Jumatano, 1 Januari 2025

Kurejeshwa kwa miaka ya hasara!


Yoel 2:25-27 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa wakati mwingine katika maisha ya mwanadamu duniani huwa kunakuwa na maafa yanayojitokeza katika nyanja mbalimbali za mifumo ya kimaisha, maafa hayo yanaweza kuwa ya kiroho, kisiasa, kiuchumi na kimwili. Aidha aina hizi za maafa sio ngeni kwa ulimwengu na kwa watu wa Mungu likiwemo taifa la Israel, Wana wa Israel walikuwa na ufahamu wa kina kuhusiana na aina hizi za maafa zilizokuwa zimewakuta na kuwapata katika taifa lao, na hivyo walikuwa na ujuzi wa kutafasiri na kuelewa kwa kina kile ambacho manabii walikizungumza kwa uwazi au kwa mafumbo na hii iliwasaidia kutambua mpango na makusudi ya Mungu katika maisha yao sawa na Maneno ya manabii. Nabii Yoeli alikuwa moja ya manabii walioweza kuainisha wazi na kuijulisha jamii yake kwa habari ya maafa hayo au majanga lakini sio hivyo tu njia ya kuondoa majanga hayo na namna ambavyo Mungu angeyakomesha maafa hayo na kuwapa miaka ya neema au ya urejesho

Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”

Unaona hapo nabii alitangaza maafa ya kiroho, kisiasa na kiuchumi kwa wana wa Israel na kisha baadaye aliwapa njia ya namna ya kufanya ili kurejesha neema ya Mungu katika maisha yao na kisha alitangaza kurejeshwa kwa miaka hiyo ya hasara, ujumbe huu leo uko wazi kwaajili ya ulimwengu, Israel, Kanisa, taifa, jamii, familia na kila mtu mmoja mmoja kwa nafasi yake na maisha yake kwa hiyo ni muhimu kuzingatia kile ambacho Mungu anataka kusema nasi leo jambo litakaloutaufanya mwaka mpya huu  na miaka mingine kwako kuwa mwaka wa neema kuliko majira na nyakati ulizozipitia katika maisha yako, kwa sababu hiyo Leo tutajifunza somo hili “Kurejeshwa kwa miaka ya hasara” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 


Kutangazwa kwa miaka ya hasara.

Namna ya kuondoa miaka ya hasara. 

Kurejeshwa kwa miaka ya hasara


Kutangazwa kwa miaka ya hasara

Nabii Yoel alipokea ujumbe wake kama neno la Mungu kwa utawala wa Yuda lakini pia ukiuhusu ulimwengu wote, Yoeli alikuwa na makusudi makubwa matatu tu, kutangaza hukumu ya Mungu inayokuja kwa utawala wa Yuda, kuwaita watu pamoja ili waweze kumrudia Mungu kwa toba na kutangaza neema ya Mungu Kwa watu wake wanapokubali kujinyenyekeza, anapotangaza ujumbe wake nabii huyu hususani katika eneo la kwanza lakutangaza hukumu ya Mungu, kimsingi nabii anazungumza kuwa hukumu hii ya Mungu kwa watu wake itahusu, maswala yote muhimu ya mwanadamu, kiroho, kisiasa na kiuchumi, kuwa endapo watu wake Mungu wangeendelea katika mfumo wa maisha ya kutokujali kuhusu Mungu, Mungu angeinua taifa lenye nguvu, au mataifa adui yenye nguvu yatakayoishambulia Yuda na kuleta maafa katika taifa lao, hali ya kiroho ya Taifa, kanisa, familia na mtu mmoja mmoja ina mchango mkubwa sana katika kuamua mustakabali wa kisiasa na kiuchumi katika maisha ya taifa, kanisa na mtu awayeyote yule.

Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”

Tangazo la nabii Yoeli limewasumbuwa watafasiri wengi wa Biblia hususani katika pigo la tunutu, nzige, parare na madumadu, hii ni kwa sababu nabii alitumia mfano wa wadudu waharibifu wa mazao kuzungumzia uharibifu wa kisiasa, kiuchumi na kiroho kwa watu wa taifa lake, Yuda.  Israel kama ilivyo hapa Afrika huwa tunafahamu kuwa ziko nyakati ambapo, katika secta za kilimo hutokea wadudu waharibifu wa mazao ambao kimsingi husababisha hasara kubwa sana na hata kuleta njaa na uharibifu mkubwa wa mazao ya chakula, wadudu hao Kwa kawaida huvamia kama jeshi, na wanajulikana kama tunutu, nzige, parare na madumadu, kwa hiyo Yoeli anawatumia wadudu hawa kutangaza miaka ya hasara kiroho, kisiasa na kiuchumi. Kimsingi Yoel hazungumzii wadudu halisi bali anazungumzia Mataifa mabaya ambayo yataivamia Israel na mataifa hayo yatakuwa yameruhusiwa na Mungu kuwaumiza na kuwaletea hali ngumu kwa sababu ya dhambi zao, Yoeli anatumia uzoefu wa wadudu waharibifu wa mazao kuwakilisha uharibifu wa taifa, kisiasa, kiuchumi na ambako kumesababishwa na hali yao ya kiroho.

Muda wa hasara ungeweza kuhusisha uharibifu katika maeneo kadhaa, kiuchumi, kisiasa, na kiroho muda huo hapa umeitwa miaka, lakini ni nyakati na majira ambayo Mungu amekusudia upite ko sio lazima iwe miaka:-

Kiuchumi – Watu  walioishi siku nyingi na wale watakaoishi siku nyingi yaani wenye uzoefu ambao nabii anawataja kama wazee watakuwa wanafahamu maafa ya kiuchumi yanayosababishwa na wadudu waharibifu kama tunutu, nzige, parare na madumadu, Yoeli aliwadhihirishia wazee yaani wenye uzoefu kufikiri na kutafakari kuwa hali kama hiyo kama umewahi kwako katika nyakati zao, wajitafakari kwani hali ambayo ingewakuta hata wazee, na wenyeji wa nchi wasingeliweza kuamini kwani lilikuwa ni pigo la kiuchumi la kihistoria ambalo halijawahi kutokea katika maisha yao

Yoeli 1:2-4 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.”

Tunutu hawa ni jamii ya panzi/nzige wakiwa katika hatua ya kuwa kama buu au kiwavi, hapa kwetu wanaitwa viwavi jeshi kwa kawaida hawa ni waharibifu sana viwavi wanapovamia shamba kwa muda mfupi huwa wanashambulia Matunda au maua ambayo yanaelekea kuzaa matunda na hivyo kusababisha tunda lisizaliwe au kama tunda limezaliwa lioze kwa hiyo wadudu hawa huharibu MATUNDA ya mimea yaliyozaliwa au yanayotaka kuzaliwa

Nzige hawa ni jamii ya panzi ambao huruka kwa makundi makubwa sana yenye kutisha nao pia kama viwavi jeshi huweza kushambulia MAJANI ya mazao na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao, na kuleta njaa na kuathiri uchumi wa watu

Parare ni jamii ya panzi ambao nao kimsingi huweza kushambualia MATAWI na vijiti na kuvitafuna na kuozesha kabisa, kama mmea unaweza kushambuliwa na nzige na kisha wasije hawa parare mmea unaweza kupata nguvu na kustawi tena lakini wakija parare wao hula kabisa matawi na kuacha miti ikiwa imesalia kama kijiti kilichosimama, kikavu na  kuharibu kabisa ustawi wa mmea na kusababisha majanga ya njaa

Madumadu wao huja kumalizia MTI wenyewe na kuutafuna mpaka kubakiza shina tu, lakini kama haitoshi Madumadu huwa wanaharufu mbaya kama utawakanyaga na kuwauwa wao ni wakubwa zaidi na ni wanye kutia kinyaa kabisa sehemu nyingine panzi hawa jamii ya madumadu huitwa panzia kunuka kwa hiyo endapo Mungu angeruhusu wadudu hao kuivamia inchi ukweli ni kuwa hali ya uchumi wanchi au taifa au kanisa au mtu mmoja mmoja ingwakuwa iko katika hali ngumu wao humalizia kabisa mmea na kuua


Kisiasa – Yoeli aliendelea kuweka wazi kuwa hukumu ya Mungu kwa watu wa Mungu isingelikuwa ya kiuchumi pekee, bali ingelihusu pia hali ya kisiasa ambayo ingewatesa Israel kwa ukoloni tofauti na ule waliowahi kuusikia huko Misri, Mungu angeleta hukumu ya kisiasa ambako Israel na Yuda wangekwenda utumwani na kuwa chini ya tawala kubwa za dunia za nyakati hizo Falme hizo zingeinuka kutoka kaskazini mwa Yuda na kusababisha maafa sawa tu na wadudu waharibifu wanavyoweza kushambulia mti au mazao, mataifa hayo yanatajwa kama mataifa nyenye nguvu na wenye jeshi kubwa na wakali na wangeharibu watu wa Mungu na kuwachukua na kuwapeleka utumwani na wangeondoa kabisa ustawi wa kiroho na kimwili na kiuchumi wa taifa la Mungu na wangejaribu kuwatawanya kabisa Wayahudi ona 


Yoeli 1:6-7 “Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe.”


Tunutu – Wangewakilisha utawala wa Ashuru na Babeli (900-600BC) Israel wangepoteza utawala wa kisiasa chini ya dola kubwa ya Ashuru na Yuda wangepoteza utawala wa kisiasa chini ya utawala wa Babeli, Amani na utulivu pamoja na furaha ya Israel au watu wa Mungu ingeweza kutoweshwa kabisa na mataifa hayo yenye nguvu 


Yoel 1:10-12 “Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu.”


Nzige – Wangewakilisha utawala uliofuata baada ya kuanguka kwa utawala wa Babeli ambao ni Waamedi na Waajemi (550-331BC) kimsingi hawa nao wangeendeleza uharibifu ule ule ulioanzishwa na tunutu, wao wangeendelea kula majani na magamba ya mti na kuuacha mti huu ukiwa uchi na chini ya aibu, kubwa sana na hatari ya kifo cha mti husika.


Parare –Wangewakilisha utawala wa Wayunani/Wagiriki (800-146 BC) wao wangesababisha ukimya kabisa kwa wana wa Israel na wangeweza kubalisha kabisa mtazamo wao na kuwaingizia elimu na falsafa na mitazamo mipya kutokana na Maendeleo ya kielimu waliyokuwa nayo wayunani, Parare walikula kabisa matawi na kuufanya mti usionekane tena wala kujulikana kuwa ni mti wa namna gani na mti ungepoteza sura yake 


Madumadu – wanawakilisha utawala wa kisiasa wa Warumi, (31 BC-476 AD) Israel wote wangekuwa chini ya utumwa  na kutiwa unajisi na watu hawa, ambao wangemsulubisha hata masihi, na kuiharibu kabisa Yerusalem na kuwaondoa kabisa wayahudi na kuwatawanya Dunia nzima wasiwepo katika nchi ya Yuda kabisa kwa hiyo sio tu kuwa Matunda ya mti yangeliwa, au majani ya mti yangeliwa au matawi na maganda yake yangeliwa lakini mti ungeliwa kabisa na kuozeshwa na kuharibiwa mpaka shinani Warumi ndio waliowaondoa Israel na kuwatawanya wayahudi wengi duniani na kuwahamisha Israel kabisa lakini pia walimsulubisha Masihi 


Kiroho – uharibifu ambao ulifanywa na mataifa haya sio tu ulihusu uchumi na siasa lakini vile vile ulihusu swala zima la kiroho, uchumi unapoguswa na siasa inapoguswa hali ya kiroho haiwezi kuwa salama kwa hiyo Yoeli anaonyesha kuwa hata Imani iliguswa katika maafa hayo aliyoyatabiri, Inawezekana wakati mwingine sio mara zote hali ya kiroho ikiwa mbovu ikasababisha hali ya uchumi na siasa pia kuwa mbovu, au hali ya uchumi na siasa ikiwa mbovu, wito wa kuweka sawa ya maswala kiroho yanaweza kurejesha uponyaji wa kitaifa, kisisasa na kiuchumi, Yoeli anaonyesha kuwa mapigo hayo pia yaliunganishwa na hali ya kiroho.


Yoeli 1: 13-14 “Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu.Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana,”


Tunutu – Wanasahambulia “TUNDA LA ROHO” au matunda ya kiroho, ile hali njema ya watu wa Mungu kuwa na upendo, furaha, Amani, uvumilivu. Utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi katika jamii sasa imetoweka imeliwa na tunutu, Yoeli analiona taifa na kanisa kuwa limepoteza haki, limepoteza ile hali ya kuwa na sifa ya watu wacha Mungu, dhuluma kila mahali, kiburi na majivuno, unibafsi na choyo, chuki na mafarakano, uchawi na uadui ndio ambao unachukua nafasi sasa na kuondoa upendo wa kwanza, sio hivyo tu kunaupungufu mkubwa wa matendo ya ajabu, miujiza na uponyaji pamoja na utendaji wa karama za Roho Mtakatifu, kanisa limeachwa jeupee na maombi ya dhati na kuugua hayapo. 


Yoeli 1:7 “Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa.”


Ufunuo 2:4-5 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”


Nzige – Inawakilisha kutoweka kwa “NENO LA MUNGU”, Hapa hakuna unabii na hali ya neno la Mungu limekuwa adimu, zaidi ya yote kuchakachuliwa kwa Neno na tafasiri zake halali, kila mmoja anatafasiri neno anavyojisikia na unabii unafifia, ni manabii wachache sana labda Daniel tu walioweza kusema chochote walipokuwa utumwani Babeli, lakini wakati wa utawala wa Uajemi na uamedi, hakukuwa tena na nabii na ukimya ukatawala kwa muda mrefu, katika maafa ya kiroho yanayoweza kuwakumba watu wa Mungu ni pamoja na kutokuwepo kwa unabii ambao kimsingi unatoa mwelekeo wa watu wa Mungu na kuwatia moyo, aidha kama hakuna wahudumu halali wa neno la Mungu wanaowasaidia watu wa Mungu kujua NENO, jamii ya watu wa Mungu inaathirika na kuwa kama imevuliwa nguo, Neno la Mungu ndilo linalochochea utendaji wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo wakati neno la Bwana linapokuwa adimu, Roho wa Mungu hutulia na hivyo kuzimishwa.


Mwanzo 1:2 “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”


1Samuel 3:1 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.”


Yoeli 1:16-17 “Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka.”


Parare – wenyewe wanahusika na kupotea kwa UTAKATIFU Parare wanahusika na uharibifu  na wakati huu wanaharibu kabisa matawi na maganda ya mti, wanaharibu muonekano halisi wa mti, hii inaashiria kuondoka kwa hofu ya Mungu, watu kuacha kuishi kwa uadilifu na mwenendo wa njia za Mungu, watu hawawezi tena kuushinda ulimwengu, wala hakuna tena mahubiri yanayozungumia au kuelekeza watu kuishi maisha matakatifu, wala watumishi wa Mungu wanaokemea dhambi kwa viwango vya juu, hakuna tena mtu na nayeweza kukaza kama na kuhubiri Utakatifu kama walivyofanya mitume ona

1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”


2Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.”


Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” 


Madumadu – Mti umeliwa mpaka shinani na unaoza hii ni hali ya kutoweka kwa matumaini na ni wakati ambapo imani imekwisha na ni kipindi cha GIZA/KUFA KIROHO – kila kitu kimekufa na limebaki jina tu, uko uwezekano wa taifa, au kanisa au mtu fulani mmoja mmoja kubakia na jina tu lakini hali ya kiroho inakuwa imekufa kabisa mmea hauna matunda, hauna majani, na matawi yameliwa na shina lake linabaki limeoza, katika hali kama hiyo hakuna matunda ya kiroho, Neno la Mungu limechakachuliwa, hakuna msisitizo wa kujaa nguvu za Roho Mtakatifu, hakuna mkazo wa utakatifu na uchafu unabaki katika kanisa, kuchukulina na dunia, hakuna haki, upendeleo unachukua nafasi, majungu masengenyi na Kila aina ya ubaya na hata kuuana na kurogana mwili mwili mwili unakuwa katika nafasi ya kiroho, hakuna imani. Watu wamepoteza umakini wa kimaadili na wameleweshwa katika anasa na upatikanaji wa mali za duniani 


Yoel 1:5 “Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu.” 


Ufunuo 3:1 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.”


Luka 18:8 “Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?


Kwa hiyo tunaweza kuona jinsi nabii Yoeli alivyokuwa akiionya jamii dhidi ya ujio wa miaka ya hasara, Mungu alikuwa amempa neno la maonyo na kuwaonya watu wake dhidi ya uharibifu na maafa ya kiuchumi, kisiasa na kiroho, huu ni ujumbe kwa ulimwengu mzima kwa kila taifa na kanisa na mtu mmoja mmoja, wakati wote kila taifa litakapopuuzia maswala ya Mungu ni lazima ijulikane wazi kuwa Mungu ataondoa mkono wake na kumruhusu yule alaye aweze kuharibu kila kitu, Ustawi wa taifa lolote na kanisa familia na mtu mmoja mmoja unategemeana na namna tunavyompa Mungu heshima katika kila eneo, kama tutaruhusu ufisadi, mmomonyoko wa uadilifu rushwa na dhuluma kila mahali, tujue wazi kabisa Mungu ataiondoa heshima yake katika kanisa au taifa  Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Hata hivyo ikiwa hali kama hizo zimelikuta taifa, au kanisa au mtu binafsi bado liko tumaini kwa kuwa Mungu ni mwingi wa rehema na si mwepesi wa hasira ni Mungu ambaye hatatulipa sawasawa na makosa yetu yeye kama Baba anavyowahurumia watoto wake ndivyo Anavyowahurumia wale wamchao naye anatoa njia ya kufanya ili kuondoa miaka ya hasara au kwa lugha nyingine muda wa hasara, hilo linatupa neema ya kutafakari kipengele cha pili.


Namna ya kuondoa miaka ya hasara

Ni ukweli ulio wazi kuwa licha ya nabii Yoeli kutoa maonyo kwa watu wa Mungu juu ya kupatwa na mambo mabaya au juu ya taifa kupitia miaka ya hasara nabii Yoeli anatoa wito wa kutubu ili Mungu aweze kuleta uamsho, na ufufuo na urejesho kwa miaka iliyoliwa na tunutu, nzige, parare, na madumadu, wakati wowote tunapotaka kuona Mungu akiliponya kanisa, taifa au watu wake katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiroho, ni silaha za kiroho pekee ndizo zinazoweza kuleta uponyaji wa mazingira yote makubwa na silaha hiyo ni unyenyekevu na toba ya kweli na hiki ndicho anachokisema Yoeli

Yoeli 1:13-14 “Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana,” 

Yoeli 2:12-17 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?” 

Wakati wowote hali inapokuwa mbaya katika jambo lolote nabii anatoa wito kwa watu wa Mungu kutubu kwa kumlilia Mungu, na kumuomba Mungu kwa kufunga na kuomba,  na hata kukesha usiku na mchana, wito huu unatolewa kwa watu wote kuanzia kwa makuhani yaani watumishi wa Mungu mpaka watu wengine wote, Nabii anaonyesha kuwa hii ndio namna ya kiroho ambayo Mungu alikuwa amemuagiza kuwa watu wafanye hivyo, akiwakumbusha kuwa Mungu ni wa neema na rehema  na kuwa amejaa huruma wala sio mwepesi wa hasira, na kuwa yeye hughairi mabaya, hii ndio njia iliyotumiwa na mataifa yote hata ya kipagani katika kujiokoa na hasira za Mungu pale zilipotangazwa

Yona 3:4-10 “Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.” 

Biblia imejaa mifano na maandiko ya kutosha yanayoonyesha kuwa kila wakati Mungu alipotaka kuadhibu au hata alipoadhibu toba ilileta mabadiliko makubwa, Bwana yuko tayari kughairi kila aina ya uovu alioukusudia au kuuruhusu endapo tu tutaitikia kwa toba kile ambacho neno la Mungu limetuagiza kukifanya hii ni kwa mtu mmoja mmoja, kwa taifa na kwa kanisa pia na watu wowote wanaotaka kuona mkono wa Mungu wa rehema ukiwa juu yao, ikiwa unaona wazi kuwa unapita katika miaka/muda iliyoliwa na tunutu, nzige, parare na madumadu basi changamkia agizo la toba na acha maovu yako nawe utaona uamsho mkubwa, mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiroho na mvua ya Baraka itanyesha juu yako., 

Unabii. Kuhusu 2025 na kuendelea!

Wakati Mungu ananipa ujumbe huu alitaka niseme wazi na mataifa ya Malawi na Kenya na Tanzania, alitaka pia niseme na ulimwengu na mtu mmoja mmoja lakini zaidi sana Malawi na Kenya, huku Tanzania ikijifunza kutoka katika unabii huo, “Mungu ameniambia kwa habari ya Malawi na Kenya, Kwamba siku za karibuni aliinua viongozi wacha Mungu katika mataifa hayo, yaani marais ambao wanamjua Mungu na wameokoka, lakini amenimeambia pamoja na hayo nchi hizo zinahali mbaya ya maporomoko makubwa ya kiroho, na kwa sababu hiyo uharibifu mkubwa unazipata nchi hizo, watapata majanga ya kawaida ya asili na njaa na mporomoko mkubwa ya kiuchumi na vurugu za hapa na pale, lakini sababu kubwa ni kuwakumbusha maraisi hao kuirudisha nchi ya Malawi na Kenya katika kilele, cha uchaji wa Mungu, hizi ni nchi ambazo Mungu alizikusudia ziwe nchi za kiinjilisti na kimisheni, lakini zimeacha wajibu huo na hivyo wanapaswa kutubu na wakifanya hivyo kutakuwa shwari Malawi na Kenya, Malawi Umisheni, Kenya Uinjilisti Kwa Tanzania Mungu amekuchagua kuwa Mwalimu wa neno la Mungu na mafundisho sahihi, lakini Mungu anaionya Tanzania kuwa nayo imeanza kuruhusu mafundisho potofu kuenea na injili imechakachuliwa katika taifa hili, Mungu anaionya Tanzania na kanisa la Tanzania kusimama imara katika kusimamia kweli ya Mungu vinginevyo iko hukumu nzito italijia taifa hili, lakini wakitubu na kila mtu akiisimamia kweli na kuacha kuichuja injili Tanzania itakuwa mfano wa kuigwa Afrika, aidha matukio ya kidunia yatakayojitokeza katika miaka hii kuanzia 2025, kutakuwa na uamsho mkubwa sana wa kasi katika Israel, katika jamii ya wayahudi, kiu ya kuwa taifa kubwa itaongezeka na kiu ya kulijenga Hekalu itawajia kwa nguvu, Israel itaendelea kuwa na nguvu kubwa sana na hakutakuwa na mtu wa kuwanyamazisha katika kile wanachotaka kukifanya Duniani, kutakuwa na maendeleo makubwa sana kwa Taifa la Saud Arabia, Jordan na Misri, lakini taifa la Iran litafifia sana kwa nguvu zake, kutakuwa na utulivu mkubwa sana katika taifa la Syria na watu wake watatulia na kujali katika kujijenga wenyewe kiuchumi na kimaendeleo na hawatatamani vita tena milele, viongozi wengi wa dunia wenye asili ya kidikteta wataangushwa madarakani, kutakuweko na viongozi wengi wenye kupigiwa kura za kutokuwa na Imani nao na wengi kuondolewa madarakani kwa kura za kibunge na maandamano ya wananchi, kutakuwa na uamsho mkubwa sana katika nchi ya Msumbiji, watanzania na wakenya wengi watahubiri Msumbiji na kuwa na makanisa makubwa sana, miujiza mingi na wahubiri wakubwa sana watapatikana Msumbiji na watu wengi watakuwa wakisafiri kwenda Msumbiji kwaajili ya maombi na maombezi, Aidha kutakuwa na watu wenye misimamo mikali wengi sana katika Imani ambao watakuwa na uelewa wa kumcha Mungu kwa viwango vya juu bila unafiki na watakuwa na wivu wa bwana hawa watainuka kwa wingi hususani Tanzania, aidha Muhubiri wa kimataifa aitwaye Bushiri huko Malawi, atang’ara sana  na kuwa tegemeo la watu wengi, Mungu atamtumia kwa viwango vikubwa sana na ninaambiwa atakuwa ni mtu mwenye upendo mwingi sana mimi simjui na simfuatilii sana, lakini Mungu atamtumia katika kilele chake”  Mwisho

Kurejeshwa kwa miaka ya hasara 

Yoeli sio tu kuwa alitangaza hukumu ya Mungu, lakini alionyesha njia ya kumrejea Mungu na kama hayo hayatoshi Yoeli anaonyesha na kutabiri kurejeshwa kwa hali ya kiroho na Baraka za Mungu ambazo kimsingi asili yake ni rohoni akionyesha kuwa Mungu atawahurumia watu wake na kusikia wivu kwaajili yao na kwa sababu hiyo atawajibu watu wake na kuwaponya kiroho, kimwili na kisiasa

Kiuchumi - Yoel 2:18-19 “Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. Bwana akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;”

KisiasaYoel 2:20-22 “lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa Bwana ametenda mambo makuu.Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.”

KirohoYoel 2:23-27 “Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza. Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.”

Hatimaye – Yoel 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”

Hatimaye Mungu ataleta uamsho mkubwa sana na kurejesha tena matunda ya roho, karama za Roho Mtakatifu na utendaji mkubwa wa Mungu, kila eneo la ustawi wa maisha ya mwanadamu litaimarika hii itatokea kwa taifa, itatokea kwa kanisa na ustawi wa mtu mmoja mmoja kwa kadiri anavyojitoa kwa Mungu na hiki ndio bwana anachotaka kukiona kama tutatudumu katika utakatifufu na imani na kuishi katika uweza na nguvu za Roho Mtakatifu basi tegemea Ustawi huu, tukidumu katika unyenyekevu na uaminifu  na kuwa mbali na ukaidi hakuna mtu atakaye tahayarika, Mungu atatuhurumia, na Roho wa Mungu atamwagwa kwa wingi na karama na madhihirisho yataachiwa katika kanisa na watu watakiri wazi kuwa Mungu yu katikati yenu.

Wishes Happy new year to you All, love you

Na. Rev. Mkombozi Samuel Kamote 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.


Jumapili, 29 Desemba 2024

Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu!


Isaya 9:1-2 “Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”




Utangulizi:

Moja ya habari za kinabii za kutia moyo na kuleta tumaini kwa jamii ni pamoja na ujio wa Masihi, Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai ambaye angeleta Nuru kwa watu waliokuwa gizani, na kuwaangazia tumaini watu waliokaa katika inchi ya uvuli wa mauti, Kimsingi giza pamoja na uvuli wa mauti ni hatia, hukumu, ni kupoteza tumaini, ni kuishi mbali na Mungu, ni kukosa muelekeo, pamoja na mateso yanayoambatana na kukata tamaa ambavyo vinawasumbua wanadamu kila iitwapo leo, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kungekuwa ni sehemu muhimu ya kutimia kwa unabii huu ambao kimsingi ni habari njema zenye kuleta tumaini la Rehema kuu za Mungu kwa watu wote, kimsingi Kristo Yesu alipokuja Duniani alijitangaza rasmi kuwa yeye ni Nuru ya ulimwengu.

Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

Nuru ni ishara ya wema wa Mungu kwa wanadamu, na giza ni ishara ya uovu uonevu na utendaji wa ibilisi, Maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo ni Nuru inayong’aa gizani, ambayo imekuja ulimwenguni kwa kusudi la kuwapa tumaini na kuwaondoa hofu wale wote waliokuwa wanakabiliwa na giza la uovu na uvuli wa Mauti. Wakati Yesu anazaliwa kimsingi watu walikuwa wamechoka sana, walikuwa wamekata tamaa, ukiacha ukoloni mzito  wa Warumi uliokuwa ukiwatawala kiserikali, maisha yao yalijawa na mateso, kukata tamaa na kufunikwa na giza la kiroho, miaka mingi karibu 400 ilikuwa imepita kukiwa na ukimya bila ya kuweko kwa nabii wala neno la Mungu la Dhahiri kwaajili yao, tumaini lilikuwa limebaki moja tu, kusubiri kutimizwa kwa unabii wa kuhusu kuja kwa Masihi, kiu yao hii inaonekana wazi hata Yohana alipokuwa ameanza kuhubiri ubatizo wake wa toba Maswali mengi yalielekea katika  kiu na hamu na shauku ya kumtamani Masihi ili aweze kukomesha mateso yao.

Yohana 1:20-23 “Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.”              

Kwa nini kulikuwa na maswali mengi sana kwa Yohana Mbatizaji, kwa sababu watu walikuwa wamechoka sana na sasa walikuwa wakimtazamia Masihi aje kuwakomboa na kuwatoa katika maisha yaliyogubikwa na giza nene, tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, neno la Mungu linatukumbusha kuwa hatupaswi tena kuishi maisha ya mashaka, ya kukata tamaa, ya kutokuwa na matumaini, maisha ya machozi, na kuweko gizani, kwa sababu Nuru imekuja ulimwenguni, kimsingi sio Israel pekee waliokuwa wakimtarajia masihi lakini mataifa yote duniani ujio wa masihi ungekuwa ni habari njema za kuleta matumaini makubwa sana na kuondoa hofu.

Luka 2:8-14 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”                 

Tutajifunza somo hili Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu. Kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-

 

·         Maana ya kwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti

·         Wale waliokwenda katika giza wameona Nuru kuu!

 

Maana ya kwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti

Neno kwenda katika giza, katika lugha ya kiebrania linatumika neno “chôshek” kwa kiingereza “destruction” kwa Kiswahili kukaa katika “uharibifu” au kukaa katika uovu, Kabla ya ujio wa Yesu Kristo watu waliishi katika giza kubwa la kiroho, watu walikuwa hawana mwelekeo na hawaijui njia kwa sababu hiyo giza lilitawala na ukiwa ulikuwa juu ya nchi, Nguvu za wakuu wa giza ndizo zilizokuwa zinatawala ulimwengu, matendo ya giza yalikuwa yanatawala ulimwengu, Giza lilitawala kabla ya Nuru ya injili kuwazukia watu hivyo watu walikuwa wanaenenda gizani, watu walikuwa hawawezi wala hawana njia ya kurejesha uhusiano wao na Mungu ambao uliharibika tangu anguko la wazazi wetu Adam na Eva, Ni ujio wa Yesu Kristo ndio ulioleta Nuru ulimwenguni.

-          Yohana 4:4-10 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua

 

-          Wakolosai 1:12-14 “mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

 

-          1Yohana 1:5-7 “Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

 

-          Mika 7:7-8 “Lakini mimi, nitamtazamia Bwana; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu.”                  

 

-          Zaburi 88:3-12 “Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako. Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini. Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote. Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka. Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu. Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi? Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu? Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?

 

Unapozisoma aya kadhaa za kibiblia hapo juu utaweza kugundua kuwa Giza ni baya sana na giza lina uhusiano wa karibu sana na mauti, giza humfanya mtu asiwe na msaada, giza ni sawa na mtu aliyetupwa miongoni mwa watu waliokufa, giza ni kukosa tumaini la kimwili na kiroho, giza ni kama kuwa shimoni, giza linakufanya usipambanue kati ya kifo na uhai, giza linamfanya mtu apoteze kibali, giza linamfanya mtu awe chukizo, giza linamfanya mtu asifurahie maisha kwa hiyo giza ni njia ya uovu, giza ni uharibifu, giza ni kuwa chini ya ukoloni wa kiroho, wa kimwili, wa kisiasa, wa kiuchumi, giza humfanya mwanadamu aishi kwa mashaka na kwa kubahatisha, mtu aliye gizani haoni mbele yake kukoje zaidi ya kuona giza, maisha ya dhambi, na ukosefu mkubwa wa kimaadili ni kutembea katika giza, giza pia linawakilisha hukumu, giza linawakilisha hofu na msahaka, giza ni bumbuwazi, giza kuchanganyikiwa na kutokuona.

Kutoka 10:21-23 “BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu; hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao.”

Sio hivyo tu Giza liliwakilisha hali ya mauti, au uvuli wa mauti “sheol” Msiba, kaburi au kuzimu yaani mwanadamu kupita katika msongo mkubwa wa mawazo wa kutokujua nini cha kufanya sawa tu na mtu aliyekuzimu, Katika Israel pia yalikuweko mapango ya kutisha ambapo watu waliokuwa wakichunga wanyama wakati mwingine walipenya katika mapango hayo ya kutisha kwa kusudi la kutokea katika eneo la kuwapa malisho wanyama wao ambayo pia waliyaita uvuli wa mauti, mapito mazito na huzuni unazozipitia ambazo hujui zitaisha lini ni giza, lakini ukiwa na Yesu ambaye ni Nuru ya ulimwengu utapita ukiwa salama kama mwandishi wa zaburi alivyoimba:-

Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.”

Kwa hiyo hali zote hizo zilikuwa zinaashiria kuwa mtu aliyepoteza uhusiano na Mungu na hana namna wala hajui njia ya kuurejesha ni sawa tu na mtu anayepita katika giza, na kuenenda katika uvuli wa mauti, Ujio wa Yesu Kristo kwakweli ulikuwa unaleta nuru kwa wale waliokuwa katika giza, wote waliokuwa wanapita katika mashaka na wote waliopoteza uhusiano wao na Mungu wangeweza kupata tumaini kwa upya kupitia ujio wa Yesu Kristo mwokozi na msaidizi wetu mkuu.               

Wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu!

Ujio wa Yesu Kristo ulikuwa ni wenye kuleta matumaini makubwa sana kwa wanadamu, kile alichokisema nabii Isaya miaka karibu na zaidi ya 700 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, ukweli ni kuwa alipozaliwa Yesu Kristo Nuru halisi ilikuwa imeingia sio tu Israel wala sio tu katika nchi za Zabuloni na Naftali na wala sio tu katika Galilaya lakini pia kwa ulimwengu mzima

Mathayo 4:13-16 “akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa,Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.”

Luka 1:78-79 “Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.”

Ujio wa Yesu Kristo duniani unamuondoa kila amwaminiye yeye katika kuenenda gizani na kukabiliana na kutembea katika uvuli wa mauti bila kuogopa, Yesu Kristo mwenyewe alijitangaza kuwa yeye ndiye nuru ya ulimwengu na kuwa kila atakayemfuata yeye atakuwa na nuru na uzima wa milele, maisha yako hayatakuwa gizani tena.

Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

Kila mwanadamu anayeumwa na kuugua, kila mwanadamu asiye na kazi, kila mwanadamu aliyekata tamaa, kila mwanadamu mwenye misiba, kila mwanadamu anayeumizwa na hatia ya dhambi, kila mwanadamu anayejisikia upweke kwa sababu ametengwa mbali na Mungu, kila mwanadamua ambaye mahusiano yake yako katika vita, kila mwanadamu ambaye hana furaha mahali pa kazi, kila mwanadamu ambaye haabudu katika roho na kweli, kila mwanadamu ambaye hana utulivu wa nafsi, mwili na roho, kila mwanadamu ambaye yuko katika machafuko, kila mwanadamu ambaye dini yake haimpi tumaini la kweli, wala mungu wake hajishughulishi na mahitaji yake, kila aliye na huzuni, misiba na changamoto za aina mbali mbali na kila anaeyeelemewa na mizigo ya namna mbalimbali huyo yumo gizani, Habari njema ni kuwa Yesu Kristo ndiye nuru ya ulimwengu, yeye anaweza kuyaleta na kuyajenga matumaini ya kweli ya mwanadamu na kuondoa hali zote za kuvunjika moyo na kukata tamaa, yeye ndiye Nuru halisi, sio ile nuru ambayo watu waliandama mwezi na kuushangilia unapotoka gizani, huitaji tena kuandama mwezi na kuushangilia sasa nuru halisi ni Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, hivyo katika majira haya ya kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa masihi lazima tuwatangazie ya kuwa Nuru imekuja ulimwenguni na ni wakati sasa wa kuifuata nuru  

Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”

Ujio wa Yesu Kristo unatupa tumaini na kurejesha uhai – Ukimuamini Yesu Kristo yeye ataitupilia mbali hofu, atakuweka huru mbali na hatia ya dhambi, atakurudishia matumaini yaliyopotea na safari yako ya kupita katika uvuli wa mauti na badala yake nawe nuru kuu itakuzukia hutakuwa gizani tena.

Yohana 12:46 “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.”

Ujio wa Yesu Kristo na kazi ile aliyokuja kuikamilisha imetuwezesha kuwa na mamlaka dhidi ya giza, giza sasa halituwezi kwa sababu nuru ina nguvu kuliko giza nasi tunayo mamlaka ya kuyakemea matendo yote ya giza.

Yohana 1:4-5 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.”

Waefeso 5:11-14. “Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

Ujio wa Yesu Kristo kama nuru unatuhakikishia wema wa Mungu katika maisha yetu kuwa hatutakuja kuwa watumwa wa hofu, nuru ni njema, nuru ni kweli, nuru ni usalama, nuru ni maisha, nuru ni uwepo wa Mungu, Bwana akiwa nuru yako maana yake ni wokovu wako na nguvu zako na hakuna jeshi linaloweza kujipanga kupigana nawe na hata wakipigana nawe hutaogopa.

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Ujio wa Yesu Kristo kama Nuru unatukumbusha kuifanya kazi yake wakati nuru hiyo inawaka, kila mtu aliyeokolewa amepewa wajibu wa kuisambaza nuru ulimwenguni, kuamka na kuitangaza injili na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi agizo la kimaandiko linamtaka kila mmoja kufanya kazi na kuinuka na kuangaza nuru kila mahali kusiko na tumaini.

Yohana 9:4-5 “Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

Isaya 60:1-3 “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Nuru inatukumbusha kuishi maisha matakatifu, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kuwaonyesha wengine njia, hatuwezi kuwa na madai kuwa tunamfuata Yesu kisha tukajificha, hatuwezi kuwa na madai ya kuwa tunamfuata Yesu kisha tukaishi kinyume naye Yesu alikuwa mtakatifu, kuishi maisha matakatifu ni agizo la kibiblia, hatuwezi kuacha kulihubiri na kulikazia, wala hatuwezi kuishi maisha ya dhambi kwa kisingizio cha neema, Nuru yake Yesu Kristo ni neema ya kutuwezesha kuishi maisha matakatifu chini ya msaada wake kwa hiyo matendo yetu mema yanapaswa kuiangazia dunia ili kila mmoja aweze kuona na kumtukuza baba wa Mbinguni, kwa sababu hiyo hatuna budi kutembea kama watoto wa nuru kwa kuishi maisha matakatifu.

Mathayo 5:14-16 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

Waefeso 5:8-9 “Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli;”

Nuru inatukumbusha kuhusu Nguvu za Mungu, za uumbaji na utendaji, wakati nguvu za uonevu zikiitwa nguvu za giza, Nguvu za Mungu ni nguvu za Nuru, wakati wowote kunapokuwa na giza ukiweka mwanga giza hutoweka haraka na kukimbia, kunapokosekana utaratibu na kuwepo kwa machafuko Nuru ikija utaratibu unakaa mahali pake na giza lote linakimbia, andiko linasema Nuru hung’aa gizani wala giza halikuiweza, Wakati huu tunapoadhimisha ujio wa Yesu Kristo Duniani na kushangilia kuzaliwa kwake, tujue ya kuwa ujio wake umekuwa na faida kubwa sana katika maisha yetu, Nguvu za giza hazituwezi tena, sisi tumehamishwa kabisa na kuokolea kabisa katika nguvu za giza na kutuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa mwana wa pendo lake, kwa hiyo nguvu zozote za uonevu wa kishateni hazituwezi, wala giza halikuiweza nuru, tuyakemee matendo yote yasiyozaa ya giza, tuiitie nuru wakati wote tunapokuwa na mashaka, au vita Bwana akiwa nuru yetu kamwe hatupaswi kuogopa, kwa kuwa sisi sasa ni miongoni mwa watu waliokaa katika giza na nuru imetuzukia, ni miongoni mwa watu waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti na nuru imetuangazia.

Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”

Yohana 1:4-5 “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.”

1Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumatano, 25 Desemba 2024

Amekirimiwa jina lile lipitalo kila jina!


Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”



Utangulizi:

Ni majira ambayo leo Wakristo wote nchini wanaungana na wakristo wenzao ulimwengu kusheherekea sikukuu ya kuzaliwa kwa masihi yaani “Chrismas”, Ujio wa Masihi “Yesu Kristo” una maana pana sana kwa mustakabali wa maisha ya mwanadamu, kuja kwa Yesu Kristo duniani ni zawadi kubwa sana kwani ujio wake unaambatana na faida kubwa sana. Isaya alitabiri kuwa ni zawadi ya mtoto wa kiume ambaye ndani yake kuna msaada mkubwa sana wa uungu ambao una faida kubwa sana kwa maisha ya mwadamu.

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Moja ya zawadi kubwa inayoambatana na ujio wa Masihi ni pamoja na kukirimiwa jina lile lipitalo majina yote, jina ambalo lina faida kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, na hili ndilo ambalo tutalijadili katika siku hii ya leo, ili kujikumbusha Baraka kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu kupitia Bwana Yesu lakini zaidi sana pia kupitia jina lake Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”

Warumi 10:11-13 “Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.”

Jina la Yesu lina umuhimu kwaajili ya wokovu wetu, katika mazingira yote yanayohitaji msaada wa kiungu, jina hili lina nguvu, lina uwezo wa kubadilisha maisha ya watu kwa vizazi vyote, lina siri ya ajabu, lina uwezo wa kuvunja minyororo ya dhambi na kutufungulia malango ya mbinguni, jina hili linatufunulia mamlaka kubwa ya kiungu na kutuonyesha upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu na kwa sababu hiyo katika msimu huu wa sikukuu ya kuzaliwa kwa masihi sisi tutachukua muda kuangalia umuhimu wa jina hili la Yesu, tutajifunza somo hili Amekirimiwa jina lile lipitalo kila jina kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Umuhimu wa jina katika neno la Mungu.

·         Siri kubwa katika jina la Yesu.

·         Amekirimiwa jina lile lipitalo kila jina.                 

 

Umuhimu wa jina katika neno la Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa kwa mujibu wa tamaduni za kibiblia, Majina hayakuwa yanatolewa kama jina tu, Majina yalikuwa ni tangazo linaloendana na tabia na mwenendo wa muhusika, majina yalikuwa ni picha halisi ya kinabii yenye kufunua kusudi la Mtu huyo kupewa jina, aidha majina pia yalikuwa yanatabiri kilele cha maisha ya mtu husika na wakati mwingine jina la mtu lilibadilishwa kwa kusudi la kubadilisha muelekeo wa maisha ya mtu huyo kutoka katika lile kusudi la kwanza la kupewa jina hilo, kwa mfano Mungu alipomuita Abrahamu, ambaye alikuwa anaitwa Abram alibadilisha jina lake hilo kuwa Abrahamu, Abram ikiwa na maana ya baba aliyeinuliwa, au mwana wa mfalme, na Abraham ikiwa na maana ya Baba wa Mataifa, au baba wa wafalme wengi, kwa hiyo Mungu alibadili jina la mwana wa mfalme, kuwa baba wa wafalme, Mungu alimpa jina linaloonyesha kuwa mwana mfalme huyu atakuwa ni baba wa wafalme wengi sana maarufu Duniani, Hali kadhalika Mungu alibadili jina la Sarai kuwa Sara.

Mwanzo 17:1-6 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako.”

Mwanzo 17:15-16 “Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake.”

Mungu alibadilisha jina la Abramu kuwa Abrahamu kwa sababu Mungu alikusudia kubadilisha mustakabali wa maisha ya Abrahamu na kumfanya kubwa Baraka kubwa kwa dunia ili kwamba kuputia yeye mataifa yote yaweze kubarikiwa, na kama mtu atakuwa kinyume na Abrahamu angeweza kumlaani naye angelaaniwa, kwa hiyo unaweza kuona jinsi maisha ya Abrahamu yalivyogeuzwa na Mungu kuwa maisha ambayo yanaweza kumgusa kila mtu duniani

Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Unaweza kuona, katika mpango huo huo wa kuleta Baraka kwa Dunia nzima Mungu alilazimika kubadili jina la Yakobo mjukuu wa Abrahamu kuwa Israel, ili kubadilisha mustakabali wa maisha ya Yakobo na kumbadilisha kuwa kitu kingine

Mwanzo 32:26-28 “Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.”

Kwa msingi huo utakubaliana nami kuwa ni ukweli usiopingika kimaandiko kuwa majina yalihusika kwa sehemu kubwa kuhusisha uweza wa Mtu tabia na mustakabali wa maisha yajayo, kwa hiyo kila mkristo anapaswa kukumbuka jambo hili kwamba tuwape watoto wetu majina mazuri kwaajili ya mustakabali mwema wa maisha yao ya baadaye na kamwe tusiruhusu wakawa na majina yenye kuwakilisha uchungu, au machungu ya maisha, hasa kama watoto hao hawahusiki na hilo walilolipitia wazazi, kwa mfano wakati Benjamin anazaliwa mama yake akiwa katika hali ya kufa alimpa jina Benon akiwakilisha mwana wa uchungu wake, lakini Yakobo alilibadilisha jina hilo mara moja jina likimaanisha mwana  wa mkono wake wa kuume ona:-

Mwanzo 35;16-18 “Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito. Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini.”

Katika hali kama hiyo majina ya Mungu katika maandiko yanafunua asili, tabia na uhusiano ulioko kati ya Mungu na wanadamu, Mfano mtu alipofadhiliwa na Mungu alimwita Mungu wa fadhili zangu Yehovah Yire, au mtu alipohakikishiwa Amani na Mungu alimuita Yehovah Shalom akikubali Amani ya Mungu, majina hayo sio tu yanamfunua Mungu bali yanatukaribisha kwake yakituonyesha kuwa Mungu anaweza kujitokeza kwetu pia sawasawa na mahitaji yetu, sasa jina la Yesu linafunua ufunuo mkamilifu wa Mungu kwa mahitaji yetu yote wanadamu kutokea upande wowote wa kiroho, nafsi, na mwili na kutufundisha au kutufunulia ukamilifu wote wa Mungu na kusudi lake kwa wanadamu.


Siri kubwa katika jina la Yesu.

Sasa tunapokuja kuangalia kuhusu jina la Yesu, utaweza kuona kuwa jina hili lilitangulia kutolewa kama zawadi kwa wanadamu wakati wa maandalizi ya kuzaliwa kwake yeye mwenyewe, jina hili lilikuja kama habari njema kwa Yusufu kuwajulisha watu wote Duniani kuwa mtoto huyu mwanaume ambaye tumepewa kama zawadi ukiacha shughuli zote za ukombozi na mafundisho yake yote jina lake tu ni msaada tosha kwa wanadamu na jina hili lilikuja vilevile wakati wa kuzaliwa kwake, kwa hiyo mojawapo ya zawadi kubwa kabisa katika siku za kuzaliwa kwa Masihi ni pamoja na jina lake ambalo ni jina lipitalo majina yote.

Mathayo 1:20-25 “Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.”

Jina Yesu kwaasili limetokana na jina “JESUS” la kiingereza ambalo lina mzizi mkuu kutoka katika lugha ya kilatini, na kwa kiyunani, “IESOUS” ambalo asili yake ni jina la kiibrania “yehōshuaYEHOSHUA au JOSHUA ambalo maana yake ni “MUNGU MWOKOZI” jina la Yesu lina maana pana katika kiibrania zinazojumuisha

Yeshua – yaani Mwokozi

Yoshua – yaani muunganiko wa maneno makuu mawili

·         Yah – ambalo ni kifupi cha neno la kiibrania ambalo lilikuwa katika mfumo wa herufi zisizo na silabii yaani Tetragrammaton zijulikanazo kama YHWH au YAHWEH

·         Yasha – ambalo maana yake wokovu au ukombozi Kwa hiyo jina la Yesu maana yake Yohova ni mwokozi,  kwa hiyo unapolitaja jina hili unaita mamlaka yote ya kiungu kwaajili ya kuleta msaada wa kiungu kokote uliko iwe ni mbinguni, duniani au kuzimu jina hili lina nguvu na mamlaka kubwa ya kusababisha ukombozi katika eneo husika, Mungu mwenyewe anashuka katika historia ya mwanadamu na kuukomboa uumbaji wake

Kwa hiyo jina la Yesu, linatimiza uhitaji mzima wa ukombozi wa mwanadamu ulioahidiwa katika agano la kale, kama Yoshua aliwaingiza wana wa Israel katika inchi ya mkanaani basi Yesu anawaingiza wanadamu wote duniani wamwaminio katika pumziko la uzima wa milele, kwa hiyo jina hili sio tu linawaokoa wanadamu na dhambi zao, bali pia na madhara ya dhambi, magonjwa na utumwa wa kila namna ambao wanadamu wanatumikishwa na zaidi ya yote kumkomboa mwanadamu na mauti ya milele, jina hili ni zaidi ya kazi za ukombozi, ni jina linaloachilia mamlaka ya kimbingu kushuka na kushughulika na mahitaji ya wanadamu duniani.

Luka 2:9-11 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”

Jina la Yesu haliondoi majina majina ya Mungu yaliyotumiwa wakati wa agano la kale lakini linayatimiza, wakati wa agano la kale Mungu alijifunua kidogo kidogo kwa vipande vipande kupitia jina lake mfano Yehova Rapha ilimaanisha, wokovu katika uponyaji, na Yehova Nisi ilimaanisha wokovu katika vita hivi vilikuwa ni vipande vipande vya ukombozi ambapo Mungu alijifunua kwa sehemu tu kulingana na uhitaji wa mtu kwa wakati huo, kwa hiyo ufunuo kuhusu jina la Mungu ulikuwa ni kwa sehemu, sivyo ilivyo katika jina la Yesu, hili linafunua wokovu kamili, ni kifurushi kamili chenye kujitosheleza katika nyanja zote, kama muumba, asili yake, wajibu wake kwa viumbe wake, na kadhalika kwa hiyo Yesu ni ufunuo kamili  wa Mungu.

Waebrania 1:1-4 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.”

Isaya 45:22-23 “Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.”

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Kwa msingi huo kila unabii katika Mungu uliotabiriwa katika agano la kale umekuja kutimizwa katika agano jipya kupitia jina la Yesu na kwa sababu hiyo tena hatuna jina lingine litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina la Yesu tu,

Matendo 4:10-12 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”


Amekirimiwa jina lile lipitalo kila jina

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, AKAMKIRIMIA JINA LILE LIPITALO KILA JINA; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Yesu Kristo sasa ni jina lipitalo majina yote kwa vitu vyote vya mbinguni na vya duniani na kuzimu neno LIPITALO katika kiyunani linatumika neno HUPER kimatamshi Hoo-per, huupa ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni Beyond across, Superior to more than, above, very chiefest, Exceeding, highly more than, very highly, jina lililo juu zaidi ya kawaida, Bora kupita yote, liko juu, la juu zaidi, limepitiliza kuliko kawaida, liko juu mno, Kwa hiyo nguvu iliyokuwa ikifunuliwa kupitia jina Yehova au Yahweh sasa inakaa katika Yesu kwa ukamilifu wake wote, bila kupuuzia majina ya agano la kale kuhusu Mungu, jina la Yesu sasa linabeba ufunuo mkamilifu wa mamlaka ya kiungu na wokovu wa mwanadamu kwahiyo ni kusema ukitoa pepo kwa jina la YEHOVA halitatoka lakini ukitoa kwa jina la Yesu litaondoka, jina hili hata shetani analijua, matumizi sahihi ya jina hili huwakilisha Serikali, ufalme, dola, mamlaka na utawala  na hivyo Pepo wakilisikia lazima wakimbie. Ni Mungu mwenyewe ambaye amempa Yesu jina hili na ametaka alitambulishe kwa wanadamu kwaajili ya kuwasaidia

Yohana 17:11-12 “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.”              

Jina la Yesu likitumika katika matamshi yoyote yawe ya Kiswahili, kiebrania, au kiyunani na kingereza nguvu yake inabakia vilevile halichuji endapo tu utamaanisha Yesu huyu wa Nazareth tunayehubiri habari zake jina hili lina nguvu, lina mamlaka, uwezo wa kuokoa na kufanya mambo makubwa unapoliitia maana yake unaiita serikali ya mbinguni kutoa msaada katika eneo husika

Jina hili linaokoa - Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”

Jina hili kanisa limeamriwa kuliamini – 1Yohana 3:23 “Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri.”

Jina hili lina mamlaka ya kuamuru lolote - Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Jina hili huitiwa na makanisa yote ya kweli – 1Wakorintho 1:2 “Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri.”

Jina hili lilitumiwa na mitume kuponya na kufanya miujiza mbalimbali.

Matendo 3:6, “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.”

Matendo 4:10 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.”

Jina hili mitume na kanisa la kwanza walilitumia katika kuhubiri

Matendo 8:12 “Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.”

Matendo 9:27-29 “Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua.”                    

Jina hili ni ulinzi na kimbilio – Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.”

Jina hili lilitumiwa na mitume kufukuza pepo wabaya.

Matendo 16:18 “Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.” 

Jina hili lilaleta Amani – Yohana 16:23-24 “Tena hsiku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”

Jina hili ni kibali cha kujibiwa maombi – Yohana 14:13-15 “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”

Jina hili Mitume walikuwa tayari hata kulifia

Matendo 15:25-26 “sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.”               

Matendo 21:12-13  “Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.”  

Jina hili linavuta uwepo wa Mungu – Mathayo 18:19-20 “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

Kwa hiyo watu wa Mungu tuna wajibu wa kulitumia jina la Yesu katika jambo lolote, najua yako mafundisho mengi duniani hata yale yanayofundisha watu kutumia damu ya Yesu na kuinyunyiza kwa Imani, maandiko yameelekeza katika changamoto yoyote ile tutumie jina la Yesu, Shetani asikudanganye kutumia kingine tumia jina la Yesu moja kwa moja, maandiko yametuagiza kulitumia katika maombi, kulitumia kwaajili ya uponyaji, kulitumia katika vita vya kiroho, na kulitumia katika kuabudu, tumeagizwa ya kuwa lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo tulifanye kwa jina la Yesu, tunapoliitia jina hili utendaji wa serikali ya mbinguni unahamia pale jina hili linapotajwa na kutimiliza matakwa yetu kwa utukufu wa Mungu, wajibu wetu ni kulitumia jina la Yesu kwa Imani, kwa heshima, kwa kulitumainia na kulitegemea, kwa kulitangaza kwa ujasiri, na kuishi sawasawa na heshima ya jina hilo, kwani jina hili ndio ufunuo mkamilifu wa upendo na wokovu wa mwanadamu kutoka kwa Mungu, jina hili lilifichwa nyakati za agano la kale na kufunuliwa kwetu wa kizazi hiki katika wakati huu wa neema hivyo ni zawadi ya kipekee ambayo hatuna budi kuitumia kwa mustakabali wa maisha yetu, unapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo basi kumbuka tumepewa jina kuu kuliko yote! Na ingawa amekirimiwa jina hili, kimsingi tumekarimiwa sisi kwa matumizi yake, kwa changamoto zozote zile unazokutana nazo katika maisha liitie jina la Yesu na utayafurahia maisha, omba kwa jina la Yesu, kemea kwa jina la Yesu, Amini  na ishi kwa  kulitegemea jina la Yesu.

Wakolosai 3:16-17. “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”

Maadui wa Yesu Kristo akiwepo shetani wakati wote hawatataka kulisikia jina hili likitumika na wakati wote watalikataa kama wanavyomkataa, Yesu Kristo mwenyewe, Shetani anatamani sana kama ikiwezekana jina hili lisiwepo au litumike lingine kwa sababu anaijua nguvu iliyomo katika jina hili. Nakusihi sana wakati huu tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kumbuka kuwa Mungu ametukirimia sio zawadi tu ya maisha yake ya ukombozi kwa wanadamu lakini ametukirimia pia jina hili zuri ambalo tunaweza kulitumia kwa mustakabali wa maisha yetu. Lakini hata manabii wa uongo watalitumia jina hili kwa kusudi la kuwadanganya wateule hivyo hatuna budi kuwa makini, si kila anayelitumia atakuwa ni mtu mzuri au mtu sahihi.

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”

Matendo 4:18 “Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.”

Matendo 5:40-42 “Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.”  

 

Na. Rev. Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Ijumaa, 20 Desemba 2024

Kuzaliwa kwa Masihi na utendaji wa Roho Mtakatifu.


Luka 1:31-35 “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”




Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa Neno la Mungu katika agano jipya limeonyesha wazi namna na jinsi Roho Mtakatifu akihusika kwa kiwango kikubwa sana katika mpango mzima wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, jambo ambalo linatupa kutafakari sana na kupata ufahamu kuwa huwezi kutenganisha habari nzima inayohusiana na kuzaliwa kwa Yesu Kristo na utendaji wa Roho Mtakatifu, Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni mojawapo ya muujiza mkubwa sana ambao unapita akili ya kawaida na utendaji mzima wa ufahamu wa kibinadamu, na Ndio maana hata kitendo cha Mariamu kuwa mjamzito bila tukio la mwanaume kuhusika Malaika alifafanua wazi kuwa ingewezekana kwa uweza wa Roho Mtakatifu, hii maana yake ni kuwa kulikuwa na utendaji wa kiungu uliokuwa unahusika moja kwa moja katika kumleta masihi Duniani. kwa hiyo tunaposheherekea wakati wa kuzaliwa kwa masihi tusimsahau ROHO MTAKATIFU.

Mathayo 1:18-21 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba KWA UWEZA WA ROHO MTAKATIFU. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni KWA UWEZA WA ROHO MTAKATIFU. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”

Hii maana yake ni nini? mpango mzima wa ukombozi wa Mwanadamu ni muujiza ambao umeratibiwa na Roho Mtakatifu kwa muujiza mkubwa sana. Roho Mtakatifu ni wa muhimu mno na anahusika kwa namna ya kipekee katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu kwa sababu hata kuzaliwa kwa Mkombozi mwenyewe tunamuona Roho wa Mungu akihusika katika muujiza huu mkubwa wa kuunganisha kazi za uungu na ukombozi wa Mwanadamu, kwa muujiza mkubwa wa Mungu kufanyika mwanadamu, au mwana wa Mungu kuwa mwana wa mwanadamu ili kuleta ukombozi wa mwanadamu, ikiwa ni hivyo basi ni muhimu kufahamu kuwa tunaweza kufurahia wakati huu wa msimu wa kuzaliwa kwa Masihi kwa kukubali pia utendaji mzima wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni sehemu ya Utatu wa Mungu, na kwa sababu hiyo, tnaposhangilia kuzaliwa kwa Yesu ambaye ni mkombozi wa ulimwengu tunakumbushwa kuwa Utatuwa Mungu yaani Baba na Roho Mtakatifu ulihusika katika mpango wa kumleta Mungu mwana duniani, Tutajifunza somo hili zuri kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa Masihi

·         Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya masihi

·         Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe

Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa Masihi

Roho Mtakatifu anaonekana kuhusika na ujio mzima wa masihi na maandalizi yake, Kumbuka nabii Yoeli alitabiri kuwa siku za mwisho Mungu angemuachilia Roho wake Mtakatifu kwa wote wenye mwili, kwa hiyo siku za mwisho zinaanzia katika msimu wote wa kuzaliwa kwa Masihi na mpaka atakapokuja mara ya pili katika utawala wake wa miaka 1000 duniani, yaani millennium ambako umwagiko huo utakuwa katika ukamilifu wake au utakuwa katika kilele chake.

Yoeli 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”

Roho Mtakatifu alihusika vipi katika maandalizi mazima ya kuzaliwa kwa masihi?

-          Alihusika katika muujiza mzima wa kutungwa kwa mimba katika tumbo la Mariamu  kwa hiyo tendo zima la Mariamu kupokea ujauzito liliratibiwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu

 

Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”

 

-          Alihusika Katika kumjaza nguvu akiwa tumboni Mtangulizi wa Masihi yaani Yohana Mbatizaji Luka 1:13-16 “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.”

 

-          Alihusika katika kuwaongoza watu waliokuwa wakimsubiria na kuona ahadi ya Mungu ikitimizwa katika maisha yao Luka 2:26-30 “Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako

 

-          Athari za utendaji wa Roho Mtakatifu katika kuzaliwa kwa masihi kunasababisha azaliwe mtu ambaye uungu unakaa ndani yake na kwa sababu hiyo nguvu ya dhambi isingelimuweza, kwa sababu huyu aliyezaliwa angekuwa ni mwana wa Mungu na hii ingeweza kumtofautisha na mwanadamu wa kawaida ambaye asili yake ni Adamu, ambaye asili yake ni udongo, wakati Yesu Kristo asili yake ni ya mbinguni.

 

1Wakorintho 15:47-48 “Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.”

 

Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

 

Kitendo cha Yesu Kristo kuzaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kimemfanya kuwa mwanadamu mwenye asili ya mbinguni na kwa sababu hiyo dhambi haingelimuweza na kupitia maisha yake ya ushindi dhidi ya dhambi angeweza kuwa msaada kwa wanadamu wote, Na kwa kufanywa mwenye dhambi ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu kupitia yeye hivyo haya yasingeliwezekana kama sio kazi za Roho Mtakatifu.

 

2Wakorintho 5:21 “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” 
    

Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya Masihi

Roho Mtakatifu anaonekana katika maisha na huduma ya Yesu Kristo kuanzia ubatizo wake mpaka kupaa kwake Mbinguni pamoja na ahadi aliyoitoa ya ujio rasmi wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wake na sisi sote tuaminio.

-          Wakati Yesu anabatizwa Roho wa Mungu alishuka juu yake  Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

 

Hii ilikuwa ni alama ya kupakwa mafuta kwa mtu huyu aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu sasa anaanza kutumikia kusudi la baba yake, na baba anampaka mafuta kwa Roho wake Mtakatifu ili sasa aweze kuwa kuhani, nabii na mfalme kwaajili ya kuwakomboa wanadamu, uwezo wake wa kufundisha, kuhudumia watu, kufanya miujiza na kila kitu alikifanya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu huku maisha yake yakiongozwa na Roho, kwa hiyo

 

a.       Aliongozwa na Roho MtakatifuMarko 1:12-13 “Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.”

 

b.   Alifanya huduma zote za kuwafungua watu kama matokeo ya Roho Mtakatifu kuwa juu yake – Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

 

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”

 

c.     Alitoa Pepo kwa Chanda cha Mungu yaani kwa uwezo wa Roho MtakatifuLuka 11:20 “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

 

Mathayo 12:28 “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

 

d.      Nguvu wakati wa kusulubiwa – Roho Mtakatifu aliyehusika katika kuzaliwa kwa Kristo, kubatizwa na kumuongoza na kumtumia katika huduma zake duniani alimtia nguvu vilevile katika huduma yake ya kuukabili Msalaba kwaajili ya ukombozi wetu, alikwenda Msalabani kwa upako ule ule uliomuwezesha kufanya huduma nyingine, Roho alimpa ujasiri, upendo na uvumilivu kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu ili kuyatimiza mapenzi ya Mungu, bila uweza wa Roho Mtakatifu uwezo wa kuvumilia mauti ya msalaba ambayo kwa asili ilikuwa ni mauti mbaya na ya aibu isingeliwezekana au kuwa jambo jepesi.

 

Luka 22:41-43 “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”

 

Waebrania 9:13-14 “Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

e.     Wakati wa kufufuka kwake  - Roho Mtakatifu anatumika pia kama muhusika mkuu wakati wa kuurejesha uhai wa Yesu Kristo, yaani swala zima la kufufuka kwa Yesu Kristo maandiko yanasema Roho Mtakatifu alihusika katika kumfufua Yesu Kristo

 

Warumi 1:3-4 “yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;”

       

Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”        

Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe

Maisha yako wewe na mimi hayawezi kuwa na ukamilifu bila kazi za Roho Mtakatifu kufanyika ndani yetu, Kristo alisema sisi hatuwezi kufanya neno lolote pasipo yeye hii ni Dhahiri kuwa kama Yesu Kristo Mwana wa Mungu alimtegemea Roho Mtakatifu katika maisha yake yote na utumishi wake na uvumilivu wake na kila kitu, ni Dhahiri kuwa, maisha yetu Bila Roho Mtakatifu na kazi zake katika maisha yetu itatufanya tuwe watu wasio na faida maana imeandikwa wala si kwa uweza wala kwa nguvu Bali kwa uweza wa Roho Mtakatifu  yeye ndiye anayetupa uwezo wa kufanya jambo lolote kwaajili ya Mungu.

Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.”

Yohana 16:7-11 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”

Roho Mtakatifu ni msaada ulio karibu katika maisha yetu – Yohana 14:26Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”           

Roho Mtakatifu ni Msaada katika maombi – Warumi 8:26-27Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.”      

Roho Mtakatifu hututia nguvu – Matendo 1:4-8Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”              

Roho Mtakatifu hutupa karama za Rohoni – 1Wakorintho 12:4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.”

Tunaweza kufaidika na maswala yote ya kiroho endapo tu Roho Mtakatifu atakuwa pamoja nasi atatusaidia katika ujuzi, hekima, maarifa na kutuwezesha kutenda mambo kwa uhodari tukiwa na Roho Mtakatifu. Najua wakati huu wa msimu wa sikukuu kuna maswala mengi sana na mada nyingi zitazungumzwa lakini mimi niliongozwa kuwakumbusha watu wote kuwa kuzaliwa kwa masihi nyuma yake uko uratibu mzima wa Roho wa Mungu na kwa sababu hiyo ni vema tukashughulika na Kusheherekea sikukuu hii huku tukijikumbusha kuwa ni kazi zipi Roho wa Mungu anazifanya ndani mwetu je kuna uhai katika maisha yetu? Kuna uhai katika kanisa la Mungu? Iwapo tunataka kufurahia msimu wa sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa furaha ya kweli kutoka mbinguni furaha hiyo itakamilishwa ndani yetu endapo tutaitumia nafasi hii kutafakari na kutubu, na kumuomba Mungu asituondolee Roho wake Mtakatifu, sikukuu ya kuzaliwa kwa masihi itakuwa tamu kama wanadamu watajiandaa kuzaliwa kwa Roho na kijazwa kwa Roho Mtakatifu.

Na. Rev Innocent Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima