1Timotheo 4:11-13 “Mambo hayo uyaagize na
kuyafundisha. Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao
waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. Hata
nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa idadi ya
watu nchi Tanzania kwa sasa inakadiriwa kufikia 61,741,120 yaani milioni 61
na katika idadi hii ya watu vijana ni asilimia 77% kati ya hao asilimia 35%
wako chini ya umri wa miaka 35 kwa Msingi huo kuna wimbi kubwa sana la vijana
katika taifa letu, na wimbi hili linaweza kuwa Baraka kubwa sana na kama kanisa
na taifa tusiposhughulika nao wanaweza kuwa sababu ya changamoto kubwa sana
endapo tu watakosa misingi itakayowapa muelekeo wa namna ya kuishi kwa Amani
duniani na kujaribu kuishi kwa kujitegemea. Kwa msingi huo Leo tutachukua muda
kujifunza kwa kina namna na jinsi Vijana wanavyoweza kuyakabili maisha kupitia
ujasiriamali kwa kuzingati misingi ya kibiblia tutajifuza somo hili kwa
kuzigatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya vijana na ujasiriamali
·
Misingi ya kibiblia kuhusu ujasiriamali
·
Mambo ya msingi ya kuyazingatia
Maana ya vijana na ujasiriamali
Neno vijana na ujasiriamali
linapowekwa pamoja inaweza kuwa ngumu kuliona moja kwa moja katika mtazamo wa
kimaandiko, lakini hili halimaanishi kuwa haliko, hapo kuna muunganiko wa
maneno mawili 1 Vijana na 2 Ujasiariamali
1. Vijana
ni kundi la watu walio katika hatua ya ukuaji wa kijamii, kiuchumi na kiroho
ambao bado wako kwenye mchakato wa kujitambua, kujitegemea na kutafuta muelekeo
kwa lugha ya vijana ni watu wale ambao bado wanajitafuta, hawana utulivu mpaka
wapate kile wanachokiota au kukitamani, ni kundi la watu wenye ndoto na maono
na ni kundi ambalo kimsingi Mungu hajawahi kuwaacha anapokusudia kuwamwagia
Baraka zake ni kundi ambalo liko katika mpangowa Mungu wa Baraka hivyo vijana
hawapaswi kujifikiri kuwa wameachwa! Mungu ametumia vijana na ana makusudi makubwa
na vijana hivyo hawezi kuwapuuzia!
Yoeli 2:25-29 “Nami
nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na
tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na
kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu;
na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya
Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu
wangu hawatatahayari kamwe. Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina
roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; wtena juu ya watumishi
wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”
2. Ujasiriamali
– Ujasiriamali ni uwezo wa kuanzisha na kuendesha biashara au shughuli za
kuzalisha mali na kutumia fursa zilizopo na tulizopewa na Mungu kwa ubunifu na
kwa njia ya kipekee ili kutimiza malengo ya kiuchumi na kijamii kwa kawaida
akili hii na uwezo huu wa ujasiriamali unatoka kwa Mungu
Kumbukumbu 8:18 “Bali
utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili
alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo”
Katika mtazamo wa
Kikristo tunaelewa kuwa maisha yetu yapo mikononi mwa Mungu, na mwanadamu
amewekwa Duniani na Mungu na msingi wa kwanza wa Mwanadamu kuwekwa Duniani
ilikuwa ili afanye kazi, Mungu alimpa fursa mbalimbali mwanadamu na kumpa kila
kitu, kwa sababu hiyo umasikini sio mpango wa Mungu, wala Mungu siye anayesababisha
umasikini lakini Mungu anauwezo wa kutufunulia fursa ambazo tunaweza kuzitumia
na kujipatia riziki zetu, pamoja na wale wote wanaotutegemea na wote wenye
uhitaji wanaotuzunguka duniani.
Misingi ya kibiblia kuhusu ujasiriamali
Ni muhimu kufahamu ya kuwa neno
la Mungu limeweka wazi ya kuwa Misingi yote ya ujasiriamali imewekwa na Mungu
na imeanzishwa na Mungu, Kumbuka Mungu ndiye aliyeumba na kutupa kila kitu, kwa
hiyo uumbaji wa Mungu ni zawadi na mtaji wa hali ya juu kwa mwanadamu, kwa
sababu Mungu alitangulia kuwekeza kwanza kisha akampa Mwanadamu umiliki wa kila
kitu katika ulimwengu huu,
Mwanzo 1:26-28 “Mungu akasema, Na tumfanye
mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa
angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu
ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba,
mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni,
mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na
ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu
akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote
pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;
na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila
kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula
chenu; ikawa hivyo.”
Mungu amempa mwanadamu kila kitu
anachokihitaji, amempa akili, anga, ardhi, maji, wanyama, ndege, miche, miti,
mbegu, madini na kila kitu na amembarikia na kumtaka akavitawale, kwa hiyo
mwanadamu amepewa kila kitu na anamuwazia mema kila mwanadamu Mungu hafurahii
maumivu yetu, kama tukimtegemea yeye atatufungulia macho yetu na kutuonyesha
Fursa aliyoikusudia kwetu kwa sababu wakati wote Mungu anatuwazia mema lakini
ili tufanikiwe kuna maswala kadhaa ambayo maandiko yanatuelekeza kuyazingatia:-
1.
Ufunuo
kuhusu Fursa – Maandiko yanaonyesha kuwa wako watu wengi waliopitia shida ma
mashaka makubwa sana, walioshi katika nyika, jangwa na kupitia maisha hatarishi
sana lakini mafanikio yao yalikuja kupitia ufunuo wa kutumia Fursa
walizofunuliwa na Mungu, Fursa ni nini? Neno Fursa kwa kiingereza ni Nafasi, au
opportunity na Mungu ni Mungu anayetoa nafasi pale tunapomuomba na kumlilia,
ukiona bado huioni fursa ujue bado hujabanwa ipaswavyo, lakini unapokuwa katika
wakati mgumu sana mpaka ukawaza moyoni nitafanya nini ndipo utakapoona Mungu
akikufungulia fursa au akikufanyia nafasi, Fursa ni nafasi au uwezekano wa
mjasiriamali kuitumia nafasi inayopatikana ili kupata faida au manufaa ya
kukufanikisha
a. Mwanzo
21:14-20 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema
akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na
kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.Yale
maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda
akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema,
Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake,
akalia.Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka
mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya
kijana huko aliko.Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa
nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha
maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na
huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.”
b. Mwanzo 26:1-22 “Ikawa
njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu.
Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea,
akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini
katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe
na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia
Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa
uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.
Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri
zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa
mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana
aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya
Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku
nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka
anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu
ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu
nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea?
Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani.
Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima
atauawa. Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa
kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa
mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao
Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake,
siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki
akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi
Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka
akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu
babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu;
naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka
wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji
yanayobubujika.Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema,
Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu
waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena.
Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho
hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA
ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”
c. Matendo 16:6-12 “Wakapita
katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri
lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia,
lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo
akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na
kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.
Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda
Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari
Njema. Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na
siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa
Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa
katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.”
Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu ni Mungu mwenye
kuonyesha Fursa anatoa nafasi na kufungua mlango, wakati nafasi moja
inapopotea, au mlango mmoja unafunga na unaona giza Mungu yeye yupo na
hutuonyesha nini cha kufanya na wapi pa kuelekea, Hajiri na Ishmael walipofukuzwa,
Mungu aliwaahidi kuwafanya taifa kubwa, walikimbilia jangwani, hali ilikuwa ni
kame, maji yaliisha, chakula kikaisha, mtoto alizidiwa kiasi cha kufa lakini
Mungu alimuonyesha Hajiri kisima, kisima ambacho kiliokoa maisha yao na bila
shaka kilikuwa sababu ya makazi mapya, kijana akawa mwindaji na akaozwa na mke,
vijana wengi hawana mke, hawana Mume na wana hali mbaya ya kiuchumi kwa sababu
hawajafunuliwa fursa, Mungu akikufunulia Fusra utakuwa mtu mkubwa na
utatajirika, Leo hii taifa la Kiarabu ni matajiri wakubwa wa Mafuta Duniani
Mungu aliwaonyesha kisima katika Jangwa,
Isaka aliweza kugundua kilimo cha umwagiliaji kwa
kutumia kisima, wakati inchi ilikuwa na njaa Isaka hakuwa na njaa kwa sababu
alinywesha mifugo yake kwa maji ya kisima na alibadili jangwa kua ardhi nzuri
na kilimo, mifugo ilimpa mbolea, maji yalitunza
mifugo na alimwagilia chakula cha wanadamu na wanyama, Chakula kilipatikana na
akauza na hivyo alikuwa mtu mkubwa sana, wafilisti walipogundua walimuonea
wivu, walifukia visima vyake, lakini alichimba vingine, hatimaye Bwana alimpa
nafasi REHOBOTH. Uko ufunuo, yako maono kwaajili ya biashara
zako, mifugo, yako mashimo ya madini yako, genge lako, Huduma yako na kadhalika
jambo kubwa na la msingi ni kuhitaji Maono kutoka kwa Mungu ili kwamba Bwana aweze
kufungua nafasi na kubariki uchumi wako.
Mungu aliwafungulia mlango, Paulo mtume na Silas, na
Timotheo na Luka, na wengineo wote wwliokuwa nao katika timu yao ya umisheni,
kila walikotaka kwenda kwaajili ya injili milango ilifunga lakini hatimaye walimuona
mtu kutoka Makedonia kwenye maono aliwaomba wavuke kwenda Makedonia, kwa hiyo
Mungu aliwafungulia mlango wakufaa sana kwaajili ya injili.
Kila mmoja anahitaji neema ya Mungu ili aweze kupata
maono na namna ya kuyainua macho ili uweze kuona fursa ambayo wengine wanaweza
wasiione, Ni Mungu akupaye akili za kupata utajiri. Kila mmoja hana budi
Kumuomba Mungu akuonyeshe fursa. Kwa mfano kunaposikika kuwa kuna mahafali
mahali Fulani, utaona watu wanauza maua ya mataji, wanapiga picha, hawa
wanatumia hilo tukio kunufaika kibiashara baada ya kujipanga kimkakati na
kuhakikisha kuwa hawatapata hasara.
2.
Hekima
na maarifa – Kutengeneza fedha na mali kunahitaji pia hekima na maarifa,
hekima na maarifa ni nyenzo Muhimu inayotusaidia kuamua kwa busara biashara
gani tuifanye, wapi ifanyike na namna ya
kufanya, tunaweza kupata hekima na maarifa kwa kujifuza katika mafundisho kama
hivi, lakini vilevile tunaweza kusoma vitabu mbalimbali na vikatusaidia
kuyapata maarifa Maandiko yanaonyesha
jinsi Hekima na maarifa ilivyo vyenzo ya Muhimu katika kujijenga
kiuchumi, tunaweza kujifunza namna ya kufuga wanyama mbalimbali, na kukuza
mazao ya namna mbalimbali hata kupitia mitandao ya kijamii na kwenye You tube,
au kwa kutumia app za akili mnemba (Artificial Inteligences Apps) kwa kupata
maarifa mbalimbali
a. Mithali 24:3-5 “Nyumba
hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika,Na kwa maarifa vyumba vyake
hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza. Mtu mwenye hekima ana nguvu;
Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;”
b. Mithali 1:7 “Kumcha
Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”
c. Yakobo 1:5 “Lakini
mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa
ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”
Maandiko yanatuonyesha wazi kuwa tunaweza kuwa na
mafanikio makubwa sana na kujijenga kiuchumi, kiroho, na kwa utajiri kama tu
tutakuwa na Hekima na maarifa, kuja katika mafundisho kama haya au kusoma
kunatupa maarifa, lakini hata hivyo maarifa ya msingi zaidi na ya muhimu
yanapatikana kwa Mungu, kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na sio hivyo tu
tunaweza kupata hekima kwa kuomba, wote tunakumbuka jinsi Hekima ilivyokuwa
sababu ya mafanikio makubwa sana kwa Mfalme Suleimani, watu wote unaowaona kuwa
wamefanikiwa Mungu aliwapa hekima hii na ujuzi wa namna ya kufanikisha mambo
yao, wakati mwingine hata bila kujali Imani yao mradi tu wamekaa katika kanuni
zake na wanamtambua na kumkubali wakiishi kwa nidhamu kwa hiyo utaweza
kukubaliana nami ya kuwa hatuwezi kumuweka Mungu pembeni linapokuja swala la
ujasiriamali.
3.
Kufanya
kazi kwa bidi - Siri nyingine kubwa mara baada ya Mungu kukuonyesha fursa
yako na kukufunulia nafasi yako, na kukupa hekima na busara lazima uongeze bidii
katika kile ambacho Mungu amekupa kukifanya, Ni muhimu kufahamu kuwa neno la
Mungu linapiga vita uvivu, na linatutaka tufanye kazi kwa bidii na ukiweka bidii maandiko yanasema utasimama mbele ya wafalme.
a. Mithali 22:29 “Je!
Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme;
Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.”
b. Mithali 6:6-11 “Ewe
mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana
akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa
jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini?
Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado
kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na
uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”
4.
Ujasiriamali
unahitaji Imani, ujasiri na kuondoa aibu – kila kitu duniani kina vikwazo,
moja ya kikwazo kikubwa cha ujasiriamali ni pamoja na kuwa na aibu, kukosa
ujasiri na hata kukosa Imani ili tuweze kuwa na hayo na kufanikiwa na kuwa
mbali na Hofu mfahamu ya kuwa tunamuhitaji Roho Mtakatifu pia, kama jinsi anavyotupa
ujasiri kushuhudia habari za ufame tunamuhitaji pia katika biashara zetu, tuwe
kama hatuoni, tuwe hatuna aibu tunapoamua kutafuta, watu wanaouza maduka,
vitumbua, mikate, chapati, na kadhalika na vyakula kama mama nitilie na
kadhalika huwa wanaweka woga kando, wanaweka mbali hofu na wanamuamini Mungu
kuwa watauza
a. 2Timotheo 1:6-8 “Kwa
sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa
kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya
upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala
usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya
Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”
Imani, ujasiri na kutokuwa na haya yaani kuona aibu
sio fungu la mtu aliyeokolewa na anayejitafutia riziki, tunahitaji Imani kuwa
Mungu atatuletea wateja kwa ile fursa aliyotufunulia na kwa lile wazo la
kibiashara, au kilimo alilotupa, na lolote lile, leo hii wako wakina mama wengi
wa kikristo ambao wanamiliki shule zao za awali, za msingi na sekondari,
walipata mawazo, walianza kwa vikwazo lakini Mungu aliwasaidia na sasa
wanamiliki uchumi mkubwa na ni vyombo vikubwa vya Mungu vya kuipeleka injili.
5.
Ujasiriamali
unahitaji kutengenezewa mkakati – Mjasiriamali anapaswa wakati wote kukaa
kimkakati, huku akihakikisha kuwa anakuwa makini na anakuwa tayari kwa kila nafasi
itakayojitokeza wakati wowote kwa kusudi la kupata faida na kuhakikisha kuwa
hapati hasara, Mpango mkakati huo pia unamuhitaji Mungu, wapendwa wengi
wanadhani usemi ule mpe kaisari yaliyo ya kaisari na Mpe Mungu yaliyo ya Mungu
ni kama umetenganisha Mungu na Biashara hapana unaenda na Mungu wako kwenye
biashara huku ukimshirikisha yeye katika njia zako zote na yeye atakupa mkakati
wa mafanikio usiomuondoe Mungu katika mkakati wako wa kibiashara na hivyo
ndivyo neno la Mungu linavyotuelekeza, hakikisha kuwa unakuja kivingine, na
unakuwa tofauti na wengine.
a. Mwanzo 41:25-40 “Yusufu
akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao
atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale
masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu,
wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu
yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo
nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi
karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.Kisha
kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika
nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika
nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. Na ndoto
ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu
amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa
akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke
wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika
miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema
ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula
katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo
saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Neno
hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. Farao
akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani
yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana
mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa
neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko
wewe.”
b. Mwanzo 30:37-43 “Yakobo
akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda,
mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito. Akazisimamisha fito hizo
alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama
wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo
fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na Yakobo
akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa
na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando
wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani. Ikawa
kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya
macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile
fito, lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu
walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo. Kwa hiyo mtu huyo
akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na
punda.”
Mungu alimpa Yusufu kutafasiri ndoto na alimpa mkakati
utakaomsaidia kuhifadhi chakula na kufanya biashara ya chakula hicho wakati wa
njaa, kwa hiyo Farao aliona wazi kuwa hakuna mtu mwingine anayeweza kulisimamia
jukumu hili isipokuwa yeye na kwa fursa hii Yusufu akawa msimamizi wa swala
zima lililompa faida yeye na familia yake na ulimwengu kwa ujumla.
Yakobo hali kadhalika alipewa mpango mkakati wa namna
ya kupata mshahara wake au kondoo wake na mbuzi na mifugo kama malipo yake
kutoka kwa Labani na ilikuwa ni Mungu aliyeingilia kati kufanya hivyo, Kwa
sababu Labani alikuwa amekusudia kumdhulumu Yakobo mara kadhaa lakini Mungu
alimpa Yakobo njia ya kufanikiwa alimpa mkakati kwa njia ya ndoto
Mwanzo 31:7-12
“Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara
wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na
madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema,
Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.
Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati
wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na
tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na
marakaraka.Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi
hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama
wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani.”
kwa hiyo ujasiriamali unahitaji mpango mkakati lakini
wakati huo huo tukumbuke mkakati unatoka kwa Mungu. Kwa hiyo Yusufu na Yakobo
walikaa kimkakati. Mungu anapokufunulia mpango Fulani wa kukufanikisha anakupa
na mkakati wake, alimpa Nuhu vipimo vya kujengea Safina na alimuelekeza na aina
ya mbao atakazotumia, alimpa Musa maelekezo ya kujenga sanduku la agano na
alimpa vipimo na namna atakavyojenga, huwezi kumtenganisha Mungu na mipango
mikakati katika kila kitu ikiwepo ujasiriamali.
6.
Ujasiriamali
unahitaji kujenga Mahusiano – Ujenzi wa mawasiliano ni muhimu sio tu
kwaajili ya ushirika kanisani, lakini hata katika biashara, Mahusiano mazuri, lugha
nzuri na tabasamu lako ucheshi na namna unavyowahudumia watu vinaweza kujenga
uhusiano Mzuri, unapojenga uhusiano Mzuri unapanua mipaka yako ya kushirikiana
na wengine, kupata taarifa, kushauriwa, kujifunza na kujiongeza, wakati
Mwingine hususani watu waliookoka wanafikiri kuwa siriasi, kununa nuna ndio
kutaonyesha kuwa wako makini na kujilinda na wokovu na kama akicheka cheka ni
kama amejirahisi na anadhani atarahisisha na mambo mengine. Mungu ametuumba na
haiba na anatutaka tuwe na mahusiano mema kwa hiyo katika ujasiriamali
tunamtegemea mtu aliye okoka kuwa bora zaidi kihuduma kuliko wale wasiomjua
Mungu
a. Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
b. Waebrania 13:2 “Msisahau
kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo
kujua.”
c. Wagalatia 5:22-23 “Lakini
tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
d. Mithali 14:28 “Utukufu
wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.”
Wajasiriamali wanatakiwa kuwa na amani na watu wote, kwa
sababu watu ndio mtaji wetu mkubwa, wajasiriamali wanapaswa kuwa na furaha,
Amani, utulivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kujinidhamu na ukarimu kwa
ujumla kwa sababu hayo yanawavutia watu, ni
jambo la kusikitisha sana kuwa mtu aliyeokoka anakuwa na lugha ya hovyo,
amenuna na hatoi huduma bora na kuwachangamkia watu alafu watu wavutiwe, ukweli
ni kuwa ukipoteza watu unapoteza ukuu wako wasambaa wanasema Zumbe ni Wanthu
yaani nguvu ya mfalme ni watu wake usipoteze wateja, aidha tunda la Roho
linamsaidia mjasiriamali wa kikristo kutokuwa na urasimu usio na maana katika
kutoa huduma kwa wateja jambo ambalo litawavutia na kuimarisha uhusiano wako
nao.
Mambo ya msingi ya kuyazingatia
Tumeona jinsi ambavyo Neno la
Mungu yaani Biblia ina mawazo mengi sana yaliyonyooka ya kuwasaidia sio vijana
pekee bali watu wote kuhusu ujasiriamali, lakini tunawalenga vijana kwa sababu
ndio wengi na ndio wenye nguvu na wengi wao wako katika rika la utafutaji, kwa
hiyo kanisa lina wajibu wa kuwafunulia ujuzi wa neno la Mungu ili vijana wajitume, wamuamini Mungu, wawe na
ujasiri na kufanya biashara, na shughuli nyingine za kujipatia kipato huku
wakimtanguliza Mungu, Tumeona ya kuwa Mungu ana mpango mwema kwa ajili yao na
hivyo hawana nafasi ya kumlaumu Mungu kwa ugumu wa maisha badala yake wanapaswa
kujua ya kuwa Mungu anawapenda na anashughulika na mafanikio yao, Kwa wakristo
masomo kama haya yanaweza kuwa kitu kipya lakini haikuwa hivyo katika jamii ya
Wayahudi na nyakati za Kanisa la Kwanza
1. Kujifunza
kutoka kwa Wayahudi – Wayahudi walikuwa na njia maalumu za kuwaandaa vijana wao
kiimani na pia waliwafundisha kujitegemea kwa hiyo swala la kujituma na
kufanikiwa halikuwa geni katika jamii ya kiyahudi wao walifanya maswala kadhaa
yafuatayo:-
a. Waliwandaa kiimani
i.
Kila kijana wa kiyahudi alifundishwa neno la
Mungu na kukaziwa kujifunza neno la Mungu hususani torati, walikaziwa wazi
kabisa kuwa siri ya mafanikio yao ni kusoma torati kuishika na kumjua Mungu
a. Yoshua 1:8 “Kitabu
hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako,bali yatafakari maneno yake mchana na
usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo;
maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”
b. 1Wafalme 2:1-3 “Basi
siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi
naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa
mwanamume;uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake,
uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa
na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo,
na kila utazamako;”
c. Ezra 7:10 “Kwa
maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na
kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.”
Kwa hiyo Neno la Mungu kwao lilikuwa ni Msingi wa
mafanikio yao, mkazo mkubwa uliwekwa hivyo kuwa bila sheria ya Mungu hawawezi
kutoboa lakini kama wanataka kusitawi sana na kufanikiwa katika kila kitu
wanapaswa kumuweka Mungu kwanza na Mungu angewafanikisha katika maswala yao
yote swa na tu na Kristo alivyotufundisha kuwa ili tuzidishiwe mambo mengine
lazima tumuweke Mungu mbele na kumpa yeye kipaumbele kwa hiyo tuseme wote bila
wewe Mungu mimi sitoboi haleluya
Mathayo 6:31-33
“Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe
nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba
yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza
ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa wapagani na watu
wasiomjua Mungu au wanaoabudu miungu hufunga maduka yao saa za ibada zao na
kutoa kipaumbele kwa miungu yao kuliko wale wenye Mungu wa kweli aliyehai, sisi
tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuliko wao
b. Walifunzwa umuhimu wa maombi na ibada
i.
Vijana wa kiyahudi walifundishwa umuhimu wa
kushiriki ibada na maombi, hivyo walishiriki ibada kuanzia ngazi ya kifamilia
na ibada za kijamii, walitumia ibada kama njia ya kuonyesha ya kuwa
wanamtegemea Mungu walijiimarisha kiimani na iliwajengea ujasiri kuwa Mungu ni
kila kitu katika maisha yao.
a. Daniel 6:10 -11“Hata
Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia
nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa
kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru
mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.Basi watu hao
wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu
wake.”
b. 1Nyakati 4:9-10 “Naye
Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake
Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana
Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na
kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda
na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”
Vijana wa kiyahudi hawakuacha kuomba kwa sababu zozote
zile, waliamini kuwa maombi yanaweza kuingilia kati shughuli zao, kazi zao,
maisha yao, na kilimo, ufugaji na biashara na kwa kweli Mungu aliweza kuingilia
kati mahitaji yao na walifanikiwa sana, kijana wa kikristo akifanikiwa Mungu
anapoteza maana na ibada na maombi zinapoteza maana hayo hayakuwa msingi wa
tamaduni za kiyahudi.
c. Waliwafunza Historia yao
i.
Wayahudi walihakikisha kuwa vijana wanajifunza
historia ya taifa lao na kwa sababu hiyo walizitumia sherehe za kidini kama
Pasaka, sikukuu ya vibanda na nyinginezo ili kuwakumbusha Israel matendo makuu
ya Mungu
a. Kutoka 12:26-27 “Kisha
itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu
kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya
nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa
nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia.”
Hayo yalikuwa maswala ya msingi ambayo jamii ya
kiyahudi iliipandikiza kwa vijana wao ili wamtangulize Mungu, wajue kuwa Mungu
ndiye kila kitu katika maisha yao kabla ya kuwafunza maswala mengine
walihakikisha vijana wao kwanza wanamjua Mungu, wanamuabudu Mungu, wanamuomba
Mungu wanamtegemea Mungu na wanaheshimu ibada na kila kitu kwenye taifa lao
kilionyesha jinsi Mungu alivyowapigania.
d. Walitoa mafunzo ya ujasiriamali
i.
Baada ya kuweka Msingi katika torati, maombi na
historia ya taifa lao, wakati huo huo pia vijana wa kiyahudi walifundishwa
ujasiriamali, wayahudi waliamini kuwa usipowafundisha vijana kufanya kazi kwa
mikono yao wenyewe unawaandaa kuwa wezi, kwa hiyo waliandaliwa kujitegemea,
hivyo kulikuwa na stadi za maisha na maswala kadhaa za kufanya ambazo wazazi
waliwazoesha ili kuwa wasimamizi wa mali zao na kujitegemea kifedha na kimaisha
a. Mwanzo 37:2 “Hivi
ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa
akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa
Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari
zao mbaya.”
b. Marko 6:2-3 “Na
ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia
wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii
aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?
Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda,
na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.”
c. Matendo 9:36-39 “Na
mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi
(yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka
alizozitoa.Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha,
wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao
wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake,
kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao.
Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia
na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa
pamoja nao.”
d. Matendo 18:1-3 “Baada
ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.Akamwona Myahudi mmoja,
jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za
karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote
watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja,
akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.”
Maandiko yanaonyesha kuwa vijana wa kiyahudi
waliandaliwa vizuri kwaajili ya kujikimu kwa mahitaji yao, Yusufu aliandaliwa
kuwa msimamizi wa mifugo ya Yakobo, Yesu aliandaliwa kuwa Seremala (Mjenzi) na
Dorkas aliandaliwa kuwa mfumaji wa nguo, Paulo, Prisila na Akila walikuwa
washona mahema, Ishmael na Esau waliandaliwa kuwa wawindaji.
Kwa hiyo Jamii ya kiyahudi
iliwandaa vijana wao kwaajili ya maswala ya kiroho, lakini vile vile kwaajili
ya maisha ya kujitegemea na kuwapa stadi mbalimbali za muhimu za maisha Maswala
haya yanawawezesha vijana kukua wakijitegemea huku wakiwa na misingi imara ya
kiimani na kiuchumi hakuna jambo la kusikitisha duniani kama kuomba au
kuwategemea watu kwaajili ya mahitaji yetu na ndio maana Paulo Mtume alifanya
kazi kwaajili ya kuwafundisha watu waache uvivu na wasimuelemee mtu
2Wathesalonike 3:7-9 “Mwajua wenyewe jinsi
iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula
chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana
tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.Si kwamba hatuna amri,
lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate.”
Kumbuka: usiilete biashara yako mahali pa ibada! Maandiko
yanaonyesha wazi kuwa Yesu hakupendezwa kabisa na watu waliopageuza mahali pa
ibada kuwa sehemu ya biashara kwa faida zao binafsi, kusudi kuu la mahali pa
ibada ni kwaajili ya kumuabudu Mungu.
Yohana 2:14-16 “Akaona pale hekaluni watu
waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.
Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe;
akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale
waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa
nyumba ya biashara.”
Ni halali kufanya biashara
kanisani? jibu ni moja kwa moja hapana, kulingana na mafundisho ya Bwana Yesu,
Maandiko yanasisitiza utakatifu wa mahali pa ibada, kila nyumba iliyojengwa kwa
kusudi la ibada linapaswa kutumika kwa makusudi ya ibada, kuleta bidhaa zako
zozote katika nyumba ya Mungu ni ukosefu wa adamu kwa Yesu Kristo
mwenyewe, kwa sababu nyumba yake
inageuzwa kuwa soko, kanisani ni mahali maalumu kwaajili ya kuhudumia watu,
kiroho na kimwili, kuwafundisha watu neno la Mungu na kuwasaidia kukua kiimani,
unapoleta biashara kanisani maana yake ni kuwa unazingatia zaidi faida za
kifedha kuliko mahitaji ya waamini, Yesu alikasirishwa san asana mpaka
akatengeneza kikoto cha mkambaa kufukuza wote wanaofanya biashara nyumbani mwake
kama una msimamo kumshinda Yesu basi leo ujue kuwa mtazamo wa Yesu ni mtazamo
wa Mungu, shughuli za kibiashara zinazotakiwa kufanyika kanisani ni zile tu
zinazohusiana na faida za kikanisa na injili, kanisa linaweza kuwa na miradi
kwa kusudi la kutoa huduma kwa wahitaji, kama hospitali, shule, vituo vya
watoto, Mauzo uya biblia na vitabu vya kiroho katika uatartibu maalumu, lakini
swala la kufanya biashara la moja kwa moja kanisani hata kama ni baada ya ibada
halikubaliki, kanisa linaweza kushiriki katika maswala ya kiuchumi kwaajili ya
kufadhili kazi zake za kihuduma
Lakini ni marufuku kuchanganya
biashara na kanisa, shughuli za kanisa zinapaswa kulenga kuimarisha Imani na
huduma za kijamii na sio kwa sababu ya manufaa ya mtu binafsi, Mtu anayekuja
kuabudu akiwa na biashara na anayekuja kuabudu kwa huku moyoni ana mpango wa
kununua kitu ulani kwa faida yake moyo wake katika ibada utagawanyika
Luka 10:27 “Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na
jirani yako kama nafsi yako.”
Ni imani yangu kuwa somo hili
litamsaidia kila kijana wa kanisani, kujifunza ujasiriamali na kuelekwa umuhimu
wa kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu, kwa wema, na kwa sifa muhimu
zinazojenga mahusiano na kujenga mtandao mzuri wa kibiashara na kufanikiwa
neema iwe juu yako!, Bila kuathiri uhusiano wetu na Mungu!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.
+255 718 990 796