Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema
nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Utangulizi:
Ni muhimu kujikumbusha kwamba
moja ya agizo muhimu sana kwa wakristo wote duniani kutoka kwa Bwana wetu Yesu
Kristo ni kuhakikisha kuwa watu wote duniani wanaisikia habari njema yaani
injili, watu wengi sana huwa wanajisahaulisha kuhusu jambo hili la Muhimu,
nimetumia miaka mingi sana kuwatia moyo, na kuwajenga kiimani na kuwafunulia neno
la Mungu kama Mwalimu wa neno lake, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kama
nitasahau kukazia jambo hili la Muhimu,
najua kazi niliyokuwa nikiifanya ni sehemu ya injili lakini nasukumwa sana
kuzungumzia injili kwa sababu kuna maonyo ya kimaandiko kwetu endapo tutaacha
kusema kuhusu habari njema, kwa sababu ni sharti yaani ni lazima kuihubiri
injili
1Wakorintho 9:16-17 “Maana, ijapokuwa
naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu;
ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.”
Kazi ya kuhubiri injili imetoka
katika agizo la kiongozi mkubwa zaidi Duniani na ni kazi ya Muhimu, kanisa
yaani watu wa Mungu hawapaswi kwa namna yoyote kupuuzia agizo lake, pamoja na
kuwajibishwa kwa watu wasiohubiri injili, lakini kuna madhara makubwa sana kwa
ulimwengu kuharibiwa na kazi za shetani, mmomonyoko wa uadilifu, kukosa Nuru,
kukosa chumvi, na kuingiliwa kwa ulimwengu na falsafa za giza zilizo kinyume na
injili zitaenea na kuifanya dunia kuingia gizani kinyume kabisa na namna Yesu
anavyotutarajia tufanye! Endapo tuntutapuuzia swala la kuihubiri injili, Kwa hiyo tuna wajibu wa kuihubiri injili na
hii ni kazi ya kila muungwana aliyeamini
duniani!
Tutajifunza somo hili umuhimu wa
kuihubiri injili kwa kuzingatia vipengele vinne muhimu vifuatavyo:-
·
Maana ya
neno injili.
·
Umuhimu
wa kufanya uinjilisti.
·
Madhara
ya kuacha kuhubiri injili.
·
Namna
nyepesi ya kuifikisha injili
Maana ya neno Injili.
Neno injili limetokana na neno la
kiingereza Evangelism ambalo kwa
kiyunani ni EUANGELIUM na kwa kilatini ni GOSPEL ambalo maana
yake (Good Story) au (Good News)kwa Kiswahili Habari njema,
au kuwaeleza watu habari nzuri, habari za matumaini au habari za kutia moyo.
Mfano Kama watu walikuwa na njaa
mbaya sana kiasi cha kula kichwa cha punda au kiasi cha wanawake kula watoto
wao kwa zamu, kisha ghafla watu hao wakatangaziwa kuwa mahindi, au ngano au
unga au chakula kitapatikana kwa bei nafuu sana basi hiyo ni habari njema
angalia mfano ona
2Wafalme 6:24-30 “Ikawa baada ya hayo,
Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru
Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha
punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya
njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita
ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme.
Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya
shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia,
Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa
mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye
amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke,
aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona,
na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.”
2Wafalme 7:1-11 “Elisha akasema, Lisikieni
neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri
kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa
Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu
yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni,
je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho
yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la
mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini,
mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile.
Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua,
tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha
Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana
Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo
cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa
Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane
nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao,
na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa,
wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho
wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na
dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya
pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana,
Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya HABARI NJEMA, na sisi tunanyamaza;
mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie
watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji;
wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko,
wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama
walivyoziacha. Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.”
Unaweza kuona ukilinganisha hapo
juu habari mbaya ya njaa mbaya iliyokuwepo zamani za Nabii Elisha na tangazo la
Nabii Elisha na muujiza wa wale wakoma waliovumbua kuweko kwa chakula uvumbuzi
kuhusu kuweko kwa chakula katika Samaria wakati kukiwa na njaa mbaya
iliyopelekea wanawake kula watoto ilikuwa ni habari njema!
Ulimwengu tulio nao umeharibika,
shetani na malaika zake wameiharibu dunia, uadilifu wa mwanadamu umeathiriwa,
uhusiano wa Mungu na mwanadamu umeharibika, wanadamu wote tunafahamu kuwa
tumeharibikiwa hatustahili tena kuwa na uhusiano na Mungu, tunastahili hukumu
ya Mungu, tunastahiki kifo tunastahili adhabu, tunastahili kutupwa motoni,
tunastahili kuharibiwa, tunastahili kukataliwa hatufai kwa sababu hakuna mtu
mwenye nia ya kutafuta uhusiano mwema na Mungu tumeharibika tumeoza wanadamu
wote kama yasemavyo maandiko ona
Warumi 3:10-12 “kama ilivyoandikwa, ya
kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye
Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”
Katika mazingira kama haya ya
haribiko kubwa la mwanadamu anapotokea Mtu anatangaza kuwa Mungu amesamehe
maovu yetu yote kwa sharti moja tu na sharti hilo ni kumuamini Mwanaye ambaye yeye
alimtoa aadhibiwe yeye kwa niaba yetu pale msalabani na kuwa kazi tunayotakiwa
sisi ni kuamini tu, na kuamini ni kukubali tu na kukiri na kushukuru na kwa
kuamini huko hatutahukumiwa na tunahesabika kuwa watoto wa Mungu tukipewa haki
sawa na mtoto wake aliyeishi maisha ya haki hizo sasa zinakuwa ni habari njema
kwetu! unaona
Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali
ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini
amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”
Unaona sasa kupitia kazi hii
aliyoifanya baba kwa upendo wake tukimuamini mwana wake tumeokolewa,
tunasamehewa hatuhukumiwi hizi ni habari njema ambazo kila mwanadamu zinapaswa
kumfikia na ni kwa sababu ya haya Kristo alikuja ulimwenguni na kutoka katika
kuamini tunasimama imara na kuokolewa, na kusamehewa na kubadilishwa mwenendo
wa tabia na maisha yetu kwa neema tu kupitia nini kupitia kazi aliyoifanya Yesu
pale msalabani
1Wakorintho 15:1-4 “Basi, ndugu zangu,
nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo
mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri
isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale
niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu,
kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya
tatu, kama yanenavyo maandiko;”
Umuhimu wa kufanya uinjilisti.
Kusudi kubwa la Mungu kumtoa
mwana wake wa pekee kuja ulimwenguni ni ili apate kuwaokoa wanadamu
watakaomwamini, na wale wote ambao hawataamini watahukumiwa
Yoahana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini
amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”
Sasa ili watu waweze kukolewa
ilikuwa ni lazima waisikie injili na wakiisha kuisikia injili, waiamini na
wakiamini kwa maneno na vitendo yaani kubatizwa na kuwa wanafunzi wa Yesu na
kusimama katika imani waokolewe, kwa hiyo tunajifunza ya kwamba watu hawawezi
kuamini mpaka wasikie tena wasikie habari za Yesu
Marko 16:15-16 “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini,
atahukumiwa.”
Habari za Yesu Kristo ni lazima zihubiriwe
kwa jamii ya watu wote ulimwenguni, kama watu wanamtii Yesu kristo hili ni
agizo la muhimu mno, na Mungu anataka tuliangalie kwa jicho la kipekee Yesu
mwenyewe hapa anasema aaminiye ataokoka asiyeamini Atahukumiwa ni Dhahiri kuwa
hukumu ipo na kama hatutaki watu waangukie katika hukumu ya Mungu basi hatuna
budi kuihubiri injili na kuhakikisha watu wote duniani na kila jamii na taifa
na kabila na lugha wanafikiwa na injili, wajibu huu wa kuihubiri injili ni wa
watu wote na sio watumishi pake yao, Nyakati za kanisa la kwanza walihubiri
kila mahali, na walitimiza wajibu wao sisi nasi hatuna budi kufanya hivyo ona
Matendo 8: 4-5 “Lakini wale waliotawanyika
wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa
Samaria, akawahubiri Kristo.”
Ikiwa watu wa Karne ya kwanza
waliweza kuihubiri injili kwa miguu yao, kwa majahazi, kwa punda na farasi,
wakati wa leo tunaweza kuwafikiwa watu kwa njia nyingi na za rahisi zaidi,
tunaweza kuifanya kazi hii kwa wepesi na kuwafikiwa watu wengi sana Duniani,
shime kila mahali nawaomba wakristo tuamke na kuieneza habari njema ya Bwana
wetu Yesu Kristo kwani mavuno yako tayari na ni sisi tu ambao tunaweza kuueneza
moto wa injili kwa njia zozote zile ambazo Mungu ametupa katika karne hii,
Tunaweza pia kutoa fedha zetu, kununua vyombo vya injili, vyombo vya usafiri,
vyombo vya kuhubiria ndani na vile vya kuhubiria nje, kujenga makanisa, kununua
mahema, kufadhili vipindi vya redio nan television zinazohubiri injili pamoja na
fadhila nyingine za aina nyingi sana za kuhakikisha kuwa tunamtaja na kumueneza
Yesu kwa kila mwanadamu, Baraka kubwa sana italifunika kanisa na taifa na jamii
yoyote ile itakayotumia kila njia kuhakikisha kuwa injili inawafikia watu wote,
hili ni agizo la Bwana wetu Yesu kwa kanisa lake kila mahali duniani, watu wa
Mungu wako tayari na wana kiu lakini wanalisubiria kanisa liamke na kuupeleka moto
wa injili haleluyaaa
Warumi 10:14-17 “Basi wamwiteje yeye
wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo
mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama
nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari
njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi
imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”
Kuhubiri injili ni sawa na kuunga
umeme katika miji yote isiyo na umeme, ni kuwasha nuru maeneo yote yenye giza,
kama hatutaihubiri injili watu wataamini mambo ya giza, watafuata falsafa nyingine, watatambikia mizimu,
wataabudu dini za uongo, watafuata mafundisho ya imani nyingine mbaya na zisizo
na ustaarabu, wote tumekuwa mashahidi kuwa kila mahali injili ilipoingia
kumekuwa na maendeleo makubwa ya kitaaluma, kiuchumi na kiuadilifu na ustaarabu
na maeneo mengi ambayo injili haijafika kumekuwapo giza Kuu, kokote Yesu
anakopelekwa ni dhahiri kuwa nuru kubwa iliwazukia watu wa jamii hiyo;-
Mathayo 4:13-16 “akatoka Nazareti, akaja
akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; ili
litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya
Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale
waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa
mauti Mwanga umewazukia.”
Kwa msingi huo mpendwa hatuna
budi kuipeleka nuru ya Yesu, kwa kuhakikisha kuwa tunawaeleza watu wote habari
njema, acha kuhisi kuwa aaa siku hizi watu wanasikia bhana, hapana fanya wajibu
wako wa kuihubiri injili na kama mtu yuko kimya muhubirie injili mpaka aseme
mimi ni muamini mwenzako, eee kama umekaa kimya tutajuaje kuwa umeokoka tayari?
Lihubiri neno. Kumbuka kuwa katika
wakati tulio nao ni rahisi zaidi kuhubiri injili
Tuige mifano ya watu mbalimbali
ambao waliihubiri injili, Billy Graham anasemekana kuwa ndiye mwanadamu
aliyeihubiri injili kwa watu wengi sana kiasi cha kuitwa muhubiri mkubwa wa
karne ya 20, alihubiri mikutano mbalimbali ya ndani na nje huku mahubiri yake
yakirushwa katika redio na television mbalimbali duniani na matokeo yake Grahamu amekuwa Muhubri
ambaye amehubiria watu wengi zaidi kuliko wote katika historia ya Ukristo na
kwa rekodi za maafisa wake watu wapatao milioni 3.2 waliwahi kumpiokea Yesu
katika mahubiri yake alihubiri injili katika maisha yeke tangu mwaka 1947 –
2005 alipostaafu. Amehubiria zaidi ya watu milioni 215 na amehubiri katika
inchi zaidi ya 185, kwa mikutano zaidi ya 400 yeye anatupa changamoto leo
kufanya kila tuwezalo kulifanya kuhakikisha kuwa dunia inajawa na injili,
hakuwa na mbwembwe, alihubiri kwenye madhabahu akiwa na uso mkali na sauti
yenye mamlaka akiwa na ushawishi mkubwa wa kuwafanya watu watubu na maelfu ya
watu walikuwa wakitubu katika kila mkutano wake, alifariki Tarehe 21 February
2018 akiwa na umri wa miaka 99
Madhara ya kuacha kuhubiri injili.
Kutokuihubiri injili ni UASI ni DHAMBI ni kwenda kinyume na
maagizo ya Mungu! Kwa sababu kwa namna
moja ama nyingine tutakuwa tu mechangia uharibifu kwa dunia ambayo kama
ingesikia habari njema Yesu angewaokoa, Nyakati za agano la kale Mungu
alipowatuma manabii kufanya kazi ya kuonya na manabii hao walionywa pia kuwa
wasiposema Mungu atawahukumu wao kwa sababu wameacha kuwa wasemaji kwa niaba ya
Mungu,
Ezekiel 3:18 -19. “Nimwambiapo mtu mbaya,
Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya,
kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa
katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini ukimwonya
mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika
uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.”
Ezekiel 33:7-9 “Basi wewe, mwanadamu,
nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani
mwangu, ukawape maonyo yangu.
Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno
la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu
wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya
kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika
uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.”
Neno la Mungu bado linatuonya ya
kuwa tunawajibu wa kuwaeleza watu habari njema, mtazamo unaweza kuwa tofauti na
wakati wa Agano la kale ambapo manabii walipeleka maonyo tu na kusisitiza toba,
lakini ujumbe wetu sisi ni mwepesi sana ukilinganisha na nyakati za agano la
kale sisi tunapaswa kuwaeleza watu habari njema na sio za vitisho, kuwaeleza
watu habari za upendo wa Yesu, habari za msamaha wa dhambi bure na kwa neema
tu, Habari ya kuwa Yesu alisulubiwa akafa akazikwa kwa niaba yetu nao
wataokolewa, lakini kwa kuwa Mungu habadiliki kama hatutaihubiri injili
tunakuwa tumewafungia watu malango ya ufalme na tutawajibika na kuhukumiwa kwa
kutokumtii Mungu kwa kufikisha agizo lake, ni nyepesi sana kwa sababu sio sisi
tunaookoa anaeokoa ni yeye mwenyewe lakini sisi ni wajumbe wake, Kila kanisa
kila mkristo aliye hai ana wajibu wa kuihubiri injili na tusipofanya hivyo
tutawajibishwa na kuhukumiwa kama ilivyokuwa maonyo ya Mungu kwa Ezekiel na
Paulo mtume
1Wakorintho 9:16-17 “Maana, ijapokuwa
naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu;
ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.”
Ndani ya habari njema kuna uweza
na nguvu za Mungu zenye kuokoa kwa hiyo wajibu wetu ni kuipeleka ni kusema ni
kutangaza, muhubiri Yesu waeleze watu habari za Yesu na uweza wa kuokoa ni wake
naye atafanya !.
Warumi 1:16- “Kwa maana siionei haya
Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa
Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”
Namna nyepesi ya kuifikisha injili
Muhubiri Kristo!, hubiri kazi
yake ya huruma aliyoifanya pale msalabani, nyakati za kanisa la kwanza hawakuwa
na maneno mengi zaidi ya kuthibitisha kuwa Yesu aliteswa kwaajili yetu alikufa
na siku ya tatu akafufuka, huyu ni Mwana wa Mungu, huyu anaokoa, huyu anasamehe
dhambi, bila kujali kuwa dhambi zetu zilikuwa nyekundu kama damu, yeye
alijiadhibu mwenyewe msalabani kwaajili yetu.
Matendo 8: 4-5 “Lakini wale waliotawanyika
wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa
Samaria, akawahubiri Kristo.”
Zingatia misingi minne tu wakati
unapoisema habari njema kwa njia rahisi ya kumuelezea mtu mmoja mmoja habari za
kristo
1.
Wote
tumefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu Warumi 3:23-24 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na
utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi
ulio katika Kristo Yesu;”
2.
Afichaye
dhambi zake hatafanikiwa aziungamaye na kuziacha atapata Rehema Mithali
23:13-14 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali
yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. Mwanadamu mwenye kicho yu heri
sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.”
3.
Tukiziungama
dhambi zetu yeye ni mwaminifu atatusamehe 1Yohana 1;9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu
na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”
4.
Mwamini
Bwana Yesu na utaokoka wewe pamoja na nyumba yako yaani Familia yako na jamaa zako Matendo 16: 30-32.
“kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa
nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka
pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo
nyumbani mwake.”
Ikiwa mtu atakubali kujitambua
kuwa sisi wote ni wakosaji, na kuwa tunahitaji rehema za Mungu, na kuwa rehema
hizo zinapatikana kwa kazi aliyoifanya Yesu pale msalabani na kuwa wajibu wetu
ni kuamini tu, mtu huyo akikubali kuamini atasema maneno haya
“Bwana Yesu ninakushukuru kwa kuwa
nimesikia neno lako, na nimeamini kazi uliyoifanya pale msalabani, nakushukuru
kwa kuwa wewe ni bwana na kwa upendo wa Mungu umeniokoa na kunisamehe mimi
nisiyestahili, nakuamini wewe kwa msamaha wa uovu wangu wote Amen”
Kwa sala hii mtu huyo atakuwa
amemuamini Bwana na atapaswa kuwa mwanafunzi wa Yesu kwaajili ya mafundisho na
maelekezo mengine zaidi, Amen
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.