2Wafalme 14-19 “Basi Hezekia akaupokea
waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda,
akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. Naye Hezekia
akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya
makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe
ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua
macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu
aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru
wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana
haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu,
ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono
wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe
Bwana Mungu, wewe peke yako.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko
yanatufunduisha kuwa maombi ndiyo nyenzo pekee inayoweza kutusaidia wakati wowote tunapokutana na changamoto za
aina yoyote zile tuwapo duniani, Jambo lolote ambalo linaweza kukuletea fadhaa
katika maisha yako au familia yako, au taifa lako, tunaelekezwa kuwa wakati wa
changamoto hizo ziwe za kitaifa, au kifamilia au za taasisi au mtu mmoja mmoja
kwamba tumtwike yeye fadhaa zetu zote angalia
1Petro 5:7 “huku mkimtwika yeye fadhaa zenu
zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Unaona sio fadhaa ya mtu mmoja
mmoja tu bali hata fadhaa za kitaifa au kitaasisi au familia, Mungu anatuthibitishia
wazi katika neno kuwa atasikiliza maombi yetu ona 2Nyakati
7:13-15 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena
nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu,
walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na
kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi
yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu
yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”
Ni kupitia maombi Mungu atakutana
na mahitaji yetu yote kwa kadiri ya
utajiri alionao katika Kristo Yesu Wafilipi
4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”
Katika kifungu cha maandiko ya
msingi Mfalme Hezekiah anaomba Hekaluni Nyumbani mwa Bwana, Hezekia alikuwa
ameletewa ujumbe kwa njia ya Barua kutoka kwa mfalme Senekarebu ambaye alikuwa mfalme mkubwa na mwenye nguvu
katika nyakati zile, mfalme huyu aliweza kuwa na historia ya kuwa mshindi kwa
kila taifa ambalo lilipigana naye
alipiga kila taifa na kila ufalme pamoja na miungu yao na kuichoma moto
na sasa mfalme huyu alikuwa anaukaza uso wake kumjia Hezekiah kwa maana
nyingine kumjia Hezekia pamoja na Mji wa Yerusalem na Israel kwa ujumla, Lakini
kabla ya kumjia aliamua kumpa taarifa ya kile alichokusudia kuja kukifanya ona
2Wafalme 18:28-37 “Kisha yule amiri
akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno
la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa
maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake. Wala Hezekia asiwatumainishe katika
Bwana, akisema, Hakika Bwana atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa
mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi,
Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake
na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe; hata
nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na
divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na
asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema,
Bwana atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati
wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi?
Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na
mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao
na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala
hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno.
Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na
Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa
Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule amiri.”
Vitisho hivi vilikuwa vitisho vya
kweli, Mfalme Senekarebu alikuwa ameshiba kiburi cha ushindi wake kila mahali
alikopita, alipiga mataifa na miungu yao aliichoma moto, Hezekia alikuwa hana jinsi ya aina yoyote ya kufanya ilikuwa
lazima akubali kushindwa na kuweka silaha chini na kukubali kulipa kodi kwa
Mfalme Senekarebu, au aingie kwenye mapigano, ilikuwa ni rahisi katika wakati
kama huu kwa Hezekia kutafuta ushauri wa kibinadamu, au kuuliza kwa wenye
hekima, au aingize majeshi yake vitani
au awe tayari kuharibiwa au
kukutwa na jambo baya tu huku macho yake yakishuhudia, Hezekia aliwashauri watu
wake wasijibu kitu, Moyoni mwake alikuwa anajua, Mungu wa Israel ni Mungu wa
tofauti na kuwa Mungu wetu ndiye Mungu wa falme zote za dunia, hivyo hangeweza
kutafuta msaada wa kibinadamu, au msaada wa kijeshi kutoka kwa mataifa rafiki,
Yeye alijikita katika kuutafuta uso wa Mungu aliye hai Mungu wa falme zote za
dunia, na hivyo Ndipo mfalme Hezekia alipoamua kumuomba Mungu na kupeleka zile
nyaraka za vitisho alizoandikiwa kwa
Mungu wa Falme zote za dunia kwa kuwa
alimjua Mungu na kumtegemea alimsifia kutoka moyoni akitambua kuwa ni Mungu
pekee mwenye uweza wa kumsaidia ona
2Wafalme 14-19 “Basi Hezekia akaupokea
waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda,
akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. Naye Hezekia
akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya
makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe
ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua
macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu
aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru
wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa
miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo
sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake,
nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana
Mungu, wewe peke yako.”
Hezekia alikuwa anataka Mungu
atukuzwe, alikuwa anataka Mungu ajidhihirishe mwenyewe kuwa yeye ni Mungu wa
wote wenye mwili, na kuwa hakuna lisilowezekana kwake, Hezekia alimsifu Mungu,
Hezekia hakuwa na woga alikuwa na ujasiri mkuu alimsihi Mungu aone yeye
mwenyewe na kusikia maneno ya Senekarebu alionyesha ya kuwa anamtegemea Mungu
tu na sio wanadamu, wala hekima ya kibinadamu, alimwambia Mungu ni kweli
Senekarebu ameshambulia mataifa mengi na miungu mingi ameichioma moto na
kuziharibu lakini hiyo haikuwa miungu na hayo mataifa hayakumjua Mungu aliye
hai, lakini yeye alijitegemeza kwa Mungu mwenye uwezo mkubwa sana ambaye
alimtambua kama Mungu wa falme zote za Dunia nani ukweli kuwa Mungu alimjibu Hezekia kwa
njia rahisi sana, Mungu ni Mungu anayesikia aliyasikia maombi ya Hezekiah na
kuyajibu ona kwa kinywa cha Nabii
Isaya
2Wafalme 19:32-34 “Basi Bwana asema hivi
katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga
mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake.
Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya
mji huu, asema Bwana. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu
mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.”
Wakati huu Mungu aliona afupishe
safari ya mfalme Senekarebu kwa kumtumia malaika wake mmoja tu, ambaye
aliwatandika jeshi zima na Senekarebu akarudi nyumbani kwake kwa njia ile ile
aliyoijia sawa na lile neno ambali Bwana alinena kwa kinywa cha nabii Isaya, na
kwenda kuuawa na watu wake mwenyewe ona katika ;-
2Wafalme 19:35-37 “Ikawa usiku uo huo
malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na
themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao
walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda
zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki,
mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya
Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.”
Ziko vita nyingine ambazo watu
watadhani uko mwenyewe kumbe liko jeshi la malaika nani makomandoo, Mungu na atume malaika wake akusaidie katika kila
changamoto unazokutana nazo, Wakati huu Mungu alimtumia malaika mmoja tu
aliyepiga watu 185000 kumbuka hii ilikuwa ni kwa watakatifu wa agano la kale,
katika agano jipya tunaambiwa kuwa Malaika ni roho wanaotumwa kuwahudumia wale
watakaourithi wokovu ona Waebrania
1:13-14 “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo
wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo
zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi
wokovu? ” unaona umuhimu wa kumuomba Mungu msaada wako utakujaje
Bwana anajua wewe tambua tu kuwa ndiye anayemiliki tawala zote za dunia,
ninakuombea kwamba katika hali uliyo nayo Bwana Mungu na atume malaika
wakabiliane na changamoto unazokutana nazo, wala usiogope liamini neno hili
ambalo Bwana amenipa kwaajili yako nakuhakikishia hutalia tena wala
hutafadhaika nina Mungu aliye hai kama wa Hezekia Na Mungu wangu atakutana na
changamoto zako zote zinazokukabili kwa ushindi mkubwa, kisha wataaibika
wanaoshindana nawe!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye hekima!