Marko 12:41-44 “Naye akaketi
kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika
sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini,
akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika
sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu
katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”
Utangulizi:
Mara nyingi sana
tumewahi kusikia neno kutoa ni moyo, katika semi zetu mbalimbali za Kiswahili,
lakini je hivi tumewahi kujiuliza kwa undani maana ya msemo huo na sababu zake?
Bila shaka msemo huu una uhusiano mkubwa sana na Mafundisho ya Bwana wetu Yesu
Kristo kuhusu Kutoa, hususani kulikotokana na mama mjane kabisa aliyefika
Hekaluni na kutoa sadaka katika hazina ya nyumba ya Mungu. Yesu alimsifika kuwa
ndiye mtu aliyetoa zaidi kuliko wote katika ibada ile aliyoikusudia!
Kila mmoja wetu
anapokuwa amejiandaa kwenda kuabudu na kumtolea Mungu anapaswa kuliweka somo
hili moyoni mwake! Kwa sababu Mungu haangalii tu nini tunatoa lakini anaangalia
ni kwa sababu gani tunaoa, Mungu hutazama moyo! Hebu tuone tena andiko la
Msingi ili tuweze kujifunza kitu kutoka kwa mama huyu! Marko 12:41-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama
jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.
Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.
Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia
zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali
iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo,
ndiyo riziki yake yote pia.” Tutajifunza somo hili Huyu Mjane masikini ametia zaidi kuliko
wote kwa kuzingatia mambo ya msingi yafuatayo:-
·
Maana ya neno masikini:-
·
Huyu Mjane masikini ametia zaidi kuliko wote!
·
Utoaji wa sadaka kama mjane:-
Maana ya neno Masikini:-
Neno masikini
lililotumika katika andiko hilo kwa lugha ya kiyunani linasomeka kama “PTOCHOS” ambalo linaweza kujumuisha
maneno ya tafasiri ya kiingereza kama
“Crouching, and Cringing” sawa
kabisa na watu wanaoombaomba na kuchakura majalalani, wakenya wana neno zuri
linalokaribiana na hilo la “CHOKORAA” yaani
masikini wa kutupwa au ombaomba, ni mtu asiye na kitu kabisa mtu anayeishi
maisha ya kuomba omba, kwa maana nyingine wakati sisi wengine tunajidhania kuwa
masikini kwa kujilinfanisha na wengine na kuona labda wametuzidi kitu Fulani na
ndipo tunapoweza kujifikiri kuwa sisi ni masikini, huyu anayetajwa hapa alikuwa
masikini kabisa asiye na lolote! Wala hata mtu wa kujilinganisha naye! Mwanamke
huyu hakuwa na kitu lakini sio tu hakuwa na kitu pia tunaambiwa alikuwa mjane,
amefiwa na mume wake! Ni Mtu wa namna hii asiye na kitu kabisa ndio Yesu
anasema ametoa zaidi kuliko wote jambo hili lina maana gani na linatufundisha
nini:-
Huyu
Mjane masikini ametia zaidi kuliko wote!
Yesu anajua
mioyo yetu na anayajua maisha yetu, lakini pia wakati wa matoleo katika
ulimwengu war oho Yesu huketi kuelekea sanduku la hazina, maana yake
anafuatilia mwenedno wa utoaji wetu kwake, anajua namna na jinsi na hisia zetu
wakati wa kutoa unaweza kuona wazi tabia
yake hapa Marko 12:41 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama
jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.”
Unaona imani yangu inaniambia kuwa tukio la Yesu kufuatilia utoaji wetu sio
tu kuwa lilikuwa katika siku hii HAPANA
kila inapofanyika ibada ni wazi kuwa Yesu yupo pamoja nasi katika ulimwengu wa
kiroho na anafuatilia kila jambo linalotendeka na namna tunavyofanya katika
ibada na uchunguiz wa mioyo yetu Neno la Mungu linasema hivi Mathayo 18:20 “Kwa
kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo
katikati yao.” Unaona kumbe tunapokusanyika wakati wowote tuwe
wawili ama zaidi kwaajili ya kumuabudu yeye mwenyewe anakuwepo katikati yetu na
saa ya kutoa maana yake ni kuwa anakuwepo pamoja nasi na kufuatilia kila kitu,
bila shaka sasa utakuwa umekubaliana nami. Kwa msingi huo Yesu aliwashuhudia
wengi wakitoa na alifanya ufuatiliaji na anafanyi hizi hata sasa, na katika
ufuatiliaji huu Yesu alibaini kwamba mwanamke Yule mjane na tena masikini wa
kutupwa ALITOA KATIKA KILA KITU
ALICHOKUWA NACHO ona Marko 12:44 “maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali
huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote
pia.” Kumbuka kuwa neno la Mungu halimaanishi kuwa tutoe kila kitu
tulichonacho, wala halimaanishi kuwa tusijiwekee akiba hapana Lakini utoaji wa
mjane huyu masikini ulimshangaza zaidi Yesu kwa sababu ilikuwa ndio chakula
chake yaani hana nyingine zaidi ya ile, lakini kwanini alitoa Mwanamke huyu
alitoa kwa sababu aliamini kwamba Mungu atamtunza tu, hata kama ametioa kila
alichikuwa nacho mungu atafanya njia kwa namna nyingine, aliamini kuwa kumpa
Mungu hakutamfanya apungukiwe na kitu Wafilipi 4:19 “Na
Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika
utukufu, ndani ya Kristo Yesu.” Hii ndio kanuni ya Mungu, tunapotoa
huwa hatupungukiwi, Mungu hujaziliza kwa namna nyingine mimi na mke wangu huwa
tunatabia ya kupunguza nguo zetu na kuzigawa kwa watu wengine, wakati mwingine
huwa tunagawa nguo zote ambazo hazitutoshi au hata ambazo huwa hatuzivai mara
nyingi tu, huwa tunahakikisha tunapunguza ili zibaki chache tu tunazotumia kwa
maisha ya kila sku hapa na pale lakini baada ya miezi kadhaa unashangaa tena Nguo
zimekuwa nyingi tena, Mungu wetu ni mchungaji mwema na hukakikisha kuwa kondoo
zake hawapungukiwi na kitu Zaburi 23:1 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.”
Awaye yote anayefanya kitu kwaajili ya Mungu na kwa imani katika Mungu
hawezi kupungukiwa na kitu, mjane Yule alitoa kwa imani hii aliamini kuwa Mungu
hatamuacha ateseke na njaa hata kidogo
ona Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni
mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.”
Mjane huyu aliamini hivyo na liishi hayo katika maisha yake hakuwaza
kujilimbikizia alimuamini Mungu kwa asilimia mia moja na alipoukunjua moyo wake
katika hili Yesu alimuona na kumtumia kama somo kuu katika maisha ya wanafunzi
wake, je ni kitu hani tunaweza kujifunza kutoka katika utoaji wa mjane huyu:-
Utoaji wa sadaka kama mjane:-
Kwa kuwa Bwana
Yesu alimfanya mwanamke huyu kuwa kielelezo, ni wazi kuwa kuna maswala ya
Muhimy ya kujifuza kutokana na utoaji wa mjane huyu masikini, liko jambo la
kujifunza kutoka kwake
a.
Alijitoa yeye mwenyewe kwanza!
Utoaji wa mwanamke huyu mjane haukuwa rahisi, na hauwezi kuwa rahisi
kama mtoaji huyu angekuwa na ubinafsi, ni wazi kuwa mtoaji huyu alitoa akiwa
hana hata chembe ya ubinafsi nah ii maana yake yeye mwenyewe alikuwa tayari
amejitoa amejidhabihu kwa Mungu Warumi
12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake
Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu,
ndiyo ibada yenu yenye maana.” Ni ukweli ulio wazi katika maandiko kuwa kabla hatujamtolea Mungu au hata
kumpa mwanadamu sisi ndio sadaka ya kwanza, mwanamke huyu alikuwa ameuua umimi
kabisa ukilinganisha na upendo wake kwa Mungu, yeye alikuwa anampenda Mungu kwa
dhati, moyo wake na mauisha yake alikuwa ameyatoa kwa Bwana, mtu hawezi kufanya
ibada ghali namna hii kama hajajichukia yeye mwenyewe kwanza Luka 9:23-24 “Akawaambia
wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake
kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na
mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.”
Unaona huyu mwanamke alitoa kwa kujikana, ni muhimu kufahamu kuwa ibada ni
kafara na hakuna kafara isiyogharimu, hatupaswi kumpa Mungu vitu visivyogharimu
nafsi zetu, ibada yenye maana zaidi inahusisha kujitoa kwaajili ya Mungu na
wengine! Nyakati za kanisa la kwanza katika makanisa yaliyokuwepo Macedonia
yaani Ugiriki Bila shaka Kanisa la wafilipi walielewa aina hii ya utoaji katika
mapenzi ya Mungu na hivyo japo walikuwa hawana kitu, walitoa tena sio kwa
kulazimishwa kwa hiyari, kwa furaha, kwa uwezo na hata zaidi ya uwezo lakini
wakitanguliwa na kujitoa kwanza nafsi zao 2Wakoritho
8:1-5 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema
ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa
dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea
utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya
uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na
kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.
Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao
kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.” Unaona huu ndio
utoaji ambao Yesu aliukusudia wanafunzi wake waelewe, kanisa la leo linapoteza
Baraka kwa sababu kwanza wao wenyewe hawajajitoa kwa Mungu na kwa sababu hiyo
wanaona taabu kutoa kwa Mungu, wakiwa hawana imani na wamejaa woga kuwa kesho
itakuwaje na matokeo yake tuna wakristo wachoyo hata kuliko waislamu na
wapagani!, unapooona makanisani kila siku watumishi wa Mungu wanafundisha juu
ya kutoa ujue watu hawajitambui na wala somo kuhusu utoaji halijaeleweka kwao!
b.
Mjane alitaka kuyatenda mapenzi ya Mungu
Mjane Yule hakuenda ibadani kutoa kama maonyesho, alikuwa ameelewa
neno la Mungu linataka nini na alikuwa kazini akiyatekeleza mapenzi ya Mungu,
akitoa hakuketi chi ni na kufikiri kuhusu ujane wake , wala hakufikiri kuwa
Mungu amemtenza mabaya kwa kumuacha katika umasikini wa kutupwa na akiwa hana
mtu wa kumsaidia, huenda alikuwa akimshukuru Mungu hata kwa kile alichokipata,
na hakusema moyoni ngoja nipate zaidi nitatoa hapana alitaka kuabudu kweli
kweli sio kwa mdomo kwa vitendo Mathayo
7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana,
atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni.” Mwanamke huyu mjane na masikini alikuwa
kazini, hakuwa kwenye maonyesho, hapiti kutoa sadaka aonekane kuwa kaja ibada,
haoiti mkunyesha nguo nzuri wala hapito kuionyesha amekuja ibada hapana yuko
kazini kwelikweli ilikuwa saa ya kutoa na alikuwa anakwenda kutoa akijua kwa
nini anatoa na tena sio kwa kulazimishwa bali kwa hiyari na uelewa ulio wazi na
kwa nia na alikusudia hivyo tangu anatoka nyumbani 2Wakoritho 9:7-8 “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si
kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa
ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na
riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;”
unaiona mwanamke huyu alitoa kwa ukunjufu wa moyo, na Mungu humpenda yeye
atoaye kwa moyo na kama sadaka inakukwaza na kukufanya ujisikie huzuni sadaka
hiyo haifai, tunapotioa Mungu huangalia nia yetu 2Wakoritho 8:12 “Maana, kama nia ipo,
hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.”
Haya ndiyo yaliyiompa maksi mjane Yule.
c.
Alitoa licha ya umasikini wake!
Pamoja na umasikini mku bwa aliokuwa nao mwanamke Yule mjane, hii
haikumfanya aka chini na kujifikiri kuwa kuwa yeye bado sana ! unajua wako watu
makanisani ukifika wakati wa sadaka na changizo nyingine za kikanisa wao huwa
wanakuwa wapole na wanakaa kimya hawanyooshi mkono kujitoa wanajifikiri wao ni
masikini, wanadhani kuwa wako watu maalumu watakaomtolea Mungu lakini wao bado
sana nisikilize katika moyo wa Mungu wewe bado sana na tena utaendelea kuwa
masikini kwa sababu unajua kutokutoa kwako kwa sababu ya hali yako kunageuka
kuwa dua mbaya kwamba ni kama unamwambia Mungu
mimi sitoi kwa sababu hujanipa, unapochangamka na kutoa kama mjane huyu
maana yeke ni kuwa unamshawishi Mungu kuona na kukuamini kuwa huyu nikimpa
vingi kwa kuwa amekuwa mwaminifu katika madogo atakuwa mwaminifu katika makubwa
pia Luka 16:10-12 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu
katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu
katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya
udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu
katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? ” unaona
mwanamke huyu mjane na masikini kweli kweli alikuwa mwaminifu katika umasikini
wake na kwa sababu hiyo alitoa katika hali hiyo hiyo ya umasikini wake wakati
wengine walitoa vilivyowazidi, walitoa wasivyovihitaji, hawakuwa wamejikana
katika kutioa kwao, Mwanamke huyu mjane alitoa kwa sababu alimpenda Bwana,
alikuwa hana ubinafsi, wala hakutaka kujilimbikizia, hakuwa na muda wa kupiga
hesabu, alikuwa akifuarahia ikiwezekana labda hata zawadi ya uhai aliyopewa na
Mungu, kutokuugua, kupata nafasi ya kuabudu akiutzama wema wa Mungu kuliko
yaliyomkuta huu ndio utoaji usio na ubinafsi
Hitimisho!
Mtu awaye yote
anayetaka kupokea kutoka kwa Mungu anapaswa kuelewa kwanini tunatoa, na lazima
ieleweke wazi kuwa Mungu huwabariki wale wanaotoa kwa Moyo, utoaji wa kikristo
ni hiyari na sio lazima, ni furaha na sio huzuni, ni moyo na sio utajiri,
Nyakati za Kanisa la kwanza watu walitoa hata mali zao na kuwagaia wengine na
kuifadhili kazi ya Mungu iweze kwenda mbele Barnaba alikuwa mmoja wao ona
Matendo ya Mitume 4:36-37. “Na Yusufu,
aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake
ni mtu wa Kipro,alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa
mitume.” Wakristo wanapaswa kujifunza kutoa na wazazi wanapaswa
kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kutoa tangu wakiwa wadogo, tusisubiri mpaka
tumekomaa au kuzeeka tukiwa na tabia ngumu ya choyo Mungu anataka tuwe na tabia
hii tangu mwanzo, iwe ni tabia ya maisha yetu na sidhani kama ni sahihi
kusubiri wakati tumechoka au umestaafu
Muhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana
wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema,
Mimi sina furaha katika hiyo.” Kuwafundisha
watu wakishakuwa watu wazima ni kuchelewa sana kuwafanya watu hawa kuja kuelewa
mapenzi ya Mungu na yanakuwa mmzigo
kwao Maombolezo 3:27 “Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake.”
Ni wachache sana wanaweza kuelewa na kujaribu kulitendea kazi somo kama
hili lenye kuhusisha kujitoa nasfi lakini wakati wote tukumbuke kutoa kwa moyo
pasipo manung’uniko na kuhakikisha kuwa tunatoa kwa sababu nia yetu ni njema na
kwa furaha katika kuhakikisha kuwa injili inakwenda mbele na wale wanaoishi kwa
injili wanapata mkate wao wa kila siku, kwa kuyajua haya utakuwa umeyatimiza
hivyo mapenzi ya Mungu, Muongezewe neema
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni