Mwanzo 14:14-23 “Abramu aliposikia ya
kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika
nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga
apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba,
ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na
Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka
kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma
akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki
mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu
sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba
mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi
mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Mfalme wa Sodoma akamwambia
Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme
wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu
na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho
chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”
Utangulizi:
Wale ambao wanadhani kuwa
Abrahamu alikuwa mtu wa kawaida tu aliyetembea na Mungu aliye hai na ni baba wa
Isaka na Ishmael na ni baba wa Imani ya kiyahudi, Kikristo na waislamu, na moja
ya baba wa taifa a Israel nataka watambue leo kuwa sivyo wanavyofikiria kuhusu
Abraham, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Abrahamu alikuwa ni mtu mkuu sana na
hakuwa wa kawaida, Tangu Mungu alipokuwa anamuita Abrahamu alikuwa ni mtu
ambaye amekulia mjini na ni moja ya watu waliotokea kwenye maendeleo makubwa
sana! Tunaelezwa wazi kuwa Abraham alitokea katika nchi ya Uru wa ukaldayo huko
Mesopotamia, Historia inaonyesha wazi kuwa ustaarabu wa kwanza kabisa wa
kimaendeleo ulitokea huko Mesopotamia
mahali ambapo mito mikubwa duniani mto Frati na mto Tigris inamwaga maji yake
katika ghuba ya uajemi, na mji wa Uru ulikuwa ndio mji wenye bandari na mji
uliokuwa na maendeleo makubwa sana Katika ghuba ya uajemi, na ndio kuotokea
huku Mungu alimuita na kufanya badiliko kubwa sana la maisha yake, Abraham
alitokea katika familia na mji wenye maendeleo makubwa na wala hakuwa mshamba!
Alikuwa tajiri mno na anayetoka katika mtazamo wa kimaendeleo wa hali ya juu
sana.
Mwanzo 13:2-6 “Naye Abramu alikuwa ni
tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka
kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli
na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu
akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye
alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili
wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.”
Unaona licha ya kuwa amekulia
kwenye mji mkubwa na uliokuwa na maendeleo makubwa sana Abraham aliitii sauti
ya Mungu ya kumuita kwenda katika nchi atakayomuonyesha yaani nchi ya kanaani,
Maandiko pia yanatuonyesha kuwa Abraham alikuwa tajiri sana Kiswahili kinasema
tajiri sana lakini biblia ya kiingereza ya Berean
Standard Bible inatumia neno HAD
BECOME EXTREMELY WEALTHY, Extremely rich yaani alikuwa tajiri kwelikweli,
alitajirika kupitiliza! Maandiko yanasema mpaka inchi ile haikuwatosha Yeye na
Lutu ili wakae pamoja maana mali zao zilikuwa nyingi!
Kwanini Bibia imetumia neno Extremely rich au tajiri sana, katika Biblia ya kiebrania
neno hilo tajiri sana linasomeka kama KABAD
KABED linatamkwa kaw-bad kaw
bade ambalo tafasiri yake kupita
kawaida, utajiri mzito, utajiri uliopitiliza, utajili uliotukuka, utajiri wenye
kuleta heshima utajiri wenye kuonyesha uungwana, kuinuliwa mno, utajiri mzito
sana strong concordance imetumia pia neno grievous na severe kwa lugha ya mtaani ni UTAJIRI
WA KUFA MTU na kama haitoshi
tunaambiwa wakati Lutu anatekwa na jumuiya ya wafalme walioungana Abraham alikwenda na jeshi lake la vijana
wapatao 318 na kusambaratisha wakorofi na kumuokoa Lutu
ile opereshini ya kijeshi mimi ninaiita Operation Lot yaani ilikuwa vita ya
kumkomboa Lutu, ona hapa kwanza
Mwanzo 14:14 “Abramu aliposikia ya kwamba
nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba
yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani.”
Je unapata picha ya aina gani hapo?
Abraham alikuwa Mfalme, He was a Prince,
Abraham alikuwa ni serikali kamili, alikuwa na meneja, alikuwa na waajiriwa,
alikuwa na Jeshi, alikuwa ni mtu mkubwa sana, alikuwa na wapelelezi, nani
walimpa taarifa kuwa Lutu ametekwa? Alikuwa na waandishi wa habari, alikuwa na
silaha, alikuwa na benki yenye akiba ya fedha na dhahabu,alikuwa na wapelelezi,
kwa hiyo nini maana yake pia Abraham alikuwa na moyo wa ukarimu alikuwa tajiri
moyoni na alikuwa mtu mkubwa anayetembea, serikali inayotembea, ufalme
unaotembea, alistawi sana kwa hiyo huwezi kumtishia Abraham kwa habari ya mali,
na utajiri wa ulimwengu huu kwa kuwa alikuwa na kila kitu! Na mali
hazikumuendesha hata kidogo, aliheshimu watu wote wakubwa kwa wadogo na
kusimamia haki, ufahamu wake ulikuwa mkubwa na wenye mtazamo mkubwa wa
kimaendeleo kutokana na mji alikotokea, Mesopotamia nchi ya mito miwili, nchi
yenye rutuba na ustaarabu mkubwa wa mwanzo. Abrahamu hakuwa limbukeni, wala
hakuinua mabega yake na kujiona mungumtu pale Mungu alipombariki kwa mali
nyingi!
·
Kiini cha mafanikio na utajiri wa Abraham.
·
Kiini cha mafanikio na utajiri wa Wakristo.
·
Sitatwaa chochote kilicho chako!
Kiini cha mafanikio na utajiri wa Abraham.
Mungu alikuwa amekusudia
kumbariki Abraham tangu mwanzo na kwa kawaida Mungu akiisha kukubariki
mafanikio mengine yote ya kimwili na kiroho yanakuja kutoka kwake, Lakini
lazima iwepo Baraka kwanza, Baraka hizo ndio zinazoleta ufunguo wa mafanikio na
utajiri hata ule unaoonekana kwa macho, Mithali
10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala
hachanganyi huzuni nayo.” Abraham alikuwa mtu aliyebarikiwa mtu
aliyebarikiwa kwanza huwa na amani, huwa na afya nzuri, huwa na furaha, huwa na
upendo, huwa na ukarimu huwa na moyo wa kitajiri, hujaa fadhili, hujawa na
utulivu na huzingirwa na ulinzi wa Mungu, Mungu hufanyika ngao kwake na Mungu
huwa ndio thawabu yake kubwa sana na mtu huyo huwa mbali na hofu, kabla ya
utajiri huo wa nje ndani ya mtu kunakuwa na baraka za Mungu hivi ndivyo Abraham
alivyobarikiwa sana
Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu,
Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka
nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki,
na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye
akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
Mungu ndiye aliyekuwa sababu ya
Baraka kubwa sana alizokuwa nazo Abraham, kwa hiyo kiini cha mafanikio na
utajiri wa Abraham ni Baraka kutoka kwa Bwana, ulinzi na usalama na kila
alichokuwa nacho kilikuwa ni kwa sababu Mungu alikuwa amembariki, zaidi ya yote
Mungu alimtuma askofu mkuu wa Yerusalem (Kuhani Mkuu) ambaye alikuwa kuhani,
mfalme na nabii ambaye alikuja kumtamkia Abraham Baraka kubwa sana hata
alipokuwa ametoka kwenye operesheni komboa Lutu ona askofu huyu aliitwa
Melekizedeki ona
Mwanzo 14:18-20 “Na Melkizedeki mfalme wa
Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki,
akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe
Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu
la kumi la vitu vyote.”
Unaona Melkizedeki kuhani wa
Mungu aliyejuu sana, alikuja kumlaki Abraham alipokuwa ameshinda vita, akatoa
huduma ya kiroho kisha kwa mamlaka aliyokuwa nayo kama kuhani alimbariki
Abraham, lakini akiwa na ujuzi kuwa hata ushindi wa Abraham yaani adui zake
kutiwa mikononi mwake kumetokana na Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwa hiyo Melkzedeki alimbariki Abraham huku
akiwa na uelewa kuwa kila kitu hata ushindi ule mkubwa kwa Abraham ulitokana na
Mungu, yaani ilieleweka wazi kuwa ukuu wa mtu huyu, nguvu na utajiri umetokana
na Mungu sijui wewe kama watu wanajua kuwa Mungu amekubariki au moyo wako
unajua kuwa umeiba? Heshima uliyo nayo umepewa na Mungu au umeipata kwa
majungu, fitina na ujanja ujanaja? Lakini chanzo cha Baraka na mafanikio yote
ya Ibrahimu ilikuwa ni Bwana Mungu wake na sio vinginevyo!
Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo neno la
BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao
yako, na thawabu yako kubwa sana.”
Mungu akifanyika thawabu yetu
kubwa sana na kuwa ngao katika maisha yetu tutakuwa na mafanikio yenye ustawi
katika kila eneo la maisha yetu kimwili na kiroho, Amani itatawala na mafanikio
yatatatwala na tutakuwa ni wafame katika ardhi ya dunia tukiwa na afya njema,
Amani na furaha na utulivu, huku tukiwa
wasimamizi wa haki na watetezi wa wanyonge na majibu ya wenye uhitaji, Bwana
ampe neema kila mmoja wetu kuwa na mafanikio makubwa sana na utajiri mkubwa
sana ambao Bwana ndio chanzo na kiini cha utajiri huo!, Mungu alimbariki hivyo
Abraham sio kwaajili yake tu na kwaajili ya mafanikio ya ulimwengu mzima na
kila anayemkubali Abraham na Mungu anayejitambulisha Duniani kupitia Abraham na
mtoto wake wa ahadi yaani Bwana wetu Yesu Kristo!.
Kiini cha mafanikio na utajiri wa Wakristo.
Kama iivyokuwa kwa baba Yetu
Ibrahimu baba wa Imani mafanikio na utajiri wa kila Mkristo kiini chake Ni
Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo, na Baraka ile kubwa iliyokusudiwa kwa
ulimwengu yaani Yesu Kristo, kila anayemuamini Yesu anapaswa kufahamu kuwa yeye
ndio chanzo cha Baraka zetu, yeye ni kiini cha Mafanikio na utajiri Duniani kwa
nini kwa sababu kwanza sisi ni warithi wa Baraka zote za Abraham!
Wagalatia 3:26-29 “Kwa kuwa ninyi nyote
mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote
mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana
mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja
katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu,
na warithi sawasawa na ahadi.”
Unaona Mungu amekusudia kumbariki
kila mtu anayemuamini Yesu bila kujali historia yake na kumfanya kuwa mrithi wa ahadi na uzao wa
Abraham kwa njia ya Imani, kwa hiyo kila mkristo amebarikiwa tayari, na hazina
zote za utajiri zimekwisha kuwekwa wazi katika ulimwengu wa roho.
Waefeso 1:3-5 “Atukuzwe Mungu, Baba wa
Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika
ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye
kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia
mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe
kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.”
Kila mtu aliyemwamini Bwana Yesu
na kazi yake iiyofanyika pale msalabani amebarikiwa katika ulimwengu wa roho,
wewe na mimi tuna Baraka zote za rohoni tayari kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni
kuzitafasiri Baraka hizo za rohoni ili kwamba ziweze kuonekana na kudhihirika
katika ulimwengu wa mwili na ziko kanuni muhimu za kuzingatiwa
1.
Kiini
cha Baraka zetu zote za rohoni na mwilini ni Yesu kristo naye tayari
amekwisha kutubariki sasa ili tuweze kuziona Baraka zake hatuna budi kumpa yeye
kipaumbele na hili ndilo alilolifanya Abraham Mathayo 6:31-33 “Msisumbuke, basi,
mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa
huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo
yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote
mtazidishiwa.”
2.
Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote Mithali 3:5-6 “Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia
zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”
3.
Mtumikie
Bwana Mungu wako Kutoka 23:25-26. “Nanyi
mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako;
nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala
aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.”
4.
Fanya
kazi kwa mikono yako na kwa bidi kumbukumbu 28:11-12 “Bwana
atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama
wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako
kwamba atakupa. Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa
mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako;
nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.”
5.
Uwe
na moyo wa ukarimu Mithali 28:27 “Mwenye kuwagawia
maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.”
Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo
cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu
watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho
mtakachopimiwa.”
6.
Usipandishe
mabega wala kuvimba kichwa Mungu anapokubariki Daniel 4:28-37 “Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza. Baada ya miezi
kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme
akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la
kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno
lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni,
ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu
umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa
pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba
zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika
ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo
likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani
kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele
zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.Hata
mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu,
fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu
Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme
wake hudumu toka kizazi hata kizazi; na
watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama
atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana
awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe? Basi wakati uo
huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi
yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja
kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita
kiasi. Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na
kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale
waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.”
Mungu huwapinga
wenye kiburi lakini huwapa neema wanyenyekevu, wako watu tena hasa wale
wanaotoka kwenye hali duni zaidi wanakuwa malimbukeni kweli kweli, Mungu
akiwafanikisha wanataka dunia nzima ijue, wanavimba kichwa na kusahau kuwa
Mungu ndiye chanzo cha Baraka na utajiri wanadhani Mungu amewainua kunyanyasa
watu, wanataka watawale kila kitu katika maisha yako mpaka hatima yako watoto
wako na mkeo, wakifika eneo la tukio utasikia hiki ni changu, hiki ni changu,
hiki ni change hawarudishi utukufu kwa Mungu, kuinuliwa kwao ndio kuwanza
kupata shida kwa wengine, kuinuliwa kwao ndio kuanza kufukuzwa kwa watu
wengine, kuteseka na kusemwa vibaya sikiliza Mungu hatubariki na kutuinua ili
wengine wanyanyasike Mungu hutubariki na kutuinua ili tuweze kuwa Baraka kwa
wengine na sio kutawala maisha ya watu wengine, Mungu alimbariki Abrahamu kwa
sababu alikuwa anajua kuwa atawafaa wengine
Kimsingi maagizo yote ya kibiblia
yanayohusiana na kanuni za kubarikiwa utaweza kuyaona ndani ya maisha ya
Ibrahimu na Isaka, na kanuni za ujanja ujanja utaweza kuziona ndani ya Yakobo,
mpaka Mungu alipombariki na kumuita Israel, hakuna muujiza zaidi ya kumpata
mtenda muujiza na hakuna ufame bila kumpata mfame kama tutamuweka Mungu mbele
hakuna jambo litakalozuia mafanikio kwa mkristo awaye yote na wote
wanaomtegemea
Sitatwaa chochote kilicho chako!
Baada ya kuwa tumejifunza maswala
kadhaa ya muhimu na kanuni za Mungu za kubarikiwa na jinsi Mungu alivyombariki
Abraham sasa ni muhimu kwetu kurejea katika kiiini cha somo letu katika maneno
ya Abraham kuwa hatatwaa chochote kilicho cha mfalme wa Sodoma
Abraham aliyasema maneno haya
akimjibu mfalme wa Sodoma, Abraham alipigana vita hii akiwa na askari wake 318
sababu kuu ya kupigana kwake ni ili kumrejesha Lutu ndugu yake ambaye alikuwa
ametekwa katika vita ile, Mungu alimpa Abraham ushindi mkubwa sana kwa
kuwashinda wafalme kadhaa na alilazimika kumsaidia mfalme wa Sodoma kwa kuwa
ndiko alikokuwa anakaa Lutu aliporejea na Ushindi Mara mfalme wa Sodoma,
aligundua kuwa Abraham ana vijana hodari sana na kama akiwapata yeye haitaji
mali, kwani atapata mali kwa kuwateka nyara wafalme wengine huko vitani kwa
kutumia vijana waliofunzwa vita vyema na kwa weledi kupitia Abraham
Mwanzo 14: 1-12 “Ikawa siku za Amrafeli
mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu
na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha
mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na
mfalme wa Bela, ndio Soari3. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu,
kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka
wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme
waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi
katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu,na Wahori katika mlima wao
Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka
Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa
Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na
mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita
panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali
mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari,
wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo
ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia
wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao
vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko
Sodoma, na mali yake, wakaenda zao..”
Mwanzo 14:21 “Mfalme wa Sodoma akamwambia
Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe.”
Huenda mfalme huyu alipoona
Abraham akibarikiwa na Mfalme wa Salem naye akatoa zaka yeye alifikiri kwamba
Mfalme wa Salem amepokea mali kumbe alikuwa amepokea sadaka, Bera yeye aliamua
kumshawishi Abraham ampe watu kisha Abraham achukue mali, hizi zote nyara
pamoja na mali zizlizochukuliwa huko Sodoma kwa kutekwa na wafalme ambao
Abraham aliwapiga na kuwashinda.
Lakini Abraham alikuwa amekusudia
na kumuapia Mungu ya kuwa hatachukua uzi wala ukamba wa kiatu, Abraham hakutaka
mtu awaye yote aje ajisifu kuwa ndio sababu ya Baraka za Abraham, Abrahama
alitaka heshima yake na ya Mungu wake na hivyo alikataa kujitia unajisi kwa
mali za watu wadhalimu Alijua Abraham kuwa watu wa Sodoma walikuwa waovu na
hivyo mali zao pia ni za uovu, hivyo alishajifunga kwa kiapo mapemaaaa kuwa hatajitia unajisi kwa mali za uovu mali
za dhuluma na wizi ona
Mwanzo 14:22-23 “Abramu akamwambia mfalme
wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu
na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho
chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”
Abraham alikuwa amekula kiapo
kuonyesha kuwa amejikabidhi kwa Mungu na aliamua kuweka wazi kuwa kila analolifanya
na kila alicho nacho kiini cha mafanikio yake ni Mungu na kwaajili ya utukufu
wa Mungu, Abraham alikuwa anelewa kuwa kiini cha Baraka zake ni Mungu aliyejuu
sana yeye ndiye anayempa ushindi yeye ndiye anayempa utajiri na mafanikio na ni
yeye ndiye aliyemfanya Abraham kuwa na Heshima na utajiri mzito, Kwa hiyo sifa
na utukufu wa mafanikio ya Abraham ni Mungu aliyejuu
Mtu wa Mungu huwa wakati mwingine
ni muhimu kupokea ushauri, lakini wakati mwingine kataa kila kitu
wanachokushauri watu kwaajili ya utukufu wa Mungu, wako watu watajisifu kuwa ni
sisi tuliomshauri akafanikiwa ni sisi tuliompa mtaji, ni sisi tuliomsomesha, ni
sisi tuliomfanikisha wakati iko wazi kabisa kuwa kiini cha Baraka zako kiko na
Mungu, hatima ya maisha yako iko na Mungu wala sio wao wanaohusika, sio kila
mtu anayekupinga anaweza kuwa “Destiny
Helpers” yaani wasaidizi
wanaokupeleka katika hatima yako, kama nduguze Yusufu walitaka kumuua au
waliamua kumuuza au alipotiwa gerezani na Potifa ili kumfikisha kwenye hatima
yake iliyokusudiwa wengine ni “Destiny killers”
kama waameleki ambao walisimama kama kikwazo kutaka kuwazuia Israel wasifikie
hatima yao, wengine ni kama Balaam wanaolaani
na kutoa mbinu za kuhakikisha unaharibikiwa, wengine ni kama Herode
wanaotaka nyota yako ichunguzwe ili
wapate kumuua mtoto uliyemzaa moyoni mwako au maono yako!
Sitatwaa chochote kilicho chako
Abraham alikuwa anamaanisha ana Mungu na hivyo ana kila kitu haitaji msaada wa
mtu wala msaada wa kibinadamu isipokuwa watu sahihi walioletwa na Mungu mbele
zake ili wawe Baraka kubwa katika maisha yake kama ilivyokuwa kwa Melkizedeki Abrahamu
alikuwa anaujuzi wa kujua watu wabaya na watu wema wako watu wazuri katika
maisha yetu na wako watu wabaya watu wabaya na wapotelee mbali na mali zao, na
maono yao na utajiri wao wa dhuluma na wenye asili ya Sodoma, Mungu muumba wa Mbingu
na nchi Mungu aliye hai aliyejuu sana ana uwezo wa kutembea na mimi na wewe
bila msaada wa mtu mwovu, mwenye roho mbaya, hatutachukua lolote wala ushauri
wala sadaka wala mali ya mtu mwovu, Mungu ana njia yake ya kumbariki Abraham
kwaajili ya utukufu wake na sio kwaajili ya utukufu wa wanadamu!, leo hii iko
misaada inayotoka katika nchi au vikundi vya watu wanaounga mkono ushoga, ni
jambo la kusikitisha sana kuwa kwa sababu ya tamaa wako watu ambao wako radhi
kuchukua fedha na mali za watu hao waovu
ili kuendesha huduma mbalimbali, nataka nikutie moyo ya kuwa chanzo cha Baraka
zetu na awe Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, chanzo cha mafanikio yako iwe
haki, unaonaje kama utafanikiwa kwa kufanya majungu, ukifanikiwa kwa uchawi,
ukifanikiwa kwa fitina ukifanikiwa kwa uongo, ukifanikiwa kwa wizi je
utamtukuza Mungu huku ukiwa unaelewa wazi chanzo cha Baraka zako ni uovu? Abrahamu
akasema sitatwaa chochote kilicho chako, Mungu ndiye sababu ya Baraka zangu na
zako mtu wa Mungu!
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye hekima!