1Timotheo 5:17-18 “Wazee watawalao
vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa
kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe
apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.”
Utangulizi:
Usimfunge
ng’ombe kinywa apurapo nafaka! Ni moja ya agizo tata la kibiblia ambalo neno la
Mungu limeamuru kanisa kulifanyia kazi ili Baraka za Mungu ziweze kumiminika
kwetu hususani katika nyakati hizo za agano jipya!. Tuusome tena mstari huu kwa
makini na kisha tuanze kuuchambua na kuufanyika kazi ili tuweze kupata uelewa
unaokusudiwa!
1Timotheo
5:17-18 “Wazee
watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao
kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe
apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.”
Katika mukhtadha
wa mstari huu kwanza tunaona Paulo mtume akitoa maagizo ya namna mbalimbali,
katika kuwahudumia wajane walio wajane kweli kweli, kisha anazungumzia Kustahili
heshima maradufu kwa wazee wanaotawala vema yaani wale watu wanaojitaabisha
katika kuhubiri na kufundisha neno la Mungu. Ni muhimu kuchambua maswala kadhaa
ya kuyatilia maanani kabla ya kuingia katika kiini cha somo letu! Tutajifunza
somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Wazee watawalao vema
·
Wahesabiwe kustahili heshima maradufu
·
Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka.
Wazee watawalao vema.
Wazee watawalao vema ni akina nani!
Neno wazee linalotumika hapo katika maandiko ya kiyunani linasomeka kama “PROESTOTES” Kwa kiingereza Presbyter ambalo maana yeke ni yeye mwenye kuongoza serikali ya kikanisa ecclesiastical Government au kwa lugha rahisi mwangalizi wa Kanisa, Mchungaji wa kanisa au askofu watu wenye sifa kama zile zilizoainishwa katika
1Timotheo 3:1-7 “Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”
Kwa hiyo maandiko yanawazungumzia watu wenye huduma ya
kichungaji, wanaotoa huduma za kiroho kwa kuwahudumia watu kwa neno la Mungu
kwa kuhutubu yaani kuhubiri na kufundisha maandiko yanataka watu hawa
waheshimiwe sana, yaani wanastahili heshima maradufu! Kwa msingi huo Biblia inatoa heshima kubwa sana na kuamuru
kuheshimika kwa watu wanaofanya kazi ya kuhubiri na kufundisha, kwa bahati
mbaya sana watu wengi na makanisa mengi na hata taasisi, wameifanya kazi hii au
kuidhania kazi hii kuwa ni kazi duni naya kiwango cha chini nani ya kujitolea
kiasi ambacho watu wanaohudumu hawapewi chochote na huishia kudharauliwa kama
watu wasiotaabika kwa kazi hiyo ngumu! Biblia inaonyesha kuwa kazi hii sio
nyepesi na kuwa wahubiri kama zilivyo kazi nyingine wanajitaabisha kwaajili ya
maisha ya watu kiroho na kimwili pia. Kwa msingi huo maandiko ni kama yanaagiza
kuwa watu hawa walipwe, angalia maneno yale mtenda kazi anastahili ujira wake! 1Timotheo 5:18 “Kwa
maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda
kazi astahili ujira wake.”
Wahesabiwe kustahili heshima maradufu.
Kwa msingi huo
maandiko yanaamuru kuwa watu wafanyao kazi hii ya kichungaji wanastahili
kulipwa, neon heshima maradufu maana yake wasihesabiwe kama watu wanaojitolea
tu, watu watoe sadaka na sadaka itumike kuwalipa maandiko hayaichukulii kazi ya
kuchunga kuhubiri na kufundisha kama kazi ya chini duni na ya kipuuzi hapana
hii ni kazi iliyoko chini ya utawala na serikali ya Mungu hivyo watu hawa
wasiachwe wakaishi maisha duni nay a mateso na kudhalilika kama kanisa litajua
umuhimu wa kuwatia nguvu wahubiri na wachungaji na kutoa kile wanachobarikiwa
na kuwasaidia watumishi hao wa Mungu wanatkuwa na uwezo mkubwa sana wa kuacha
kujitafutia vipato vyao na familia zao na badala yake watajitoa zaidi na kutoa
kipaumbele katika kulihudumia neno ona
Matendo 6:1-7 “Hata siku
zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya
Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa
katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi,
wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi
ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye
kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu
katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa
mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na
Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa
Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka
mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana
katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.”
Petro alikuwa
anaonyesha wazi kuwa kulihudumia neno la Mungu sio kazi ya kukurupuka tu, inahitaji
kujitoa kwenye kiwabngo kikubwa sana kunakoitwa kulihudumia neno, yaani hii
hujumuisha kuomba na kufanya maandalizi ya neno la Mungu kwaajili ya watu wake
na kufanya huduma za kichungaji, kazi hii hata ukiacha kuwa maandiko yamesema
watu hawa walipwe lakini pia Mungu amekusudia kuwapa taji ya utukufu huko
mbinguni baada ya kuja kwake Bwana ona
1Petro 5:1-4 “Nawasihi
wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya
Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la
Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama
Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama
wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile
kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile
isiyokauka.”
Utaratibu wa
kuhakikisha kuwa watumishi wa Mungu wanapata posho yao kutokana na kuhudumu
madhabahuni haukuanza tu katika nyakati za agano jipya lakini umeendelezwa
kutoka katika agano la kale, tangu mwanzo Mungu akliandaa mazingira yaliyokuwa
wazi kwa manabii wa kale zaidi na hata kwa jamii ya makuhani walawi kuwa waishi
kutokana na madhabahu, huduma ya kichungaji haiitaji mtu adhurule inahitaji mtu
awe na muda wa kuutafuta uso wa Mungu na kuyajua mapenzi yake ili awajulishe
watu wake na kuwaonyesha njia pia kuomba kwaajili ya wenye mahitaji mbalimbali,
hivyo tangu enzi za agano la kale walielewa kuwa huwezi kumwendea mtumishi wa
Mungu mikono mitupu!, sio hivyo tu lakini hata watu waendao kwa waganga wa
kienyeji pia huwa hawaendi mikono mitupu
1Samuel 9:5-8 “Hata
walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye,
Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri
sisi. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu
mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda
yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea. Ndipo Sauli akamwambia
mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani?
Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu
wa Mungu; tuna nini sisi? Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama,
mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha
hiyo, atuambie njia yetu.” Unaona katika hali ya kawaida Sauli aliweza kufikiri na kuelewa kuwa
ni mapenzi ya Mungu kumuendea Mtu wa Mungu Nabii au Mchungaji kwa wakati huo
ukiwa na zawadi, kwa sababu yeye anashughulika kuyatafuta mapenzi ya Mungu
kwaajili yatu/yenu/yao Mungu analitambua hilo vema.
Watumishi wa
Mungu pia ni watu waliko mstari wa mbele katika vita ya kupamba na shetani na
kuipeleka injili kwa msingi huo wao huitwa askari ona 2Timotheo 2:3 “Ushiriki taabu pamoja nami,
kama askari mwema wa Kristo Yesu” kuwaacha watumishi wa Mungu bila
msaada wetu ni sawa na kumuachia askari aende vitani kwa gharama zake mwenyewe
jambo hili limekemewa vikali katika maandiko angalia mafundishi ya Paulo mtume
kuhusu kazi hii ona
1Wakoritho 9: 7-14 “Ni askari gani aendaye vitani wakati wo wote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi? Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo? Kwa maana katika torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe? Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake. Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.”
Unaweza kuona ni amri ya Mungu na ni mapenzi yake kuwa wote
wanaomtumikia kwa njia mbalimbali wapate riziki yao kwa njia ileile
wanayotumika, Mungu anatarajia kuwa utakuwepo utaratibu maalumu wa kuwapatia
watumishi wake fedha kwaajili ya kujikimu, Kuwatumia watu wa Mungu bila
kuwafikiria mahitaji yao ni dhambi? Hii ndio heshima maradufu wanayoweza kupewa
wale wanaojitaabisha katika kazi ya Mungu kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja
kuhutubu na kufundisha angalia, Kanisa lazima ufikie wakati tuache uchoyo, uko
wakati eti mtu anaumia kuona kuwa mchungaji analipwa, wako watu hawaoni raha
hata kuona wachungaji wakifanikiwa kwa hiyo kwa miaka mingi sana kazi hii
imefikiriwa kuwa duni, na kuwa ni ya kujitoa tu, matokeo yake tumeidhoofisha
kazi ya kichungaji na kupoteza Baraka za Mungu kwa muda mrefu!
Usimfunge
kinywa ng'ombe apurapo nafaka.
1Timotheo 5:17-18 “Wazee watawalao
vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa
kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe
apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.” Tunarejea
sasa katika mstari wetu wa msingi ambao ndio una kiini cha somo letu!
Kimsingi andiko
hili Paulo mtume amelinukuu kutoka katika agano la Kale hususani Kumbukumbu la torati 25:4 Biblia mahali
hapo inasema “Ng'ombe
apurapo nafaka usimfunge kinywa.” Ingawa
andiko hili lilitumika kwa lugha ya mficho lakini linafafanuliwa wazi katika
mtazamo wa agano jipya na Paulo amelieleza kwa kina zaidi kama tulivyoona
Katika 1Wakoritho 9:7-14, Kwamba
hakuna askari aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe! Mafundisho kuwa mtenda
kazi anastahili ujira wake yaani mshahara wake ni swala ambalo liko wazi
kuanzia na Bwana Yesu mwenyewe katika mafundishi yake kwani aliligusia mara
kadhaa! Katika Mathayo 10:10 na Luka 10:7 ambazo zinasema Mathayo 10:9-10 “Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini
mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu
mbili, wala viatu, wala fimbo; MAANA MTENDA KAZI ASTAHILI POSHO LAKE.” Luka
10:7 “Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na
kunywa vya kwao; maana, MTENDA KAZI AMESTAHILI KUPEWA UJIRA WAKE. Msihame-hame
kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii” Unaona maandiko hayo yote
yanasisitiza kuwa Mtenda kazi anastahili ujira wake, Hakuna askari anayekwenda
vitani kwa gharama yake mwenyewe hivyo watumishi wote wa Mungu ni lazima
walipwe, ni lazima wafikiriwe namna ya kuishi, wamisionary, wachungaji, walimu,
wainjilisti, manabii na mitume ni lazima waheshimike katika kanisa na kuepwa
riziki yao, Kanisa ambalo haliwajali watumishi wa Mungu au haliwalipi watumishi
japo hata posho ya utumishi wao ni kanisa linalolidharau neno la Mungu.
Kwa hiyo kwa Msingi
huu ni halali kimaandiko kwa watumishi wa Mungu kutunzwa, Kanisa linapaswa
kuandaa utaratibu maalumu wa kuwalipa na kuwalisha watumishi wa Mungu ili
wasiwaze mambo mengine walitumikie kundi la Mungu kwa ufasaha, kumekuwapo na
maneno ya kejeli mengi kuhusu watu wa Mungu, mara ooo wanakula sadaka zetu mara
ooo wanatajirika kwa fedha zetu na kadhalika jambo la namna hii sio jema kwa
watu wa Mungu, Hatuna budi kuhakikisha kuwa watumishi wa Mungu wanatunzwa
sawasawa na kipato na mzunguko wa ugumu wa maisha ili waweze kukabiliana na
changamoto za kimaisha zinazowazunguka lakini wakati huohuo wakitoa huduma bila
manung’uniko. Kama liko kanisa linawatumiwa watumishi wake bila utaratibu wa
kuwapatia posho basi kanisa hilo limelaaniwa, Laana hii inakuja kwa sababu
gani? Mungu ameitoa sadaka iliwe itumiwe na watumishi wake Hesabu 18:24 “Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa
sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo
nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote.” Mungu
aliwapa zaka walawi kwa vile walikuwa wakitumika nyumbani mwa Mungu ili wapate
chakula, au ili kiwemo chakula katika nyumba ya Mungu, kuwadharau watumishi wa
Mungu na kutokutoa zaka, dhabihu na matoleo ili wao walipwe stahiki zao ni
kudhoofisha kazi ya Mungu na hapa ndipo laana inapojitokeza na baraka kufungwa Malaki 3:7-12 “Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande,
mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia
ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? Je!
Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema,
Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.Ninyi mmelaaniwa kwa
laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani,
ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana
wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni
baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea
yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu
hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana
wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza
sana, asema Bwana wa majeshi.” Unaona
laana hii inatamkwa katika mazingira ambayo wana wa Israel walikuwa hawajali
tena kuwepo kwa chakula katika nyumba ya Mungu yaani haki na posho ya walawi na
hivyo walipigwa na ukwasi, mtu yeyote anayetakamkuwadhalilisha watumishi wa
Mungu kwa kuwanyima Posho yao kwa makusudi hata kama zitatumika kwa nia njema
amelaaniwa!. Kwa msingi huo kwa watumishi wa Mungu wote wakiwemo wale wenye
huduma za kitume, kinabii, kiinjilist, kichungaji na hata walimu wa neno la
Mungu wanastahili heshima hii, yaani kutunzwa kupitia kile wanachokifanya
katika madhabau Mpaka hapo neno la Mungu liko sawa.
Kuwanyima posho
watumishi wa Mungu kunafananishwa na kuwafunga kinywa ng’ombe wanyama kazi
ambao ni wao wanaotaabiika kulima lakini mkulima anawafunga midomo yao eti
wasipure nafaka, ni tendo la ukatili wa
hali ya juu kuzuia posho, ujira wa watumishi wa Mungu usiwafikie ni kuwavunjia
Heshima na ni kumvunjia Mungu heshima ni kumdharau Mungu, Mungu anawaona watumishi wake kama chanzo cha
Baraka kwa watu wake, Mungu huwabariki watu wake kupitia matamko ya watumishi
wake kwa hiyo kitendo cha kuwanyima mapato watumishi wa Mungu kiko sawa kabisa
na kukosa ubinadamu kunakoweza kufanywa na mtu ambaye anawatumia ng’ombe
nkulima ardhi kubebea mazao na mavuno lakini anamchapa fimbo nyingi sana
ng’ombe huyo akila mazao bila kukumbuka kuwa ni ng’ombe huyo huyo ndiye
aliyesababisha wao wawe salama, kwa hiyo ukiacha ya kuwa Mungu anataka tuwe na
utu kwa wanyama ni zaidi sana anataka tuwe na utu uliotukuka kwa watumishi
wanaohudumu Madhabahuni, ikiwa Mungu aliwafundisha Israel kuacha ukatili dhidi
ya watu wanyama wake na watumwa ni zaidi sana mtu wa haki hataacha watumishi wa
Mungu wateseke bali atawalisha kwanza!
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni