Andiko la Msingi:1Wakoritho 10:12“Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”
Utangulizi:-
Ni muhimu kufahamu kuwa kifungu hiki cha maneno ya
Paulo mtume kinafunga au kinahitimisha mfululizo wa maonyo muhimu sana
aliyoyatoa Paulo mtume ambayo tunayapata kama somo kutoka kwa wana wa Israel
Kwamba kama mababa wa waisrael waliweza kufurahia
neema maalumu ya kuokolewa kutoka Misri chini ya utawala wenye nguvu wa Farao,
na kuona miujiza mingi na uwepo wa Mungu, bado waliweza kukataliwa na
kuangamizwa jangwani, maiti zao ziliangukia katika jangwa zito, hawakuweza
kufika na kuingia katika inchi ya ahadi, na kwa sababu hiyo kupitia wao
tunajifunza kwamba watu wanaojikinai wenyewe na kufikiri kuwa wao ni maalumu
sana na wenye kujiamini kupita kawaida na wenye kujivunia kipawa cha aina
fulani, upendeleo wa aina fulani, na kumsanifu awaye yote hii ni moja ya dalili
mbaya inayoweza kumpelekea mtu katika anguko
la aina yoyote!
Ujumbe:
Kulikuwa na mti mmoja mrefu sana
unaojulikana kama mti wa mtiki na karibu yake kulikuwa na miti mingine
iliyokuwa laini kama nyasi,
Mtiki ulianza kujisifu kwa nyasi
kuwa mimi ni mzuri mrefu na ni mwenye nguvu sana kuliko ninyi, Nyasi
ziliposikia ziliuonya mtiki na kuuamnbia rafiki yangu majivuno ya kupita
kawaida ni hatari, Hata wenye nguvu huanguka siku moja
Mtiki ulizizarau nyasi, na
kuendelea na kujisifu wenyewe!
Upepo mkali sana ulipuliza na
mtiki ulisimama imara, na hata mvua kali ziliponyesha mtiki bado ulisimama
imara na uliendelea kutanua majani yake, wakati wote huo nyasi na mbogamboga
ziliinama kabisa, na mtiki ukawacheka sana nyasi na mboga mboga.
Siku moja kukatokea dhoruba kali
sana msituni kama ilivyo desturi Nyasi ziliinama chini na kama kawaida yake mtiki
haukukubali kuinama, Dhoruba iliendela kuwa kali sana kiasi ambacho mtiki
haukuweza kustahimili tena, ukaishiwa na nguvu
ukaanguka chini, ulijaribu kwa nguvu zake kusimama na ikashindikana
kabisa na huo ndio ukawa mwisho wa mti wenye kiburi, Mambo yalipokuwa sawa
Nyasi zilisimama na kushangaa kuwa mtiki hauko na nyasi zilipoangalia vema
ziligundua kuwa mtiki umeanguka!
Tunajifunza nini ?
Biblia inasema kijapo kiburi ndipo ijapo aibu, tena
kiburi hutangulia uangamivu Mithali 16:18 “Kiburi
hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko”. Biblia inaonya kuwa kila ajikwezaye
atashushwa Mathayo 23:12 “Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote
atakayejidhili, atakwezwa.” Mithali 29:23 inasema “ Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya
unyenyekevu ataheshimiwa.” Baadhi
ya wasomi wa kibiblia wanasema kuwa kiburi kinasababisha kutokujali ambako
kunaongoza katika kufanya makosa makubwa ya kutisha na kushangaza na Wengine
wanasema Mungu mwenyewe huwatia nidhamu watu wenye kujikinai wakijidhani wao ni
bora kuliko neema ya Mungu kwa kuwaachilia wajikute katika matukio
yatakayowanyenyekesha.
Iko mifano mingi sana Katika Historia
ya dunia ambayo inaweza kutufunza jambokatika mitazamo hii, wote tumewahi
kusikia au kuona habari ya Meli ya kifahari sana Duniani ijulikanayo kama
TITANIC Meli hii ilitangwazwa na watengenezaji kuwa ni meli ISIYOWEZA KUZAMA
kutokana na kujiamini huko kwa kupitakawaida meli hii haikuwa na meli
ndogondogo za uokoaji, lakini kilichotokea kimetoa funzo katika Historia ya
dunia
Matengenezo ya Titanic.
Meli ya Titanic ilianza
kutengenezwa mwaka 1909. Kampuni iliyoagiza meli hiyo kutengenezwa ni White
star, lengo la kampuni hii ilikuwa ni kuweza kushindana na kampuni ya Cunard
line meli hii ndiyo maarufu kuliko zote katika historia ya dunia. TITANIC
ilikuwa meli ya pili kwa ukubwa baada ya meli ya Olympic kwa wakati huo, meli
ya tatu kwa ukubwa ilikuwa ni Britannic.
Titanic yaanza Safari.
Baada ya matengenezo yake
kukamilika mwaka 1912 maandalizi ya kuanza safari yalianza.
Aprili 10, 1912 meli ya Titanic
inaanza safari ikitokea Southampton- Uingereza kuelekea New York- Marekani.
Huku ikipambwa na maneno yaliyo kuwa yameandikwa ubavuni mwake kwa ustadi
mkubwa yakisomeka T I T A N I C Meli hiyo ilibeba watu wapatao 2,200 wengi wao
wakiwa ni matajiri na baadhi ya watu walikuwa wakihamia Marekani kwenda kuanza
maisha mapya. Kapteni wa meli hiyo alikuwa ni E.J.SMITH, Meli hii ilikuwa na
eneo la Matajiri wa juu, wa kati na wa chini, ilikuwa na kumbi za starehe,
viwanja vya michezo na basket ball, ilithibitishwa na wataalamu mbalimbali kama
meli isiyoweza kuzama na yenye usalama wa hali ya juu duniani. Mmiliki wa meli alipohojiwa na vyombo vya habari kuhusu usalama wa meli hii alisema "Hata Mungu hawezi kuizamisha"
Titanic yaginga mwamba wa Barafu
Baharini.
Aprili 14, 1912 saa 5:40 usiku,
Titanic ikagonga mwamba wa barafu. Ilikuwa ni siku ya nne tu tangu ianze safari
yake. Kapteni wa meli hii alikuwa amearifiwa kuwa kuna mwamba mbele yao, hivyo
arijaribu kukwepa lakini alikuwa kachelewa ubavu wa meli uligonga kwenye mwamba
wa barafu na kupasuka ndipo maji yakaanza kuingia ndani ya meli. Ni mashua 16
tu za uokoaji zilizokuwa ndani ya meli hiyo ambazo zingeweza kubeba watu 1,178
hata hivyo mashua nyingi hazikujaza watu na hivyo watu 705 tu ndiyo
waliokolewa.
Titanic yazama.
Mnamo tarehe Aprili 15, 1912 saa
8:20 usiku TITANIC ilizama. Watu 1,500 hivi walipoteza maisha. Tangu saa hii
histori mpya ya TITANIC yaanza kuandikwa. Ama kweli ni historia ya kusikitisha
sana.
Ndugu yangu je wewe ni maalumu
sana kama Titanic? Wewe je mgumu kama mtiki? Unajivunia nini Duniani? Mungu
yuko nyuma yako anakuangalia, Yeye ni wa kutukuzwa na kuogopwa sana yeye ndiye
aliyeshikilia kila kitu hatuna budi kuwa wanyenyekevu kama Nyasi na kukubali
kuinama ili tuinuke tena!
Ajidhaniaye kuwa amesimama na
aangalie asianguke!
Wa salaam
Na Mkuu wa wajezni Mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni