Jumapili, 30 Agosti 2026

Huduma ya watoto


Waamuzi 2:8-13 “Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.”




Utangulizi:

Mojawapo ya jukumu kubwa la Kanisa pamoja na mambo mengine ni pamoja na kuwahudumia watoto, Mungu amewapa watoto kipuambele kikubwa sana na kwa sababu hiyo kuwapuuzia watoto ni kumpuuzia Mungu, Kanisa lina wajibu wa kuwajenga na kuwahudumia watoto kwa uaminifu vilevile kama linavyowahudumia watu wazima iko dhana potofu kwa wahudumu wengi wa injili inayofikiri kuwapuuzia watoto na kutokutaka kuwaleta karibu na Yesu kufanya hivi ni kufanya makosa makubwa sana ambayo Yesu mwenyewe aliyakemea.

Mathayo 19:13-15 “Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.” 

Kama tunamtumikia Mungu kwa haki na kweli na kama tunatanguliza maslahi ya ufalme wa mbinguni basi hatutaweza kamwe kuwaacha nyuma watoto katika mambo ya Mungu ni lazima twende pamoja na wao na kuwakuza katika neema hii kwani malezi ya wototo wadogo katika njia ya Mungu ni maagizo ya kibiblia Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”

Kumbukumbu 6:4-9 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.”

Kwa msingi huo wakati huu sisi kama watendakazi na wahudumu katika shamba la Mungu tutachua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na swala zima la huduma ya watoto kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

  • Umuhimu wa huduma ya watoto
  • Umuhimu wa walimu wa watoto
  • Jinsi ya kufanikisha huduma ya watoto

 

Umuhimu wa huduma ya watoto

Tumeona katika utangulizi wa somo hili jinsi Mungu alivyowapa watoto kipaumbele watoto, Mungu anataka watoto wajulishwe njia zake, aliwaamuru Israel kufanya hivyo na kwakweli wao wamekuwa hodari katika kuhakikisha kuwa watoto wao wanafuata njia zao na imani yao, sisi nasi kama Kanisa hatuna budi kulishika hili vile vile na kuhakikisha kuwa hatuwaachi watoto wetu bila ujuzi wa neno la Mungu ili wakue katika njia hii na imani hii

Zaburi 78:5-7 “Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake.”

Mungu anaeleza baadae siri ni kwanini alimchagua Abrahamu, Mungu anasema alimjua Abrahamu kwamba atawafundisha watoto wake waishike njia yake baada yake na kuwaamuru kutenda haki, Kumbe basi Mungu anapogundua kuwa tumemaanisha katika kuwahudumia watoto na washirika kwa ujumla atatufurahia na kuruhusu maelfu ya watu wake waje kwetu akijua ya kuwa watoto watafundishwa njia za Mungu katika Kanisa letu, Kanisa linalowajali watoto Mungu hulibariki sana!

Mwanzo 18:18-19 “BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”

Huduma ya watoto ni kazi maalumu ya kuujenga ufalme wa Mungu, hii sio huduma ya malezi ya kuwatunza watoto wakati wazazi wanasali au wako katika ibada, hii ni huduma maalumu ya kumjenga mtoto kiroho, kimaadili na kitabia, kwa kuushika moyo wake mapema na kumfundisha njia za Mungu katika hatua za awali kwa lugha, mbinu na njia zitakazowafanya watoto kuelewa kwa haraka Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”

Endapo kanisa litaacha wajibu huu muhimu na kuwaacha watenda kazi wake, wanafunzi, wahudumu na wenye hekima wakiwa hawana ujuzi kuhusu maswala ya watotoni Dhahiri kuwa tunaandaa kizazi ambacho hakitakuwa kinamjua Mungu kama kile kilichoinuka nyakati za wazee wetu katika Israel baada ya kufa kwake Yoshua na wakati wa kizazi cha nyakati za waamuzi ambao walicheza sana na mambo ya hvyo na kuwapa adui zao nafasi ya kuwaonea na kuwakandamiza

Waamuzi 2:8-12 “Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.”

Mungu atupe neema na hekima kizazi cha leo, tusipuuzie swala hili nyeti linalohusiana na huduma hii ya watoto ili kwa upendo na kwa masalahi ya ufalme wa Mungu tusimtengenezee Bwana kizazi au Kanisa la baadae lisilomjua Mungu wala njia zake kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamkosea Bwana hivyo huduma hii ya kuwafudnisha watoto njia za Bwana ni mapenzi yake, kumbuka neno la Msingi Kikainuka kizazi kingine hapo maana yake ni kizazi kilichokosa mafundisho, kizazi kisichorithishwa imani, kizazi kilichokosa uangalizi wa kiroho, kizazi ambacho hakuna mtu anakijali, kizazi ambacho hata stori kuhusu Mungu na matendo yake makuu hawakuwahi kuyasikia. 


Umuhimu wa walimu wa watoto

Wahudumu wanaohusika na kuwafundisha watoto wanapaswa kuwa na uelewa wa kina kuwa wao ni wa muhimu sana kuliko mtu yeyote yule kwa sababu wao ndio wanaouweka msingi wa mwanzo kabisa wa imani kwa watoto, wanaipanda mbegu ya imani na uadilifu na kuwajengea watoto tabia njema na kuwafunda ili wakue na kuwa kama Yesu katika upendo, imani mwenendo na usafi, wanalazimika kujikoki na kufanya maandalizi ya kutosha na ya kina ili kuboresha mwenendo mzima wa malezi elekezi  kwa watoto hawa, kwa kufanya hivi wao wanaandaa kile kizazi kijacho cha watu waliofunzwa na wenye nidhamu ya hali ya juu watakaokuwa nuru na chumvi kwa ulimwengu ujao.

-          Wao ni wajenzi wa msingi na ukuaji bora wa watoto kiroho, wanawasaidia watoto kukua wakiwa imara kiimani na kuhakikisha kuwa msingi huo unadumu siku zote za maisha yao, hapo tunawatengenezea uwezo wa kusikia na kulitendea kazi neno la Mungu jambo litakalowafanya wakue wakiwa imara  na wenye ujuzi kuhusu Mungu.

 

Luka 6:47-49 “Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.”

 

-          Wao ni warithishaji wa mila na tamaduni za kiimani (Pedagogies) walimu wa watoto katika Kanisa wanafanya kazi ya kuwaandaa wana wa kifalme kusimama imara na kuwa hodari katika  maneno na matendo ya kazi zao za kifalme, Nyakati za Biblia watoto wa kifalme walikuwa na waalimu wao ambao kazi zao zilikuwa ni ni kuwafundisha watoto wa kifalme kwa kuwarithisha mila miiko na desturi za kifalme ili watakapokuja kuwa wafalme wasikiuke mila na desturi hizo, wakiwa na uwezo wa kusema na kutenda, au kufundisha na kufanya.

 

Matendo 1:1 “Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,”

 

Matendo 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.”

 

-          Wao ni wawezeshaji wa kusikia na kutenda  Msingi mkubwa sana wa walimu wa neno la Mungu unakazia katika kusikia na kutenda, kimsingi kama mtu hajatenda kibiblia humaanisha hajasikia, Mwalimu mzuri na mwema ni yule aneyewawezesha watoto kusikia kisha wakatenda huu ndio mkazo wa waalimu wa kibiblia na ndicho wanacho paswa kukifanya walimu wa watoto.

 

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

 

Yakobo 1:22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”

 

Mathayo 21:28-32 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.”

 

-          Wao ni chachu ya makuzi ya kiroho Msingi wa ukuaji wa kiroho, kumpenda Mungu na kumtumikia ni mchakato wa muda mrefu sana unaojumuisha toba, maendeleo ya kukua kiroho, kiimani na kimafundisho, ili mtoto akue akimpendeza Mungu na wanadamu anapaswa kuwa na walimu bora wanaojua wanampeleka wapi mtoto, wao wenyewe wakiwa ndio kielelezo cha ibada, heshima na utumishi, Kanisa hatuna budi kuwekeza katika mioyo ya watoto kwa mafundisho sahihi, tuwalishe kondoo wa Mungu bila kujali umri wao au kuwapuuzia.

 

Yohana 21:15 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”

 

-           Wao huwajengea tabia njema mapema – walimu wa watoto ndio wanaopanda msingi wa tabia njema mapema, na hata mtu anapokuja kuwa mtu mzima kimsingi mambo mengi sana yanakuwa yamejengeka tangu utoto, Bibi yake Timotheo na mama yake licha ya kuwa wazazi lakini pia walikuwa walimu wa awali wa Imani safi isiyo na unafiki wakiipandikiza hivyo kwa Timotheo na kumfanya Timitheo kuja kuwa mtu mwenye sifa njema sana miongoni mwa wanafunzi wa nyakati za kanisa la kwanza, vigezi vulivyomfanya Paulo aambatane naye.

 

2Timotheo 3:13-15. “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”

 

2Timotheo 1:5-7 “Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

 

Matendo 16:1-3 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani.”

                                                       

Jinsi ya kufanikisha huduma ya watoto

Watoto ni urithi wa Mungu, kwa maana ya kwamba Mungu anataka kuwekeza kwa watoto kwa faida ya ufalme wake na kazi yake ya baadae wakati ambapo adui naye anakusudia kuwamaliza mapema ili waweze kutimiza mapenzi yake hapa duniani, kwa msingi huo kama kanisa hatuna budi kuhakikisha kuwa tunawekeza nguvu zetu mapema ili kujikinga na yale yaliyotokea wakati wa  waamuzi baada ya kifo cha Yoshua ambako kuliinuka kizazi ambacho hakikumjua Mungu wala matendo yake, Ni huduma ya watoto ndiyo itakayolinda kizazi kijacho, na bila ya hivyo tutakatikia sehemu fulani na kuishia hapo, kwa hiyo ni muhimu kwa kila kanisa na watendakazi  na wahudumu wa injili kuhakikisha tunaifanikisha huduma hii  ya watoto kwa gharama yoyote ile Lazima kila kanisa:

Kuweko na maono kwa maswala ya watoto Mithali 29:17-18 “Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako. Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”

Walimu walioandaliwa vema – Huduma ya walimu wa watoto ni wito maalumu kabisa sio kila mtu anaweza kuwahudumia watoto, kwa hiyo lazima kuweko mkakati wa kuwapata na kuwaleta kwa Yesu walimu, waliookoka, wanaowapenda watoto, wenye mzigo na wenye huduma hii, hata kama wamesomea ualimu wa awali pia lakini wawe wamejazwa Roho Mtakatifu, wanaopenda watoto, wenye uvumilivu na subira wanaojua kuchukuliana nao wenye kuomba na wawe mfano wa kuigwa

Waefeso 4:11-12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Kuandaliwa kwa mfumo wa mafundisho yanayofaa - Watoto wana namna yao ya kufundishwa, zinaweza kutumika hadithi za kibiblia, michoro, michezo yenye ujumbe, mistari ya kukariri, uimbaji, nyimbo, na lugha inayoendana na umri wao, ikiwa kwa watu wazima kuna maziwa na chakula kigumu basi ni zaidi sana lazima kuwe na namna njema ya kuwekeza mafundisho kwa watoto wadogo kulingana na umri wao pia

Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”

Mazingira salama, uadilifu na ushirikiano na wazazi - Watoto wanahitaji ulinzi na usalama wa kimwili, kiroho na kihisia, kwa msingi huo ni lazima kanisa lijiwekee kanuni za ulinzi wa Mtoto, tuwatengenee mazigira rafiki yasiyo na unyanyasaji na ushirikiano mkubwa na wazazi hatuwezi kuwapata watoto kwa sababu wako chini ya mamlaka ya wazazi wao kwa hiyo ni lazima wazazi watoe ushirikiano mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwaleta ibadani au kuwaleta katika makusanyiko na makambi ya makongamano ya watoto, Yusufu na Mariamu hawakuacha kumpeleka Yesu Hekaluni tangu wakati wa utoto wake, mpaka ikatokea kuwa mtoto huyu akawa anapenda kujifunza neno.

Luka 2:21-24 “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana,(kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili

Luka 2:40-46 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.”

Mwisho kabisa maombi ni jambo la msingi sana kwa huduma hii, kama tunavyojua kila kitu cha kiroho kinahitaji maombi basi ni muhimu kwetu kuhakikisha kuwa kama kutakuwa na huduma hii basi walimu wake waombewe, na watoto waombewe na wazazi waombewe na kwa ujumla watoto waombewe na wafunguliwe vilevile kama tunavyowasikiliza watu wazima na kuwaombea

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: