Mathayo 15:17-20 “Hamjafahamu bado ya kuwa
kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Bali vitokavyo
kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. Kwa maana moyoni
hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na
matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono
hakumtii mtu unajisi.”
Utangulizi:-
Mafarisayo na waandishi walitoa
shutuma nzito kwa wanafunzi wa Yesu, kwamba hawanawi mikono mpaka kwenye kiwiko
wakati wanapokula chakula, na kuwa kwa kufanya hivyo wanayahalifu maagizo ya
wazee, Kimsingi hakuna maagizo ya kibiblia yanawataka watu kunawa mpaka kwenye
kiwiko cha mkono, lakini mafarisayo walikuwa wameyashika mapokeo hayo kana
kwamba ni agizo la kiungu na kutumia kigezo hicho kuwahukumu wengine. Yesu
aliwakemea Mafarisayo kwa tabia yao yenye kutoa kipaumbele kwa mambo yasiyo ya
msingi na kusahahu mambo ya msingi, kimsingi Yesu hakuwa amedharau kanuni za
kiafya kwamba labda watu wasinawe mikono wanapojiandaa kula chakula na
kadhalika, Lakini yesu alikuwa anaikemea ile tabia ya kinafiki ya kupuuza mambo
ya msingi na kushikilia mambo yasio na msingi ambayo kimsingi hata neno la
Mungu halikuwahi kuyaagiza, Yesu alitaka kuonyesha wazi kuwa kula bila kunawa
kiwiko cha mkono au kuingiza kitu tumboni kulicho nasisi kunaweza kusiwe na
maana sana kwani vinapita tu, lakini alitaka jamii ielewe kuwa kuna mambo ya
hatari zaidi ya kuyashughulikia yanayokaa moyoni na kujitikeza hata mdomoni
kuliko yale yanayoingia mdomoni kisha yakaenda zake! Kwa mafundisho ya Yesu
mambo hayo ndio yamtiayo mtu unajisi! Leo tutachukua muda kuangalia kwa undani
mambo yanayomtia mtu unajisi na kumuomba Mungu atuokoe na mambo hayo ili tupate
kibali mbele zake!
1.
Mawazo
mabaya (evil Thoughts)
Ni muhimu
kufahamu kuwa kwa mujibu wa Mafundisho ya kibiblia usafi wa Mtu huanzia kwenye
moyo wake, yaani kwenye akili na ufahamu, uhusiano wetu na Mungu unategemeana
sana na mkao wa moyo, kujibiwa kwetu maombi na kupata thawabu katika kila jambo
kunategemeana sana na mkao wa Moyo, hivyo ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa
wakati wote tunakuwa safi moyoni kwanza, bila kupuuzia usafi mwingine wanje
Neno la Mungu linasema Mathayo 5:8 “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.” Uhusiano
wetu na Mungu haujengwi pekee kwa matendo ya nje bali zaidi hasa na mkao wa
mioyo yetu ndani Neno la kiyunani wenye moyo safi husomeka kama “KATHAROS” yaani mtu safi, asiye na
hatia asiye na lawama, mtu ambaye hata dhamiri yake haimuhukumu kuwa ana kesi
ya kujibu, hakuna hila ndani yake, hakuna unafiki, hakuna kitu kilichojificha,
muwazi kwake kwa Mungu na kwa wanadamu mtu mwenye nia ya kumpendeza Mungu, ni
ukweli wa kibiblia usiofichika kuwa Mungu haangalii kama wanadamu waangaliavyo,
Mungu hutazama moyo, 1Samuel 16;7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake,
wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama
binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana
huutazama moyo.” Kipimo kikubwa cha mtazamo wa Mungu kwa mwanadamu
ni Moyo, hii ndio chemichemi ya mambo yote tuyaonayo ulimwenguni, kwa hiyo ili
mtu asinajisikie aiwe muovu anapaswa kuhakikisha kuwa anakuwa na mawazo safi,
anajilinda sana ndani kusiharibike, Mithali
4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana
ndiko zitokako chemchemi za uzima.” Mtu safi hapimwi kwa kile
anachikifanya, mtu safi anapimwa kwa mtazamo wa moyo wake yaani mawazo yake
unawaza nini kabla hujatenda, kupata kibali kwa Mungu kunategemeana sana na
unawaza nini, yaani nia ya moyo wako
Zaburi 19:14 “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya
moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.”
Kama tutakuwa safi nje tu lakini katika mawazo yetu tumejaa kila aina ya uovu
kamwe Yesu hawezi kutukubali katika viwango vya usafi anaouhitaji Bwana wetu ni
ndani kwanza! Mathayo 23:25-28 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa
mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na
kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili
nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa
kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa
mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi
nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na
maasi.” Unaona Bwana Yesu alikemea vikali sana dhambi inayokaa
katika mawazo, alikuwa anaelewa wazi kuwa kuwa safi nje lakini ndani hakufai ni
unafiki, uhalisia wa Mtu na uzuri na usafi wake huanzia katika mawazo, na mtu
akiwa safi ndani nan je yake hupata kuwa safi, kwa msingi huo ni jambo gani
linatutia unajisi ili tuweze kulishughulikia ni mawazo yetu kwanza na kwa
sababu hiyo hatuna budi kumuomba Mungu mawazo ya mioyo yetu yapate kibali mbele
zake yaani tuwaze mema na Mungu awe shahidi wa ule wema ulioko ndani yetu, hapo
hatutakuwa najisi, kumbuka kuwa mawazo ndio chemichemi ya kila kitu kiovu!
2.
Wivu (envy)
Ni muhimu
kufahamu kuwa katika maisha haya hatuwezi kuwa na kila kitu, kadiri
unavyotembea katika maisha haya ukiwa na fedha unaweza kuwakuta wenzako wana
fedha kuliko wewe, una ndoa iliyotulia unaweza kukuita kuna watu wana mahusiano
mazuri na matamu kuliko yako, umejenga nyumba unaweza kukutana na wenzako wana
Mahekalu makubwa na makasri mazito kuliko wewe, unanunua gari utakutana na
wenzako wenye migari, unaweza kuwa u mzuri na ukautana na mtu mzuri kuliko wewe
halafu wala hana maringo kama yako, unaweza kuwa na cheo lakini ukakutana na
wenzako wenye cheo kikubwa kuliko chako, je unajisikiaje moyoni mwako unahisi
wivu? au unaposikia maono na mawazo yamwenzi wako unajiskia kushindana naye, au
kumuharibia, au kumuua wivu umewaharibia watu wengi sana maisha na kuwatia
unajisi wazee wetu ndugu wa baba moja
wana wa Israel walichukizwa tu na Ndoto za Yusufu ndugu yao na kwaajili ya wivu
walifikia hatua ya kutaka kumuua na hata kumuuza Misri ona ni wivu wao ndio uliozalisha chuki na hata
kutaka kumletea uharibifu Mwanzo 37:2-11
“Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa
mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye
alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake.
Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu
kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu
zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia,
wala hawakuweza kusema naye kwa amani.
Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia,
Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga
miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda
yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je!
Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa
ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia
ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi
na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba
yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako
na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba
yake akalihifadhi neno hili.” Agano jipya linaweka wazi sababu ya
Yusufu kuchukiwa na ndugu zake na hata kutaka kumuua au kuamua kumuuza kule
Misri kuwa ilikuwa ni wivu, Matendo
7:9-10 “Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu,
wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote,
akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe
mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote” wakati wote tukiruhusu
roho ya wivu kutawala mioyo yetu na kutkuridhika na kile ambacho Mungu
ametubarikia na kukosa shukurani tutajikuta tunajiharibia maisha yetu na
kuyatia unajisi, wivu unaweza hata kuleta mauaji, taama pia na ugomvi wa moyoni
yakobo anautaja wivu kuwa ni hekima ya kishetani, wako watu wana hekima ya
kishetani, wanaweza au wanajua kuleta magomvi, wanajua kuchonganisha hatuna
budi kumuomba Mungu atukinge na unajisi wa namna hii ambao Yakobo anauita wivu
wenye uchungu Yakobo 3:13-16 “N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi
zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima. Lakini, mkiwa na wivu
wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya
kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya
kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo
machafuko, na kila tendo baya.” Hekima ya Mungu haitaki
tujilinganishe na wengine wala hairuhusu tujione bora kuliko wengine, namna
pekee tunayoweza kujilinda na wiu wenye uchungu ni kufanya mema
yatakayotuhakikishia kibali kwa Bwana, kwani Mungu yuko tayari kumbariki kila
mmoja na hubariki kila mmoja kwa namna yake kama apendavyo yeye!
3.
Tamaa
(Greedy).
Ni moja ya tabia
ambayo imeharibu wengi sana na kuwaletea hasara katika maisha, neno tamaa greedy katika kiingereza ina maana ni
ile hali ya kutaka kuwa nacho zaidi, kula zaidi, kuvaa zaidi, kila kitu zaidia
ya kile ulicho nacho au unachohitaji, kwa hiyo mtu mwenye tamaa sio kuwa hana
isipokuwa ni anahitaji zaidi haridhiki na kile alichonacho! Tamaa inapaswa
kudhibitiwa katika hatua za mwanzoni kabisa ili isikomae na kusababisha madhara
makubwa Yakobo 1:14-15 “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana
Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila
mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu
ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa
huzaa mauti.” Watu wengi sana duniani wameharibiwa na tamaa, wanavyo
lakini wanataka kuwa navyo zaidi, halii hii ikiuandama moyo wa mwanadamu
inapelekea kwenye kuleta madhara makubwa sana na kumtia mtu unajisi, Biblia inatueleza habari ya mfalme
mmoja aliyeitwa Ahabu, ambaye ingawa alikuwa mfalme na alikuwa na kila kitu
lakini bado alitamani shamba la mtu, ambaye shamba lile lilikuwa la urithi na
katika Israel mila zao hazikuruhusu kitu cha urithi kiuzwe au kubadilishwa
lakini kwa tamaa jamaa alishindwa hata kula na mkewe aliyeitwa Yezebeli
akapanga njama ya kumuua Nabothi ili shamba lile liwe na Ahabu, Mungu liona
tulio lile na kutangaza hukumu mbaya sana kwa familia ya Ahabu 1Wafalme 21:1-19 “Ikawa
baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli,
karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na
Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga,
maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu
lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake.
Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu.
Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu
ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba
zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini
Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile
chakula? Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia,
Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la
mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu.
Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka,
ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi
Myezreeli. Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake,
akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika
mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema,
Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu
wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu
na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji
wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli
alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu
ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu
wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia
Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo
wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli
habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia
ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka,
ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha,
maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba
Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi
Myezreeli, ili alitamalaki.Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema,
Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko
katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki.
Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia,
kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa
watairamba na damu yako, naam, damu yako.” Ni tamaa inayoweza
kusababisha watu wakadhulumu, ni tama inayoweza kusababisha watu wakaua, ni
tama inayoweza kusababisha watu wakashindwa kuridhika na kuharibu mioyo yao,
Bwana ampe neema kila mmoja wetu kutokuwa na tama katika jina la Yesu Kristo.
4.
Kutokujiamini
(Insecurity).
Kutokujiamini ni
moja ya tabia inayonajisi watu wengi sana, wengine wameingia katika mtego wa
dhambi kwa sababu tu wamekosa kujiamini, kutokujiamini ni tatizo la kisaikolojia,
na kiroho pia, yaani mti haisi usalama kwa sababu anataka kutawala wengine,
control au kwa sababu ya kutokujiamini ananyanyapaa wengine au anataka sifa
zote ziende kwake, na hataki wengine wasifiwe, wakisifiwa wengine anaponda,
uadui kati ya Daudi na Sauli ulianza tkwa sababu wanawake walimsifia Daudi na
kumpa sifa kubwa kuliko walizompa Sauli 1Samuel
18:6-8 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi
aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya
Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari,
na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema,
Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika
sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi
wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli
akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.” Unaona ni ukweli ulio wazi kuwa Sauli hakujisikia salama kutokana na
kusifiwa kwa Daudi, wanawake waliimba kwa kelele za furaha na kumsifia daudi
kuwa ameua Makumi elfu na Sauli maelfu, ujumbe huu tu ulileta roho mbaya katika
moyo wa sauli aliona wazi kabisa kuwa sasa ufalme ni kama amepewa Daud, wivu
uliingia na mipango na vitendo vya kutaka kumua Daudi vilianza tangu wakati
ule, Ndugu zangu wako watu, hawataki sifa ziende kwa mwingine, wanajisikia kutokujiamini
pale wanapokuwepo watu wenye sifa na uwezo au umahiri kuliko wao, wanadhani
wanapoteza nafasi zao na wanaanza kuzitetea kwa nguvu, wakati mwingine unapoona
umeandamwa na vita za aina mbalimbali huenda wakati mwingine inasababishwa na
watu wasiojihisi kuwa salama, na usalama wao ni mpaka wewe uwe pembeni maana
unawazidi kwa kila jambo, jambo la kumshukuru Mungu ni kuwa Daudi hakuuchukua
utukufu wa Mungu watu walimsifu yeye na jambo hili lingemfanya kujifikiri mkuwa
yeyeni bora zaidi. Angekuwa na kiburi na neema ya Mungu ingemuacha!, Fikiria
magomvi mengi yanayojitokeza kati ya wana ndoa kwa sababu tu mmoja ahajiamini,
wivu unainuka na kusababisha vita na magombano, hatuna budi kumuomba Mungu
atupe kujiamini na kumtegemea Mungu ni njia pekee ya kutuwezesha kujiamini!
Unajisikiaje wengine wanaposifiwa?, unajisikiaje unapiokuwa na mtu amekuzidi
mabo fulani? Unajisikiaje mtu Fulani
anapofanikiwa? Je inakukwaza au kukuumiza hii ni hali ya kuonyesha wazi kuwa
hujiamini, hii ni moja ya tabia ngumu kuibadilisha lazima ukubali kuwa duniani
kuna watu wana mambo mazuri kukuzidi na uridhike na kile ulicho nacho na kuwa
mwaminifu tu katika talanta uliyokabidhiwa na Mungu! Kutokujiamini vilevile
kulimfanya Sara aharibu sifa yake ya kuwa na ukarimu kama mama wa imani ni yeye
aliyetoa wazo la Ibrahimu kuingia kwa Hajiri sawa na mila za kiibrania, lakini
Hajiri aliposhika ujauzito sara alijihisi kuwa duni na hivyo alianza kumtesa
Hajiri mpaka hajiri akakimbia ona Mwanzo
16:1-6 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana,
naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu,
Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata
uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa
Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka
kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata
mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni
pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa
mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa
duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu
akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema
machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake”
unaweza kuona kutokujiamini (insecurity) katika maisha ya mtu awaye yote
inaweza ikatufanya tusiwe sisi katika uhalisia wake na tukajikuta tunaingia
katika uadui au kutesa watu wengine kwa sababu tu za kutokujiamini! Na hivyo
kunaweza kutuletea unajisi katika maisha yetu!
5.
Kukosa
subira (intolerance)
Kukosa subira ni
mojawapo ya adui mkubwa anayewatia watu wengi unajisi na kuwaacha
watunwakashindwa kujitambua, kukosa subira kunaweza kutufanya tushindwe
kusamehe, kushindwa kukubali mabadiliko na kujiweka katika ya kutokukubali
mabadiliko, Maandiko yanatufundisha sana numuhimu wa kuwa na subira na biblia
inatueleza wazi kuwa subira inalipa
Yakobo 5:8-11 “Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo
yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung'unikiane, msije
mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni
manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa
uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira
yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye
huruma.” Kutokuwa na subira au uvumilivu kumepelekea watu wengi sana
kupoteza sifa zao, wakati mwingijne Mungu anaweza kuruhusu mitihani Fulani
katika maisha yetu, ili kupima muelekeo wa moyo na utii kwa Mungu, hili suio
jambo jepesi kama tunavyoweza kufikiri, wengi, wetu, tunahitaji neema ya Mungu
wakati Fulani Sauli aliagizwa na Nabii Samuel, kwamba wamsubiri ilia je kutoa
sadaka za kuteteketezwa kabla hawajaenda vitani, Lakini Samuel akachelewa kuja
na askari wakaanza kutawanyika badala ya kupigana na wafilisti, kwaajili ya
kushindwa kuvumilia Sauli aliamua kutoa sadaka ya kuteteketeza yeye mwenyewe,
alipomaliza tu Samuel alitokea na kumwambia kuwa amefanya upumbavu na kuwa
hakuitii sauti ya Mungu, kwa sababu agizo la Mungu kupitia Samuel nabii kwa
Sauli lilikuwa hivi 1Samuel 10:8 “Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia,
nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za
amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa
kuyafanya”. Unaona Sauli alipaswa kusubiri maelekezo kutoka ka Nabii
ambaye alikuwa ni msemaji kwa niaba ya Mungu, alipaswa kungoja, huenda kule
kupangiwa kusubiri kwa siku saba ilikuwa ni kipimo cha kuona utii kwake lakini
hata hivyo alisubiri hata siku ya saba bure, kwani dakika chache tu zilisalia
Samuel angewasili, lakini Sauli alishindwa kuvumilia, alishindwa kuwa na
subira, Dhambi hii ni yetu wote mara nyingi sana tumeshindwa kumsubiri Mungu au
hata kungoja wakati wa Mungu na mara kadhaa tunataka kukabiliana na hali Fulani
sisi wenyewe badala ya kufuata maelekezo ya Mungu 1Samuel 13:8-13 “Akangoja siku saba, kwa
kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao
watu wakatawanyika mbali naye. Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya
kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. Hata mara
alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye
Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. Samweli akasema, Umefanya nini? Naye
Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na
wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko
Mikmashi; basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla
sijaomba fadhili za Bwana; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya
kuteketezwa. Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri
ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako
kuwa imara juu ya Israeli milele.” Mmmh tunaweza kujifunza mambo
kadhaa katika mfano huu wa sauliSubira na uvumilivu sio kitu rahisi, lakini ni
wazi kabisa kuwa Mungu anatamani sana kuona utii wetu kwake anahitaji kuona
uvumilivu wetu katika kuliamini na kulitendea kazi neno lake, lakini pia
tunajifunza ya kuwa kuna hasara kubwa sana tunapoamua kufuata njia zetu kuliko
njia za Mungu, japo sio rahisi kwa ubinadamu wetu lakini tunahitaji neema ili
tumtii yeye na kuchagua njia aliyoichagua yeye lakini vinginevyo watu wengi
sana wamejitia unajisi kwa sababu walishindwa au tumeshindwa kuwa na subira.
6.
Hasira (Anger)
Hasira ni
mojawapo ya tabia ya kihisia ambayo inapaswa kuangaliwa kwa umakini na kila
mwanadamu, inaonekana kila mwanadamu ana hasira lakini hasira ya kupita kawaida
inaweza kutupelekea katika hali ya kutokuona mambo kwa uwazi zaidi, Paulo mtume
alifahamu kuwa wakristo wanaweza kuwa na hasira lakini aliwataka waimalize
hasira yao mapema na kuiondoa uchungu wote ikiwezekana kabla jua halijachwa ona Waefeso 4:26-27 “Mwe
na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;
wala msimpe Ibilisi nafasi.”Kukasirika kupita kawaida kunaweza kuwa
nafasi ya shetani kutushambulia na tukajikuta tumefanya upumbavu, watu wengi
kwa sababu ya kukasirika kwa haraka na a hata kufanya maamuzi wakiwa
wamekasirika wamejikuta wakiharibu mambo maandiko yanatutaka tusifanye haraka
kukaririka na lakini vilevile tusiiachie hasira kuleta madhara katika maisha
yetu ona Muhubiri 7:9 “Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira
hukaa kifuani mwa wapumbavu.” Wengi wetu tumeshuhudia na kuona mara
kadhaa migogoro yenye madhara makubwa sana katika nchi yetu na mapigano ya
kijinga yakifanyika kati ya wakulima na wafugani, unajua nini vita ya wakulima
na wafugani ndio vita ya zamani zaidi kupata kutokea na ndio vita ya kwanza
kurekodiwa katika kitabu cha mwanzo nilikuwa nikisoma stori ya Kaini na Abeli,
na Roho wa Mungu akataka nichunguze kwanza maana ya majina yao nikaona jina
Kaini linasomeka kama “qyn” kwa
kiarabu na maana yake ni “metalsmith” au
mfua vyuma na kazi yake kubwa ilikuwa ni shughuli za kilimo, na jina Abel “hbl” kwa kiarabu na maana yake
ni “herdsman” au mfugaji na kazi
yake ilikuwa ni shughuli za ufugaji, na ilikuwa rahisi sana kwa Kaini kumuua
Habili kwa sababu Kaini alikuwa mtengenezaji wa silaha vilevile hapa tunapata
picha ya mgogoro wa wakulima na wafugaji, lakini zaidi ya yote tunaona jinsi
Hasira hasa aliyokuwa nayo Kaini ilivyopelekea kufanya upumbavu na kumtia
unajisi, yeye alijaa ghadhabu na hasira na hakua tayari kutenda vizuri ili naye
abarikiwe na Mungu ona Mwanzo 4:3-7 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa
BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona
za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali,
wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.BWANA
akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea
mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Unaweza kuona
kumbe kila mara tunapokuwa na ghadhabu na kukasirika na uchungu mioyoni mwetu
tufahamu kuwa vinaweza kutuletea hasara na tukajikuta tunatenda dhambi na hata
kuyatia maisha yetu unajisi mkubwa, watu wengi sana wameharibu maisha yao na ya
wengine kwa sababu ya hasira, Bwana ampoe kila moja wetu neema kuishinda hasira
na ghadhabu katika maisha yetu katika jina la Yesu amen!
7.
Uadui
(enmity)
Uadui ni hali
ya kutokumpenda mtu au kumchukia mtu au watu kwa muda mrefu katika hali ambayo
wakati mwingine sababu zake zinaweza kuwa wazi au zinaweza kutokuwa wazi, watu
wanaweza kukuchukia bure tu, wakati mwingine sio kwa sababu unatenda mabaya
lakini kwa sababu ya ule wema ulionao unasababisha wengine wajione duni Yesu
alichukiwa bure tu bila sababu ona Yohana
15:25 “Lakini litimie lile neno lililoandikwa
katika torati yao, Walinichukia bure.” Kwa namna yoyote ile maandiko
yanatutaka tuhakikishe kuwa hatuna uadui na mtu, tuhakikishe kuwa tuna amani na
watu wote ona Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo
utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” kuwa
na uadui katika maisha kunaharibu sana mwenendo wa uhuru wa mtu na kuyafurahia
maisha, mtu wa haki anapaswa kuwatendea haki watu wote na bila kubagua kuwa
huyu ni adui au laa na maandika yanakwenda mbali zaidi kiasi
cha kututaka kuwatendea mema adui zetu kwa kuwapa mahitaji yao ikiwezekana
chakula wakiwa na njaa au maji wakiwa na kiu ona Mithali 25:21-22 “Adui yako akiwa ana
njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa
ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu.” Hii maana yake ni
kuwa hata kama mtu atatutendea vibaya hatupaswi kumlipa mabaya na badala yake
hata kama ni kisasi basi hatuna budi kumuachia Mungu alipe lakini sisi tutende yaliyo mema ona Mithali 20:22 “Usiseme,
Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa.” Kipimo cha
wema wa kiagano jipya kinatutaka kwenda zaidi ya kawaida yaani ikiwa ni pamoja
na kuwapenda, na kuwaombea na kuwa kwa kutenda hayo tutakuwa wakamilifu kama
baba yetu wa Mbinguni alivyo mkamilifu! Mathayo
5:43-48 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako,
na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowaudhi,ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye
huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana
mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao
hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la
ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa
wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Kuendeleza
uadui katika maisha yetu na kutokutafuta kuwa na amani na watu wote kumeyaweka
na kuyaharibu maisha ya watu wengi pabaya na kusababisha madhara makubwa kwa
jamii, Bwana atupe neema na kutusaidia kuwa na utulivu pande zote na tusiwe na
roho ya uadui!
8.
Kuhukumu
wengine (Prejudice)
Kuhukumu wengine
kwa kiingereza neno linalotumika ni prejudice
ambalo kwa mujibu wa Dictionary ya
Oxford maana yake inasomeka –
preconceive opinion that is not based on reason or actual experience, giving an
opinion about someone which is covered with bias. Kwa tafasiri isiyo rasmi
ni kutoa mawazo, au maelezo kuhusu mtu
ambayo huna uthibitisho au utafiti wa kina kuwa yana ukweli au usahihi, au
kutoa hukumu katika mtazamo wa fikra zako, Kwa mfano mtu anaweza kuwa na
tatizo la iana Fulani au ulemavu wa aina Fulani na tukafikiri kuwa amepatwa na
ulemavu huo kwa sababu yeye au wazazi wake walifanya dhambi Fulani Yohana 9:1-3 “Hata
alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake
wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake,
hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake;
bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.” Hapa tunaona wazi kuwa
kwa mtazamo wa wanafunzi wa Yesu au wayahudi kwa ujumla walikuwa wanadhani
ikitokea mtu ana tatizo basi walihesabu kuwa ni laana ya kiungu au ni adhabu
inayotokana na dhambi, kwamba huyu alikuwa mlemavu au kipofu tangu kuzaliwa
walidhani ni labda huenda wazazi wake au yeye mwenyewe amefanya dhambi, Lakini
mtazamo wa Yesu Kristo ulikuwa tofauti sana,
hivi ndivyo tulivyo wanadamu, tunahukumu kwa haraka wakati mwingine
tukifikiri kuwa tuko sahihi, wakati Fulani nilipiokuwa Korea moja ya wanafunzi
nwa chuo cha Biblia cha Methodist aliyekabidhiwa sisi ili kututembeza sehemu
mbalibali alikuwa na tattoo kubwa limechorwa mwilini mwake, na kwa haraka sana
nilifikiri kuwa huenda mtu huyu hajaokoka na au kama atakuwa ameokoka basi
kiwango mcha wokovu wa watu hawa kiko chini, mno wanawezaje kutupa mtu wa aina
hii na tena anayeonekana mhuni, na tena yuko chuo cha Biblia? Ukweli ni kuwa
mtu yule alikuwa ameokoka na anayeokoa ni yesu Kristo na yhakunamkiwango cha
thamani ya wokovu wa mahali Fulani kwani wote tumeokolewa kwa damu ya Yesu, mtu
huyu alikuwa ameokolewa na Yesu kutoka katika janga la uhuni uliokuwa
umepindukia na sasa alikuwa ni mtu mwema na hata kule kututembeza walikuwa
wakiangalia usalama wetu, sio kila mtu aliyechorwa tattoo ni mhuni au ni mtu
mbaya kumbe wengine ni watumishi wa Mungu wametolewa huko duniani na wamekuwa
kiumbe kipya, kuhukumu wengine au kuwa na mawazo mabaya dhini yaw engine
kunaweza kutuweka katika upande usio sahihi wa kimtazamo kuliko vile Mungu
anavyotazama mambo,angalia kisa hiki kwa mfano:- Luka 7:36-48 “Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake;
akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama,
mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa
ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari
yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza
kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake,
akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu. Basi, yule Farisayo
aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii,
angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba
ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo
kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena.
Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia
dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa,
aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni
akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua
haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu?
Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu
amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.
Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu
yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu
marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi,
kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha
alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako.” Umeona! Simon alikuwa
mtioza ushuru aliyemualika Yesu kwenye karamu ya jioni na mara anaingia
mwanamke kahaba anasimama karibu na Yesu, moyoni Simon anajihoji hivi nimealika
nabii au chokoraa maana kama huyu jamaa angelikuwa nabii angejua kuwa mwanamke
huyu ni wa kufukuza tu maana hafai, Lakini Yesu alitambua kile kilichokuwa
kinaendelea katika mawazo ya Simeon, alionyesha wazi kuwa huyu mwenye dhambi
nyingi hivi zikisamehewa atampenda Yesu kwa kiwango kikubwa zaidi!, wakati
mwingine tumefikiri vibaya kuwa watu wenye dhambi kubwa sana hawawezi
kusamehewa na Mungu, au tumefikiri kwa kuwa tumeua hatuwezi kusamehewa ndio
maana katika mitazamo ya kiungu biblia inatuonya juu ya kuhukumu wengine kwa
haraka Mathayo 7:1-5 “Msihukumu,
msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa;
na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi
kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako
mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje
nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani
ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe,
itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema
kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.” Unaona maandiko ni
kama yanatutaka kujitathimini wenyewe kwa kina zaidi tunapoona shida kwa
wenzetu na kujishughulikia sisi zaidi ili ikiwezekana ndipo tuone vema
kushughulikia ya wengine kama sisi tuna yetu ya kuyashughulikia na tukaacha na
kujihusisha na ya watu wengine huo ni unafiki, kwa hiyo ni lazima tujifunze
kuacha kuhukumu wengine, wakati mwingine hata kama kile tunachokihukumu kina
ukweli, maandiko yanatuonya kuwa sio kazi yetu kushughulikia hilo kwani Mungu
mwenyewe ana njia sahihi ya kushughhulikia mambo ona Warumi 14:4 “Wewe u nani unayemhukumu
mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam,
atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”
9.
Zinaa/Uasherati
(Adulterry and Sexual immorality)
Kwa mujibu wa
mafundisho ya Yesu Kristo, Zinaa na uasherati ni miongoni mwa mambo yanayomtia
mtu unajisi, kwa lugha nyingine yanayoharibu na kumchafua mwanadamu, uasherati
na zinaa katika lugha ya kiyunani vinaitwa “PORNEIA” kwa kiingereza sexual immorality , hii inajumuisha maswala
ya kufanya ngono nje ya utaratibu unaokusudiwa na Mungu, inajumuisha swala zima
la kuangalia picha za ngono kumbuka neno Porneia ndilo mzizi wa neno la
kiingereza Pornography, via vya uzazi ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini Mungu
alikusudia kuwa vitatumika kwa utaratibu maalumu, nje ya utaratibu maalumu
zinaa na uasherati humtia mtu unajisi, na ndio maana torati ilikataza zinaa Kutoka 20:14 “Usizini”
Hata hivyo kwa maelezo ya Yesu Kristo zinaa inatoka ndani, inatoka moyoni na
isipodhibitiwa huweza kumtia mtu unajisi, na ndio maana Yesu akataka
kulishughulikia jambo hili kutoka ndani Mathayo
5:27-28 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini
mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini
naye moyoni mwake.” Kwa lugha nyingine Yesu alikuwa anataka kila
mmoja ajue kuuweza mwili wake yaani aweze kuidhibiti akili, aweze kuidhibiti
tama ili tama hiyo isizae dhambi na kuleta uharibifu ona Yakobo 1: 13-15 “Mtu ajaribiwapo, asiseme,
Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye
mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe
huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa
dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” Unaona Zinaa na
uasherati hukaa moyoni, na kwaajili ya hayo, Yesu alitaka kila mmoja ajue namna
ya kuudhibiti moyo wake ili asifikie ngazi ya kujitia unajisi, kwa kawaida
zinaa huweza kuathiri maeneo matano Muhimu katika maswala ya kimwili na kiroho
a. Inaharibu uhusiano wetu na Mungu kwa
sababu ni Mungu aliyeelekeza katika neno lake kuwa tusizini kwa msingi huo
tunapofanya zinaa, maana yake tunaharibu uhusiano wetu na Mungu na kuhesabika
kama wavunja sharia au mtu aliyelidharau neno la Mungu 2Samuel 12:9 “Kwa nini umelidharau neno la
Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga,
nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.”
Unaona Daudi alipofanya zinaa nabii alimhoji kwanini umelidharau neno la
Bwana, kwa hiyo zinaa na uasherati unapofanyika mtu huathiri uhusiano wake na
Mungu
b. Inaharibu maisha yako ya ndani - 1Wakoritho
6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu
ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake
mwenyewe.” Maandiko yanatufundisha kuwa zinaa na uasherati unaharibu
maisha yetu ya ndani, andiko hili linazungumzia kuwa mtu akifanya zinaa
anatenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe! Neno mwili katika lugha ya
kiibrania ni “NEPHES” ambalo maana
yake ni nafsikwamba zinaa na uasherati ni dhambi inayoharibu nafsi yaani
inakamata akili na kuinajisi akili na kuifanya akili yako kutawaliwa na dhambi
hiyo na hivyo kutoa nafasi ya kuirudia tena na tena hivyo kuliharibu Hekalu la
Mungu, kwa hiyo kufanya zinaa ni
kuangamiza nafsi yako kabisa ona Mithali
6:32 “Mtu
aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi
yake.” Unaona maandiko yuako wazi kuwa unaharibu nafsi yako!
c. Inaharibu uhusiano wetu na wengine – ni
muhimu kufahamu kuwa kusudi lingine kubwa la Mungu kukataza zinaa ni kulinda
uhusiano wetu na watu wengine, unapofanya zinaa au uasherati unaharibu
mahusiano, lakini sio hivyo tu utavunjiwa Heshima watu watakudharau na
kukupuuza watakapogundua kuwa huna adabu hujiheshimu na wanaweza kukudhani kuwa
wewe ni Malaya au kahaba, Mithali
6:32-33 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa;
Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa
heshima; Wala fedheha yake haitafutika.”
d. Inaharibu huduma na ushuhuda – Mungu
anatarajia kila mtu mwadilifu kuwa ni chumvi ya ulimwengu na nuru ya ulimwengu,
kuwa sisi tutauangazia ulimwengu na kuwa kielelezo au mfano wa kuigwa hivyo
sisi tunasioma na ulimwengu, ulimwengu unaangalia na kujifunza kutioka kwetu 2Wakoritho 3:2-3 “Ninyi
ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu
wote;” unaweza kuona kwa msingi huo Neno la Mungu halitaki wakristo
wasomwe vibaya na wala mambio mabaya yasitajwe kwetu kamwe Waefeso 5:3-5 “Lakini uasherati usitajwe
kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo
watakatifu; wala aibu wala maneno ya
upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili
mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa,
ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.”
Kwa misingi hiyo sasa ni muhimu kwa kila mtu mwenye kupendezwa na uadilifu
kujilinda na zinaa na uasherati kwani vinaharibu na kunajisi mioyo yetu nay a
watu wengine.
10.
Ushirikina
“Witchcraft” – Ni hali ya kuacha kumtegemea Mungu na kutegemea vitu
vingine, au kuchanganya kati ya mambo ya Mungu na miungu au mashetani, kwa kiingereza witch craft, Sorcery,
spiritism, black magic, bad eye, fellowship with demons kwa kiyunani “PHARMAKEIA” kwa mujibu wa maandiko
ushirikina pia hupelekea mtu kuharibu maisha yake na kujichafua au kujitia
unajisi, maandiko yanatukataza kushirikiana na mashetani 1Wakoritho 10:20-21 “Sivyo, lakini vitu
vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi
ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe
cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.”
Kitendo cha kumshirikisha shetani katika mahitaji yako au tamaa zako ndio
kinaitwa ushirikina yaani wewe mwanadamu ni mali ya Mungu, lakini badala ya
kumtegemea Mungu kukuitana na mahitajhi yako unamtegemea shetani au nguvu za
giza, Mungu hapendezwi na watu washirikiana na hivyo kushiriki mambo ya kichawi
ni kujitia unajisi katika uhusiano wako na Mungu na wanadamu Walawi 19:31 “Msiwaendee
wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi
BWANA, Mungu wenu.” Unaona maandiko yanaonyesha kuwa kuwaendea
waganga yaani wenye npepo na wachawi kutaleta unajisi, wataharibu uwezo wako wa
kumtegemea Mungu, kuwaendea waganaga
na wachawi kwaajili ya kutafuta msaada kunaleta hukumu ya Mungu kwa haraka sana
, kunajenga imani bandia ya kinafiki isiyotokana na neema wala nguvu za Mungu,
Mungu alitangaza hukumu kwa watu kadhaa na kifo kwa sababu walipokuwa na shida
hawakwenda kuutafuta uso wa Mungu bali mashetani ona 2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika
dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe,
akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona
ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende
ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu
hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa
Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda
ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.” Ukweli ni kuwa
Mungu alichukizwa na mfalme Ahazia kutokana na moyo wake wa kijinga wa
kutokumtegemea Mungu na kutegemea nguvu za giza na hivyo alihukumiwa kufa, Sauli
mfalme wa Israel naye alikataliwa na Mungu na kufia vitani kwa sababu moyo wake
haukumtii Mungu na hivyo aliamua kwenda kwa mpiga ramli ilimkuuliza huko na
aliambiwa kuwa Bwana amekuwa adui yake 1Samuel
28:5-16 “Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti,
huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana. Lakini Sauli alipouliza kwa
Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Ndipo
Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi,
nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko
mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa
mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia
yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi,
ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako. Yule mwanamke akamwambia, Angalia,
unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa
utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili
kuniua? Naye Sauli akamwapia kwa Bwana, akasema, Aishivyo Bwana, haitakupata
adhabu yo yote kwa jambo hili. Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani
nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli. Hata yule mwanamke
alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli,
akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia
Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka
katika nchi. Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye
amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe,
akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona
umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika
sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu
tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe
unijulishe nifanyeje. Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa Bwana
amekuacha, naye amekuwa adui yako? ”
Ushirikina ni zinaa ya kiroho, Mungu ameapa katika neno lake kuwa ataukaza uso
wake yaani hatakuwa na rehema kwa mtu atakayewaendea wachawi au waganga ona Walawi 20:6 “.Na
mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza
uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.” Unaiona uso wa
Mungu utakazwa dhidi ya mtu mshirikina sio hivyo tu mawasiliano yoyote na wenye
pepo au waganga ni machukizo kwa Mungu
Kumbukumbu la torati 18:10-12 “Asionekane kwako mtu
ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye
bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi,
wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana;
kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.” Unaweza
kuona ni wazi kabisa kuwa Mungu anachukizwa mno na ushirikina, nani jambo la
kushangaza kama mtu ajiita mkristo au hata muislamu kisha akawa mshirikina
kwani vitabu vyote vimekataza maswala kama haya, tulisoma kisa cha sauli na
maandiko ynaweka wazi kuwa sababu ya kifo chake ilichangiwa pia na kuwaendea
waganga 1Nyakati 10:13-14 “Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa
Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa
mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake, asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na
ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.
11. Dharau au Kutokujali “insensitivity” – Moja
ya maswala yanayoweza kuwatia watu unajisi ni pamoja na dharau, au kutokujali
insensitivity jambo hili pia huondoa thawabu ya Mungu na kutukosesha neema kama
mtu akiwa na Dharau na majivuno ya ndani yenye tabia ya kupuuzia vitu au kitu,
mtu mwenye dharau hachukui tahadhari, hajilindi, hafikiri katika kile
anachofanya jambo ambalo linaweza kuwa lenye kuleta madhara, Mithali 3:34 “Hakika yake huwadharau
wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.” Biblia inaonyesha
kuwa kwa sababu ya dharau pia watu hujinyima nafasi ya kujifunza na kupokea
maarifa na hekima kutoka kwa Mungu Mithali
1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali
wapumbavu hudharau hekima na adabu.” Watu wengi sana nyakati za Yesu
walishindwa kupokea neema ya kumjua Yesu kwa sababu tu walidharau hata kule
alikotokea na kwa sababu hiyo Yesu hakufanya miujiza mingi kwa sababu
hawakumuamini yaani walimdharau Mathayo
13:54-58. “Na alipofika nchi yake, akawafundisha
katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii
na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na
nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo
hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu
akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na
nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya
kutokuamini kwao” mtu mwenye dharau anaweza kukudharau hata kutokana
na eneo unalotokea, Yesu alitokea kwenye mji usioheshimika sana na ambao hauna
historia ya kutoa nabii, kwa hiyo iliposemekana kwamba anatokea Nazareth watu
walipuuza na kudhani kuwa haijawahi kutokea nabii akatokea huko!, Yohana 7:46-52 “Wale
watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. Basi
Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu
amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati
wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni
mmoja wao),Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua
atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta,
ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.” Dharau ya viongozi wa
dini na baadhi ya mafarisayo kuhusu eneo Fulani liliwanyima uwezo wa kumkubali
masihi, na hivyo walibaki katika dhambi yao kwa kutokumuamini Yesu, wengi wetu
tunaweza kuwadharau wengine kwa sababu ya hali zao, muonekanio wao, upole wao,
kabila lao, historia yao na kule wanakotokea! Yohana 1: 45-46 “Filipo akamwona
Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na
manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza
neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.” Kwa bahati
njema Nathanieli na filipo walimuamini Bwana Yesu lakini jamii yao ilikuwa
imeelekezwa wazi kuwa hakuna kitu chema kinaweza kutokea huko hivyo wengi
walidharau na kuikosa neema ya kumjua masihi, dharau imewanajisi wengi na
kuwafanya wengi kupoteza mahusiano na
Mungu au wanadamu wengine hatupaswi kupuuzia au kutokujali, na ndio maana ni
muhimu kwetu kumuheshimu na kumsikiliza kila mtu kwa vile hatuwezi kujua nani
atakuwa nani siku moja! Kudharau kumetufanya tusiwajali wengine, kumetufanya
pia tuache kutioa kipaumbele kwa mambo ya muhimu kwa sababu ya kudhau kwetu!
12. Kutokusamehe (Unforgiveness)
Kutokusamehe
kunaharibu maisha ya mtu, kunatuweka katika kifungo! kutokusameheni moja ya
maswala yanayomtia mtu unajisi, tunajisikia amani na furaha tunaposamehe, na
tunaposamehewa, kwa msinmgi huo maandiko yanatufundisha umuhimu wa kusamehe
wengine, Ni msamaha ndio unaotupa ufunguo na neema ya kupokea msamaha na sisi kutoka
kwa Baba wa Mbinguni Mathayo 6;14-15 “Kwa
maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.
Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa
yenu.” Kuna shida kubwa sana tusiposamehe Bwana Yesu katika
mafundisho yake anatupa stori inayotufundisha umuhimu wa kusamehe,kwa sababu
sisi nasi tunahitaji kwa namna Fulani kusamehewa na Mungu baba yetu wa
mbinguni, maana kumbuka hakuna mwanadamu aliyemkamilifu, sisi tumemkosea Mungu
mara nyingi sana na hivyo ili iweze kuwa rahisi kwetu kusamehewa na Mungu ni
muhimu sana na sisi tukasamehe wanaotukosea ona Mathayo 18:23-35 “Kwa sababu hii ufalme wa
mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.
Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.Naye
alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake,
na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka,
akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa
mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka,
akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika
koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi,
akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda,
akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.
Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda
wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia,
Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je!
Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?Ndivyo na Baba
yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu
ndugu yake ”
Kutunza uchungu
wa kutokusamehe sio tu kunaendeleza uhasama kati yako na aliyekukosea bali kunakuharibu
wewe mwenyewe na kukutia unajisi, kutkusamehe kunakufanya uwe mtumwa wa watu,
kutokusamehe kunakufanya uwe chini ya udhibiti wa mtu yaani dunia inakuwa chungu
anapotokea mtu unayemchukia usiyempenda na usiyemsamehe, kutokusamehe
kunakufanya uwe mfungwa katika gereza lake, unafungwa katika huzuni, unafungwa
katika gereza la kukosa amani, unafungwa katika gereza la vita vya moyoni,
unafungwa katika gereza la hasira, unafungiwa nje ya furaha na ushirika,
uchungu huu ni matokeo ya kiburi na kujihesabia hakli au kutokutaka kupoteza
haki zako, na kutaka kulipiza kisasi, kusamehe ni kukubali kupoteza haki zetu,
ni kukubali kuachilia ili mtu mwingine asi tu control, na hivyo tutakuwa free
kwa mtu huyo na kwa Mungu pia.
13.
Choyo
(Greed).
Moja ya vitu
ambavyo pia huutia moyo unajisi ni pamoja na tabia ya kupenda kujilimbikizia
kila kitu sisi wenyewe, tabia ya choyo, choyo kinawafungia watu wengi Baraka za
Mungu, Yesu amewahi kuonya kuwa uzima wa mtu hauko katika wingi wa vitu
anavyomiliki akituonye dhidi ya tabia ya choyo ona Luka 12:15 “Akawaambia, Angalieni,
jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo
navyo.” Utoaji na kuwahudumia wengine hutuletea furaha ya kweli, angalia kisa hiki cha tajiri mmoja
Bilionea
MNigeria Femi Otedola alipoulizwa
kwenye interview, ya Simu na Mtangazaji wa Radio, "Sir ni kitu gani
unachokumbuka kilichokufanya uwe na
furaha maishani?" Femi alijibu:
"Nimepitia
hatua nne za furaha katika maisha yangu na mwishowe nilielewa maana ya furaha
ya kweli." Hatua ya Kwanza ilikuwa ni kutafuta Mali na kulimbikiza. Lakini
katika hatua hii sikupata furaha niliyoihitaji. Nikaingia hatua ya pili ya
kujinunulia vitu vya thamani. Lakini niligundua kuwa vitu vyote hivi vinakupa
furaha ya muda tu ambayo haidumu. Nikaingia hatua ya tatu ya kufanya miradi
mikubwa. Ni katika hatua hii nilikuwa ninasambaza 95% ya Diesel Nigeria yote na
Africa Kwa ujumla. Pia nilikuwa mmiliki mkubwa wa Vessel Africa na Asia. Lakini
pia hapa sikupata furaha niliyokuwa nimeifikiria. Hatua ya nne ilikuwa ni
kipindi ambacho Rafiki aliniomba kununua Wheelchairs Kwa ajili ya watoto
walemavu. Walikuwa kama watoto 200 hivi. Baada ya kuombwa na rafiki yangu
nilinunua Wheelchairs 200 mara moja. Lakini pia aliniomba niambatane naye ili
nikawakabidhi watoto zile wheelchairs. Nilijiandaa nikaambatana naye. Nikawagawia zile wheel chairs Kwa mikono
yangu mwenyewe. Niliona furaha ikitawala kwenye nyuso za hawa watoto. Nikawaona
wamekaa kwenye wheelchairs, wakizunguka na kufurahia. Ilikuwa ni kama wako
Picnic wakisherehekea ushindi wa bahati nasibu. NiIihisi furaha ya kweli ndani
yangu. Nilipotaka kuondoka mtoto mmoja alinishika miguu yangu. Nilijaribu kujinasua
taratibu lakini alinikazia macho akinitazama usoni. Niliinama chini
nikamuuliza, kuna kitu kingine unahitaji? Jibu alilolitoa mtoto huyu sio tu
kwamba lilinipa furaha bali pia lilinifanya nibadili kabisa mtazamo wangu juu
ya maisha. Mtoto huyu alisema:
"Ninakuangalia ili niikumbuke Sura yako, siku nikikukuta mbinguni
niweze kukutambua na kukushukuru tena." Maandiko yanasema ni heri kutoa
kuliko kupokea
Matendo
20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu
hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo
yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge,
na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa
kuliko kupokea.”
Utoaji unaleta
Baraka za kiungu, utoaji ni kuwatangauliza wengine au kumtanguliza Mungu kwanza
kabla yetu, kutokutoa ni ubinafsi, tunapotoa Mungu hufungua milango ya Baraka
kwetu na kututumia kama bomba la kutiririsha Baraka utoaji ni moyo na sio hali
ya kuwa na kitu, wako watu wana moyo na wako tayari hata kile kiduchu
alichonacho aweze kushirikiana na wengine ona 1Wafalme 17:8-16 “Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta,
ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko
akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji,
kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee,
nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.
Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande
cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina
mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami
ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule
tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini
unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.
Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka,
wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya
nchi. Basi akaenda, akafanya kama
alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku
nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha,
sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.” Tunapomtanguliza Mungu katika utioaji Mungu
hatatuacha na kamwe hatutapungukiwa na kitu, utoaji wa kikarimu kama huu aliokuwa
nao mjane wa Sarepta umeweza umeweza
kuwekwa Rekodi zake katika maandiko kwa sababu ulikuwa ni utoaji wa namna ya
pekee sana utoji unaleta Baraka na kwa sababu hiyo Mungu na atupe neema ya
kutokuwa wabinafi na atulinde na choyo katika jina la Yesu amen!
14.
Kiburi
(Pride)
Moja wapo ya
maswala ya msingi naya muhimu ambayo katika maisha yetu tunapaswa kujihami nayo
siku zote ni kiburi, kiburi ni mojawapo ya tatizo na changamoto ambayo imewatia
wengi unajisi, ni ukweli usiopingika kuwa mtu akiwa na majivuno na kiburi moja
kwa moja anakuwa adui wa Mungu hata kabla ya kuwa adui wa shetani 1Petro 5:5 “Vivyo
hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,
mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema.” Unaona
kiburi kinatutenga na neema ya Mungu, na kwa kawaida kiburi huenda pamoja na
maangamizi, kila wakati huwa ninaogopa sanasana ninapoipitia Biblia na kuona
jinsi Mungu anavyoonya katika neno lake na nnamuomba sana Mungu anilinde na
maangamizi ya aina hii, inaonekana wazi kabisa hakuna neema wala rehema kwa mtu
mwenye kiburi, biblia ni kama inatangaza vita na kueleza wazi kuwa kama una
kiburi hautatoboa, inaelezea wazi kuwa kuna maangamizi pale kiburi kinapokuwepo
ona Mithali 16:18-19 “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari
hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini,
Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.” Unaona kuna uangamivu na maanguko hii inatisha
ujue ni lazima kuomba rehema kila wakati kwa sababu Biblia inaonyesha pia kuna
kuaibishwa kwamba kijapo kiburi ndipo ijapo aibu ona Mithali 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo
aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.” Kwa mujibu wa maelezo ya
kibilia ni dhambi hii ilianza kujipenyeza ndani ya moyo wa ibilisi na kwa kweli
hukumu yake haikukawia Isaya 14:13-15 “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua
kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano,
Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu,
Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za
mwisho za shimo.” Unaweza kuona shetani kwa kiburi alijiambia moyoni
tendo hili, la kujieleza moyoni Mungu alilichungulia na kuleta hukumu kwa
haraka, Luka 14:11 “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye
atakwezwa.” Shetani alijiinua kinyume na mamlaka kwa kiburi chake na
hivyo aliharibiwa na kushushwa Ezekiel
28:13-18 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu;
kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na
almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na
baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako;
katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye
kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa
Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika
njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa
wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda
dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu
kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe
hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima
yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme,
wapate kukutazama. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako,
umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao
umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote
wakutazamao.” Mungu alimhukumu shetani na kumtupilia
mbali kwa sababu ya moyo wake wa kijiinua moyo wake wa kujivuna na kiburi, kiburi
ni tatizo ambalo ni vigumu sana kulijua au kujijua linapokuwa limekuingia
lakini kuna dalili chache zinazoweza kutusaidia kujielewa kama kimetuingia
-
Kutokulitetemekea neno la Mungu Isaya 66:1-2 “Bwana
asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu
yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni
mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote
vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu
aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”
-
Kutokubali kushauriwa – Mithali 13:10 “Kiburi huleta mashindano tu;
Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.”
-
Hujifikiri kuwa yeye ni bora zaidi ya watu
wengine – Wafilipi 2:3-11 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno;
bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi
yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya
wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo
Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa
sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana
utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena,
alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia
Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu
vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
-
Hujawa na maneno ya kujivuna wao tu – 1Samuel 2:3 “Msizidi
kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana
ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.”
-
Hujifikiri kuwa wanajua kila kitu 1Wakoritho 8:2 “Mtu
akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”
-
Wana majivuno na ukaidi Mithali 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia
uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.”
-
Hawampi Mungu utukufu na hufikiri kila kitu
wamefanya kwa uweza wao - Isaya 10:13 “Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda
jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka
ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama
afanyavyo shujaa.”
-
Hufikiri kuwa njia yake ni sahihi zaidi – Mithali 16:25 “Iko
njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
Madhara ya kiburi Mungu atatoa adhabu – Mithali 16:5 “Kila
mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu.”, kiburi
kinaleta uharibifu Mithali 18:12 “Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla
ya heshima hutangulia unyenyekevu.” Mungu alimshughulikia Mfalme
Nebukadreza kwa sababu ya Kiburi Daniel
4:28-33 “Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.
Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme
katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga
mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa
enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja
kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe;
Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa
mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni;
utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata
utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye
humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata
Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili
wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama
manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.”
Bwana atupe
neema kuwa mbali na mambo yote yanayotia unajisi na kutuletea madhara ya aina
mbalimbali katika maisha yetu sawa sawa na mapenzi yake na atupe neema ya
kuishi maisha matakatifu na ya kumpendeza yeye na kutulinda na kiburi na
majivuno na atupe neema ya kuwa wanyenyekevu katika jina la Yesu Kristo amen!
Na. Rev.
Innocent Kamote
Mkuu wa
wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni