1Wafalme 1:1 – 4 “Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao
wakamfunika nguo, lakini asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia,
Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya
mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi
wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi,
Mshunami, wakamleta kwa mfalme. NAYE KIJANA HUYO ALIKUWA MZURI SANA; akamtunza
mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.”
Utangulizi.
Ni muhimu kwetu kuwa na ufahamu
ya kwamba uko uhusiano mkubwa sana wa uzuri na ulimwengu wa roho, kuwa mzuri
pekee bila kuwa na hamu ya kumpenda Mungu,
au kuwa na tabia ya kumcha Mungu kunauweka uzuri wako katika hatari
kubwa sana ya kushambuliwa kiroho na ulimwengu wa kiroho wa shetani na kukuweka
katika matumizi ya haribiko kubwa la mwili wako na roho yako, yaani uzuri wa
mwili wako bila tabia ya kumcha Mungu ni msiba mkubwa sana, Wakati kuna fahari
kubwa sana mtu anapokuwa mzuri kimwili, kimaadili na kiroho, jambo hilo huleta
Baraka kubwa sana! Maandiko yanatuonyesha wazi kuwa Mungu aliwatumia watu
wazuri kimwili na kiroho kuwa Baraka kubwa sana kwa ulimwengu hata leo mfano:-
Kutoka 2:1-2 “Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi
akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa
mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.”
1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia
Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama,
anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa
sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao.
Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza.
Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa
pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana
ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake
Rama.”
Esta 2:7 “Naye alikuwa amemlea Hadasa,
yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana
huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake,
yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye.”
Maneno yanayotumika kuelezea uzuri wa sura, umbo, mvuto na maumbile
yenye kukubalika na kuvutia katika maandiko ya kiebrania ni pamoja na:-
-
Tob -
kuelezea uzuri wa sura na umbo neno hili
limetumika mara 361
-
Yapheh –
kuelezea mvuto na mwenye kupendeza limetumika mara 21
-
Mareh
–uzuri wa kimaumbile na muonekano hili limetumika mara 35
Maneno yote hayo yalitumika kuelezea muonekano wa nje wa kibinadamu, na
ambao pia Mungu aliutumia kwa faida zake au kwaajili ya utukufu wake, maneno
hayo yalitumika kumuelezea mwanaume na mwanamke aliyekuwa mzuri kwa muonekano
lakini vilevile ambao Mungu aliwatumia katika kazi zake kwa utukufu wake.
Katika vifungu kadhaa vichache
hapo juu tumeona maandiko yakitueleza habari za Musa, Daudi na Esta hawa
walikuwa wazuri sana kama maandiko yanavyosema lakini vile vile tunaona Mungu
akiwatumia vijana hawa wazuri Katika kazi zake kwaajili ya utukufu wake, ni
wazi hapa utaona kuwa kuna uhusiano wa uzuri na ulimwengu wa roho, lakini
vilevile shetani hutumia watu wazuri, vijana kwa wasichana wazuri katika
kutimiza mpango wake wa kuharibu dunia kwa hila. Hivyo katika somo kama hili
tunataka kujifunza umuhimu wa kuutumia uzuri kwaajili ya utukufu wa Mungu,
Mungu hakukupa uzuri ili uutumie vibaya bali amekupa uzuri kwaajili ya utukufu
wake! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
Ø Uhusiano wa uzuri na matumizi ya Mungu
Ø Uhusiano wa uzuri na matumizi ya shetani
Ø Matumizi ya sahihi ya uzuri katika ulimwengu
wa mwili na roho.
Uhusiano wa uzuri na Matumizi ya Mungu.
Kama tulivyoona katika utangulizi
wa somo hili ya kwamba Mungu aliumba kila kitu na kila kitu alikifanya kizuri
kwaajili ya utukufu wake, tunaona pia Mungu akiwatumia watu mbalimbali katika
kuyatimiza mapenzi yake lakini wakati huo huo tunaambiwa kuwa watu hao ambao
Mungu aliwatumiwa maandiko yanatuambia kuwa walikuwa wazuri:-
-
Sara
ambaye ni mama wa Imani mama aliyemzaa Isaka, mke wa Ibrahimu maandiko
yanatueleza ya kuwa alikuwa mzuri sana ona Mwanzo
12:11-14 “Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri,
akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi
itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na
wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili
yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. Basi ikawa Abramu alipofika Misri,
Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana.”
Lakini pamoja na
kuwa Sara alikuwa mwanamke Mzuri sana katika muonekanao wa mwili bado mwanamke
huyu alikuwa ni Mwanamke wa Imani, alimcha Mungu na alikuwa na tabia njema
sana, alimuheshimu mumewe na alikuwa na upendo dhidi ya mumewe kiasi cha
kupitiliza, Sara hakuutumia uzuri wake kwa kiburi na Mungu alimtumia kama
mwanamke aliyeleta Baraka kupitia Isaka ambaye ni mwana wa ahadi kwao na kwetu
pia maandiko yanamsifia Sara kuwa alikuwa
na roho ya upole, na utulivu na alimuheshimu sana mumewe na kuwa mfano wa
kuigwa katika jamii kama mama wa Imani. Ona
1Petro 3:1-6 “Kadhalika
ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe
kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na
wa hofu. Kujipamba kwenu, kusiwe
kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho
ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo
walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii
waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto
wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote.”
Unaona Sara
alikuwa mzuri wa Uso lakini hakuwa na kiburi, Petro anamtumia kama mfano au
kielelezo kwa wanawake wote kuwa kama yeye alikuwa mpole, mwenye utulivu,
akimtii Mungu pamoja na mumewe na Mungu
alimtumia kama Baraka kwa ulimwengu mzima kama tulivyoona
-
Rebeka
- anatajwa katika maandiko kama mwanamke aliyekuwa mzuri wa uso, lakini
vilevile ni mwanamke aliyemcha Mungu, alikuwa na tabia nzuri pamoja na ukarimu
uliokithiri kwa wanadamu mpaka kwa wanyama, Mungu alimpa neema ya kuolewa na
kijana wa Ibrahimu yaani Isaka na baadaye alifanikiwa kuzaa mapacha Esau na
Yakobo ambao wamekuwa Baraka kubwa sana kwa ulimwengu na wamekuwa kielelezo cha
mafundisho mengi mema ya kifamilia, kiroho na kiuchumi hii ni kwa sababu Rebeka
alikuwa mzuri wa uso na mzuri wa tabia na mcha Mungu ona
Mwanzo 24:10-26 “Kisha
huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake,
maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka
Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu
na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka
maji. Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo
yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama!
Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka
maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako,
nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia;
basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua
ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka
anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu,
naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake,
bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake,
akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali
unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu,
akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata
alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha
kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga
mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Basi yule mtu akamkazia
macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo.
Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake
ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa
shekeli kumi za dhahabu, akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je!
Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema,
Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia,
Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. Yule mtu
akainama akamsujudu BWANA.”
Unaweza kuona
Rebeka alikuwa mzuri sana lakini pamoja na uzuri aliokuwa nao alikuwa na tabia
njema na alikuwa amejawa na ukarimu, baadaye pia tunamuona Rebeka akipokea
muujiza wa kuwa na mapacha tumboni baada yakuombewa na Isaka na sio hivyo tu
pia alitaka kujua mapenzi ya Mungu juu ya watoto wake, na hivyo kuhusika katika
unabii mkubwa wa kujua mapenzi ya Mungu kwa watoto wake waliokuwa tumboni, Mwanamke
mzuri, tabia nzuri na alimuweka Mungu mbele.
-
Yusufu -
Mwana wa Israel au Yakobo, alikuwa ni kijana ambaye maandiko yanamtaja kuwa
alikuwa mzuri, lakini licha ya kuwa mzuri wa uso pia alikuwa na tabia nzuri,
aliwavutia watu akiwemo baba yake, lakini vilevile alimpendeza Mungu alimcha
Mungu wa Mbinguni, Mungu alisema naye kuhusu kusudui la kuweko kwake duniani,
alimtumia Kule Misri kuhifadhi watu wa dunia ya wakati ule, aliweza kutabiri
kurudi kwa wana wa Israel katika inchi ya kanaani kwa kuamuru wabebe mifupa
yake baadaye, alitembea na Mungu alikuwa na hofu ya Mungu ona
Mwanzo 39:2-9 “BWANA
akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana
wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa
BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake,
akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo
akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya
nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa
ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika
nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu;
wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa
baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala
nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui
kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi
mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho
chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose
Mungu? ”
Yusufu alikuwa kijana
mzuri na wa kuvutia sana, mke wa Potifa alimpenda sana na kuvutiwa naye kiasi
cha kutaka kumbaka Lakini Yusufu hakukubali, sio kwa sababu alikuwa mjinga
hapana alikuwa anamjali Mungu, alimcha Mungu aliogopa kuharibu uhusuano wake na
Mungu na hivyo aliutunza na ndio maana unaona Mungu alikuwa pamoja naye.
-
Mfalme
Sauli – Mfalme wa kwanza wa Israel ambaye Mungu alimuelekeza nabii Samuel
amtie mafuta ili awe mfalme wa Israel maandiko yanaeleza kuwa kijana huyu
alikuwa mzuri sana na katika Israel
nzima hakukuwa na kijana Mzuri kama yeye ona
1Samuel 9:1-2 “Basi,
kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli,
mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu
shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana,
tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu
mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.”
Hili ni jambo la
kushangaza sana katika maandiko kwani inaonekana wazi kabisa kuwa uzuri ulikuwa
unaambatana na mambo mengi sana kuanzia muoneako, akili na ushujaa, ujuzi
hekima na werevu, n ahata urefu wake, ilikuwa wazi kabisa kuwa Mungu alikuwa na
anatumia watu wazuri mpaka sasa, kwa hiyo uko uhusiano mkubwa kati ya utumishi
wa Mungu na uzuri.
-
Abigail
- maandiko yanamtaja mwanamke huyu kuwa alikuwa mzuri sana lakini utaweza kuona
pia alikuwa na akili sana bahati mbaya tu mara ya kwanza aliolewa na mwanaume
mpumbavu mpaka pale Daudi alipomuoa baadaye baada ya kufa kwa mumewe mpumbavu
aliyeitwa Nabali ona kisa chao kinatumika kutufundisha kuhusu Torati na Injili
kama waume na Abigaili kama mke au kanisa Mume wa kwanza ni Torati na Mume wa
Pili ni injili kwa mwanamke yule yule tunaambiwa mwanamke huyo alikuwa mzuri na
mwenye akili nyingi sana ona
1Samuel 25:2-3 “Na
huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli;
naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye
alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa
Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye
akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu
katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.”
Unaona mwanamke
alikuwa mwenye akili njema na pia alikuwa mzuri wa uso, hapa utaweza kugundua
jinsi ambavyo uzuri wa kimaumbile ulivyokuwa unakamilishwa na uzuri wa tabia na
mwenendo na akili, na roho njema nay a ukarimu kwa hiyo tunaweza kupata piacha
iliyo wazi kuwa Mungu alikusudia watu wazuri wa uso wawe vilevile na tabia
nzuri na kili ili zitumike kwa utukufu wa Mungu!
-
Vijana wa
kiibrania Daniel, Hanania na Mishael (Daniel Shadrak na Meshaki na Abednego)
Daniel 1:3-6 “Mfalme
akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa
Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi
wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza
kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo,
na lugha yao. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai
aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye
wasimame mbele ya mfalme. Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda,
Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.”
Muda usingeweza
kutosha kupitia vijana na mabinti wazuri ambao Mungu aliwatumia katika maandiko
lakini ni wazi kuwa utakubaliana nami kuwa Mungu anapenda na kutumia watu
wazuri, wenye maadili mema kwaajili ya utukufu wake unaona! Tumewaona vijana
waliochukuliwa mateka utumwani Daniel na wenzake maalumu kabisa walichaguliwa
vijana wazuri, waungwana , wasio na mawaa wenye hekima akili na werevu na wenye
maarifa hawa walichaguliwa na mfalme Nebukadreza ili wamtumikia lakini wote
tunajua uhodari wao vile vile wa Imani katika Mungu wa kweli, lakini walikuwa
wazuri ni katika hali kama hiyo pia uzuri hutumiwa na ibilisi pia kwa faida
zake kama tunavyojifunza katika kipengele kifuatacho:-
Uhusiano wa uzuri na matumizi ya shetani
Kama jinsi ambavyo tumeona jinsi
ambavyo Mungu aliwatumia vijana wa kike na kiume walio wazuri kuwa watumishi
wake naye akitukuzwa kupitia imani zao na matendo yao, hali kadhalika shetani
huutumia uzuri kwa kusudi la kuwatumia watu wazuri wa muonekano na sura
kwaajili ya kazi zake huku yeye mwenyewe akiwa ni kielelezo cha Matumizi mabaya
ya uzuri ona:-
Ezekiel 28:13-17 “Ulikuwa ndani ya Adeni,
bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na
yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti
samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi
zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.
Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa
juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.
Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu
ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu
ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika
mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi
ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya
uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa
chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”
Yeye mwenyewe Shetani (LUSIFA) maandiko yanatueleza wazi kuwa
alikuwa ni malaika mzuri sana mwenye
utukufu mwingi yeye aliyekaa katika uwepo wa Mungu, lakini inaelezwa kuwa MOYO WAKE ULIINUKA KWA SABABU YA UZURI
WAKE, kwa hiyo zawadi ya uzuri
wakati mwingine imewaletea wengi majivuno na kuuwafanya wautumie uzuri
kutekeleza matakwa ya kishetani matokeo
yake wanakuwa ni wazuri wa sura na muonekano lakini wakiwa hawana uadilifu
unaokusudiwa na Mungu, kinyume na makusudi ya Mungu ya kuumba watu wazuri ili
awatumie shetani amekuwa akiwatumia wanaume wazuri na wanawake wazuri kwaajili
ya tabia mbaya
-
Uzuri umetumiwa
kwa kusudi la umalaya Mithali 6:24-26 “Yakulinde na
mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani
uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana
kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba
humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani”
-
Uzuri
unatumiwa na ibilisi kwa makusudi ya ubakaji wakati mwingine 2Samuel 13:1-2. “Ikawa
baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake
akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni,
hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa
mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote.”
Unaona
tunaelezwa kuwa Absalom mwana wa Daudi alikuwa na dada mzuri kiasi ambacho kaka
yake Ammnoni alimpenda sana mpaka akaugua yaani aliumwa kwaajili ya ndugu yake
ambaye alikuwa mzuri, uzuri wa Tamari ulimpoza kiasi ambacho kaka yake hakuweza
kuvumilia wala kusubiri michakato ya kuomba kwa mfalme ili amuoe na badala yake
akambaka na kufanya upumbavu ona
2Samuel 13:6-14 “Basi
Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni
akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate
miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe
aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako,
ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa
amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka
mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye
Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake. Amnoni
akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi
Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani.
Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia,
Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze
nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami
nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli.
Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini
yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye,
akamtenza nguvu, akalala naye.”
Tunajifunza hapa
kuwa wakati mwingine uzuri wa watu umewaponza, shetani amatumia tamaa za watu
kuwashambulia watu wazuri, kama Tamari ambaye alibakwa kwa sababu ya uzuri
wake, unaweza kushambuliwa na shetani kwa sababu ya uzuri, sio lazima kwa
kubwakwa tu, unaweza kuteswa na mapepo kwa sababu tu wameona u mzuri, unaweza
kutupiwa majini na watu kwa sababu tu wameona u mzuri, unaweza kufanyiwa
ulaghai wa kila aina kwa sababu tu watu wameona u mzuri, uzuri unaweza kumfanya
adui akushambulie, uzuri unaweza kumfanya mtu akakushawishi, uzuri unaweza
kufanya hata mumeo akauawa, au hata kama umeolewa bado watu wakaingilia ndoa
yako na kukuchukulia ukipendacho kwa sababu ya uzuri, uzuri wako ndio jaribu
lako, uzuri wako unaweza kukaribisha changamoto nyingi
Uzuri unaweza kuiponza ndoa yako na nyumba
yako ona 2Samuel 11:2-4 “Ikawa wakati wa jioni,
Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na
alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri
sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule
mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe
Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye
akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha
akarudi nyumbani kwake.”
Unaiona
tunaambiwa kuwa Bathsheba binti Eliamu huyu ndiye mama yake Mfalme Sulemani
alikuwa mzuri sana wa kupendeza macho, na Daudi alipomuaona alimtamani na
kuagiza aletewe na kuingia kwake, kumbuka kuwa alikuwa mke wa mtu, lakini mtu
mwingine mwenye fedha, mamlaka na utawala anaingiwa na tamaa na kuona kuwa
mwanamke huyu anafaa kuwa wake na sio hivyo tu alienda mbali na kufanya njama
za kumuua mumewe ili amuoe yeye mwanamke yul, uzuri wa mwanamke huyu unamleta
katika majonzi na sababu kubwa sana ya maangamizi na dhambi katiika familia ya
Daudi, Kwa nini kwa sababu shetani alimpa moyo wa kutokuvumilia alipoona uzuri
wa mwanamke huyu, tunajifunza kuwa uzuri wako utawavutia watu wa kila aina
wenye tabia mbaya, wenye tamaa, wenye mamlaka na mali ili umuone mumeo au mkeo
kuwa mtu duni na wao wakuchukue kwajili ya fahari ya miili yao, wako watu ambao
watakuona kama hicho ulicho nacho haustahili kuwa nacho, na ulicho nacho ni
chao pia, watataka waonje uzuri wa mumeo watataka waonje uzuri wa mkeo.
-
Uzuri
unaweza kutumiwa na shetani kukufanya uwe na kiburi na kukosa adabu – 2Samuel
14:25 -27 “Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu
hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za
miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka
hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima
nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa
kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari;
naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso.”
Tunasoma hapo
katika maandiko ya kwamba Absalom mwana wa Daudi alikuwa gumzo katika Israel
kijana alikuwa mzurii, kijana alisifiwa Israel yote kwa sababu ya uzuri wake
alikuwa mzuri kutoka utosini mpaka kwenye unyao wa miguu yake na inaelezwa kuwa hakuwa hata na doa lolote,
alikuwa ananyoa mara moja kwa mwaka hivyo alikuwa na nyele nzito, nzuri ndefu
zinazoangukia mgongoni au mabegani n
ahata alipofanikiwa kuna na binti binti yake naye alikuwa mzuri uzito wa nywele
zake ziliponyolewa ilikuwa ni shekel mia mbili kwa vipimo vya wakati ule shekeli
moja kwa sasa ni sawa na kilogram 0.0114 kwa hiyo 0.0114 x 200 = 2.28 hii
ni sawa na kusema Nyele za Absalom ziliponyolewa zilipatikana kilo mbili na
gram 28 kwa kweli alikuwa ni kijana
mzuri mno mzuri sana na ilikuwa halali aweze kuwa gumzo katika Israel na
alipendwa na kukubalika na watu, hata hivyo tunasima mwisho mbaya wa kijana
huyu, uzuri wake ulimpa kiburi, akili yake ilijaa hila shetani alimuharibu
alimpingua baba yake na nyele zake ambazo zilikuwa ni moja ya fahari yake kubwa
sana zilikuwa sababu ya kifo chake licha ya kulala na wake za baba yake na
kumuasi na kupigana naye vita tunasoma
hivi
2Samuel 18:6 -16 “Hivyo
watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani
ya msitu wa Efraimu.Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi,
kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu. Kwa maana vita
vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi
kuliko wale walioliwa na upanga. Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi
wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita
chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika
mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa
chini yake akaenda mbele. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu,
akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni. Naye Yoabu
akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi,
hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi. Yule mtu
akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo
singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu
alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote
asimguse yule kijana, Absalomu. Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa
hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe
mwenyewe ungalijitenga. Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe
hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni,
alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni. Kisha vijana kumi, waliomchukulia
Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua. Kisha Yoabu
akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia
watu.”
Ni jambo la
kusikitisha sana ya kuwa nyele zake zilezile Absalom ambazo zilikuwa moja ya
sababu kubwa ya uzuri wake ndizo zilinasa kichwa chake juu ya mti wa mwaloni na
hivyo kuuawa kwa kuchomwa moyoni na
kushambuliwa kwa silaha na ukawa mwisho wake ni somo kwetu kuwa wakati mwingine
sifa ile ile njema na uzuri ule ule tulio nao unaweza kugeuka au kutumiwa na
adui kuwa maangamizi yetu
Kumbuka pia kuwa
ni uzuri wake Vashti uliosababisha akapoteza umalikia na kuonyesha dharau kwa
mumewe ambaye alitaka kuonyesha fahari kwa wenzako ya kuwa ana mwanamke mzuri
na matatat sana ona
Esta 1:10-21 “Hata
siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani,
Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale
wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti,
malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na
maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa
kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme
akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia
wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya
mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena,
Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba
wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme;
akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama
vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi
Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa
mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika
majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na
wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa
mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata
na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za
tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea
dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya
kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba
Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe
mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga
itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu
waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida;
naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.”
Muda usingeweza
kutosha kuona namna shetani alivyotumia uzuri kuharibu maisha ya watu tofauti
na namna Mungu alivyokusudia, watu wengi tunawasoma kuwa walipata hasara katika
maisha yao na machungu katika maisha yao kwa sababu shetani alitumiz uzuri wao
kama sababu ya kuharibikiwa kwao, leo hii wanawake kwa wanaume wazuri wasio na
ila wala madoa ndio wanaotumiwa katika kupiga picha za ngono, na kurekodi mikanda
ya ngono, wanatumiwa kutangaza bidhaa mbalimbali, wanatumiwa katika kutangazaa
pombe, sigara na wanatumiwa kama wanengua viuno katika miziki ya dansi, maarufu
kama (video queens) na katika anasa
nyingi, wanatumiwa kama vivutia na sehemu ya viburudisho katika jamii sehemu za
starehe mbalimbali, wanatumiwa katika madaa, na makasino wanatumika katika
maeneo mbalimbali ya kuharibu aina binadamu kwa sababu tu ya uzuri
Katika andiko
letu la Msingi tunasoma habari za Mwanamke aliyeitwa Abishagi nib inti
aliyekuwa mzuri sana mzuri mno, washauri wa mfalme walumuona Daudi kuwa
amezeeka na hivyo walitaka kumtia moyo mfalme ili achangamke na kupewa joto, na
ndipo alipotafutwa binti huyu aliyekuwa kijana mzuri ili amuhudumie mfalme mzee
ambaye kimsingi hakuweza kumgusa lakini alimtumia kwaajili ya kujiburudisha tu,
asingeliweza kuzaa naye wala kulala naye lakini binti wa watu alitwaliwa na
kutumiwa hovyo tu kwa sababu ya uzuri Abishagi alitumika kama nesi wa mfalme tu
na muhudumu wa mfalme tu wa kumpa joto ashukuriwe Mungu kuwa baadaye aliolewa
na Mfalme Suleimani lakini ni jambo la kusikitisha kuona uzuri wake ulikuwa
kama unapotezewa muda na kutafuta namna ya kubebeshwa ujane, nyakati za leo
tunaweza kuona matukio ya namna hii ambapo wazee wanatafuta kujifariji kwa
wanawake vijana tena wazuri, hatuwezi kuhukumu lolote lakini tunaweza kukiri
kuweko kwa matumizi mabaya ya uzuri na kupotezewa muda na kuachwa ujane kwa
sababu ya uzuri
1Wafalme 1:1 – 4 “Mfalme
Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini
asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe
kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako,
ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote
mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. NAYE KIJANA
HUYO ALIKUWA MZURI SANA; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme
hakumjua.”
Matumizi sahihi ya uzuri katika
ulimwengu wa mwili na roho.
Ni muhimu kwanza kuelewa kuwa
uzuri ni karama ni zawadi anayoitoa Mungu, kama apendavyo yeye mwenyewe
tunasoma katika maandiko jinsi Mungu alivyombariki Ayubu baada ya majaribu moja
ya zawadi aliyompa ni pamoja na mabinti watatu ambao tunaambiwa walikuwa ni wazuri
sana mabinti hao wa Ayubu waliitwa
YEMIMA, KESIA NA KEREN ona Ayubu
42:12-15 “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho
wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na
ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na
wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na
wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika
nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na
baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume.” Kwa msingi
huo utaweza kukubaliana name kuwa uzuri ni zawadi ambayo Mungu huitoa katika
familia kadhaa kama apendavyo Mungu yeye mwenyewe hata hivyo, zawadi au karama
ya uzuri ni vema ikatumika vizuri kwaajili yake
Ni ukweli ulio wazi kuwa uzuri wa
mwili bila kujali uadilifu na tabia za kiroho uzuri huo unakuwa ni ubatili
mtupu, inaonekana wazi kuwa uzuri wa mwili haujitoshelezi ukibaki pake yake bila
uzuri wa kiroho mwili wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na hivyo Mungu amekusudia
atukuzwe katika miili yetu ona
1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa
mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?
Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi,
mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
Unaona maandiko yanataka Mungu
atukuzwe katika miili yetu kama Mungu ametuumba vizuri na kisha tukashindwa
kuutumia uzuri wetu kwa uzuri wa kiroho tutasababisha majaribu makuwa kwa watu
na kumuudhi Mungu, tutasababisha majaribu kwa watu na kwetu wenyewe na kumpa
shetani nafasi ya kukufuru katika miili yetu, uzuri wa mwili bila uzuri wa
kiroho ni sawa na kuwa na ugonjwa unaoambukiza, utasababisha kuenea kwa
uharibifu kwa wengine na kwako mwenyewe, uzuri wa mwili bila uzuri wa rohoni ni
hatari sana, wote tunakumbuka jinsi Hekalu la Yerusalem lilivyokuwa zuri, hata
wanafunzi wa Yesu walikuwa wakimuonyesha Yesu kuwa hekalu lile ni zuri mno,
Lakini Yesu aliwaambia haltasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa kwa
sababu uziri wa nyumba ile ungekuwa bora kama watu wake wangesimamisha ibada
lakini watu walipikuwa waasi na kumsukumia mbali masihi aliyetumwa kwao mbele
za Mungu nyumba ile ilionekana kuwa haina maana tena ona
Mathayo 24:1-2 “Yesu akaenda zake, akatoka
hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye
akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa
jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”
Mungu alipokupa uzuri ilikuwa ni
dalili iliyo wazi ya kuweka uzuri wake ndani yako, kwa hiyo uko uwezekano
mkubwa sana kuwa katika kila mwanadamu aliyeumbwa vizuri ilikuwa Mungu ajifunue
kupitia uzuri wake kwaajili ya utukufu wake na ndio maana tunatangulia kuuona
uzuri wa kiwmili lakini yamkini Mungu alikusudia pia baadaye kufunua uzuri wa
kiroho ndani yake, lakini shetani anapowahi na kuanza kuleta uharibifu ndipo
tunapoweza kufikiri kuwa vizuri vizuri viliumbwa kwaajili ya shetani tu hapana
Mungu aliumba vitu vizuri kwaajili ya utukufu wake, Hakuna jambo linatia moyo
kama kuona wadada wazuri, wakaka wazuri, wamama wazuri, wababa wazuri alafu
wakati huo huo wanamcha Mungu kupita kawaida na wana msimamo ya kiroho, wa
akili na huku wakiwa mstari wa mbele katika kazi za ukombozi, kama alivyokuwa
Musa, Esta, Mariamu, Daniel na wenzake, Daudi, na kadhalika watu ambao walikuwa
wazuri sana kwaajili ya utukufu wa Mungu
na wakamtumikia Mungu, shukurani tunayoweza kumrudishia Mungu kwa kutuumba
vizuri ni pamoja na kumcha yeye, Lusifa aliumbwa vizuri sana lakini badala yake
akawa na kiburi, na kuutumia uzuri wake vibaya Mungu aliahidi ya kuwa
atamfukuzilia mbali kwa sababu moyo wake uliinuka kwa sababu ya uzuri, badala
ya kuutumia uzuri kwa utukufu wa Mungu, kilichompata Lusifa kinaweza kumpata
yeyote ambaye ni mzuri, Mungu anatoa wito kwa wazuri wote leo kugeuka na
kuyatoa maisha yao kwa Yesu, msifikiri kuwa uzuri wenu ni kwaajili ya duania
hii hapana ni kwaajili ya utukufu wa
Mungu, kila mmoja autumie uzuri kwa kwaajili ya kuonyesha namna
anavyoweza kumuadhimisha Mungu balada ya kuwa na kiburi na majivuno kama
shetani, aidha nitoe wito kwa wakristo mambibi na mabwana kutokuutumia uzuri
wao vibaya wako watu wengine huutumia uzir wao kama ukarimu wa kukubali kila
kitu, kwa kuwa ni wazuri basi wanataka kuonjesha uzuri wao kwa kila mtu au
kuutumia uzuri wako kwa kiburi na majivuno na kujiinua, bwana ampe neema kila
mmoja wetu kuimarisha uzuri wake alionao mwilini kwa kumcha Mungu na kutembea
katika uwepo wa Mungu!
Ezekiel 28:13-19 “Ulikuwa ndani ya Adeni,
bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na
yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi,
na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako
ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe
ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu
ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.
Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu
ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa
uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa
sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho
najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya
moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa
sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate
kukutazama. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia
unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao
umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote
wakutazamao. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu
cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.”
Na Rev. Innocent Mkombozi Samuel bin Jumaa, bin Athumani Bin Zumbe
Salim Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !