Mstari wa Msingi 1Samuel 25:10-11
“Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi,
akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa
wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na
maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya
kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?”
Utangulizi.
Katika kifungu cha maandiko hapo
juu tunajifunza habari za Daudi na Nabal ambazo kwa ujumla zimeshehemi mambo
mengi sana ya kujifunza kulingana na mtazamo wa msomaji, lakini leo mmi kama
mkuu wa wajenzi katika kisa hiki najifunza mfano wa watu wasio na shukurani
tulio nao duniani, watu ambao wanasahau fadhili, watu ambao wanaweza kuwa na
kiburi na kusahau kuwa uwepo wao umechangiwa na watu wengine pia.
Wote tunafahamu jinsi ambavyo
Daudi, alivyo mtu muhimu sana na wote tunatambua jinsi alivyo maarufu sana,
Daudi ndiye aliyewaokoa Israel nzima wasiwe watumwa wa wafilisti, 1Samuel 17
:8-9. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya
Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi
si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza
kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na
kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.” Kwa msingi huo
Hakuna mtu aliyekuwa hatambui kuwa Daudi ni nani na nini alikifanya katika
taifa la Israel nzima kwani aliwaokoa watu wote wasiwe watumwa wa Israel, na
kama haitoshi Maalumu sana kwa mtu anayeitwa Nabali Daudi alimtendea mema
binafsi kwa kulinda mifugo yake na wachungaji wake.
Wakati Daudi aliposikia kuwa
Nabali mtu aliyekuwa mkubwa sana na tajiri anakata manyoya kondoo aliomba
chakula, huku akimkumbusha namna na jinsi alivyomtendea mema lakini kwa jeuri
kubwa Nabali alimpuuza Daudi na nyumba
ya Baba yake, Daudi ni nani na Mwana wa Yese ni nani?, lugha hii ilikuwa lugha
ya zarau kubwa yenye matusi makubwa lakini kama aitoshi Nabali alimtukana Daudi
kuwa ni mkimbizi tu, amemkimbia Bwana wake, aliwakuza watumwa wake na kuwaona
ni wa muhimu sana kuliko Daudi aliyeokoa taifa zima Jambo hili lilimuudhi sana
Daudi na Mungu pia, Hivyo daudi alikusudia kumuua Nabali na ukoo wake wote
kutokana na Kauli mbaya na maneno yasiyofaa kwa Daudi.
1Samuel 25:2-17 “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali
yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu
na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina
la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke
alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana
adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi
Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya
kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana,
Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo
mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani
mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu
wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala
hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.
Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni
pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote
kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika
vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la
Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi,
akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa
wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji
yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo
zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi
wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno
hayo yote. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga
wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake;
nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili
wakakaa na vyombo vyao. Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili,
mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili
kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema
sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati
wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu
usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue
na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na
juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi
kusema naye.”
Unaweza kuona jinsi Nabali
alivyoweza kupuuzia mambo yote mema aliyokuwa ametendewa na Daudi kitaifa na
kwa binafsi na badala yake alilipa mabaya na kumtukana Daudi. Hivi ndivyo ilivyo
kwa watu wengi sana ambao tunaweza kuwatendea mema lakini wao wakatulipa maovu.
Mfano
Mtu mmoja wa makamo alipata
bahati mbaya akapotea njia walipokuwa msituni na rafiki zake, Yeye na rafiki
zake walikuwa katika safari ya kuvunjari
msituni, baada ya chakula cha mchana aliamua kutembea kidogo, Rafiki zake
walimuonya kwammba asiende ndani sana msituni asije akapotelea nyikani, ingawa
hakujali ushauri wa rafiki zake.
Msitu ulikuwa mzuri na wenye
kuvutia, licha ya kuonywa kuwa asiende mbali alipotelea msituni, alijaribu
kurudi lakini hakuona njia wala pa kutokea na alianza kuogopa, Mara alianza kusikia sauti
ya Simba akiunguruma na sauti hiyo ilimuogopesha sana, alitambua kuwa ni sauti
ya simba, lakini wakati huo hakumuona simba,
Aliamua kutimua mbio ili kuokoa
maisha yake na hatimaye alimuoina simba akimkaribia, kwa haraka na kwa hofu
alikimbia na kupanda juu ya mti na kujibanza katika tawi mojawapo la mti ule na
kutulia vema,alijishangaa hata namna alivyoupanda ule mti, alipoangalia pembeni
ya mti ule aliona sokwe mkubwa akiwa amelala kwenye tawi lingine.
Simba alifika na kuona mti, sokwe
na binadamu, simba alimwambia sokwe msukume chini huyu mwanadamu nimle mana
nina njaa mbaya!, Sokwe kwa upole
alijibu kwa unyenyekevu mti huu ni wangu na mtu huyu amekimbilia hapa kuokoa maisha yake
hivyo siwezi, kumuacha afe wala aanguke na aliposikia maneno hayo mwanadamu
yule alijisikia furaha sana.
Simba alinyamaza kimya kwa muda kisha alimwambia mwanadamu
tafadhali msukume sokwe chini nam nitakuacha wewe, Jamaa bila kufikiri hata kwa
dakika moja alimsukuma sokwe chini, ingawa kwa uhodari mkubwa sokwe alirukia
tawi lingine la juu zaidi na kuokoa maisha yake.
Simba alicheka sana na kisha akaondoka zake.
Mtu yule aliona aibu kwani ukweli ni kuwa sokwe alikuwa
ameokoa maisha yake kutoka katika mikono ya simaba hatari, lakini yeye
alijaribu kumsukuma chini, ni muhimu kuwa kama sokwe kwa kuwasaidia wengine na
kamwe tusiwe kama mtu yule mbaya.
Hivi ndivyo ilivyo kwa watu wengi, Hawana shukurani,
unawakaribisha, unawapokea wewe mwenyewe lakini kesho wakifanikiwa wewe
unahesabika kuwa sio kitu, nimara nyingi sana hata walimu wamewasaidia sana
wanafunzi wametunza maisha yao miaka miwili, mitatu au minne lakini unaweza
kushangaa wanafunzi wakilipa dharau kwa walimu, wakiwavunjia heshima, wengine
wamewapuuzia hata wazazi wao waliowalea na kadhalika.
Tabia ya mwanadamu huyu na tabia ya Nabali hazitofautiani
sana Mungu hakupendezwa na Nabali kwani baada ya siku kumi tu Nabali alifariki,
ingawa daudi hakumuua, lakini Mungu alimtetea Daudi na kumlipa Nabali sawasawa
na matusi yake
1Samuel 25:36-39 “Kisha Abigaili
alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu
ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa
kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata
kulipopambazuka. Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe
alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe. Tena
ikawa, yapata siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa. Naye
aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe Bwana ambaye
amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake
asitende maovu; tena uovu wake Nabali Bwana amemrudishia juu ya kichwa chake
mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe”
Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kuwa na moyo wa
shukurani na kutokuwalipa mabaya wale wanaotutendea mema, iweni watu wa
shukurani na kuwalipa mema wanaotutendea wema”
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni