Mithali 23:7 a “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”
Utangulizi:
Ni muhimu
kufahamu, kwamba Biblia inaonyesha ya kuwa maisha yetu yanaweza kutabiriwa na
kila tunachokifikiri au kukiwaza, yale tunayoruhusu yaingie katika mioyo yetu
ndiyo yenye nafasi kubwa sana katika kuamua hatima na muelekeo wa maisha yetu,
kwa msingi huo kile tunachokisema na kukitenda ni matokeo ya pili ya kile
tunachokiwaza, hatuwezi kujificha kuwa sisi ni watu wa namna gani, kwani kusema
kwetu na kutenda kwetu kutafunua hatimaye kuwa sisi tukoje, ndio maana ni
vigumu sana kumsoma mtu anayenyamaza. Mtu halisi ni vile tunavyofikiri, Biblia
inaonyesha udhahiri wa watoto wa Mungu na watoto wa ibilisi kutokana na
utendaji waoa au usemaji wao. 1Yohana
3:10 “Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na
watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye
asiyempenda ndugu yake.”
Mkuu wa wajenzi Rev. Innocent Kamote wa pili Kutoka kushoto akiwa na waalimu wa Living Stone, Mwalimu Oscar, Kushoto, Nicolous Luchenja watatu kushoto na Jimmy Molel wanne kutoka kushoto wakiwa katika mazoezi ya Taekondoo. Aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo!
Mithali 23:7a “ Maana aonavyo mtu ndivyo alivyo”
Proverbs 23:7a “For as he thinketh in his heart, so he is”
Kwa msingi huo vile tunavyofikiri
ndivyo, uhalisia wa utu wetu
I.
Wewe ni
matokeo ya kile unachokifikiri na kwa sababu hiyo ni muhimu kufikiri pia kuhusu
nini unakiwaza na kama kina kibali mbele za Mungu Zaburi 19:13-14 Biblia
inasema “Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi,
Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa
lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali
mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu”. Kwanini mwandishi
wa Zaburi anataka mawazo ya moyo wake yapate kibali mbele za Mungu? Maana yake
ni kama anamuomba Mungu amsaidie kuwaza sawasawa, hii ni Muhimu sana vile
tunavyowaza ndivyo tunavyoweza kusema na kutenda, kama tutawaza sawasawa
tutakuwa tumejizuia, kutenda, kutawaliwa, kusema na kijiepusha na makosa
makubwa na uovu.
Yale tunayoyafikiri yana vyanzo, Mtu ili aweze kuwa kama alivyo ni lazima
kuweko maswala kadhaa ynayochangia katika kumjenga moja ikiwa ni wakati wa
kuzaliwa kwetu, lakinimengine ni vile tunavyopokea kutoka ulimwenguni kutokana
na mazingira na milango yetu mitano ya fahamu kwa msingihuo ni muhimu kwetu
kujilinda na vyanzo vinavyoingiza taarifa katika nafsi zetu na akili zetu mfano
:-
a.
Yale
tunayoyasoma?- Tunayoyasoma yanaingia katika akili zetu na kwa hivyo yana
mchango mkubwa sana katika kuyajenga maisha yetu na ndio maana biblia inasema
tujae nenola Mungu mioyoni mwetu Wakolosai 3:16-17 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima
yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku
mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
2Timotheo 3:14-17 “14. Bali wewe ukae katika mambo
yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao
ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo
yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila
andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa
yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe
kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” Maandiko
matakatifu yanaweza kutuhekimisha na kutuongoza katika haki, kwa msingi huo
yale tunayoyasoma yanaweza kuathiri maisha yetu na hivyo ni muhimu kwa mtu
mwema kuhakikisha anaingiza mambo yaliyo mema katika moyo waake “Ubongo”
b.
Yale
tunayoyaangalia Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho
yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?” Ayubu aliweka agano na
macho yake kuwa hataangalia mwanamke kwa tamaa yaani kumwangalia kwa nia mbaya,
kumbe kuangalia kunaweza kuathiri mitazamo yetu na mfumo wa maisha yetu ni
muhimu kwetu pia kujilinda katika yale tunayoyaangalia.
i.
Kuyaangalia kupitia
Internet,jihanadhari angalia vitu vyema
ii.
Kuyaangalia
kupitia Movies, TV, na kadhalika watoto wetu wengi siku hizi wanangalia sana ngumi
na uharibifu wa kwenye sinema na hivyo vijana wengi sana wa leo wamekuwa ni
waharibifu wakubwa wa vitu na vifaa majumbani na mashuleni
c.
Yale
tunayoyatafakari Wafilipi 4:8.” Hatimaye,
ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote
yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye
sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Kuna maswala ya kutafakari ambayo biblia
inayapendekeza hapa kwenye kutafakari ndipo panapoweza kutusaidia kujenga
misimamo yetu iliyo thabiti, ni muhimu kwa kila mmoja kujipima kuwa anatafakari
nini.
d.
Yale tunayoyasikia,
ukisikia taarifa zisizo sahihi hutakuwa sahihi na ukisikia taarifa sahihi
unakuwa sahihi. Hakikisha kuwa unasikiliza mambo ya msingi, Biblia ya Kiswahili
inasema Mazungumzo mabaya huaribu tabia njema, kwa maana ya kuwa tunapozungumza
pia tunasikia, Biblia ya kiingereza inasema “Bad Company corrupt Good
Character” sawa na kusema marafiki
wabaya huaribu tabia njema kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuangalia wale
wanaotuzunguka kwa vile wanahusika kwa kiwango kikubwa katika kuyajenga maisha
yetu
II.
Mioyo yetu ndio
chemichemi ya tabia zetu.
a.
Mti
hutambulikana kwa matunda yake Luka 6:43-45 “Kwa
maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda
mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba
hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika
hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu
ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale
yaujazayo moyo wake”. Unaona kile Yesu anakizungumza hapa ni kama
anasema aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo! Kumbe kusema kwetu na kutenda
kwetu ni matokeo ya asili yetu ya moyoni, tunza saba moyo wako! Kuna athari
kubwa sana katika kuwaza kwetu au katika yale tunayoyajaza mioyoni mwetu kwani
hatima yeke ni kuyazalia matunda. Kipengele kifuatacho kinasaidia kutujulisha
namna tutakavyokua endapo tutaielekeza mioyo yetu katika maswala mhaya:-
III.
Maisha yako
yanafafanuliwa na moyo wako na fikira zako:-
1.
Kama
unajifikiri mwenyewe sana utakuwa mbinafsi sana 2Timotheo 3:1-2 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako
nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda
fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio
na shukrani, wasio safi,”
2.
Kama
utafikiri sana kuhusu wengine utakuwa mkarimu, na mwenye kujali Warumi12:10-13.
“Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa
heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika
roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri;
katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika
kukaribisha wageni mkijitahidi.”, Waefeso 4:32
3. Kama
unafikiri sana kuhusu fedha utakuwa mtu mwenye tamaa 1Timotheo 6:9-10 “. Lakini hao watakao kuwa
na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana,
zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina
moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani
hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
4. Kama
utakuwa mwenye kushukuru sana utakuwa mtu mwenye kuridhika 1Timotheo 6:6-8 “6. Walakini utauwa pamoja
na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana
hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula
na nguo tutaridhika na vitu hivyo.”
5. Kama
utafikiri sana kuhusu ngono utakuwa
mwenye tamaa au kahaba Mathayo 5:
27-28 “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini
mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini
naye moyoni mwake.”
6.
Kama tutafikiri sana kuhusu uadilifu
tutakuwa wenye moyo safi 1Wakoritho 6:18, Mathayo 5:8 “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.”
7.
Kama
utafikiri sana kuhusu kutenda hila utakuwa muongo mkubwa Wakolosai 3:9-10 “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja
na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na
mfano wake yeye aliyeuumba.”
8.
Kama utakuwa
mwenye kufikiri kuhusu ukweli utakuwa mtu muaminifu Waefeso 4:25 “Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa
maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.”
9.
Kama utakuwa mwenye kutaka sifa kutoka
kwa watu utakuwa mnafiki Mathayo
6:5,23:12 Mathayo 6:5 “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda
kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane
na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.”
10. Kama
utakuwa mwenye kufikiri sana kuhusu kumuinua Mungu, utakuwa mtumishi wake
mkubwa sana 1Petro 2:1-3. “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na
husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini
maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye
fadhili.”
Hitimisho.
Wewe ni mtu wa namna
gani, na je Mungu anaona nini kwako? Matendo
1:24, Waebrania 4:13
Ni lazima uamue kuwa
mtu wa aina gani kwa kuhakikisha kuwa unawaza vema wakati wote
Kila unachokitafakari
na jinis unavyojiona ndani ndivyo unavyoamua maisha yako yawe Mungu alichukizwa
na wana wa Israel ambao walijiona nafsi zao kama panzi walipojilinganisha na
wakanaani na kusahau ukuu wa Mungu na hivyo Mungu alichukizwa nao Mafanikio yetu
na maisha yetu ya kiroho na kimwili yanategemeana sana na namna tunavyojiona
ndani na namna tunavyojiona ndani inategemeana sana na yake tunayoyaingiza katika mioyo yetu, ukijiona
duni wewe ni duni, ukijiona shujaa wewe ni shujaa, ukijiona huwezi wewe
hutaweza, ukijiona mbaya wewe ni mbaya, ukijiona mwema wewe utakuwa
mwema,ukijichukia hakuna mtu atakayekupenda, ukijipenda utapendwa, ukiwa na
amani, utazalisha amani ukiwa na uchungu utazalisha uchungu, Aonavyo mtu
nafsini mwake ndivyo alivyo
Na Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni