Jumatatu, 27 Oktoba 2014

Mguu Ukapotea Kwa Sababu Ya Nguvu Hasi

Ni na mguu mmoja mwingine niliupoteza katika ajali ambayo imepelekea kubadili kabisa mfumo wa maisha yangu na nikaona niandike kisa hiki ili kuwasaidia wenzangu ambao wanatenda yale yaliyonifikisha hapa na kujiepusha na maswala kama yaliyonikuta mimi, Nilikuwa mtumishi wa idara ya serikali mkoani Iringa kuanzia mwaka 1977 hadi 1983 nilipopata ajali ambayo ilibadilisha kabisa maisha yangu kutoka kwenye matarajio hadi maisha yaliyosheheni giza totoro.

Nikiwa hapo Iringa familia yangu ilizoeana na familia nyingine ya bwana mmoja ambaye alikuwa na maduka ya vyakula. Mke wa bwana huyo alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi, mke wangu alikuwa ni mwalimu wa shule ambapo mwanamke huyo alikuwa akifundisha katika harakati za urafiki huo wa kifamilia mimi nliingiwa na tamaa au ibilisi kama tunavyosingiziaga, na kumtamani Yule mke wa mafanya biashara, amabaye naweza kusema kuwa alikuwa ni rafiki yangu , kwani kuzoeana kwetu kulikuwa kumepevuka kidogo, mwanamke huyu naye kumbe alikuwa amevutiwa na mimi , wakati huo nilikuwa badi kojana ninayependeza, tulianza uhusiano mwaka 1979, miaka miwili baada ya mimi kufika Iringa na kujuana na familia hii , wakati huo ndoa yangu ilikuwa na miaka sita tu maana nilikuwa nimeoa mwaka 1973. Tulianza kukutana kwa siri na mwanamke huyu ambaye alikuwa mdogo ukilinganisha na mumewe kwani mumewe alikuwa ni mtu mzima kidogo akiwa kwenye umri mwanzoni mwa miaka 50 yeye alikuwa na umri wa miaka 25,
Uhusiano wetu na mke wa jamaa yangu ambaye hapa nitamwita mfanya biashara , ulianza kwa kasi kubwa sana , tulikuwa tumehemkwa kwa nguvu kubwa kiasi kwamba nilianza kuhofia , nilijitahidi sana kuweka mipaka ili tusifikie mahali tukajisahau. Mwaka 1981 habari zilianza kuvuja kuhusu uhusiano wetu . 


Mke wangu ambaye alikuwa anafundisha na huyu hawara yangu shule moja huku wakiitana marafiki aliniambia kuna jambo linanong’onwa kwamaba nina uhusiano na rafiki yake , mke wa mfanya biashara ambaye hapa mke huyo namuita Waridi ambayo ni tafasiri ya jina lake kwa Kiswahili ya jina lake halisi, niliposikia habari hiyo kutoka kwa mke wangu nilishituka sana , lakini nilimudu kujifaragua na kujitetea kiasi kwamba hata kama angekuwa ni mtu mwenye moyo mgumu sana angelainika nilisema hivi “Watu hawapendi wakiona familia mbili zinaelewana hasa familia kama zetu, mimi bado kijana mdogo na nina kazi nzuri na fedha , wewe una kazi, hawa wenzetu, wana biashara nyingi sana hapa mjini kwa hiyo ni lazima utasikia mengi we huwajui waswahili? Shemeji Waridi hawezi hata kufikiri kuhusu upuuzi huo na mimi wala sijawahi kuota, sio kwa Waridi bali kwa mwanamke yeyote nilimaliza kujitetea.


Nilimuonya sana Waridi baada ya kukutana naye, aliniambia naye mumewe alikuwa amemuulizia swala la madai hayo anayoyapata kuhusu uhusianao wetu.Niliogopa sana, Lakini alisema alikuwa amemudu kumtuliza na wala hilo mhalikuwa swala tena , Nilipata moyo na mapenzi yetu yaliendelea kupamba moto, mwaka 1982 mke wangu alinisakama tena , safari hii akidai kuwa ana vyanzo vya kuaminika kuhusu uhusiano wetu na Waridi, nilimwambia kwamba sina haja ya kubishana na wewe niko tayari kushika kitabu cha dini , tuape kwa laana zote. Nilipomwabia hivyo alinywea, nilimwabia hivyo kwa makusudi , nilijua kwamba alikuwa alikuwa ni mtu wa dini sana Aliogopa akiamini kwamba kusema kwangu vile kulikuwa na maana ya uhakika kwamba sikuwa nashiriki jambo hilo.Alisema hao watu wanaomwambia wana sababu gani ya kudanganya, Nimekwambia watu wana hila mke wangu, Dini inasema kufumania ni kuona kwa macho na sio mtu mmoja bali mashahidi wanne, Unadhani inasema hivyo bure tu hapana , ni kwa sababu ya mambo kama hayo, nilizidi kumfanya aniamini.
Ilibidi sasa tubadili mikakati yetu na Waridi , nilikuwa nachukua gari la kazini na tukawa tunaondoka wote hdi nje kabisa ya mji wa Iringa, wakati mwingine tulikuwa tunaingiza gari porini na kufanyia mambo yetu garini na hili lilitupa raha zaidi, tuliamua kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba kuingia gesti za pale mjini ilikuwa ni kujichongea bure, ilisaidia kwani mwaka 1982 uliisha bila kero na 1983 ukafika bila kusikia lolote.Lakini kama ilivyosemwa mkizini mtafumaniwa tu hata iweje, yalinitokea kwa aibu na fadhaa. Hiyo juni 1983 mume wa Waridi alipata safari ya kwenda Malawi kibiashara . wiki hiyo mimi nilikuwa na safari ya Dar es Salaam, tulikubaliana kwamba tuondoke wote wakati mimi nakwenda dar tuje Morogoro tulale pale hadi kesho yake mimi niendelee na safari yeye arudi iringa kwa bahati nzuri shule zilikuwa zimefungwa Waridi alisema kuwa angemwabia mumewe akirudi kuwa amekwenda Morogoro,kumuona dada yake ambaye alikuwa ameumwa ghafla, Niliona ni wazo zuri na kweli tuliondoka wote


 Tulifika Morogoro na kupiga kambi, waridi alikwenda kwa dada yake na kumwambia kwamba amesikia kwamba anaumwa hivyo amekuja kumwona , Ni kweli alikuwa anaumwa kidogo wiki hiyo, lakini alikuwa ana nafuu, baada ya kuzungumza naye kwa muda wa saa mbili alimuaga kwamba anarudi Iringa .Alisindikizwa hadi stendi, ambapo mimi nilijitokeza na gari na kujifanya tunajuana na Waridi nakujifanywa kwamba natoka Dar na ninaenda iringa , Waridi alijifanya ananiomba lifti na nilimkubalia Dada yake alisema “una bahati kweli haki ya Mungu” wenywe tulijiona wajanja wakubwa sana.
Tuliondoka hadi mzunguko wa Msamvu na kurudi mjini. Tulilala Morogoro na asubuhi yuake Waridi aligoma kurudi Iringa , akisema ni lazima afike na kulala dar, niliogopa kidogo lakini name wakati huu Ibilisi alikuwa amenikalia kichwani vinaya sana , Nilimkubalia na tuliondoka Moro saa 1;45 asubuhi kuelekea dar, ilikuwa ni kama kilomita mbili hivi kutoka mlandizi ndipo ilipotokea , Nilikuwa nimeshuka kimlima kutoka mji wa Mlandizi na kupanda halafu nikakanyaga mafuta hadi gari ikwa inaenda kilomita 100 kwa saa. Nilisikia mlio mkubwa sana na gari iliyumba na nikanyang’anywa usukani, halafu niliona tukipaishwa na kutupwa kando ya njia kwenye mti wa mwembe upande aliokuwa amekaa waridi ulifikia kwenye shina la mwembe , sikusikia tena kitu waka sikujua kilichotokea.
Ni siku ya pili jioni niliposhituka nilamka na kujikuta nimefunikwa shuka zilizoandikwa Muhimbili, nilimuona mke wangu akiwa kando ya kitanda change pamoja na watumishi wa makao makuu ya idara niliyokuwa nikifanyia kazi, nilijihisi kuwa mwepesi sana upande wa chini, Nilipokagua niligundua kwamba sikuwa na mguu upande wa kushoto, ilinichukua muda kabla sijakumbuka kilichotojkea, Polepole nilikumbuka kuoka Iringa moro hadi Mlandizi,Sikukumbuka tena kitu, ilinichukua Muda kumkumbuka Waridi, Nisingeweza kumuuliza mke wangu au yeyote pale kuhusu waridi lakini nilikuwa na uhakika kwamba alikuwa amekufa. Nilianza kububujikwa na machozi, nilijaribu kusema lakini sikuweza ni midomo tu iliyokuwa ikicheza, “Amekufa amekufa uso wangu sasa naupeleka wapi nauweka wapi jamani…” mke wangu alisema na kuangua kilio, nilimwelewa wale watumishi wenzangu walimtuliza, tuangalie na kujali hali ya mgonjwa kwanza walimwambia
Ni kweli waridi alikufa palepale kwenye tukio la ajali na mimi ni bahati tu kupona na kukatwa mguu mmoja badala ya miwili na mikono, nilikuwa na uhakika kwamba baada ya kupona makovu ya mwilini yangekuwa yanatisha sana, Kila kitu kilifahamika baada ya sikui tatu Mume wa marehemu Waridi alirejea safari na kusimuliwa kila kitu, alihaidi mbele za watu kwamba angenimaliza na mimi iwe kwa mvua au kwa jua , nilipopata taarifa hizo nilicheka kwani niliona akifanya hivyo atakuwa amenitua mzigo mzito wa aibu niliokuwa nao, labda aliambiwa baadaye nilivyokuwa nasema na ndio maana hakunifanya lolote.
Nilitoka Hospitalini nikiwa na mguu mmoja baada ya miezi mitatu nilkuwa na nafuu kidogo, mke wangu alishaanza uhusiano na Yule mfanya biashara na hakunificha , ilinibidi nifikie mahali pa kuomba talaka. Talaka ilitolewa na nikawaacha waendelee, hatimaye mwaka 1985 walioana ingawa ndoa yao ilivunjika mwaka 1990 kwa makeke na vurugu kubwa.
Mimi nimepunguzwa kazi mwaka juzi na hivi sasa nina shughuli zangu, nilikuja kuoa mwaka 1987 mke ambaye tunaelewana sana na amekuwa ndiye kiongozi wangu kwa mambo mengi na tuna watoto wanne, kuna watu wanapenda kuniita Zuber kaguu kwa siri Nawaomba waniite kabisa kwa nguvu kwa sababu ninastahili.
Jina langu ni Zuber Zando (kaguu) naamini hutakuwa umekodoa mimacho tu kupenda umbeya lakini utakuwa umejifunza kitu kwani tunajifunza pia kutoka kwa wengine na kama umeamua kujifunza utakuwa umejifunza kitu kikubwa kupitia habai hii wataalamu wa mahusiano wanaamini kuwa ukitembea na mke wa mtu au mume wa mtu kwa siri ni ndani ya miaka mitatu tu mtakuja kufumaniwa na ikipita bsi hamtafikisha mika sita bila kufumwa najua unaweza kujiamini kuwa wewe ni mjanja na una maarifa mengi sana katika kukanusha au kuteleza ili usifumaniwe lakini kwa sababu ni nguvu mbovu unayoipanda ni lazima utalipwa tu utake usitake unapotoka nje jiandae kunaswa sio kwa sababu u mjanja bali kwa sababu nguvu hasi uliyoipanda itakuja kukamilisha mzunguko wake, unapoonewa wasiwasi na mpenzi wako au mkeo au mumeo au watu wengine kama unafanya kweli acha lakini uklitaka kuendelea jiandae kwa aibu na kuumia baadaye

Makala na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
ikamote@yahoo.com
0718990796
0784394550

Hakuna maoni: