Jumapili, 13 Machi 2016

Laiti ningekunywa maji ya kisima cha Bethelehemu !



  1Nyakati 11:17.
1Nyakati 11:10 – 19
Ni muhimu kwetu kufahamu kuwa hakuna kitu au jambo linatokea tu hivihivi duniani, bila baadhi ya watu, kuhatarisha Maisha yao, ili kwamba wengine waweze kufikia Ndoto zao, Ndoto za kila mmoja wetu haziwezi kufikiwa ikiwa kwa msaada wake peke yake, ni lazima wengine wahusike, katika kuzifanikisha ndoto hizo!.

 Kisima cha Daudi Mjini Bethelehemu

Unapoona mataifa Mengi yako huru leo ni lazima ufahamu kuwa uhuru huo, haukupatikana kirahisi, wako walioupigania, unapoona kuna haki zimepatikana mahali Fulani ambako hakukuwa na haki, ni lazima ujue kuwa, kuna watu waliopigania haki hizo hata zikapatikana na wakati mwingine iligharimu maisha yao na hata kufa!, Uhai, Elimu na mafanikio yamtu moja moja pia yatategemea kwa namna moja ama nyingine kujitoa kwa watu wengine ili kutimiza azima ya mafanikio yetu na kuishi kwetu.

Askari mmoja Nchini Marekani wakati wa kimbunga kikali sana kijulikanacho kama Hurricane Sandy alijitosa katika mafuriko na kuokoa watu wazima sita na mjomba wake mdogo sana na baada ya kufika Ng’ambo aligundua kuwa Baba yake hakuweko, hivyo alirudi tena ili amuokoe Baba yake aliporejea, hakufanikiwa kumuona na baba yake kwa bahati njema alikuwa ameokolewa kwa njia nyingine na kufika n’gambo lakini baadaye ilibainika kuwa Artur Kasprizak alikuwa amefariki dunia alipokuwa akijaribu kumtafuta baba yake.

Mtakatifu Maximilian Kolbe wakati wa vita vya wanazi WANAZI wa Hitler waliamua kujaribu kuuwa waqtu kumi kwa njaa ili waona itakavyokuwa, wafungwa hawa kila mmoja alikuwa akiogopa , Wanazi walichagua mtu mmoja mfungwa aanze zoezi la kufa na Njaa na mtu huyu alilia sana akiitaja Familia yake Ndipo Maximilian Kolbe aliamua kujitoa yeye ili achukue nafasi ya mfungwa huyo, na akaanza zoezi la kushinda na njaa, Kolbe aliimba na kuomba kwa sauti kwa wiki tatu ili kuokoa roho za wengine lakini wanazi walidhihaki na wakaamua kumchoma sindano ya sumu akafa na baadaye Kanisa Katoliki lilimtangaza kuwa Mtakatifu.

 Mtakatifu Maximilian Kolbe

Mwaka 1984 mwezi kama wa tano na wa sita hivi mwaka huo nikiwa kijana mdogo sana niliugua sana, wakati huo tulisafiri na baba kutoka Lindi mjini tulipanda Ndege na kuja Dar es Salaam, kisha tulipanda basi kuja hapa Muheza kumpa Pole shangazi kwani alikuwa amefiwa na Mumewe, kwa bahati mbaya nilianza kuugua njiani huku nikiishiwa na nguvu na nilumwa sana sana, hali yangu ilikuwa ngumu kiasi ambacho Madaktari walikata tamaa na kusema labda tukajaribu maswala ya nyumbani, mama alikuwa amebaki Lindi na kaka na mdogo wangu mdogo sana aliyekuwa na miaka mitatu tu, Shangazi aliyekuwa amefiwa na ndio tumekuja kumpa pole alilazwa name katika Hospitali ya teule hapa Muheza, likizo yote iliishia hospital mama yangu alipoambiwa kuwa ninaumwa sana alipiga magoti na kumuomba Mungu sana, aliambiwa kuwa wakati wowote lolote lingeweza kutokea, “Mama yangu aliomba Ee Mungu tafadhali unichukue mimi badala ya Mwanangu!” Nilipona kwa njia ambazo Mungu alikuwa anajua na tulifanikiwa kurudi Lindi nikiwa salama lakini nilikuwa Nimekonda sana mama alifurahi kuniona lakini kabla ya mwezi kumalizika July 19 Alhamis 1984, Mama yangu alifariki baada ya Operesheni ya kidole tumbo kushindikana

Maisha yalianza kuwa tofauti, tulianza kuishi katika mikono ya watu wasio na Huruma, na wakatutenda kila walichojisikia, Nafahamu wazi kuwa Maisha yangu yaligharimiwa na watu Hata sasa sifahamu kuwa nitampata wapi Mama japo nilipe fadhila, ama nifanye nini ili niweze kuifurahisha roho yake, 

Katika Maandiko wote tunafahamu kuwa Daudi alikuwa ni shujaa na ni mtu wa Vita, alimpiga Goliath, aliuwa wafilisti wapatao Miambili alipoagizwa na Sauli kuwa anataka Govi za wafilist mia moja ili amuoze Binti yake.

Lakini hata hivyo Ushujaa wa Daudi hauwezi kukamilishwa na Daudi peke yake, huwezi kuamilisha Jambo lolote mwenyewe, wala kwa kudharau wengine wanaokuzunguka, mafanikio yako hayatokani na wewe mwenyewe na akili zako na nguvu zako bali pamoja na wale Mungu anaokupa kukuzunguka, wako wanaokuombea, wako wanaochukuliana nawe, wako waliokusamehe, wako wanaokutia moyo, wako waliokuelekeza wako wanaokutetea, na mengineyo.

Daudi aliweza kutiwa Moyo na makamanda ambao walikuwa wapiganaji Hodari sana kupita kawaida licha ya kupigana kwaajili yake pia walimlinda na Mungu alimpa Ushindi ushindi Daudi kupitia wao.

1.       Yashobeamu mhakmoni 1Nyakati 11:10-11
2.       Eleazar mwana wa Dodai 1Nyakati 11:12
3.       Mwingine aliitwa Abishai 1Nyakati 11:20 

Majemadari hao ndio waliosababisha Ufalme wa Daudi kuwa Imara
Siku Moja Daudi alifanya jambo la kipumbavu sana hatujui ilikuwa ni kwa sababu Gani, lakini alitamani kunywa maji ya Kisima cha Bethelehemu, Daudi alizaliwa Bethelehemu, alikulia hapo alitumia maji ya kisima kile huenda yalikuwa matamu au aliyazoea na hivyo aliyakumbuka
Hata hivyo wakati huu alipokuwa akiyadai, hali ilikuwa ni Mbaya kulikuwa na Vita kali sana kati yao na Wafilisti na kisima kile pale kilipokuweko ndiko kulikokuwa na Ngome ya Wafilisti yaani maadui wa Israel lakini wakati huohuo Ndio Daudi anatamani maji ya kisima kile tena anayadai kwa Nguvu kubwa LAITI NINGEKUNYWA MAJI YA KISIMA CHA BETHELEHEMU ! 

Majemadari wake Daudi waliposikia kauli ya mfalme wao, bila kujalia kuwa wanajidhihirisha kwa maadui zao na kuhatarisha Maisha yao, tena bila ya kuuliza haya maji yana tofauti gani na mengine? Mfalme leo ana wazimu au inakuwaje anataka maji ya Bethelehemu ni Udhaifu wa namna gani huu? Hawakuwa na maswala dhidi ya kutii, walisema liwalo na liwe wakapenya ngome ya Wafilisti safari hii sio kuokoa taifa au kuokoa mtu aliyetekwa hapana ni kuleta maji kwa mfalme mwenye kiu ya kijinga tu!

Daudi alipogundua kuwa amefanya Ujinga wa kipuuzi, aliamua naye kujitesa aliyapokea maji yale na kuyatoa dhabihu kwa Bwana, Hakukubali kuyanywa akasema MUNGU wangu apishie Mbali, nisifanye Hivi je “NINYWE DAMU YA WATU WALIOHATARISHA MAISHA YAO”,  hatuwezi kumpuuzia bwana wetu Yesu alikufa Msalabani akamwaga Damu yake, tunatumia jina lake, kupata ushindi na mafanikio mbalimbali ni muhimu kumuenzi Bwana wetu, Tukumbuke wote waliotusaidia kufikia hapo tulipofikia, tuache kupuuza maswala na michango ya watu wengine, wako watu wenye dharau Duniani ambao hawaoni michango ya watu wengine katika jamii, wanatamani hata kufuta Historia zao, hawataki kuona hata picha za waasisi na waliopoteza maisha kwaajili yao, Kusoma kwetu na kulipiwa kwetu Ada kuna michango ya watu mbalimbali ambao wanataka kufurahia ndoto zako kufikiwa wanataka kuhakikisha kuwa kiu yako inatimilizwa na wako tayari wao wafe ili wewe uisho usihesabu mchango wao kuwa ni Upuuzi.

Ujumbe na Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: