1Timotheo 5:21 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo.”
Utangulizi:
Mojawapo ya agizo Muhimu sana
alilopewa Timotheo, Kama mwangalizi wa makanisa yaliyokuwako Efeso katika
waraka alioandikiwa na Paulo Mtume Pamoja na maagizo mengine ni pamoja na
kuhakikisha kuwa asifanye neno lolote kwa upendeleo, Upendeleo katika nyakati
za leo limekuwa mojawapo ya tatizo kubwa sana katika jamii, jambo linalopelekea
kutokutendeka kwa haki, kumekuwepo na tatizo la upendeleo kila mahali leo,
Katika mazingira ya kibiashara, mazingira ya kisiasa, katika michezo, na hata
makanisani, katika familia, ndugu, serikalini na hata kwenye ndoa, Bila ya aibu
yoyote leo hii watu wanaweza kufanya upendeleo na kusahau kabisa kuwa kufanya
upendeleo ni dhambi nani kinyume na sheria ya kifalme.
Yakobo 2:8-9 “Lakini mkiitimiza ile sheria
ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda
vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa
wakosaji.”
Sisi kama wakristo tunapaswa
kumfuata Kristo kama mfano wetu, Yesu Kristo hakuwahi kupendelea watu, sisi
tunaomfuata yeye kamwe hatupaswi kuonyesha upendeleo maandiko yanatukataza
kufanya hivyo, kuonyesha upendeleo ni moja ya tatizo kubwa sana katika jamii
nani kinyume na haki ya Mungu, kama mtu anasema ni mkristo na anamwamini Mungu
na hata kama sio mwamini awaye yote ambaye ana moyo wa kutenda haki hawezi
kuruhusu upendeleo.
Yakobo
2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.”
Kwa bahati mbaya mambo hayako
kama maandiko yanavyoagiza, leo hii ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na connection na watu au mtu Fulani, uwe
kwenye kundi au chama Fulani, watu wanapendelea watu au kundi Fulani la watu
kwa sababu ni ndugu, au ni wa jinsia yake, au ni masikini, au amepokea rushwa
au ni wa ukoo wake, au shemeji zake, au ana hadhi Fulani au ana hela, au
wanafahamiana kwa muda mrefu na kadhalika hivyo kuna namna watu wanapewa
heshima au upendeleo kwa sababu Fulani, Fulani kama uko na upendeleo leo hii ni
lazima utubu na kuelewa kuwa upendeleo ni dhambi mbaya kama zilivyo dhambi
nyingine!
Maana ya upendeleo.
Neno upendeleo katika biblia ya
kiyunani husomeka kama PROSOPOLEPSIA
ambalo kiingereza linasomeka kama FAVORITISM ambalo maana yake ni “respect of persons” au
“to give judgement with the respect of outwards circumstances of a man” pia
inaweza kutafasirika kama giving unfair treatment of a person or group on basis
of prejudice kwa Kiswahili Upendeleo ni hali ya kutoa haki au kipaumbele kwa
mtu asiyestahili kutokana na maslahi ya mtoa haki, ni hali ya kutoa kipaumbele
kwa mtu kulingana na mazingira ya nje au ya muonekano, au kuonyesha heshima kwa
mtu au kundi la watu katika mtazamo au maoni yasiyo sahihi, au yasiyo sawa
kimsingi upendeleo ni sawa na hakimu anayetoa haki mahali pasipostahili haki,
au mwamuzi refa anapowapa watu penalty ambayo kimsingi na kiyushahidi
haikupaswa kuwa penalty ni tabia ambayo kibiblia haikubaliki na wala haitokani
na Mungu wetu tunaelezwa kuwa Mungu wetu
hana upendeleo na watu wa Mungu wanaonywa kutokuwa na Upendeleo kwa sababu
zozote zile Yakobo anajaribu kutioa mfano ulio hai kuhusu upendeleo alipokuwa
anajaribu kufafanua somo lake kuwa watu wasiwe na upnendeleo ona
Yakobo 2:2-5 “Maana akiingia katika
sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na
maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na
kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe
pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa
waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu
hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme
aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri
hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?”
Upendeleo sio tabia ya uungu wala
haipaswi kuwa tabia ya watu wa Mungu, kama watu wa Mungu wanaonyesha upendeleo
je wana tofauti gani na watu wa dunia hii, ni ukweli usiopingika kuwa dunia
inatarajia kujifunza kitu kutoka kwa watu wa Mungu na Mungu mwenyewe kama Mungu
mwenyewe hana upendeleo wewe unayefanya upendeleo huoni ya kuwa una kesi ya
kujibu, Maandiko yanatuelekeza kuwa Mungu hana upendeleo na kuwa tunapaswa
kujifunza kutoka kwake na kwa neno lake kisha tuishi sawa na haki ya Mungu!.
Mungu hana upendeleo!
Matendo ya mitume 10:34-35 “Petro akafumbua
kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali
katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”
Petro alitambua kuwa Mungu hana
upendeleo, kuna wakati ambapo wayahudi walijidhani ya kuwa huenda wao ni wa
Muhimu sana kuliko mataifa mengine dhana hii ilijengeka kwao wakasau kuwa Mungu
alitaka kuwaandaa wao kama watumishi wake ili kutoka kwao injili ienee kwa
mataifa yote , Lakini ni ukweli unaosmama wazi kuwa Mungu hana hati milikia ya
mtu Fulani wako watu hudhani ya kuwa Mungu ni wao nan i wa kwao peke yao na
hudhani ya kuwa Mungu anawawasikiliza wao tu nisikilize Mungu ni wa watu wote yeye hana upendeleo wala hapokei
uso wa mwanadamu Mungu husimama upande
wa kila mtu atendaye mema bila kujali ni wa kabila gani ona
Warumi 2:10-11 “bali utukufu na heshima na
amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; kwa maana
hakuna upendeleo kwa Mungu.”
Ndugu zangu hakuna kabila, wala
mtu wala kiongozi anayeweza kudhani au kufikiri ya kuwa yeye ni wa muhimu sana
kuliko wengine, wako watu wengine wamepata nafasi za uongozi na usimamizi wa
mambo lakini hawatendi haki ya Mungu, na badala yake wanafanya upendeleo am,bao
uko wazi wazi katika jamii au taasisi wanayoiongoza, Mungu anachukizwa wazi na jambo
hilo, huo ni uwakilishi mbaya na mbovu wa kumtangaza Kristo, kila mtu aliyemjia
Kristio na kubatizwa kwa Mungu ni sawa na hakuna upendeleo.
Wagalatia 3:27-29 “Maana ninyi nyote
mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana
mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja
katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu,
na warithi sawasawa na ahadi.”
Unaona maandiko yanaonyesha kuwa
sisi wote tumemvaa Kristo, sisi wote tumekuwa wamoja katika Kristo, haijalishi
wewe myahudi, au myunani, haijalishi wewe mnyakyusa au mbondei, haijalishi wewe
kijana au mzee, haijalishi wewe mtumwa au huru, haijalishi wewe ni wa namna
gani sisi sote tunazo ahadi sawasawa na Ibrahimu na Isaka na Yakobo, kama Mungu
alimlinda na kumtetea Abrahamu anatafanya hivyo kwa yeyote yule aliyemwamini
mwana wake Yesu Kristo laizma ufikie wakati tuache kiburi na majivuno na
kudhani kuwa mtu Fulani ana umuhimu sana kwa Mungu kuliko mwingine, Hakuna mtu
ambaye anaweza kudhani ya kuwa amefanya makubwa sana kuliko mwingine au labda
anasikilizwa sana na Mungu kuliko wengine kama mtu anajiona yuko hivyo nataka
nikuambie wazi hicho ni kiburi, Mungu hapokei uso wa mwanadamu wala hapokei
rushwa ona
Kumbukumbu la Torati 10:17 “Kwa maana
Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu,
mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa”.
Wakati mwingine tumeona watu
wakitetewa waziwazi tena waliostahili hukumu tena wakiwa hawajatubu lakini kwa
sababu wanajuana na wakubwa wanapewa upendeleo, kwa sababu wana connection wako
tu, kuna watu ambao walifanya makosa madogo tu na wamehukumiwa vikali, kuna
watu wana makosa makubwa lakini wako, kuna watu wako magerezani kwa sababu ya
kusingiziwa tu, kuna watu kwa sababu wanachukiwa wanatafutiwa makosa hata ya
kupakaziwa tu ili wahukumiwe hii ni tabia mbaya ya kibinadamu nadhani hakuna
mtu ambaye ameishi kwenye jamii yenye upendeleo ambaye anaweza kuwa na furaha,
wana michezo ambao timu zao wakati mwingine zimechezeshwa na marefarii wabaya
wameonekana kukata tama sana pale timu nyingine inapobebwa na juhudi za wale
waliotumia nguvu zao na akili zao zikipuuzwa na kutokuonekana kuwa kitu hapo
ndipo utakapoelewa kuwa upendeleo sio kitu kizuri, katika ndoa vilevile pale
ambapo wazazi wa upande mmoja wameonekana kupewa kipaumbele kuliko wazazi wa
upande mwingine zimekuwa ni chachu na changamoto zenye kukatisha tamaa sana
katika familia mbalimbali narudia tena hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha na
amani pale udhalimu wa upendeleo unapofanyika katika jamii yake, unakwenda
mahakamani mahali ambapo unatarajia utapokea haki na unakuta hukumu inapotoshwa
je unaweza kuwa na furaha na sehemu hiyo? Mwalimu anaposahihisha na kumuongezea
marks mwanafunzi ambaye hakustahili je unaweza kufurahia kuweko katika jamii
yenye upendeleo? Ashukuriwe Mungu hana upendeleo kwa Mungu kila mtu atahukumiwa
sawa na matendo yake bila upendeleo ona
Wakolosai 3:23-25 “Lo lote mfanyalo,
lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa
mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo. Maana adhulumuye
atapata mapato ya udhalimu wake, wala hakuna upendeleo.”
Unapofanya upendeleo unaweza
kudhani kama sio dhambi hivi, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa unapofanya
upendeleo unafanya dhuluma, unadhulumu wanaostahili, kwa wasiostahili, maandiko
yanaonya kuwa adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake wala hakuna upendeleo, ni Muhimu kwa kila mtu aliye katika nafasi ya
maamuzi akajifunza kutenda kwa haki na kumcha Mungu Mungu anataka watu wote
watendewe haki na kamwe kusiwe na aina yoyote ya upendeleo unaoshakiziwa na
jambo lolote lile kifedha au uso wa mwanadamu ona
2Nyakati 19:5 -7 “Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote
yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; akawaambia hao makadhi, Angalieni
myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja
nanyi katika neno la hukumu. Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni
mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za
watu, wala kupokea zawadi.”
Usifanye neno lolote
kwa Upendeleo !
Nyakati za Kanisa la kwanza
walijitahidi sana kuhakikisha kuwa wanakuwa mbali na upendeleomoja ya
changamoto kubwa za kibinadamu zilizojitiokeza mapema nyakati za kanisa la
kwanza ni pamoja na upendeleo jambo lililopeleka Mitume kuwa makini katika
uchaguzi wa viongozi na mashemasi ambao kimsingi walipaswa kuwa watu wa haki
watu wasio na upendeleo ona
Matendo 6:1-7 “Hata siku zile wanafunzi
walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa
Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya
kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi
sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba
miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili
tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile
Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu
aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na
Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya
mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu
likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya
makuhani wakaitii ile Imani.”
Haki inapotendeka katika jamii
kunakuwa na baraka kubwa sana, lakini dhuluma inapotendeka watu huwa na
manung’uniko Mungu anawataka watu wake wote kuwa mstari wa mbele katika kutenda
haki na ndio maana utaweza kuona katika mstari wa Msingi Paulo akiagiza kwa
kiapo akimwapisha Timotheo mbele za Mungu na mbele za malaika asifanye neno
lolote kwa upendeleo hili sio agizo la mchezo maana yake Mungu na malaika
mbinguni wanatutazamia tutende haki na huku ya Mungu iko pale pale kwa
wasiotenda haki
1Timotheo 5:21 “Nakuagiza mbele za Mungu,
na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo
kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo.”
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!