Jumatatu, 27 Februari 2023

Kufanyiwa nafasi wakati wa shida!



Zaburi 4:1-3 “Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.”


Utangulizi:

Leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani kuhusiana na kifungu hiki cha Zaburi 4:1-3, lakini hususani zaidi maneno Umenifanyizia nafasi wakati wa shida!  Maneno haya ni ya Muhimu sana kwetu kama yalivyokuwa ya muhimu sana wakati wa Mfalme Daudi mwana wa Yese Mbethelehemu alipokuwa akiandika maneno hayo!,  Wanatheolojia wengi sana wanafikiri kuwa huenda zaburi hii iliandikwa wakati wa mgogoro kati ya Daudi na mwanae Absalom, Lakini mimi nadhani kuwa Zaburi hii iliandikwa wakati Daudi alipokoswa koswa kuuawa na Mfalme Sauli kwa kutaka kupigwa mkuki mara kadhaa, hii ni kwa sababu Zaburi hii ni ya mapema zaidi kabla ya mgogoro wa Daudi na kijana wake Kipenzi Absalom! Hata hivyo kabla ya kuangalia kwa undani kifungu hiki ni muhimu kwetu kuligawa somo hili katika vipendele vitatu vifuatavyo:- 


·         Maana ya neno Nafasi

·         Maana ya kufanyiwa nafasi wakati wa shida

·         Kufanyiwa nafasi wakati wa shida 


Maana ya Neno nafasi

Neno nafasi linalotumika hapa lina maana pana sana inayohusiana na swala la kuokolewa katika mazingira magumu, tafasiri nyingi za kimaandiko zimetumika kulielezea neno hili katika maneno ya namna mbalimbali, mfano  King James Version imetumia neno “..Thou hast ENLARGED me when I was in distress” Biblia ya kiingereza ya English Standard Version imetumia neno “…You have given me RELIEF when I was in distress, New Language translation imetumia neno “…Oh God who DECLARE ME INNOCENT, FREE ME from my Troubles”  nyingine ijulikanayo kwa kifupi kama MSG imeandika namna hii “ …God take my side in a tight place” na nyingine imesema “…Free me from affliction  unaona unaposoma matoleo tofauti tofauti ya Biblia mbalimbali inatusaidia kupata maana halisi iliyokusudiwa kwa sababu neno NAFASI lililotumika kwenye Kiswahili linaweza kutunyima uwanja mpana wa kuelewa lile lililokusudiwa lakini kama unajua kiingereza kwa mbali sasa unatkuwa umeanza kufahamu kuwa Daudi alifanyiwa na Mungu tukio kubwa sana la WOKOVU,  Mungu ALIMKUZA baada ya kupitia shida, Mungu alimpa AHUENI baada ya kupitia shida, Mungu alimpa NAFUU baada ya kupitia dhiki, Mungu alimuhesabia HAKI, au KUWA HANA HATIA na kumuweka huru kutoka katika taabu,  unaona neno hilihilo ndilo alilolitumia Isaka alipokuwa akisumbuliwa na Wafilisti kuhusu visima vya baba yake kila alipochimba kisima walipata mgogoro na akwaachia, akachimba kingine wakaleta mgogoro akawaachia hatimaye pale walipoacha kumsumbua ndio akasema Bwana ametupa Nafasi, ahueni,  ona  


Mwanzo 26:18-25 “Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.  Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko  


unaona Isaka alipata changamoto kutoka kwa maadui zake hakupata nafuu, hakupata auhueni hakupata hata nafasi ya kumuabudu Mungu kwa kumjenge madhabahu maana maisha hayakuwa na utulivu kwa sababu alichukiwa kwa sababu alionewa wivu kwa sababu alifukuzwa kwa sababu waligombana sana sasa anapata kisima ambacho hakikugombewa na hapa anapaita REHOBOTH asili ya neno Nafasi katika lugha ya kiibrania  linakotokea neno REHOBOTH ni “RACHAB” kwa matamshi ni RAW-KHAB  au aliyeshinda changamoto kwa kiarabu RAQEEB.  Kila mwanadamu anahitaji utulivu, anahitaji nafasi, anahitaji usalama anahitaji kushinda changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo katikka maisha watu wanaweza kukuchukia pasipo sababu, unaweza kuandamwa hata na watu wenye nguvu sana, matajiri kuliko wewe, wenye mali kuliko wewe unaweza kuhisi uonevu kila mahali, unaweza kuionewa na kutafutwa na adui zako, magonjwa mateso, dhuluma bna changamoto za aina mbalimbali na unahitaji ufikie nafasi ambayo Mungu atakupa ahueni, atakupa nafasi, atakuondolea mashaka atakupa kuponyoka katika mikono ya adui hii ndio nafasi kwa ujumla inazungumzia wokovu katika kifurushi chake kamili tunahitaji nafasi! 

Maana ya kufanyiwa nafasi katika shida! 

Zaburi 4:1-3 “Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu. Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo? Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.” 

Baada ya uchambuzi wa kina hapo juu kuhusu kufanyiwa nafasi, nadhani sasa unaweza kuelewa vema zaburi hii kuwa mtumishi wa Mungu Daudi alikuwa anapitia changamoto ya aina gani, narudia tena kusema wazi kuwa changamotio yake haikuwa wakati wa Absalom bali ni wazi kabisa ukiangalia maana ya chimbuko la Neno nafasi Daudi anayodai kufanyiwa na bwana ni wazi kuwa Daudi hapa anakumbuka nanma alivyoponyoka katika mikono ya Sauli, wakati wa vita na Absalom Daudi alikuwa ni Mfalme hivyo tayari alikuwa ana nafasi, alikuwa na majemadari wajuzi wa vita na wapelelezi wa kutosha pamoja na kuwa moyo wake ulibaki ukimtegema Mungu, Lakini wakati huu alikuwa mpiga kinubi tu, alikuwa masikini bado alikuwa akijifunza maswala ya utawala alikuwa mnyonge na eti mfalme anataka kumuua kwa kumpiga mkuki maandiko yanatuonyesha kuwa sio mara moja wala sio mara mbili na katika matukio yote hayo Mungu aliingilia kati 

1Samuel 18:9-14 “Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.  Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye.” 

1Samuel 19: 10-12 “Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule. Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa. Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.” 

Ni ukweli ulio wazi kabisa kuwa ukiangalia asili ya kuchomoka kwa Daudi katika mikono ya Sauli ilifanywa na Mungu mwenyewe haikuwa akili ya Daudi,  ni mpaka Adui wa daudi walitambua ya kuwa Mungu yuko Pamoja naye, unajua kuna wakati watu wanaweza kukutafuta waklufanyie mabaya wanaweza kukusudia  mabaya dhidi yako, lakini kila wanapopanga mbinu zao na mikakati yao wanakuja kugundua kuwa unateleza kama samaki mbichi Mungu anakulinda na kukuepusha na kila kitu kibaya mpaka wanagundua ya kuwa Mungu yu Pamoja nawe!, umeona Adui wa Isaka walimfuata eee mwisho waalipogundua kuwa kila wakimdhulumu Bwana anamfanyia nafasi wakagundua kuwa Bwana yuko pamoja naye , na sauli vilevile alimuogopa Daudi kwa sababu alijua kuwa Bwana yuko pamoja naye 

Mwanzo 26: 26-30 “Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe  ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.  Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.” 

Unaona Mungu anapokufanyia nafasi anakupoa utulivu, anakubariki, anakupa amani, anakupatanisha na adui zako, anakupa kibali lakini ili nafasi iweze kupatikana ni lazima shida ziwepo, hatupendi kupita katika shida na mateso ya aina mbalimbali lakini Mungu huwa anaziruhusu kwa makusudi na mapenzi yake mema ili ziweze kutuinua na kuzalisha kitu kingine cha ziada katika maisha yetu 

Kufanyiwa nafasi wakati wa shida 

Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuwa kila changamoto unayoipitia haimaanishi kuwa Munghu hajajibu maombi yako, haimaanishi kuwa Mungu anakuhukumu kwa sababu umefanya dhambi, haimaanishi kuwa Munu hakujali lakini vyovyote ilivyo Mungu ndiye haki yetu, Na amemfanya Yesu Kristo kuwa haki yetu sisi hatuna haki yetu wenyewe, Lakini sio hivyo tu yeye ndiye Mwokozi nan i yeye ndiye mwenye haki ya kutuhukumu na sio mtu mwingine, unaweza kuwa unapitia changamoto, za aina mbalimbali na ukadhani kuwa umerogwa au Mungu amechukizwa naye au hayuko pamoja nawe inaweza kuwa una taabu kubwa sana zinakusonga adui mkubwa mara tatu zaidi yako, unatafutwa kuuawa, unajiona una nuksi, unajina una balaa, unajiona hufanikiwi unajiona umechelewa unaweza kuchoka na kujiuliza nini kinanitokea katika maisha yangu wengine wanaweza kudhani labda wameoa mwanamke mwenye mikosi au mwameolewa na abila lenye mikosi au balaa na unaweza kujiuliza maswala nini kinaendelea katika maisha yangu lakini dhiki zetu ni nafasi ni opportunity, Mungu anatupa  Nafasi itakayotupeleka katika ngazi nyingine na kutuinua, kutupa ahueni, kutupa nafuu, kutupa tahafifu, kutuponya kutuweka huru, kututangaza kuwa hatuna hatia kutupa raqeeb kutuweka panapo nafasi 

1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” 

Daudi alivumilia na kuliitia jina la Bwana katika dua zake na hatimaye Mungu alimpa upenyo, Leo nakutangazia na ninakutabiaria na ninatamka na kuzushuhudia mbingu na ardhi na kuziap[iza kwa jina la Yesu Kristo ya kwamba changamoto zako unazozipitia na shida unazipitia zikuletee mafanikio, zikuleteee amani na furaha, zikuletee Baraka, zikuletee tumaini, zikuletee nafuu, zikuleteee kibali, zikuletee ahueni, zikuletee uponyaji, zimletee Mungu utukufu, zikuletee kutoboa zikupatanishe na adui zako kumbuka kila wakati upitiapo shida kuna nafasi nasema kuna nafasi na Mungu ni mwaminifu! Utachanua katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 20 Februari 2023

Ikawa Mwanzo wa Mwaka Mpya!


2Samuel 11:1-4 “Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kifungu hiki cha maandiko kina jambo kubwa la msingi la kutufundisha ambalo mwandishi wa kifungu hiki alikuwa anakusudia kukileta kwetu! Wengi wetu tunafahamu sana habari ya anguko la Daudi katika zinaa, na tunafahamu madhara makubwa yaliyompata kutokana na dhambi hii, lakini vilevile tunaweza kukubaliana wazi kuwa Daudi alikuwa na udhaifu sawa na ule walionao wanaume wengine, kwamba aliona mwanamke mzuri anaoga akamtamani, na kuzini naye na wengi wameweza kumalumu Daudi kwa sababu mbalimbali hata ikiwa ni pamoja na kujenga Ghorofa lenye dari ya kutembelea na kusababisha kuona mke wa jirani yake ambaye alikuwa anaoga, tunaweza kuwa na sababu lukuki kuhusu anguko la Mfalme Daudi na sababu hizo zikawa na mashiko kadhaa, Lakini mwandishi wa kifungu hiki ana sababu mojawapo ya muhimu zaidi ambayo kimsingi ndio nataka tuiangalie kwa kina katika siku kama hii ya leo!

Ikawa Mwanzo wa Mwaka mpya!

Mwandishi anaanza kwa kueleza Habari ya anguko la Daudi akiwa na sababu nyingine tofauti mno Ikawa Mwanzo wa Mwaka Mpya! Wakati watokapo wafalme kwenda vitani!  Majira ya nchi katika mashariki ya kati yanafanana sana kwa kiwango kikubwa na majira ya Afrika ya mashariki, Mwezi wa Januari na February Mpaka March ndio miezi ambayo tunaweza kuyaita majira ya Mwanzo wa mwaka kunakuwa na Joto kali na ukavu wa aina Fulani, katika majira haya kwa wana wa Israel huangukia kati ya mwezi wa Abibu au mwezi (Nisani) katika majira haya ardhi huwa kame na kavu, na hivyo ndio majira ambayo wafalme wengi waliyatumia kuingia vitani kwa kusudi la kupanua mipaka ya mataifa yao, kuteka nyara, kulipisha kodi wale utakaowashinda au kulinda mipaka yako, wakati huu ulikuwa ni wakati muafaka kwa vita kwa sababu ardhi ilikuwa kavu, na hivyo iliweza kurahisisha vita vya miguu, magari ya kukokotwa na farasi lakini pia kusafirisha silaha na wanajeshi kwa urahisi zaidi kuliko wakati wa baridi na wakati wa mvua ambapo ardhi huwa na matope na vita vinakuwa ni ngumu,  wakati huu pia ilikuwa ni rahisi kuteka nyara vitu na kuvibeba kwa hiyo ilikuwa ni desturi ya Wafalme kutoka kwenda kupigana vita mwanzoni mwa mwaka mpya, Hata Mungu aliwaokoa wana wa Israel kutoka Misri katika majira kama haya.

Kutoka 12;1-2”BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu”.

Kwa hiyo wataalamu wa nyakati waliweza kuuelewa vema kuwa ulikuwa ni wakati gani na wanapaswa kufanya nini, Mwandishi anataka kutuonyesha kuwa Sababu zilizopelekea Daudi kufanya dhambi au kuanguka dhambini ilikuwa ni  pamoja na:-

1.       Aliudharau wakati – kumbe ilikuwa wazi kabisa na ilikuwa inajulikana kabisa kwamba Mwanzo wa mwaka mpya ni lazima wafalme watoke kwenda kupigana vita, Lakini yeye aliupuuzia wakati  Moja ya tatizo kubwa linaloweza kumleta mwanadamu katika anguko la maisha yake ni kutokujua kuutumia wakati, kuna madhara mengi na majuti makubwa sana kwa kila mwanadamu ambaye hakujua kuutumia wakati, wakati tuliopewa duniani ni mfupi sana na unaenda haraka mno, wastaafu wengi wanajua leo kwa sababu hawakujua kuutumia wakati, vijana wengi wanafikiri wataendelea kuwa vijana tu, wasichana wengi wanadhani wataendelea kuwa wasichana tu, wanafunzi wengi sana wanadhani iko siku watakaa ajipange na kusoma kwa bidii na sasa wengi wanalala na kupoteza muda wakifikiri uko wakati, Hakuna jambo linaumiza sana kama kuja kugundua baadaye kuwa sikuutumia wakati, nilikuwa wapi mimi? Hakuna jambo linaumiza kama kupotezewa wakati!  Kila mmoja wetu anapaswa kufahamu kuwa wakati usipoutumia vema anguko lake ni kubwa  na lenye kuleta madhara makubwa sana duniani, kwa hiyo ni vema kuutumia wakati na kutokuupuuza Yesu alilalamika kwa njia ya kinabii kwa mji wa Yerusalem kwamba utabomolewa na kuharibiwa vibaya sana na Majeshi ya warumi tukio ambalo lilitimizwa mwaka wa 70 baada ya Kristo lakini malalamiko ya Yesu kwa Yerusalem ni kwa sababu tu ya kutokuujua majira na wakati hususani Mwokozi wa ulimwengu alipowatembelea.

 

Luka 19:41-44 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”

 

Daudi alifahamu wazi kuwa ulikuwa ni wakati wa wafalme kwenda vitani lakini yeye hakwenda vitani, alibaki anarandaranda mjini tu na hiki ndio moja ya sababu ambayo mwandishi anaiona kuwa Daud alikosea!

 

2.       Aliudharau wajibu -  Kupigania watu ulikuwa ni moja ya wajibu wa waamuzi na wafalme Daudi alikuwa anawajibika kabisa kwenda vitani, huu ulikuwa ni wajibu wake na wajibu wa wafalme wa mataifa yote, ndio kuna wakati unaweza kumtuma mtu aende, Lakini mwandishi anaonyesha kuwa tatizo hapa lililopelekea habari kuwa nyingine kwa Mfalme Daudi ni kutokwenda vitani yeye alimtuma Yoabu aende, wakati mwingine ili Mungu aweze kuleta ukombozi kwa jamii ni lazima waweko watu watakaokubali kubeba wajibu, kama kila mmoja wetu akibeba wajibu wake kwa ufanisi tutaweza kuona mwanga

 

Luka 1:38 “Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.”

 

Mariam alikubali kuubeba wajibu wa kumzaa Yesu na akaleta faida Kubwa sana Duniani, walimu wakifanya wajibu wao, wanafunzi wakifanya wajibu wao, wanasiasa wakifanya wajibu wao na  wananchi wakifanya wajibu wao hakuna kitakachoshindikana, mke naye afanye wajibu wake na mume naye afanya wajibu wake kila mmoja atimize wajibu, wake kila mmoja akitimiza wajibu wake hakuna changamoto itakayojitokeza popote, Daudi alikwepa wajibu, na kudharau muda na majira aliyotakiwa kwenda vitani na matokeo yake alipatwa na anguko la kihistoria, hatuwezi kumlaumu yeye kwa sababu zozote zile kwani kuna kitu cha kujifunza kutoka kwake lakini mwandishi anatuonyesha kuwa moja ya sababu ya anguko lake ni kudharau wajibu, inapotokea kuwa shetani akatutia katika kishawishi cha kutokuzingatia kutimiza wajibu tunaweza kujikuta tunajutia maisha yetu yote na kusema laiti ningelijua kwa msingi huo ni muhimu kwetu tukatimiza wajibu, najua ziko ndoa nyingi sana zinapitia kwenye changamoto ambazo kimsingi ni kwa sababu tu watu hawataki kutimiza wajibu wao, kila mmoja akimfanyia mwenziwake kile ambacho maandiko yameagiza basi, katika jamii yetu kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu kamwe haitakuja tuone madhara na majuto baadaye timiza wajibu.

 

3.       Kupenda rahisi/au uvivu – kupenda rahisi au uvivu kuna madhara makubwa sana katika maisha yetu tunaambiwa kuwa Daudi alikaa tu onaLakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.”Maana yake alikaa tu hakufanya kazi, Daudi aliingiwa na uvivu, mtu akikaa tu bila jambo la Muhimu la kufanya, kinachofuata sasa ni kumpa ibilisi nafasi, “Idlenes gives great adavantage to the temper  Neno la Mungu linapingana vikali sana na swala zima la la uvivu, na wakati wote neno la Mungu linatutaka kupingana na tatizo la uvuvi na linawataka watu wafanye kazi likiwa na mifano mingi sana na maelekezo mengi sana mfano

 

Mithali 6:6-11 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”

 

Biblia ina la kusema kuhusu uvivu. Kitabu cha Mithali imejawa na hekima kuhusu uvivu na onyo kwa mtu mvivu. Mithali inatuambia kwamba mtu mvivu anachukia kazi:

 

Mithali 21:25 "Matakwa yake mtu mvivu humfisha, kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi."

 

Mithali 26:13-14 “Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu. Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake.“

 

Mithali 18:9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu. Newton's first law states that, “if a body is at rest or moving at a constant speed in a straight line, it will remain at rest or keep moving in a straight line at constant speed unless it is acted upon by a force”. Mwandishi anaonyesha kuwa taabu nyingine ambayo Daudi ilimpelekea kuingia katika hali hii nzito ya anguko ni kukaa tu bila kufanya shughuli 2 Wathesalonike 3:10 “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula”. Kila mmoja wetu anapaswa kuhakikisha kuwa hatumpi ibilisi nafasi, kila mmoja ahakikishe kuwa anaukomboa wakati na hapotezi muda, muda sio wa kuchezea muda ni mali, lakini wakati huo huo kila mmoja atimize wajibu wake na mwisho tuhakikishe kuwa tunapiga vita uvizu, maswala haya yalipodharauliwa na daudi yalileta anguko kwake ashukuriwe Mungu yeye alianguka katika zinaa lakini anguko baya kuliko yote ni kushindwa maisha hili linaleta majuto makubwa na machungu sana Duniani kuliko naguko la iana nyinguine lolote tunaweza kujiokoa kwa kujituma kwa bidii kwa kutumia nafasi na vipawa tulivyopewa na Mungu na kukamilisha kusudi la Mungu alilolikusudia kwetu Duniani, Neema ya Mungu na ikufunike ikiwa unataka kuishi kama Mfalme katika wakati ujao ni vema ukiyazingatia hayo!

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Waoga katika ziwa liwakalo Moto!


Ufunuo 21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya tabia ambayo inawakosesha watu wengi sana Baraka za kiungu ni Pamoja na tabia ya kuwa na WOGA, Mungu ameuweka woga kama moja wapo ya dhambi ya kwanza katika orodha ya watu watakaotupwa katika ziwa la Moto kutokana na kukosa ushindi wa kuingia Mbinguni, kama tunavyoweza kuona katika mstari wa Msingi

Ufunuo 21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

Ni aina gani ya woga inazungumzwa hapo?  Katika Biblia ya kiingereza ya New international Version neno waoga linasomeka kama COWARDLY  au katika Matoleo mengine ya Biblia kama KJV neno linasomeka kama FEARFUL kwa mujibu wa Lugha ya asili iliyotumika kuandikia agano jipya neno la kiyunani linalotumika hapo ni DEILOS kimatamshi DILOS au DEOS maana yeke ni TIMID  ambalo tunaweza kulitafasiri kwa kiingereza kama a Person who is lacking Courage, au a person who lacks endure  dangerous au a person who fear unpleasant things kwa lugha yetu tunaweza kusema Mwoga ni mtu asiye na ujasiri, au mtu asiyeweza kuvumilia mambo magumu, au anayeogopa hatari, au kuogopa mambo yasiyopendeza au ya aibu,  watu wa aina hiyo utaweza kuona kuwa katika maandiko Mungu hakupenda kuwatumia, watu wa Mungu ni kama askari  na kila mara Mungu anapotuita katika ushirika nayeye huwa anatuagiza kwamba tusiogope, Mungu anajua namna ambavyo woga ni adui mkubwa sana na urithi wetu, woga ni adui wa maendeleo, watu wenye hofu huwa hawafanikiwi sio tu katika maisha haya lakini hata Mbinguni ni vigumu kuingia kama u mwoga!

Nyakati za Biblia Mungu alipowaita watu vitani alihakikisha kuwa waoga wote wanaondolewa kwenye orodha ya wapiganaji na waliobaki walikuwa ni wale waliokuwa na moyo wa ujasiri tu, na haikupaswa wao kuogopa chochote zaidi ya kuku mbuka tu kuwa Bwana yuko pamoja nao, ilikuwa ni lazima kila mwenye sababu zinazoonyesha kuwa hafai kwenda vitani aondolewe na wale waliokwenda walitiwa moyo na kuhani na kuelekea vitani wakiwa wana muamini Mungu tu ona

Kumbukumbu la Torati 20:1-9 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu, awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;  kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi. Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine. Ni mtu gani aliye hapa aliyepanda shamba la mizabibu, wala hajatumia matunda yake? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, yakatumiwa na mtu mwingine matunda yake. Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine. Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake. Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu.”

Mungu wakati wote aliwataka watu wake wawe na moyo wa ushujaa ona katika Yoshua 1:5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”   

Yesu Kristo vile vile anawataka watu wake wawe na ujasiri na ndio maana wakati wote aliwataka wanafunzi wake wawe watu wenye kujikana nafsi lakini vilevile hakutupoa roho ya woga  ona


Luka 9:23-25 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?


Unaona wanajeshi wakati wote huwa hawayahesabu maisha yaio kuwa kitu, wanapokwenda vitani wanajua kuwa wako tayari kuyatoa maisha yao kwaajili ya taifa lao au kwaajili ya ndugu zao wanajua wazi kuwa unapokwenda vitani kuna kufa na kupona hivyo husimama kidete wakijionyesha kuwa wanaume, Kristo anataka kila mtu anayemfuata kuubeba msalaba wake na kumfuata kila siku, ziko changamoto za kila siku katika maisha yetu zinazohitaji imani yetu kwa Mungu na kwa msingi huo kamwe hatupaswi kuogopa ndio maana Mungu ametupa Roho Mtakatifu ili tuweze kukabiliana na hofu ya maisha haya ona


2Timotheo 1:7-9 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,”


Wakati wote ushindi wetu unapatikana kwa njia ya imani katika Mungu, kwa hiyo pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamwamini Mungu kiasi kwamba tunamtegema yeye kiasi kwamba hatuogopi hatari ya aina yoyote, watu wanaoogopa aibu hawawezi kufanya biashara yenye mtaji mdogo, watu wanaoogopa mitihani wanaweza kufeli hata kama mitihani hiyo ni myepesi, woga unaweza kutukosesha ushindi, 

Nyakati za ikanisa la kwanza  wakati Yohana anaandika kitabu cha ufunuo ulikuwa ni wakati ambapo watu wanaomwamini Yesu kristo walikuwa wanauawa kwa kukatwa na misumeno, kwa kuchimwa moto kama mishumaa baada ya kumwagiwa lami, kwa kukatwa kiungo kimoja kimoja, kwa kuchunwa ngozi huku wakiwa hai, kwa kufunguliwa simba wenye njaa, kwa kusulubiwa na kutundikwa misalabani, kuuawa kwa mikuki na mambo mengine ulikuwa ni wakati mbaya na w mateso ya hali ya juu, katika wakati huu watu wengine walimkana Yesu na kuachiwa huru kwa sababu ndio lilikuwa sharti kubwa ukimkana Yesu unaachiwa huru, kwa hiyo kila Mkristo alipaswa kukubali kukabiliana na kila aina ya mateso atakayokutana nayo na kuvumilia kila hatari utakayokutana nayo na kufa kwaajili ya Kristo ilikuwa ni alama ya ushindi,  wale waliomkana Yesu kutakana na mitihani waliyokutana nayo waliitwa waoga na hawa waliwekwa katika orodha ya kwanza ya watu watakaotupwa katika ziwa la Moto! Kwa nini kwa sababu walimkana Yesu na kuihesabu damu aliyoimwaga kama kitu cha hovyo, wako watu wanaogopa kumkiri Yesu hadharani, wako watu wanamkataa Yesu kwa sababu ndugu zao baba zao na mama zao ni wa imani nyingine neno la Mungu linasema waoga wote sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto, Heri leo umkubali Yesu, heri leo upokee roho ya nguvu ya ujasiri na ya upendo, heri leo ukatae mashetani na mkizimu na majini na mapepo, heri leo ukiri Yesu katika njia zako zote! 

Woga wako ndio kizuizi cha muujiza wako!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

               

Jumatatu, 23 Januari 2023

Ni nani atakayetutenga na Upendo wa Kristo?

Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu


Utangulizi:

Nyakati za kanisa la Kwanza na hata katika siku zetu za leo ni rahisi sana watu kufikiri kuwa wanapopitia mambo magumu au changamoto za aina mbalimbali hudhani kuwa labda Mungu huwa anaadhibu au anakomesha au amepunguza upendo wake kwetu, Lakini ni muhimu kufahamu kuwa hakuna kituchochote tunachokipitia ambacho kinaweza kumaanisha kuwa Upendo wa Mungu umepungua kwetu HAPANA, Paulo Mtume alikuwa anawaandikia Wakristo wa makanisa ya  Rumi na maeneo mengine ambao wakati huo walikuwa wakipitia majaribu ya namna mbalimbali na kuwataka wajifunze kuwa hakuna jambo baya linaloweza kumtokea mtu wa Mungu kisha likamaanisha kuwa  labda Mungu amemuacha ! Paulo aliandika waraka huu akitaka kuitambulisha injili anayoihubiri hasa kwa sababu alitaka kufika rumi mara kadhaa lakini shetani alimzuia, na katika kutaka kuwafikia aliandika waraka huu akiwafunulia maswala mbalimbali anayoyahubiri na pia alitaka kujibu maswali kadhaa ikiwa ni pamoja na hoja ya kuteseka kwa wakristo ili wakristo wasijenge dhana kuwa  au labda upendo wa Mungu umepungua na kuwa njia ya Mungu ni njia sahihi,  Kulikuwa na maswali kadhaa wa kadhaa kwamba mbona  sasa tumefuata njia iliyo njema lakini Serikali ya kirumi na mahakama zilizokuwepo zilikuwa na wakuu wa dini walikuwa kinyume na Imani hii, 

1.       Je kweli imani hii ni sahihi? Kweli Mungu yuko upande wetu?

2.       Kweli Mungu anasikia maombi na kukutana na mahitaji yetu

3.       Mbona watu wa Mungu wanashitakiwa?

4.       Mbona sasa watu wa Mungu wanahukumiwa?

5.       Na je njia sahihi ni kuachana na imani ?

Maswali hayo yalilitatiza sana kanisa la kwanza kwa sababu walikutana na upinzani mzito kwaajili ya injili na hivyo Mitume wliifanya kazi ya kujaribu kulijibu swali hilo kwa ufasaha  Matendo 4:1-3, 23-26

Matendo 4:1-3, “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.” 

Matendo 4:23-26 “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.” 

Kwa kadiri imani katika Kristo ilivyozidi kuenea hali ilizidi kuwa ngumu sana, kwani wakristo walipigwa kwa mawe na kuuawa na kutiwa magerezani  na hivyo kuendelea kuleta maswali mengi sana miongoni mwa wanatheolojia wa wakati ule ya kwamba imani ni nzuri lakini mbona inaleta majaribu magumu na maswali yasiyoweza kujibika ?

Matendo 8:1-3 “Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani

Dhiki na mateso, usumbufu na taabu zilizokuwa zinalikumba Kanisa la kwanza zilipelekea Mitume kujenga hoja na kujibu hoja ili wakristo waweze kuelewa kuwa kinachowatokea kina maana pana sana katika Mungu:-

1.       Wasione ni ajabu 1Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.”

               

2.       Imani huwa inajaribiwa 1Petro 1:7 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;”

 

3.       Dhiki inatuumbia uwezo wa kuvumilia Yakobo 1:2-3 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”   

 

4.       Ufalme wa Mungu  sio bei rahisi Matendo 14: 21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”

 

5.       Hakuna wa kututenga na Upendo wa Kristo Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” 

Kwa sababu hiyo ni Muhimu kufahamu kuwa kwa kadiri unavyojitoa kwa Mungu na kuendelea kuwasaidia wengine kukua katika imani na kwa kadiri siku zinavyokwenda utagundua kuwa njia ya Mungu sio nyepesi kama tunavyoweza kudhani lakini hatuna budi kuhakikisha kuwa tunafurahia wakati wote na wala hatupaswi kuhuzunika Pale Mungu wetu anaporuhusu Mambo yakawa tofauti na namna tunavyodhani, hivyo ni muhimu kuufahamu upendo wa Kristo katika kile eneo na kukumbuka kuwa wakati wote tunapopitia sintofahamu ya aina yoyote ile Mungu yuko Karibu mno kuliko tunavyodhani, usifikiri kuwa hayuko upande wetu, usifikirikuwa hatakutana na mahitaji yetu, Usifikiri kuwa kuna mwanadamu anaweza kutuhukumu, wala usifikiri kuwa Upendo wa Mungu umepungua kwetu upendo wa Mungu ni mpana sana  na wakati wote anaandaa Mambo mazuri zaidi kwaajili yetu. Hakuna lolote lenye nguvu ya kututenga na upendo wa Mungu. Wakati mwingine kwa kadiri unavyojitoa zaidi kwa Mungu ndivyo unavyokutana na changamoto zilizokubwa zaidi 2Wakorintho 11:21-33, CV ya ufalme wa Mungu inatengenezwa kwa kupitia mambo magumu na sio hizi changamoto ndogo ndogo.


Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima .


Ijumaa, 30 Desemba 2022

Ikawa mwisho wa Mwaka!


2Nyakati 24:23 - 25Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote. Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu. Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.” 



Utangulizi:

Yosia alikuwa mfalme wa Yuda aliyetawala kati ya mwaka wa 640-609 Kabla ya Kristo, jijini Yerusalem, Ni mtawala aliyeingia madarakani akiwa kijana mdogo sana, Yeye ni mwana wa Amon Mwana wa Manase ambao kimsingi walikuwa wafalme waovu mno katika wafalme waliowahi kutawala Israel ya Kusini, Lakini hata hivyo Yosia alikuwa mfalme mwema sana na aliyemcha Mungu! Yeye alitawala akiwa na miaka 8 baada ya kuuawa kwa baba yake. Mfalme huyu alikuwa mcha Mungu na alitenda yaliyo haki mbele za Mungu!

2Wafalme 22:1-2 “Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi. Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.”

Wakati wa utawala wake alifanya kazi kubwa sana ikiwa ni pamoja na kuchangisha fedha za ujenzi na ukarabati wa Hekalu nyumba ya Mungu ambayo ilikuwa na nyufa kutokana na kutokujaliwa na watu wakati wa utawala wa babu yake na baba yake, Kuhani Hilikia aligundua vilevile kitabu cha torati ambapo alipomsomea mfalme alirarua mavazi yake na kutubu, kisha kuwaita watu wote wapate kuitubu na kumgeukia Mungu, walifanya agano kuwa watamtumikia Mungu kwa mioyo yao yote kwa ujumla kulikuwa na uamshi mkubwa sana wakati huo

2Wafalme 23:1-25 “Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya Bwana. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile. Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli. Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni. Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya Bwana, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu. Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa Bwana, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera. Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji. Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa Bwana katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao. Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki. Akawaondoa farasi ambao wafalme wa Yuda waliwatoa kwa jua, hapo pa kuingia nyumbani mwa Bwana, karibu na chumba cha Nathan-Meleki, towashi, kilichohuwako kiungani; akayapiga moto magari ya jua. Nazo madhabahu zilizokuwako darini juu ya chumba cha juu cha Ahazi, wafalme wa Yuda walizozifanya, nazo madhabahu alizozifanya Manase katika behewa mbili za nyumba ya Bwana, mfalme akazivunja, akazitelemsha huko nje, na kuyatupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni. Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi. Akazivunja-vunja nguzo, akayakata-kata maashera, akapajaza mahali pake mifupa ya watu. Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera. Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la Bwana, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo. Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli. Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria. Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha Bwana, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli. Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu. Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni Bwana, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano. Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda. Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa Bwana ndani ya Yerusalemu. Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya Bwana. Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.”

Unaona ni wakati wa Yosia kwa kweli kulikuwa na uamsho mkubwa sana kila kitu cha kipagani kiliharibiwa na kila aina ya miungu iliyoabudiwa iliharibiwa, alifukuza na kuharibu wenye pepo wa utambuzi, makhanithi na wachawi, anasifika kuwa alikuwa mfalme mwema ambaye kbla yaka na baada yake hakuwahi kutokea!

Sababu kubwa ya mafanikio ya Yosia

Uwezo mkubwa na uadilifu mkubwa alioupata Yosia ulitokana na malezi mazuri na thabiti kutoka kwa kuhani mkuu maarufu sana aliyeitwa Yehoiada kuhani huyu alikuwa mwaminifu na aliweza kutumika kwa miobgo kadhaa chini ya wafalme wa Yuda, Kuhani huyu alioa dada wa Mfalme Ahazia, mwaka mmoja kabla mfalme Ahazia hajauawa, Athalia mama wa mfalme alishikwa na tamaa ya madaraka na kuamua kuua watoto wote wa kifalme na kila mtu aliyeonekana na ushawishi wa kiutawala, baada ya adhima yake hiyo kufanikiwa alijitangaza kuwa mtawala ona

2Wafalme 11;1-3 “Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme. Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa Bwana, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi.” 

Yehosheba na Mumewe Yehoiada walimficha kijana pekee aliyeponyoka katika sakata hilo ambaye ni Yosia na walimlea vizuri na ilipotimia miaka sita yaani ya kufichwa kwake hii ikiwa na maana alifichwa akiwa na miaka miwili sasa Yehoiada alifanya mpango wa kumtyawaza Yosiah kuwa Mfalme wa Yuda  ona

2Wafalme 11:4-17. “Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme. Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoingia siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya mfalme; na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo mtayalinda malinzi ya nyumba, kuzuia watu wasiingie. Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya Bwana kumzunguka mfalme. Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa Bwana. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote.Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi. Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa Bwana; akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina! Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa Bwana. Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko. Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya Bwana na mfalme na watu, ili wawe watu wa Bwana; tena kati ya mfalme na watu.” 

Unaona chini ya uangalizi wa Yehoiada, Mfalme Yosia aliweza kutawala vema na kwa mapenzi ya Mungu, kumbuka kuwa ni yeye na mkewe ndio waliomsaidia na kumuongoza na kuuondoa utawala wa malikia na kumrudisha mfalme katika kiti cha Enzi cha baba zake kama ilivyokuwa kwa mapenzi ya Mungu kwa Daudi, kupitia kuhani mkuu huyu inchi ikawa na amani na watu wakamcha Mungu mno, Yosiah katika wakati wote wa kuhani mkuu aliweza kufanya vizuri, Mfalme alikuwa na ushawishi mkubwa, aliwaongoza watu kumrudia Bwana kila mtu aliitii sharia ya Mungu, jambo hili lilimfurahisha Mungu sana na klilikuwa Baraka kubwa sana kwa kila mtu, maandiko yalikuwa yamepuuzwa kabisa lakini alipokuwa mfalme Heshima ya kimaandiko ilirejea, watu wote wenye kutoa dhabihu mbaya za watoto na kila aina ya uovu iliharibiwa kabisa kwa ujumla alikuwa mfalme ambaye aliushawishi moyo wa Mungu na Mungu alimsikiliza ona

2Wafalme 22:19 “kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekesha mbele za Bwana, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema Bwana.”

Ikawa mwisho wa Mwaka!

Pamoja na uzuri aliokuwa nao Mfalme huyu ambaye aliifanya kazi nzuri wakati wote wa uongozi wa kuhani mkuu Yehoiada ambaye aliishi miaka 130 kuhani huyu mkuu aliheshimika na watu wote kutokana na ushauri wake mzuri kwa Mfalme na watu wake alikuwa amejaa hekima ya kiungu hata hivyo jambo la kusikitisha ni kuwa baada ya kifo chake Yosia alibadilika moyo na kuanza kuwa na washauri wabaya ambao walirudisha tena ibada ya baali na maashera ona

2Nyakati 24:17-20 “Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao. Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao. Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.”

Mungu alipeleka manabii mbalimbali kwaajili ya kuwaonya hata hivyo hawakukubali, wala hawakuwasikiliza, Hata hivyo Kuhani mkuu Marehemu Yehoiada alikuwa na kijana aliyeitwa Zekaria ambaye Roho Mtakatifu alikuja juu yake ili aweze kuwaonya, Nabii Zekaria bin Yehoiada aliwaonya kuwa kama wanamuacha Bwana ni dhahiri kuwa Bwana naye atawaacha hata hivyo hawakutaka kusikia maonyo na badala yake walipanga mpango wa kumuua ona Na mfalme Yoashi alimuua zekaria akasahau wema wote ambao mama yake na baba yake walimfanyia hili lilikuwa jambo la kusikitisha sana ona

2Nyakati 24:20-22 “Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi. Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana. Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.”

Wakati Zeakaria anauawa alikumbuka wazi mema yote ambayo baba yake alimfanyia mfalme Yosia ni ukweli usiopingika kuwa Yosia alikuwa mtu asiye na shukurani hakulipa mema na badala yake alilipa mabaya Zekaria alimuomba Bwana wakati anauawa akasema  BWANA AYAANGALIE HAYA AKAYATAKIE KISASI, ni ukweli usiopingika kuwa Mungu wetu hujilipia kisasi wakati watu wanapokutendea yasiyopaswa wewe uwe na uvumilivu tu kwa dhambi hii aliyoifanya Yosia ukweli haikuchukua muda tangu wakati ule iluipofika mwisho wa Mwaka Bwana akajilipizia kisasi ndio maana tunasoma IKAWA MWISHO WA MWAKA ona

2Nyakati 24:23-25. “Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote. Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu. Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.”  

Hitimisho

Inawezekana wako watu umewawaidia lakini wamekugeuka, inawezekana umedhulumiwa, na watu hawataki kukulipa inawezekana umetukana, inawezekana umeonewa, leo nataka nikupe habari njema ya kuwa yuko Mungu anayelipa kisasi, kama maandiko yasemavyo ni haki mbele za Mungu kuwaluipa kisasi wale wanaowaonea ninyi

2Wathesalonike 1:6 – 9 “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;”

Mungu anao wakati wake wa kujilipizia kisasi dhidi ya wale wote wanaokuonea na kukutesa, kila unapopitia uonevu unayo haki ya kumwambia Mungu liangalie na hili ukalitakie kisasi na Mungu mwenyewe atausbiri wakati wake na wakati mwingine itakuwa mwisho wa Mwaka, ikawa nmwisho wa Mwaka, ikawa mwisho wa Mwaka, ikawa mwishio wa Mwaka Mungu alijilipizia kisasi dhidi ya Yosia aliyemuua Zekaria ili hali baba yake alimtendea mema hakuna sababu ya kuogopa kila aina ya uonevu katika maisha yako italipwa mwisho wa mwaka, umeonewa wewe kumbuka ikawa mwisho wa mwaka, umekopwa hujalipwa wewe kumbuka ikawa mwisho wa Mwaka, umekataliwa, mumeo au mkeo ameibiwa, ikawa mwiho wa Mwaka, umedhulumiwa paka kumbuka ikawa mwisho wa Mwaka  IKAWA MWISHO WA MWAKA   

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Jumapili, 25 Desemba 2022

Kuokolewa katika mikono ya Herode!

 


Mathayo 2:12-16 “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”



Utangulizi.

Moja ya  wafalme aliyekuwa katili sana na mroho, mwenye tamaa na mbinafsi na muongo alikuwa ni mfalme Herode mkuu, kwa ujumla alikuwa ni mfalme mwenye kutisha sana, ni katili na muuaji aidha ni mwenye dhuluma, Huyu alikuwa tofauti sana na mfalme wetu Yesu Kristo, ambaye alikuja kwaajili ya ukombozi wa wanadamu, wakati Herode alikuwa na mpango wa kuangamiza na kuua, Mfalme Yesu alikuja na mpango wa wokovu, Herode alikuwa na mpango wa mateso, Yesu alikuja akileta matumaini na upendo, Herode alikuwa ni mkatili mwenye chuki na mwenye mpango wa kuangamiza, Kristo alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea tena alikuja ili watu wawe na uzima tena wawe nao tele, Katika wakati huu wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo hatuna budi vilevile katika wakati huu kujikumbusha Mambo ya msingi na ya muhimu yanayoyakabili maisha yetu na kisha kupata hekima ya kiungu namna ya kuokolewa katika mikon ya adui zetu.

Yesu alizaliwa wakati ambapo mfalme muovu na adui wa maisha yake alikuwa anatawala na mfalme huyu aliposikia habari kuwa Yesu Kristo amezaliwa ni ukweli ulio wazi kuwa badala ya kufurahi alifadhaika sana ona

Mathayo 2:1-3 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.”

Mfalme Herode aliita baraza la wazee wa kiyahudi na wakuu wa makuhani na kufanya uchunguzi wa kina, na sio hivyo tu aliwahoji mamajusi na kutaka kujua kuwa ni kwa muda gani na wakati gani sahihi mtoto huyo atakuwa amezaliwa kufuatia mwenendo ya nyota waliyoiona nani wapi, na zaidi ya yote alitaka aletewe habari kamili kuhusu huyo mtoto kwa kusudi la kutaka kumuangamiza ona

Mathayo 2:4-8 “Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.”

Ni muhimu kufahamu kuwa roho ya Herode inatenda kazi hata leo, katika ulimwengu wa kisiasa, makazini, duniani na hata makanisani, katika nyakati hizi za mwisho hatuna budi kuhakikisha kuwa wakati wote tunaendenda kwa hekima sana kwani hali halisi ya kiroho ya watu wengi imebadilika sana, wauaji wakubwa kabisa, wenye chuki, waharibifu, wabambikiaji, wasingiziaji, wenye siasa chafu, wachawi na watu wenye wivu wenye uchungu nyakati za leo hawako nje ya kanisa bali sasa wako ndani ya kanisa na hata madhabahuni, tunazungukwa na mbwa mwitu wakali huku wewe na mimi tukiwa kama kondoo tu, Bila kuweka tumaini letu kwa Mungu ni rahisi sana kujeruhiwa, kuumizwa na kutendewa kila aina ya ubaya na hata kuuawa kwa njia za ajabu au kuwekewa sumu, na watu ambao wala hatukuwahi kudhani kuwa wanaweza kuwa wasaliti na wenye kupingana na mpango wa Mungu katika maisha yetu, hali inatisha sana kwa sasa, watu wanatuma mpaka watu watushambulie, wako watumishi wa Mungu ambao sasa wamekuwa wachawi hata wokovu sijui waliuacha lini, wako washirikina pia hali inatisha hata hivyo Mungu aliye hai yuko macho na bila shaka atakuokoa na kila mpango mbaya wa ibilisi na maajenti wake katika maisha yako na yangu!

Herode alikuwa ni mtu wa namna gani?

Herode ambaye pia alijulikana kama Herode mkuu alikuwa ni mtawala wa Israel iliyokuwa chini ya utawala wa Warumi, Kimsingi yeye alizaliwa mwaka wa 72 kabla ya Kristo na kwa asili alitokea maeneo ya Idumeya yaani Eneo la Edomu wana wa Esau, Yeye na ukoo wake waliwekwa kuwa watawala vibaraka kwa niaba ya utawala wa warumi, Mwanzoni yeye alitawala Galilaya na uyahudi kabla ya utawala wa watoto wake watatu ambao waligawana majimbo baada ya kifo chake na Herode Akleo akatawala Idumeya, Uyahudi na Samaria na Herode Antipas alitawala Galilaya na Philip alitawaka huko Jordan, Kwa mujibu wa mwanahistoria maarufu wa kiyahudi wa  karne ya Kwanza Josephus, Herode mkuu alikuwa ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa sana ambaye ili kuongeza ushawishi wake alimuoa binti wa kuhani mkuu wa kiyahudi Kayafa na pia wakati wa utawala wake alilikarabati Hekalu la pili la Yerusalem na  kuliongezea eneo mlima wa Hekalu kwa upande wa kaskazini, Jambo lililopelekea yeye kukubalika na Wayahudi wengi.  Hata hivyo pamoja na umaarufu wake mkubwa hivyo ni jambo la kushangaza ya kuwa alipozaliwa Yesu Kristo Mfalme huyu alifadhaika na kugadhibika na ili aweze kujihakikishia usalama wake alihakikisha kuwa anawaua watoto wote wapatao miaka miwili kule Bethelehemu ili yamkini aweze kumuua Yesu Kristo ona

Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”

Unaweza kuona Herode alikuwa ni mtu mwenye ghadhabu, mbinafsi na aliyekuwa hataki upinzani, alitamani kuwa yeye katika madaraka wakati wote, alitamani kuwa yeye abaki kuwa maarufu wakati wote, alikuwa mtu katili aliweza kuua watoto wote ili kujihakikishia usalama wake ni jambo la kusikitisha kuwa hii roho ya Herode ni roho inayotenda kazi katika nyakati zetu na katika kanisa la leo, Mara ngapi tumesikia viongozi wakubwa na maarufu wakiwaua wengine kisiasa na kuwachafua wengine kwa skendo za kutengeneza ili yamkini waweze kubakia wao tu madarakani, au wao tu waonekane kuwa ni safi na wenguine waonekane kuwa hawafai, au kuharibu umaarufu wa wengine  na wao tu waweze kuwa maarufu, hujawaona watu wenye kila kitu na wenye nguvu zote lakini wakifukuzana na watu masikini wasio na kitu wala nguvu yoyote wakitaka kuwazima ili yamkini wabakie wao tu hii ni roho chafu na mikono mibaya ya Herode, roho ya Herode ni roho ya watu wenye uchungu, hasira na tama mbaya wakiwa wamejawa na ubinafsi wa kila aina ni roho ya watu ambao hawawezi kufurahi nyota za wengine kung’aa lakini pamoja na hayo Bwana ana ujumbe muhimu leo Usiogope Bwana amenituma nikupe ujumbe huu kama nabii wake na kama malaika wake leo nakuletea habari njema ya kuwa wakati Herode anataka kusababisha misiba katika jamii, Mungu atakunusuru wewe na atakulinda na kukupa mlango wa kutokea mpaka atakapokufa Herode, Bwana atakuficha katika mikono yake nawe utakuwa salama hutaogopa madamu Mungu anakukubali, leo ziko habari njema kwaajili yako ona Yesu amezaliwa kwaajili yako na yeye ni mwokozi sio wa mtu mmoja tu wa ulimwengu mzima na hivyo amani inapaswa kutawala duniani kwa kila mtu ambaye Bwana ana mridhia najua wewe na mimi Bwana anaturidhia   

Luka 2:8-17 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.”

Kwaajili ya hayo ni imani yangu nani mpango wa Mungu ya kuwa pamoja na changamoto unazozipitia katika huduma, kazini ndoa na maeneo mengine Mungu hatimaye atatuokoa na mipango mikakakati ya heriode katika maisha yetu

Kuokolewa katika mikono ya Herode !

Mathayo 2:12-15 “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.  Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”

Kila mtu mwenye mapenzi mema Mungu ana mpango mkakati ulio mwema na maisha yako na kwa jinsi Mungu alivyomwema anatuwazima mem, Mungu hana mpango wa kusababisha maombolezo katika maisha yetu wala hana malipizi anayotulipiza kwaajili ya maovu yetu, Mungu ni mwema mno yeye anatuwazia mema hana kisasi juu yetu yeye sio mwanadamu ana mpango mwema na mahususi kuliko mpango alionao Herode wako na wangu ona ;-

Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote..”       

Vile adui zako na zangu wanavyotuwazia sivyo Mungu anavyotuwazia nataka kuanzia Christmas hii uweze kuelewa kuwa hakuna adui anayeweza kusimama mbele yako na kupingana au kushindana na mapenzi ya Mungu yaliyowekwa ndani yako, kila baya linalokusudiwa na adui dhidi yako Mungu ataligeuza kuwa Baraka, kila adui anayekutafuta akuangamize ataangamiza wengine na wewe utajikuta umefichwa; msomaji wangu nataka nikuhakikishie yakuwa ujumbe huu ni halisi katika maisha yako hakuna wa kukupata, hakuna atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako sio kwa Herode huyu tu lakini kwa kila mkono wa Herode yeyote atakayeinuka juu yako Mungu atakuokoa na mikono yake, wakati wa Petro alikuweko herode mwingine aliyaangamiza maisha ya Yakobo mtume na akataka kumuangamiza na Petro, lakini Mungu akawa mwaminifu akamfungua Petro kutoka katika mikono ya Herode Mungu huyu huyu atakufungua na wewe   atakuweka huru na Herode wako atatokwa na roho Hakuna herode aliyewafuatilia watu wa Mungu na kuwatesa na kuwaua ambaye  alibaki salama, Herode aliyetaka kumuua Yesu alikufa Yesu akiwa amefichwa Misri na herode aliyemuua Yakobo alipotaka kumuua Petro Mungu aklituma malaika wake ona

Matendo 12:1-23 “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.  Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine. Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje Petro. Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko. Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”

Hitimisho.

Ujumbe wangu wa Chrismas hii ni unabii, ni ujumbe ambao sio tu wa sikukuu hii lakini ni ujumbe wa maisha ya siku zote wote wanaoonewa na watu wenye nyadhifa zilizokubwa kupita wao wasiogope ni ujumbe wa matumaini na kukutia moyo ya kuwa Mungu yuko na anaifuatilia mipango ya Herode na ata shughulika naye ni ujumbe wa maonyo pia kama una roho ye herode lazima utubu na kubadilika Mungu hawezi kufurahia udhalimu, kusudi lake ni pana mno na yuko tayari kulilinda kusudi lake kwa gharama yeyote wewe sio wa Muhimu kuliko wanaochipukia uwe na roho ya malezi walee wengine na kuwainua na kuwaunga mkono usijidhanie ya kuwa uko mwenyewe au kuwa wewe ndiwe maalumu sana kwa Mungu, kujenga hekalu hakutakusaidia, kuoa mtoto wa kuhani mkuu hakutakusaidia, kuwa na wapelelezi hakutakusaidia, kuwa na jeshi hakukusaidiaa kitu Mungu wetu ni mwenye Nguvu na hekima yake ni kubwa kuliko hekima ya kibinadamu, hii ni Chrismas ya wokovu nani ya habari njema kwa wote wanaoonewa na maonyo  makali kwa waonevu! Kamwe asitokee mtu akashindana na kusudi la Mungu lililoko ndani yako kwani atapotea kama walivyopotea wakina herode na kusudi la Mungu ndilo litakalosimama.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!