipawa chake kujenga wengine -
Apolo hakuitumia Elimu yake na ujuzi wake kwaajili ya majivuno au ili
aonekane alikuwa msomi hapana aliitumia kuwajenga wengine alikaa katika kusudi lile lile kubwa la huduma ambazo Mungu
ameziweka katika Kanisa kwa kusudi la kujenga mwili wa Kristo hata kazi ya
huduma itendeke hata mwili wa Kristo ujengwe na watu wakue na kufika katika
cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo
Waefeso 4:11-14
“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa
manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa
kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa
Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu
sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo
cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na
huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja,
tukizifuata njia za udanganyifu.”
Matendo
18:27-28 “Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka
Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye
alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa
maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa
maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.”
1Wakorintho
3:5-7 “Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni
wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda,
Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala
atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”
Kila mtumishi wa Mungu ana nafsi yake katika mwili wa
Kristo, lakini pia kuna nafasi ya mwingine Mwenye kazi ni Mungu, Apolo
anatufundisha kuwa Madhabahu inahitaji maandalizi, Kipawa kinahitaji kunolewa
kwa kusoma zaidi, Upako unahitaji nidhamu, Ufunuo wa kweli ni maandiko yaani
neno la Mungu, Ushawishi una mvuto mkubwa tukiwa na tabia njema kwa sababu hiyo
ni lazima tujifunze neno la Mungu, tujijengee uwezo wa kulifundisha, tukubali
kukosolewa na kuwarekebisha wengine kwa upendo, lazima tuhakikishe tunamuhubiri
Kristo, lazima tuujenge mwili wa Kristo na mwisho tumpe Mungu utukufu, Apolo
alikuwa na thamani katika Kanisa kwa sababu alitumia kile alichokijua kumwinua
Yesu Kristo na kuwajenga watu wa Mungu
Rev. Innocent Samuel Kamote.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni