Luka 7:33 - 35 “Kwa kuwa Yohana Mbatizaji
alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na
kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza
ushuru na wenye dhambi. Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake
wote."
Utangulizi:-
Bill alikuwa ni mtu mwenye umri
wa miaka ipatayo 40 na alikuwa akifanya biashara ya kuuza nguo, aliuza nguo za
aina tofauti tofauti, kwatika miji na vijiji mbalimbali, siku zote alitumia
punda kubeba mizigo ya nguo alizokuwa akiziuza.
Siku moja aliamua kumchukua
kijana wake mwenye umri wa miaka 15 aliyeitwa Ron na kwenda naye katika miji na
vijiji vilivyokuwa karibu,Punda alibeba behi mbili za nguo walizokuwa wakiuza,
wote walikuwa na furaha kubwa sana Bill na Ron, baada ya kuuza na kufanya
biashara kubwa sana na kupata faida , Bill alikuwa na furaha yeye na mwanaye
ron na punda wao waliamua kurudi nyumbani.
Walitembea umbali mrefu sana
mwishowe walichoka, wote watatu walitembea pole. Pole wakirejea nyumbani.
Watu wawili waliwaona wakiwa
wamechoka sana, wakaanza kusema “angalia hawa wajinga wamechoka mbaya
inavyoonekana, wana punda lakini kwanini mmojawao asipande juu ya punda
wanapata shida ya bure hali wanaye punda si wangemtumia!”
Bill na Ron walisikia lililokuwa
likizungumzwa na watu walke wawili kuhusu wao na Ron alimwambia baba yake
apande juu ya Punda.
Alikubali na akakaa juu ya punda,
lakini baada ya dakika chache Mzee mmoja alimuona Bill juu ya punda na
akamwambia “we mzee huna hata huruma mwangalie kijana wako alivyochoka bado
mdogo mno, wewe unapanda ju ya punda na unamuacha mtoto atembee ?”
Bill aliamua kumpandisha mwanae
juu ya punda na wakaendelea na safari lakini baada ya muda kidogo Mgeni mmoja akapiga
kelele akimkemea Ron “ weee bado ni kijana sana huwezi kutembea? Unaachaje mzee
anatembea wewe kijana uko juu ya punda uvivu tu shuka haraka”
Bill na mwanaye Ron
walichanganyikiwa na wasijue nini cha kufanya, wakaamua wote wakae juu ya Punda
na kuendelea ingawa punda alitembea kwa shida sana kwa vile uzito wao ulikuwa
ukimuelemea.
Mtu mwingine akawaona kwa mbali
akawakimbilia na kuwaambia kwa kupiga kelele akiwaambia Bill na mwanaye, hivi
ninyi mna kichaa?inawezekanaje wote wawili mumpande punda mmoja je hamuwezi
kutembea? Kwanini mnamtesa huyu mnyama?
Bill na Ron walishangaa sana
wakanyamaza kimya kwa Muda.
Sio rahisi kumpendeza kila mtu, kila mmoja ana mawazo tofauti na maoni
tofauti, ni vigumu kumpendeza kila mtu au kufuata wazo la kila mtu, wakati
mwingine ni lazima kuamua kile tulichokiamua na kwa kweli fuata moyo wako na
Mapenzi ya Mungu.
Mungu katika hekima yake
amejaribu kwa kilanjia kuwapata wanadamu, alituma manabii kwa njia nyingi na
kwa namna mbalimbali
Yohana mbatizaji alitumwa kwa
Israel akihubiri mahubiri makali sana akiishi maisha ya kujikana, aliishi
porini, akila nzige na asali ya mwituni, alivaa ngozi na singa za ngamia,
hakuhudhuria sherehe za aina zozote, alionya kuhusu hukumu ya Mungu na kukemea
dhambi akiwataka watu watubu na kugeuka kwa Mungu lengo kuu ikiwa ni kuwaleta
watu kwa Yesu hata hivyo walisema ni kichaa ana pepo na hatimaye walimuua.
Yesu alikuja kwa kusudi la kuokoa
alijichanganya na wenye dhambi alifanyika rafiki, alikula na kunywa naovyakula
vyao vya kawaida na vinywaji vyao vya kawaida lakini hata hivyo walimuita mlafi.
Kristo anatufundisha kuwa Hekima
ya Mungu imejulikana kuwa na haki kwa watoto wake, ni wazi tu kuwa kwa njia
yoyote wanadamu hawapendi kuitikia wito wa Mungu aidha kwa kuwachezea au kwa
kuwahuzunikia, ukiwaita kwa sherehe hawaji au ukiwaita kwa huzuni hawaombolezi,
Luka 7:31- 32. “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao
wamefanana na nini? Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema,
Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.”
Wanadamu hawana jema ukiwa mpole
watasema huyu naye kazidi sana upole, ukiwa mkali watasema mmh huyu naye mkali
mno, ni vema kila mmoja akatimiza kusudi la Mungu kama alivyokusudiwa na hii ndio
hekima hatuwezi kuwa vile wanadamu wanavyotaka tuwe lakini tunaweza kuwa vile
Mungu anavyotaka tuwe, Mungu alimuita Yohana kwa Kusudi lake na alimtuma Yesu
vilevile kwa kusudi lake, hii ndio hekima ya Mungu, hatupaswi kujali watu
wanasema nini timiza kusudi la Mungu uliloitiwa, Faida ya wito wako itaonekana
baadaye.
Kikwete hawezi kuwa Magufuli na
Magufuli hawezi kuwa Kikwete, Tulimuomba Mungu atupe Rais tumuachie atomize kusudi
lile ambalo Mungu amempa kwaajili ya watanzania, iwapo Mungu angekuwa anataka
mfumo uleule na aina ileile ya uongozi, angeachia mtu anayefanana na Kiwete
atawale, hakuna anayeweza kusema yeye alikuwa Rais Mzuri zaidi ya mwingine kwa
vile kila mmoja ameitwa kwa kusudi lake, Hali kadhalika katika Huduma, Mtume,
Nabii, Mwinjilisti Mchungaji na Mwalimu, hakuna aliye mkubwa kuliko mwingine,
kila mmoja anatimiza kusudi lake, Mtume hawezi kusema kuwa yeye ni mkuu kuliko
Mwalimu kwa vile amefundishwa na mwalimu, Nabii, Mtume mwinjilisti wanalelewa
na wachungaji Kanisani, ipi ni huduma iliyokuu ni ile inayohitajika kwa wakti
huo. Na hii ndio hekima ya Mungu.
Sio rahisi kumpendeza kila mtu, kila mmoja ana mawazo tofauti na maoni
tofauti, ni vigumu kumpendeza kila mtu au kufuata wazo la kila mtu, wakati
mwingine ni lazima kuamua kile tulichokiamua na kwa kweli fuata moyo wako na
Mapenzi ya Mungu.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekim.
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni