Yuda 1:3-4 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana
kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu
kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu
mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa
tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi,
nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.”
Mji wa
Nicaea wa kale unavyoonekana leo, katika Nchi ya Uturuki zamani ilikuwa ni
sehemu ya Ugiriki
Utangulizi:
Nicaea au Nicea Ni moja ya mji wa kale
zaidi katika nchi ya Ugiriki kaskazini-mashariki ya mji wa Anatolia, ambao
kimsingi unajulikana kama eneo ambalo Mkutano mkuu wa kwanza na wa pili wa kanisa
ulifanyika kwa mujibu wa Historia ya kanisa na ndio chimbuko la Msingi wa imani
ya Kikristo ambayo inajulikana kama Imani ya Nikea!
Mnamo mwanzoni mwa Karne ya Nne moja
ya fundisho muhimu sana liliinuka na kuleta Utata miongoni mwa Kanisa, mijadala
iliinuka kupitia wanatheolojia wakubwa
na wenye nguvu, pia kukiwa na utetezi wenye nguvu na mawazo mbalimbali
yaliyopelekea kuitishwa kwa mkutano wa uliofanyiika katika mji huo wa Nicea ili
kupata msimamo wa kweli wa kikanisa kuhusiana na imani yetu.
Yuda
1:3-4 “Wapenzi,
nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi
sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani
waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa
siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya
Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu
Yesu Kristo.”
Neno la Mungu linatuagiza kwamba tunao
wajibu wa kuilinda imani yetu, na vilevile neno la Mungu linatutaka kujilinda
na upotofu! Kama watu watakuwa wanaipotosha imani yetu nasi tukanyamaza kimya
swala hilo linaweza kusababisha wakristo wakapotea na kujitenga na imani iliyo
hai ona Waebrania 3;12 Biblia inasema “Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo
mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.”
Nyakati za Kanisa la Kwanza mitume
walikuwa na tabia ya kukutana pamoja kwa kusudi la kujadili mafundisho yasiyo
sahihi katika imani yetu na kisha kutoa matamko ambayo yangeweza kurekebisha na
kuweka wazi msimamo wa Imani yetu angalia kwa mfano Matendo ya Mitume 15:1-2 “Wakashuka
watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama
desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na
watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na
wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari
ya swali hilo.”
Unaona nyakati za mitume walikuweko
walimu ambao walifundisha watu mafundisho yasiyo sahihi, fundisho lao ni kuwa
“mtu asipotahiriwa hawezi kuokoka” fundishi hili lilikuwa haliko sawa na injili
ya Yesu na ile iliyohubiriwa na Mitume kwamba Yesu anaokoa watu wa mataifa yote
na wa desturi zote kwa imani bila masharti ya sheria ya Musa, ili kupata
muafaka wa kipi kiwe fundisho sahihi la Injili Paulo na Barnabas walikwenda Yerusalem
na kukusanyika na mitume na kupata tamko la pamoja kama tunavyoweza kuliona katika
Matendo
ya mitume 15:7-20 “Na baada ya hoja nyingi Petro
akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza
Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa
kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia,
akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti
kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona
mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu
wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya
Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza
Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu
aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo
akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu
hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya
jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa, Baada ya
mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka.
Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha; Ili wanadamu waliosalia
wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa
sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika
Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati,
na nyama zilizosongolewa, na damu.”
Hivi ndivyo namna na jinsi nyakati za
kanisa la kwanza walifanya kwa kusudi la kuitetea imani, na kuilinda, kuitetea
dhidi ya mafundisho yasiyo sahihi kutokana na walimu wa uongo na vilevile kutoa
matamko yenye kuweka misingi ya kweli ya injili. Hata hivyo kama tumeiona kuwa
nyakati za kanisa la kwanza waliwategemea Mitume kutoa muongozo wa kweli za
kiungu, kwa kuwa wao walipewa neno, mtume wa mwisho kabisa kufa alikuwa Yohana
mwandishi wa kitabu cha ufunuo ambaye alikuwa mwaka wa 100 Baada ya kristo.
Karne mbili baadaye mafundisho mengi
ya uongo yalitokea au wakati mwingine mabishano ya kitheolojia kutoka miongoni
mwa viongozi wa Kanisa, Kwa desturi kama ile ya mitume mababa wa kanisa
walikusanyika NICEA kwa kusudi la
kujadili na kupata kweli zinazoweza kuwaongoza vema bila kuchukuliwa na
mafundisho yasiyo sahihi ya kibiblia. Mkutano huo uliitishwa kwa mamlaka ya
Mfalme Contantine aliyetawala RUMI kati ya 306-337
BK.
Katika mkutano wao wa Kwanza mjadala ulikuwa kuhusu Mafundisho ya Arius na
Athanasius ambao walikuwa na mitazamo ifuatayo
a.
Arius
wa Alexandria 256-336 BK
Alikuwa
ni kiongozi mkubwa wa imani ya Kikristo na mwanzilishi wa imani ya Arianism moja ya imani potofu iliyokuwa
inapinga uungu wa Yesu Kristo, Arius alikuwa mwana theolojia aliyesomea huko
Antiokia (Antakya ya Leo huko Uturuki) alijifunza theolojia chini ya Msomi
aliyejulikana sana aliyeitwa Lucian na huenda ndiko alikotoka na fundisho hilo
alijulikana kwa kusisitiza maswala ya kihistoria na njia zanye kujenga na
kuzalisha za kidini pamoja na maswala ya utafiti kuhusu umoja wa Mungu na Utatu
Mtakatifu shule yake ilijulikana pia kama shule iliyokuwa ikimuona Kristo
kama yuko chini ya Mungu Baba,.
Arius
alizaliwa Afrika na alikuwa mwangalizi wa Kanisa la Alexandria nchini Misri,
alikataa kuweko kwa ushirika wa milele kati ya Yesu na Mungu usemi wake maarufu
unasema “kuna wakati ambapo Yesu Hakuweko”na kuwa Mungu alimpitisha Yesu kuwa
mwana wake baada ya ufufuo wake na kumpa baadhi ya majukumu ya uungu, alisema Yesu
alikuwa na mwili wa kibinadamu lakini hakuwa na Nafsi ya Kibinadamu na hivyo
hakuwa Mungu wala hakuwa mwanadamu wa kawaida Yuko mahali Fulani hapo katikati.
Arianism wanaamini Yesu alimumbwa kwa tafasiri ya andiko hili Ufunuo 3:14c unaosema “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya
ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, MWANZO WA
KUUMBA KWA MUNGU”
b.
Athanasius
293-373 B.K.
Mtakatifu
Athanasius aliishi kati ya mwaka wa 293-373 B.K. Ni mwanatheolojia mkubwa wa
Kikristo na Doctor wa Kanisa Pia alikuwa Askofu ni miongoni mwa watu
walioshindana na kusababisha kuundwa kwa kanisa la Orthodox katika karne ya 4
akishindania imani dhidi ya Arianism
alisimikwa kuwa shemasi akiwa kijana, akitumika kama Katibu wa askofu wa
Alexandria na ndipo alipopata nafasi muhimu ya kitheolojia ya kuongoza
mapambano dhidi ya fundisho la Arius
ambalo lilijadiliwa katika mkutano wa Nicea
mwaka wa 325 na kwa ujumla alikuwa
na nguvu ya ziada ya kupambana na imani hiyo na aliweza kueleza sawia kuwa
mwana wa Mungu Yesu Kristo ni sawa na Mungu Baba ingawa Arius
aliendelea kudai kuwa sio sawa kwani Yesu ni kiumbe tu aliye mkamilifu kuliko
viumbe wengine na kuwa alitumiwa na Mungu katika uumbaji na kazi nyingine za
uumbaji baada ya kuumbwa kwanza.
Mijadala
hii ilipelekea kuzuka kwa mjadala mkubwa kuhusu Utatu wa Mungu mjadala huu
ulikuwa umekita miguu yake katka kutaka kujua kuhusu Uungu wa Yesu kwamba je
Yesu ni Mungu? Na kuna uhusiano gani kati ya Roho na Mwili wa Yesu Je Mungu ni
Watatu au mmoja? Na wana uhusiano wa aina gani?
Arius
alikuwa ameshindwa kutafasiri andiko la Ufunuo 3:14 na kuelewa vema neno MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU katika
Biblia ya kiyunani linatumika neno
“PROTOTOCOS” ambalo ni sawa na neno Protocol la kiingereza, Neno hilo Prototocos kwa kiyunani maana yake ni WAKWANZA KATIKA CHEO, kwa kiebrania
maana yake Mzaliwa wa Kwanza, Uzaliwa wa kwanza katika kiyunani na kiebrania
ulikuwa na maana ya cheo na hivyo kingeweza kuhama kwa yeyote Mungu
aliyemchagua mfano Esau kwenda kwa Yakobo, au Manase kwenda kwa Efraimu, Hivyo
linapotumika katika Biblia linamaanisha Yesu ndiye mwenye cheo cha juu zaidi
kuliko chochote duniani au mbinguni
katika kiingereza maandiko hay ohayo yanasomeka hivi ona :-
Biblia ya
Kiingereza ya King James Version
inasomeka hivi;-
• Revelation 3:14c “And unto the angel of the
church of the Laodiceans write; These things saith the Amen, the faithful and
true witness, THE BEGINNING OF THE CREATION OF GOD” KJV
Na biblia ya kiingereza
the Amplified Bible inasomeka hivi;-
• Revelation 3:14 “To the angel of the Church
in Laodicea write: These are the words of the Amen, the faithful and true
witness, “THE RULER OF GODS’ CREATION”
Kwa kuwa Biblia ya
Kiswahili SUV. Swahili union Versio imetafasiriwa moja kwa moja tioka KJV
inasomeka MWANZO WA
KUUMBA KWA MUNGU, tafasiri halisi ilipaswa kuwa Mtawala wa
uumbaji wa Mungu unaona.
Chanzo
cha tatizo:
Kwa nini imani Potofu zilitokea ziko
sababu kadhaa za msingi;-
Mabadiliko makuu matatu katika kanisa.
-
Kanisa
katika hatua za mwanzoni lilikuwa ni kanisa kama shirika lisilo na sheria au
kanuni au makusudi ya kimaadili au kimuuundo
-
Hakukuweko
na Muundo maalumu wa kimaongozo wala wa kitaratibu na baadaye lilikumbwa na
mabadiliko hususani katika karne ya pili ambapo waamini walianza kufikiri
kuhusu ushirika na kuweka viwango vya kimaadili na mafundisho, aidha agano
jipya yaani maandiko ya agano jipya na mitume yalikuwa hayajafanyika neno
kamili la Mungu yaani kukusanywa maktaba na kupata Agano jipya. Kwa hiyo kanisa
lilikuwa na mabadiliko kwa sababu za msingi zifuatazo:-
a. Kufa
kwa Mitume wa Bwana.
Mwishoni
mwa Karne ya kwanza Mitume wote wa Bwana walikuwa wamekwisha kufa wao walikuwa
ni kama Mamlaka ya juu kabisa ya Kanisa na kila kulipotokea tatizo walikuwa
wakitoa suluhisho je nani atakuwa mwenye mamlaka kama ile?
Je
kanisa lingewezaje kutunza umoja wake wa imani bila kuweko kwa Mitume? Ilikuwa
ni lazima na muhimu jibu lipatikane na zaidi sana Mchanganuo wa majibu ya
Misingi ya Imani ilikuwa lazima Isitawishwe.
b. Mateso
dhidi ya Kanisa.
Wafalme
wengi wa Kirumi makaisari walitaka kuabudiwa wao kama miungu, aidha wayahudi
walianza kuwaona wakristo kama dhehebu lililo kinyume na sheria ya Musa na kuwa
ni imani pinzani au tishio kwao Kanisa lingeweza kukabili vipi dharula hizo
zilizojitokeza ndipo ilipoonekana haja ya kuwepo na Ushirika thabiti pamoja na
sauti kamili ya kimafundisho au mafundisho sahii ambayo ungekuwa ndio msingi wa
Imani ya wakristo wote.
c. Kuweko
kwa mafundisho ya uongo.
Mafundisho
ya Mitume yalikuwa yanakubalika na kuheshimika kama Mamlaka ya mwisho hususani
walipokuwa wakiwa hai, Lakini baada ya wao kufariki waalimu wa uongo wengi
walitokea, je ni nani angesimama na kuzungumzia maswala ya imani na misingi ya
mafundisho ya kweli ya kanisa? Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa kuwa na Msimamo
mmoja wa kiimani na sasa Tatizo lilikuwa
kubwa zaidi wakati jamii ya wakristo wa Mataifa walipoamini na kuingia kanisani
kulizuka mawazo tofauti falsafa tofauti na migogoro iliinuka hapa na pale.
Namna ya kupata muafaka.
Waefeso 2:20 “Mmejengwa
juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la
pembeni.”
Katika kufikia muafaka Mkutano mkuu wa
Nicea ambao pia ni maarufu kwa jina la Nicaeno-Contantinopolitan Creed mababa wa kanisa waliadhimia kwa
pamoja kutengeneza ukiri wa imani ambayo ni mukhtasari wa mafundisho ya Msingi
yaliyosadikiwa na Mitume na kufundishwa na mitume kwa kuzudi la kuzuia uzushi
ukiwemo wa Arianism na aina nyingine
za uzushi ambazo zilisumbua kanisa kwa karne nne, kwa msingi huo kanisa la
Mashariki na Magharibi waliamua kwa pamoja kuwa na ukiri, ambao huo ndio
utakuwa msingi wa kanisa la kweli kokote duniani, na kwa msingi huo kanisa au
dhehebu lolote linalofundisha kinyume na misingi hii ya imani ndio inaitwa
imani potofu, ni kutokana na mkutano huo uliofanyika Nicea ndio tunapata msingi
wa Imani uliokuwa unafundishwa na mitume, na kwa heshima ndio misingi hiyo
ikaitwa Imani ya Nikea, imani hiyo ilikuwa na maneno yafuatayo;-
“Twaamwamini Mungu mungu mmoja, Baba mwenyezi, Muumba wa mbingu na Nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.”
Na Yesu Kristo mwana wake wa pekee Bwana wetu, Atokaye kwa Baba kabla ya ulimwengu kuwako, Mungu kutoka kwa Mungu, Nuru kutoka katika Nuru, Mungu kweli kutoka katika Mungu kweli mwana wa azali asiyeumbwa, Mwenye uungu mmoja na Baba, ambaye kwa yeye vitu vyote viliumbwa, kwaajili yatu na kwa wokovu wetu, aliyeshuka kutoka Mbinguni, aliyechukuliwa mimba, kwa uweza wa Roho Mtakatifu akazaliwa na bikira Mariam, akawa mwanadamu, zamani za Pontious Pilato aliteswa, akasulubiwa akafa akazikwa, siku ya tatu akafufuka kama yanenavyo maandiko matakatifu akapaa mbinguni ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, toka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu watu walio hai na wafu na ufalme wake hauna mwisho,
Twamwamini
Roho Mtakatifu Bwana mtoa uzima atokaye katika Baba na Mwana, anayeabudiwa na
kutukuzwa Pamoja na Baba na mwana aliyenenwa kwa vinywa vya manabii,
Twamini
Kanisa takatifu Catholic na apostolic, ushirika mtakatifu, twakiri ubatizo
mmoja wa kuondolewa dhambi, Twatazamia kufufuliwa kwa wafu na uzima wa
ulimwengu ujao Amen.”
Huo ndio Ukiri wa Imani yetu, kila
kanisa na kila dhehebu, maswala yote wanayohubiri na mafundisho yote
yanayofundishwa hutokana na msingi wa imani hii waliyokuwa wakiiamini Mitume na
kuifundisha, kanisa lolote dhehebu lolote au fundisho lolote lililo kinyume na
misingi hii linakuwa limetoka nje ya njia, kwa hiyo ukifuatilia kwa makini
utaona hiki Mafundisho yote ya kweli yanasimama katika fundisho hili, Mtu
akisema Yesu sio Mungu, au akisema hakuna Roho Mtakatifu, au akisema wafu
hawafufuliwi, au akisema Yesu hajasulubiwa msalabani basi hayo ni mafundisho
potofu, Hivyo imani ya nikea ni mukhtasari wa misingi ya imani yetu ya kweli, Kanisa
linapewa wito wa kujsomea maandiko na kujifunza kweli tunapoikumbuka imani ya
NIcea ambayo ndio ilikuwa misingi ya kweli ya mafundisho ya Mitume.
Uongezewe neema!
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni