Ijumaa, 24 Oktoba 2014

UJUMBE: Mbona Njia Ya Wabaya Inastawi?


Moja ya maswala makubwa ya falsafa ya kikristo na ambayo manabii wengi waliotutangulia waliweza kujiuliza ni pamoja na swala hili la muhimu ambalo hata wengi wetu tunaweza kujiuliza ni swali hili MBONA NJIA YA WABAYA INASTAWI?

Yeremia aliambiwa na Mungu shughuli ngumu bado inakusubiri!
Yeremia 12 1-4 Biblia inasema Hivi

1. Wewe u mwenye haki, Ee Bwana, nitetapo nawe, lakini nitasema nawe katika habari ya haki. Mbona njia ya wabaya inasitawi? Mbona wote watendao hila wanakaa salama? 2. Umewapanda, naam, wametia mizizi, wanakua, naam, wanazaa matunda; katika vinywa vyao u karibu, bali katika mioyo yao u mbali. 3. Lakini wewe, Bwana, wanijua; umeniona, umeujaribu moyo wangu, jinsi unavyokuelekea; uwakokote kama kondoo waendao kuchinjwa, ukawaweke tayari kwa siku ya kuchinjwa. 4. Hata lini itaomboleza nchi, na kukauka majani ya nchi yote? Kwa ajili ya mabaya yao wakaao ndani yake, wanyama wameangamia na ndege pia; kwa sababu walisema, Hatauona mwisho wetu.  
  
Unaona swali hili liliulizwa na manabii akiwemo Yeremia, hali kama hii inawapata watu wema wengi hapa duniani, watu waliojitoa kwa moyo na wanaompenda Mungu na kumtumikia kwa uaminifu, unaweza kushangaa njia za Mungu jinsi zilivyo na hekima yake katika maisha yetu, swali hili halikumsumbua Yeremia pekee lakini hata wayahudi waliorudi kutoka uhamishomi nyakati za nabii Malaki waliuliza swali kama hilo  baada ya kumtumikia Mungu kwa moyo na kujituma lakini wakashangaa maisha yao ni kama Mungu hashughuliki nayo mwisho walisema angalia soma Malaki 3:14-15 Biblia inasema hivi: -
14. Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? 15. Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.

Unaona? Msomaji wangu hii ni hali ya kushangaza unajituma na kujishughulisha kwa Mungu lakini ni kama hakuna kitu cha ziada ukilinganisha na watu hovyo wasiomjali Mungu wana raha wanafanikiwa, wana uwezo kuliko wewe au sisi wala hawamjali Mungu wana kiburi lakini wanafanikiwa? Je umewahi kuwaza Hivyo?
Nabii Habakuki naye alikuwa miongoni mwa Manabii waliopata kujiuliza swali kama hili, na kwa ujumla kitabu chake cha unabii ni kama maswali na majibu kati yake nabii na Mungu angalia Hababuki 1:1-4  inasema

“1. Ufunuo aliouona nabii Habakuki. 2. Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. 3. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.4. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.”

Habakuki anamuuliza Mungu utaachilia udhalimu hata lini? Mtu anaonewa na anakwenda mahakamani ili apate haki, badala ya kupata haki mambo yanageuka, unakimbilia Polisi ukifikiri ni salama badala ya kupata ulinzi unabambikiwa kesi mwisho nabii akabwatuka!

Habakuki 1:12-13 ona “12. Ee Bwana, Mungu wangu, Mtakatifu wangu, wewe si wa milele? Hatutakufa. Ee Bwana, umemwandikia hukumu, nawe, Ee Jabali, umemweka imara ili aadhibishwe.13. Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao kwa hila; na kunyamaza kimya, hapo mtu mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye;”
Habakuki anamuuliza Mungu mbona watu waovu wanawameza wanawaonea watu wema na wewe umekaa kimya? Mbona ni kama hujishughulishi na mtu mwenye haki? Haya ni maswali yanayousumbua ulimwengu huu wa leo, wewe na mimi tunaweza kuwa na maswali yetu kama hayo unapoangalia maisha ya dunia hii unaweza kujiuliza na kisha ukashangaa na kuona mfano

·     Viongozi wenye maadili na waaminifu wakifa masikini na kuchekwa kuwa walishindwa kutumia nafasi zao, Huku viongozi mafisadi wakisifiwa kwa utajiri na mali walizojilimbikizia
·        Mtu mwaminifu mcha Mungu akifanya na kufungua miradi inakufa na haifanikiwi mtu asiye haki kinamchanganyia
·        Binti anajitunza maisha yake na kuishi kwa uaminifu anaolewa na Mume korofi levi na lisilojali

·        Mtu mwema anaangamia na kufa mtu muovu anadunda tu
·        Waovu na makahaba wanafanya uasherati na zinaa  na hawapatwi na Ukimwi we kujaribu tu unao! Mitaani watu wanashika mimba hovyo hovyo wanazitoa na kutupa watoto wewe uko kwenye ndoa takatifu huna mtoto hata wa kutuma chumvi?
·       Umekaa kanisani miaka yote ukimtumikia Mungu kwa uaminifu wanakuja nyuma yako watu wa ajabuajabu walioishi hovyo wanaolewa na kukuacha wewe
·        Mtu wa ajabuajabu anamuomba Mungu na kufanikiwa  mtu wa Mungu anaomba na miaka inakatiza.
Mungu unatufundisha nini?
Ni muhimu Kufahamu kuwa Mungu hutenda kazi kwa namna tofauti na fikra za wanadamu Luka 4:25-27 Yesu alisema maneno haya Muhimu sana akiwaonya waisrael

Biblia inasema hivi Luka 4:25-27 “25. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; 26. wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. 27. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu”.

Yesu alionyesha kuwa utendaji wa Mungu katika ulimwengi wa kiroho ni tofauti na fikra zetu, Israel walifikiri maishani mwao kuwa wao ni wema kuliko wengine na ndipo Eliya akatumwa kwa Mjane wa Sarepta katika nchi ya Sidoni, na wakoma walikuwa wengi wakati wa Elisha nabii lakini alimponya mkoma wa Shamu yaani Syria na sio wakoma wa Israel.

Kwenda Mbele za Mungu na kiburi cha kujihesabia haki kutwanyima watu wengi sana mafanikio na kuwatenga mbali na neema ya Mungu na utendaji wake unaweza kuona wale tunaofikiri kuwa ni wabaya Mungu akiwafanikisha na sisi tunaojifikiri kuwa wema tukiachwa hatuna kitu, sababu ya kiburi na majivuno, Mungu hana upendeleo kamwe usijifikiri mbele za Mungu kuwa wewe ni maalumu sana, hasa unapojilinganisha na wengine.
Yeremia alipouliza mbona njia ya wabaya inasitawi majibu ya Mungu yalikuwa magumu zaidi kwake kama ifuatavyo Yeremia 12:5 “Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Na ujapokuwa katika nchi ya amani u salama, lakini utafanyaje hapo katika kiburi cha Yordani?
Jibu la Mungu kwa Yeremia ni Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Ni wazi kuwa badala ya kumponya Mungu alimuhahidi Yeremia dhiki nyingi zaidi kuwa zinamsubiri na kuwa kile alichokiona ni kama alikuwa anafukuzwa na waenda kwa miguu na kuwa sasa waenda kwa farasi wanakuja? Najua unaweza kuchanganyikiwa zaidi na kujiuliza leo Mjenzi anazungumza nini? Ina maana magumu yanatusubiri zaidi? Je nipite short Cut kama wengine ili nifanikiwe jibu ni hapana Mungu anataka nini kwako?
Habakuki alijibiwa hivi! Habakuki 2:4 Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.!

Mungu alimjibu nabii Habakuki kuwa mwenye haki wangu ataishi kwa imani. unaona? nilazima tuishi kwa imani na kwa matumaini thabiti katika Mungu na katika Kristo, mtu anayekubali kuishi kwa imani ni lazima akubali kuvumilia magumu na kuwa na subira ni lazima ukubali njia za Mungu bila kujali nini kinaendelea upande wapili, kuendenda kwa imani sio kuendenda kwa kuona ni kumuamini Mungu na kukubali kua anabaki kuwa Mungu, kwamba Mungu amekupa mtoto au hajakupa yeye ni Mungu tu, na hakuna kumuacha wala kurudi nyuma, kuwa Mungu amekuponya au hajakuponya anabaki kuwa Mungu, kuwa umetajirika hukutajirika anabaki kuwa Mungu tu, kuwa umefanikiwa hukufanikiwa Mungu anabaki kuwa Mungu tu, kuwa Umeolewa au hujaolewa Mungu anabaki kuwa Mungu tu mwenye haki wangu ataishi kwa Imani akisitasita Roho yangu haina furaha naye asema Bwana uwe na Subira acha kujilinganisha na wengine na Mungu wa haki atakutokea haijalishi ni muda gani unapia uwe na subira.

Haleluyaaaaaaa!

Na Rev. Innocent Kamote Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni: