Jumapili, 18 Oktoba 2026

Kujengwa kwa Hekalu bila kelele!


1Wafalme 6:7. “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.”      

         


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Ujenzi wa hekalu la Mungu lililojengwa na mfalme Sulemani unatufundisha mojawapo ya kanuni muhimu sana inayohusiana na kazi ya Mungu hususani katika Kanisa lake, Kwamba Mungu anataka kazi yake ifanyike kwa utulivu bila kelele lakini ikifanyika katika viwango vikubwa sana na vyenye ubora wa hali ya juu, huku kila kitu kikifanyika kwa utaratibu na hekima ya hali ya juu, Hatupaswi kamwe kuchanganya kelele na maendeleo, kazi kubwa na njema zaidi hufanyika mahali ambapo hakuna kelele! Hivi ndivyo Hekalu lile lilivyojengwa!

1Wafalme 6:7. “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba”

Teknolojia ya ujenzi iliyotumiwa na mafundi wa Suleimani ilikuwa ni ya ajabu na yenye uwezo mkubwa sana, Mafundi walionyesha weledi, uhodari na ustadi kwani walilijenga Hekalu kwa ubora wa hali ya juu sana kiasi ambacho Hekalu hili liliiingia katika idadi ya mojawapo ya maajabu ya kale sana ya dunia, lilikuwa bora na zuri lakini mojawapo ya jambo la kushangaza na la kuvutia sana ni kuwa ujenzi wake ulitawaliwa na utulivu mkubwa na wa hali ya juu, ma tunataarifiwa kuwa chombo chochote cha chuma, kama nyundo, shoka na vinginevyo havikuhusika katika ujenzi, Kwa hiyo Suleimani alihakikisha ya kuwa zinakuwako sehemu kuu mbili moja ni Mgodini au machimboni huko ambako mawe yalikuwa yanachongwa  na eneo la ujenzi ambako mawe yalikuja kupachikwa bila kelele, tukuo hili la kushangaza linatufundisha nini, leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu kujengwa kwa hekalu bila kelele kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Kwa nini Hekalu halikuhitaji kelele

·         Maana ya kelele wakati wa ujenzi wa Hekalu

·         Kujengwa kwa Hekalu bila ya kelele

Kwa nini Hekalu halikuhitaji kelele!

Ni muhimu kwanza kufahamu kuwa Mungu katika mpango wake hakuwa ameruhusu chombo chochote cha chuma kihusika katika kutengeneza madhabahu yake, hii ni kwa sababu chombo chochote cha chuma kilikuwa ni najisi kwa sababu vyombo hivyo vilitumika kama silaha za mauaji na visingeliweza kutumika katika madhabau ya kutafuta Amani na Mungu, kwa vile chuma kilitumika maranyingi kutengenezea silaha za vita na umwagikaji wa damu, kuhusisha dhana hizo katika ujenzi wa madhabahu kungeitia unajisi madhabahu, sio hivyo tu chuma ni matokeo ya kazi ya Mwanadamu lakini Jiwe lisilochongwa kwa mikono ni kazi ya Mungu wa mbinguni

Kutoka 20:24-25 “Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia. Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi.”

Kumbukumbu 27:5-6 “Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake. Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;”

Mungu alikataza kutumia chombo chochote cha chuma kujengea madhabahu kwa sababu vyombo hivyo ni najisi, na sio hivyo tu Mungu alitaka kutufundisha kuwa wokovu ni kazi ya Mungu na sio ya Mwanadamu, kuchonga mawe kunawakilisha nguvu na akili na jituhada za kibinadamu, lakini Mungu alitaa kuonyesha kuwa wokobu na upatanisho ni matokeo ya kazi yake mwenyewe na sio sisi

Sasa wakati wa Suleimani katika ujenzi wa Hekalu Mawe yaliyotumika hayakuwa madogo na wala hayakuwa na maruturutu yaani yalikuwa yamenyooka, waliyaleta mawe hayo yaliyokuwa makubwa, na ya thamani sana ambayo yalikwishachongwa mgodini ona Mafundi wa Suleimani waliamua kuyachongea mawe hayo mbali na eneo la ujenzi lakini wakati wa ujenzi mawe yalikuwa yakipachikwa tu kulingaana agizo la mafundi:-

1Wafalme 5:17-18 “Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa. Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba.”

Mawe hayo ya thamani kubwa yalichongwa na kuandaliwa mgodini, mbali na eneo la ujenzi, kisha yakaletwa mjini wakayaweka tayari, Wajenzi wa Suleimani na Hiramu na Wagebali hawa walikuwa wataalamu maalumu wa shughuli ya ujenzi huo wa Hekalu. Inasemekana kuwa jiwe moja lilikuwa na urefu wa mita 27 upana mita 9 kwenda juu mita 13, sawa na madarasa matatu ya kusomea. Kwa kuwa ujenzi huu wa hekalu ulihitaji mawe makubwa sana Suleimani aliamuru wayachonge lakini sio eneo la ujenzi wa nyumba ya Mungu bali yachongwe chimboni, au Kware katika eneo lingine mbali na eneo la ujenzi.

Katika namna zote mbili yaani kimwili na kiroho, uzuri na ufahari na taratibu za ujenzi wa Hekalu ulikuwa ni mradi unaosimamiwa na Roho Mtakatifu maandiko yako wazi kuwa sisi ni kazi ya Roho Mtakatifu. Mradi huu kinabii ulikuwa unazungumzia Kanisa, kila mtu aliyeokoka anafananishwa na jiwe la thamani na katika maandiko sisi tunaitwa mawe yaliyo hai, tunachongwa huko duniani machimbo au kware na tunatolewa huko na kuletwa katika jengo la Mungu na kuenea katika eneo lililokusudiwa, mawe haya yalichongwa kwa agizo la mafundi waashi, na kila jiwe lilitosheleza pale lilipotakiwa!

1Petro 2:4-5 “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.”

Waefeso 2:19-22 “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”

Kila mtu aliyeokolewa ni hekalu la Roho Mtakatifu, kila mmoja ana thamani kubwa sana wote tumechongwa kwa jinsi ya kipekee mgodini na wote tumeletwa ili tuwe nyumba ya Mungu, na kuwa tumuabudu yeye na kuishi kwa amani bila malumbano wala mafarakano, kwa sababu kama mawe ya thamani kila mmoja lina thamani yake na linafaa kukaa pale lilipokusudiwa, endapo jiwe lile limekaa mahali pasipo pake au halijachongwa vizuri huko kware kama ilivyokusudiwa litasababisha kelele na kama nyundo na shoka na vyombo vya chuma vitatumika kulichongea hekaluni litatia unajisi unaona

1Petro 2:4-5“Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”        

1Wakorintho 3:16-17 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.”     

1Wakorintho 6: 19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

Kwa hiyo tunakubaliana na maandiko kuwa kila aliyeokolewa ni Hekalu la Roho Mtakatifu na kwa umoja wetu ni jengo la Mungu na kila mmoja ni jiwe la thamani lililochongwa kwa ustadi, kutoka katika mgodi au kware ya giza iliyoko duniani na kuletwa na kuungamanishwa na Yesu Kristo ambaye ni jiwe kuu la pembeni, jiwe la msingi, hatujajichagua wenyewe bali ni Mungu ndiye aliyetuchagua na kutuleta katika jengo lake, ili tumtukuze yeye na tena tumuabudu yeye na kumtumikia bila ya hofu yoyote. Kwa hiyo ukisikia kelele wakati waujenzi ujue kuna jiwe limaingia mahali pasipolihusu!

Kwa nini hekalu halihitaji kelele?

Mungu amekusudia kutufanya sisi kuwa watu wake, na amekusudia kutupa utulivu, kelele asili yake ni huko mgodini, wakati wote unapotembelea mgodi au kware utasikia milipuko mikubwa ya kuvunjwa kwa mawe na mafundi wakitumia makrasha au mashine maalumu za kuvunja mawe, huko mafundi watayachonga mawe lakini yanapoletwa katika Hekalu yanakuwa tayari yanafaa kwa ujenzi, kelele zinawakilisha maisha ya duniani, kelele zinawakilisha taabu na uusumbufu wa kuwa nje ya uwepo wa Mungu, Kelele zinawakilisha hofu, kelele zinawakilisha kuwa uwepo wa Mungu umetoweka, kelele zinawakilisha hakuna ujenzi, bali kuna kuvunja vunja na kubomoa, na kuharibu.

Mahali kwenye hofu ya kifo, hofu ya utumwa hofu ya uvamizi, hofu ya uharibifu, hofu za maisha, hofu ya njaa, hofu ya kesho itakuwaje  ni mahali penye kelele  ni nje ya uwepo wa Mungu sio hekaluni, unapokuja kwenye uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu tunapata utulivu wa ajabu na amani na tunatengwa mbali na kelele. Mungu amekusudia kumtenga kila mmoja wetu na kelele na kumpa kila mmoja wetu utulivu na amani.

Hutaogopa majeshi hodari yatatapopanga vita kwaajili yako Bwana anajua kuwa wewe ni hekalu lake kwa hiyo majeshi ya upinzani yatanyamazishwa, wakati wote Mungu Kama Mchungaji wetu hutuongoza katika maji ya utulivu

Zaburi 23:1-2, “Bwana ndiye Mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabishi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza”

Israel walipomlilia Musa kwa sababu ya Majeshi ya farao yaliyokuwa yakiwafuatia kwa nyuma ili kuwarejesha tena utumwani, Musa alitoa unabii ya kuwa Bwana atawapigania nao watanyamaza kimyaa! Mungu anafahamu ya kuwa wanadamu wanahitaji utuilivu wanahitaji ukimya! Wanahitaji amani, wanahitaji kuwa mbali na hofu, wanahitaji maisha ya ushindi, wanahitaji kuthibitishiwa kuwa watakuwa mbali na kelele za kila aina:-

Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya”

Mungu atakustarehesha katika maskani yake utaburudishwa hata kutokee matetemeko, mafuriko sunami na mabadiliko yoyote yale sisi tunaokimbilia kwa Mungu kamwe hakuna atakayeogopa hakuna atakayetetemeshwa ukiwa katika uwepo wa Bwana ushindi unapatikana mapema asubuhi tu

Zaburi 46:1-5 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”

Wewe unapokuwa Hekalu la Mungu huna sababu ya kupiga kelele, wala huna sababu ya kutikisika Mungu anafahamu wazi kuwa tunahitaji utulivu, tunahitaji kuwa kimya kisha yeye ataleta ukombozi, Daudi kila alipokuwa anakabiliwa na changamoto za aina mbalimbali alikumbuka anapaswa kutulia kimyaaaa na Mungu huyu yeye mwenyewe atazimaliza kelele

 Zaburi 62:1-2 “Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.”

Wanadamu hawapaswi kusumbuka, kama umechoshwa na kelele za dunia umechoshwa na wavunja mawe, kelele za kware, kelele za migodini wewe mfanye Bwana kuwa ndio mchungaji wako, utapata kila aina ya utulivu, utaandaliwa meza mbele za adui zako machoni pa watesi wako, hutakufa, hutaogopa mauti, utafarijiwa, utapata upako, nafsi yako itahuishwa, Baraka zitafurika nawe utakaa nyumbani mwa Bwana milele yaani kwenye utulivu!

Zaburi:23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

Maana ya kelele wakati wa ujenzi wa Hekalu

Unaposikia kelele wakati wa ujenzi wa hekalu maana yeke ni nini? Kelel zinaashiria kuna uharibifu umeingia mtu mmoja alizungumza maneno haya yenye hekima kwa lugha ya kingereza “Destructive work is noisy, constructive work is silent” Kwa tafasiri isiyo rasmi ya Kiswahili “Kazi ya uharibifu ina kelele, na kazi ya ujenzi ni ya utulivu” mahali ambapo panafanyika kazi ya Mungu au panapotakiwa kuwa na uwepo wa Mungu ni mahali panapozingatia utulivu, Mahali panapofanyika kazi ya Mungu panatakiwa kuheshimiwa sana  mahali pa ibada hapatakiwi kusikika mlio wa nyundo, wala shoka wala kelele za (crashers) mashine maalumu za kuvunja mawe, mawe yakijakuchongewa Hekaluni yatasababisha kelele na kulitia unajisi hekalu, Nyumba ya Mungu sio mahali pa mazoea ni mahali panapoogopesha na panatisha, mahali maisha ya watu yanakoshughulikiwa kimwili na kiroho hapahitaji kelele wala chokochko za aina yoyote kelele na milio ya nyundo na mashoka ni ishara ya kuingia kwa unajisi

Mwanzo 28:10-17 “Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”

Kutoka 20:25 “Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi.”

Kumbukumbu 27:5-6“Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake. Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;”

Kwa hiyo unapoona kelele Katika ujenzi wa hekalu maana yake ni kuwa;-

*      Watu wameacha kufanya kazi waliyoitiwa wanafanya biashara nyingine Marko 11:15-17 “Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”

       

*      Watu wakiwa mwilini, yaani udunia ukiingia, hekalu linakuwa na kelele 1Wakoritho 3:1-7  “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.”

 

*      Watu wameingiwa na tamaa ona Yakobo 4:1-5 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?”

 

*      Kila mtu anapokuwa na nia yake 1Petro 3:8-13 “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya. Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?”

 

*      Watu wema wanaposhikamana na waovu 2Wakoritho 6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

 

*      Watu wanapoanza kuzaa matunda ya mwili Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

 

*      Watu wanapoanza kutafuta utukufu binafsi 3Yohana 1:9-10 “Naliliandikia kanisa neno, lakini Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali. Kwa hiyo, nikija, nitayakumbuka matendo yake atendayo, atoavyo upuzi juu yetu kwa maneno maovu; wala hatoshwi na hayo, ila yeye mwenyewe hawakaribishi hao ndugu, na wale watakao kuwakaribisha, huwazuia, na kuwatoa katika kanisa.”

 

Diotrefe alikuwa ni mtu mwenye tabia ya kutaka sifa na kutaka kuwa juu kwenye kila kitu cha kanisa neno apendaye kuwa wakwanza katika lugha ya kiyunani linatumika neno “Philoprōteuō” ambalo ni muunganiko wa maneno mawili “Philo” ambalo ni love au kupenda na Proteuo ambalo kwa kiingereza ni Distinction au Preeminece yaani mtu anayependa kutambulika au mtu mwenye kimbelembele, mtu anayependa kuingilia maswala yasiyomuhusu, mtu anayetafuta umaarufu hawa husababisha kelele makanisani

 

*      Watu wasiokubali matengenezo au maandalizi – Mawe yalipokuwa machimboni yalihitaji kukatwa na kutengenezwa ili likakae mahali panapolohuzu, lakini jiwe hiko halikutakiwa likatengenezewe katika eneo la ujenzi wa Hekalu, Mtu asiyekubali kubadilika na anasimamia msimamo yake tu ya zamani hata kama ni ya kipoumbavu anaweza kuwa tatizo katika kanisa na kuleta matatizo yaleyale kila sehemu anakokwenda

 

Mithali 24:3-9 “Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika, Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza. Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo; Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu. Kwa mpumbavu hekima haipatikani; Hafumbui kinywa chake langoni. Mtu afikiriye kutenda maovu, Watu watamwita mtundu; Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.”

Kujengwa kwa Hekalu bila ya kelele:

Ili hekalu liweze kujengwa bila kelele ni lazima kila mmoja wetu akubali kutengenezwa kwanza kabla ya kutaka kuonekana, Mungu alipowachagua wat kuwa watumishi wake aliwapitisha katika shule zake kwanza yaani kila mtu alikuwa na kipindi cha maandalizi kabla ya kuffikia hatua ya kuonekana au kuwa na nafasi ya utawala kwa hiyo huwei kuruka hatua ya machimbo, ukiruka hatua hiyo utatuletea kelele, tujifunze kufundishika, tujifunze kuomba, tujifunze kusikiliza, tusitake ushindi tu wakati wote, tukubali kurekebishwa, tusijijengee tabia ya kutafuta cheo, na tukiwa nacho tusijivune , tujifunze kunyamaza pale ambapo majibu sio lazima, tujifunze kusema kweli, tujifunze kuinua wengine, tusipende kutatfuta mashindan, tujijenge katika neno la Mungu tukubali kuchongwa kama mawe yalivyokuwa yanachongwa, fanya wajibu wako kwa bidi, usishindane na mtu, usitumie muda wako kufuatilia mambo yaw engine, hatujaitwa kuwa mawakala wa wengine, Mungu atatumia watu waliojengwa, Kanisa linahitaji watu wenye vipawa, lakini pia wenye tabia nzuri, linahitaji wahubiri wenye ujasiri, linahotaji viongozi walezi na wenye maono, linahitaji watu wanyenyekevu, hekaluni hakukuhityajika makelele, kwa sababu watu waliandaliwa kabla wewe ni jiwe  la namna gani?  Je utaingia mbinguni na kuwa nguzo katika hekalu la Mungu?

# Mbinguni hakutaingia chochote kilicho kinyonge

Ujenzi huu wa ajabu ambapo mawe yalikuwa yakichongwa mbali, huko kware au mgodini, yaliletwa katika kiwanja cha hekalu yakiwa yamekamilika unatukumbusha wazi kuwa shemu ya kuchongwa watu ni hapa duniani, Roho Mtakatifu hufanya maandalizi ya kutuandaa na kutuchonga tukiwa hapa Duniani, anatukarabati ndani na nje ili tufae kuwa chombo cha sifa na ibada lakini zaidi kwamba baadaye tuweze kufika Mbinguni ambako huko ni eneo la utulivu na hakuna kuchongwa tena tutaingia tukiwa tumekamilishwa baada ya kupitia mchakato wa utakatifu duniani kule mbinguni hakuna chochote kilicho kinyonge kitakachoingia,

Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”

Kila mmoja anapaswa kujiweka wakfu kwa maneno kama yale ambayo Suleimani aliyasema siku alipokuwa akiliweka wakfu Hekalu, alisema

1Wafalme 8:13 “Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Maneno ya kiingereza ya mstari huu ni matamu zaidi kwani yanasema hivi “I have indeed built you exalted house, a place for you to dwell in forever” Mungu anataka tuwe makazi yake milele. Lakini atakaa na watu ambao wameandaliwa vizuri kwaajili ya utukufu wake

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Hakuna maoni: