Ayubu 14:5 “Kwa kuwa siku zake zimeamriwa,
hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;”
Utangulizi:
Kumekuwepo na mijadala
mbalimbali, mitazamo na falsafa kuhusu kifo!, Baadhi wakiamini kuwa kila kifo
ni mapenzi ya Mungu, wengine wanaamini kama Mungu akiamua usife huwezi kufa na
akiamua ufe unakufa, na wengine wakiamini kuwa kila mwanadamu ana siku zake
zilizoamriwa kuishi duniani na zikikamilika anaondoka, wengine wanaamini kuwa
Mungu huwa anahuzunika sana mtu anapokufa kama sisi nasi tunapohuzunika matukio ya kifo
yanapotokea, lakini kwa sababu tunaishi katika ulimwengu wa dhambi Mungu
huruhusu kifo kutokea Ni muhimu kufahamu kuwa ni neno la Mungu pekee yaani
Biblia inayoweza kutupa majibu ya maswali yetu kuhusu kifo na maana halisi ya
kifo kinapotokea! Lakini ni lazima kwanza tufahamu kuwa Mungu hapendi kuwatesa
wanadamu wala kuwahuzunisha ona
Maombolezo
3:31-33 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.
Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana
moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.”
Kifo katika mpango wa Mungu!
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
katika mpango wake hakuwa amekusudia kifo kiwepo katika maisha ya mwanadamu, na
ndio maana kwa asili hakuna mwanadamu anayekubali au kukipenda kifo kwa sababu
kimsingi sio maumbile ya asili yetu Mungu alimuumba mwanadamu ili aishi milele
na ndio maana kifo kimekuwa kinampa taabu sana mwanadamu kwa maana haukuwa
mpango wala mapenzi kamili ya Mungu
Muhubiri 3:10-11 “Nimeiona taabu ambayo Mungu
amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa
wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi
mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata
mwisho.”
Kifo na taabu zake kimekuja kama matokeo ya kuasi kwa
mwanadamu, kwa hiyo Mungu alimuwekea mwanadamu uchaguzi kuchagua uzima au mauti
kupitia kutii au kuasi na kwa bahati mbaya mwanadamu akaasi na hapo ndipo
ilipokuja adhabu ya kifo ambayo Mungu alikuwa amemuonya nayo Adamu ona
Mwanzo 2:15-17 “BWANA
Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza
kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku
utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”
Kwa msingi huo kifo
kipo Duniani leo kwa sababu ya kuasi kwa mwanadamu mmoja baba yetu Adamu na
mama yetu Eva kwa sababu sisi tulikuwa viunoni mwao wakati wana wanaasi na kwa
sababu hiyo wanadamu wote wanaonja mauti ona
Warumi 5:12 “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja
dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti
ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;”
kwa hiyo
kifo kiliingia ulimwenguni kwa sababu ya dhambi na kikawafikia watu wote kwa
nini kwa sababu wote tulikuwa katika viuno vya wazazi hao kwa msingi huo tuwe
wema au tuwe waovu ni lazima tutaionja mauti, Kama mwanadamu hangelifanya
dhambi, muda wetu wa kutimiza makusudi ya Mungu Duniani ungekuwa kama
umekamilika Mungu angetutwaa kwenda mbinguni kukaa naye bila kuonja mauti ona
Mwanzo 5:24 “Henoko
akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa
.” Huu
ndio ulikuwa mpango kamili wa Mungu
(Perfect will of God), kwa msingi huo kifo sio mpango kamili wa Mungu bali
ni matokeo ya dhambi ambayo yameruhusiwa na Mungu
(permissive will of God).sasa
kifo kimekuwepo na Mungu aliandaa mpango mwingine wa kukikomesha wakati wa
utimilifu wa dahari utakapowadia.
Je kila kifo
kinachotokea ni mpango wa Mungu?
Swali hili linaweza kuwa na
majibu NDIO na HAPANA kulingana na mazingira ya kifo chenyewe kwa mujibu wa neno
la Mungu sio kila kifo kinachotokea ni mpango wa Mungu wala sio mapenzi yake
kamili, Maandiko ynashuhudia wazi kuwa Mungu hapendi wala hafurahii kufa kwake
mtu mwenye dhambi! Ona
Ezekiel 33:11 “Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU,
SIKUFURAHII kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake
mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka
kufa, Enyi nyumba ya Israeli? ”
kwa hiyo kumbe linapokuja swala la
Mtu kufa Mungu hapendi afe mtu mwenye dhambi, Mungu hafurahii kufa kwake mtu
muovu, Mungu anatamani mtu awe ametubu, awe amegeuka na kuacha njia mbaya kabla
ya kifo ili waweze kuungana naye, haya ndio mapenzi kamili kwa kila mwanadamu
na ndio maana wakati mwingine Mungu huwaacha waovu kwa kitambo na kuwavumilia
ili yamkini ikiwezekana wafikie wakati wa kutubu ona
2Petro 3:9 “. Bwana hakawii kuitimiza ahadi
yake, Kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana HAPENDI
mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.
kwa hiyo Mungu
hapendi, na hafurahii na hivyo kuna nyakati huwacheklewesha waovu wasife kwa
haraka au wasife kabla hawajafikia toba, kwa hiyo kuna mazingira ambayo kwayo
Mungu hatafurahia au hafurahii kufa kwa mtu hususani mtu mwenye dhambi. Kwa
hiyo Mungu husubiri mtu aifikie toba mtu ageuke na kuiacha njia yake mbaya
Hata hivyo kifo ni kanuni, ni kanuni
ya adhabu kwa kitokumtii Mungu, kifo kama kanuni ya adhabu ya kutokumtii Mungu
ni hitimisho la hatua kadhaa zisizochukuliwa katika hatua ya dhambi, angalia
andiko hili kwa mfano
Yakobo 1:14-15 “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku
akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi,
na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”
Kanuni ya kifo ni dhambi
kuna namna ambavyo Mungu katika hekima yake anakiruhusu kifo kwa nafi yenye
dhambi, japo kifo sio mapenzi yake kamili lakini ni mshahara wa dhambi kwa hiyo
kama nafsi itajaribiwa dhambini na kukawia kufanya toba na kwa bahati mbaya
hatuwezi kujua muda ambao Mungu anatupa wa toba kanini ya kifo ambayo ni dhambi
ikikomaa inaleta mauti kwa hiyio Mungu pia huruhusu mtu kufa endapo nafsi ya
mtu huyo itatenda dhambi ona mfano
Ezekiel 18:20-23 “Roho itendayo dhambi, ndiyo
itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa
mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu
utakuwa juu yake. Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote
alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki,
hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake
hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa
kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia
yake, akaishi?”
Unaona hivyo basi kutokana na kanuni Fulani za
dhambi zinapoendelea kutendwa na nafsi basi Mungu huweza kuruhusu Dhambi hiyo
kusababisha kifo na kukatiza uhai wa nafsi husika kwa ain azote za uzima huu na
ule ujao
Kutoka 21:14,-16 “Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi
apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe. Ampigaye
baba yake au mama yake, sharti atauawa.Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au
akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo” Katika mazingira
kama kifo kinachotokea hapa ni mpango wa Mungu katika mantiki kwamba uovu
umepelekea kufa, tama imepelekea nafsi itendayo dhambi kufa, kwa hiyo sio
mapenzi ya Mungu mtu kufia katika dhambi, lakini ni mwanadamu anapokuwa na
ukaidi Fulani kinyume na amri za Mungu mungu huruhusu mtu huyo kufa. Kwa hiyo
yako mazingira jibu linaweza kuwa ndio na yako mazingira jibu linaweza kuwa
sio!
Kwa mfano sio mapenzi ya Mungu
kwa watoto wasiowahehimu wazazi wao kufa kabla ya wakati ona Waefeso 6:1-3 “Enyi
watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba
yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae
siku nyingi katika dunia.” Kumbe ni mapenzi ya Mungu kwamba watoto
wawaheshimu wazazi wao ili siku zao zipate kuwa nyingi tena na za heri duniani,
Lakini mtoto ambaye atamlaani baba yake au mama yake Mungu ameamuru apigwe kwa
mawe mpaka kufa, kwa lugha nyingine maisha ya mtoto asiyewaheshimu wazazi
yatafupishwa
Kutoka 21:15, 17 “Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. Yeye
amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.” kwa hiyo ni wazi
kuna mazingira ya aina fulani Mungu hataki mtu afe kwa dhambi na kuna mazingira
fulani Mungu huruhusu mtu afe kwa sababu ya dhambi.
Je Mungu hujisikiaje wanapokufa watu wengi?
Swala lingine nyeti ni je Mungu
hujisikiaje wanapokufa watu kwa wingi? Kimaandiko bado Mungu huuzunishwa sana
wanapokufa watu wengi wakiwa dhambini, Mungu huuzunishwa dhambi inapozidi na hivyo
huweza kuruhusu maangamizi mfano
Mwanzo
6:5-7 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni
makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu
sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika
moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi;
mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya
kwamba nimewafanya.”
Wakati wa Nuhu Mungu aliufutilia ulimwengu kwa
gharika kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, kimsingi Mungu hafurahii udhalimu
na uovu unaofanywa na watu, hapendi watu wafe lakini dhambi hupelekea Mungu
kuruhusu vifo.
Dunia inaweza kukabiliwa na
majanga kama watu hawatatubu, mji au nchi au taifa kama halitamjali Mungu Mungu
anaweza kuachilia roho ya mauti ikafanya kazi yake na kuleta madhara kwa watu
wema na wabaya wote wakaathirika kutokana na ule ukaidi wa kibinadamu wa kufa
kwa dhamiri na kutaka kuendelea kuishi katika maisha ya dhambi ona
Mwanzo 18:20 “BWANA
akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao
zimeongezeka sana,”
Dhuluma na uharibifu wa dhambi uliofanywa na
watu wa Sodoma na Gomora ulimsukuma Mungu kuruhusu miji hiyo kuangamizwa kwa
wingi wao, Kimsingi watu wengi wa mji au taifa wanapomgeukia Mungu na kuomba
rehema zake kwa toba na kuacha njia yao mbaya Mungu huwarehemu watu hao ona
Yona 3:11-10 “Neno
la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule
mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi,
kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo
wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti
yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi
wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye
aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye
akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za
magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika
mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu,
wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala
wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao
wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya,
na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na
kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? Mungu akaona matendo
yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya,
ambalo alisema atawatenda; asilitende.”
Ni wazi kuwa Ninawi ulikuwa mji mkubwa
yaani wenye watu wengi na waliishi maisha ya dhambi na dhambi hiyo ilifikia
mstari wa kuwaletea mauti lakini walipogeuka na kutubu Mungu aliwasamehe na
kifo kikaahirishwa kwao, hii ni ahadi ya Mungu kwa miji yoye, nchi zote na
mataifa yote ya kuwa watu wafikilie toba na kuwa watu wakigeuka kuacha njia zao
mbaya Rehema za Mungu zitakuwa juu ya watu hao ona
2Nyakati 7:13-14 “Nikizifunga mbingu isiwe
mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa
watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na
kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na
kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” Kumbe basi yanapotokea
majanga ya aina mbalimbali, na matukio yenye kuua watu wengi na matukio mengone
ya asili yanayodhuru wanadamu na kuumiza wengi haimaanishi tu kuwa watu wale
wanaweza kuwa waovu kuliko wale wanaobaki salama lakini kwa Mungu wakati wote
matukio hayo yanakuwa ni wito wa toba kwa watu wote wapate kumgeukia Mungu ona
Luka 13:1-5 “Na
wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao
Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani
ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata
wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote
mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko
Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote
waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia
vivyo hivyo.”
Kwahiyo hata yanapotokea majanga katika upande wa
Mungu inabaki vilevile Mungu hafurahii kufa kwa wenye dhambi na angepeda
wafikie toba lakini ni wazi kwetu kuwa yanapotokea majanga na kuchukua watu
wengi, sisi tunaosalia hatuna budi kukaa katika toba na kuacha njia mbaya
tukikumbuka kuwa wale walioangamia sio kuwa walikuwa wabaya kuliko sisi.
Heri wafu wafao katika Bwana !
Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka
mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema
Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.”
Kifo ni jambo la kuhuzunisha sana
lakini ni tamko la Mungu, kwa hiyo Mungu hawezi kuwa kinyume na neno lake kwa
sababu hiyo kifo kitamchukua mtu awaye yote mwema au muovu, kwa wakati wake
ambao Mungu ameukusudia chini ya Mbingu, Yesu alipokuwa duniani alidhihirisha
kuwa anahuzunishwa na kufa mtu tena hata wale waliokuwa rafiki zake ona Yohana 11:35 “Yesu
akalia machozi.” Yesu alilia kwa sababu alihuzunishwa na kifo cha
mtu wa karibu na rafiki yake yaani maana yake anahuzunishwa na kila mtu
anayemuamini na anayeishi maisha ya haki bila kujali mtu huyo amekufa katika
umri wa namna gani. Lakini Maandiko yanaeleza kuwa Heri wafu wafao katika Bwana
yaani bila kujali umri au miaka lakini kama mtu huyo amekufa akiwa na imani
katima Mungu akiamini kuwa yesu ni Bwana mtu huyo ana Baraka kubwa sana na
maandiko yanaonyesha kuwa anapata pumziko baada ya taabu
Kwa sili andiko hilo ni matokeo
ya maonyo kwa watu waovu ambao maandiko yanaonyesha kuwa wao wanapokufa
hawatakuwa na nafasi ya kupumzika na badala yake watapata taabu sana Ufunuo 14:11 “Na
moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana
wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa
ya jina lake.”
Maandiko hayo yanaonyesha kwa asili wale watakaokufa
wakati wa dhiki kuu, na tofauti yake kati ya wale watakaokufa kwa imani na wale
watakaokuwa wamemuabudu mpinga kristo, Lakini maandiko hayo kuwa katika
muktadha wa nyakati za dhiki kuu, hayaachi uole ukweli ulio wazi wa hata sasa
kwamba wale wanaomuamini Yesu watapata raha na wale wasiomuamini watapata taabu
sana kwani hayo ni matokeo yanayotokea haraka sana mara mtu anapokufa na aina
ya maisha aliyoishi huamua hatima ya maisha yake ya umilele mara moja baada ya
kufa ona Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada
ya kufa hukumu;” Maandiko ynaonyesha wazi kuwa mara baada ya kufa
hukumu hujitokeza pale pale kwa aidha kwenda katika raha au kwenda katika
mateso mtu aliyemuamini Bwana Yesu anasamehewa na kuwanywa kuwa kiumbe kipya 2Wakoritho 5:17 “Hata
imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita
tazama! Yamekuwa mapya.” Watu hawa ambao neema ya Mungu imefunuliwa
kwao watapata raha nafsini mwao kama maandiko yasemavyo Mathayo 11:28-29. Kwa hiyo anapokufa mtu mcha Mungu Mungu hufurahia
anahuzunika anapoona wale walioko duniani wanalia na wanahuzunika na huhuzunika
pamoja nao lakini mtu wa Mungu anapokufa kuna faidha kubwa sana na Mungu
hufurahia mauti yake maandiko yanatuambia ina thamani kama nini mauti ya wacha
Mungu wake ona Zaburi 116:15 “Ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake.”
Haijalishi mtu wa Mungu atakufa katika mazingira ya aijna gani vyovyote
vile kama Mungu ameruhusu mauti hiyo ina thamani kubwa sana mbele za Mungu
aliyekuwa Askofu wa Antiokia aliuawa wakati wa mateso ya Decian askofu huyu
ambaye katika historia ya kanisa aliitwa Babylas alikufa akiwa anaimba zaburi
hii ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake!, Mtume Paulo
aliungana na wazo kama hili kuhusu mauti ya mtu wa Mungu yeye alihesabu hivi
kwake yaani kwa mtu kama yeye kuishi ni Kristo na kufa ni faida ona
Wafilipi 1:21-24 21. “Kwa maana
kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili,
kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa
katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni
vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu”
kumbe basi kufa katika imani kwa mtu wa Mungu na kwa watu wema ni busara ya
Mungu ambaye anakwenda kuwapumzisha na kukaa pamoja na wao, bila kujali ni
mazingira gani anakuchukua nani katika umri gani anakuchukua kwa msingi huo kwa
uelewa mwembamba kifo ni kupoteza katika akili za kibinadamu na hasa anapokufa
mtu mwema lakini kwa uelewa mpana kifo cha mtu mwema kina thamani kubwa sana
kwa Mungu, Mara kadhaa wakati mwingine nimeshangazwa na Kocha wa mpira wa miguu
anaweza kumtoa mtu ambaye amefunga magoli mengi siku hiyo au mwenye uchu wa
kufunga zaidi, na ukatamani aendelee kucheza kwa vile unakuwa na matumaini naye
lakini unashangaa kocha anamtoa! Unaweza kumtukana au kumlaumu lakini kwa nini
anatolewa kocha ndiye anayejua Katika Biblia kama kuna mtu binafsi
nisingelipenda Mungu amchukue Mapema ni Stefano mimi nahizi kuwa angakuwa
muhubiri mkubwa na alikuwa ni mtu muhimu, mitume walimtegemea sana na alikuwa
na uwezo wa juu sana kulitetea kanisa lakini Mungu kama Mungu aliruhusu Stefano
auawe kwa kupigwa mawe na kuwa mtu wa kwanza kuifia Imani, hivyo wakati
mwingine Mungu hufanya mambo kama apendavyo yeye na hata hivyo wanatheolojia
wanajua faida ya kifo cha Stefano lakini pia tunaijua Furaha ya Yesu
aliyesimama kumpokea Stefano!
Je mtu akifa ni kweli kuwa siku yake imefika?
Tumewasikia watu mara kadhaa
wakisema mara baada ya mtu kufa kuwa siku yake imefika, au amemaliza kazi
iliyokusudiwa au siku yako ikifika bwana hakuna cha kuzia na kadhalika na
kadhalika je Mungu amekusudia mwanadamu awe na wakati Fulani muafaka wa kuishi?
Je kuna uwezekano wa siku kufupizwa au kuongezwa na nini faida zake na makusudi
yake? Maandiko yanatufundisha wazi kuwa kwaajili ya dhambi umri wa kuishi
mwanadamu umefupizwa ona Mwanzo 6:1-3 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa
kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni
wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu
haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake
zitakuwa miaka mia na ishirini.”
Mwanzoni wanadamu waliweza
kuishi hata karne 9 yaani miaka mia tisa na kitu na mwanadamu aliyepata kuishi
miaka mingi zaidi aliitwa Methusela yeye aliishi miaka 969 katika rekodi za
Biblia ona Mwanzo 5:27 “Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda na sitini na
kenda, akafa.” Kutokana na kuongezeka kwa maasi duniani Mungu
aliipunguza miaka ya kuishi mwanadamu na kuwa 120 kama tuonavyo katika maandiko, hivyo 120 ndio kiwango cha wastani wa juu zaidi ambao mwanadamu anaweza
kuishi, Wakati wana wa Israel wakiwa Jangwani kutokana na kuasi kwao mara kwa
mara Mungu aliwapunguzia wao wana wa Israel Miaka ya kuishi hususani wale
walikuwa jangwani wakati wa Musa na miaka yao ikakadiriwa kuwa kati ya
70-80 ona Zaburi 90:10 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu
miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi
tukatokomea mara.” Musa aliyasema maneno hayo wakati wa hukumu ya
wana wa Israel ambao walikuwa wanakufa jangwani kwa sababu ya kutokumuamini
Mungu, lakini kibiblia swala la msingi linabakia kuwa wastani wa mwanadamu
kuishi ni kati ya miaka “70-120” hata
hivyo hii haimaanishi kuwa ni lazima mwanadamu afiikishe miaka hiyo au kwamba
anayekufa chini ya umri huo ni muovu hapana hata kidogo bado maisha ya
mwanadamu yanabaki kuwa katika mipaka aliyoiweka Mungu! Kama itafikiriwa kuwa
mtu akifa chini ya umri huo amekufa kijana basin i vema kuyafikiri maisha ya
Yesu ambaye alipokuwa duniani aliishi miaka 33 tu, au kufikiri maisha ya Nabii
Yohana mbatizaji ambaye aliishi miaka 30 tu na akauaawa! Ni Mungu tu ndiye
anayejua kwanini na lini kifo kitokee kwa mtu kwa sababu zake mwenyewe, siku za
mwanadamu za kuishi kwa ujumla sio nyingi kama hata kama mtu ataishi 120 bado
ni siku zenye kupita haraka mno. Kwa mujibu wa maandiko
Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na
mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama
vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe”
mwandishi mwingine wa Biblia anayafananisha maisha ya mwanadamu kama vile maua,
maua na majani ndio mfano wa vitu vyenye muda mfuoi sana wa kuishi, ni kama
wanasema muda tuliopewa ni mdogo sana ona
Zaburi
103:15 “Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua
la kondeni ndivyo asitawivyo.” Pia maisha ya mwanadamu
yanafananishwa na kivuli yaani kitu kinachopita na kutoweka kwa haraka sana Zaburi 144:4 “Binadamu
amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.”
Katika
namna ya kibinadamu wengi tunaweza kufikiri kuwa maisha ya duniani ni matamu
sana lakini kwa Mungu katika uwepo wake ndio kuzuri zaidi, Mungu amepangilia na
kuweka mipaka katika maisha ya mwanadamu kwamba ukifika wakati huo aliouweka
mwanadamu ataondoka tu kwa sababu siku zake zimeamriwa zimeratibiwa ziko
programed kwamba huyu zitakuwa hizi tu
Ayubu 14:5 “Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu
ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;”
kwa hiyo iko wazi kuwa Mungu ameweka mpaka katika maisha yetu ambao huo
hatuwezi kuuvuka iwe tuna pesa kiasi gani, wema kiasi gani na kadhalika aidha
pia Mungu huweza kuitimiza ile iliyokusudiwa au kuipunguza maika iliyokusudiwa
kwa wanadamu kwa sababu zake na kanuni zake mfano
Kutoka 23:25-26 “Nanyi mtamtumikia BWANA,
Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea
ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika
nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.” Aidha Mungu anaweza
kuhakikisha kuwa miaka iliyokusudiwa kwa mtu inatimizwa au anaweza kuiongeza
lakini pia anaweza kuipunguza kutokana na kanuni mbalimbali za maisha na neno
lake mfano Mithali 10:27 “Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio
haki itapunguzwa.”
Kila
mwanadamu anatamani sana kuishi muda mrefu sana lakini wakati mwingine Mungu
hutuepusha na mambo kadhaa na dhiki au mambo mabaya ambayo yeye hangependa
ukumbane nayo Hezekia alikuwa moja ya wafalme wazuri ambaye Mungu alitaka
kumchukua mapema lakini aliomba Mungu amuongezee muda wa kuishi na Mungu
alimuongezea muda wa miaka 15 2Wafalme
20:1-6 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika
hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema
hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia
akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema,Nakusihi,
Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo
mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.
Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema,
Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako
asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama,
nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana. Tena, nitazizidisha siku
zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na
mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa
ajili ya Daudi, mtumishi wangu.”
Hata hivyo jambo la kushangaza ni
kuwa baada ya miaka hiyo ya nyongeza Hezekia alipata mtoto na ambaye
aliwaongoza watu kufanya mambo mabaya sana na kufanya machukizo mabaya zaidi
ambayo hata baba yake angalikuwa hai asingeliweza kuyavumilia mauozo hayo ona 2Wafalme 21:9 “Walakini
hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana
aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.”
Ni kama kusema afadhali
Hezekia angelikubali kwenda kwa bwana wakati wake ulipofika kuliko miaka
aliyoongezwa. Wakati mwingine Mungu
katika hekima yake hufanya mambo kwa manufaa makubwa sana anayoyajua mwenyewe
kwaajili ya hayo ni vigumu kumuuliza Mungu kwanini, kwanini hili litokee,
lakini tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo na kutokumkufuru Mungu
linapofanyika tukio lenmye kushangaza tuendelee kumuamini yeye katika njia zake
zote na tusizitegemee akili zetu wenyewe
Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote,
Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye
atayanyosha mapito yako.” Wakati mwingine Mungu anaweza kumchukua
mtu mwema akapumzike nyumbani kwa kusudi la kumuepusha na machukizo ya aina
Fulani bila kujali njia itakayotumika kwa kuondoka kwake,
Isaya 57:1 “Mwenye haki hupotea, wala
hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya
kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.” Mungu anaweza
kumchukua mtu ili kumuepusha na mabaya au maumivu makali au ulemavu, au kupooza
na maswala mengine mengi,Jambo kubwa la msingi ni kila mmoja kuwa tayari kwa
kifo wakati wowote tangu siku unapozaliwa
Hata hivyo Yesu Ndiye mwenye funguo yaani mamlaka na kifo na hivyo hutaweza
kuondoka mpaka Mungu ameruhusu Shetania anaweza kutujaribu kwa kiwangochochote
kile lakini hana ruhusa kuondoa uhai wetu mpaka Mungu mwenyewe afanye hivyo
Ayubu 2:6 “Bwana
akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake”
Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka
miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu,
akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa
nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti,
na za kuzimu.”
Adui wa mwishio atakayeangamizwa ni kifo:
1Wakoritho 15:26 “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti” Hatimaye
Yesu Kristo ambaye ana mamlaka dhidi ya kifo na mauti na ambaye alionja mauti
ya msalabani na kuishinda kwa kufufuka siku ya tatu mwisho wa dahari atambatilisha
adui huyu ambaye amekuwa akisumbua kili zetu na kutuchukulia wapendwa wetu na
kutuondolea tumaini duniani na kutufanya tuione dunia kuwa haina maana na ni
batili na kutukatisha tamaa na kutufanya tuishi kwa hofu, habari njema ni kuwa Mungu ataibatilisha mauti
yaani kifo na hakitakuwepo tena mjadala wake utafungwa na Mungu mwenyewe kwa
kutupa uzima wa milele na kujibu maswali yote ya msingi kuhusu Kifo, kwa sasa
kifo ni siri ya ajabu, na Mungu ndiye aijuaye.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!