Jumapili, 30 Oktoba 2016

Bwana atasimama pamoja nawe!


Andiko: 2 Timotheo 4:16-18
 
16. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. 17. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. 18. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina

Kuokolewa katika kinywa cha Simba 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Nyakati za kanisa la kwanza wakristo walipitia vipindi mbalimbali vya Mateso na kulikuwa na aina kuu mbili za maadui, walikuweko maadui wa nje wa kanisa na wa ndani, wote walikuwa ni hatari sana, katika mwaka wa 54-68 baada ya Kristo Mateso ya Kanisa yaliongezeka sana na ndugu wengi katika Kristo waliuawa, kwani mfalme katili zaidi kuliko wote alitawala aliyejulikana kama “NERO CLAUDIUS” wakati huu ulikuwa wakati mgumu sana na hasa kwa viongozi wa Kanisa na washirika pia, Paulo mtume wakati huu aliandika waraka wake wa mwisho ili kumtia moyo Timotheo kuendelea kusimamia kanisa la Mungu bila kuogopa Mateso.

Licha ya Paulo mtume kumtia moyo Timotheo lakini vilevile alijitia Moyo yeye mwenyewe ingawa wakati huu alifahamu kuwa atakufa na kuwa huduma yake ilikuwa imefika mwisho, lakini aliandika waraka huu akiwa kifungoni Rumi na mtawala Nero akiwa hataki kabisa kusikia Injili ikihubiriwa, lakini hata wakristo na ndugu waliokuwa pamoja na Mtume Paulo walikimbia na hakuna mtu alitaka kusimama upande wake hivyo wakati huu Paulo alivunjika moyo na kukata tamaa lakini katika mistari hii hapo juu kuna mambo Muhimu ya kujifunza kutoka kwake

·         Lakini Bwana alisimama Pamoja nami
·         Kuokolewa katika kinywa cha Simba
·         Kuokolewa na kila neno baya.

Lakini Bwana alisimama Pamoja nani

Paulo ingawa alikuwa anajua kuwa mwisho wake umekaribia na kuwa sasa anamiminwa "2Timotheo 4:6-7" hakutaka Timotheo akate tamaa yeye alikuwa na ujuzi kamili ya kuwa Bwana angesimama pamoja naye, Mungu kusimama pamoja naye halikuwa jambo geni katika maisha ya huduma yake, Mara kadhaa kila alipokutana na jambo gumu hata kukaribia kutaka kufa Yesu alikuwa Pamoja naye, Neno KUWA PAMOJA, AU KUWA KARIBU kwa Kiyunani ni “PARISTEMI” kiingereza chake place beside, put at disposal, to present, to stand before, to provide, or come to aid or present offer na standing near, tafasiri rahisi ya Kiswahili ni “KUWEPO KWA KUSUDI LA KUSAIDIA” Neno kama hilo limetumika mara kadhaa katika huduma ya Paulo 

Matendo 23:11Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.”

Matendo 27:23 - 25 “23. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, 24. akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. 25. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.

Ni kawaida ya Mungu kuwepo karibu nasi na kutoa msaada pale tunapohitaji msaada wake ama pale watu wengine wanapokuwa wameshindwa kutoa msaada, Inaonekana wazi kuwa alipokuwa Gerezani Bwana alimtia nguvu, Mungu ataendelea kututia nguvu mpaka dakika ya mwisho

Kuokolewa katika kinywa cha Simba

Paulo mtume anazungumza jambo lingine lililokuwa likiwakabili watu wa nyakati za Kanisa la kwanza na Bwana pia alimuokoa nalo na hii ilikuwa ni kuokolewa katika kinywa cha samba, Nyakati za Kanisa la kwanza wakati wa mateso kulikuwa na samba wa aina tatu waliokuwa wakilisumbua kanisa

·         Simba wa kawaida wanyama – Hawa walikuwa wakitumika kuwatesa wakristo kila mtu aliyesimama kuihubiri injili na kumkiri Yesu kuwa ni Bwana kama akikamatwa auwakikamatwa walitupwa viwanjani na kufunguliwa simba wenye njaa na kuwatafuna wakristo, watu wengi katika maombi yao waliomba waokolewa na simba hao, huenda Paulo mtume pia alimuomba Mungu akaokolewe na simba wakristo wengi waliomba muujiza utokee kama Daniel lakini walitafunwa hivyo hofu kubwa iliingia 

·         Simba aliwakilisha mtawala wa Rumi – Nero Claudio alikuwa ni mtawala katili aliyeuawa wakristo wengi bila Huruma na hivyo wakristo wengi walimuogopa na walitumia jina simba pia kama lugha ya mficho dhidi ya mtawala katili

·         Simba aliwakilisha Shetani  - katika wakati huu kwa kweli shetani alikuwa amekasirika kama simba akipania kabisa kuisambaratisha injili kwa kulisambaratisha kanisa sura ya shetani ilionekana wazi kupitia Nero na simba halisi waliokuwa wakitumiwa kama njia ya mateso 1Petro 5:8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Kukesha ni kuomba Yesu alisema Ombeni ili msije mkaingia majaribuni

Kuokolewa na kila neno baya 

Ni muhimu kufahamu kuwa mitume kamwe hawakuwa wanaogopa kufa lakini walikuwa wanaogopa kusalitiwa na watu wa baya ndani ya injili “deliver me from every evil work” Neno baya au evil katika kiyunani ni “PONEROS  ambalo kiingereza chake ni  The negative moral quality of a person or action opposed to God and his goodness” Paulo alijiombea kuwa asije akamkosea Mungu akapoteza Ufalme wa mbinguni, Paulo alijiombea kumaliza vizuri mwendo wake, kuvipiga vita vilivyo vizuri vya imani, alijiombea asinenwe vibaya asichafuke kwaajili ya injili, Mungu na awe karibu na kila mmoja wetu na kutupa msaada na kutuokoa na kinywa cha simba na kutuokoka na kila neno baya.

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: