Jumamosi, 16 Machi 2019

Msinichunguze kwa kuwa mimi ni mweusi mweusi!


Wimbo ulio bora 1:5-6Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za Kedari, Kama mapazia yake Sulemani. Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda
 

Utangulizi:

Maandiko Matakatifu yanatufundisha maswala ya Msingi sana kuhusu Maisha, hususani katika nyakati hizi za siku za mwisho ambapo watu wanajituma sana kutafuta maisha na kufanya kazi zao kwa bidii ili waweze kukidhi haja ya mahitaji ya familia zao, Katika nyakati hizi watu wengi sana wamekuwa wakifanya kazi sana (busy) kiasi ambacho licha ya kufanikiwa sana katika maeneo mengine lakini wameharibikiwa na kupoteza maswala ya msingi, au kupuuzia maswala ya muhimu sana katika maisha yao.

Kifungu cha maandiko tulichokisoma kinafaa kabisa kusomwa sambamba na kitabu cha Mithali 24:30-31 inayosemaNalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili. Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.

Somo kubwa tunaloweza kulipata hapa ni onyo kuhusu kuwa :busy” katika maisha na kusahau kushughulikia maswala ya msingi, tunaweza kujishughulisha sana na kazi, na maswala yanayoonekana kuwa ya muhimu kwetu na tukasahau maswala muhimu na ya msingi katika maisha yetu wenyewe, Katika mstari wa msingi tunaona mwandishi akionyesha kulalamaika kwamba amekuwa mweusi mweusi ijapokuwa yeye ni mzuri, lakini sababu kubwa ni kuwa amepigwa na jua kwa sababu ya kufanya kazi na kujishughulisha na mambo ya wengine akitunza mashamba yao ya mizabibu kwa kiwango ambacho yeye mwenyewe alikuwa anashindwa kushughulikia mambo yake na hata ya shamba lake binafsi la mizabibu hapa ndio tutachukua muda kujifunza na kuangalia kwa undani kwamba kuna nini ambacho maandiko yanataka kutufunza:-

Wajibu wa kufanya kazi tulizopewa!

Ni muhimu kufahamu kuwa sisi ni watumishi wa Mungu, na kuwa ni Bwana ndiye aliyetuchagua tumtumikie katika eneo ambalo ametuita kumtumikia ni neema kuu kwa Mungu wetu kufanya kazi katika eneo ambalo Mungu amekupa kufanya ni Baraka kubwa sana kwa vile huenda wengine wametamani kufanya unachokifanya lakini hawakupata neema hiyo, kwa hiyo hatuna budi kumshukuru Mungu kwa wito aliotuitia kwa kuwa ni wito wa ki Mungu (Divine appointment) so kimsingi Mungu anataka sana tufanye kazi zetu kwa bidii, kumbuka kuwa hatukuchagua kufanya hiki tunachokifanya kwa hiyari yetu wenyewe ila Mungu alikusudia “Waliniweka niwe mlinzi” ni wazi kuwa mtu huyu hakuchagua awe na hali ile alichaguliwa Mungu ndiye anayechagua kwamba sisi tutimize wajibu gani hapa ulimwenguni Yohana 15:16Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.” Unaweza kuona kumbe ni Mungu aliyekusudia tuwepo katika wajibu huu tulio nao sasa na sisi tumefanya vema kutii wito wake Mathayo 21:28Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu.” Unaona? Kila mmoja yuko katika shamba la mzabibu, tumeitikiwa wito alioweka Mungu ndani yetu kutokana na upendo wake kwetu na upendo wetu kwake tumetii , Shamba lako la mzabibu ni pale ambapo Mungu amekuweka umtumikie nawe ni mtoto mwema kwa kuwa umetii na unafanya kazi kwa bidii katika shamba lako la mizabibu uliloitiwa yaani:-

·         Kama ni mama wa Nyumbani shamba lako la mizabubu ni pale Mungu alipokuweka kuhakikisha unailea familia yako na kuongoza watoto wako katika njia iliyonyooka, unafanya wajibu wako wa kumlinda mumeo kumtunza, kumpikia na kuhakikisha kuwa ana afya njema ili aweze kutiwa moyo kutafuta kwaajili yako na familia yako.

·         Kama ni mwalimu utafanya yaliyo wajibu wako wote kama mwalimu, utafundisha kwa bidii yako yote na kufanya kila kilicho wajibu wako kuwaelimisha vijana, na kuwarithisha maadili na tamaduni na uzalendo kwaajili ya taifa letu na faida ya kizazi kijacho utaifanya kazi hiyo kwa bidi.

·         Mwanajeshi basi shamba lako la mizabibu ni jeshini, kulinda na kulipigania taifa lako, utawalinda wananchi wa-nchi yako, na kuhakikisha kuwa mipaka ya taifa lako iko salama na mipaka ya majirani zako, na wakati wote utahakikisha unalinda na kuisimamia amani ya dunia kwani umeyatoa maisha yako kwaajili ya jamii.

·         Daktari au muuguzi mlezi basi shamba lako la mizabibu ni Hospitali, utawapenda na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wa upendo ukijitoa kwa uaminifu na kutunza siri za wagonjwa wako, na kuwahudumia kwa moyo wako wote ukiifanya kazi hii ya kuokoa uhai wao mpaka dakika za mwishi isipokuwa tu pale ambapo Mungu ameingilia kati na kuchukua kiumbe wake, utatia moyo na kuwapa pole waliopoteza ndugu yao kwa kuwa uwezo wako wa kibinadamu wa kuokoa maisha yake umeishia hapo.

·         Muhubiri shamba lalo la mizabibu ni injili, kwamba utahakikisha unalihubiri neno, kwa bidii, wakati unaofaa na usio faa, utahakikisha kuwa injili inawafikiwawale wanaokuzunguka na eneo lile ambalo mungu amekupa kumtumikia.

·         Mfanya biashara shamba lako la mizabibu ni biashara ambazo Mungu amukupa uzifanye huko ndiko Mungu alikokukusudia utumike na kumtumikia na kutimiza mapenzi yake.

·         Mwanafunzi wajibu wake nikusoma kwa bidii, kujiandaa vema na kuhakikisha kuwa unapata maarifa yote ambayo serikali na walimu wako wamekusudia uyapate, uwe tayari kufaulu pia mitihani yako na kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maisha mara baada ya kumaliza masomo yako.

·         Kila mmoja kwa sehemu yake kazi yoyote ile ni muhimu kukumbuka kuwa popote ulipo unamtumikia Mungu na kuwa wapaswa kufanyakwa bidii kile ambacho Mungu amekupa kukifanya. Hayo yote ni mapenzi ya Mungu kabisa.

Hatari inayomkabili mtunza mizabibu!

Wimbo uliobora 1:6bWana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda

Ni muhimu kufahamu kuwa kuna hatari kubwa sana katika kujishughulisha na wajibu wa kile ambacho Mungu amekusudia tukifanye na kwa urahisi sana tukasahau mambo ya msingi, watu wengi sana kwa sababu ya kazi na kwa sababu ya biashara na masumbufu ya maisha haya wamesahau kushughulikia maswala ya msingi ya ndani katika maisha yao, kumbuka kuwa ni rahisi kuwapigia watu kiwi katika viatu vyao na kuving’arisha lakini ukasahau kung’arisha cha kwako, ni rahisi kuwa mjenzi wa majengo na ukajengea watu majengo ya kifahari na ukasahau kujenga ya kwako au usiwe hata na kajumba, ni rahisi kulima vibarua na ukapalilia mashamba ya watu wengine kisha kwako majani yakaota, ni rahisi pia kuwahubiri watu wengine injili na kuwaelekeza katika neno la Mungu kisha wewe kuwa mtu wa kukataliwa, hii ndio hatari kubwa sana kwa sababu hakuna mwajiri atakayekuhurumia duniani (Kukasirikiwa) na akakupa nafasi ya kukuacha ufanye mambo yako, Israel kule Misri walitumikishwa na walinyimwa kabisa muda wa kumuabudu Mungu, walifanya kazi siku zote na hawakuwa na muda wa mapumziko wala muda wa kuwa na uhusiano na Mungu ndivyo walivyofanywa na Farao kule Misri, mpaka walipofika Sinai ndipo Mungu aliwakumbusha kupumzika na kufanya kazi siku sita na moja kuitoa kwaajili ya Mungu Kutoka 1:13-14 “Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali unaona mfumo wa Dunia hii na hali yake hauruhusu wala kutoa muda wa kushughulikia mambo yako ya muhimu na-ya ndani kabisa Hali kama hii ilitokea Afrika wakati wa ukoloni, wakoloni walifanya mambo kadhaa yenye kuwalazimisha waafrika waweze kuwa watumwa wao wakati wa ukoloni na walime na kulipa kodi kwa matakwa ya wakoloni na kuwaminya kiasi ambacho iliwalazimu waafrika na baba zetu kuona umuhimu na kuudai uhuru wao.

1.      Walitaifisha ardhi nzuri zenye rutuba – land alienation
2.      Walibadilisha mfumo wa uchumi kutoka biashara ya kubadilishana kwenda kwenye biashara kwa njia ya fedha – Money economy
3.      Waliwalazimisha raia kulipa kodi- Taxitation
4.      Walianzisha mazao ya biashara – Cash crops
5.      Waliwaajiri watu kwa ujira mdogo sana – Cheap labor
 
Kutokana na mazingira ya aina hii, watu walipoteza uhuru wa kufanya mambo yao. Na ili wapate fedha walilazimika kufanya kazi katika mashamba ya wakoloni au kuzalisha mazao ya biashara ili wauze hali hii ilikuwa ngumu na kuwafanya wapoteze uhuru wao na wasifanye mambo yao wenyewe, hali hii ni sawa na kulazimika kutunza mashamba ya mizabibu ya watu wengine na kutokutunza mizabibu yao wenyewe, Dunia na mfumo wake unakulazimisha ushughulike zaidi na mambo ya wengine kuliko mambo yako ya msingi.

Kama walimu tunaweza kufundisha watu na wakafanikiwa kwa kiwango kikubwa na wakafaulu lakini nyumbani tukawa na watoto wetu au ndugu zetu wanafeli na kudidimia kimasomo, ama tunaweza kukemea na kuchapa watoto wa wengine mpaka wakabadilika kitabia wakawa watoto wazuri na hata wazazi wake wakakushukuru lakini wetu wakatushinda wakawa ni watovu wa nidhamu wa hali ya juu.

Unaweza kuwa Muhubiri na ukahubiri vema na kuwaelekeza watu njia ya Mungu lakini ukasahahu kuwa na Muda wako binafsi na Mungu,ukasahau wajibu wa kuisimamia nyumba yako vema ukawa na washirika wanaokutii lakini mke na watoto wasiokuheshimu wala kukutii.

Unaweza kuwa mshauri wa ndoa na mwalimu mzuri sana wa ndoa na ukasaidia ndoa za watu wengi sana lakini ya kwako ikawa ni majanga, unaweza kuwafundisha watu kuomba lakini wewe ukakosa nafasi ya kuomba japo kwa saa moja, unaweza kuwa mlinzi mwema na askari mwema lakini ukashindwa kuilinda ndoa yako, ukashindwa kuwatiisha watoto wako wakawa na heshima na adabu.
Unaweza kuwashauri watu kwa habari ya afya au ukawa daktari mzuri, lakini wewe ukawa una matatizo makubwa sana, Maandiko yanatulaumu kuwa tumeacha kuangalia mzabibu wetu wenyewe
Nyakati hizi tulizo nazo mambo yameharibika sana, kumekuweko na aina nyingi za uharibifu katika maisha ya watu kutokana na kukosa malezi mazuri kutoka kwa wazazi kutokana na wazazi kutokuwa na muda na watoto wao leo hii uzao wa ma-house girl ndio unaotawala dunia au watoto wanalelewa katika vituo vya malezi au shule za boarding zisizo na uadilifu wa kidini na kumruhusu shetani kuharibu kabisa maisha ya kizazi hiki, wahubiri wengi wako busy na kazi wanazozifikiri kuwa ni za Mungu na wamepoteza uhusiano wa karibu na Mungu, watu wanazunguka huku na huko wakiwahubiri wengine lakini wao wamepoteza kabisa uelekeo, watu wamekuwa busy na kazi na kusahau wajibu wao wa kujijenga wao binafsi, watu hawana muda wa kusali, hawana Muda wa kusoma hata neno la Mungu na hata kukidhi haja za tendo la ndoa kwa wanandoa wengi leo hii unasikia tu nimechoka nimechoka kila kitu kinaparaganyika kwa sababu watu wamesahau kutunza shamba lao la mizabibu, uko busy na maisha ya wengine yako je? Waimbaji wanashinda studio kurekodi nyimbo zitakazoburudisha wengine na kuwajenga wengine na hata kuokoa wengine lakini katika familia zao mambo yanaparaganyika Kiroho chako je, nyumba yako je? Mke wako? Mume wako je ? watoto wako je? Maisha ya watu wengi yameharibika na mashamba yao ya mizabibu yameota magugu kwa sababu wamesahau wajibu wao wa kutunza mashamba yao ya mzabibu pia maisha yao ya binafsi, watu wameshindwa hata kufanya mazoezi kwaajili ya afya zao, busy busy busy na wamejawa na stresses kibao wamekuwa weusiwesu japokuwa wana uzuri ndani yao lakini nini kimewaharibu wamesahau wajibu wao wa kuwa na Mungu binafsi, hali inasikitisha mno sasa, watu wamesahau kushughulikia maswala muhimu yanayowahusu, jua limewapiga wamepoteza uzuri wao wamechakaa na kuwa weusiwesui sababu ya kutunza mashamba ya wengine na kusahahu mashamba yao ya mizabibu. Mungu wangu!  Hapa simaanishi kuwa zile kazi tuzifanyazo sio za muhimu hapana lakini namaanisha unaporudi katika maswala ya msingi unafanya nini kwaajili yako na kwaajili ya familia yako na kwaajili ya maendeleo yako ya kimwili, kiakili, kiroho na kisaikolojia lakini vilevile ya watu wale wa karibu wanaokuzunguka tunawezaje kuangalia mambo yetu?

Wajibu wa kutunza shamba lako la mzabibu.

1.      Moyo wa Kiasi – Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;” ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi leo wanaharibikiwa kwa sababu ya kukosa moyo wa kiasi, neno kiasi maana yake ni “Self-control, au Displene”  yaani ni swala la kujitia nidhamu, yaani mtu anakosa kiasi, wako watu wengine wanakunywa pombe kiasi ambacho wanahatarisha maisha yao na kazi zao na za wengine pia, ni abubu kufukuzwa kazi au kuitwa na kiongozi wako na kuonywa kwa sababu ya ulevi, wengi siku hizi hawana muda wa maongezi na watoto wao, wake zao na familia zao, kwani wanaporejea nyumbani ndio wanapata wasaa wa kuoga na kula na kutulia wakifuatilia tamthilia za aina mbalimbali, na wengine wanataka kila tathilia iliyo nzuri waifuatilie, watu wako kwenye facebook, twiters, instergrams na mitandao mingine ya kijamii wanajua kila kinachoendela lakini kama haitoshi hatra muda wa kazi wengine wameshindwa kujicontrol na wamekuwa busy na simu zao, laptop zao wamekosa muda wa kuwaweka sawa watot  kuongea na wapenzi wako na wengine huko huko wamenaswa na mapenzi yasiyo rasmi, tatizo kubwa watu wameshindwa kuwa na kiasi na kujitia nidhamu.

2.      Kuukomboa wakati – Waefeso 5:15-16 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.” Maandiko yanatuonya kwamba tunapaswa kuenedna kwa hekima katika nyakati hizi tilioznazo ambazo ni nyakati za uovu na kwamna inatupasa kuenedna kwa kuukomboa wakati, Katika wakati huu ni muhimu kuyapa kipaumbele  mambo yaliyo ya muhimu na kuyapa kipaumbele, inasemekana katika utafiti wa kitaalamu kuwa Marekani watu hutumia wastani wa masaa 30 kwa wiki wakiangalia TV,  katika zama hizi za uovu ni muhimu kupangilia muda (time management) na kujipangia mambo ya kufanya, wapi utakuwa na marafiki zako, wapi lini na muda gani utakuwa na familia zako, ni muda gani utaabudu na kusoma neno la Mungu na kuomba na kufundisha familia yako na kusikiliza mahubiri  nakuhudhuria ibada, wengi wameshindwa kutunza shamba lao wenyewe la mizabibu kwa sababu wamemezwa na mifumo ya ulimwengu huu.

3.      Ondoa kila tawi lisilozaa Yohana 15:2 “Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.” Lazima ufanye Pruning yaani kuondoa maatawi yasiyozaa, matawi ambayo yatazuia matawi yenye afya ya kuzaa matunda, lazima ujue na kukubali kuwa yako mambo yasiyofaa katika maisha yetu yanahitaji kuachwa yanahitaji kuondolewa ili mambo yako yaweze kufanikiwa, wako wengine wamebeba mizigo ya watu wengine wana uchungu hawajasamehe, wengine wana uchungu na wake zao na watoto wao na waume zao na wazazi wao maombi yao yanazuiliwa na hakuna mafanikio kwa sababu mzabibu wake binafsi haujapaliliwa umesongwa hawajapogolea matawi ya muhimu ili mzabizu uweze kukaa matunda kwa wakati wake, lazima umuombe Mungu aondoe pando asilolipanda yeye Mathayo 5:29-30

4.       Hakikisha kuwa unasafisha tawi lizaalo Yohana 15:2Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”  Tawi lizaalo pia linapaswa kusafishwa, wakati tawi lisilozaa huondolewa lizaalo linapaswa kusafishiwa 1Wakoritho 6:12 Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.”  1Wakoritho 10:23Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.” Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila kitu kisichompendeza Mungu tunakiacha, tunakitupilia mbali 2wakoritho 7:1 na 2Timotheo 2:19-22 lazima tufanye hayo ili bwana atutumie.

5.      Hakikisha kuwa unajitunza na kujirutubisha hii ni hali kama kumwagilia, kuwekea mbolea na katika udongo wa shamba lako, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunakuwa na Muda wa ukimya na Mungu, tunaomba, Mathayo 6:6 tunasoma neno la Mungu 2Timotheo 2:15 ili kunufaisha roho zetu na kustawisha uhusiano wetu na Mungu.

6.      Hakikisha kuwa unajilinda yaani kama tumechukua hatua za kujitakasa na kuachana na dhambi na kujiimarisha katika neno la Mungu na uhusuiano wetu na Mungu, sasa ni vema kwetu tukahakikisha kuwa tunalilinda shamba letu la mizabibu hususani na mbeha wale wadogo waharibuo mizabibu Wimbo uliobora 2:15, vitu vinavyoharibu na kutuondolea uwepo wa Mungu sio vile vikubwa bali ni vile tunavyovizarau na kuviona vidogodvidogo Zaburi 139:23-24

Hatuna budi kumshukuru Mungu na kumfurahia kwa kila alilolifanya kwaajili yetu na kila wajibu alioutupa kuutekeleza duniani, lakini hatuna budi kuwa makini na kuhakikisha kuwa tunaendeleza maisha yetu ya kiroho ya ndani ya familia zetu wakati tunaposhughulika na mengineyo, tuhakikisha tunadumisha uhusiano wetu na Mungu na kufurahia uwepo wake kila iitwapo leo, nasi tutakuwa na uzuri

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.” 

Jumapili, 3 Machi 2019

Maana Mungu hakutupa roho ya woga.


2Timotheo 1:3-7.

Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie ;tazama,Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5

Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa kuna aina mbili za hofu, hofu ya kwanza ni hofu yenye manufaa, hofu yenye faida, aina hii ya hofu ndio inayotufanya tuogope kujiumiza, au tuogope kufanya mambo mabaya, na tuweze kumcha Mungu na kuogopa kutenda maovu hii ni hofu njema na yenye ufanisi, Lakini hofu ya pili ni hofu mbaya,  aina hii ya hofu ni hofu yenye hasara ni hofu mbaya na ni roho hii ndio hofu ambayo maandiko yanatufundisha kuwa haitokani na Mungu ni hofu mbaya sana na ni hofu inayowafanya wengi waogope kuthubutu au kufanya jambo.

Hofu ya Mungu.

Hofu ya Mungu huambatana  pamoja na baraka nyingi na faida. Ni mwanzo wa hekima na inaongoza kwa uelewa mzuri Zaburi 111: 10. “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.” Pia unaweza kuona katika Mithali 1: 7Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”. Zaidi ya hayo, hofu ya Bwana inaongoza kwa maisha, pumziko, amani, na ridhaa Mithali 19:23.Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya” kumcha bwana kunaongeza Maisha ni chemichemi ya uzima inayoepusha na mauti Mithali 14:27 “Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti” Kwa msingi huo hofu ya Mungu yaani lkumcha Mungu ni jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu na ndani yake  Nguvu, upendo na moyo wa kiasi hofu hii inafaida kubwa sana na biblia imewekea mkazo umuhimu wa aina hii ya hofu.

Roho ya woga (Hofu isiyotokana na Mungu)

Katika mstari wa msingi tuliousoma sasa Paulo mtume anaorodhesha aina nyingine ya Hofu na anamuieleza Timotheo kuwa hofu hii haitokani na Mungu wala Mungu hatupi hofu ya aina hii na zaidi sana anaiita hofu hii “ROHO YA WOGA” maana yake ni kuwa ainha hii ya hofu ni dhahiri kuwa inatokana na shetani ni hofu mbaya  2 Timotheo 1: 7: "Kwa maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi."

Katika Biblia ya kiyunani neno hili roho ya woga linaweza kutafasiriwa kama Hali ya kujiona Duni, “inferiority complex”  hili ni tatizo kubwa la kisaikolojia linaloweza kuwapata hata watu wa Mungu, hata watu ambao wamekua vizuri katika imani, lakini kwa vile ndani wanajiona duni basi wanafikiri kuwa wao hawafai, wanaogopa, wanaogopa wanadamu, wanamuogopa shetani, wanaogopa ni namna gani watazungumza mbele za watu, wanaogopa kukosea, wanaogopa kwa sababu hawajui kiingereza vizuri, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu fulani wa mwilini ambao wanao, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu katika roho zao, na kwa sababu hiyo wanadhani kuwa hawataweza kufaa kwa namna yoyote kuwa watumishi wa Mungu, wana jiona duni, wanajiona hawafai na hivyo wanajumlisha na kutoa na kupata jawabu kuwa hawasytahili kuwa wachungaji, waisnjilisti au walimu, mitume na manabii kwa sababu eti hawatoshi katika vipimo vya Mungu.

Hali ya aina hii ndio aliyokuwa anaipitia Timotheo, aliwekwa kuwa mwangalizi wa Kanisa la Efeso, hili lilikuwa moja ya Makanisa makubwa sana nyakati za kanisa la Kwanza, Na Timotheo alikuwa tayari amekwisha chunga kanisa la Thesalonike, lakini Timotheo alikuwa ni kijana mdogo, na alikuwa akiugua mara kwa mara lakini alitiwa moyo kwa uwepo wa Paulo mtume, hofu ya aina hii bila shaka halikuwa tatizo kwa Timotheo lakini Paulo alijua kuwa kwa vile Paulo alikuweko Duniani, aliweza kumtia moyo Timotheo lakini sasa Paulo yuko gerezani na siku zake za kuondoka Duniani zilikuwa zinakaribia na alijua kuwa kwa vyovyote vile Timotheo angeogopa au angepoteza ujasiri na sasa anataka kumtia moyo kuwa asiogipe hofu ya aina hii sio sehemu ya maisha ya mtu aliyeokoka.
Mungu hajatuita, tuwaogope wanadamu, Mungu hajatuita, tuogope kusimama mbele ya umati mkubwa wa watu, Mungu hajatuita tuwe waoga, Mungu hajatuita tuwe duni miongoni mwa wanadamu, waluimu wa uongo na kazi za shetani na nguvu za giza kinyjme chake sisi tuna Roho Mtakatifu, Roho wa Bwana, tuna roho ya nguvu, tuna roho ya hekima, tuna roho ya uchaji wa Mungu, tuna roho ya Ushauri, tuna roho ya maarifa na ujuzi Isaya 11:1-2 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;

Roho ya ya woga haitoki kwa Mungu. 

Hata hivyo, wakati mwingine sisi uhofu, wakati mwingine hii "roho ya woga"inatulemea, na kuishinda tunapaswa kumwamini na kumpenda Mungu kabisa . "Hakuna hofu katika upendo. Lakini upendo kamili unatoa nje hofu, kwa maana hofu inatumika na adhabu. Mtu mwenye woga hajafanywa mkamilifu katika upendo "1 Yohana 4:18. Hakuna mtu mkamilifu, na Mungu anajua hilo.  Mungu wakati mwingine hataondoa kabisa madhaifu tuliyo nayo lakini badala yake atataka tumtegemee yeye hivyo hivyo hivyo pamoja na udhaifu wetu naye ataleta utoshelevu wa neema na upendo wetu kwetu kwaajili ya utukufu wake, kamwe usingije eti uwe mkamilifu kisha ndio umtumikie Mungu, Biblia inatuhimiza wakati wote tusiogope, Roho ya Hofu ina nguvu sana ya kuharibu vipawa na uwezo wa watu, na ndio maana Mungu anataka tumuamini, bila kujali kuwa tuna umri mdogo, au hatuna elimu ya kutosha, au hatujui kiingereza, au hatuna ujuzi na jambo fulani.
Isaya 41:10 inatuhimiza, "Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifahdaike, kwa maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu, maana nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Zaburi 56:11 "Nimemtumaini Mungu sitaogopa, mwanadamu atanitenda nini?" 

Yeremia 1:5-8Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”

Joshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.  Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

Mungu wakati wote atatoa neema kwa kila aina ya ulemavu tulio nao anajazilizia, nimekutana na watu ambao hawakusoma kabisa lakini wana akili za ajabu sana, Bibi yangu alikuwa ni moja ya watu waliokosa elimu kabisa wakati wa Mkoloni, alitokea familia duni, lakini yeye ndiye aliyekuwa analima na kulisha watu nyumbani, wenye fedha walikuwa wakinunua mboga tu, lakini ugali na mahindi na mihogo bibi alileta kutoka shambani, alisimamia watoto wake wote wakaenda shule na kuelimika na kuwa watu wakubwa, leo tuna wanasiasa, wakubwa, tuna askari, tuna mainjinia, tuna pilisi, tuna usalama wa taifa, tuna walimu, tuna madereva, tuna mafundi, mchundo, waashi, lakini walilelewa na Bibi ambaye hakusoma Mungu atakupa neema katika mapungufu uliyonayo, Usiogope simama na mtumikie Mungu kwa kile Mungu alichoweka ndani yako Usiogope Mungu hakutupa Roho ya woga. Uwe na ushujaa Yesu ni Simba wa kabila la Yuda tukiwa naye msituni hatupaswi kuhofia lolote.

Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5

Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.
0718990796.

Jumatatu, 25 Februari 2019

Tukalia tulipoikumbuka Sayuni!

Zaburi 137: 1-4 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

 
Utangulizi: 
  
Kila mwanadamu katika maisha yake ana historia ambayo imejaa milima na mabonde katika mapito mbalimbali ya maisha, Ukimuuliza mtu swali akuelezee au akuandikie siku ambayo hatakuja kuisahau katika maisha yake kwamba siku ambayo ilimpa furaha kubwa sana (Golden Age) au siku ambayo aliwahi kuuzunika sana (Ashes Age) utaweza kugundua kwamba wengi wataandika siku zao ambazo hawatazisahahu katika maisha yao kutokana na huzuni na mapito mazito waliyoyapitia.
Wengine wataeleza siku yao wasioweza kuisahahu kama siku ya harusi yake, au siku ya msiba wa mtu wake aliye karibu, au siku timu yake ilipofungwa, au siku timu yake ilipopata ushindi, au siku alipopata kazi, au siku alipofukuzwa kazi, kila mmoja anaweza kuelezea siku yake ya huzuni za wakati wake wa furaha hii ni hali ya kawaida katika maisha ya mwanadamu, na ndio maana waswahili wanasema maisha ya mwanadamu yana milima na mambonde. Halii hii pia inaweza kugusa hata taifa fulani au bara fulani na kadhalika. 

Zaburi hii ya 137:1-9 imegawanyika katika sehemu kuu tatu. 

·         Mstari wa 1-4 inaelezea hali halisi ya huzuni waliyokuwa nayo wayahudi huko utumwani, walilia na walivitundika vinubi vyao juu ya miti kwa sababu wasingeliweza kuimba wimbo wa kumuabudu Mungu ugenini 

·         Mstari 5-6 inaelezea jinsi walivyojipa moyo na kujiapiza juwa haitakuja itokee waisahau Sayuni yaani Yerusalem yaani uwepo wa Mungu, na ni afadhali kusahahu mkono wa kulia au kuwa bubu kuliko kuisahai Sayuni 

·         Mstari 7-9 jamaa anaomba kwamba Mungu ashughulike na Babeli pamoja na Edomu ambao walishangilia kuangamia kwa Wayahudi na kuboibmolewa kwa Yerusalem    

Katika kifungu za Zaburi hii leo tunaweza kupata picha ya wana wa Israel waliorejea kutoka utumwani, ambao walishuhudia uzuri wa Taifa lao lilipokuwa chini ya uongozi wa Mungu na baadaye lilipoadhibiwa na kuruhusiwa kwenda utumwani 

Zaburi 137:1-4Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Mwandishi wa zaburi hii japokuwa wengine wanadhani ni Yeremia lakini mimi bila shaka naamini atakuwa Ezra au mojawapo ya watu waliorejea kutoka uhamishoni  kwa sababu anajaribu kuelezea hali halisi waliyoipitia walipokuwa nje ya Israel yaani utumwani huko Babeli, na historia haionyeshi kuwa yeremia alikwenda uhamishoni Babeli kama ilivyo kwa Ezekiel na Daniel, kwani inasemekana huenda yeye Yeremia alikwenda Misri.  Ingawa nchi ya Babeli yaani Iraq na Iran ya leo zilikuwa na mito mkubwa na mizuri na yenye matawi mengi sana yaliyochangia taifa hilo kuwa na uwezo mkubwa wa kujitosheleza kwa chakula na umwagiliaji na ujenzi ulioruhusu maji kupita katikati ya majiji yao mito kama Mto Kebari, Mto Frati na mto Tigris na ustaarabu mkubwa na wa hali ya juu, Babeli ulikuwa mji wa kifahari sana ndio ulikuwa mji wenye bustani zinazoelea angani na kuingizwa katika moja ya maajabu saba ya kale ya dunia (The Seven wonders of the ancient world ) ukiacha pyramid la Chiops lililoko Gezer nchini Misri hata leo, Bustani na uzuri wa jiji la Babeli lilikuwa linashika nafsi ya pili kwa ajabu zake duniani, Mfalme Nebuchadnezar aliwahi kujisifia kuhusu ujenzi wa mji huu na akaadhibiwa na Mungu kwa kiburi chake akidhani kuwa alifanya kwa nguvu zake na utukufu wake  

Daniel 4:29-33 “Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.” 

Unaweza kuona Babeli kulikuwa ni kuzuri sana kuliko hata Sayuni, lakini wana wa Israel walilia walipoikumbuka Sayuni kwanini? Unaweza kuwa na ndoa ya kifahari sana lakini huo sio uthibitisho wa furaha ya kweli, unaweza kuwa na kila kitu lakini kama Mungu hamo haiwezi hiyo kitu kukupa furaha ya kweli unaweza kuwa katika nchi iliyoendela sana lakini hili sio suluhisho la furaha ya kweli ya mwanadamu, unaweza kuwa na mume mzuri na mke mzuri lakini bila uwepo wa Mungu ni sawa na shamba la miwa karibu na shule ya msingi, wako watu wengi wanalia japokuwa wanaishi katika mageti, na nyumba nzuri, na magari mazuri si dhambi kuwa navyo lakini the best ni kuwa na uwepo wa Mungu, Mungu ndiye furaha yetu ya kweli, Elimu na ujuzi na maendeleo hayatupi guarantee ya uhakika wa furaha yetu.

Kwa nini walilia walipoikumbuka sayuni?

Wayahudi waliketi na kutafakari, kwamba wao ingawa walikuwa katika nchi nzuri sana yenye mito mingi, Machozi yaliwatoka kwa sababu sasa walikuwa wametengwa mbali na uwepo wa Mungu, walipotafakari juu ya Nyumba ya Mungu iliyokuwako Sayuni yaani Yerusalem, walipokumbuka makaburi ya baba zao, walipokumbuka sikukuu zao namna na jinsi walivyokuwa wakipanda kwenda kumuabudu Mungu wa baba zai Ibrahim na Isaka na Yakobo, Jinsi walivyokuwa na fahari kuu wakati wa utawala wa Daudi na Solomon, walikumbuka walivyokuwa wakikwea kwenda kuabudu na makuhani wakiwaongoza, walivyokuwa wakitoa sadaka za kuteketeza na kumuabudu Mungu wa kweli kwa furaha na uhuru wao waliokuwa nao, jinsi walivyotumia vinubi na vinanda kumsifu na kumuheshimu Mungu huu ulikuwa ni wakati ambao ni kama golden age kwao, ulikuwa ni wakati wa furaha

Sasa Israel wako utumwani hawana uhuru wao wenyewe, hawawezi kuabudu kama walivyozoea, wanapangiwa kila kitu, waliowachukua mateka wanawasanifu wanasema wawaimbie kama walivyokuwa wakiimba huko sayuni, wakati wao wakiwa na huzuni waliowateka kama mateka wanataka waimbiwe wanataka wafurahie, wao kwao ilikuwa ni swala gumu, uzuri wa Babeli haukuwa na maana kwao, walikumbuka misiba mikubwa, walikumbuka walivyoamuriwa wawaue ndugu zao kwa upanga, wamepoteza mali zao, hawana mashamba yao, hawana nyumba zao,  hawana serikali yao, hawana wafalme wao matumaini waliyokuwa nayo yametokweka, walikumbuka mateso waliyoyapata, walikumbuka walivyochomwa moto, walikumbuka manabii waliokuwa nao, walikumbuka jinsi Mungu alivyowadekeza na kuwapa kila walichokihitaji, sasa ni kama mbingu zimefungwa, ni kama wameondolewa kwenye uwepo wa Bwana, hakuna tena hekalu kubwa kama lile la Sulemani,Unawezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya Ugenini

Waliikumbuka Sayuni waliikumbuka Yerusalem, waliweka nadhiri na kujiapisha kuwa hawatakuja waisahau Yerusalem na kama ikitokea ni sawa na kusahahu mkono wa kulia au mdomo ugande kwa kushikana na ulimi kuliko kuisahau Israel, lakini pia walikumbuka jinsi wakati wanaondoka watu wa Edomu walikuwa wakishangilia kuharibiwa kwa mji huo Bomoeni bomoeni bomoeni walisema na pia waliomba kisasi dhidi ya Babeli kwamba isiachewe salama 

Zaburi 137:5-9 “Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau. Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini! Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia, Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi. Heri yeye atakayewakamata wadogo wako, Na kuwaseta wao juu ya mwamba.” 

Hivi ndivyo inavyotokea katika maisha yetu na maisha ya kanisa la Mungu, hakuna jambo ba ya sana kama kutengwa mbali na uwepo wa Mungu, hatuwezi kufurahia fahari za dunia na dhambi, hatuwezi kuabudu kwa uhuru ikiwa tumechukuliwa mateka, aidha inatia uchungu sana wakati unapopitia mambo magumu kisha wakawepo kando watu wa kufurahia unayoyapitia au kuunga mkono kile unachokipitia, Maandiko yanaonyesha kuwa mwandishi aliomba Mungu akutane na watesi na mashabiki wao pia awalipize kisasi, hatuwezi kuwa na furaha kamili kama maadui zetu wanaisshi na wanashangilia kuangamia kwetu, ni lazima Mungu afanye kitu ili yamkini hata kama wanaishi waweze kuona na kujua kuwa Mungu hawatupilii mbali watu wake, ni lazima wasikie na wajue, Mungu awapatilize,  Natangaza habari njema kwako ya kuwa uko wakati wako wa golden age unakuja ikiwa utakubali Yesu Kristo akutawale, jitegemeze kwake yeye atakutetea anatayafuta machozi yako yote nawe utapata raha nafsini mwako, jitie katika utawala wake nawe utaonja ya kuwa Yesu hatakuacha yeye ni mwema katika maisha yako, hatakusahau kamwe. Kumbuka kurudi katika uwepo wa Mungu, usikubali kutengwa mbali na uwepo wake, uwepo wa Mungu ndio furaha ya kweli, ndio ushindi wa maisha yetu, kila kitu kitakuwa na maana kwetu iwapo tutajikinga katika uwepo wake Zaburi 27:1-4, wale wote wanaotazamia kuwangamia kwetu lazima wajue na wasikie kuwa Mungu wetu yu hai nay a kuwa anafanya kazi kubwa ya kutukomboa pale tunapojitegemeza kwake.

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.