Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Nabii Hosea



A.       Mwandishi wa kitabu cha Hosea.

-          Alikuwa Nabii kwa Israel katika Dakika za mwishoni kabla kidogo sana Israel kuanguka katika mikono ya waashuru mwaka 722 K.K
-          Ni Nabii maarufu kama Nabii wa Upendo na uaminifu jina lake Hosea ni la Kiebrania Hoshea ambalo maana yake ni wokovu au msaada,jina kama Yoshua na Yesu yanatokea katika mzizi wa jina kama hilo.
-          Ni wazi kuwa Hosea alikuwa Mwiisrael alizungumza kama ndugu na aliyataja mataifa kama Lebanon,Tabori, Bethel na Samaria
-          Baadhi ya wasomi wanaamini kuwa alikuwa na asili ya ukuhani kutokana na kutaja kwake maswala mengi yanayohusiana na ukuhani
-          Alikuwa na Mambo mengi ya kukatisha tamaa aliyokutana nayo katika familia yake, Huduma na hali halisi ya Taifa lake.
-          Hosea anazungumza na kuonyesha kwa nguvu upendo wa Mungu kwa Israel licha ya kuwa na uovu mwingi, Dhuluma, mateso, udanganyifu, Rushwa, kukosa uvumilivu, ulevi na maisha ya anasa, Mungu aliwataka warejee kwake.

B.       Tarehe ya uandishi wa kitabu cha Hosea.

Inakisiwa kuwa kati ya Mwaka wa 750-725 wakati wa utawala wa Uzzia, Jothamu, Ahazi na Hezekia Mfalme wa Yuda na Yeroboamu ii mfalme wa Israel Inaonekana Nabii ananukuu Wafalme wa upande wa Yuda kwa sababu kwanza alikuwa anaamini kuwa walikuwa wafalme wa kweli na warithi halisi wa kiti cha enzi cha Daudi pili wafalme wengi wa Israel waliomfuta Yeroboamu wa ii walioishi muda mfupi sana na kuuawa hivyo huenda majina mengi yangeorodheshwa mfano ni orodha hii ifuatayo;-                            

                                                    Utawala wa wafalme wa Israel 2Falme 14-18

Yeroboamu
Miaka 41
2  Falme 14;23-29
Alikufa
Zekaria
Miezi 6
               15;8-12
Aliuawa
Shalumu
Mwezi 1
               15;13-15
Aliuawa
Manahemu
Miaka 10
               15;16-22
Alikufa
Pekaiya
Miaka 2
               15;23-26
Aliuawa
Peka
Miaka 20
               15;27-31
Aliuawa
Hoshea
Miaka 9
               17;1-41
Alifungwa.

                                    Mwisho wa utawala wa Israel wakachukuliwa utumwani Ashuru

-          Watu wa Israel walikuwa wamekataa kurudi kwa Mungu Pamoja na mahubiri ya Nabii Amosi na matokeo hali ilizidi kuwa mbaya
-          Badala ya kumrudia Mungu watu waliendelea kuwa waasi huku wakiwaua wafalme wakifanya mapinduzi kwa mapinduzi Mafalme Tiglath – Pileser wa Ashuru aliishinda mashariki ya kati na kupanua mipaka yake mpaka Misri na mataifa yoote  yaliyotawaliwa yalitakiwa kulipa kodi kwa waashuru
-          Syria na Israel waliamua kuishambulia Yuda kwa sababu walikataa kuungana nao katika kuasi kulipa kodi kwa Ashuru
-          Hivyo Mfale Hoshea aligoma kulipa kodi na akaomba msaada Misri kuungana nae katika kujitoa chini ya utawala wa Waashuru jambo hili lilisababisha uvamizi wa majeshi ya waashuru huko Israel na kuwahamisha ambapo Hoshea mfalme aliwekwa kizuizini.

C.       DHAMBI YA ISRAEL ZILIKUWA  SURA YA  4-10

*      Kukosa maarifa ya kumjua Mungu Hosea 4;6,11
*      Kiburi 5;5
*      Kutokuridhika 6;4
*      Udunia na kuwa kama mataifa  7;8
*      Rushwa 9;9
*      Kurudi nyuma 11;7
*      Kuabudu sanamu 13; 2,4;11-12.

D.      Upekee wa kitabu cha Hosea na ujumbe wake.

-          Hosea ni mojawapo ya kitabu kirefu ukilinganisha na vingine katika Manabii wadogo na kinakaribiana kidogo na cha Zekaria
-          Ujumbe wake unawezekana ulitolewa kwa muda mrefu kiasi kwani kitabu kinaonyesha Upendo wa Mungu kwa Taifa lisilo na uaminifu la Israel na kinatumia maisha ya Mwandishi yaani Nabii Hosea kama mfano hai wa jinsi Mungu anavyojisikia kuhusu watu wake
-          Hosea anaonya  juu ya hukumu inayokuja ambayo inaweza kuepukika kwa kumrudia Mungu tu

E.       Mstari mkuu na mistari ya Msingi.

-          Kiini kikuu cha kitabu hiki ni Pendo la Mungu kwa Israel na hukumu dhidi ya dhambi
2; 19, 4;1, 4;6, 6;6, 7;8, 8;7.

F.       Mgawanyo wa kitabu cha Hosea

-          Zinaa ya Israel ilikuwa ni kukosa uaminifu kwa Mungu sura ya 1-3
-          Hoja za kinabii kutokumcha Mungu na hukumu ijayo isiyoepukika 4-13
-          Kuamini kwa Israel na kusamehewa sura ya 14;

G.      Mchanganuo wa kitabu cha Hosea

a.       Familia ya Hosea na Israel sura 1-3
i.                     Mungu alimuagiza Hosea kuoa mwanamke kahaba hata hivyo kuna mjadala wa kitheolojia kuhusu ukahaba wa mke wa Hosea kuwa ulikuwa ni ukahaba wa aina ipi Zinaa au kuabudu miungu ambako nako kuliambatana na ibada za zinaa? Katika Israel wazinzi walipigwa mawe je ni zinaa ya aina gani?
ii.                    Mungu alitaka kuwafundisha Israel kitu  kwani walikuwa wazinzi kiroho na Hosea alikuwa ndio somo lenyewe
iii.                  Mungu huihesabu tabia ya kuabudu miungu kama zinaa ya kiroho na kwa kuwa Hosea alikuwa mwaminifu kwa mkewe Gomeri ambaye Yeye hakuwa mwaminifu ndivyo na Mungu alivyokuwa mwaminifu kwa Israel.
iv.                  Hosea aliwaita wanawe majina yaliyokuwa yakiashiria unabii.
1.       Yezreel jina hili lilikuwa na maana ya kuwa Mungu “ametawanya au Muangu atapanda” hii ilikuwa ni kwa ajili ya kuwakumbusha watu wa mji wa Yezreel juu ya mauaji yaliyofanyika Yehu alipokuwa mfalme,Yehu aliagizwa na Mungu kuwashughulikia watoto wa Ahabu lakini aliwashughulikia zaidi ya kiwango kwa sababu ya ubinafsi aliwaua watoto70 wa Ahabu huko Yezreel, Mungu alimwambia Yehu kuwa wanawe kizazi cha nne watamiliki kiti cha enzi, Yeroboamu wa pili alikuwa ni uzao wa tatu na Zekaria mwane ndipo unabii ulikuja kutimia 2Falme 10;30,1-8,Zekaria alitawala miezi sita tu kisha akauawa
2.       Lakini hata Hivyo Yezreel walikuwa na ujumbe mzuri pia  kuwa Mungu hupanda 1;45 yaani pamoja na kuwa wana wa Israel walichukuliwa mateka utumwani Mungu angewarejeza tena katika inchi yao
3.       Lo-Ruhama 1;6-7 mtoto mwingine wa Hosea jina hili maana yake Hakuna rehema
4.       Lo-Ammi maana yake sio watu wangu 1;8-9 majina haya mawili yanatufundisha na kuwakumbusha wana wa Israel na Gomeri juu ya dhambi zao na jinsi walivyolivunja agano lao na Mungu
v.                    Kwa mujibu wa sheria ya Musa wazinzi walitakiwa kuuawa kwa mawe lakini Hosea alimpenda mkewe na Mungu aliipenda Israel hivyo Gomeri na Israel walikuwa wanapewa Muda ili kwamba waweze kubadilika lakini haikuwezekana na hivyo talaka iliwakumba wote
vi.                  Mwishowe Hosea aliamua kumrudia tena mkewe na Mungu alikusudia kuwarejeza tena Israel matukio haya yana mambo ya kutufundisha sisi wa kizazi hiki cha leo
vii.                 Kwa ufupi sura ya 1-3 Inazungumzia maisha ya kielelezo ya Nabii Hosea ambaye anamwakilisha Mungu  Hosea alimuoa mwanamke kahaba anayefanya zinaa kwa sababu hatosheki na mume mmoja hatosheki ashiki zake ni Malaya anafanya zinaa pia kwa ajili ya kupata faida mapato, Huyo ni Gomeri mke wa Hosea anayeiwakilisha Israel, Baada ya kuwa amezaa watoto watatu alimwachia Hosea watoto hao na kwenda kuishi na mwanaume mwingine, wanaume wengine wakamgombea na ikalazimu wamuuze mnadani ndipo Hosea akamnunua  kwa upendo akamrudisha nyumbani.

b.       Ujumbe wa Nabii Sura ya 4-14

i.                     Kuanzia sura ya nne hadi ya 14 Nabii analeta mashtaka ya Mungu kwa wana wa Israel
1.       Anaonyesha jinsi ambavyo hakuna rehema, Hakuna kweli, hakuna kumjua wala kumjali Mungu katika Israel
2.       Kwa kusudi walijiingiza katika Ibada za sanamu na kuabudu miungu mingine
3.       Nabii anatoa wito wa kutubu lakini Israel wanakataa na kuendelea na dhambi zao
ii.                    Kwa kukataa kwao kutubu Nabii analeta ujumbe wa adhabu kwao anaitabiria Samaria kuanguka na Yuda pia wataadhibiwa
iii.                  Mwisho Nabii anatabiri kurejezwa upya kwa Yuda na Israel kuwa taifa moja na nchi moja na kuwa baadae watamtafuta Bwana Mungu wao na Daudi mfalme wao bila shaka huu uatakuwa wakati wa utawala wa miaka 1000 ya Kristo Duniani.

Hakuna maoni: