Jumapili, 11 Oktoba 2026

Watu hawa wana nini, hata wakalia?


1Samuel 11:1-5 “Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi, na sisi tutakutumikia. Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea. Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.”



 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa hapa duniani kuna aina nyingi sana za uonevu na aina nyingine za uonevu kimsingi haziwezi kuvumilika!, Katika maandiko yetu ya msingi, tunapata picha ya aina hiyo ya uonevu iliyowahi kuwakuta watu wa Yabeshi-Gileadi, Mfalme wa wana wa Amoni aliyeitwa Nahashi, aliwatokea na kuwazingira watu wa Yabeshi-Gileadi akitaka kuwapiga vita, watu hao walipojipima waliona uwezo wao ulikuwa mdogo walikuwa wanyonge na wakataka amani na mfalme huyu, na kwa kuona kuwa watu hawa ni wanyonge na wanataka amani naye Nahashi mwamoni, alipata kiburi zaidi na kuwapa sharti la kikatili sana aliwataka ili wawe na amani na yeye basi Israel wote wang’olewe jicho la kulia, jambo hili liliwatia hofu sana wana wa Israel na wakaomba siku saba za kutafakari na kutafuta mtu wa kuwasaidia, walipofika mjini na hasa mji wa Sauli ulioitwa Gibea ya Sauli na kueleza taarifa hizo watu wote wakainua sauti zao wakalia, Sauli alikuwa akitokea mashambani kwa bahati alikokuwa amefuata ng’ombe na kukutana na kilio kikubwa sana na ndipo alipouliza “Watu hawa wana nini hata wakalia?“

Inawezekana unausikia ujumbe huu nawe ukiwa katika hali ya kulia  na unainua sauti yako kulia kwa sababu mbalimbali, umefanyiwa mambo ya kikatili, umedhulumiwa, umetapeliwa na mtu uliyemuamini, uko katika mateso yasiyoweza kuelezeka, unazingirwa na hali zinazokuzidi nguvu, umekata tamaa kuna maeneo unahitaji mwokozi, umefunga siku saba kutafuta msaada, uko kwenye maswali makubwa yasiyokuwa na majibu, unajiuliza msaada wako utatokea wapi, najua leo Sauli hayuko Lakini Roho Mtakatifu yupo na kwa jina la Yesu Kristo atakutokezea msaada leo Mwokozi wetu Yesu Kristo anauliza watu hawa wana nini hata wakalia? Tegemeo letu kuu na la uhakika sio wanadamu, tegemeo letu kuu linatoka kwa Mungu mwenyewe na Roho wa Mungu anaguswa na kilio chako!

Zaburi 121:1-4 “Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.”

Zaburi 124:6-8 “Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.”

Tutajifunza somo hili, “Watu hawa wana nini hata wakalia?” kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-

 

·         Kilio chako sio ishara ya udhaifu!

·         Watu hawa wana nini hata wakalia?

·         Kilio chako ni mwanzo wa wokovu wako!

 

Kilio chako sio ishara ya udhaifu!

1Samuel 11:1-5 “Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni, akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi; na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi,na sisi tutakutumikia. Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea. Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.”

Nimuhimu kufahamu kuwa wana wa Israel wakati huu walikuwa ni wanyonge, walikuwa hawana uhakika wa kupata utetezi kutoka kwa wana wa Amoni, na Nahashi alikuwa anajiamini sana na kwa sababu ya uonevu aliokuwa nao aliweka sharti la kikatili kwaajili ya uonevu tu, akijua kuwa sio rahisi kutokea mtu akawasaidia wana wa Israeli, na wana wa Israel walifahamu unyonge wao hivyo walilia, kilio chao kilichojawa na huzuni hakikuwa udhaifu kwani walimpa Nahashi siku saba, wao walilia kwa sababu walimuhitaji mwokozi, waliona kuwa Nahashi,  alionyesha ukatili uliopitiliza na kuwa kama hakuna wa kumshughulikia basi ilikuwa ni aibu kubwa sana kwa taifa, kwamba watu wa mji wa Gileadi na Israel nzima kila mwanajeshi ang’olewe jicho moja la upande wa kulia,  hii ilikuwa sio tu uonevu lakini adui alikuwa anataka kuweka alama ya milele na ya miaka mingi ya kuwashinda Israel,  wangwezaje kurusha mishale wakiwa na jicho moja, tena la kushoto, wangewezaje kujikinga na ngao, wangewezaje kutumia Kombeo, walilia na kupaza sauti kwa sababu walihitaji mkombozi katika janga hili, Mungu wa Israeli kamwe hangeweza kudharau machozi yao, kilio chao kilimfikia Mfalme mpya Sauli ambaye aliposikia watu wanalia Roho Mtakatifu alimshukia kwa nguvu na kuamsha nia na hari yake ya kutaka kuwasaidia, Maandiko yanatufundisha wazi kuwa Mungu huyajali machozi ya watu wake hasa wanapokuwa katika shida zao:-

Zaburi 34:17-19 “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

Zaburi 105:13-15 “Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine. Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”

Inawezekana unausikia ujumbe huu au kuusoma ukiwa katika kuelemewa na huzuni, najua ya kuwa bila shaka unahitaji msaada wa Mungu na neno lake limeahidi kuwa anayajali machozi yako anajua maumivu yako, inawezekana machozi yako ni matokeo ya unyanyaswaji mahali, ni matokeo ya mateso mahali, ni matokeo ya dhuluma, ni matokeo ya uonevu wa pepo, uonevu wa wachawi, mateso yako ni matokeo ya majungu kazini, ni matokeo ya watu wasiopenda maendeleo yako, ni matokeo yauonevu wa unyonge wako, ni matokeo ya umasikini wako, ni maumivu ya moyo uliojeruhiwa, ni kukosa ada, ni kudhulumiwa shamba, kiwanja, nyumba, mirathi, ujane, yatima, uonevu nataka nikuhakikishie ya kuwa Mungu anasikia kilio chako anayajua maumivu yako na anayaona mateso yako, Mungu ameyahifadhi machozi yako na ameyaweka katika kichupa na bila shaka kimejaa

Zaburi 56:8-9 “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?) Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;”

Watu hawa wana nini hata wakalia?

Sauli alikuwa anarudi kutoka shambani na ng’ombe zake, hakuwa tayari kwa vita alikuwa anatokea kwenye shughuli zake za kawaida lakini alisikia watu wanalia kilio cha kukata tamaa, watu wanaombolezea macho yao, hata kabla hayajang’olewa, Roho Mtakatifu alimjia kwa nguvu mara tu aliposikia habari za mateso ya watu wake na kukatatamaa kwao, hasira yake ikamuwaka akawaambia watu wa Yabeshi-Gileadi wasilie kwani kesho watapata wokovu wakati wa jua kali yaani mchana kweupeee, leo nasema usilie, utapa wokovu wako wakati wa jua kali.

1Samuel 11:5-11. “Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi. Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja. Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu. Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa. Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema. Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.”

Mungu anafanya hivyo hata leo, Mungu anaweza kuamsha watu kwaajili yako, Mungu anaweza kukufungulia mlango, Mungu anaweza kubadilisha hali yako ya kushindwa kuwa ushindi, Mungu anaweza kubadilisha hali yako ya unyonge kuwa ujasiri, Mungu anaweza kuwatumiwa wale wanaoonekana kuwa wa kawaida kuleta wokovu, Mungu anakuahidi leo kuwa adui zako watapigwa mchana kweupee, haitakuwa kwa kificho, haitakuwa wakati wa asubuhi, wala haitakuwa wakati wa jioni ni mchana wakati wa jua kali wokovu wako utaonekana na kila mtu

Zaburi 34:15-17 “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.”

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Zaburi 136:10-12 “Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.  Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.”

Kumbukumbu 26:6-8 “Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.  Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu;”

Wakati unapokuwa unalia na unahisi kama hujaona mabadiliko yoyote usufikiri ya kuwa Mungu amekusahau, kwa sababu bado hujaona dalili zozote Roho Mtakatifu hutulia lakini huamka na hasira zake hufurika yeye ndiye anayeitwa mkono ulionyooshwa yeye atafanyia kazi hitaji lako na atatumia njia mbalimbali kukuokoa na kukusaidia lakini kumbuka mkono wake ulionyooshwa utashughulika na kila aina ya uonevu Mungu hawezi kamwe kufumbia macho aina yoyote ya uonevu kilio chako kinamgusa kuliko unavyoweza kufikiri, yeye anauliza wakati wote watu hawa wana nini hata wakalia? Na hasira zake zinawaka akisha kujua ni kwanini unalia ananyoosha mkono wake na nikuhakikishie wokovu wako utapatikana mchana wakati wa jua kali!  Wazi wazi bila kificho adui wengine hawapaswi kushughulikiwa usiku wanapaswa kuoigwa mchana kweupee ili habari zienee mapema kuwa wametandikwa huku 

Kilio chako ni mwanzo wa wokovu wako!

Watu wa Yabeshi-Gilead walipoanza kulia ndipo Mungu alipowaletea msaada na kuwapa ushindi mkubwa, watu hawa waliokolewa kabisa na aibu iliyokuwa ikiwakabili, aibu yao ikageuzwa kuwa shangwe, ni muhimu kuwa na ufahamu kuwa unapoanza kulia leo sio ishara ya kushindwa, adui zako wanaweza kudhani kuwa wamekuweza kwa sababu ya sharti gumu walilokuwekea, lakini kumbe wanakuandalia safari ya kuelekea kwenye ushindi wako,  kilio chako ni sehemu ya mwanzo ya wokovu wako itakayokuletea ukombozi mkubwa, maandiko yanaonyesha kuwa unaweza kulia usiku na asubuhi ikawa ni furaha

Zaburi 30:2-5 “Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya. Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni. Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake. Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.”    

Mungu aliyewaokoa watu wa Yabeshi ni yule yule anayeweza kukuokoa na wewe kutoka katika ukatili, dhuluma, uonevu na maumivu unayoyapitia, kilio ulicho nacho sasa au leo kitageuzwa kuwa furaha! Kaka yangu na dada yangu unayelia usikate tamaa, swali la Sauli lilikuwa ni swali kutoka kwa Mungu watu hawa wana nini hata wakalia? Swali hili linajibiwa na Mungu mwenyewe yeye ndiye anajua ni kwa nini unalia, anayajua maumivu yako anaujua uchungu wako na yuko tayari kuingilia kati machana wa jua kali Bwana analeta wokovu! Mungu wangu aliyenilinda mimi na watu wabaya akamtuma malaika wake na kunitetea siku zote za maisha yangu atakutetea nawe pia katika jina la Yesu Kristo mwana wake aliye hai amen! Watu hawa wana nini hata wakalia?

Zaburi 56:8-11 “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?) Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu; Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?”

 

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.

Hakuna maoni: